Mwanangu, hali ilivyo sasa, sio rahisi kwa walio wengi
kuchukua maamumuzi niliyoyachukua siku ile, kwani hata mimi baadaye nilihisi
nimefanya makosa makubwa katika maisha yangu, lakini sikuwa na jingine, kwani
nilitarajia kuwa mambo yatakuwa hivyo, lakini kila ulipangalo sio lazima liwe
hivyo. Wakati mwingine najuta nakusema huenda mimi ndiye nilifanya makosa,
labda ningechukua uamuaiz wa wengi, ingelisaidia, lakini ..hayo ni `huenda
tu.....’yameshapita.
Kwa ujumla mwanasheria alikuwa na sifa zote, alikuwa
mwanaume ambaye kila mwanamke angetamani kuishi naye, kitabia, kielimu, na hata
kisura, alikuwa amekamilika,..na mengineyo ambayo wanawake wengi wanayahitajia
kwa mwanaume,...na kwahiyo sikuona kwanini nimkatalie,..
Lakini kila mara nikikumbuka maneno haya ambayo kila
ninapotaka kuamua hivyo, maneno haya hunijia na kujirudia rudia kichwani;
‘Hilo niachie mimi,
kwa vile mimi ni baba mdogo wa mtoto, bado nina jukumu la kumlea huyo mtoto,
kama alikataa kabisa, mimi siwezi kumlazimisha japokuwa nilikuwa na nia hiyo,
ila nilikuwa nafanya hivyo kwa shinikizo la kaka, vinginevyo, ....sikuwa na
haja ya kuoa wake wawili kwasasa...’
‘Kumbe huyu mtu anafanya haya yote kwa vile, ananionea
huruma, au kwa vile ndugu yake kampa kazi hiyo, sio kwa mapenzii kama
anavyodai, ...’nikajikuta nikisema hayo moyoni, na hapo nikamtupia macho
mwanasheria ambaye alikuwa ka[piga mgoti, na pembeni yake yupo mwanangu, na
sauti za watu ziendelea kunisihi kuwa nikubaliane na hilo ombi.
Nikasimama, ...ni kabla sijasogeza mguu, nikageuka kuwaangalia wazazi wangu, na hapo nikakumbuka
jinsi gani nilivyongea nao jana yake nilipokwenda kuwapa taarifa hiyo kuwa
mwanasheria anataka kunioa, kama walivyo wazazi wengine, wao waliiona hiyo ni
faraja kwao na kwangu pia, hasa kipindi kama hiki ambacho sina kazi, na nina
mtoto wa kulea, kwani biashara ya duka ilikuwa imesimama kabisa,....wao, wakaniambia;
‘Binti yetu, Ingekuwa kipindi kile cha mfarakano
tungelikuambia, hiyo sio familia ya kwenda kuolewa,hata hivyo, hatuoni kwanini
ulipinga hilo, wakati ulishaamua mwenyewe kuwa sehemu ya hoyo familia,
unakumbuka tulivyokukataza usiwe na mahusiano ya marehemu mume wako, ukatuona
sisi hatuma maana, ...’akaanza kusema baba.
‘Baba lakini hayo yalishapita....’nikaanza kujitetea
‘Tumeshafahamu kuwa hayo yamepita, na kukumbusha hayo sio
kwamba tunakusimanga, hapa nia ni kukuonyesha kuwa , wewe huna haja ya kuogopa
kuolewa kwenye hiyo familia tena,hasa kwa kipindi kma hiki, na kwanini
tukukatalie kwa mtu kama huyo, ....yeye kama yeye kakamilika kuwa mwanaume
mwema kwako, na kwetu ni faraja kubwa, sisi tunaona ni vyema ukubali, na pili hatuoni kwanini
umkatae wakati mtoto wako anamtambua kama baba yake...’akasema mama
‘Hata mimi naona hivyo hivyo...., japokuwa toka awali,
sikuipenda hiyo familia, baada ya yule mume wako kukuharibia maisha yako, yule
ndiye alianza kukuonyesha njia isiyo sahihi, akaja kukupa ujauzito, lakini hayo
yalikuwa ya kale, muelekeo wa familia hiyo sasa ni mzuri, hakuna matatizo tena
kwenye hiyo familia maana mwanasheria sasa ndiye atakuwa kiongozi wa hiyo
familia, na wewe utakuwamwenza wake, kubali tu uolewe naye...maana hiyo ni
baada ya dhiki sasa imekuja faraja...’akasema baba.
‘Baba mimi nilikuja kusikiliza ushauri wenu, lakini
nilishaamua mwenyewe nini cha kufanya, ...nashukuruni sana kusiki kauli zenu,
kuwa mpo na mimi, na nawaomba kesho, kama mwanasheria atalileta hilo, muwe na
mimi kwa maamuzi hayo nitakayoyachukua.’nikawaambia wazazi wangu.
‘Binti yetu, wewe sasa ni mtu mnzima, hatuwezi kuingilia
maisha yako, ila kama watu wazima, tuliokuzidi umri tuna haki ya kukushauri
lile tunaloona ni la busara kwako na maisha yako ya baadaye....na kila mmoja
ana uoni wake, lakini uoni ulio na hekima ni ule unaoona jambo kwa upande wa
pili yake, na kwa mapana yake...na maamuzi mazima ya hili yapo kwako wewe
mwenyewe....’akasema baba na kabla hajaendelea mama akaongezea kwa kusema;
‘Kwanza jiulize kama kweli unampenda, pili je ataweza
kukidhi haja zako,mtaelewana, atakuwa karibu na mtoto wako, maana huyo ni mtoto
wako....japokuwa yeye ni baba yake mdogo, lakini wewe ndiye utakuwa na uchungu
na mtoto kuliko yeye..na la ziaidi ujue kuwa huyo ana mchumba wake, kwahiyo
uwezekano mkubwa wa kuolewa wawili au zaidi upo....’akaongezea mama, na mimi
moyoni nikasema hayo yote kwa mwanasheria nampa mia kwa mia.
‘Katika maisha ya binadamu kuwa wawili kuna umuhimu wake,
huwezi kujitenga kwa hilo, leo sisi tupo hai, lakini kesho na kesho kutwa
tunaweza tusiwepo,...Je utategemea majirani ndio waje kukusaidi aukikwama, je
kuna maswala ya ndani ambayo yanahitajia mke na mume, ina maana wewe utakuwa na
nguvu gani ya ajabu ya kuweza kuhimili hayo ....usijidanganye..’akaendelea
kuongea mama.
‘Na hilo alilosema mama yako ni muhimu sana, na tunakupa
hilo kama angalizo, kuwa mungu alivyotuumba katuumba mke na mume ili tuje
kusaidiana, unaweza ukazidiwa ndani , unahitaji hata maji, kama upo peke yako
atakupa nani hayo maji,..kuna mengi ambayo mke na mume wanahitajiana ambayo
wewe mwenyewe hutaweza kuyatatua...’akasema baba.
‘Mwanangu , hala hala,..usije ukaamua na kusema nitaweza
kuishi mwenyewe, na kufanya nipendavyo, kama ni mwanaume nitampata nikitaka,
...tabia hiyo haipo kwetu, nakuomba usije ukaniabisha kwa hilo, ukaja kufanya
mambo ya aibu,ya kukaribisha wanaume, leo huyu kesho yule, hilo hatutakuwa
radhi nalo, hata kama tumeshakufa...., tunachosema ni kuwa sisi sote ni
wanadamu tunahitajiana....kuishi mume na mke, ikishindikana basi ujue
imeshindikana kwa matakwa ya mungu sio kwa kujiamulia wewe mwenyewe...’akasema
mama
‘Unaweza ukasema ngoja nivute muda huenda nikapata mtu
mwingine, hilo sio wazo baya, kama unaona kuna kikwazo kwahilo, ninafahamu kuwa
mwanasheria alikuwa na mchumba wake, ambaye baadaye tulisikia uchumba huo
umekufa...je wakati anakuomba hilo, ulimuuliza kuhusu huyo mchumba wake, je
huyo mwanadada mliwahi kukaa mkaongea naye kuhusu yeye na mwanasheria, hayo pia
yana umuhimu wake, japokuwa uamuazi wa mwisho ni kati yako wewe na mwanasheria,
nyie wawili mkikubalina, mwanadada hana nguvu za kuwapinga,maana walishavunja
uchumba wao....’akasema baba.
Baba alipotamka hayo, nikawa kama mtu aliyezindukana na
kujikuta nawaza ni nini nifanye, sikuwa nimejiaminisha sana na maamuzi yangu
niliyokwisha kuyafikia, ...sikuwa nimemuamini sana mwanadada kwa kauli yake
hiyo ya kunishinikiza nikubali kuolewa na mwanasheria, lakini pia sikuona ni
kwanini nisikubali kuolewa na mwanasheria kwa vile kweli moyoni nimeshamkubali,
na ..lakini kauli ya mwanasheria wakati anaongea na mwanadada, iliniweka kubaya,..nikajikuta
nikisema;
‘Yote hayo yalishafanyika, na mwanadada mwenyewe ndiye
aliyekuja kunishauri nikubaliane na hilo, lakini hapo hapo nikawasikia
wakiongea, wakati tupo hospitalini kuwa yeye mwanadada yupo tayari kuolewa na mwanasheria..hapa
ndipo paliponiweka njia panda, nishindwe kuwa na maamuzi yenye uhakika, ndio
maana nikaamua kuja kwenu wazazi wangu, ili niweze kusikia kauli yenu...’ akawa
kama anauliza
‘Hiyo ipo wazi, kwa hali kama hiyo, inaonyesha kuwa
mwanasheria yupo njia panda, huenda wote anawapenda, na hapo alipo anashindwa,
amuoe yupi, na kwa hali kama hiyo wengine hubakia kusema mwenye kisu kikali
ndiye atakayekula nyama,...hali kama hiyo hutokea katika maswala ya ndoa, na
inapifika hali kama hiyo, maamuzi ya mwisho ni nyie ambao mtakuja kuishi
pamoja, sisi kama wazazi tumeshakuambia maoni yetu,..tunachoweza kukuhakikishia
hap ni kuwa tupo pamoja kwa vyovyote utakavyoamua,...’akasema baba.
‘Sawa wazazi wangu nimeshawasikia, na nawashukuru kuwa mpo
na mimi, na mpo tayari kwa lolote lile, kutokana na hilo, kwa hivi sasa
nawaombeni muendelee kukaa na mjukuu wenu huyu, nisingelipendea awe anakutana
mara kwa mara na baba yake mdogo, kabla hili swala halijamalizika, naogopa,
asitumiwe kama kisingizio, akaja kuumia kimawazo baadaye, ......’mwanamama
akawaambia wazazi
‘Huyu tena, mume wangu huyo, hawezi kuniacha, hapa
keshafika, ...usiwe na wasiwasi, nyumba ikiwa na watoto inakuwa na uhai, inachangamka,
...na ukimchukua huyu utatufanya tukae kama wakiwa, usiwe na wasi wasi na
hilo...’akasema mama
**********
Mwanamama alipokumbuka hayo mazungumzo akamwangalia
mwanasheria aliyekuwa bado kapiga magoti mbele yao, na akainua mkono na
kuiangalia ile pete, ambayo mwanasheria kaishikilia, ambayo alitakiwa kuipokea
kuashiria kukubali uchumba, .....halafu akaangalia ile pete ya marehemu mume
wake ambayo bado ipo kidoleni, akahisi mwili mzima ukimsisimuka.
Akageuka kumwangalia mwanadada, na mwanadada, amabya ehakuwa
tofauti na watu wengine, waliokuwa wakishangilia, na kumtaka akubali kuipokea
ile pete kutoka kwa mwanasheria, mwanamama aakzidi kushangaa, hasa alipoliona
lile tabasamu la mwanadada lililoashiria
kabisa kwua kweli yupo radhi na hilo, ...je ni kweli, yupo radhi na hilo, ...hapo
akasikia sauti ya mwanadada ikiongelea sikioni mwake,ikisema kumwambia
mwanasheria ....
‘Mpenzi wangu
nimefurahia kwa kauli yako hiyo, maana nilisubiri uzindukane tu, niisikie hiyo
kauli yako, kuwa upo tayari tuoane, na mimi nakutamkia moja moja, kuwa nipo
tayari kuolewa na wewe hata sasa hivi....’
Sauti hiyo ilikuwa kama upepo unapita, na hakutaka iendelee
kumzonga akili yake, akainamisha kichwa kumwangalia mwanasheria,...akainua
hatua ya pili, na akaongeza nyingina, sasa akawa karibu kabisa na pale
alipopiga magoti mwanasheria.
Kwanza kabisa mwanamama akamshika mtoto wake mkono na
kumuinua, akamsogeza pembeni, nikamuashiria aendee kukaa kwenye kiti, na yule
mtoto akawa kama anasita huku akimwangalia baba yake mdogo, na halafu
akamwangalia mama yake tena,, akatii amri ya mama yake na kwenda kukaa kwenye
kiti, huku akiwaangalia wazazi wake hawo kwa hamu kubwa.
Mwanamama akainamisha kichwa kumwangalia mwanasheria, na
hapo akahisi huruma ikimpenya moyoni, hakutaka kumuumiza huyu mtu, kama kweli
nia yake ni hivyo, lakini hakumwamini moja kwa moja kwa kauli yake ule,...lakini
ni lazima achukue hatua, ni lazima afanye linalowezekana kwa muda huo,
akaumuomba mungu wake, na akanyosha mkono kuichukua ile pete mkononi mwa
mwanasheria...
Kilichofuata hapo ilikuwa kama goli limefungwa, maana
nderemo vifijo na vigelege, vilikuwa vimetanda hewani, na wengi wakawa wanaimba
‘Kakubali, kaipokea,
kakubali kaipokea, kakubali kaipokea.....’
********.
Watu wakashangilia, na hata kusimama, wengine wakipiga
vigelegele, mimi nikatulia, nikisubiria hiyo hali ipite na mwanasheria akawa
keshasimama, akisubiria hatua nyingine ya kuvikana hizo pete, na wakati huo
alikuwa kaniangalia moja kwa moja usoni, akiwa kajawa na furaha, tabasamu la
nguvu likiwa limetanda usoni mwake, mimi nikakwepa kuangaliana naye usoni moja
kwa moja,nikawa upande nawaangalia watu na upande namwan galia yeye nikasema
kwa sauti.
Ile hali ya nderemo na vifijo ilipotulia, nikaomba niongee,
na watu wakatulia kimiya, kila mmoja akitaka kusikia kitu gani nataka
kuongea,....nikageuka na sasa tukawa tunaangalia moja kwa moja na mwanasheria,
ambaye bado alikuwa na tabasamu kubwa usoni, hakuweza kuificha furaha yake,
nikasema;
‘Nakushukuru sana mwanasheria kwa hili, inaonyesha jinsi
gani unavyinipenda, siwezi nikathibitisha ukweli wa nafsi yako, lakini kwa hili
hapa umathihirisha upendo wako, kwahiyo mimi kama mwanadamu, sina budi
kukushukuru sana, na nawashukuru sana wenzangu..hasa wale ambao kwa namna moja
au nyingine wamajikuta wakiwa jina hili la huzuni, jina lijulikanalo kama
Mjane....
‘Kwakweli jina hili ni mtihani, na unapopewa cheo hiki, ujue
wewe huna sifa tena, huna thamani tena, na kila mmoja,anakuangalai kwa jicho la
kuuliza, je, yupo salama, je atakwenda wapi, je ....ilimradi wewe huna amani
tena ....lakini yote hayo ni mapenzi ya mungu, inabidi tukubali huo ukweli,
kwani hakuna aliyependa kuitwa jina kama hilo....’nikatulia.
‘Mengi yametokea, na wengi wamajikuta wakiumia, na hata
wengine kupoteza maisha, siwezi kusema ni kwasababu ya wadhifa huu wa ujane,
hapana, maana ukweli umeshadhihiri, ila naweza kusema kuwa pamoja na haya, sio
vyema, wengine tukatumia nafasi hizi kuwadhulumu wenye haki zao,...kwa hilo
inabidi nawashukuru sana wazazi wangu, kwa kuwa name katika kipindi hicho
kigumu, bila wao ningejikuta ni mkiwa...ukifiwa na mume ambaye ulishamvika joho
la mzazi wako, unakuwa ni mkiwa, lakini wazazi wangu hawakunitupa.
‘Nawashukuru sana wazazi wangu wa kufikia, baba yngu wa
kufikia, alifikia hatua ya kutaka kuuwawa kwa ajili yangu, ...sitasahahu hilo,
na moyo wangu umempa nafasi ya ubaba, baba wa hiari, na mama wa hiari ambaye
kapitia maschungu wanayoyapata wanawake wengi dunia, .....mungu atamjalia an
ali yake itareeja kuwa kama ilivyokuwa....’nikatulia, kuwaangalia wazazi wangu
hawa wa hiari, ambao walichelewa kufika, na sasa walikuwa wameshakaa karibu na
walipokuwepo wazazi wangu.
‘Wanasema katu wema hauzi, mtenda wema wakati wote yupo na
neema za mungu, na nasema hili nikimwangalai mwanadada, huyu ni ndugu yangu wa
kweli, ambaye alinifaa wakati wote wa dhiki, nani angalidiriki kunisadia wakati
kama huo, na ilihali sina pesa tena, nimeshafirisika, lakini yeye hakujali
hayo, akabeba mzigo wote namshukuru sana ndugu yangu huyu wa hiari mwanadada,
na hili nalifanya kwa moyo safi, nawaomba mnielewe wote mliohudhuria hapa...’akasema
mwanamama
Mwanamama akaiangalai ile pete aliyopewa na mwanasheria na
badala ya kuweka kidole kama ilivyotarajia, akachukua ile pete kwenye na kuiina
juu, na kusema;
‘Mwanadada nakuomba uje hapa mbele....’akasema na mwanadada
akasita, na kwanza aaksimama na bila kujua afanye nini, lakini baadaye akainuka
na kufanya kama alivyoambiwa, akasogea hadi pale waliposimama wawili hawa, na
kumwangalia mwanamama kwa macho ya mshangao, na mwanamama, akainua ile pete na
kuielekeza kwa mwanadada na kusema;
‘Mwanadada kutokana na wema wako, ambao sitaweza kuulipa,
nakuomba,...ukubali pete hii kama makubaliano ya udugu wetu, na kwa moyo safi
nakuomba ukubali uchumba huo ili uje uolewe na mwanasheria, nafahamu unampenda
sana mwanasheria, na unanipenda sana mimi..., na mimi sitatenda fadhila, kwa
kuwa mchoyo kwa hili,...’nikasema huku mwanadada akitikisa kichwa kukataa,akainua
mikono na kuiweka kichwani kama mtu aliyekuwa hakutarajia hilo,
Llakini nikaiondoa ile mikono kichwani, na kumshika mkono
wake mmoja, na kuendelea kusema;
‘Kama kweli unanipenda, nakuomba ukubali hili, kubali huu
uchumba, ili uje uolewe na mwanasheria, na mimi nitakuwa dada yako wa kweli,
dada yako wa hiari....’akasema mwanamama na bila kupoteza muda, akachukua
kidole cha mwanadada na kukivalisha ile pete kidoleni kwa mwanadada....akachukua
mkono wa mwanasheria akawashikanisha, na baada ya kitambo cha wao kuangaliana,
wakakumbatiana, huku machozi yakiwalenga lenga.....
Kwanza watu walikaa kimiya, na mara minong’ono ikaanza, na
baadaye yakapigwa makofi japokuwa hayakuwa na nguvu...
******** MWISHO*********
Mwanangu huo ndio mkasa
wa maisha yangu....’akasema mama
‘Lakini
mbona.....’akataka kusema mtoto
‘Mwanangu nafahamu
mengi yametotokea ...kinyume na matarajio ya wengi, lakini yote yaliyokuja
kutokea baadaye, ni mipango ya mungu, huenda yametokea ili kuthibitisha ukweli
ulivyo.....Kijiji chetu kilanza kubadilika na kuwa na maendeleo kidogo , lakini
baada ya miaka kadhaa, ndio unaona eneo limavamiwa, wachimbaji wadogo wadogo
wakawa wanamiminika, na wenyeji ambao bado walikuwa hawajajifahamu wengi wakiwa
bado wamegubikwa na adui ujinga, mifarakano, ...na ubinafsi,...wakawa wanauza
maeneo yao kwa wageni.
Umoja ambayo ndio ngao
ilikuwa haipo kwao tena, kila mmoja yupo na ile hali ya
`changu..mimi,.langu.’na
adui akapanta mwanya.
‘Wanakijiji, hawakujua
neema waliyojaliwa nayo, hawakujua kuwa ardhi ile ni mali, na ndani yake kuna
mali , wakajikuta wakisogezwa kidogo kidogo na wageni, wao wakawa wanauza
maeneo yao na kusogezwa mbali na ardhi yao yenye mali, na baadaye ndio
wakaja wawekezaji, na kumiliki maeneo
karibu yote, tukafukuzwa mwanangu,....’akasema mama kwa uchungu
‘Wengi mpaka leo
wanamkumbuka mtaalamu licha ya ubaya wake....’akasema mama na mtoto aliyekwua
akihadithiwa hiki kisa akasema.
`Mama huoni kuwa huo
sasa ndio unaoitwa ukoloni mambo leo tunao-usoma kwenye vitabu, mama huo ni
ukoloni sio maendeleo...maana maendeleo hayo yanakuja kumilikiwa na
wachache kiujanja-ujanja.’
‘Ndio mwanangu kazi
kwenu, lakini yote yana mwisho, yanayotokea kwa wengine chanzo ni hiki hiki..ila
mwanangu nakushauri sana,someni mje mu-ijenge nchi yenu, mkizubaa, mtajikuta
mnatawaliwa kiujanja ujanja hivyo hivyo kama ulivyosema....’akasema mama
‘Sasa mama imekuwaje
tena, mbona baba mdogo hajamuoa mwanadada....?’ akauliza mtoto
‘Hayo yaliyotokea kwa
mwanasheria, huenda ndivyo ilivyopangwa iwe hivyo na mungu, ni kweli hawakuweza
kuoana,baada ya lile tukio siku ile mwanadada alikubali huo uchumba, lakini baadaye
wenyewe wakaona wasubiri kwanza, wasikimbilie kufunga ndoa.....
Mwanadada akaenda
kusoma, wakiwa wachumba, waliona wasubiri mpaka mwanadada amalize kusoma, na
mwenzake huku nyuma, akampa binti mmoja uja uzito. Inasemekana hiyo ilikuwa ni mbinu ya familia ya binti wa huyo
binti, kumtegea mwanasheria,..na mwanasheria bila kujua,akanasa, akampa huyo
binti uja uzito, mwanadada akapata taarifa akavunja uchumba.
Ile familia ya binti
ikashinikiza hadi mwanasheria akalazimika kufunga ndoa na huyo binti, ndio
wakawa mume na mke, hadi leo hii..
Mwanadada naye akiwa
abdo anasoma huko akapata mchumba huko huko, na wakaoana huko huko, wakarudi
wakiwa mke na mume,maisha ndivyo yalivyo,utegemeavyo iwe ianweza isiwe hivyo.
Mungu ni mkubwa
`Ndivyo hivyo mwanangu
kumbuka wema ndio kila kitu, tenda wema kila uwezevyo, maana wema katu
hauozi......’
************
Nawashukuruni sana wote
kwa kuwa pamoja nami kwenye kisa hiki, na mwisho wa kisa hiki ndio mwanzo wa
kisa kingine, je nimefikisha ujumbe, je niliyoandika yana maana katika jamii,
wewe ndiye mdau wa kuthibitisha hili, kama hayana maana basi niachieni mwenyewe
kama yana maana naomba mue wajumbe wa kuyafikisha haya kwa wengine, Mungu
awabariki sana.
WAZO LA LEO: Wema
unapotoweka, ukatili huchukua nafasi, na hili huanzia kwenye chuki ndogo ndogo
tu. Visasi , ubinafsi, na propaganda potofu za uzushi, huziteka nafsi za watu.
Tujitahidi sana, kuwa wema, tuwe waadilifu, na haki itolewe bila ubaguzi, ili
kuyakwepa haya, tusije tukaja kujijutia wakati tumeshachelewa.
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
KWA KWELI KISA HIKI KINAMAFUNZO MENGI SANA, KINAFURAHISHA, KINAHUZUNISHA PIA KINAFUNDISHA KUWA DHULMA SIO NJEMA PIA JINSI YA KUISHI NA WATU. KIKUBWA NI KUTENDA MEMA HUKU UKITARAJI MALIPO KWA MWENYEZI MUNGU KWANI YEYE NDIO WA MWANZO NA WA MWISHO. HONGERA SANA M3 HATA KUISHA KWAKE KIMEISHA VIZURI.
Pamoja sana jirani yangu
Post a Comment