Mwanangu wakati naelekea nyumbani ,kichwani kulikuwa na
mambo yanajirudia rudia, hadi kichwa kikawa kama si changu, mara nikasikia
sauti nyingi, zikijirudia rudia...;
‘Mpenzi wangu
nimefurahia kwa kauli yako hiyo, maana nilisubiri uzindukane tu, niisikie hiyo
kauli yako, kuwa upo tayari tuoane, na mimi nakutamkia moja moja, kuwa nipo tayari
kuolewa na wewe hata sasa hivi....’
‘Sasa iliyobakia ni
kumwambia mwanamama, maana mimi namuonea huruma sana mtoto,....nampenda sana
mwanamama, na nipo tayari kuishi naye, hata kwa uke wenza....’
‘Hilo niachie mimi,
kwa vile mimi ni baba mdogo wa mtoto, bado nina jukumu la kumlea huyo mtoto,
kama alikataa kabisa, mimi siwezi kumlazimisha japokuwa nilikuwa na nia hiyo,
ila nilikuwa nafanya hivyo kwa shinikizo la kaka, vinginevyo, ....sikuwa na
haja ya kuoa wake wawili kwasasa....’nikasikia
Mazungumzo hayo yalijirudia sana kichwani mwangu na
sikuelewa jinsi nilivyo nyumbani, kwani muendesha bajaji ilibidi aniulize;
‘Shangazi, si ndio
hapa au?’ akaniuliza na mimi nikawa kama mtu aliyetoka kwenye usingizi, na
kuangalia nje, nikasema;
‘Oh, kumbe tumefika, samahani sana, nilikuwa
mbali..’nikasema huku nikimkabidhi pesa yake, na kwa haraka nikakimbilia ndani
hadi kitandani, nikajibwaga kichwa chini, na kuanza kulia, ...nililia hadi
shuka likalowana, ...na baadaye nikainuka na kukaa, nikavua shati langu la mikono mirefu na kubakiwa na nguo ambayo inaacha mabega wazi....nilihisi joto...
‘Hivi kwanini ninalia, ninalilia nini?’ nikajiuliza, na kwa
haraka nikasimama, nikainua mikono juu, na kusema;
‘Ahsante mungu, naona umenipa jibu ambalo najua wewe ndiye
unayejua ni kwanini iwe hivyo, na sio kwa ajili ya matamanio yangu ambayo
huenda hayana manufaa kwangu, nakuomba uniongoze katika njia sahihi, ili nisije
nikajutia kwa maamuizi hayo, huenda niliteleza, na kuvutika na matamanio yangu,
lakini sasa nimebaini ukweli, ninaomba kwa ukweli huo inipe ujasiri, ...
‘Nakuomba mola wangu, uniongoze ...kwani mimi mja wako unaufahamu
udhaifu wangu, hata kama nitajikakamua vipi, wewe ndio unayefahau njio
iliyosahihi kwangu, ukiniachia mwenyewe, sitaweza..nitapotea, niongoze na
unionyeshe njia iliyo sahihi.....’nikatulia na hapo yakanitoka machozi, na
safari hii yalikuwa sio yale ya kukosa, yalikuwa ya unyenyekevu na maombi...
Sijui nilisimama pale kwa muda gani, lakini ilichukua muda
kidogo, hadi nilipozindukana kutoka kwenye hiyo hali ya maombi, nikainua uso
juu, kichwa kikiwa chepesi, nikahisi manzito yameondoka, na nilikuwa tayari kwa
lolote lile na mara nikasikia mtu akigonga mlangoni, na nikajua huenda ni
jirani yangu kaja kuniulizia mambo ya huko mahakamani, kwani nilimuahidi
nikitoka huko nitakuja kumuhadithia.
‘Karibu jirani...’nikasema huku nikifungua mlango, na mlango
ulipokuwa wazi, nikajikuta ninaangaliana na yule yule aliyenifanya nitoe
machozi, yule yule aliyenigusa moyo wangu, na kutaka kuivunja ile ahadi yangu
niliyokuwa nimeiweka, nikamwangalia machoni huku nikihangaika kwani nilikuwa nimevua lile shati langu la mikono mirafu na kuacha sehemu ya mabega wazi, na ukumbuke nilikuwa sijafuta vile nilivyojikwatua wakati nipo kule hospitalini, na hali hiyo ilinifanya nijisikie vibaya,, lakini sikuwa la kufanya kwa muda ule...
Shemeji, yeye aliniangalaia mara moja, na baadaye akawa anaonyesha wasiwasi, akiwa anaangalia huku na kule na kuanza kuuliza;
‘Vipi nimesikia umeitwa huku nyumbani kwa haraka, je kuna
nini, mtoto kapatwa na nini, mtoto yupo wapi..?’ akawa anauliza mwanasheria
huku akiangalia huku na kule akionyesha kuwa na wasiwasi, na mimi nikamwangalia
kwa muda bila kusema kitu, halafu nikasema;
‘Hakuna tatizo mtoto hajambo, kachukuliwa na bibi
yake,....’nikasema
‘Oh, ....karibu nizimie kwa wasiwasi, maana niliposikia tu,
sikujali chochote kwa haraka nikakimbilia kuja huku, na aheri ningelimuona moyo
wangu ukatulia, na nina hamu sana na yeye, kwanini umpeleke kwa bibi yake, oh,
kwa vile upo na shughuli za kesi yako, natumai hayo sasa yamekwisha tigange
yajayo...’akasema huku akiendelea kuangalia huku na kule,
‘Unajua shemeji, ..natamani niendelee kukuita mke wangu,
...lakini hilo linakuja tu, nataka iwe hivyo, ila kwa ridhaa yako....’akasema
huku akitabasamu, na sasa alikuwa akiniangalia usoni, na kuendelea kuongea.
‘Unajua shemeji katika watu ambao nilihitajia kuwaona baada
ya kutoka huko kwenye hiyo safari sijui niite safari ya kuzimu,au niite safari
ya uzima, ....ni huyo mtoto, zawadi muhimu kwa familia yetu, unafahamu hilo,
hebu mwangalia, na mwangalai kaka, ni kama nakala, ...shemeji we acha tu, ...kila nikimwangalia namuona kaka,
....’akaingia ndani na kunipita hadi kwenye sofa na kujipweteka kwenye sofa, na
alionekana kuchoka, na akalaza kichwa kwenye sofa na huku akiniangalia moja kwa
moja usoni.
Na mimi nikajaribu kumwangalia kwa muda, nikiwa nawaza ujio
wake huu una maana gani tena, sizani kama alikuja tu kwa ajili ya mtoto. Kwa
leo sikutaka kabisa kuoanana na yeye au kuingia kwenye malumbano ya hoja, ya
kuwa mimi niwe mke wake. Nikawa ansubiri, na kuombea hilo asiliongee.
Moyo ulikuwa unanienda mbio, kichwa ambacho kilianza
kutulia, sasa kiliaanza kuingia mambo mengi kwa haraka, maswali yasiyo na
majibu yalianza kunisakama. Mimi nilijua nimewakimbia na nimemalizana nao, na huyu
hapa kaja tena, ...nikatamani nimfukuze....lakini sikuwa na mamlaka hayo yeye ni shemeji yangu, ana hiari ya
kuja hapo wakati wowote, nikajaribu kutuliza kichwa, nikajitutumua na kusema;
‘Lakini shemeji wewe unaumwa, kwanini usingelipumzika
nyumbani kwanza, ukapata nguvu, ..kama kuna matatizo ya mtoto, ningelikuambia,...matatizo
ya mtoto ni ya kawaida tu, ..kwanza jiulize, kwani wakati unaumwa, ni nani
alikuwa akimshughulikia huyo mtoto, ni mimi na wazazi wangu, wapo babu na bibi
yake tunasaidiana kumlea huyo mtoto...hakuna shida...’nikamwambia na yeye akawa
ananiangalia tu machoni, hadi nikajisikia vibaya.
‘Shemeji, unakumbuka kauli yangu , nilivyowaambia wewe na
mwanadada, kauli yako hiyo inazidi kunitonesha kidonda, kwani ukisema wewe na
wazazi wako ndio mliokuwa mkiwajibika kwa mtoto huoni unatusuta sisi baba zake,
kuwa hatuwajibiki kwa mtoto wetu,...sasa nimepona , na nimekuja kutimiza wajibu
wangu, naomba usinizuie,.....’akasema huku akionyesha huzuni usoni.
‘Shemeji sitaki kuyarejea maelezo yangu tena, ila
ninachotaka kukuambia ni kuwa, sitaacha kutimiza majukumu yangu, na
ikizingatiwa kuwa ninachokifanya nakipenda, kinatoka moyoni mwangu..sio
kwasabbu ya kitamaa binafsi, kama wengine.....hapana nafanya hili nikiwa kweli
nalipenda na niwajibu wangu kufanya hivyo...’akasema
Mimi nikatembea kuelekea kwenye jokofu, kumchukulia
kinywaji, huku nikisema kimoyomoyo,
‘Ni yale yale nisiyotaka kuyasikia...’
Nikafungua jokofu huku nikiwaza ni fanye nini, ...nikachukua
muda kidogo kulitoa kile chimbo kilichowekea hicho kinywaji, namtambua sana
shemeji yangu huyu anapenda sana kinywaji cha matunda, ninachokitengeneza
mwenyewe,...nilitembea huku nikiwaza nifanye nini, na huku nikisikliza maneno
ya huyu shemeji yangu. Nilitamani aondoke haraka iwezekanavyo, lakini siwezi
kumfukuza...
Nikachukua gilasi, na nikiwa na chombo kikubwa kilichohifadhia hicho
kinywaji, nikaenda pale alipokaa,
nikasogeza kimeza kidogo mbele yake, kama ada za mila zetu zilivyo, nikainama
kidogo, na kuweka gilasi mbele yake na kuanza kumimina, na nilipomaliza,
nikaishika ile gilasi, na kuiinua kumkabidhi yeye huku nikimkaribisha kwa adabu,...na
kuashiria ishara ya kupiga magoti.
Akawa bado ananiangalia tu machoni, nikasimama hivyo hivyo,
sikutaka kusema neno, nilitaka yeye aanze kuongea, na baadaye akatabasamu na
kusema;
‘Mungu wangu, shemeji, sijui niseme nini unielewe, najisikia
vibaya sana, kuendelea kuliongelea hili, lakini wewe kwa vile ni mtu mzima,
nafahamu umeshanielewa....nasema hili kutoka kwenye moyo wangu,siwezi kuishi
bila wewe kwani shemeji umekamilika sifa zote za mke mwema....oh, ’akasema na mimi
kauli hiyo ilikuwa kama imekuja na kuzibua fahamu zangu zilizokuwa zimejificha,
na kuanza kuhisi vingine, kwa huenda huyu shemeji ana tuchezea mimi na
mwanadada. Na kauli yake ikanirejea kichwani;
‘Hilo niachie mimi,
kwa vile mimi ni baba mdogo wa mtoto, bado nina jukumu la kumlea huyo mtoto,
kama alikataa kabisa, mimi siwezi kumlazimisha japokuwa nilikuwa na nia hiyo,
ila nilikuwa nafanya hivyo kwa shinikizo la kaka, vinginevyo, ....sikuwa na
haja ya kuoa wake wawili kwasasa...
Nikataka kusema ovyo, lakini kitu kikaniambai nivute subira,
sikusema kitu, na halafu akapokea ile
gilasi na kunywa ile juisi kwa fujo, hadi akaimaliza, na kuweka ile gilasi
mezani, nikataka kumimina tena, lakini akaweka mkono juu ya gilasi kuzuia, na
mimi nikainua uso kumwangalia, tukawa tunaangaliana.
Kwakweli sijui kuna nini kinanitokea hasa ninapoangaliana na
huyu mtu, najihisi mwili wangu wote ukiniishia nguvu, na kutamani...kitu
nisichoweza kukielezea, ni hisia za ajabu sana siwezi hata kuzielezea..ni hivyo
ndivyo ninavyoweza kusema, na hali hii ilinitesa sana kiakili, lakini sikuwa na
jingine, ila kukubali matokea, nikageuza kichwa na kuangalia pembeni, nikatulia
na moyoni nikitafakari cha kusema lakini akili ilikuwa hainipi neno la
kuongea...nikatulia...
Nikahisi ukaribu wake, kumbe alishasimama, na kunisogela, nikageuka kumwangalia, akawa na yeye ananiangalia moja kwa moja usoni, akawa kama anataka kunishika, kama kunikumbatia, lakini niliona akisita kufanya
hivyo, mikono yake ikawa inacheze cheze pembeni yake, akijaribu kufanya analotaka
kulifanya, lakini kwa sababu nyingine akawa anasita, na mimi nikatulia kimiya,
japokuwa moyoni, katika nafasi nyingine nilitamani anishike, tukumbatieni japo
kwa muda...ibilisi akawa hachei mbali...
‘Shemeji nimekuja
nataka kukuambia jambo..’, akasema na safari hii akajitahidi na kunishika viganja vyangu vya mkono, na akainua kile kiganja chenye pete, na kuuinua mkono wangu juu kama anatakua
kuubusu, mkono ule wenye pete yangu na marehemu mume wangu, ... ule mgusano
ulinifanya mwili mnzima usisimuke, na kujikuta nikitetemeka kama vile mtu
aliyeshikwa na umeme...siju kwanini mwili ulikuwa hauna nguvu ya kusogea, nilikuwa kama nimenasishwa.
Kwa hali kama ile, akili haiwezi kusema sogea, ondoka..., joto la haraka likatanda mwilini..yaani
ilikuwa kitu cha ajabu, ghafla baridi, ghafla joto..na sikutaka hali hiyo
iendelee, kwanza niliangalai chini, ili tusiangaliane, na pili,nikajaribu kuiondoa ile hali, lakini sikutaka kumfanay ajisikie vibaya, ..nikamtupia jicho la haraka tukaangalia, na muda huo tupo karibu, karibu sana, kama
vile tunakaribia ukumbatiana,....baaadaye nguvu zikanijia.
Kwa haraka nikautoa mkono wangu kwenye kiganja chake na
kusogea mbali na yeye, huku nikihema kama mtu aliyekuwa akikimbizwa, halafu
nikamwangalia tena, na yeye alikuwa kasimama vile vile, huku akiniangalia, na tukawa
tunaangaliana japokuwa tulikuwa safari hii kwa mbali kidogo na ulipita muda mchache, mwishowe
nikaona nisipoteze muda, nikasema;
‘Shemeji tafadhali, sipendi nikuambie toka humu
ndani,...sina mamlaka hayo, ila ...oh, nakuomba uniembie unachoataka kuniambia,
halafu uondoke, nahitaji muda wa kukaa peke yangu, akili yangu haipo sawa,
imechoka..naomba unielewe shemeji...’ nikasema na shemeji akaniangalia kwa
macho a huruma na kusema.
‘Lakini shemeji....’akaanza kujitetea na mimi nikamkatiza na
kusema;
‘Unataka kuniambia nini, najua muda huu mwanadada
anakuhitajia sana, naomba, uniambie lililokuleta halafu urejee kwa
mwanadada...’nikasema na sauti yangu iliashiria huzuni, na yeye akawa kama
kashikwa na mshangao, akasema;
‘Mwanadada, hana shida yule niachie mimi mwenyewe, tunajuana
sana, kwasasa yupo mahakamani anafuatilia maswala yako, tuliachana pale
hospitalini, maana hata wakati mnafika, nilisharuhusiwa, sikuwa na haja ya
kukaka tena pale, nikamuomba docta aniruhusu, na wakati huo huo nikawa
nawasubiria nyie, ila wakati mnafika nilikuwa nimetoka kwenda dukani...kununua
kitu muhimu sana...’akasema
‘Yaani ulitoka kwenda dukani wakatii wewe ni
mgonjwa....’nikasema
‘Nimeshapona shemeji, imeshapona kabisa, huwezi amini,
ugonjwa uliobakia ni wa moyoni, nahisi kuna kitu kinakosekana, ambacho
kinahitajia matibabu, ...amabayo dakitari wake ni wewe’akasema
‘Shemeji acha hiyo...mimi sio mtoto, achana na kauli hizo za
ujana, mimi sipo huko tena, kwanza, unanishangaza kweli, ...shemeji mimi,nina
akili zangu timamu, na nakuelewa sana, lakini huki unapotaka kwenda, sio
sahihi, jaribu kutulia, na kutafakari, usichukulie mambo kwa pupa, ndio hata
kama unavyodai kuwa uliambiwa uje utimize wajibu wako, hilo unaweza kulitimiza
hata bila ya mimi kuwa kama unavyotaka wewe,kwahiyo tulia, na tafakari kwanza...’nikasema
na kauli hiyo ikamfanya ashituke, na kusema;
‘Shemji ni kweli unayoyasema, na sio kwamba nimekurupuka tu,
nimeyawaza hayo kiundani, na sio kwamba nimekuja hapa kwa haraak tu,
nimeshaongea na mwanadada, na tumekubaliana, japokuwa hatukuwa na muda mrefu wa
kuongea,....nakuomba unisikilize kwana ni nini kimenileta hapa...na anomba
unikubalai ombi langu hilo...’akasema.
‘Nakusikiliza, sema unalotaka kusema...’nikamwambia na yeye
akasema
‘Mke wangu....’ akasema maneno hayo na mimi nikamkatisha na
kusema
‘Shemeji acha utani, nafahamu unayesema hayo kiutani, ...na
sizani yanatoka moyoni kwako kama ulivyoanza kuyaongea pale hospitalini,...haya
niambie lililokuleta, kama ni mtoto hajambo, hakuna shida, kuna jingine, maana
nataka kuhangaika, siunajue tena mke ni kujishughulisha kwa mambo ya ndani, sio
kuongea, kuongea sana kunaleta umbea...’nikasema huku nikichukua ile gilasi
mezani, na kabla sijaishika, akaniwahi na kuushika mkono wangu, kiganja chake
kikawa ju ya kiganja cha mkono wangu ambao ulikuwa umeshaishika ile gilasi,
nikainua uso wangu tukawa tumeangaliana tena..
Sijui kwanini, maana nilijikuta namwangalia tu machoni, na
yeye akawa ananiangalia, hadi niliposikia kama mtu anakaribia mlangoni,
nikainua mkono wangu haraka na yeye akageuka kuangalia mlangoni, na yeye kwa
haraka akausogelea mlangoni na kusema.
‘Unatarajia mgeni?’ akaniuliza
‘Ndio, natarajia mgeni ndio maana nakuomba uondoke...’nikasema
kumdanganya, sikuwa natarajia mgeni yoyote, zaidi ya huyo jirani yangu, ambaye
kwangu sio mgeni, ni mtu niliyezoeana naye na akija anaweza hata asipige hodi.
Huwa anamazoea ya kuja na kuingia ndani moja kwa moja ndani.
‘Oh, mbona nina maongezi muhimu sana, huwezi kumwambia kuwa
aje baadaye...’akasema na mimi nikasogea pale mlangoni na kuangalai nje,
kulikuwa hakuna mtu, nikaufunga mlango na kurudi pale nilipokuwa nimesimama, na
shemeji akanisoegela na kusema.
‘Basi shemeji,tuongee haraka, maana hapa nilipo nateseka,
nateseka sana moyoni mwangu, na wakati wote nikiwa nakuja hapa, moyo wangu
umekubali kuwa wewe ndio chaguo langu, nakuomba sana..’akasema na ghafla
akapiga magoti mbele yangu huku akinishika mkono, nikashikwa na butwaa na
moyoni nikasema;
‘Imekuwa hayo tena..’ sikuema kitu, kwa sauti, nikamwangalia akiwa kanipigia magoti mbele
yangu.
‘Shemeji nataka uwe mke wangu..’akasema huku akiwa kashika
kiganga changu cha mkono huku akijaribu kuniivika pete kidoleni...
NB. Naona twende pole pole, sehemu hizi za kumalizia ili tuelewe vyema, sehemu ijayo kesho,
naimalizia malizia,kuna vitu muhimu nahitajia kuvihakiki, lakini ipo tayari.
WAZO LA LEO: Moyo
ukipenda, hauoni kasoro, ndio maana wanasema ukipenda, chongo utaliita kengeza,
hayo yapo na kila mmoja anayapitia, kwako ewe kijana, mtarajiwa, ukijikuta
katika hiyo hali usichukulie pupa, cha muhimu ni kuwa na subira, ili uweze
kulipima hilo pendo hilo.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment