Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, October 4, 2013

Mkuki ni kwa nguruwe-7



‘Shemeji samahani nilikuwa nataka kukuuliza maswali kama hutojali...’akanishitua docta yaani rafiki wa mume wangu kutoka kwenye dimbwi la mawazo, nikamwangalia machoni kabla ya kumjibu, na yeye kwanza akatabasamu, pili akaonyesha uso wa kushangaa, na kabla hajasema lolote zaidi nikasema.

‘Naomba usiniulize maswali ya kuzidi kuniumiza, maana leo imekuwa siku ya mikasa kwangu....’nikasema.

‘Mikasa mingine umejitakia mwenyewe, usimlaumu mtu, ...sitaki kurudi nyuma, lakini wewe mwenyewe unalitambua hilo...’akasema .

‘Sio kweli, nafahamu unamaanisha nini, haya yanayotokea hayana msingi kabisa na mambo yetu ya nyuma, na unafahamu kabisa kwanini nilichukua uamuzi huo, na sitajutia kwa hilo...’nikasema.

‘Kulipa fadhila...eeh, haya endelea kulipa fadhila...’akasema

‘Najua wewe na wazazi wangu mtasema hivyo, ..lakini hamjui ni nini kilicho moyoni mwangu, mume wangu nampenda na nilimpenda toka siku ile ya kwanza, nilipomuoana, hilo hamtaki kulisikia, je kuolewa na mtu unayempenda ni kosa, eti kwa vile anatoka kwenye koo za masikini, hebu niambie sasa hivi ana umasikini gani, mbona mpo sambamba....’nikasema kama namuuliza.

‘Mimi sijakulaumu kwa uamuzi huo, lakini tabia za watu hazijifichi, zingine ni za kihistoria, hata ufanyaje ni kama vile wanavyosema watu kuwa kunguru hafugiki,.. na ndivyo maisha yetu yalivyo, misingi ya kizalia ni vigumu sana kuigeuza...unajaribu lakini ipo siku itatokea...’akasema.

‘Tatizo lako wewe ni dakitari lakini ukifikia kwenye maswala haya unaacha udakitari wako pembeni, hutaki kuutumia hata katika mambo kama haya, kizalia kina nini na maswala ya mapenzi, ..kukukataa imekua ni nongwa, kwani huyo mkeo uliyempata humpendani...mbona mimi sijaingilia maisha yenu..?’ nikamuuliza.

‘Tuyaache hayo nataak kukuuliza mambo ya msingi, maana pamoja na yaliyotokea nyuma, bado nakuona urafiki yangu, na mumeo ni rafiki yangu mkubwa, ndio maana nilipogundua kuwa ndio yeye unayemtaka, sikutaka kuingia kwenye ushindani, niliona nikuachie tu, kwa vile ulinitamkia mwenyewe kuwa unampenda,..na mimi ukasema hunipendi, nikaona kwanini ning’ang’anie mtu asiyekupenda,.....’akasema.

‘Uliza maswali yako ...’nikasema na yeye akaniangalia kwa muda, halafu akasema;

‘Nataka nikuulize maswali ya ndoa yenu,...’akasema

‘Kama ni maswali kuhusu ndoa yangu, ningelifurahi kama ungeyaacha kama yalivyo, kwani akili yangu haijatulia, siku ya leo imekuwa ni ya mitihani, tangu asubuhi, matatizo, ofisi matatizo..nyumbani matatizo, huko kwa rafiki yangu matatizo..tena hili kubwa lao, ....nimechanganyikiwa kabisa,...ulikuwa unataka kuniuliza nini?’ nikasema nikijua ni yale yale ambayo mara kwa mara ananilaumu eti kwanini nilimkataa yeye nikaamua kuolewa na huyo rafiki yake.

‘Shemeji ...rafiki yangu ,‘Ili kuondokana na huko kuchanganyikiwa ni bora ukajaribu kuyaongea hayo matatizo uliyo nayo, hasa kwa mtu kama mimi ambaye niliwahi kuwa rafiki yako wa akribu, ukiyaweka kichwani mwenyewe utaumia, huenda ungelinieleza nikajua jinsi gani ya kukusaidia....’akasema.

‘Hapana, mimi nakufahamu bwana, ...wewe na wazazi wangu siku zote mnaombea ndoa yangu ivunjike, hebu nikuulize, kwa mfano ndoa yangu ikivunjika utapata faida gani, maana wewe sasa una mke, utamuacha mkeo ili uje unioe mimi, au ndio mnataka kunikomoa...?’ nikamuuliza.

‘Hahaha..hivi wewe unafikiri mimi nachukia ndoa yenu, kuwa natamani ivunjike eti kwa vile ulinikataa, acha hiyo, mimi mumeo ni rafiki yangu,...unalifahamu fika, na kama asingelikuwa ni rafiki yangu ningelipambana hadi nihakikishe nimekuoa, lakini niliona hakuan haja, kwanza ungepata muda wa kumsaidi arfiki yangu ambaye katokea kwenye shida,....sitaki hata kumuongelea kuhusu maisha yake ya huko nyuma...’akatulia.

‘Najua hilo mtalirudia kila siku...na hamtafanikiwa, maana sasa mnaishia kumuonea wivu, ana kampuni, ana masiha mazuri,..nini tena cha kumsuta , hakuna, iliyobakai sasa ni majungu...’nikasema.

‘Haya bwana, ngoja nikuulize hayo niliyotaka kukuuliza ili uone kuwa mimi najali sana ndoa yenu,...’akasema

‘Uliza, na nitakujibu,....lakini kama ni mambo ndani ya familia yangu,sitaki...’nikasema

‘Hebu niambie ukweli, mume wako alikuwa wapi, kwani watu walioona hiyo ajali wanasema mume wako alikuwa akiendesha gari kwa mwendo wa kasi sana...kama vile alikuwa akikimbizwa,au akikimbia jambo?’akaniuliza na mimi hapo nikashituka, nikikumbuka kuwa hata mimi nilifanya hivyo hivyo.

‘Unataka kusema nini’ nikamuuliza.

‘Nataka kujua kama unafahamu wapi mumeo alikuwepo leo hii, kabla ya hiyo ajali?’ nikamuuliza

‘Kwani hawo watu wanasema alikuwa akitokea wapi...!?’ nikamuuliza huku nikiashiria kushangaa na sijui kwanini niliuliza swali hilo badala ya kujibu swali.

‘Shemeji mimi nakuuliza swali na wewe unaniuliza swali, kwani siku ya leo toka asubuhi, ...mliagana vipi,  na mchana kutwa, hamkuwahi kuwasilina, hamkuonana, au kuambizana mnakwenda wapi, mnafanya nini....nafahamu unafahamu wapi alipokuwa akitokea au hufahamu?’ akaniuliza.

‘Shemeji mimi na mume wangu tuna mishughuliko tofauti, kila mmoja akiamuka asubuhi anakwenda kwenye shughuli zake kivyake vyake, hakuna kufuatana..hayo ndio maisha yetu na sitaki uniulize kwanini maana hata mimi sijakuulizia kuhusu maisha yako, nilishawahi kukuuliza kuwa wewe ukiamuka asubuhi unafanya nini na mkeo, au kwa vile ni mimi na rafiki yako, ambaye hamkutaka mimi niolewe nay eye..manatafuta visababu...’nikasema.

‘Sio hivyo, ninachotaka hapa ni kusaidia, na wala sio kubomoa, na hata kama wewe ungeliona kwenye nyumba yangu kuna matatizo na tufahamiana, tuna urafiki wa muda mrefu, na unanijali ungeniuliza, ili uone kama unaweza kusaidia....’akasema.

‘Sijaomba msaada kwako, mimi na mume wangu tuna utaratibu wetu na hatuna shida nao,...’nikasema.

‘Lakini mwenyewe kwa akuli yako hapa, umesema siku ya leo imekuwa mitihani kwako na ukasema mattizo nyumba, matatizo kwa rafiki yako....hii inaashiria nini, kama sio mna matatizo wewe na mume wako...?’ akaniuliza.

‘Hatuna matatizo, na kama yapo ni ya kawaida tu , ya mume na mke..hayakuhusu...’nikasema.

‘Sawa, bado hujanijibu swali langu, ....’akasema.
Swali lipi shemeji....?’ nikamuuliza

‘Hebu niambie utaratibu wenu wa leo ulikuwaje, ..?’ akaniuliza na mimi nikamwangalia kwa amkini, nikaona nisibishane naye sana nikamwambia;

‘Sisi utaratibu wetu ni kuwa, kwa vile kila mmoja ana kampuni yake, na ana mambo yake, tukiamuka kila mmoja ana hamsini zake, hatuaingiliani kabisa, wakati mwingine kama ni lazima ndio tunapeana taarifa, ...’nikasema.

‘Hiyo ni kwa ujumla je kwa leo ilikuwaje, ...?’ akaniuliza, na sikumuelewa ana maana gani, kwani maswali yake niliyaona kama ya polisi nikasema.

‘Ama kwa leo, nakumbuka aliniambia kuwa akitoka kazini anaweza kupitia kumona mke wa rafiki yake ambaye kajifungua, ...nakumbuka aliniambia kitu kama hicho, na sikuwa makini sana kumsikiliza maana nilikuwa na mambo mengine ya kikazi yalikuwa yamenitinga...’nikasema.

‘Mke gani wa rafiki yake, aliyejifungua, alikwenda kumuona mzazi, au mume wa huyo mzazi, maana mimi nijuavyo mara nyingi mke akijifungua wanaokuwa karibu na huyo mzazi ni wanawake, kwahiyo ilitakiwa wewe uende naye....au nimekosea?’ akauliza

‘Kwahiyo unataka kusema nin?’ nikamuuliza

‘Sitaki kusema kitu, ninachotaka ni ukweli ili niweze kusaidia,...kama ningelikuwa nataka kusema kitu, kwanini nikuzunguke, wakati wewe ni rafiki yangu, na mume ni rafiki yangu pia....’akasema.

‘Nakuuliza hivi kwa maelezo yako una maanisha nini kuhusu rafiki yako?’ nikamuuliza

‘Inawezekana  hakuwa katokea kazini,....maana mimi nilimpitia na nikaambiwa kuwa ametoka mapema tu...’akasema docta.

‘Mimi siwezi kujua  mipangilio yake, na siwezi kutabiri kuwa alikuwa wapi, ...kama hakuwepo kazini, basi alikuwa kwenye shughuli nyingine nje ya kazini kwake, hilo linawezekana na hilo la kusema mzazi ni lazima muandamane na mke wako, halina mantiki yoyote , wewe unachotaka hapa ni kujenga sababu ya kumuona mume wangu ana tabia mbaya....’nikamwambia.

`Shemeji lakini nakumbuka tulishaliongelea hili kabla, nilishawahi kuwakanya haya maisha yenu mnayokwenda nayo, ...sio mazuri kwa mke na mume, kiukweli kwa wanafamilia hilo sio jambo jema, hata kama mnaona kuwa huo ni usasa, au wengine wanasema ni uzungu...mimi siupendi. Mimi nawajali sana, kuliko unavyofikiria wewe....’akasema.

‘Nashukuru kama unatujali, na ningelishukuru kama unalosema linatoka moyoni na lina ukweli, kwani hata wazazi wangu wanasema hivyo hivyo, wakati walishatamka kuwa,....nikiendelea na mume wangu watahakikisha maisha ya mume wangu yanakuwa ni mashaka, na huenda akaishia jela...nikakumbuka kauli ya wazazi wangu wakisema;

 ‘Achana na huyo mtu, kama unataka kumuona akiendelea na maisha yake, achana naye, na kama unataka akaishie jela, endelea naye....hatuwezi kukuona ukituzalilisha ....atapotea kama alivyoptea baba yake....’

‘Wazazi ni wajibu wao kumlinda mtoto wao, hata wewe ukifikia mahali pako, utasema hivyo hivyo kwa binti zako, hutapenda aende kuishi na mtu ambaye humuamini..’akasema.

‘Haya unatushauri nini Docta...’nikasema kwa dharau.

‘Mimi nasema hivi maisha hayo mnayoishi yana madhara yake hasa katika maisha yetu haya ya kiafrika,...miundo mbinu ni mibaya, hali za barabarani tunazijua wenyewe, usalama hauna uhakika, kwahiyo ni vyema kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na kila mmoja kumjua mwenzake yupo wapi na anafanya nini, kwani simu zina kazi gani?’ akaniuliza.

‘Unanichekesha kweli, ...yaani umefikia hatua ya kutudharau kiasi hicho...’nikasema

‘Lakini mwenyewe umesema kuwa kila mmoja ana mambo yake, na leo hukujau kabisa kuwa mume wako alikuwa na taratibu gani, za nje ya kiofisi....sasa utajueje mwenzako yupo wapi, kama likitokea la kutokea....’akasema huyo docta na mimi sikuwa nimemuelewa sana, nikamsikiliza tu aendelee kuongea.

‘Endelea doct-aah’ nikasema kwa dharau

‘Mimi siwapingi kwa utaratibu wenu huo wa maisha, lakini ni vyema mkajenga tabia ya kuambizana wapi mmoja anakwenda, baada ya muda mkapigiana simu tena, kujua ni nini mwingine kapanga, atakwenda wapi, ...ni nini kinafanyika, halafu mkirudi nyumbani jaribuni kukaa na kuongea, sio kila mtu akirudi nyumbani yupo kwenye laptop yake ...kila mtu yupo bize, na kazi zake, mnasahau majukumu yenu ya ndoa...’akasema kama mzazi anayemuelezea mtoto wake aliyekosana na mkewe.

‘Umekuwa kungwi siku hizi au mwanandoa mzoefu, ...nyie mnajipa moyo kuwa ndoa yenu ipo safi eehe,  haina matatizo au sio, unaiona ndoa yangu ndiyo yenye matatizo au sio....?’ nikamuuliza.

‘Mimi siwezi kujigamba kuwa ndoa yangu haina matatizo, yapo na kila ndoa ina matatizo yake, lakini yakizidi ni lazima tuambizane, ni mimi nawaasa, kama wewe ungeliniasha mimi ukiona utaratibu fulani sio mnzuri kwenye ndoa, hasa huo mnakwenda nao.’akasema na mimi nikahisi kukerwa na hayo maneno yake, niliona kama ananiingilia maisha yangu ya ndoa, japokuwa sikutaka kumkatiza, nikatulia tu.

‘Mimi kiukweli sifurahishwi na tabia hiyo, halafu rafiki yangu huyu, siku hizi anaonekana kunywa kupita kiasi inaashiria kuna tatizo, naufahamu unywaji wake, huu wa sasa ni ulevi, sio unywaji...anaonekana kama ana msongo wa mawazo, ...mimi kwasabbu ya safari zangu za hapa na pale, sijaweza kukaa naye tukaongea kwa kina, ila kila muda nilipopata nafasi kidogo ya kuwa naye, nimemuona sio yule rafiki yangu ninayemfahamu..hana raha, anaonekana anakerwa na jambo fulani..nahisi kuna tatizo ndani ya ndoa yenu..’akasema.

‘Wewe unahisi kuna tatizo kwenye ndoa yetu....kwani hiyo kuhisi imeanza leo?’ nikawa kama namuuliza

‘Ndio maana nataka tusaidiene kwa hilo,...kama kuna tatizo lolote niambie shemeji, hiyo dalili aliyo nayo rafiki yangu inatokana na msongo wa mawazo, shemeji jaribuni kukaa na kuliongelea hili nahisi kuna tatizo..ongeeni ambizaneni, ili muwewe kuishi kama wana ndoa, na sio wabia...’akaniambia huyo dakitari nikacheka kwa dharau aliposema `wabia...’

‘Eti eti kama wanandoa an sio wabia...dharau ya ajabu kabisa...’nikasema na kutulia

Nilitulia kwa muda bila kusema neno..hayo maneno ya mwisho yalinichefua,, hasira zikanikaba, maana sikuona tatizo lipo wapi, na sikupenda mtu aniingilie maisha yangu, hasa huyu, ambye alikuwa ni mpinzani mkubwa, kwa vile alitaka anioe yeye, ...ndio kiukweli kuna tatizo lipo, lakini kwangu mimi nililiona ni tatizo dogo la kindoa, ni tatizo la ndani ya ndoa, ambalo halikuhitajia mtu wa nje kuliinglia....’nikatuliza hasira kidogo, nikikumbuka hali ya mume wangu ..sijui anaendeleaje huko ICU.

‘Sina maana mbaya kwa maneno hayo, nisema kwa fano, wanadnoa wanaishi kama mtu kaja washirikiane kwenye kazi ...na wanasahau mambo muhimu yanayasababisha ndoa iwepo, ndio maana nikatumia neno mbia....’akasema na mimi sikumjibu

Moyoni nafahamu kuwa kweli kuna tatizo kwenye ndoa yangu,lakini hata hivyo sikuona kwanini huyu mtu aniingilie, kama kulikuwa na tatizo linahitajia msaada wake ningelimwambia,...na kwanini anilaumu mimi kwa hiyo ajali ya mume wangu, maana niliona kama ananitupia lawama mimi....nikahema kidogo, halafu nikashusha pumzi kuondoa hilo donge moyoni, nikasema;

‘Shemeji mimi sijui kama kuna tatizo kubwa kihivyo, kama yapo ni mambo ya kawaida ya mume na mke. 

Na sijui kwanini unisakame, mi-mi, kwani  kama kulikuwa natatizo ilikuwa ni juu yake mume wangu kuniambia, yeye ni mwanaume bwana, na mwanaume ni kiongozi ndani ya familia, kama ameogopa kuniambia ukweli, basi ni unyonge wake mwenyewe, sijawahi kumpinga kwenye mambo yake, ...sijawahi kumuingilia kwenye taratibu zake, na yeye ndivyo anavyofanya kwangu...sasa tatizo lipo wapi, mnataka mimi nifanye nini...kama umeona kuna tatizo , huyo ni rafiki yako mkubwa nenda kamuulize yeye...’nikasema huku nikionyesha kukerwa.

‘Shemeji ni sawa...sio kwamba nataka kuingilia maswala yenu ya ndani, hapana, ...na nafahamu kila tkiongelea maswala haya unayaunganisha na yaliyopita, mimi nakuhakikishia kabisa sipo huko, nipo kwenye kuijali ndoa yenu,...ninachotaka mimi ni kujaribu kuwekana sawa, na hata kama ingelikuwa ni mimi ...kama majirani, kama marafiki wema, mngelishauri....hivyo hivyo’akasema.

‘Sawa, ....na tungefanya hivyo, kama kweli tunaliona tatizo au kama ungelikuja kwangu ukaniambia kuna tatizo kwenye ndoa, yako, na kuomba msaada wa ushauri, lakini sisi hatujafikia hatua hiyo...ikifikia hapo tutakuja..ombeeni hivyo hivyo.....’nikasema

‘Shemeji samahani nikuulize swali muhimu sana, nililokuwa nataka kukuulizia...usinielewe vibaya, na wala usilipeleke kwenye urafiki wetu wa zamani, ninachotaka kufanya hapa ni kujaribu kuangalia kama kuna tatizo maana nyie mnaweza msilione, lakini mimi kama docta ninaweza kuliona hata kama hujajieleza kwangu, nakuomba nikuulize maswali ya ndani ya ndoa yako, kama hutojali, ...’akasema.

‘Wewe uliza tu, sioni ajabu na maswali yako,..nitakujibu kama ninavyojua, ..lakini mimi siwezi kumjibia rafiki yako, yeye huenda anaweza akawa matatizo yake binafsi, lakini kama hajaniambai siwezi kuyajua,..kweli mimi ni mke wake, lakini kama mmoja atakuwa sio mkweli kwa mwenzake, basi hilo ni tatizo lake, na huwezi kukimbilia kumlaumu mke au mume, bila kujua undani  wa maisha yao....’nikasema.

‘Shemeji sasa mimi nataka nijue undani wa maisha yenu,..niamini mimi, nina nia njema kwenu, kama mlivyoniamini siku ya ndoa yenu, kama rafiki mkubwa wa mume wako, kama rafiki yako mpenzi wa zamani, nataka niingie ndani ya ndoa yenu, nijaribu kuangalia undani wa ndoa yenu, kama kuna tatizo....tusaidiane’akasema.

‘Haya ....Unakaribishwa....ingia maana nimeshachoka kukuambia kuwa hakuna tatizo...sijui nikueleze vipi,..haya uliza hayo maswali ya ndani ya ndoa...’nikasema nikiwa sijamuelewa vyema huyu mtu anataka nini kwangu,, ni nini lengo lake, au ana kitu gani kakigundua ndani ya ndoa yetu, huenda rafiki yake amemlalamikia jambo, na huenda atalifahamu kwa kumkubalia kujibu maswali yake.

‘Shemeji, je katika mambo ya unyumba mnashirkiana kama kawaida?’ akaniuliza swali lililonifanya nsihituke na kugeuka kumwangalia uoni, halafu nikageuka kuangalia mbele. Hilo swali likanishitua kidogo, maana kiukweli  mambo hayo nilishakuwa kama sina habari nayo sikumbuki lini niliwahi kukaa na mume wangu tukafurahia hilo tendo.

Nilijikiuta nikitulia huku nikiwazia tatizo hili lilianzia wapi, nakumbuka kabisa tatizo hili lilianzia baada ya kupata mtoto wa pili...ambaye sote tulitarajia kuwa atakuwa mtoto wa kiume, lakini tukapata tena mtoto wa kike, kwangu mimi sikujali, na nilifurahia sana lakini mwenzangu alionekana kama hana raha, japokuwa hakuonyesha...na tulikuja tukaliongelea tukalimaliza hilo tatizo, na anawapenda sana watoto wote, sioni kuwa hilo ni tatizo kwetu, je kuna nini kingine, na hayo mahusiano ya kitandani, hapana, haiwezekani iwe hivyo....

Kwakweli sikutaka kumwambia huo ukweli, nikajifanya hakuna tatizo, na hata hivyo sikuona kuwa ni tatizo, maana kama kweli ilikuwa ni tatizo, tungeambizana, ..mwenzangu hata siku moja hajawahi kunilalamikia hilo swala, ....kama angelinihitaji angeliniambia....hata hivyo, kazi zimekuwa zikitutinga sana, sio mimi tu, hata yeye,...mimi hilo sikuona ni tatizo..nikasema;

‘Shemeji hilo ni swali gani tena,...na unahisi sisi hatujui umuhimu wa hilo tendo, au umetuona sisi ni watoto wadogo, au mwenzangu alishawahi kuja kulalamika kwako,..nikuulize wewe swali, nani ana haki ya hilo tendo kwa mwingine...?’ nikamuuliza

‘Nyote, mna haki , yeye kama mumeo ana haki zote kwako wewe, kama ulivyo na haki zote kwake yeye...ni muhimu sana hilo ’akasema.

‘Je hizo haki, unazozizungumzia ambazo umesema ni za unyumba, ni nani anastahili kumuelezea mwenzake?’ nikamuuliza.

‘Wote mnastahili kuelezana , kila mmoja kwa nafasi yake anastahili kumwambia mwenzake, kumuelezea mwenzake hisia zake, kama kuna tatizo limejitokeza,  ni wajibu wa kila mmoja kumwambia mwenzake na kusaidiana na kila mmoja awe tayari kwa mwenzake...’akasema docta.

‘Umejibu vyema,...je rafiki yako aliwahi kuja kukulalamikia kuwa mimi simtizmizi hayo?’ nikamuuliza.

‘Hajawahi kunilalamikia....’akasema na kutilia.

‘Kwahiyo hizo ni hisia zako tu,ambazo nahisi umezijenga tu, kwa vile....’ nikakatiza.

‘Kwasababu ya historia yetu ya nyuma...’akamalizia, na mimi nikasema;

‘Shemeji hilo swali lako linaingilia mambo yetu ya ndani ya familia siwezi kukujibu, kwani jibu lake lipo wazi...kama kungelikuwa na tatizo juu ya hilo, kama mimi ningelikuwa nimekiuka hayo, na nikawa sitimizi wajibu wangu kwake,angeliniambia, na kama nimekuwa mkaidi basi angekuja kulalamika kwako, je aliwahi kufanya hivyo?’ nikamuuliza.

‘Hajafanya hivyo moja kwa moja, mara nyingi, wanandoa wanaweza wakawa na tatizo kama hilo, wakanyamaza, na wengine hasa wanaume wakawa na mambo ya kutoka nje ya ndoa, badala ya kulitafutia hilo tatizo ufumbuzi wake....’akasema.

‘Unasema hivyo ukiwa na maana gani, umeona dalili zozote kama hizo kwa mume wangu?’ nikaumuuliza.

‘Nimesema kwa ujumla wake, sio kwa mume wako tu...nimesema kuna wanandoa wana matatizo kama hayo, na hawataki kuwa wawazi kwa wenza wao, na matokea yake, hasa wanaume, walio wengi, wanajikuta wakitafuta nyumba ndogo, na wengine wanakuwa walevi, wanakunhywa kupita kiasi.....’akasema.

‘Shemeji, kama akili zetu zitajikita kwenye maswala haya ya ndoa, ya mahusiano ndani ya familia, mambo ya kindoa, mapenzi ya ndani, hatutaweza kabisa kupiga hatua za kimaendeleo, maana hilo sio tatizo, .. tendo la ndoa ni kitu kidogo sana kwa wanandoa, ndio maana likaitwa hivyo, tendo la ndoa, halina mjadala, lipo wakati wote, kama hawo wanandoa wapo...kama mtu ana tatizo kwa hilo, mimi nashindwa kumuelewa...’nikasema.

‘Wewe unaliona ni dogo sana, kwasababu muda mwingi upo kwenye shughuli zako, na shughuli zako umezifanya ni muhimu sana, kuliko hiyo ndoa, ndio maana hulitiliii maanani, na matokea yake mnajisahau, na kulisahau hilo jukumu la msingi wa ndoa..hilo ndilo msingi wa ndoa, mengine ni kusaidiana tu,....’akasema.

‘Hapo shemeji unavuka mipaka, huwezi kunisuta kwa mambo kama hayo..kuwa siyajui, hatuyafanyi,..., hata kama wewe ni dakitari, sijaja kwako kukuambia nina tatizo kama hilo, na halina hata haja ya kuliongelea, maana kila mwanandoa anafahamu umuhimu wake, na wajibu wa kila mmoja kuwa muwazi kwa mwenzake hilo  ni la msingi pia, kama mmoja akiwa kimya, akajitwika matatizo yake mwenyewe, utasema nini hapo?’ nikawa kama nimemuuliza. Na kabala hajasema kitu, nikaendelea kuongea;

‘Hata kama wewe ni best man wa mume wangu ,...hutakiwi kuchimba chimba maswala ya ndani kama hayo kwenye ndoa za watu, hayo ni maswala ya ndani ya wanandoa wenyewe, hayakuhusu...nakuomba shemeji unielewe hivyo, kama ingelikuwa kweli rafiki yako kakulalamikia ingelikuwa ni hoja hapa....na mimi ningelikuwa radhi kusikiliza na kukuomba ushauri...kama umesema hajawahi kulalamika kwako, basi wewe una lako jambo’nikasema kwa hasira.

‘Kwa jinsi ulivyotahayari... shemeji naona kuna tatizo...na hali kama hiyo nijuavyo mimi kwa wanaume wengine wanaweza kutumia mwanya huo kama kisingizio cha kwenda nje...siwezi kusema rafIki yangu huyo ana tabia hiyo, maana wakati mwingine, tunatembea wote kwenye majumba ya starehe,kuangalia mziki, unatufahamu  sana, na yeye anajitahidi sana kuwa mbali na mambo hayo ya nyumba ndogo, sijawahi kumuona kwenye mambo hayo,, ....’akasema huyo dakitari bila kujali jinsi  gani nilivyomjibu kwa hasira.

Sikusema kitu maana niliona nikiongea tena nitaongea vibaya zaidi nikatulia kumsikiliza yeye, anavyoongea, kwakweli alijaribu kuongea kwa upole, kama ujuavyo madakitari wanaofahamu kazi yao vyema.

‘Lakini yule rafiki yangu niliyemfahamu enzi hizo, sio huyu wa sasa, nahisi kuna tatizo, tena inaonekana sio tatizo dogo kama wewe unavyolichukulia, na nahisi kuna chanzo, na wewe unakifahamu ila hutaki kusema ukweli...’akasema na kuniangalia machoni , mimi nikamkwepa na kuangalia pembeni.

‘Je na huko kwa rafiki yako kulikuwa na tatizo gani?’ akaniuliza na hapo nikashituka na kumwangalia machoni, na moyo ukaanza kunienda mbio,....

NB: Msichoke, hii ndio diary yangu bwana, inachimbia tatizo.


WAZO LA LEO: Ndoa nyingi zimekuwa na sintofahamu kwasababu ya kuzarau mambo muhimu kwenye ndoa, na mengine yanaonekana ni madogo au hayana maana , na mengine ni msingi wa ndoa, lakini wengine wanayaona ni ya kawaida tu ..kama wana ndoa, ni vyema mkayaongelea, maana dogo kwako linaweza likawa kubwa kwa mwenzako, na kama hamtayaongelea wenyewe ni nani atawaongelea, kwanza ongeeni wenyewe, mkishindwa ndio mtafute msaada.

Ni mimi: emu-three

2 comments :

Anonymous said...

My programmer is trying to persuade me to move to .net from PHP.
I have always disliked the idea because of the costs. But
he's tryiong none the less. I've been using Movable-type on
several websites for about a year and am nervous about switching to another platform.
I have heard good things about blogengine.net. Is there a
way I can import all my wordpress content into it? Any kind of help would be greatly appreciated!3

Anonymous said...

Duh we ni mkali.