Ilikuwa siku ambayo mshitakiwa mkuu, alitakiwa kusimama kama
alivyoomba kujielezea mwenyewe, na hakuna aliyemuamini tena, baada ya kesi hiyo
kuendeshwa kwa siku tatui mfululizo, na kama ilivyotarajiwa mshitakiwa mkuu,ambaye
alikamatwa hivi karibuni, alikana mashitaka yake yote, na kudai kuwa hayo
aliyoyakubali awali, alifanya hivyo baada ya kuteswa na askari polisi.
Kesi ilipoanza siku ya kwanza mshitakiwa alisema yeye
hahitajii wakili, atajitetea mwenyewe, lakini siku ya pili, akapata wakili,
ambaye alijitahidi kumtetea kadri ya uwezo wake, na kila ushahid ulipotolewa ilionekana wazi mshitakiwa
ana hatia, japokuwa yeye mwenyewe hakuonyesha dalili ya kuogopa, na wakati wote
alikuwa akijaribu kutabasamu, kuonyesha kuwa yeye hana hatia.
Siku ile aliposimamishwa mama mkunga ndipo mambo yalipoanza
kuharibika kwa mshitakiwa huyo, kwani ukumbuke mama huyo alikuwa hajaonyeshwa
dhahiri, na wengi walikuwa bado wanaamini kuwa mama huyo alikuwa keshafariki,
na hata huyo mshitakiwa alikuwa hana imani kuwa hata kama mama huyo
atasimamishwa, asingelweza kuleta chochote kipya cha kumfanya yeye aingie
hatiani.
Tukumbuke kuwa mama huyu kwa mara ya kwanza alifika akiwa
kajifunga khanga mwili mzima, lakini safari hii alipofika, alikuwa kavalishwa
gauni rasmi, pana, ambalo lilikuwa kama vipande vipande vilivyounganishwa na
ungeliweza kufunua sehemu sehemu za gauni hilo maalumu, bila kucha sehemu
nyingine wazi, na ilifanyika hivyo
kwasababu maalumu.
Leo hiii mwanadada, alitakiwa kuhitimisha ushahidi wake, na
alianza kuelezea kwa kirefu toka kesi ilipoanza na akaanza kuhitimisha kwa
kusema ;
‘Tangu awali keshi ilipoanza, washitakiwa walidai kuwa mama mkunga
hakuwa huyo mama mkunga wanayemdai wao, eti ni mama tuliyemchukua na kumpa
usifa huo wa mama mkunga, na wakadai kuwa wanachojua wao ni kuwa mama huyo
alitoweka ghafla na haijulikani wapi alipo…’akatulia.
‘Kwa kauli yao hiyo iliashiria kwa wao wanafahamu ni kitu gani
kilimpata mama mkunga, japokuwa kulitokea maelezo awali yenye utata, watu
wawili kila mmoja akidao kuwa yeye ndiye aliyemchukua mama mkunga na kumtibia,
lakini sasa mama mkunga mwenyewe atathibitisha ni nani aliyemtibia na kutokana
na ushahidi mbalimbali, washitakiwa wanahisi mama huyo alifariki kweye huo
moto, kama walivyotaka wao iwe hivyo, ….na kuonekana kwake, ikawa ni pigo kwa
dhamira yao…’akatulia.
‘Wakati tunaanza kesi yetu, aliyeonekana kuwa ni mshitakiwa
mkuu, aliomba mama huyo atolewe na aonekane hadharani, …hii ilitokana na y a kuwa
hakuwa na uhakika na hilo, kwa vile yeye ni ndugu yake, na taarifa za nyuma zilionyesha
kuwa dada yake huyo kauwawa,….na kutokana na ujanja wa mshitakiwa mkuu, yaani
mtaalamu, ilionekana kuwa kiongozi wa kijiji ndiye aliyefanya njama za kumuua
dada yake, kitu ambacho sio kweli…na hili leo tutalithibistisha. Na kwa vile
kama mtu alijua kuwa dada yake keshafairiki na kuonekana kwake sasa ni jambo hakulitegemea,
akawa na hamu sana amuone huyo ndugu yake, …na aliomba sana apate muda wa
kuongea naye…’akatulia.
‘Mpango huo tukaufanya tukiwa na lengo maalumu na kweli
ndugu hawa wakakutana, na hapo kaka na dada wakaonana, mkiona hilo tukio la
kuonana kwa ndugu hawa, mtathibistisha ukweli wa mambo kuwa kweli ndugu hawa
walikuwa wakipendana, na sio kweli kuwa kaka mtu ndiye aliyepanga njama za
kumuua ndugu yake, ushahidi huo upo, wa makutano ya ndugu hawa, kama
muheshimiwa hakium atakubali tunaweza kuuonyesha …..’akatulia akimwangalia
hakimu ambaye alikuwa akindika jambo na hakimu akasema
‘Endelea kwanza na maeelzo yako…’akasema hakimu,
akimwangalia wakili upande wa utetezi kama anapingamizi, na alipoona wakili
yule hana pingamizi akasema wakili mwanadada aendelee na maelezo yake, haina
haja ya kuonyesha hayo hilo tukio la kukutana ndugu hawo wawili kwa sasa, na
mwanadada akaendelea kuongea kwa kusema;.
‘Kutokana na ushahidi mbali mbali, tulioutoa, na kauli za
mashahidi waliotangulia kuwepo hapa mbele, aliyepanga tukio hilo ni mtaalamu,
akiwa na sura ya kiongozi wa kijiji, kama mlivyoona kwenye ushahidi uliopita
kuwa ndugu hawa walikuwa wakifanana, sana, utafikiri mapacha,
kinachowatofautisha ni ile alama ya kuzaliwa.
‘Mwanzoni tulimuita mama mkunga kuja kumtambua huyo mshitakiwa
mkuu, na mnakumbuka ilivyotokea…..na jinsi gani alivyojielezea, na leo kama
mlivyosikia kuwa mshitakiwa mkuu anataka kujielezea, lakini tunataka ieleweke
wazi, kuwa tunachokitafuta hapa ni haki, na haki ipo kwa pande zote mbil, na
nia yetu sio kumkandamiza yoyote yule, kwahiyo mshitakiwa anayo haki ya
kujitetea…
‘Sisi kama waendesha mashitaka hatuna kipingamizi kwa hilo,
na hapo mwanadada akatulia, akikumbuka tukio la jana yake ambapo, mama mkunga
alisimamishwa na kuwepo kwake, ikaleta athari kubwa mioyoni mwa watu, na huenda
hata mshitakiwa mwenyewe iliona unyama wake ndio maana aliamua leo kusimama na
huenda kutubu dhambi zake, au kuendelea kuleta ukaidi, lakini yote hayo
hayatamsaidia kitu.
Mwanadada akawa anarejea kwenye meza yake huku akijaribu
kukumbuka tukio la jana yake, wakaiti mama mkunga aliposimamishwa;
*********
‘Mama mkunga, tumekuita hapa tena, ili uweze kuelezea
ilivyotokea, hebu tuelezee siku ile ya tukio ilikuwaje? Mwanadada akakumbuka
jinsi alivyoanza kumuweka sawa mama mkunga ili aelezee tukio la kuchomwa kwake
moto na jinsi alivyokoka na moto huo, hakutaka kumkatiza, akamuacha aongee
mwenyewe jinsi ilivyokuwa.
‘Siku hiyo, tulikuwa na mume wangu nyumbani kwetu, na baada
ya kazi za mchana kutwa, tulijikuta tumechoka sana, na kila mmoja alitamani kulala
tu, na kweli, tulijikuta tukilala kama magogo, na mara ilipofika saa sita za
usiku, ….nakumbuka sana muda huo, kwani tulikuwa na saa kubwa ya ukutani
tuliyowahi kupewa kama zawadi, na wakati mlio kwa kuashiria kuwa ni saa sita na
ndipo hodi hiyo ikawa inasikika toka mlangoni,…mgongaji aligonga kwa fujo kiasi
kwamba sote tuliamuka tukiwa na wasiwasi.
Mume wangu aliamuka na kuchukua panga lake, kwani huwa na
kawaida ya kutembea na panga hilo mara kwa mara, na mimi sikuweza kulala tena,
nikainuka pale kitandani kusikiliza ni nani aliyekuja muda kama huo, na huko
nje nikasikia mume wangu akiongea na huyo mtu;
‘Unaitwa kwa mjumbe haraka, …kuna tatizo limetokea, na wewe
kama mmoja wa wazee wa kijiji, unahitajika kusaidiana kulitatua…’nikasikia
akiambiwa na kweli mume wangu ni mmoja katika baraza la wazee wa kijiji, hasa
katika mambo ya usuluhishi.
‘Ni tatizo gani, na mbona ni usiku sana?’ akauliza mume
wangu.
‘Ndio mzee, ni usiku lakini matatizo mengine hayachagui muda
cha muhimi ni wewe twende, tunahisi ni kesi za ugomvi, wa wakazi wa hapa,…..sisi
tumetii agiza la kiongozi wetu kuwa tukuite haraka iwezekanavyo, hatukuwa na
muda wa kudadisi zaidi…’akasema huyo mtu aliyetumwa, na nahisi hakuwa peke yake.
‘Kwanini wasisubiri hadi asubuhi, maana huu ni usiku sana,
saa sita za usiku, tutaongea nini muda kama huu…si alifajiri itatukuta tukiwa
tunaongea kwani hamna tetesi ni tatizo gani? ’akalalamika mume wangu.
‘Mzee sisi hatujui, hata sisi tumekurupushwa hivyo hivyo
tuje kukuita, na kwa kifupi mzee sisi hatuna muda , tunahitajika kurejea huko
kwenye malindo yetu, unafahamu kazi yetu, kama hutaki tukatoe taarifa, nyie
ndio wazee mnaotarajiwa kutatatua matatizo, na ujue kuwa ni muhimu sana, ndio
maana tumetumwa kwako….’akasema huyo mtu aliyetumwa.
Mume wangu alirudi na kuniambia kaitwa kwa mjumbe, na
nihakikishe kuwa nimefunga milango yote, na kutokumfungulia yoyote kabla yeye
hajarudi, na kweli nikafanya hivyo, na mume wangu akaondoka…’akasema mama
mkunga.
‘Haikupita muda, nikasikia michakato huko nje, na hapo
nikaingiwa na wasiwasi, nikafunua pazia la dirisha, kwani tulikuwa tumeweka
khanga kama pazia la dirisha nikawa nachungulia nje…na mara nikaoana vijana
wakizunguka, wakiwa na magongo, nikahisi kuna tatizi, lakini sikuhisi kuna
tatizo gani…’
‘Baadaye nakihisi harufu ya mafuta ya taa,au petrol,
nikafunua tena pazia, na kwa mbali nikamuona mtu kasimama akiwa anatoa
maelekezo, nikamchungulia vyema, na aliposogea sehemu yenye mwanga, nikamgundua
kuwa ni nani…
Alikuwa ni kiongozi wa kijiji, …nikaanza kujiuliza kuna
nini, maana mume wangu kaitwa kwenda kwa kiongozi huyo, lakini kwa muda ule
namuona yupo hapo, akiwa anatoa maelekezo kwa vitendo, na nilisikia wazi wazi
akisema;
‘Mwagia kote-kote, hakikisha hatoki mtu hapo, na lindeni sehemu
zote asitoke…’nikasikia kauli hiyo na hapo nikajua kuna hatari, na nilichofanya
ni kutoka pale kitandani na kuvaa nguo za kikazi zaidi, …na kuelekea chumba chetu tunachofanyia
ibada, nikaanza kufanya ibada, kumuomba mungu…
‘Mara moto ukaanza kuwaka kwa kasi, ulikuwa mkali sana, na
hata pale nilipokimbilia mlangoni, sikuweza kufika, moto huo utafikiri ulianzia
ndani, na nyumba nzima ilikuwa imetanda moto, nikajua tena mimi sio wa kupona,
lakini sikukata tamaa, kwani nilishamkabidhi mungu, maombi yangu.
Nikatembea kwa shida, maana kote kulikuwa ni moto,
nilikwenda hadi jikoni, tunapopikia na kuweka, mitungu ya maji, na hapo
kulikuwa na mtungi mmoja mkubwa wa maji, nikamuomba mungu, na kujitumbukiza
ndani ya mtungi huo, japokuwa haukuweza kunihifadhi lakini angalau sehemu ya
mwili iliweza kuzama kwenye maji hayo, na maji yaliyomwangaika yakazima moto
sehemu hiyo iliyokuwepo karibu,…kwa wakati huo maji yalishaanza kupata moto kwa
jinsi moo ulivyokuwa mkali..
Nilikaa mle hadi maji yanachemka, nikaona siwezi kuvumilia,
ni bora nitoke maana nitaiva kama nyama, ndio nikatoa taratibu, na kwa muda huo
nje kulikuwa hakuna watu nikatoka na kuanza kukanyaga kwenye moto, sikujali
tena, maana mwili mzima ulikuwa umekufa ganzi, na nilipofika kwenye mfereji wa maji
machafu, mrefeji ambao tuliutumia kumwanga maji kwa ajli ya mabata,nikashikwa
na kizungu zungu na kudondoka ndani ya mfereji huo, kichwa kikiwa chini, ..Nikapoteza
fahamu.
Nilipozindukana ndio nikajiona nikiwa nimepakawa majani ya
dawa, na majani hayo nayatambua vyema kuwa yanatibu majeraha ya moto kwa haraka
sana, na nilipotizama kwa mbali nikamuona mtu,….nikajifanya kama bado
nimezimia, ..nikamchunguza huyo mtu, na nikagundua kuwa ni mganga, mganga wa
kijiji cha jirani…
Na yule mganga aliponiona, ninaanza kama kupata unafuu,
nikamuona akiondoka, na sikuweza kumuona tena…’akasema mama mkunga
‘Una uhakika huyo uliyemuona ni mganga, sio mtaalamu?’
akaulizwa
‘Sio mtaalamu…japokuwa alivaa kama yeye,…lakini uvaaji wa
mtaalamu na huyo unajulikana, na isingelikuwa vigumu kwangu kumgundua kuwa ni
mtaalamu au ni huyo mganga wa kijiji cha jirani..’aaksema
‘Unasema uliyemuona akielekeza watu katika uchomaji moto ni
kiongozi wa kijiji, hebu tuambie ni yule pale?’ akaulizwa akionyeshwa
mshitakiwa mkuu, aliyekuwa kakaa, nahakimu akamuamrisha mshitakiwa huyo asimamishwe,
na mshitakiwa akasimama huku akitabasamu
‘Ndio yeye, ….’akasema mama mkunga
‘Unauhakika gani kuwa ndio yeye…?’ akaulizwa
‘Hata nguo alizokuwa kavaa siku ile ndio hizo hizo alizovaa
leo…ndio huyo huyo kiongozi wa kijiji’akasema
‘Unafahamu kuwa kiongozi wa kijiji ni ndugu yako?’ akaulizwa
‘Ndio ninafahamu, na nilishangaa kweli, kwa jinis
ninavyomfahamu ndugu yangu, sikuamini…, kama kweli ndio yeye aliyekuwa
akiwaelekeza watu wafanye hilo lililofanyika, sikuamini, maana mara nyingi
ninaongea naye, na sikuwahi kuona chuki za kiasi hicho…kwakweli dunia hii
imeharibika, …na acha ajabu siku ile mliponikutanisha na yeye anasema sio yeye
aliyekuwepo hapo siku hiyo….’akasema na mwanadada akamkatisha kwa kumuuliza
‘Hamjawahi kuzozana na ndugu yako huyo kuhusu, maswala ya
eneo lako?’ akaulizwa.
‘Hilo lilikuwepo, na tulifikia muafaka wa jinis ya
kulitatua, lakini hakukuwa na chuki kubwa kiasi hicho, na hatukuwahi kugombana
kuhusiana na hilo..kwangui mimi sikujali sana, na hata kama wangelitaka
kulichukua, sikuwa na tamaa kiasi hicho…lakini nilijua kwa vile ni mali yangu,
ndugu yangu hataweza kunidhulumu….’akasema
‘Sasa iweje aamue kuja kukuchoma moto, au ni kwasababu ya
imani za kishirikina ulizowahi kuambiwa unazo?’ akaulizwa.
‘Na mimi nahisi ni hivyo,… lakini sio kutoka kwa kaka yangu,
maana hata yeye alilipinga hilo, na alisema yeye atajitahidi hadi watu waamini
kuwa mimi sio mshirikiana, na kama mimi ni mshirikina ina maana hata yeye atakuwa
mshirikina, na sisi mama yetu hakuwa na tabia hiyo…je huo uchawi nimeupatia
wapi, sasa hapo sielewi jamani…’akasema mama mkunga
‘Je unamfahamu mtaalamu kuwa ni ndugu yenu?’ akaulizwa
‘Namfahamu sana, ila sikuwahi kuishi naye kwa karibu sana,
kwahiyo simfahamu fika, …niliporejea hapa kijijini na kuolewa, muda wote
anakuwa na nguo zake za kitaalamu, kwahiyo sijawahi kuwa naye karibu na kumjua
vyema zaidi ya kutambua kuwa ni ndugu yetu, ambaye tuliachana tukiwa wadogo…na
alishabadilika sio yule mtoto nilyekuwa nikimjua…hasa kwa vile muda wote kavaa manguo
yake.
‘Je mtaalamu na ndugu yako, yaani kiongozi wa kijiji
wanafanana?’ akaulizwa
‘Ndio ankumbuka, wakati huo tukiwa watoto, kabla mimi
sijaachana nao, watu walikuwa wakiwaita mapacha, yaani kaka na huyo wanayemuita
mtaalamu walikuwa wakifanana sana…’akasema
‘Kama walifanana kihivyo wewe uliwezaje kuwatofautishai, kwa
kipindi hicho?’akaulizwa
‘Kaka yangu alikuwa na alama kama hii yangu iliyopo hapa
shingoni, ni kitu kama kidoti, na kma unavyoona ni kikubwa, na hata niliporejea
kutoka huko nilipokuwa nilikiishi na kuja hapa baada ya kuolewa, nilikiona
hicho kidoti kwenye shingo ya kaka
kikiwepo kama kilivyo changu , lakini huyo mtaalamu hana kitu kama hicho….’akasema.
Wakili mwanadada akamgeukia hakimu na kusema;
‘Muheshimiwa hakimu, mwenzetu mtaalamu, alitumia umbile,
lake la kufanana na ndugu yake na kuanza kufanya machafu, kwa kupitia kwa jina
la ndugu yake….na kutokana na mipango yake, alitumia udhaifu wa wanakijiji,
kuwezesha kufanikiwa mambo yake hayo, na, ili kuyathibitisha hayo, kuwa ndugu
hawa wanafanana, ningelimuomba kiongozi wa kijiji aletwe hapa, na asimama
karibu na mshitakiwa mkuu…’akasema mwanadada
Kiongozi wa kijiji aliitwa kutoka chumba cha mashahidi baada
ya kuonekana hana hatia na alitakiwa kuja hapo kama shahidi, akaitwa, na kuja
kusimama karibu na mshitakiwa mkuu…kila mmoja alishikwa na butwaa;
Mwanadada akamgeukia mama mkunga na kumwangalia kwa makini
na wakati huo mama mkunga naye alikuwa naye kashikwa na butwaa na alipoulizwa;
‘Ni yupi kati ya yule ni kiongozi wa kijiji, unayesema
ulimuona akitoa maagizo, na hapo mama mkunga akabakia ameduwaa, na kusema;
‘Mimi ninachokumbuka ni kuwa nilimuona ….oh, …ina maana
kweli, maana isingeliwezekana, ndugu yangu afanye hayo …haiwezekani, kumbe …wewe,
…. nimeelewa, …huyo mtaalamu ndiye aliyekuwa akitoa maagizo, ….ndio
yeye..angalia na jinsi anavyo….oh, ndio yeye ’akasema mama mkunga akionyesha
uso wa kutahayari
‘Kwanini unasema hivyo, umegundua nini?’ akaulizwa
‘Kichwa…, kichwa cha kaka kwa nyuma hakina kisogo kirefu
kama cha mtaalamu, na …nakumbuka usiku ule nilipomuona huyo kiongozi wa kijiji,…hakuwa….oh,…nimekumbuka,
pale alipgeuka, na kuvua lile kofia pana alilokuwa kalivaa, kisogo chake sio
kama cha kaka,…ingawaje kwa muda huo sikuwa na akili ya kuwaza hilo…lakini sasa
nimekumbuka, …ndio huyu huyu…aliyekuwa akiagiza nichomwe moto….’akasema mama
mkunga.
‘Haya hebu sogea pale kwa watu hawa wawili uwaangalia kwa
makini na kweli uliyemuona pale kwenye tukio ni yupi,…usiangalie ukaka, angalia ukweli,
maana tunahitajia haki itendeke….’akaambiwa na kusogea akawachunguza kwa
makini, na akasema huku akimwangalia mshitakiwa mkuu kwa hasira;
‘Yaani wewe unajiita mtaalamu kumbe ni muuaji,…nilishaanza
kukushuku toka awali, pale niliposikia kuwa umewaambia watu kuwa mimi ni mwanga….mungu
atakulipa kwa uovu wako huo…’akasema akimwangalia mshitakiwa mkuu kwa hasira,
na mshitakiwa mkuu akawa anatabasamu kama vile haogopi.
Na baadaye mama mkunga akamgeukia kaka yake wakaangaliana
kaka yake aliyekuwa akitokwa na machozi, na wote wakaanza kulia.
Ilipita dakika chache kila mmoja akishuhudia tukio lile, kwa hisia za huzuni, na baadaye mama mkunga alirejea kwenye sehemu ya ushahidi hapo mwanadada akasema;
‘Ili muone huo uovu, sasa natambulisha ushahidi wa mama
mkunga, ambaye watu walidai, wathibitishe hilo, haitakuwa vizuri kuondoa nguo
zake zote, lakini tumetayarisha jinsi gani ataweza kuonyesha sehemu chache za
mwili wake, …sehemu kubwa ya mwili, mgongoni, na tumboni, …hadi miguuni,
kuliungua, na ngozi yote imekunjanama, ila dawa alizowahiwa kupakwa ndizo
zilizomuokoa,…
Mwanadada akawa anaangalia kwenye laptop yake akionyeshea
kwa vitendo sehemu za nyuma yake kuwa mama mkunga kaungua, na alionyeshea hivyo
akiwa anaangalia picha kwenye lap top yake,….na kuendeea kusema;
‘Hata wataalamu wa ngozi, madakitari, wameshangaa, kwa mama
huyu kupona, kwani inaonyesha aliungua asilimia kubwa ambayo kihali halisi
asingeliweza kupona, ni kwa mapenzi ya mungu, lakini pia tumshukuru mganga wa
kijiji cha jirani liyewahi na kumpaka hizo dawa….’akasema mwanadada
Ikafika wakati mama mkunga anaonyesha baaadhi ya mwili wake,
akageuka na kufunuliwa sehemu ya mgongoni,, na miguuni, kilichofuata hapo ni
kilio, watu wengi hawakuweza kuvumilia, walijikuta wakilia…ni unyama
usioelezeka, mwili wa mama huyu ulikuwa na mgamba magamba na umkunjamana,japokuwa
sehemu mbali mbali zilishaanza kubabuka ngozi…..
‘Huo ndio ushahidi wetu muheshimiwa hakimu, na shahidi
anaweza kuulizwa maswali na upande wa utetezi.
Wakili wa upande wa utetezi,
alibakia ameduwaa, na kugeuka kumwangalia mteja wake, na alipogeuka tena, akawa
kama kashikwa an butwaa, akasema;
‘Sina swali …na mara mshitakiwa mkuu, akasimama, na kusema
kwa sauti
‘Kama wakili wangu hana swali mimi nina swali….?’ Akasema kwa
sauti kubwa na hakimu, akamwangalia wakili wa utetezi, na wakili huyo, akageuka
kuteta na mteja wake huyo, wakawa kama hawalewani, na baada ya kuongea wao
wawili wakili huyo akageuka na kumwangalia hakimu na kusema;
‘Mteja wangu anasema yupo tayari kuelezea kila kitu, lakini
anahitajia muda wa kutafakari vyema, aliniambia hili kabla hatujafika hapa, na
nikamshauri kisheria, lakini kwa hali tuliyoiona leo, mimi nipo tayari yeye
mwenyewe asimame,na kuelezea, hilo analotaka kulisema;
Muheshimiwa hakimu, akawaita mawakili wote wawili, na kuteta
nao kwa muda, halafu wakili wale waliporejea sehemu zao, hakimu akasema;
‘Kesi hii tunaiahirisha hadi kesho, na waendesha mashitaka
mutahitimisha ushahidi wenu na baada ya hapo tutamsimamisha mshitakiwa …..’akatulia
hakimu, na baaadaye akamgeukiwa wakili mtetezi na kusema;
‘Wakili upande wa utetezi kazi yako ni kumtetea mteja wako,
ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka, na sio kuonyesha hisia zako…natumai
umenielewa..’akasema na kesi ikaahirishwa, hadi kesho yake.
NB: Nafikiri kila kitu sasa kipo wazi, je mshitakiwa huyu
atasema nini,..
WAZO LA LEO:
Unapokosa na ikadhihiri hivyo, lililo jema ni kukiri kosa na kutubu, huenda kwa
kufanya hivyo ikawa ni heri kwako,…ujanja, uwongo,na kupindisha maneno na
wakati unafahamu kuwa wewe umekosa kweli hilo ni kosa jingine na inaonyesha
dhamira yako sio njema. Kutenda kosa sio
kosa , kosa ni kurudia kosa.
No comments :
Post a Comment