Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, September 24, 2013

WEMA HAUOZI-67


Mwanangu, hali ilivyo sasa, sio rahisi kwa walio wengi kuchukua maamumuzi niliyoyachukua siku ile, kwani hata mimi baadaye nilihisi nimefanya makosa makubwa katika maisha yangu, lakini sikuwa na jingine, kwani nilitarajia kuwa mambo yatakuwa hivyo, lakini kila ulipangalo sio lazima liwe hivyo. Wakati mwingine najuta nakusema huenda mimi ndiye nilifanya makosa, labda ningechukua uamuaiz wa wengi, ingelisaidia, lakini ..hayo ni `huenda tu.....’yameshapita.

Kwa ujumla mwanasheria alikuwa na sifa zote, alikuwa mwanaume ambaye kila mwanamke angetamani kuishi naye, kitabia, kielimu, na hata kisura, alikuwa amekamilika,..na mengineyo ambayo wanawake wengi wanayahitajia kwa mwanaume,...na kwahiyo sikuona kwanini nimkatalie,..

Lakini kila mara nikikumbuka maneno haya ambayo kila ninapotaka kuamua hivyo, maneno haya hunijia na kujirudia rudia kichwani;

‘Hilo niachie mimi, kwa vile mimi ni baba mdogo wa mtoto, bado nina jukumu la kumlea huyo mtoto, kama alikataa kabisa, mimi siwezi kumlazimisha japokuwa nilikuwa na nia hiyo, ila nilikuwa nafanya hivyo kwa shinikizo la kaka, vinginevyo, ....sikuwa na haja ya kuoa wake wawili kwasasa...’

‘Kumbe huyu mtu anafanya haya yote kwa vile, ananionea huruma, au kwa vile ndugu yake kampa kazi hiyo, sio kwa mapenzii kama anavyodai, ...’nikajikuta nikisema hayo moyoni, na hapo nikamtupia macho mwanasheria ambaye alikuwa ka[piga mgoti, na pembeni yake yupo mwanangu, na sauti za watu ziendelea kunisihi kuwa nikubaliane na hilo ombi.

Nikasimama, ...ni kabla sijasogeza mguu, nikageuka  kuwaangalia wazazi wangu, na hapo nikakumbuka jinsi gani nilivyongea nao jana yake nilipokwenda kuwapa taarifa hiyo kuwa mwanasheria anataka kunioa, kama walivyo wazazi wengine, wao waliiona hiyo ni faraja kwao na kwangu pia, hasa kipindi kama hiki ambacho sina kazi, na nina mtoto wa kulea, kwani biashara ya duka ilikuwa imesimama kabisa,....wao, wakaniambia;

‘Binti yetu, Ingekuwa kipindi kile cha mfarakano tungelikuambia, hiyo sio familia ya kwenda kuolewa,hata hivyo, hatuoni kwanini ulipinga hilo, wakati ulishaamua mwenyewe kuwa sehemu ya hoyo familia, unakumbuka tulivyokukataza usiwe na mahusiano ya marehemu mume wako, ukatuona sisi hatuma maana, ...’akaanza kusema baba.

‘Baba lakini hayo yalishapita....’nikaanza kujitetea

‘Tumeshafahamu kuwa hayo yamepita, na kukumbusha hayo sio kwamba tunakusimanga, hapa nia ni kukuonyesha kuwa , wewe huna haja ya kuogopa kuolewa kwenye hiyo familia tena,hasa kwa kipindi kma hiki, na kwanini tukukatalie kwa mtu kama huyo, ....yeye kama yeye kakamilika kuwa mwanaume mwema kwako, na kwetu ni faraja kubwa, sisi tunaona  ni vyema ukubali, na pili hatuoni kwanini umkatae wakati mtoto wako anamtambua kama baba yake...’akasema mama

‘Hata mimi naona hivyo hivyo...., japokuwa toka awali, sikuipenda hiyo familia, baada ya yule mume wako kukuharibia maisha yako, yule ndiye alianza kukuonyesha njia isiyo sahihi, akaja kukupa ujauzito, lakini hayo yalikuwa ya kale, muelekeo wa familia hiyo sasa ni mzuri, hakuna matatizo tena kwenye hiyo familia maana mwanasheria sasa ndiye atakuwa kiongozi wa hiyo familia, na wewe utakuwamwenza wake, kubali tu uolewe naye...maana hiyo ni baada ya dhiki sasa imekuja faraja...’akasema baba.

‘Baba mimi nilikuja kusikiliza ushauri wenu, lakini nilishaamua mwenyewe nini cha kufanya, ...nashukuruni sana kusiki kauli zenu, kuwa mpo na mimi, na nawaomba kesho, kama mwanasheria atalileta hilo, muwe na mimi kwa maamuzi hayo nitakayoyachukua.’nikawaambia wazazi wangu.

‘Binti yetu, wewe sasa ni mtu mnzima, hatuwezi kuingilia maisha yako, ila kama watu wazima, tuliokuzidi umri tuna haki ya kukushauri lile tunaloona ni la busara kwako na maisha yako ya baadaye....na kila mmoja ana uoni wake, lakini uoni ulio na hekima ni ule unaoona jambo kwa upande wa pili yake, na kwa mapana yake...na maamuzi mazima ya hili yapo kwako wewe mwenyewe....’akasema baba na kabla hajaendelea mama akaongezea kwa kusema;

‘Kwanza jiulize kama kweli unampenda, pili je ataweza kukidhi haja zako,mtaelewana, atakuwa karibu na mtoto wako, maana huyo ni mtoto wako....japokuwa yeye ni baba yake mdogo, lakini wewe ndiye utakuwa na uchungu na mtoto kuliko yeye..na la ziaidi ujue kuwa huyo ana mchumba wake, kwahiyo uwezekano mkubwa wa kuolewa wawili au zaidi upo....’akaongezea mama, na mimi moyoni nikasema hayo yote kwa mwanasheria nampa mia kwa mia.

‘Katika maisha ya binadamu kuwa wawili kuna umuhimu wake, huwezi kujitenga kwa hilo, leo sisi tupo hai, lakini kesho na kesho kutwa tunaweza tusiwepo,...Je utategemea majirani ndio waje kukusaidi aukikwama, je kuna maswala ya ndani ambayo yanahitajia mke na mume, ina maana wewe utakuwa na nguvu gani ya ajabu ya kuweza kuhimili hayo ....usijidanganye..’akaendelea kuongea mama.

‘Na hilo alilosema mama yako ni muhimu sana, na tunakupa hilo kama angalizo, kuwa mungu alivyotuumba katuumba mke na mume ili tuje kusaidiana, unaweza ukazidiwa ndani , unahitaji hata maji, kama upo peke yako atakupa nani hayo maji,..kuna mengi ambayo mke na mume wanahitajiana ambayo wewe mwenyewe hutaweza kuyatatua...’akasema baba.

‘Mwanangu , hala hala,..usije ukaamua na kusema nitaweza kuishi mwenyewe, na kufanya nipendavyo, kama ni mwanaume nitampata nikitaka, ...tabia hiyo haipo kwetu, nakuomba usije ukaniabisha kwa hilo, ukaja kufanya mambo ya aibu,ya kukaribisha wanaume, leo huyu kesho yule, hilo hatutakuwa radhi nalo, hata kama tumeshakufa...., tunachosema ni kuwa sisi sote ni wanadamu tunahitajiana....kuishi mume na mke, ikishindikana basi ujue imeshindikana kwa matakwa ya mungu sio kwa kujiamulia wewe mwenyewe...’akasema mama

‘Unaweza ukasema ngoja nivute muda huenda nikapata mtu mwingine, hilo sio wazo baya, kama unaona kuna kikwazo kwahilo, ninafahamu kuwa mwanasheria alikuwa na mchumba wake, ambaye baadaye tulisikia uchumba huo umekufa...je wakati anakuomba hilo, ulimuuliza kuhusu huyo mchumba wake, je huyo mwanadada mliwahi kukaa mkaongea naye kuhusu yeye na mwanasheria, hayo pia yana umuhimu wake, japokuwa uamuazi wa mwisho ni kati yako wewe na mwanasheria, nyie wawili mkikubalina, mwanadada hana nguvu za kuwapinga,maana walishavunja uchumba wao....’akasema baba.

Baba alipotamka hayo, nikawa kama mtu aliyezindukana na kujikuta nawaza ni nini nifanye, sikuwa nimejiaminisha sana na maamuzi yangu niliyokwisha kuyafikia, ...sikuwa nimemuamini sana mwanadada kwa kauli yake hiyo ya kunishinikiza nikubali kuolewa na mwanasheria, lakini pia sikuona ni kwanini nisikubali kuolewa na mwanasheria kwa vile kweli moyoni nimeshamkubali, na ..lakini kauli ya mwanasheria wakati anaongea na mwanadada, iliniweka kubaya,..nikajikuta nikisema;

‘Yote hayo yalishafanyika, na mwanadada mwenyewe ndiye aliyekuja kunishauri nikubaliane na hilo, lakini hapo hapo nikawasikia wakiongea, wakati tupo hospitalini kuwa yeye mwanadada yupo tayari kuolewa na mwanasheria..hapa ndipo paliponiweka njia panda, nishindwe kuwa na maamuzi yenye uhakika, ndio maana nikaamua kuja kwenu wazazi wangu, ili niweze kusikia kauli yenu...’ akawa kama anauliza

‘Hiyo ipo wazi, kwa hali kama hiyo, inaonyesha kuwa mwanasheria yupo njia panda, huenda wote anawapenda, na hapo alipo anashindwa, amuoe yupi, na kwa hali kama hiyo wengine hubakia kusema mwenye kisu kikali ndiye atakayekula nyama,...hali kama hiyo hutokea katika maswala ya ndoa, na inapifika hali kama hiyo, maamuzi ya mwisho ni nyie ambao mtakuja kuishi pamoja, sisi kama wazazi tumeshakuambia maoni yetu,..tunachoweza kukuhakikishia hap ni kuwa tupo pamoja kwa vyovyote utakavyoamua,...’akasema baba.

‘Sawa wazazi wangu nimeshawasikia, na nawashukuru kuwa mpo na mimi, na mpo tayari kwa lolote lile, kutokana na hilo, kwa hivi sasa nawaombeni muendelee kukaa na mjukuu wenu huyu, nisingelipendea awe anakutana mara kwa mara na baba yake mdogo, kabla hili swala halijamalizika, naogopa, asitumiwe kama kisingizio, akaja kuumia kimawazo baadaye, ......’mwanamama akawaambia wazazi

‘Huyu tena, mume wangu huyo, hawezi kuniacha, hapa keshafika, ...usiwe na wasiwasi, nyumba ikiwa na watoto inakuwa na uhai, inachangamka, ...na ukimchukua huyu utatufanya tukae kama wakiwa, usiwe na wasi wasi na hilo...’akasema mama

                                      **********

Mwanamama alipokumbuka hayo mazungumzo akamwangalia mwanasheria aliyekuwa bado kapiga magoti mbele yao, na akainua mkono na kuiangalia ile pete, ambayo mwanasheria kaishikilia, ambayo alitakiwa kuipokea kuashiria kukubali uchumba, .....halafu akaangalia ile pete ya marehemu mume wake ambayo bado ipo kidoleni, akahisi mwili mzima ukimsisimuka.

Akageuka kumwangalia mwanadada, na mwanadada, amabya ehakuwa tofauti na watu wengine, waliokuwa wakishangilia, na kumtaka akubali kuipokea ile pete kutoka kwa mwanasheria, mwanamama aakzidi kushangaa, hasa alipoliona lile tabasamu la  mwanadada lililoashiria kabisa kwua kweli yupo radhi na hilo, ...je ni kweli, yupo radhi na hilo, ...hapo akasikia sauti ya mwanadada ikiongelea sikioni mwake,ikisema kumwambia mwanasheria ....

‘Mpenzi wangu nimefurahia kwa kauli yako hiyo, maana nilisubiri uzindukane tu, niisikie hiyo kauli yako, kuwa upo tayari tuoane, na mimi nakutamkia moja moja, kuwa nipo tayari kuolewa na wewe hata sasa hivi....’

Sauti hiyo ilikuwa kama upepo unapita, na hakutaka iendelee kumzonga akili yake, akainamisha kichwa kumwangalia mwanasheria,...akainua hatua ya pili, na akaongeza nyingina, sasa akawa karibu kabisa na pale alipopiga magoti mwanasheria.

Kwanza kabisa mwanamama akamshika mtoto wake mkono na kumuinua, akamsogeza pembeni, nikamuashiria aendee kukaa kwenye kiti, na yule mtoto akawa kama anasita huku akimwangalia baba yake mdogo, na halafu akamwangalia mama yake tena,, akatii amri ya mama yake na kwenda kukaa kwenye kiti, huku akiwaangalia wazazi wake hawo kwa hamu kubwa.

Mwanamama akainamisha kichwa kumwangalia mwanasheria, na hapo akahisi huruma ikimpenya moyoni, hakutaka kumuumiza huyu mtu, kama kweli nia yake ni hivyo, lakini hakumwamini moja kwa moja kwa kauli yake ule,...lakini ni lazima achukue hatua, ni lazima afanye linalowezekana kwa muda huo, akaumuomba mungu wake, na akanyosha mkono kuichukua ile pete mkononi mwa mwanasheria...

Kilichofuata hapo ilikuwa kama goli limefungwa, maana nderemo vifijo na vigelege, vilikuwa vimetanda hewani, na wengi wakawa wanaimba

‘Kakubali, kaipokea, kakubali kaipokea, kakubali kaipokea.....’

                                                      ********.

Watu wakashangilia, na hata kusimama, wengine wakipiga vigelegele, mimi nikatulia, nikisubiria hiyo hali ipite na mwanasheria akawa keshasimama, akisubiria hatua nyingine ya kuvikana hizo pete, na wakati huo alikuwa kaniangalia moja kwa moja usoni, akiwa kajawa na furaha, tabasamu la nguvu likiwa limetanda usoni mwake, mimi nikakwepa kuangaliana naye usoni moja kwa moja,nikawa upande nawaangalia watu na upande namwan galia yeye nikasema kwa sauti.

Ile hali ya nderemo na vifijo ilipotulia, nikaomba niongee, na watu wakatulia kimiya, kila mmoja akitaka kusikia kitu gani nataka kuongea,....nikageuka na sasa tukawa tunaangalia moja kwa moja na mwanasheria, ambaye bado alikuwa na tabasamu kubwa usoni, hakuweza kuificha furaha yake, nikasema;

‘Nakushukuru sana mwanasheria kwa hili, inaonyesha jinsi gani unavyinipenda, siwezi nikathibitisha ukweli wa nafsi yako, lakini kwa hili hapa umathihirisha upendo wako, kwahiyo mimi kama mwanadamu, sina budi kukushukuru sana, na nawashukuru sana wenzangu..hasa wale ambao kwa namna moja au nyingine wamajikuta wakiwa jina hili la huzuni, jina lijulikanalo kama Mjane....

‘Kwakweli jina hili ni mtihani, na unapopewa cheo hiki, ujue wewe huna sifa tena, huna thamani tena, na kila mmoja,anakuangalai kwa jicho la kuuliza, je, yupo salama, je atakwenda wapi, je ....ilimradi wewe huna amani tena ....lakini yote hayo ni mapenzi ya mungu, inabidi tukubali huo ukweli, kwani hakuna aliyependa kuitwa jina kama hilo....’nikatulia.

‘Mengi yametokea, na wengi wamajikuta wakiumia, na hata wengine kupoteza maisha, siwezi kusema ni kwasababu ya wadhifa huu wa ujane, hapana, maana ukweli umeshadhihiri, ila naweza kusema kuwa pamoja na haya, sio vyema, wengine tukatumia nafasi hizi kuwadhulumu wenye haki zao,...kwa hilo inabidi nawashukuru sana wazazi wangu, kwa kuwa name katika kipindi hicho kigumu, bila wao ningejikuta ni mkiwa...ukifiwa na mume ambaye ulishamvika joho la mzazi wako, unakuwa ni mkiwa, lakini wazazi wangu hawakunitupa.

‘Nawashukuru sana wazazi wangu wa kufikia, baba yngu wa kufikia, alifikia hatua ya kutaka kuuwawa kwa ajili yangu, ...sitasahahu hilo, na moyo wangu umempa nafasi ya ubaba, baba wa hiari, na mama wa hiari ambaye kapitia maschungu wanayoyapata wanawake wengi dunia, .....mungu atamjalia an ali yake itareeja kuwa kama ilivyokuwa....’nikatulia, kuwaangalia wazazi wangu hawa wa hiari, ambao walichelewa kufika, na sasa walikuwa wameshakaa karibu na walipokuwepo wazazi wangu.

‘Wanasema katu wema hauzi, mtenda wema wakati wote yupo na neema za mungu, na nasema hili nikimwangalai mwanadada, huyu ni ndugu yangu wa kweli, ambaye alinifaa wakati wote wa dhiki, nani angalidiriki kunisadia wakati kama huo, na ilihali sina pesa tena, nimeshafirisika, lakini yeye hakujali hayo, akabeba mzigo wote namshukuru sana ndugu yangu huyu wa hiari mwanadada, na hili nalifanya kwa moyo safi, nawaomba mnielewe wote mliohudhuria hapa...’akasema mwanamama

Mwanamama akaiangalai ile pete aliyopewa na mwanasheria na badala ya kuweka kidole kama ilivyotarajia, akachukua ile pete kwenye na kuiina juu, na kusema;

‘Mwanadada nakuomba uje hapa mbele....’akasema na mwanadada akasita, na kwanza aaksimama na bila kujua afanye nini, lakini baadaye akainuka na kufanya kama alivyoambiwa, akasogea hadi pale waliposimama wawili hawa, na kumwangalia mwanamama kwa macho ya mshangao, na mwanamama, akainua ile pete na kuielekeza kwa mwanadada na kusema;

‘Mwanadada kutokana na wema wako, ambao sitaweza kuulipa, nakuomba,...ukubali pete hii kama makubaliano ya udugu wetu, na kwa moyo safi nakuomba ukubali uchumba huo ili uje uolewe na mwanasheria, nafahamu unampenda sana mwanasheria, na unanipenda sana mimi..., na mimi sitatenda fadhila, kwa kuwa mchoyo kwa hili,...’nikasema huku mwanadada akitikisa kichwa kukataa,akainua mikono na kuiweka kichwani kama mtu aliyekuwa hakutarajia hilo,

Llakini nikaiondoa ile mikono kichwani, na kumshika mkono wake mmoja, na kuendelea kusema;

‘Kama kweli unanipenda, nakuomba ukubali hili, kubali huu uchumba, ili uje uolewe na mwanasheria, na mimi nitakuwa dada yako wa kweli, dada yako wa hiari....’akasema mwanamama na bila kupoteza muda, akachukua kidole cha mwanadada na kukivalisha ile pete kidoleni kwa mwanadada....akachukua mkono wa mwanasheria akawashikanisha, na baada ya kitambo cha wao kuangaliana, wakakumbatiana, huku machozi yakiwalenga lenga.....

Kwanza watu walikaa kimiya, na mara minong’ono ikaanza, na baadaye yakapigwa makofi japokuwa hayakuwa na nguvu...

                                 ********  MWISHO*********

Mwanangu huo ndio mkasa wa maisha yangu....’akasema mama

‘Lakini mbona.....’akataka kusema mtoto

‘Mwanangu nafahamu mengi yametotokea ...kinyume na matarajio ya wengi, lakini yote yaliyokuja kutokea baadaye, ni mipango ya mungu, huenda yametokea ili kuthibitisha ukweli ulivyo.....Kijiji chetu kilanza kubadilika na kuwa na maendeleo kidogo , lakini baada ya miaka kadhaa, ndio unaona eneo limavamiwa, wachimbaji wadogo wadogo wakawa wanamiminika, na wenyeji ambao bado walikuwa hawajajifahamu wengi wakiwa bado wamegubikwa na adui ujinga, mifarakano, ...na ubinafsi,...wakawa wanauza maeneo yao kwa wageni.

Umoja ambayo ndio ngao ilikuwa haipo kwao tena, kila mmoja yupo na ile hali ya 
`changu..mimi,.langu.’na adui akapanta mwanya.

‘Wanakijiji, hawakujua neema waliyojaliwa nayo, hawakujua kuwa ardhi ile ni mali, na ndani yake kuna mali , wakajikuta wakisogezwa kidogo kidogo na wageni, wao wakawa wanauza maeneo yao na kusogezwa mbali na ardhi yao yenye mali, na baadaye ndio wakaja  wawekezaji, na kumiliki maeneo karibu yote, tukafukuzwa mwanangu,....’akasema mama kwa uchungu

‘Wengi mpaka leo wanamkumbuka mtaalamu licha ya ubaya wake....’akasema mama na mtoto aliyekwua akihadithiwa hiki kisa akasema.

`Mama huoni kuwa huo sasa ndio unaoitwa ukoloni mambo leo tunao-usoma kwenye vitabu, mama huo ni ukoloni sio maendeleo...maana maendeleo hayo yanakuja kumilikiwa na wachache kiujanja-ujanja.’

‘Ndio mwanangu kazi kwenu, lakini yote yana mwisho, yanayotokea kwa wengine chanzo ni hiki hiki..ila mwanangu nakushauri sana,someni mje mu-ijenge nchi yenu, mkizubaa, mtajikuta mnatawaliwa kiujanja ujanja hivyo hivyo kama ulivyosema....’akasema mama

‘Sasa mama imekuwaje tena, mbona baba mdogo hajamuoa mwanadada....?’ akauliza mtoto

‘Hayo yaliyotokea kwa mwanasheria, huenda ndivyo ilivyopangwa iwe hivyo na mungu, ni kweli hawakuweza kuoana,baada ya lile tukio siku ile mwanadada alikubali huo uchumba, lakini baadaye wenyewe wakaona wasubiri kwanza, wasikimbilie kufunga ndoa.....

Mwanadada akaenda kusoma, wakiwa wachumba, waliona wasubiri mpaka mwanadada amalize kusoma, na mwenzake huku nyuma, akampa binti mmoja uja uzito. Inasemekana hiyo  ilikuwa ni mbinu ya familia ya binti wa huyo binti, kumtegea mwanasheria,..na mwanasheria bila kujua,akanasa, akampa huyo binti uja uzito, mwanadada akapata taarifa akavunja uchumba.
Ile familia ya binti ikashinikiza hadi mwanasheria akalazimika kufunga ndoa na huyo binti, ndio wakawa mume na mke, hadi leo hii..

Mwanadada naye akiwa abdo anasoma huko akapata mchumba huko huko, na wakaoana huko huko, wakarudi wakiwa mke na mume,maisha ndivyo yalivyo,utegemeavyo iwe ianweza isiwe hivyo. Mungu ni mkubwa

`Ndivyo hivyo mwanangu kumbuka wema ndio kila kitu, tenda wema kila uwezevyo, maana wema katu hauozi......’
                                             ************

 Nawashukuruni sana wote kwa kuwa pamoja nami kwenye kisa hiki, na mwisho wa kisa hiki ndio mwanzo wa kisa kingine, je nimefikisha ujumbe, je niliyoandika yana maana katika jamii, wewe ndiye mdau wa kuthibitisha hili, kama hayana maana basi niachieni mwenyewe kama yana maana naomba mue wajumbe wa kuyafikisha haya kwa wengine, Mungu awabariki sana.


WAZO LA LEO: Wema unapotoweka, ukatili huchukua nafasi, na hili huanzia kwenye chuki ndogo ndogo tu. Visasi , ubinafsi, na propaganda potofu za uzushi, huziteka nafsi za watu. Tujitahidi sana, kuwa wema, tuwe waadilifu, na haki itolewe bila ubaguzi, ili kuyakwepa haya, tusije tukaja kujijutia wakati tumeshachelewa. 


Ni mimi: emu-three

2 comments :

Amina K said...

KWA KWELI KISA HIKI KINAMAFUNZO MENGI SANA, KINAFURAHISHA, KINAHUZUNISHA PIA KINAFUNDISHA KUWA DHULMA SIO NJEMA PIA JINSI YA KUISHI NA WATU. KIKUBWA NI KUTENDA MEMA HUKU UKITARAJI MALIPO KWA MWENYEZI MUNGU KWANI YEYE NDIO WA MWANZO NA WA MWISHO. HONGERA SANA M3 HATA KUISHA KWAKE KIMEISHA VIZURI.

EDNA said...

Pamoja sana jirani yangu