Tulipofika hospitlini moja kwa moja tuliingia chumba ambacho
alikuwa kalazwa mwanasheria, na cha ajabu tulipoingia tulikuta kitanda ni
kitupu, hakuna mgonjwa aliyelala hapo na ilionekana kabisa hakuna mtu humo
ndani, tukashikwa na mshangao, tukawa tunaangalia huku na kule tukiwa hatujui
ni nini kinachoendelea,
‘Huyu mgonjwa kaenda wapi, na sisi tumepita haraka haraka
kuja huku bila hata kuuliza mapokezi...’akasema mwanadada.
‘Au yupo washroom,
anajisaidia.....’nikasema na mwanadada akageuka kuangalia mlango wa kwenda
chooni, na akatikisa kichwa.
‘Unaona mlango ule kama upo wazi, kama mtu yupo washroom,
angelifunga huo mlango, na pia tungelisikia angalau sauti, inaonekana kabisa
humu ndani hakuna mtu...’akasema mwanadada.
Mimi kwa kuhakikisha nikawa ansogelea kuelekea mlango wa
kwenda chooni, huku moyoni nikijiuliza mgonjwa wetu kapalekwa wapi, au
kahamishiwa kwenye wodi za wagonjwa wa kawaida, maana hicho chumba kilikuwa
mahususi kwake yeye, mgonjwa mahututi. Kabla hata sijaufikia huo mlango sauti
ikatokea nyuma kwenye mlango wa kuingilia hicho chumba ikisema;
‘Niwasaidieni nini...?’ sote wawili tulishikwa na mshituko,
kutokana na sauti hiyo, kwani ni sauti ya mtu tunayemfahamu, na sote tukageuka
kumwangalia aliyetoa hiyo sauti, na moja kwa moja tukawa tunaangaliana na
mgonjwa wetu, ambaye alikuwa kajawa na tabasamu mdomoni
Mwanasheria akiwa keshabdili na kuvaa nguo zake za kawaida, alituangalia
akiwa anatabasamu, na kiukweli ugonjwa huo ulimdhoofisha sana, alionekana
kuchoka, na mwili ulikuwa umepungua kwa kiasi kikubwa, lakini tabasamu lake la
haiba halikuondoka na hilo ndilo linalomfanya mwanadada awe akilikumbuka kila
mara. Na hata siku moja nilipokuwa nikiongea naye, aliwahi kuniambia, pamoja na
mengine anayompendea mwanasheria ni pamoja na tabasamu lake, anasema tabasamu
hilo humuacha hoi.
‘Oh, mpenzi...’ilikuwa sauti ya mwanadada, ambaye aliitamka,
na alipogundua kitu akashituka na kuniangalia mimi pale niliposimama, mimi
nilikuwa karibu sana na mwanasheria, lakini nilikuwa nimesimama huku
namuangalia mwanadada, kwa upande na kwa upande mwingine namuangalia huyo
mgonjwa nikasema;
‘Shemeji, umepona...pole sana..siamini, tuliingia na
wasiwasi sana tulipoingia na kukuta chumba ni kitupu.’ Nikasema, na nikamuona
mwanadada akija kutukaribia, na akamsogelea mwanasheria kwahiyo akawa yupo kati
kati yangu na mwanasheria, alishindwa kuvumilia, akamkumbatia mgonjwa, na
mgonjwa naye hakufanya hiyana akalipokea hilo kumbatio huku akiguna kwa furaha.
Mimi nilibakia pale pale nikiwa nimesimama huku natizama chini.
Waliachiana na mwanasheria akanisogelea na kunishika mkono, huku mwanadada akiwa kamshikilia mwanasheria begani akiniangalia mimi na wote wawili wakawa wakiniangalia mimi kwa furaha na mimi ikabidi niwasogelee, na mwanasheria akawa mkono mmoja kamshika mwanadada na mkono mwingine kanishika mimi
na akawa anatuvuta kuelekea pale kwenye kitanda alichokuwa amelala siku zote
alizokuwa hapo. Mashine zilishaondolewa, pale kitandani zilikuwa zimewekwa
pembeni.
‘Oh, jamani wake zangu, nimefurahi sana, kuwaona, maana kila
dakika iliyokuwa ikipita niliiona kama masaa mengi tu, na hata nilipotuma
ujumbe wa kuwa mje haraka, haikufanyika hivyo, sijui mlifahamu kuwa sipo katika
hali mbaya, ila nilitaka kuwaona tu, kuwathibitishia kuwa nimerejea kwenye
safari hiyo nzito....’akasema
‘Safari gani hiyo tena mpendwa....?’ akauliza mwanadada
akimwangalia mwanasheria usoni, na mwanasheria akatabasamu na kusema;
‘Kwakweli nilikuwa mbali...mbali sana, na huko, ilikuwa kama
ni sehemu ambayo hutakiwi kurejea tena,ila nawashukuru sana,ndugu zangu walionitetea
, walinitetea nikanusurika kufa...., walijitahidi kunitete baada ya kuonekana
sistahili kureeja tena huku duniani, wakaniombea kuwa kwa vile bado nina majukumu
ambayo sijayakamilisha ni vyema nipewe muda nije kuyakamilisha, na baada ya
hapo siku yangu ikifika basi nirejee huko tena..’akasema mwanasheria.
‘Ina maana huko unakozungumzia ni akhera..au ni wapi?’
akauliza mwanamama
‘Labda ndiko akhera, lakini mimi sijui, ila nilijiona
nikisafisrishwa juu kwa juu, nikapita milima na mabonde, nyika na tamabarare,
bahari na nchi kavu, halafu nikatua kwenye uwanja mkubwa, usio onekana mwisho
wake, na hapo, nikawa kama nimelazwa, ...na kujiona kama nipo peke yangu,
lakini inavyoonekana kuna watu wengine kama mimi, na kila mmoja anajihisi yupo
peke yake..’akatulia
‘Sikuweza kuinuka, nilikuwa nimelala tu, kilichokuwa
kikiweza kufanya kazi ni akili, mdomo, na masikio, vingine vyote vilikuwa kama
sio vyangu...’akasema
‘Na mara nikasikia sauti ikiuliza nimletwa hapo kufanya
nini?’
‘Ameletwa kuhukumiwa, kwani haijajulikana ni mtu wa wapi,
...’sauti nyingine ikasema.
‘Kwanini aletwe kuhukumiwa ana makosa gani?’ sauti ikauliza.
‘Ndio maana tumemleta hapa, kwani hayupo kwenye orodha ya
watu wa kuja huku, lakini tumeletewa hapa, sasa sijui tufanyeje?’ sauti
nyingine ikasema.
‘Basi kwa ajili ya kumsaidia, tu, tuangalia matendo yake, ya
wema na mabaya yake’sauti ikasema.
‘Basi niambieni makosa yake,kama makosa yake ni mengi kuliko
mema, basi itabidi ahukumiwe, kubakia huku huku, na kama mema yake ni mengi,
itabidi arejee huko alipotoka....’ile sauti ikasema.
‘Ina maana kwa kusema hivyo unamaanisha kuwa wanaokwenda
huko ni wale wenye makosa?’ nikawa najiuliza na kabla sijatulia, nikajisikia
nikiambiwa;
`Kwa vile siku zangu za kwenda huko zilikuwa bado, lakini ni
lazima kutafutwe njia ya kuhalalisha kuwepo huko, basi njia peke yake ni
kuchagua kati ya mema na mbaya, yapi yawe ya huko na yapi yawe ya kurejea
nilipotoka,....’sauti ikawa kama inanijibu swali langu,
‘Tuchague kwasasa mema yawe ya kukurejesha huko ulipotoka, na mabaya yawe ya
kukufanya ubakia huku, japokuwa hiyo sio kanuni ya kuja huku, mtu huja huku
siku zake zikifika bila kujalia mema na mabaya yake...hili limetokea kwasababu maalumu, tunayoifahamu sisi wenyewe.’ile sauti ilibainisha hivyo..’
Basi kilifanyika kitu kama mahakama, na mimi nikatakiwa
kuwaita mashahidi wangu wa kunitetea, nikauliza mashahidi ndio nani, nikaambiwa
ni viuongo vyangu...’nikabakia nimeduwaa.
Ikaanza kazi ya kulinganisha mabaya na mema, yangu, ilikuwa
kitu kama mizani, upande mmoja, kunaweka mabaya yangu, na upande mwingine
kunawekwa mema yangu, na viuongo vyangu vinathibitisha, ...kila
nilichotenda,...yaani ilikuwa ni ajabu sana, kwani hata kama nilifanya kachembe
kadogo ka wema, kaliwekwa hapo, na kumbukumbu zote za hilo tendo
zililetwa,...sikuwa na ujanja wa kujitetea zaidi.
Kama ni kesi basi ilikuwa kesi ya aina yake, maana wengi waliokuja kutoa ushahidi
kuwa mimi ni mksoaji, walikuwa na hoja nzito, na ushahidi ni viuongo vyako, ambayo vilithibitisha hayo....na baaada ya hapo kukaja nafasi ya watu kuja kutoa yale niyowafanyia au kunifanyia, mabaya na mazuri,...
Na ikaja na fasi ya kuulizwa, mfano kuna muda niliulizwa, mikono
yangu nilitumia vipi, katika kutenda mema, je niliwahi hata kushukuru kuwa mimi
nina mikono, ..kuna ambao hawana mikono, lakini mimi nimefadhiliwa mikono, je
niliwahi hata mara moja kushuru kwa hilo,...nikajikuta nikisema hapana, ikawa
inapunguza mema,,...nikauliza kuhusu macho, kuhusu masikio, yaani kila kiuongo
kilikuwa ni shahidi wa kunihukumu...’akatulia
‘Mara nyingi tunasema tunamuomba mungu, tunamuomba tukila,
tunamuomba tukiwa na shida, je kweli kuna mtu anakumbuka kukaa na kuanza
kumshukuru mungu kuwa kamjalia mkono, au kamjali mguu, au kamjali macho, au kajaliwa
neema moja baada ya nyingine kwa kuvigusa vile viuongo vyake..ni mara chache
kuyasema hayo japokuwa kwa ujumla tunamshukuru mungu..’akasema mwanasheria .
‘Nikalalamika hilo kuwa kila siku najitahidi kumshukuru mungu
kwa ujumla, kwahiyo kila kiungo kinahusishwa, je unaweza ukajenga nyumba mara
moja bila kuanza msingi, ukaweka ukuta, hadi kufikia bati, ina maana kila sehemu
ina umuhimu wake, je nilishawahi kuona umuhimu wa kila kiuongo, je mkono
ukiumia ninajisikiaje...je macho , je masikio, je wasio navyo hivyo, wanajihisi
vipi, kwanini mimi niliye na viuongo hivyo sishukuru, kiasi cha kushukuru
tu....
‘Ikabidi niombe msamaha kuwa nikapatiwa nafasi hiyo nitakuwa
nikishukuru neema za huyo aliyenijalia mwili ukakamilika, na kila kiungo kikawa
na kazi yake, ambayo ni muhimu katika mwili....hapo mashahidi hao wakaondoka,
na mwisho wa siku kwenye mizani yangu ikaonekana nina daiwa, makosa ni mengi
kuliko mema..
Nikaambia kama kuna njia yoyote nyingine ya kujitetea
nijitetee, nikaona labda nijitetee kwa uwakili wangu kuwa mimi ni wakili na
mara nyingi ninafanya kazi ya kutetea watu wasihukumiwe bila kosa,..mmh, najuta
kwanini nilisema hivyo, kwani kuliletwa watu ambao niliwatetea kumbe ni
wakosaji, kuna watu niliwafunga kumbe hawana hatia, kwani ukija kuangalia yale
makosa, unaona kuwa kumbe mtendaji hakutenda kwa makusudi, ...ila tu walishindwa
kujielezea, na yote yalipopimwa, wema na ubaya wake, ikaonekana nina makosa
ziaidi ya mema..
Kwahiyo kila nilipojitahidi kuleta yale niliyoona ni mema,
nilijikuta ndio naingia kwenye makosa zaidi maana yale mema yakilinganishwa na
mabaya yaliyowezesha kupatikana kwa huo wema, inaonekana maovu ni makubwa
zaidi, maana ili upate jambo lina gaharama yake kulifanikisha, na utagundua
kuwa mengi tuyoyafanya ili kupata jambo ambalo tunaliona ni jema, tunapitia
kwenye michakato isiyo halali,....pale nilionyeshwa lakini kwa kuelezea inakuwa
ngumu, na mwisho wake utaona kuwa wema upo lakini ubaya wa kuufanya huo wema
uwepo ni mkubwa zaidi ya huo wema....
Mwisho wa siku ikaonekana nina maovu zaidi ya
mema,...ikasuburiwa hukumu, ..na hapo nikaambiwa nijitetee kwa mara ya mwisho, maana
nilishaandaliwa kukabidhiwa kwa watu wa huko, kuwa mimi sistahili kuerejea tena
huku duniani, na hapo hisi zinajia, na kihisia nikawaona ndugu zanu wakiwa
upande wa kushoto kwangu, na wao wapo kama nilivyo mimi, lakini wao
wameshapigwa muhuri wa watu wa huko , na walionekana hawana raha, nikauliza je
ndugu zangu hawawezi kunitetea.
Nikaambiwa nina uhuru huo, kama ninaona kuwa wanaweza
kunitetea wanakaribishwa, ila na wao wapo kwenye kusubiria hukumu yao, ambayo
inasubiria siku huyo ya mwisho wa dunia...japokuwa wao wameshakaribishwa huko,
hawawezo tena kurejea duniani....
Wale ndugu zangu wakaulizwa, na wakajaribu kusema mema
niliyowahi kuwatendea, lakini kila walilolirtaja lilikuwa limeshaorodheshwa na
lipo ....’akasema mwanasheria.
‘Kwakweli ndugu zangu walitaja mema yote, ambayo hata mimi
sikuwahi kuyakumbuka, maana walitakiwa kutaja yale mema ya ukweli..na hakuna
kudanganya huko, kila kiuongo kinathibitisha kuwa ni kweli ilitokea hivyo..ooh,
mizani ikasogea kidogo kuongeza mema, lakini haikuweza kuzidi ubaya..
Ndugu zangu wakaulizwa, je mnasemaje huyu ndugu yenu arejee
huko alipotoka, au aje aungane na wao, kusuburia siku ya hukumu, hapo ndugu
zangu, wakaniangalia, kuonyesha upendo wao, kuwa wananihitajia niwe nao,lakini
waliona nirejee ili nikatimize majukumu, ambayo pia yanawakwaza wao, kwani
walitakiwa kuyafanya na hawakuweza kuyafanya, kwahiyo waliniombea nirudi,
huenda katika kuyafanya hayo na wao wataweza kuokoka ....wao wakaniuliza swali.
‘Je unatupenda sisi
au unawapenda hao waliobakia huko duniani?’ lilikuwa swali la mtego, na bila
kufikiria zaidi nikasema.
‘Nikasema ninawependa waliobakia duniani, kwa vile bado
wanahitajia msaada wangu..na hata kabla sijamaliza, nikaona nikiinuliwa juu kwa
juu, na ikawa safari ya kurejeshwa huko nilipotoka....kama vile vile nilivyoletwa,
unajiona kabisa unapita milima mabonde, miti, bahari, nyika, na mwisho wake,
unatua kwenye nyumba, nikazindukana na kujiona nipo katikati ya jopo la
madakitari, wakiwa wanaondoa mipira ya kunisaidia kupumua...
Kumbe madakitari hawo walishafikia uamuzi huo, kuwa sitapona
tena, na kwahiyo walikuwa katika harakati za mwisho za kuondoa ile mipira
iliyokuwa imechomekwa mdomoni, puani, ambayo ikiondolewa ndio basi tena..
‘Huyo dakitari aliyekuwa akifanya hiyo kazi hiyo, aliniambia,
wakati anatoa ule mpira uliokuwa umewekwa puani, akahisi ujoto ukitokea
puani,akawa kama kashituka, na kutokana na ule mshituko, akawa kauvuta kwa
nguvu ule mpira, na mimi kwa muda huo nikafunua macho, tukawa tunaangaliana, na
yeye akabakia mdomo wazi akinikodolea macho.
Wenzake ambao walikwua wakiwa wanasubira kuandika taarifa,
kuwa nimefariki saa ngapi, wakashangaa kuona mwenzao akiwa kanitolea macho, na wakasogea kuniangalia, na
kunikuta nipo macho ninawaangaliana na wao waakjikuta kwenye mshangao na mimi
neno la kwanza kuongea walisema nilisema hivi;
‘Nawaomba wake zangu waje hapa..’ na wale madocta wakawa
wanaangaliana na docta ambaye ananifahamu vyema akaniuliza.
‘Ni akina nani hao wake zako wakati tunafahamu kuwa wewe
hujaoa..?’
‘Ni mwanadada na mwanamama...’nikasema.
‘Watakuja lakini kwasasa sio rahisi kwa vile wapo
mahakamani...’wakasema wakihangaika kunisaidia kwani walihisi nipo kwenye
kuchanganyikiwa.
Nahidi walipigia sindano ya usingizi, kwani nilirejea kwenye
usingizi mnzito na ulikuwa usingizi wa kawaida tu, na nilipoamuka tena, nikawa
na nguvu, na hapo nikaomba karatasi na kalamu ndipo nikaandika huo ujumbe
uwafikie huko mlipo ili mje haraka iwezekanavyo..’akamaliza kuelezea
mwanasheria na kusema tena.
‘Na ndivyo ilivyokuwa wake zangu..’akasema mwanasheria.
‘Kwanini unatuita wake zako, maana hakuna hata mmoja wetu
hapa uliyewahi kufunga ndoa naye?’ akauliza mwanadada.
‘Kiroho, ...hasa nikirejea huko nilipotoka inatambulikana
hivyo, hata ndugu zangu wakati wananitetea walisema hivyo hivyo, kuwa mimi nina
majukumu ya wake wawili na mtoto,nahitajika kurudi duniani nikayatimize hayo
majukumu, ndio maana hata nilipozindukana kilichokuwa kichwani mwangu kilikuwa
hicho, na ndilo maana nikawataja nyie wawili, ...kwahiyo nyie ni wake
zangu....’akasema kwa furaha.
‘Hiyo haipo, ni lazima taratibu zote zifuatwe,..hayo
yalikuwa yako ndoto za safari yako, lakini katika maisha yetu ya kawaida tuna
taratibu ambazo ni lazima tuzifuate, kwani jamii haitakuelewa,...kwahiyo
tunakuomba upone, na uweze kutimiza hayo uliyokusudia...’akasema mwanamama
‘Nafahamu hilo ndio maana nikawaita wote mje, ili tuweze
kuliongea, na mimi sitaweza kuvunja ahadi yangu, kwani niliahidi huko kuwa nitaitimiza...naombeni
mnielewe hivyo na mkubali ili muweze kunisaidia mimi, ..kwani mwanadamu ni
mwepesi wa kusahau.’akasema na kumgeukia mwanadada, na mwanadada akageuka
kuniangalia mimi..
Kwa jumla pale nilipokuwa nilihisi hali sio ya kawaida,
sijui ni uwoga, sijui ni wasiwasi,nikaona ni bora niende nikanawe, angalau
huenda nitaweza kujisikia vyema, nikawatafadhalisha nakukimbilia chooni....moyo
ulikuwa ukinienda mbio sana, na sikuwa na amani, hadi nilipofika huko chooni,
nikajimwagia maji kichwani halafu, nikajikausha na kujiweka sawa...kidogo
nikajisikia afadhali.
Nilkwenda kujiangalia kwenye kiyoo kilichokuwa humo ndani ukutani,
na kuanza kujiweka safi, nilitaka nionekane wa pekee usoni mwa mwanasheria ili
hata nikimjibu kuwa nimekubali, nije kuwa mke wake, arizike kuwa kweli kapata
mume, ni zile hisia za kike-kike.
‘Lakini nitamkubalia kwa sharti moja kuwa tufunge ndoa, sio
kurithiwa,..’ hilo neno sikulipenda,...ninajua mwanasheria atafurahi kusikiwa
kuwa nimemkubalia, anione ...’ikawa nimefikia uamuzi huo.
Nilijuwa huko mwanadada atakuwa akimweka sawa, kuwa yeye
anakwenda kusoma Ulaya, kwahiyo hana haja ya ndoa tena nikawa naendelea kujipa
matumaini, kuwa sina upinzani hasa kwa mwanadada ambaye niliona kuwa ndiye
aanstahili kuolewa na mwanasheria na sio mimi.
Nikakumbuka jinsi mwanasheria alivyoongea muda mchache
uliopita, kuwa sisi sote wawili ni wake zake,kitu ambacho nilikiona
hakiwezekani, ni kitu ambacho hata mimi sikukipendelea nilitaka kama ni mimi,
ni mimi kwanza, baadaye anaweza kuja kumuoa mwanadada, kwangu mimi ndoa ya
mitala haikuwa na shida, ikizingatiwa kuwa mwanadada nimeivana naye sana, kama
mdogo wangu...mmh nitafurahia nikiishi naye..
‘Lakini....’nikawa na mashaka na maamuzi yangu hayo nikaanza
kuomba kwanza, nilimuomba mungu anisaidie kwa hayo ninayotaka kuyafanya, na
kama yana uhalali, na yanafaaa, basi ayafanikishe na kama hayafai basi
anitafutie njia ya kunisaidia hasa kwa ajili ya mtoto....’nikatulia nikiomba
huku nimefumba macho.
‘Ewe mwenyezi mungu, kama mwanadada kakataa kuolewa, naona
niolewe mimi tu, kama kweli kaayzungumza hayo akiwa na nia thabiti, na kama ni
muhimu kuolewa yeye basi aolewe yeye tu, mimi nipo tayari kuacha na hilo....’nikaomba.
Lakini moyoni nilifahamu kuwa mwanadada alishakikataa
hilo...hataki kuolewa kwasasa, na mimi pia sipendi aolewe yeye halafu eti
baadaye ndio nije kuolewa mimi kama mke mdogo wa mdogo wangu, kwani mwanadada
ni mdogo wangu kiumri...
Sijui nikaa muda gani mle ndani, ilionekana nilikaa muda
kidogo, nikajiandaa kutoka huku nikijihakikishia moyoni kuwa mwanadada hataki
tena kuolewa na huyo mwanaume, kwa kauli yake, hilo nikawa sina shaka kabisa
moyoni mwangu , kwahiyo hadi natoka pale chooni, nilijua kabisa kuwa swala la ndoa kwa mwanadada halipo.
Nikatoka taratibu nikiwa nimejiweka msafi , nimejikwatua
ipasavyo, nikafunga ule mlango wa chooni, kwani kile chumba cha mgonjwa,
kilikuwa na choo cha ndani kwa ndani, na nikawa kwenye eneo la kile chumba, na
unapotoka pale chooni, hutokezi moja kwa moja kwenye hicho chumba anapolazwa
mgonjwa, kuna kama ka sehemu kamejengwa kama sehemu ya mapokezi, kwahiyo
unaweza ukasimama hapo usijulikane kuna mtu kwa upande ule waliopo akina
mwanadada na mwanasheria.
Hapo nikatulia kidogo, sijui kwanini moyo ulikuwa ukinienda
mbio,nilikuwa na wasiwasi sana, nikatulia kwanza pale nikiwasikia wakiongea, na
masikio yangu yakawa na hamu ya kusikiliza hicho wanachokiongea, sijui kwanini
niliingiwa na hamu hiyo ya kuwasikiliza kwanza wanachoongea, nikatulia na
kutega sikio, ....nikasikia.
‘Mpenzi wangu nimefurahia kwa kauli yako hiyo, maana
nilisubiri uzindukane tu, niisikie na mimi nakutamkia moja moja, kuwa nipo
tayari kuolewa na wewe hata sasa hivi....’hiyo ilikuwa sauti ya mwanadada,
iliyonifanya nishike mdomo kwa kutoamini,...mwili wote ukaisha nguvu,
nikajikuta nikiona aibu, na kwa jinsi nilivyokuwa nimejikwatua, nikatamani
nirudi huko chooni nijisafishe, nilijihisi kama nimejipaka uchafu mwilini...
‘Sasa iliyobakia ni kumwambia mwanamama, maana mimi namuonea
huruma sana mtoto, nilijaribu kumshawishi kadri ya uweo wangu kuwa umuoe yeye,
lakini alikataa kata kata, sasa sijui tutamsaidiaje...’akasema mwanadada.
‘Hilo niachie mimi, kwa vile mimi ni baba mdogo wa mtoto,
bado nina jukumu la kumlea huyo mtoto, kama alikataa kabisa, mimi siwezi
kumlazimisha japokuwa nilikuwa na nia hiyo, ila nilikuwa nafanya hivyo kwa
shinikizo la kaka, vinginevyo, ....sikuwa na haja ya kuoa wake wawili
kwasasa....’nikasikia sauti ya mwanasheria iliyonivunja nguvu kabisa,
kumbe...ooh, hapo sikutaka kusubiri tena nikageuka, na kuelekea mlango wa kutoka
nje kabisa..
Taratibu nikaufungua ule mlango wa kutoka nje,na kutokea nje
ya korido la hiyo hospitali na nikakutana na dakitari akielekea huko walipo
mwanasheria na mwanadada, alikuwa dakitari aliyekuwa akimshughulikia
mwanasheria tangu mwanzo, na tulishafahamiana naye, na mara kwa mara tukikutana
naye anapenda kunitania kuwa anataka kunioa, ulikuwa utani tu, na aliponiona
akanisogelea kutaka kuanza utani wake, mimi nikamkwepa na kumwambia;
‘Tafadhali docta nimepata simu ya haraka nyumbani kwangu,
naomba uwaambie mwanasheria na mwanadada, wapo humo ndani kuwa nimepokea simu
kuwa niende nyumbani haraka, nahisi kuna tatizo kwa mtoto, sitaweza kuwaaga,...’nikamwambia
na docta akawa ananiangalia kwa mashaka, maana mimi nimetokea huko ndani na
badi ninamwambia kuwa awaambie walioko huko ndani kuwa nimepokea simu ya
haraka, na yeye akasema;
‘Hamna shida, lakini upo sawa sawa kweli, maana nakuona kama
umetaharuki, kuna tatizo kubwa?’ akaniuliza.
‘Ni huo ujumbe wa simu umenichanganya,..ahsante docta,
bye...’nikasema huku naondoka kwa haraka, na yule docta akawa bado kasimama
ananiangalia, lakini mimi sikujali, nikatoka nje, nikatafuta bajaji na kuondoka
zangu...
.
NB: `Mbona kisa hakiishi tu..' watu wandai hivyo, je ni kweli tumalize kisa hiki?
WAZO LA LEO:
Shukuru kwa neema alizikupa mola wako hata kama unaona ni kidogo, hata kama
unaona hazitoshi, hata kama unaona kuna walakini, hata kama hujapata kile
ulichotarajia,kwani kuna ambao hawana kabisa neema kama hizo.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Greetings from Los angeles! I'm bored to tears at work so I decided to
browse your blog on my iphone during lunch break.
I really like the knowledge you present here and can't wait to take a look when I get home.
I'm surprised at how quick your blog loaded on my cell phone ..
I'm not even using WIFI, just 3G .. Anyhow, superb blog!
Also visit my web page - home building facts
Post a Comment