‘Shemeji nataka uwe
mke wangu..’akasema huku akiwa kashika kiganga changu cha mkono huku akijaribu
kuniivika pete kidoleni...
Hayo yalikuwa maneno ya shemeji yangu, huku akiwa kanipigia
magoti, na alipoyamtamka, ilikuwa kama mtu kanipiga kisu kifuani, ilikuwa kama
kitu ambacho sikikutarajia, japokuwa nilikuwa nafahamu dhamira yake, na sikuwa
na jibu la haraka kumjibu japokuwa nilishajipanga kwa hilo, nilimwangalia
mchoni, na kwanza niliguna, kama mtu anayetabasamu, na pili kwa haraka nikautoa
mkono wangu na ile pete aliyokuwa kaishikilio mkononi akitaka kunivika ikadondoka chini, akaniangalia kwa huzuni, na
kusema;
‘Shemeji nina sema hili kutoka moyoni, na nitalisema hili
kwa yoyote yule, na hata ikibidi mbele ya wanafamilia, sitaogopa, kwani kweli ninakupenda
sana shemeji, naomba usiendeee kuniumiza moyo wangu, mimi mwenyewe nahisi kuwa
hata wewe mwenyewe unanipenda, hata kama hutaki kukubali hilo,...’akasema.
Nikamwangalia kwa muda, na kucheka, kicheko kidogo,
nikageuka kuangalia dirishani na mawazo yangu yakanipeleka mbali, kipindi kaka
yake na mimi tunachumbiana, ilikuwa kama hivi hivi, nilimgomea kabisa japokuwa
nilikuwa nampenda, kwasababu wazazi wangu walikuwa hamtaki, lakini hakuchoka, akawa
anahangaika kila mara kuniomba uchumba...
Nakumbuka sana, jinsi mume wangu alivyopata taabu ya
kunibembeleza, hadi siku moja nikaamua kumkubali na kuamua kuwa japokuwa wazazi
wangu hawampendi, lakini mimi nimpenda na mim ndiye nitakayeishi naye, na siku
hiyo nilipomkubalia, iliyokuwa siku ya furaha sana kwangu na kwa mume wangu,
hatukutaka kuachana...lakini ilishapita, na sasa imebakia kumbukumbu tu, na
sitegemei siku kama kutokea tena, kwani ule ulikuwa ni ujana, na sasa akili
yangu inatakiwa kuyatafakari haya kwa makini kabla ya kusema `ndio’.
‘Hilo niachie mimi,
kwa vile mimi ni baba mdogo wa mtoto, bado nina jukumu la kumlea huyo mtoto,
kama alikataa kabisa, mimi siwezi kumlazimisha japokuwa nilikuwa na nia hiyo,
ila nilikuwa nafanya hivyo kwa shinikizo la kaka, vinginevyo, ....sikuwa na
haja ya kuoa wake wawili kwasasa...’
Haya maneno yalinijia akilini, na kuanza kuwaza, huyu
shemeji ana mipango gani na mimi, je ina maana mimi sikuelewa hiyo kauli
alipomtamkia mwanadada.Hapana, ...maneno haya yanaeleweka, siwezi ..hapana
siwezi...
Nikageuka bila kujali kuwa shemeji alikuwa bado kapiga
magoti pale chini, na sikusumbuka kumwambia ainuke, nikainua mguu hatua moja
mbili, kutembea kuelekea mlangoni, nikafika na kuufungua mlango, nikageuka
kumwangalia huyo shemeji yangu na hapo hapo akili ikaninijia nikasema;
‘Shemeji usijitese kwangu, nafahamu sana kuwa hizo ni hisia za
kimwili na hasa wanapokutana mke na mume, na wakati mwingine ni ushawishi tu wa
kiibilisi, na usipoweza kumshinda ibilisi atakuchezea nafsi yako, ukajikuta
ukitenda jambo ambalo utakuja kulijutia baadaye, naomba tumpige vita huyu
ibilisi,...nakuomba utilize kichwa chako na uangalia maisha yako ya mbeleni...’nikasema
na yeye akaniangalia kwa muda bila kusema neno, akawa kama haamini maneno hayo
yametoka kwangu.
Mimi niligeuka mara moja kumtupia jicho, na kwa haraka
nikaangalia mbele, sikutaka tuangaliane tena moja kwa moja usoni, nikawa
nimeangalia dirishani na kumpa yeye mgongo, kumbe alishasimama na akanisogelea,
na mimi nikasogea pembeni na kusema;
‘Shemji achana na hayo...acha kabisa, usitake kunifanya
niongee yasiyotakiwa, nakushukuru kwa moyo wako huo wa kumjali mtoto, na sitaki
uendelee kubeba jukumu kwa kisingizio cha yeye, ukawa unautesa moyo wako kwa kubeba
majukumu ambayo sio stahili yako, mimi nimekuelewa...na sitakulaumu kwa
hilo....’nikasema
`Shemeji...sio kwamba.. , ‘ akataka kujitetea mimi
nikaendelea kuongea
‘Mimi ni mtu mnzima, itakuwa natenda kosa kama na mimi nitachukua mwanya huo wa
kisingizio cha mtoto, ili eti wewe unioe
mimi, ..., hapana, hilo limeshapita na naomba lisije kurudia tena..’nikasema
huku nikiangalia ile pete ambayo alikuwa kashikilia mkononi.
‘ Shemeji tatizo
lako, huamini kuwa ninayoyasema yanatoka moyoni mwangu, sitanii, ...hujui jinsi
gani ninapata shida, ..hujui tu, wakati mwingine nabaki kuangalia picha yako,
nikiomba iwe kweli uwe karibu yangu, lakini nashindwa kukulazimisha maana wewe
ni shemeji yangu, wewe ni mtu ninyekuheshimu sana, na sitaki nikufanye kama
wasichana wengine..nataka twende kiheshima ..sijiu nifanye nini ili
unielewe...’akasema
‘Mimi nimeshakuelewa shemeji , mimi sio mtoto mdogo,
kinachokusumbua hapo ni tamaa za nafsi yako, na usipoangalia utajikuta kwenye
wakati mgumu, na utawaumiza wengine hasa mwanadada, na matokea yake unaweza
ukakosa vyote, ...nakuomba uwe na maamuzi sahihi,mimi sio waakti wako kwa sasa,,
....wakati wako kwa sasa ni mwanadada fungeni ndoa mtulie...’nikasema
‘Shemeji, hilo nimeshaongea na mwanadada halina shida...’akawaa
anongea kama anataka kulia, ilikuwa sauti ya masikitiko ya kukata tamaa, na
mimi sikujali nikasema
‘Huo ndio msimamo wangu,... ninawatakia kila-laheri, na nitafurahi
sana siku hiyo ikifika...’nikasema lakini sauti yangu ilionyesha unyonge, na
yeye akanisogelea, na safari hii sikusogea nikatulia, akaweka mkono wake,
kwenye kiganja change tena na kuinua mkono wangu na kiganja kile akawa
anakipeleka mdomono kuubusu mkono wangu.
Nikautoa mkono wangu kwa haraka na y eye akawa kama
anaulizimisha, tukawa tunavutana na mara nikasikia mlango ukigongwa, nakageuka
kwa haraka na kuangalia kule mlangoni, na yeye akawa kaushikilia mkono wangu
akiwa anataka kunivika ile pete na mlango ukafunguka, akaingia mwanadada akiwa
kashikilia makabrsaha, kuashiria kuwa anatoka huko mahakamani
********
Mwanadada alipoingia akatutupia macho, na kujifanya kama
hajali, akapitiliza hadi kwenye sofa, na sisi tulikuwa tumesimama vile vile, na
mkono wake mwanasheria ulikuwa umshikilia kiganja changu na kwa haraka
nikauvuta na kujibaragua, na mwanasheria akawa bado kasimama akimwangalia
mwanadada.
‘Vipi nimewaingilia nini, maana naona mumesimama na
mnaonekana mpo kwenye jambo muhimu, kama nimeingilia kati naweza kutoka ...’akasema
mwanadada akisimama,
‘Hapana mdogo wangu...ni utani wa shemeji yako, hajui mimi
ni mkubwa kwake, japokuwa kanizidi umri, mimi ni mkubwa kwake, kwa vile
niliwahi kuolewa na kaka yake, kwahiyo anahitajika aniheshimu, lakini bado
analeta utani wa kitoto...’nikasema huku nikielekea kwenye jokofu kumletea
mwanadada kinywaji.
‘Hahaha....eti yeye ni mkubwa kwangu, wakati nilimuona
akikua...’akasema shemeji na mimi sikujali kauli yake hiyo nikaelekea kwenye
jokofu na mwanadada akasema;
‘Kama ulijua vile dada, maana hapa nina kiu, na kiu hiyo
inatulizwa na kinywaji chako,sijui nitafanyaje nikiondoka nitakuwa nimekosa
kitu muhimu sana....’akasema.
‘Nichukue niwe mfanyakazi wako wa ndani...’nikasema na
tukacheka, na kipindi hicho mwanasheria alikuwa bado kasimama na alionekana
kutahayari zaidi, na hakuweza kusema neno tena, akagueuka na kuelekea dirishani na kusimama
hapo akitupa mgongoi, nilimuonea huruma sana, lakini niliona iwe hivyo, na
hakuna kitakachobadili nafsi yangu.
‘Haya niambie dada kuna habari gani muhimu huko?’ nikamuuliza
mwanadada, na mwanadada ambaye alikuwa akinywa kile kinywaji, akageuka kwanza
kumwangalia mwanasheria na kunionyeshea ishara ambayo sikujua ana maana gani
mimi nikatikisa kichwa kama kumkubalia, nikamuona akitabsamu na kunionyeshea
kidole cha gumba, kama kuniap heko, sikuelewa kabisa ana maana gani.
Mwanadada akamaliza kunywa kinywaji chake, na halafu
akaniangalia, wakati nachukua ile gilasi, akawa kama kapitiwa na wimbi la
huzuni usoni, na hiyo hali ya mabadiliko ikawa inanipa mawazo, kuna nini
kiliendelea kati yao wawili, na nisingeliweza kumuuliza hilo swali kwa wakati
huo, nikasema yote ni heri, vyovyote iwavyo ninatakiw aniwe na msimamo..
Mwanadada akachukua
moja ya makabrsha yake kutoka kwenye mkoba wake, na kuanza kuyafungua, akasema;
‘Mwanasheria, sogea hapa, maana haya mambo tunatakiwa
tushirikiane, haya sasa yanakugusa haat wewe maana wewe unashikilia jahazi
hili, wewe sio asimu tena, ni muhumi sana, na pia ukumbuke kuwa wewe ndiye
uliyekuwa umeandikishwa kwenye hati miliki za nyumba na duka ...’akasema mwanadada,
na mwanasheria akageuka na kutuangalia, kwanza alikuwa kama anasita halafu
akahema kwa nguvu kama vil mtu anaye toa hewa iliyokuwa imemjaa mwiili, halafu
akawa anakuja upande tuliokuwa tumekaa, na mimi nikasimama, kumpisha akae aribu
na mwanadada, nikachukua stuli na kukaa mbele yao katikati kulikuwa na meza,
ambayo mwanadada alikuwa kaweka makabrasha yake, kwahiyo hapo nilipokuwa
nimekaa, nilikuwa nawatizama moja kwa moja usoni.
‘Sasa ni hivi, hakimu aliniita, pamoja na kunifafanulie
mengi kutokana na ile hukumu, kwamba yule jamaa anakula mvua nyingi, ni kama
kifungu cha maisha, maana na ule umri, hadi kifungo hicho kiishe, atakuwa keshajifia,...si
jambo la kufurahia lakini ndivyo sheria ilivyo, ukitenda kosa, likathihiri,
utahukumiwa, hata kama wewe unaona ulikuwa na nia njema....’akasema mwanadada.
‘Kiukweli namuonea sana huruma...’akasema mwanadada.
‘Na hakimu je, hakumuonea huruma..?’ nikamuuliza mwanadada,
na mwanadada akacheka, na kusema;
‘Hakimu alimuonea
huruma na katika hukumu yake, alitoa angalizo kuwa huyo mtu ni mtu muhimu sana,
kwani anafahamu mengi ambayo yakitumiwa yanaweza kusaidia jamii, kwa vile ni
mtaalamu, na hakusema utaalamu wa mambo ya kishirikina, hapana alikuwa
akimaanisha kuwa huyo jamaa ni mtaalamu wa ujuzi mbali mbali...’akasema
mwanadada.
‘Yule mtu kiukweli kajaliwa kipaji cha kuzaliwa, anafahamu
ujenzi, useremala, uwashi,umakenika,..udakitari,...uhandisi, na mambo a
kumputa. Unajua kule kwenye handaki lake alitengeneza kumputa iliyokuwa
ikionyesha mambo yanayofanyika huku kijijini, na akawa anahifadhi kumbukumbu za
matukio mengi yaliyotokea hapa kijijini , ambayo pia yalikuja kutusaidia sana
kwenye ushahidi wetu...’akasema mwanadada.
‘Aliweza kubuni mtandao amabo aliweka tafiti zake, na humo
alibainsiha kuwa ardhi hii ya kijiji ina madini...kwahiyo hayo aliyokuwa
akisema kuwa eneo hili lote limetanda mali asili kama madini, hakuwa akiyaongea
kama kujitetea, aliweka hata tafiti zake alizofanya kwenye huo mtandao wake...na
ndio maana alitaka kama ingeliwezekana akawafukuza watu wote na kumiliki eneo
lote hili...lakini zilikuwa ni ndoto za Alinacha, kwani badala ya kutumia ujuzi
wake huo vyema, akajitambulisha kwa serikali, yeye akatawaliwa na tamaa za
kibinafsi..’akasema mwanadada.
‘Je ni kweli kuwa eneo hili lina madini....?’ akauliza
mwanamama, na mwanadada akaendelea kuongea bila kujibu hilo swali moja kwa
moja.
‘Hakimu alisema huyu mtu atumiwe, ili utaalamu wake uje
usaidie, kama kweli kuna madini, basi asaidiane na serkali, na wataalamu wa
serikali watakuja kuhakiki hilo. Lakini cha ajabu jamaa yetu huyo alikakataa ,
kata kata, kasema yeye ni mfungwa, sio mtaalamu tena, na akasema kuanzia siku
anaanza kutumikia kifungo, hataki mtu amuulize chochote kuhusuiana na utaalamu wake wowote ule,..anadai kuwa jamii
imemusaliti, kwani alijitolea kwa ajili yao, lakini haikumuelewa, kwahiyo
hataki tena urafiki na jamii, yeye kwasasa sio mtu wa duniani tena...’akasema
mwanadada.
‘Kwanini alisema hivyo kuwa yeye sio mtu wa dunia tena?’
akauliza mwanamama
‘Keshachanganyikiwa, na wasipomchunga vyema atakuja kujiua..’akasema
mwanasheria kwa mara ya kwanza kwani muda mwingi alikuwa katulia akisoma ile
hukumu, na ilionyesha kuwa keshamaliza kuisoma, na akawa ananiangalia usoni, na
mimi nikainama chini, kama vile naangalia yale makabrasha
‘Ni kweli hilo limeonekana, na ndio maana kwanza atakuwa
katika usimamizi maalumu, na ikishindikana atapelekwa kwenye jela ya watu wanye
matatizo ya akili...hakimu katoa taarifa hiyo kwa wahusika,...natumai
watamchunga vyema’akasema mwanadada, kukatulia kidogo na mwanadada akafungua
kabrasha jingine, ambalo alikuwa hajalifungua na kusema;
‘Sasa kuna mambo ya mali iliyopatikana kwenye hilo handaki
lake,mali yote inataifishwa, kisheria,
maana madini aliyokuwa nayo kayapata kwa njia isiyo halali, ni mali ya uma, ni
mali na serikali inayo jukumu la kuichukua kwa masilahi ya uma. Inatkiw aiwe
hivyo, kama kuna mtu kaiba, kachukua mali za serkali, na ikathibitishwa mali
zake zote hutaifishwa, ....’akasema mwanadada.
‘Angalieni mali za serkali zilizokuwepo kabla, mashirika na
viwanda,kuna watu wachache waliiba, wakatumia mali hizo vibaya, kwa masilahi
yao,...na hawajaulizwa, kama alikuwa kiongozi msimamizi hadi kampuni au kiwanda
hicho kinakufa, ilitakiwa aulizwe, awajibishwe, na wachunguze mali zake, na
ikibainika kuwa yeye ndiye kasababisha hayo mali zake zote zinastahili
kutaifishwa...je hayo sasa hivi yanafanyika...’akasema mwanasheria, na akawa
kama anauliza.
‘Ndio hivyo, hayo ni ya serikali tuangalia kesi yetu....’akasema
mwanadada, na mwanasheria akawa kama anatka kuongea jambo, lakini mwanadada
akasema;
‘Kwahiyo mali zote alizolimbikiza huyu jamaa zimetaifishwa
na serikali, zitauzwa, na kitakachopatikana kitafidia wale wote walioathirika
na mpango wake huo, ikiwemo kumpeleka mama mkunga India , ambapo atakwenda
kufanyiwa upasuaji na kurekebisha ngozi yake, hasa ya upande wa tumboni, kwani
umekunjamana na kuvuta utumbo..ukimuona sehemu hiyo utaogapa...’akasema
mwanadada.
‘Pesa hiyo itawasaidia pia kuwafidia wale wote walipoteza
vijana wao, kujenga nyumba ya mama mkunga na mume wake, kulipia gharama za hiyo
kesi, na wewe mwanamama utapata kifuta jasho chako,...’akasema mwanadada.
‘Na kama nilivyowaambia gharama zote za kesi hii zitalipwa
na hawo wakosaji, na mimi nitalipwa gharama zangu zote kwa pesa hiyo hiyo, na
pesa iliyobakia itasaidia kuendeleza kijiji, hasa katika utafiti huo wa kuweza
kuhakikisha mali asili ya kijiji, inabakia kwa manufaa ya kijiji....’akasema
mwanadada.
‘Una uhakika na hayo kweli...?’ akauliza mwanamama.
‘Uhakika kwa vipi?’ akauliza mwanadada.
‘Kuwa kweli hayo yatafanyika maana mimi naona itakuja kuwa
kama alivyosema huyo mtaalamu, watakuja wanaoitwa wawekezaji na mali yote hiyo
itahamishwa kinyemela kwenda nje, na huenda isije kusaidia lolote kwa masilahi
ya wanakijiji...’akasema mwanamama.
‘Hakimu aliweka hayo kwenye maandishi kuwa ifanyike hivyo
kwa masilahi ya kijiji, sasa inapofika kwenye utekelezaji sio kazi yake tena,
hiyo ni kazi ya serikali, na serikali itaweza kulifanikisha hilo kama
kutakuwepo na viongozi wa kijiji wataoweza kusimamia hayo kwa masilahi ya
kijiji chao, cha muhimu ni kuwezesha uongozi wa wenye masilahi ya kijiji,
wazalendo wa kiukweli, na wanaojua uongozi, na hapo ninazungumzia viongozi
waliokwenda shule, ili hayo yafanikiwe, ni kazi yenu mwanasheria, maana hiki ni
kijiji chenu..’akasema mwanadada.
‘Lakini kijiji kama kijiji, hakihitaji sana kiongozi
aliyekwenda sana shule...’akasema mwanamama.
‘Utapozungumzia kazi za utaalamu, kama mipango ya kijiji,
mapato na matumizi , huwezi kuweka kiongozi kwa vile ni mtu wa heshima
tu,...ndio atakuwepo mjumbe, mtu anayeheshimika, ambaye anaweza kusimamia,
lakini ni lazima awe na timu ya wataalamu, ...na hao wanaweza kujitolea, mfano
kwenye kijiji, anaishi muhasibu, mtu wa uchumi, dakitari, hawo wanaweza kuwepo
kwenye timu ya uongozi, sio lazima wawe wameajiriwa moja kwa moja na kijiji,
hapana, ...wao wanatakiw kujitolea kwa masilahi ya kijiji chao, kumsaidia
mjumbe...huo ndio utamaduni wetu ...’akasema mwanasheria.
‘Ni kweli mwanasheria, ndio maana ningelipenda wewe uwepo
kwenye hiyo timu ya kijiji, maana umekuwepo, na umeliona hili, na umeyasikia haya,
ambayo yamebainishwa kisheria, na utaweza kulitetea hili kisheria, ukiondoka na
kwenda kuishi sehemu nyingine, ...kijiji chenu kitadhulumiwa...’akasema
mwanadada.
‘Hayo tutaona mbele kwa mbele labda nije nigombee ubunge ili
niweze kuyawezesha hayo, lakini mimi sipendi kazi ya kisiasa...sijui, hayo ni
mambo ya baadaye, kwasababu gani, hiki kijiji na kifahamu sana, kuna watu
wagumu sana kwenye eno letu, kuna watu wabinafsi, kuwa watu wametawaliwa na
mambo ya kishirikana, sasa hayo yote yanatakiwa kusafishwa...ni kazi ya muda
mrefu...’akasema mwanasheria.
‘Ni kazi kweli...lakini kila jambo huanza kidogo kidogo, na
kukiwa na mipango endelevuu yenye tija,mimi nina imani elimu itasaidia, nina
imani kizazi kijacho kitakuja kuleta mabadiliko makubwa....’akasema mwanasheria.
‘Haya ngojeni tuone....’akasema mwanamama akimwangalia
mwanadada ambaye alikuwa akiangalia ile pete aliyokuwa kashikilia mwanasheria,
na mwanasheria alipogundua hilo akaiinua na kuiangalia akawa anataka kusema
neno, lakini mwanamama akadakia na kusema;
‘Napenda nichukue nafasi hii kuwashukuruni nyote, na
nilipanga mimi na wazazi wangu tufanye kishereha kidogo cha kifamilia, cha
kuwashukuru kwa yote mliyotufanyia, nashindwa hata kuelezea jinsi gani
ninavyojisikia....naomba kesho tuifanye hiyo shughuli, kama mtakuwa na nafasi,
...’akasema mwanamama.
‘Mimi sina shaka, ila kama unavyoona nina mambo mengi ya
kufuatilia, lakini kila kitu kinawezekana kama kuna mpangilio ...tutalipanga
hilo kwa pamoja, ili niweze kuratibu mambo yangu, na mwanasheria sizani kama
una kikwwazo na hilo, natumai umeshafanikisha yale tuliyokubaliana...’akasema
mwanadada akimwangalia mwanasheria usoni na mwanasheria akabetua mdomo
akitabasamu na kumtupia macho mwanamama.
‘Kama kuna sherehe kama hiyo, basi tuone itakuwaje, na mambo
yote tutayamalizia huko huko....’akasema mwanasheria.
‘Kwani kuna mambo mengine ambayo mimi siyajui?’ akauliza
mwanamama na mwanadada akamwangalia akionyesha mshangao, akamgeukia
mwanasheria, na mwanasheria akainuka akitaka kuondoka, na simu ya mwanadada ikalia
kuashiria kuna ujumbe umeingia na mwanadada akaangalia ujumbe huo umetoka wapi,
akausoma na baadaye akasema;
‘Naona hakimu ananiita, ...nahisi ni kuhusu mambo ambayo tulikuwa hatujamalizana , basi
tutaonana hiyo kesho...’akasema mwanadada, wakaondoka pamoja na mwanasheria, na
kumuacha mwanamama akiwa na mawazo mengi kichwani..
‘Hawa watu wamepanga nini dhidi yangu...’akajiuliza
NB: Hadi hapo, mumeona kila kitu, natumai iliyobakia ni
hitimisho, je kuna kilichobakia, ...tusaidiane kama tumesahau jambo
WAZO LA LEO:
Maendeleo ya jamii, ni jukumu la kila mmoja wetu, kama kweli tunajali . Tujue
kuwa kila mmoja ana kipaji chake , kila mmoja ana ujuzi wake, basi tutumie
vipaji hivyo, ujuzi huo na elimu hiyo kwa pamoja, kwa masilahi ya jami zetu,
tuondolee tamaa binafsi za dhuluma,kwani katu dhuluma haitajenga, na ndio
mwanzo wa chuki , mifarakano na uvunjifu wa amani.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment