Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, August 29, 2013

WEMA HAUOZI-57



Ilikuwa siku nyingine ya kesi, na watu wengi walifika siku hiyo, wakiwa na hamu ya kumsikia yule waliyemtambua kama mtaalamu, ambaye sasa yupo hapo mahakamani kama mtuhumiwa mkuu, wa kesi za mauaji , utapeli , wizi na utekaji na ubakaji.

Hakuna aliyeamini kuwa mtu kama huyo ambaye aliheshimika wa utaalamu wake wa tiba, na mambo ya mazingara, angelishitakiwa kwa makosa kama hayo, mtu ambaye  aliogopwa hata kusengenywa, kwani ilifikia wakati mtu anaongea ndani na mkewe, yeye anafahamu, ….
je haya na mengine mengi aliwezaje kuyafanya, je ni kweli yeye ni mmoja wa makuhani, au wanajimu, au ni tapeli fulani aliyetumia kipaji hicho kwa ajili ya kujinufaisha,…

Tuendelee na kisa chetu, tukiwa mahakamani…

Muda wa kesi ulifika na hakimu akaingia, na baada ya taratibu mbali mbali za kimahakama, mshitakiwa alisimamishwa kama alivyotaka, kabla hukumu haijatolewa, na leo alionekana tofauti na siku nyingine, alikuwa mnyonge, na alionekana kama anaumwa, na hata alipokuwa kitembea alikuwa kama anapepesuka,lakini alijikaza asionekane yupo katika hiyo hali.

Aliposimama pale mbele, kwanza alitulia kimiya kwa muda, na wengi walihisi anamuomba mungu wake, au anawaza ni nini cha kusema, lakini sio mtu kama huyu kwa wale wanaomfahamu, huwa ni msemaji wa papo kwa papo, na hachukui muda kuwaza la kusema , na akisema utafikiri alijua ni nini cha kusema kabla…..anajiita `mtaalamu’

Ilipopita dakika chache, akiwa kimiya, hakimu akainua kichwa kumwangalia, na ilionekana kama hakimu anataka kumuuliza `kulikoni’ mbona yupo kimiya, lakini kabla hakimu hajasema neno yule jamaa akaanza kuongea ….

Kwanza alianza kuongea kwa sauti ya chini, sauti ya kinyonge, lakini kila muda ulipokuwa ukipita,  akawa anaongeza sauti  kidogo kidogo, kama vile redio inayoongezwa sauti kidogo kidogo…

‘Ndugu muheshimiwa hakimu,najua mimi mnaniona  ni mkosaji, na hata kama nitajitetea vipi hakitabadilika kitu, najua kabisa hakuna ambaye atanielewa, na ndio maana nikaona, kuliko kuendelea kupoteza muda, na kuwapotezea watu muda wao wa  kwenda kuzalisha ni bora niseme ukweli, japokuwa ukweli huu hautaonekana ni ukweli, kwa vile mumeshaniweka kwenye kundi ambalo sio kweli nastahili kuwa kwenye hilo kundi…

‘Kama ningelikuwa kwa wenzetu wanajua umuhimu wangu, …ningelikuwa mtu mwingine mwenye heshima ya hali ya juu, lakini……nasikitika kusema, …nipo kwa watu ambao, …hata nifanyeje, hawataniamini, hata nifanyeje hawataweza kujua umuhimu wangu..huenda nimezaliwa kwenye karne ambao huenda ikaja kutokea miaka ijayo….’akasema na watu wakaguna.

‘Nafahamu hamtanielewa, lakini ngoja niseme haya, ili yawepo kwenye kumbukumbu zenu,….’akawa kama anatabasamu, halafu akatikisa kichwa kama kukubali kitu, na kuendelea kuongea;

‘Mimi japokuwa nakiri haya na kwenu nyie mtatambua kuwa nakiri kuwa ni mkosaji, lakini wakati mwingine najisifia kuwa nimefanya yale ambayo hakuna kati yenu angalidiriki kuyafanya, nimeweza kutumia kipaji changu alichonipa mungu kwa kufanya jambo lenye manufaa, japokuwa kwenu mtaona sio la manufaa…na ni heri kufanya hivyo, kuliko kufa na kupotea bila kufanya lolote na mwisho wake mungu ataniuliza kile kipaji nilichokupa umekifanyia nini…ni heri nimefanya hivi niwe nimeanzisha

Hebu niwaulize ni nani angelijua kuwa nina kipaji kama hicho, kama nisingelifanya hayo niliyoyafanya…je ningelikaa kimiya ingelikuwa bora kuliko hivi nilivyofanya…je hamuoni kwa kufanya hivi nitakuwa nigusa jambo, na huenda likaja kusaidia badaye…mtaona katika maelezo yangu…’akatulia kwanza na baadaye akaongeza sauti na sasa kwa sauti ya juu kama mhubiri, au mwanasiasa akiwa jukwaani.

‘Nilipokuwa jeshini, nikiwa kitengo muhimu, …mmh,….’akatulia na kuguna kidogo, huku akiangalia huku na kule, kama anayemtafuta mtu, halafu akawa kama karizika na usalama wake, akasema;

‘Nafahamu  wengi hawataamini hilo kuwa mimi nilikuwa jeshini, tena sio jeshi kama mnavyojua nyie, hapana, nilikuwa kwenye kitengo maalumu, kitengo ambacho hutakiwi  kijulikane, na naomba ijulikane hivyo, kuwa nilikuwa kwenye kitengo nyeti…na sitakiwi kuongea zaidi ni kitengo gani,…’akatulia na akamtupia jicho hakimu na alipoona hakimua anamwangalia, akainama na kuendelea kuongea.

‘Nikiwa huko…huko… huko, ndipo haya yote niliyoyafanya, yalipoanzia, nasema huko  huko….nasema hivyo, wao ndio chanzo cha haya yote, kama isingelikuwa wao, huenda ningelikuwa mtu mwingine. Nakiri kusema wao ndio walionitenda, ….na nakiri kuwa kama wangelitendea yaliyo mema huenda bado ningelikuwa huko nikilitumikia taifa langu…’akainua kichwa na kuwa kama anaangalia juu.

‘Jamani dunia hii ukiwa mnyonge, ukiwa masikini, kila mtu anakuzarau…utaongea nini wewe, hata kama unachotaka kukiongea ni muhimu, kuna faida kwao, lakini kwa vile umesimama wewe masikini, usiye na jina, usie na kitu, watu hawatakusikiliza…ngoja asimame, fulani, mwenye nacho, hata akiongea utumbo, maneno yake yatasikilizwa na hata kuwekewa pambio….huo ni ujinga, na mimi sio mjinga, ndio maana nikaona nifanye yangu, na niishi kivyangu…hamtanielewa, na sijali….’akasema huku akitikisa kichwa na kutabasamu.

Mimi niliingia huko nakuita jeshini, na eleweni hivyo hivyo….wengine wanakuita usalama wa taifa,…..lakini sina uhakika kama jina hilo linatendewa hivyo, ….sizani kama kunastahili kuitwa hivyo, sizani….niliingia huko, nikiwa mtoto wa mkulima, hata wenzangu walishangaa jisni gani nilivyoweza kuingia huko,…’akageuka kumwangalia mlinzi, na akawa kama aanmchunguza.

‘Kiukweli sehemu kama hizo, huwezi kuingia ovyo ovyo, hebu niwaulize, ni wapi mliona tangazo kuwa wanatafutwa wafanyakazi kwenye kitengo kama hicho….au hata mkiwa jeshini, mliwahi kusikia kati yenu kuna watakaohitajika kujiunga na nafasi hizo…hakuna, …..mnafahamu sehemu kama hizo, huingii ovyo ovyo, lakini mimi niliingia kwa miujiza ya mungu, na hata hivyo, wale wanaojiona kuwa huko ni kwao, wakaanza kunisakama…na hata kunitungia majungu, kwanin , kwanini…’akacheka huku akiwa bado anamwangalia huyo askari.

‘Watu hawa, wanajiona wameukata, kasimama hapa anajiona, kuwa yeye ni mtu mashuhuri….hakuna kitu, …’anyway, tuyaache hayo….’akasema na kuinama na kuendelea kuongea;

‘Nikiwa huko, nilijikuta kila siku nipo kwenye mitihani…na sio mitihani kama hii ya kwenu, …ooh, ni mitihani kweli kweli….moja baada ya mwingine, na sitaki kuielezea yote kinaga ubaga….naomba mnivumilie maana haya ninayoyaongea ni kwa ajili ya kumbukumbu zenu, na huenda mkanifikiria kivingine, lakini mimi sitajali…acheni niongee, ili muweze kunihukumu, mtakavyo…..’akageuka kumwangalia hakimu.

‘Nikiwa huko siku moja nikajikuta nipo kwenye kesi ya kubaka mtoto wa mkuu mmoja…hebu fikiria mimi mtoto wa mkulima niende kumbaak mtoto wa mkuu, hivi kweli inaingia akilini..ningelimuanzaje, ….lakini niliambiwa nimefanya hivyo, japokuwa sikufanya hivyo,..ilikuwaje , kwa ufupi, siku hiyo nilichukuliwa na wenzangu, wakisema kuna kazi maalumu, …na walitaka niwasindikiza tu, na mimi sikuwa na hiana, maana sikujua kuna nini, nikijua ni kazi maalumu tu, kama ilivyo kazi zetu, kumbe wenzangu walijipanga, nikajitosa kichwa kichwa…

‘Oh, tukafika maeneo ya wakubwa, na mimi nikawa nashangaa mabustani, na maeneo ya kifahari ya hawa waitwayo wakuu, waheshimiwa, …mara wenzangu wakaja huku wakiwa na kimuhemuhe, na bila kuniambia jambo, wakatimuka kurudi kambini, mimi nikawa narejea pole pole, nikiwa naondoka ndoto za Alinacha kuwa huenda siku moja nikawa kwenye mijengo kama hiyo na kuitwa muheshimiwa,…sikujua kuwa wenzangu wamefanya tendo baya, ile namaliza eneo la wakubwa ili kuingia eneo la kambini, mara nikasikia sauti ya filimbi ya hatari, hata kabla sijakaa sawa hawa jamaa wenye nembo iliyoandikwa MP, wakanidaka, na kesi ikaangukia kwangu kuwa mimi ndiye niliyefanya hivyo..

‘Hiyo ni kesi ndogo tu…..

‘Kuna kesi nyingi zilitokea kabla ya hiyo, na zote ni kubambikiwa,…wakawa wananikomaza kidogo kidogo, na kesi hiyo ya kubambikiwa kubaka, ikawa kesi angu ya mwisho, kwani…..iligusa seehmu nyeti, ilimgusa bosi, …mkuu, na binti yake, alikuwa muhimu na kipenzi chake…oh,  nikaonekana  sifai…na hatimaye ikapitishwa amri kuwa nifukuzwe....nikafukuzwa.

'Nikafukuzwa na, hakuna aliyejali kuchunguza zaidi, na hata pale nilipojitetea sikusikilizwa, ….hakuna aliyejali kipaji changu ambacho wengi walishaanza kufaidika nacho, kwani mara kwa mara nilikuwa naitwa kwenye majumba ya wakubwa kutengeneza hiki na kile, na kwa vile nilikuwa na nafasi hiyo, wenzangu wakaona ….ehe, huko huko, tutamtafutia ubaya.

‘Hakuna aliyejali wema, wangu,hakuna aliyejali uhodari wangu nikiwa kwenye vitendo,  kwani nilikuwa mlenga shabaha mashuhuri, na katika mambo ya medani za kivita, nilikuwa ambari wani….yote hayo yalitupwa kapuni, na kilichobakia kwangu ni kuwa mimi sifai….

‘Nilikuwa fundi wa kila kitu, ujenzi, makenika,…kutengeneza silaha….sijui ungelinipeleka wapi nishindwe, na yote hayo niliweza kujifunza kwa kuangali tu…nikikuona unatengeneza kitu, nikakifuatlia basi mimi nitakuwa mtaalamu zaidi yako…wenzangu wakaniona mimi nitakuwa zaidi yao,wakaniona kuwa nitakuwa kikwazo,nitakuwa maarufu….na ndio maana wakawa wananifanyia visa…haya ninayoyasema ndio ukweli wenyewe, japokuwa kwenye faili langu hakuna vitu kama hivyo, kuna ubaya..ubaya..ubaya…sawa jidanganyeni hivyo….

‘Nikafukuzwa kazi nikiwa na majeraha moyoni, nikiwa na visasi moyoni, na hasa kwa hawa wanaoitwa maafande,…wakuu, watu hawa nawamaindi kishenzi…. na azima yangu ikawa ni kufanya lolote,….angalau niondoe hasira zangu, na niliahidi kuwa kwa vile wameniona kuwa nilibaka , basi ni lazima nifanye hivyo kwa yoyote anayeitwa afande, au mkuu, au sijui nani…’akageuka kumwangalia yule askari, na akatabasamu, na yule askari akawa anamuangalia tu.

‘Nyie watu nyie…nikiwaangalia hasira …unajua hasira….lakini …anyway, tuendelee…’akaangalai chini.

‘Kwa vile waliniona mimi ni mwizi, wakati sikuwa mwizi, na wazazi wangu wanalifahamu hilo…basi niliazimia, nifanye hivyo, niwe mwizi kiukweli kweli,….kwa kila nitakapopata nafsi,niibe, ili kweli hukumu yao iwe na mshiko…’akasema huku akiwa kakunja uso.

‘Sikupenda kabisa niwe hivyo, ila wao walinilazimisha na kuniweka kwenye kundi hilo….eti mimi ni mwizi…jamani…, sasa niiteni mwizi, nakubali, lakini sio kipindi hicho, na siwezi kujiita mwizi, kama wezi wengine, mtanivunjia hazi yangu, mimi ni `mtaaamu…’akacheka.

‘Mimi huko waliniona kuwa mimi ni tapeli,…lakini sikuwa hivyo, sasa, nikaona ni bora nifanya hayo yanayoitwa utapeli, na sikuwa tapeli kama matapeli wenu, nilitumia ujuzi wangu nilijaliwa na kuwa tapeli, wa aina yake,…. nikatumia ujuzi wangu kutapeli..lakini kwa taaaluma niliyo nayo..mtaalamu…

‘Nilipofukuzwa, sikuchukulia pupa,. Kwanza nikawa porini, nikiwa na vitabu mbali mbali , mimi nimesoma muheshimiwa…usinioene hivi…nilitafuta chakula na matunda , mizizi, ndivyo vilikuwa vyakula vyangu porini, huku nikifanya tafiti za miti mbali mbali, nikagundua dawa….sijui ni kwa sababu ya asili, kwa vile kuna wakati nilikuwa naota kuwa dawa fulani ni tiba ya ugonjwa fulani, na kweli nilipochukua dawa hiyo na kwenda kumtibia mtu, ilifanya kazi..

‘Kwa vile nimesoma, na sikwenda shule kukariri, kama wanavyofanya hawo mnaowaita wasomi, ambao kazi yao ni kukariri..wewe kwanini ukariri, kwanini usigundue chako, ..mimi nawashangaa, …eti kama alivyosema mtu fulani, kama alivyofanya mtu fulani, kwanini usifanye wewe kivyako, na ukasema kama nilivyofanya mimi…siamini..na siwezi kuwaita hawo watu wasomi…..ndio maana maana mimi sitaki kujiita msomi, nikajichanganya na wao, najiita mtaalamu…

‘Kwahiyo nikawa naweka kumbukumbu kimaandishi,….nikawa  namchunguza binadamu, nikamgundua kuwa binadamu ni mtu dhaifu sana, licha ya kutembea kwake kwa tambo na maringo, lakini ndani ya nafsi yake, kuna `udhaifu’….ni udhaifu mkubwa aliona ni ni uwoga, hajiamini,…usituone hivi, sisi wanadamu ni waoga sana, na hasa ukifikia sehemu muhimu sana…’nafsi’…nafsi zetu zimegibikwa na uwoga, kutojiamini….

‘Sasa kama kuna udhaifu huo, kama askari ukiwa vitani, ukigundua udhaifi wa adui yako unafanyaje….nikutafuta silaha inayofaa, ili uambushi….nikagundua kuwa kitu muhimu, silaha muhimu, ambayo nikiitumia basi, nitapaat ninachokitaka kwa haraka,  `uchawi…’

Nikuambie muheshimiwa, watu wanaogopa sana `uchawi’…hata wewe hpo muheshimiwa, …ukafiak kwenye meza yako asubuhi ukakuta paka, kafa, ..kaweka kwenye kiti chako utawazia nini…umelogwa…moyoni utashikwa na mshituko, …hata ujifanye hujali, lakini kwenye `nafsi’ utakuwa na kitu..mshituko…

Nikaufanyia kazi huo udhaifu, na ili niweze zaidi, nikaona sio mbaya kuwa karibu na watu wanajulikana kwa mambo hayo, kwanza nikawa  rafiki wa waganga wa kienyeji, na wale waliosadikiwa kuwa ni wachawi, sikuwaambia dhamira yangu, bali nilitumia kile kipaji changu, cha utundu, nikiona mtu anafanya jambo nalinasa….nilijitolea hata kuwa kibarua, mfanyakazi wa ndani ili mradi nifahamu ninachokitaka…mtaalamu…

Miaka mitano ilikuwa ya namna hiyo, tafiti , kujitolea na kuchunguza….na nilipotulia na kuweka tafiti zangu vyema, nikagundua kuwa kumbe mimi ni jembe….sio utani, muheshimiwa, kama serikali ingelinigundua kuwa mtu kama mimi ni jembe, na kuniweka kiwandani, au huko nilipokuwa, ningefanya mambo ambayo yangelisaidia taifa na watu wake…lakini we bwana we,chuki, ..wivu….vikanifanya nifukuzwe..na ..sijui wamepata faida gani,….

‘Haya nikafukuzwa kazi,…, sasa nifanyeje, nijiue, niwe jambazi moja kwa moja, maana najua kutumia silaha, nina utaalamu wa kila namna, nifanye nini….nitafanya nini na ujuzi huo…sipendi kuajiriwa tena, maana ninajua mwisho wa siku inaweza ikatokea kama ilivyotokea huko, nilipokuwa …kazi mbali mbali nazijua, niende wapi pataakponifaa, hakuna,…na nafahamu nikienda mahali watu watanitumia tu kwa manufaa yao, na mimi sitaki kupoteza muda wangu bure hivihivi…kwa wezi, kwa watu ambao lango lao ni kujishibisha wao na familia zao.

Nikiwa porini, …niligundua hayo mahandaki, na habari zake zilinivutia sana, nikaona huko huko ndipo naweza kuweka makao yangu…lakini ilihitaji gharama, na sikutaka makao ya ovyo ovyo, nikaanza kutumai utaalamu wangu wa ujenzi, ndio nikatafuta handaki moja, nikaanza kazi ya ujenzi..muheshimiwa mimi ni mjenzi, hakuna mjenzi anayenifikia, kama unabisha nenda kaangalie vitu nilivyovifanya….

‘Utaniuliza pesa nilizipatia wapi…?’

‘Pesa sio tatizo, pesa wanazo watu, na nyingi sio zako….wameiba, lakini kwa vile ni wakubwa, ni waheshimiwa, wao hawaitwi wezi,….mimi mtoto wa mkulima, ndiye mwizi,….hata kama sikuiba, hata kama nilichukua haki yangu iliyoibiwa na huyu muheshimiwa, naambiwa ni mwizi, yeye aliyeniibia kiukweli haambiwi mwizi….kwanini nisichukue haki yangu…

‘Nikagundua kuwa haki yangu siwezi kuipata kwa kuomba…utamuomba nani, nije kawako muheshimiwa nikuambia kwua naomba nikapata haki yangu iliyochukuliwa na muheshimiwa , tajiri, au nani, utanisikiliza, huwezi….huwezi…na hili ndilo linalotokea hapa, utanihukumu kwa vile hutanielewa, ….na kwa vile hamjasoma, nyie mumekariri tu, …eti kutona na kifungu fulani, kutokana na kesi iliyofanyika mahali fulani..huko ni kukariri tu…

‘Tumieni akili yenu…tumieni hekima yenu, kama kweli mnafuata haki, kwanini Marekani ilipovamia Iraq, hawa jamaa japokwua ilionekana wazi hawakufuata hicho walichokitaka, lakini walifanywa nini…anyway tuyaacha hayo…

‘Ila ninahotaka kusema hapo ni kuwa, ili uweze kupaat jambo, ili uweze kufika mahali, wakati wingine inakubidi utumie `akili’ ..hata ikibidi kuua,…kama walivyofanya hawo mabwana wakubwa….kama ningelikuwa nao wangelinielewa, lakini sio mtu kama nyie, mnaokariri…waakti mwingine, wekeni vitabu pembeni, tumieni hekima na akili…akili mnazo …lakini hamtaki kuzitumia, kazi ni kutunisha matumbo na kula viyoyozi…nyie watu nyie..niwamaindi kishenzi…’akawa anamwangalia hakimu kwa jicho la hasira.

‘Sasa kwanini nisichukue pesa zangu,walizodhulumu, na hata kama sio mimi niliyedhulumiwa, lakini wamechukuwa kwa walalahoi, na kwa vile mimi ni mjanja, nahitajia nichukue kilicho changu. Muheshimiwa kuna watu matajiri humu nchin, na hawajui kabisa jisni gani ya kuzitumia hizo pesa, nikaona hawa ni kazi ndogo tu, nikajenga utundu wa vitisho,…uchawi kidogo, utapeli kidogo, uganga kiddogo, na mbinu chache tu, nikawa nakusanya pesa, na hizo nikawa najengea hilo handaki…kidogo kidogo, na mwaka ulipoisha nikawa na ofisi iliyopo chini ya ardhi, ikiwa na kila kitu…

‘Muheshimiwa hakimu, hapa nilipo naona napoteza muda, maana kama ningeachiwa mwaka mwingine, nina imani ningeliweza kugundua kitu kingine, muhimu sana…lakini ….’akatulia na kumwangalia wakili mwanadada.

‘Nafahamu mnataka nieleze yote hayo yaliyotokea yalitokea vipi, na niliwezaje kuwahadaa watu na wakaniamini, lakini ..kwangu mimi haikuwa kazi kubwa, maana kichwa changu kinafanya mambo mengi sana, kinafikiria zaidi ya mnavyofikiria nyie…..mimi ni `mtaalamu…’

Nilikuja kugundua kuwa kuna rasilimali ambayo watu wanaichezea, kwanza ardhi,….muheshimiwa nashangaa kiongozi anaiuza ardhi kwa wageni hivi huyu mtu ana uzalendo kweli, uliwahi kuona wapi, wanzetu wazungu wakiwauzia wakuja ardi yao….hapa kwetu, ipo, na …sio ardhi, viwanda, vya asili, walivyojenga mababu zetu, mwalimu alijitahidi akawezeka wenye viwanda, leo hii, wanakuja viongozi waliokariri madarasani wanawauzia wakuja viwanda vyetu, kwanini hawo wakuja wasije wakajenga viwanda vyao vipya, ili vishindane na viwanda vyetu, ….tatizo la elimu ya kukariri…..mimi mtaalamu sipo huko.

‘Ardhi, ndio uasili wa nchi, huwezi ukauza uasili wako…ukifanya hivyo, wewe sio mzalendo, wewe ni tapeli, wewe ni mwizi, naona ajabu mimi mzalendo mnaniita mwizi,….wakati wezi wa kiukweli wapi, kwanini wauze uasili wetu, ardhi,..kwa vie wanaafhamu kuwa watapata kitu kidogo,…ni watapata nini basi  kama sio mtu anauza nyumba yao, na kwenda kuishi kibarazani, …unafikiri huyo uliyemuuzia, atakufanya nini , kama sio kukufukuza…ni ujuha…

‘Samhani sana muheshimiwa, lakini viongozi wanaofanya hivyo, kuuza ardhi yetu, viwanda vyetu vya asili, …mambo muhimu ambayo yanashikiia nchi, kama reli, ..umeme,….sijaona kama wanafanay haki, hawajatumia elimu yao, wanatumia elimu ya kukariri, sio elimu ya kitaalamu, na watu kama sisi wataalmu, wanatupiga vita…..ndio wanatuona wachochezi,…na mtatufunga sana, lakini kila siku atazaliwa mwingine mpya kama mimi…’akasema na watu wakacheka.

‘Nyie mtaaklia kucheka tu, hamjui…na hamtajua, nyie ni bendera fuata upepo,…wenzenu wanakula wanshiba wanawatapikai, hata kuwanyea, hamshituki….lakini ndani ya ardhi yetu kuna madini..kuna rasilimali nyingi, ndio maana nasema kama ningeliachiwa mwaka mwingine nisingelikuwa mwenzenu….ningeligundua mafuta,….hamtaamini hilo, lakini mimi nafahamu jinsi gani, maana nilisoma vitabu, nikagundua mengi…sikwenda shue kukariri, nilisoma nikawa mbunifu, hiyo ndio shule, na huo ndio utaalamu …ok…’akawaangalia watu akiwa katoa macho

‘Tuanze hilo la hii kesi yetu, kwanza nasema hivi….yote yaliyosemwa juu yangu, sio kweli kwa mantiki ya ukweli,…nataka munithibitishie kosa langu ni nini, ….’akamwangalia mwanadada.

‘Huo ushahidi na mashahidi, hawajathibitisha kosa langu ni nini…hivi ni kosa kutengeneza njia ya kulinda uasilia wetu, mlitaka aridhi yetu ije ichukuliwe hivi hivi…hiawezakani, ni lazima kuwa na wazalendo kama mimi, hata kama hamtanikubali kwa sasa….’akasema huku akiwa katoa macho kwa hasira.

‘Mtauliza kwanini nilifikia hatua ya kuua, kuchoma watu moto….ku..ku…’akatulia kidogo

‘Mengine nilifanya iwe kama kiini macho tu, hayo ya kumchomea mama mkunga moto…ni jinsi tu ya kuweza kulinda mali yetu kwa mbinu mbadala, nyie simnaamini uchawi, sasa kwanini tusipitie kwenye mambo hayo mnayoyaamini, kuondoa vizingiti…hamtanielewa…’akainamana kidogo.

‘Yote yanayofanyika mtafikiri ndivyo yalivyo, hamjui kila jambo linafanyika kwa minajili fulani, hamjui nyie…mtabakia kufangana, kugombana, …mkifikiria ni umila, udini, ukabila….hakuna kitu kama hicho, akili mkichwa…wajanja wanataka kuingia kitaalamu, sasa mimi nalifahamu hilo,ndio maana nilitaka kudhibiti….kuziwahi mali zetu,…’akatulia

‘Tatizo naona naongea na watu ambao hawatakuja kunielewa…, lakini nina uhakika, kama watatokea wasomo wa kiukweli, wataalamu, …sio wa kukariri, kama….mmh, watanielewa, kama wangelikuwepo Wamarekani hapa wangenielewa, lakini wangelipiga vita na hata kuniita gaidi, kwa vile wanafahamu mimi nitakuwa kikwazo kwao….’akatulia.

‘Jamani linden mali yako, lindeni uasili wenu..linda mali kwa vizazi vyenu vijavyo, hivi mnataka watukuuu wetu waje kukuta mahandaki, madini hayazai kama mbegu,yakichimbwa nadio basi tena, je watukuu wetu watapata nini..mbona hamlioni hilo, sina kosa, sina hatia, kama nina kosa, kama nina hatia, niueni, ili damu yangu iwe shahidi..…’akasema na kuinamisha kichwa chini, akisubiria.

Halafu akainua kichwa tena na kusema;

‘Sio kama naota, sio kama kichaa, kwa haya ninayoyaongea,mimi nilipanga mpango wa kuhakikisha mama mkunga anaonekana mwanga….kwasababu eneo la ardhi yake nilikuja kugundua kuwa ina mali…ipo siku wataalmu watakuja kugundua hilo….lakini sio leo….ndio maana nilifanya kila jitihada nipate sehemu hiyo…ili niweze kuimiliki kabla hawajafika hawo wataalamu kutoka nje, ambo walikwenda shule, sio hawa wa kwetu, wa kukariri..

‘Nilitaka nimiliki eneo lote hili la kijiji, kabla hawajafika wageni, na nafahamu kabisa watafika hivi karibuni na watakaribishwa kuja kuiba uasilia wetu, hawo hawataonekana wezi, na huenda wananchi watajaribu kupinga, na cha moto watakiona, watauwawa, nab ado huo hautaonekana ni uuaji,…

‘Nafahamu kabisa bila ajiza wageni hawo wakifika watapewa ardhi, na watatuibia uasili wetu, na kuhamishia huko nje kwa visingizio vya kupima, kujaribu nk…sisi huku tunaendelea kuwa masikini, wakati utajiri tunao….ila mambumbu, hawajui, na hawatajua…na kama wanajua wanafahamu ile ya juu juu, ndio maana leo hii nipo hapa, napoteza muda wangu bure.

‘Niwaambie ukweli sehemu nyingi  za eneo la kijiji chetu kuna mali, ukienda eneo alilojenga mwanamama kuna madini , kuna mali,..lakini mnachoona nyie ni kujenga,…ni jengo ambalo thamani yake ni ndogo sana,  unajenga kitu kidogo, wakati chini kuna thamani kubwa…sasa unataka kuipata hiyo thamani, unasikia, hii ni mali ya mtu fulani, ….lakini wakija wazungu watapewa , mtafukuzwa kama sio kwenu…hilo mtanikumbuka mimi..

‘Sasa kwa hali kama hiyo utafanyaje,…hebu niambie muheshimiwa hakimu, utafanyaje ili uweze kumiliki eneo hili na kuliwekeza kwa ajili ya vizazi vyetu…ukae kimiya waje wakuja walichukue, au uondoe huu uzumbuekuku,ikibidi hata kama ni kuua, basi..’akasema huku akiweka ngumi shavuni na kukunja uso kuashiria uchungu mwingi.

‘Hebu niambieni, Wenzetu mataifa makubwa wanafanya nini, wakigundua kuwa kuna watu wana mali, lakini hawajui kuzitumia, wanatafuta njia ya kuingia,… wataingiaje kwenye eneo hilo , wanatafuta kisingizio hata kugombanisha makabila, dini  nk,..nia na lengo lao lipo mbele, ujanja kidogo, utapeli, kidogo, na ikibidi kama sisi tunatumia njia hiyo ya kuwaaogopesha watu, uchawi, huo ndio udhaifu wetu, unautumia uchawi kidogo,baadaye watu wanagombana, wanashutumiana, na wewe unapata mwanya wa kupenya na unakuja kumiliki…, lakini kwa ajili ya vizazi vyetu….

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, nafahamu hamtanielewa, hasa wewe mwenyewe uliyekariri vifungu, na kujifanya unatetea haki, haki gani bwana, au unataka nifichue siri yako…tunajidanganya sana, lakini ipo siku mtaumbuka, …muheshimiwa tumia akili yako, kwanini ukariri vifungu vya kuikandamiza nchi yako, huoni hayo yalitungwa na wakoloni….., lakini akija mzungu hapo, hivyo vifungu havifanyi kazi….mimi naumia sana, kwanini…kweli usilolijua ni kama usiku wa giza…’akainama kwa muda na alipoinua uso, akamwangalia wakili mwanadada, na kusema;

‘Nawaomba, msinipotezee muda wangu, muamue moja, kuniua, au kuninyonga, au mniachie huru, nikafanya vitu vyangu tuokoe rasilimali ya nchi yetu, asilia yote hii itauzwa, na wewe mwanadada, nawenzako mtabakia kulinda haki isiyo hakikika…wenzetu watakuja wataichukua hiyo haki na kuipeleka kwa vizazi vyao….

‘Kwahiyo kwa muhutasari ndio hayo, sasa ili twende sawa nataka uniuliza maswali yenye kichwa, ilikuwaje, nitawaelezea,  kwanini nilifanya hiki, kwa nani…, nitakuelezea, ila mwisho wa haya nataka muamue moja, mniue, au mniachie nikalinde asili ya mababu zetu….muamue kipi bora, na ipo siku mtanikumbuka…’akamwangalia mwanadada, huku akiwa kakunja uso kama anatafakari jambo na mwanadada akawa naye kamkazia macho, akiwa kama anamshangaa, na ikapita kitambo kukiwa kimiya

NB: Huyu mtu ana kili au kachanganyikiwa…..?


WAZO LA LEO: Elimu ya nchi yetu ni ya kurithi, ikiwa na taratibu ambzo ziliwekwa na wakoloni, na huenda zilikuwa na lengo maalumu, sio la kutoa wataalamu, bali watekelezaji tu au wanyapara. Inabidi tujipange kivyetu, tuwe na mikakati yenye manufaa yetu, ya kupata wataalamu wetu, wazalishaji wetu, wabunifu wetu..

Hilo ni wazo tu la leo,kutokana na huyo jamaa, anayejiita `mtaalamu’

Ni mimi: emu-three

No comments :