Kila nilipokuwa nikimtupia macho mume wangu, niliona hali
yake ikiwa inabadilika, alionekana kama anazidiwa, na wasiwasi wangu ukazidi,
na hadi tunamfikisha hospitalini, alikuwa hajitambui....akawa kapoteza fahamu
kabisa, na mimi nikageuka kumwangalia docta nikitaka anipe angalau matumaini,
lakini docta mwenyewe alionekana kuonyesha wasiwasi.
‘Docta kuna nini tena kwa mume wangu....?’ nikamuuliza, na
yeye akaniagalia mchoni, na hakusema kitu hapo hapo, lakini baadaye akasema;
‘Tutajua baada ya uchunguzi....’akasema huku akigeuka
kuelekea huko ICU.
Endelea na kis chetu................
***************
Wakati mume wangu yupo huko ICU, mimi nilibakia kwenye
sehemu ya mapokezi na huyo rafiki wa mume wangu, ambaye ni dakitari pia, lakini
sio dakitari wa hospitali hiyo ndio maana hakuruhusiwa kwenda huko ndani, kwani
sio kituo chake. Akili yangu sasa ilikuwa kwa mume wangu, mambo mengine yote
nilishayaondoa kichwani.
Jinsi nilivyomuona mume wangu akiingizwa chumba cha wagonjwa
mahututi hajitambui, keshapoteza fahamu, nilihisi kama sitaweza kumuona tena....na
nilitaka kumlaumu docta kwa kutokumlazimisha rafiki yake wafike hospitali
mapema, lakini nikajizuia, na nikageuka kumwangalia huyo docta, na huyo docta
alikuwa akinitizama wakati wote, na alionekana anatka kuniambia jambo, lakini
alikuwa akisubiria nitulie.
Docta huyu pamoja ya kuwa ni rafiki ya mume wangu, lakini
aliwahi kuwa rafiki yangu mpenzi, na huenda nikasema yeye ndiye aliyeniingiza
kwenye dunia ya mapenzi, na ilitarajiwa kuwa ndiye atakayenioa, hadi wazazi
wangu walifahamu hivyo, lakini haikuja kutokea hivyo, pindi nilipokutana na na
huyu mume wangu.
Ilivyotokea tunaweza kusema ni mipango ya mungu, maana
kipindi nipo na huyu docta , kwenye moja ya shughuli, nilikutana na huyu mume
wangu, ilikuwa ni usiku, na kipindi hicho nilikuwa najifunza funza kunywa,
japokuwa sikuwa mpenzi wa pombe, na aliyenifundidh kunywa na huyo huyo docta.
Nilikuwa nimekunywa kidogo, nikawa anjisikia vibaya, na
nilijuta kwanini nilikunywa, na muda huo nilikuwa natamani niondoke hapo, kwani
roho ilishachafuka, natamani kutapika, nikawa nimeenda chooni, na kuwaacha
docta na watu wengine.
Nilipokuwa natoka chooni, nikahisi kizungu zungu,na kama
asingelikuwa huyo jamaa kunidaka ningelidondoka vibaya kwenye sakafu,
‘Pole sana dada, ....’akanidaka na kunisaidia kusimama
vyema, lakini sikuweza, mwili ulikuwa hauna nguvu, na hapo hapo nikaanza
kutapika, na matapishi ya mwanzo yakaenda moja kwa moja kwenye nguo za huyo
jamaa.
‘Oooh...pole pole, inaonekana umelewa, wewe..oh, ..tulia
kidogo,....’akasema bila kujali kuwa nimemchafua, na hakujaribu kufanya lolote kwenye nguo yake
iliyokuwa imeloweshwa na matapishi yake, alichojali ni kunisaidia
mimi,....akanishika vyema, akichelea nisichafuke nay ale matapishi yaliyokuwa
kwenye nguo yake,....na kunisaidia hadi chooni, ilibidi aingie choo cha
wanawake ili niweze kujisafisha,..alipohakikisha nipo sawa, yeye akakimbilia
choo cha wanaume kujisafisha, nilijiskia vibaya sana.
Na hadi muda huo nilikuwa sijaweza kumtizama usoni, nilikuwa
nimejawa na aibu , kwani haijawahi kutokea hivyo, na mimi sipendagi kunywa
pombe, kwanza harufu yake siipendi, lakini ilibidi niwe nakunywa kidogo kwa
ajili ya kumrizisha rafiki yangu huyo docta, ambaye kila mara alikuwa
akinishinikiza ninywe angalau kidogo.
Hali ilipotulia nikatoka, kumbe huyu jamaa alikuwa hapo nje
akinisubiria, alikuwa keshamaliza kujisafisha, na kukausha nguo zake
usingeliweza kujua kuwa nilimchafua, na aliponiona nikitoka akanifuata pale
mlangoni, na kuniuliza.
‘Upo na nani maana naona hiyo hali unahitajia msaada...’akasema
huku akinisogelea, na sikutaka kuongea na mtu, nilichotaka ni kuondoka, na
kwenda nyumbani kulala.
‘Nipo na na...’nikasita kusema
‘Na mume wako off
course....’akamalizia na mimi nikakubali kwa kutikisa kichwa, ili nitimize
ule usemi wa kubali yaishe, ili aondoke zake, na mimi niende kumuaga docta kuwa
narejea nyumbani, na sikutaka yoyote afahamu hicho kilichotokea, yeye akasema;
‘Basi ni bora nikusaidia hadi kwa huyo mume wako,maana
unavyoonekana hujawa sawa, kwanini unakunywa pombe, wakati unaona
hazikupendi,.....achana na pombe,pombe zinawenyewe bwana....’akasema.
‘Sinywi tena....’nikasema na nikamtupia jicho huyo mtu, na
ilikuwa kama mshituko fulani , ni kama kuna kitu nilikihisi, lakini niliona ni
sababu ya pombe, maana mtu mwenyewe sifamhamu kwanini nihisi kitu kama hicho,
nikapotezea, na sikutaka kumwangalai tena machoni.
‘Samhani nikuulize, inakuwaje mume wako asijitokeze, kwani
umekaa huku muda, hajashutuka tu kukuona umechelewa ....?’akasema kama
kuniuliza, hata mimi nililiona hilo , lakini sikujali, na sikutaka huyo docta
afahamu kilichotokea.
‘Wenyewe wameshalewa, sizani kama hata wanatambua kuwa
nimechelewa....na nisingelipenda wanione kuwa nimetapika kwa ajili ya pombe,
wala usije ukawaambia hata hivyo nipo safi, haina haja yaw ewe kunisaidia
nashukuru kwa wema wako huo..na sitakunywa tena pombe, ....’nikasema.
‘Pole sana....mimi hata nilewe vipi sitaweza kumsahau
mwenzangu, ...’akasema.
‘Hongera ....’nikasema na nikatamani kumwangalia tena usoni,
nikawa kama nakumbuka kuiona hii sura mahali lakini sikuweza kukumbuka ni wapi,
na sikutaka kuwaza sana, nikapotezea.
‘Ina maana hunikumbuki mimi kabisa...?’ akaniuliza, na hapo
nikamwangalia tena, lakini sikuweza kumkumbuka kuwa ni nani, akili ilikuwa
haitaki kufikiria sana, na sikutaka kufanya hivyo nikasema;
‘Samahani kwakweli sikukumbuki kabisa,..zaidi ya kukufahamu
hapa kuwa wewe ni mtu mwema, ...tuliwahi kukutana wapi kabla?’ nikamuuliza ili
tu kumuonyesha kuwa namjali kwa fadhila zake hizo, lakini sikuwa nataka
kuongea...
‘Kweli ukiwa mtu wa chini, ..watu hawakukumbuki kabisa, wewe
sio wa kwanza kusema hawanikumbuki, lakini nafahamu ni kwanini...’akasema
hivyo, na nikamwangalia tena kwa makini, lakini akili iliona kuwa nilishawahi
kukutana na mtu kama huyo, na sio kukutana tu, lakini moyoni nilikuwa kaam
nimeguswa na hamasa, ...hisia nisizoweza kuzitambua,..niliona ukaribu wake kama
ni wa kawaida kwangu, ni kama mtu uliyemzoea na unapenda ukae naye karibu,
lakini kwa muda huo sikutaka niendelee kukaa hapo.
Samahani sana, labda kwa vila nipo katika hii hali, ndio
maana akili haifanyi kazi, na nisingelipenda kufkiria zaidi,labda unikumbushe
tu, kama hutojali...’nikasema na huku nikikwepa kumwangalia moja kwa moja usoni
na yeye akaniangalia na kusema;
‘Mimi ni mtoto wa mzee Mchapakazi, unakumbuka yule mzee,
aliyekuwa mlinzi na pia alikuwa akiwalimia
mashamba yenu na mimi nilikuwa nafika kumletea baba chakula, na siku moja
ukanisadia pesa za ada ya shule, kipindi mzee anaomba mkopo kwa baba yako, na
baba yako akakataa kumpa hizo pesa..umeshanisahau ehe...’akasema na mimi
nikainua kichwa kumwangalia na mdomo wangu ukabakia wazi kuonyesha mshangao,
nilitamani nimrukie nimkumbatie, lakini nikajizuia.
‘Oh, ndio wewe, mbona umebadilika hivyo...ooh,
nimeshakukumbuka, ..oh jamani , mimi nilikuwa kasichana kadogo kipindi kile, na
sikuwa napendelea sana kuwaangali watu hasa wanaume, na sikupendelea kuwakariri
watu hasa wanaume, nilitokea kuwachukia sana hasa baada ya lile tukio, na
nailijiskia vibaya sana kwa yale yaliyotokea, hata hivyo nilitamani nikuone tena,
lakini hukuja, nilishaahidi kukusaidia ..kukulipa fadhila ulizonitendea...’nikasema.
‘Iliniuma sana kumuona baba yangu anazalilishwa, na sikutaka
kurejea tena kwenu, na nikawa nafanya vibarua , waliponiachia jela, ...hadi
nikapata pesa za kujisomesha, unakumbuka nilifaulu, na kwasababu ya kufungwa
sikuweza kwenda sekondari, na nilipotoka nilimuomba baba tuhame hapo kijiji
kabisa, tukaenda kuishi kijiji cha mbali, huko nikaweza kujisomesha kwa kufanya
vibarua...Baba yangu aliumwa sana kutoka na hilo tukio hadi umauti
ulipomfika...’akasema kwa uchungu.
‘Oh, pole sana, ina
maana yule mzee alihsfariki...?’ nilishikwa na fadhaa, na nilitamani nimkaribie
ni mkumbatie kumuonyesha jinsi gani nilivyojisikia.
‘Alifariki......ndio mapenzi ya mungu, na siwezi kusema ni
kutokana na mshutuko kwa hayo yaliyotokea kwangu, baba alinipenda sana, na hali
yake hiyo ya kuumwa, ilitokana na pale alpofariki mama, na hutaamini, alikuwa
haishi kumkumbuka mama, na hicho ndicho kilichomfanya hali yake iwe vile....na
hakupenda mimi niteseke, ...’akasema.
‘Oh, jamani, poleni sana, sizani kama wazazi wangu
walifahamu hilo, kwa vile alikuwa mfanyakazi wao kwa muda mrefu wangeniambia,
na hata kufika kwenye msiba...’nikasema.
‘Alikataa kabisa, alisema hata akifariki, nisje kuja
kuwaambia...na ndivyo ilivyotokea, alizikwa na watu wachache, na wengi
hawakufahamu .....ndio hivyo, lakini mimi sikukata tamaa ya maisha, nikasonge
mbele, ....’akasema.
‘Sasa hivi unafanya kazi wapi?’ nikamuuliza.
‘Nipo hapa kwenye hii hoteli nabangaizabangaiza, nilipata
tenda ndogo hapa, ndio naifukuzia, ikiisha nakwenda sehemu nyingine, maisha
yanakwenda kidogo ninachokipata kinanisaidia.Ndio maisha sisi watu wa chini
kupata kazi inakuwa shida, na sipendi
kwenda kuwapigia watu magoti kuwa wanipe kazi, sitaki nizalilike kama
alivyozalilika baba yangu, mimi nimeona nijia iliyorahisi ni kujiajiri kwa njia
hii...’akasema na hapo nikamwangalia na kumbukumbu za nyuma zikanirejea...
***********
Kumbukumbu za nyuma nikiwa binti mdogo zikanirejea, maana
siku nilipomuona huyu mwanaume, kipindi hicho yeye ni mvulana mkubwa,
nilivutika naye sana, sijui ni kwanini, ila nakumbuka, kila mara alipokuwa
akija nyumbani kuonana na baba yake, nilikuwa nikimuona, na sikuwa naongea naye
sana, kutokana na hali ilivyokuwa wakati huo.
Lakini cha ajabu, nilikuwa nikimuwaza, na nilitamani sana
nimuone, nilitamani sana niwe naye karibu, na ilikuwa akifika nachukua kinywaji
au chakula nampelekea anakula kwa uficho,na ilipotokea hilo tukio, baba yake
akaacha kazi na kuondoka kabisa hapo kijijini, na sisi baadaye tukalihama na
kuja huku Dar, ambapo baba yangu alihamishia kampuni yake, na huko kijijini
tukawa hatufiki mara kwa mara.
Siku hiyo ikawa mara
nyingine kukutana naye na nilipomtupia jicho kwa mara nyingine, nikawa
nimemtambua vyema na ile hisia ya usichana ikaanza kunijia, nikabakia kumwangalia
na yeye akageuka kama anataka kuondoka, nami nikamwambia.
‘Kwanini
hukunitafuta...?’ nikamuuliza.
‘Kwanini nikutafute..ulitaka niendelee kuumia, maana mimi
nitasemaje kwako, ..hebu jishushe kwenye hali yangu, halafu uone ilivyokuwa
ngumu, nakumbuka niliwahi kuandika barua kuja kwako, lakini sikuwahi kupata
majibu...’akasema.
‘Ulindika barua kwangu ukampa nani..mbona sijawahi kuona
barua yako,...?’nikasema kwakweli sikuwahi kupata barua kutoka kwake, na
niliona kama ananitania tu.
‘Basi nahisi kuna mtu alikuwa akizipkea na kuzichana....’akasema
akitabsamu .
‘Kwanini usingelinipigia hata simu...?’ nikamuuliza
‘Nikupigie simu, simu hiyo ningeliipata wapi...anyway, hayo yameshapita na wewe una
mume wako, ...naona nisikupotezee muda, ...’akasema na kutaka kuondoka, mimi
nikamfuata na kumshika mkono.
‘Sikiliza, nataka tuonane tuongee, natamani zile siku
zirejee tena, mimi sijaolewa, na sisemi hivyo kwasababu kuwa nataka uwe
...mpenzi wangu, hapana mapenzi hayalazimishwi, ila ningelifurahia niweze
kukifanya kile nilichokuwa nimekiahidi moyoni,....unakumbuka ulivyoniokoa kwa
wale wabakaji,..sitasahau hilo kamwe, japokuwa fadhila zako ziligeuka kuwa
fadhila za punda, ...’ nikamwambia.
‘Usijali sana ndio ubinadamu ulivyo, hasa mnapokuwa kwenye
hadi tofauti, hadhi yetu hatuna maana, kabisa..hata uongee nini huwezi
kusikilizwa, sikuona ajabu kwa yale yaliyotokea, ila baba ndiye aliyeumia
sana,...ndio hivyo tena, ndio maisha, na nikuambia ukweli, sio mara ya kwanz
kukuona kwenye hi hoteli, na sikupenda nije nikusmbue....’akasema.
‘Umefanya vibaya sana, ungelifahamu nilivyokuwa nakuwaza...lakini
kafika mahali nikasema basi tena, mungu ndiye atakupeni yale yote mliyotutendea
wema wenu kwangu ni mkubwa sana, hasa wewe..hata bab yako, alinpenda
sana,..nilimuona kama baba yangu mkubwa...sikupenda kumuita babu, kama
walivyozoea wengine, mimi nilipenda kumuita baba mkubwa.....’nikasema.
‘Nashukuru kusikia hivyo, kumbe wewe ni tofauti kabisa na
wazazi wako, ...nashukuru sana, na pia nawashukuru wazazi wako, kwani pamoja na
hilo tukio lakini walitusaidia ...’akasema.
‘Mimi nilikutafuta sana, lakini sikutaka wazazi wangu
wafaahmu hilo, nilitaka kukulipa fadhila zako, niliahidi moyoni kuwa nikikuona
nitafanya lolote ninaloweza ili tu nihakikisha nimelipa fadhila zako, japo
kidogo....’nikamwambia na hapo kumbukumbu za tukio lile baya likanijia
kichwani, na huyu ndiye aliyeweza kunikoa, kutoka kwa wale vijana wahuni
waliotoka kunibaka, nikiwa natokea shule.
Ilionekana walikuwa wakinivizia siku nyingi, na siku hiyo
gari la baba lilichelewa kuja kunichukua, nikaamau kutembea na wenzangu, na kwa
vile shule ilikuwa mbali, wenzangu wakawa wametawanyika kila mmoja na njia
yake, ikafikia mahali nimebakia peke yangu, na ghafla wakaja vijana wanne,
wakanivamia.
Walinibeba juu kwa juu, hadi vichakani, na wakaanza kunivua
nguo, ukumbuke nilikuwa binti mdogo, japokuwa nilikuwa nimevunja ungo, lakini
sikuwa na mawao hayo kabisa, na sikujua ni kitu gani kinataka
kunitokea,..japokuwa nilifahamu ni kubakwa......na sikuwahi kuwa hilo linaweza
kutokea kwenye maisha yangu.
Nilijitahidi kupigana lakini sikuweza kufanya lolote, na
kabla hawajafanya lolote mara akaja kijana mmoja, akiwa na gongo akaanza
kuwapiga nalo, na wale vijana wakakimbia huku wakilaani kuwa watahakikisha
wananifanyia hivyo...
Sikuweza kuongea nililia hadi nyumbani, nikiwa nimechafuka,
na huyo kijana alinsiindikiza hadi nyumbani, nikawaahdithia wazazi wangu, na
wao haraka wakaifahamisha polizi na hawo vijana wakatafutwa lakini
hawakupatikana.
Cha ajabu wazazi pamoja na polisi wakamshkilia huyo kijana
kuwa anawafahamu hawo watu, na alitakiwa kuwataja, na aliposhindwa kuwataja,
wakamshikila na kesi ikamgeukia yeye, ..waansema walivyomuhoji, inaonekana
anafahamu hilo tukio na yeye alikuwa mwenza wao, japokuwa alikana kabisa.
Wakamshikilia na hata kumfungulia mashitaka, na yote hayo
wakati yanaendelea mimi nilikuwa sijafahamu, maana baada ay tukio hilo wazazi
wangu walinihamisha shule nikawa ansomea sehemu nyingine. Nilikuja kaupata
taarifa kuwa huyo kijana kafungwa, ..na wale waliofanya hivyo, mmojawapo
walipatikana na kusema kuwa huyo kijana alifahamu....alimsingizia hivyo,
kumkomoa.
Baba wa huyo kijana akawa anafika mara kwa mara kumomba baba
amsamehe kijana wake, lakini haikusaidia kitu, na alichoambulia ni kufukuzwa
kazi...hayo yote nilikuja kuyafahamu baadaye, na nilipofanua nikawaambia wazazi
wangu kama hawatamuachia huyo kijana nitajiua...
Wazazi wangu waliogopa, na baadaye wakaenda kuongea na
polisi na huyo kijana akaachiwa, na sikuweza kuwaona tena, kumbe walihama
kabisa kwenye hicho kijiji, na sisi tukawa tumeshahama hapo kijijini na kuja
kuanza maisha mapya huku mjini.
‘Kwakweli sitaweza kusahau wema wako huo, uliniokoa kwenye
janga, huenda ningelikufa, maana nilikuwa bado kasichana, na ile midume..mungu
wangu najaribu kuwaza, lazima ningelikufa, na wewe ukaweza kuniokoa, ..kweli
uliokoa amisha yangu...sijui nikulipe nini..lakini nitafanya jambo ambalo nina
iamani litakuja kukusaidia katika maisha yako....’nikasema.
‘Ile ni kawaida tu, mtu yoyote muadilifu angelifanya hivyo
hivyo, na haina haja, kulipwa kwa kitendo kama kile, na sizani kama kuna kitu
unaweza kunilipa kikazidi yale ya moyoni kwangu...’akasema na kuinama chini.
‘Una maana gani,..ya kuwa unanipenda au ?’ nikamuuliza.
‘Ndio maana mpaka leo sina rafiki wa kike, umekuwa ndani ya
moyo wangu miaka yote, na nimekuwa nikikuona kimawazo huku nikiomba mungu ije
iwe kweli..lakini zote hizo zilikuwa ni ndoto za Alinacha, toka lini mtoto wa
masikini akaweza kumpenda mtoto wa mfalme..inawezekana kweli,..kwahiyo hisia
zangu si chochote ni kujitesa tu...’akasema na mimi nikajikuta nikimwangalia
kwa macho ya huruma.
‘Sikiliza, ......mimi nataka tuonane, tuongee....usijishushe
kiasi hicho, kama kweli ulikuwa na mapenzi ya dhati ungelinitafuta, mapenzi y a
kweli hayajali uhali , umasikini au utajiri, mimi sio sawa na wazazi wangu, lakini
hata hivyo hakijaharibika kitu, tuwasiliane tuone jinsi gani tutasaidiana, hasa
kimaisha kwangu mimi nathamini sana maisha kuliko mapenzi, mapenzi....haypo
moyoni sana, na nilitokea kuwachukioa wanaume baada a lile tukio, sijui kwanini,...mimi
ninachotaka kukifanya ni kutimiza ahadi yangu...’nikasema.
‘Sawa nimekuelewa, nitakuachia wewe upendavyo...mimi mwezi
mzima nitakuwa hapa, .....kwahiyo tutakutana....’akasema na kuondoka, na mimi
nikarejea kule walipokuwepo docta na watu wengine, tulikuwa kwenye sherehe ya
kumbukumbu za kuzaliwa kwa mmoja wa majirani zetu.
‘Umechelewa wapi...’akaniuliza huyo docta , aliponiona
nimetokea huko chooni, na kipindi hicho alikuwa hajawa docta kamili,....ndio
alikuwa akimalizia masomo yake ili aweze kukamilika na kuwa docta,.....wazazi
wangu walimpenda sana, na walitaka yeye ndiye awe mume wangu...lakini moyo
wangu haukuwa na mapenzi naye, ...sijui ni kwasaabbu ya hiyo hali ya kuwachukia
wanaume.
‘Nilikuwa najisikia vibaya, na sasa nataka kuondoka...’nikasema.
‘Huwezi kuondoka sasa hivi, huoni ndio sherehe imeanza kunoga,..na
mimi ndio natakiwa nikurudishe nyumbani mwenyewe, utarudije peke yako, ukumbuke
mimi nilikuomba kwa wazazi wako na walinikabidhisha
kwa msharti kuwa nikulinde...wakasema nihakikisha unarejea nyumbani salama..’akasema.
‘Mimi sio mtoto mdogo, nafahamu nini ninachokifanya, kwani
siku zote nikiwa nimetoka kwenye shughuli kama hii narudishwa na nani...’nikasema kwa ukali.
‘Vipi kwani kumetokea nini, nakuona umebadilika ghafla, kuna
tatizo lolote?’ akaniuliza.
‘Kuna tatizo lolote!....unadiriki kuuliza hivyo, nimekaa
muda gani huko, ...hukudiriki hata kuja kuniangalia kama kuna tatizo lolote
limetokea,..kilichotokea huko sitaki hata kukuhadithia maana hakikuhusu, ila ni kutokana na mipombe yenu, sitaki tena
kunywa, hali imekuwa mbaya, na kama nisingelipata msaada sasa hivi ningelikuwa
hospitalini, bado unadiriki kuona kuwa unanijali...wewe endelea na sherehe,
wala usisumbuke kunipeleka nyumbani....’nikasema.
Toka siku hiyo tukawa hatuelewani na huyo docta, nikawa
anmjibi mkato mkato,hadi mwenyewe akagundua kuna jambo limetokea, lakini
sikumwambia lolote . Mimi kwa siri nikawa naonana na huyu mume wangu mara kwa
mara mpaka ikaka kugundulikana kwa wazazi kuwa nina mtu ninayekutana naye mara
kwa mara, na aliyekwenda kulalamika ni huyo docta.
Wazazi wangu walifany auchunguzi mpaka wakamgundua kuwa ni
nani huyo ninayekutana naye mara kwa mara, na kipindi hicho nimeshamsaidia hadi
akawa kafungua kampuni yake.
Siku moja wakanikalisha kikao wazazi wangu, walikuwa wamekasirika kweli kweli..
‘Hivi wewe una akili kweli,..hivi wewe hujaona wanaume,
..kama kweli nia yako ni kupata mwanaume wa kuja kukuoa, unakwenda kuwa rafiki
kwa yule mlalahoi, mtoto wa mlinzi wetu...bwana shamba, asiye fanana kabisa na
hadhi yako, mbona unataka kutuaibisha....kwanini unamkataa docta, msomi , familia
yao ni ya kiheshima, matajiri.....’akasema baba.
‘Baba mimi sio mtoto mdogo, na sina lengo la kuwaabisha,
mnakumbuka nilitaka kubakwa nikiwa kule kijijini, niliwaambia ni nani aliyeniokoa,
....mlifanya nini kwa huyo aliyeniokoa, ..badala yake mlikimbilia kumshika yeye
ati alikuwa anawafahamu hawo watu waliotaka kunibaka, mkafunga hata bila ya
mimi kujua, kwa vile tu ni mtoto wa masikini..iliniuma sana na niliahidi kuwa ipo
siku nikipata nafasi nitamsadia ili kulipa fadhila zangu kwake...’nikasema.
‘Hivi wewe utabadilika lini...sikiliza, kama sisi ni wazazi
wako, tunasema achana na huyo mtu, sisi ni wazazi wako tulijua ni nini
tunachokifanya, hukuona baada ya kumshika yeye na kumfunga, kijiji pale tuliogopewa,
hakuna hata mtu aliyewahi kuichezea familia yetu tena....sisi tulifahamu ni
nini tulichokifanya, kutoa fundisho kwa wengine....’akasema baba
‘Mtuoe fundisho kwa mtu asiye na kosa,...kunikoa kwake ndio
imekuwa taabu, kama asingelifanya hivyo nikabakwa, huenda ningelipoteza maisha
au kuambukizwa magonjwa, mngelisemaje, ndio fadhila za wema hizo,...hamuwezi
kujua ubaya huo unaweza ukawageukia nyie wenyewe siku moja, au ubaya utendwe
kwa wengine tu, ili iwe fundisho, ...hamjui kibao kinaweza kuwageukia nyie siku moja kwa tatizo jingine...msijione
kuwa nyie ni matajiri hamtaweza kupata shida...’nikasema kwa sauti ya huzuni na
mama akanionea huruma na kuniuliza
‘Sasa wewe ulikuwa unatakaje, tukae kimiya tu, wakati watoto
wahuni waliashaanza kuiingilia familia yetu, tulifanya vile kwa ajili ya
kuilinda famila yetu, na tulipofanya hivyo ilisaidia. Na baadaye tulimtoa, na
tukampa pesa za pole,...japokuwa mzazi wake alizikataa lakini baadaye
akazichukua....ile ni kawaida kwa mzazi yoyote anayetaka kulinda familia
yake...’akasema mama.
‘Mimi siwaelewi....kwanini mumuhukumu mtenda wema?, ndilo
swali langu, yeye hana kosa, alitenda kosa gani, kuniokoa ndio kosa lake, mimi siwaelewi...’nikasema.
‘Wewe hujui hayo, wewe huwafaahmu hawo watu, ..yule alikuwa
anawafahmu, lakini kwa vile alitishwa hakutaka kuwataja, kwanini hakutaka kuwataja,..kwasababu
alikuwa akiwaogopa, au alijua nini kilichotendeka, ....’akasema baba.
‘Baba mimi naona hatutafika popote kwa hili, ila nawaomba,
..kwa vile mimi ndiye niliyefanyiwa hilo, na namfahamu ni nani aliyenifanyia
wema kwa kuniokoa, mniache nimlipe fadhila zake, maana kwangu mimi ni
deni...niliahidi kuwa nitamlipa fadhila zake, ....’nikasema.
‘Kwahiyo unataka kumlipa fadhila gani...?’ akauliza mama.
‘Hilo niachieni mwenyewe....sijaja kuwaomba chochote kwenu
kwa ajili yake....’nikasema.
‘Achana na huyo mtu, kama unataka kumuona akiendelea na
maisha yake, achana naye, na kama unataka akaishie jela, endelea naye....hatuwezi
kukuona ukituzalilisha ....atapotea kama alivyoptea baba yake....’akasema baba.
‘Ina maana mnafahamu kuwa baba yake alifariki,,...?’
nikauliza kwa mshangao.
‘Tumeshakuambia achana na hiyo familia, vinginevyo utajua
kwanini hukutusikiliza....’akasema baba, na mimi moyoni nikasema; ‘mimi
hamnifahamu eeh, nikitaka kitu mpaka nikipate....’
NB: Kisa ndani ya kisa
WAZO LA LEO:
Utofauti wetu wa hali za kiuchumi usiwe ni tija ya kutokujali utu wa mtu, utu
wa mtu haununuliwi kwa pesa au mali, utajiri wako usiwe tiketi ya kudharau
wengine, na kuwaoana hawana thamani, ukifanya hivyo,hutakuwa na amani katika
maisha yako, kwani kilio cha hawo unaowatendea hivyo kitakuandama.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment