Mwanangu wakati
mwingine haki inaweza ikawa ngumu kuipata, lakini kama unafahamu kuwa ni haki
yako katu usikate tamaa,…itafute, kwani usipoitafuta wengine wanaweza kutumia
mwanya huo kukunyang’anya haki yako. Mimi ninawashukuru sana wote walihakikisha
kuwa haki yangu inapatikana, hasa mwanadada na kundi lake…’mama akaendelea
kumuhadithia mwanae.
Ni siku ambayo mwanadada alirejea kutoka huko msituni
walipokwenda kumtafuta mtaalamu, na wakati wanaondoka ilijulikana kuwa
wanakwenda kumuomba aweze kubainisha zile sumu mbili ni ipi iliyokuwa sahihi,
ili kuweza kuziwakilisha mahakami, ….
Na ilitajiwa kuwa haitachukua muda, masaa yalizi kwenda na
jioni ikawa inagia, na hapo kila mwenya laki akaanza kulitoa moyoni, na hata
mimi ilifikia muda nikakata tamaa kabisa hasa nikisikia maneni ya watu, kwani mengi
yalianza kuongolewa, hasa yakihusishwa na imani za huo msitu na mambo ya kishirikina
yaliyogubika hicho kijiji, eti kutokana na kesi yetu ilivyokuwa, wanadai eti mizimu
imeshakasirika eti kwa vile mimi mwanamke ninadai haki ambayo ilitakiwa idaiwe
na wanaume. Na wanadai kuna kiwingi cha popo,kimeonekana kikitokea milimani, na
hiyo ni ishara ya kukasirika kwa mizimu.
Na wakati nawaza hivyo, akanitembelea mama mkwe, na tukawa
tunaongea na yeye kama walivyokuwa akina mama wengine wenye umri kama wake,
akaanza kunilaumu. Ikabidi nianze kujitetea kwa kusema;
‘Kwanini mimi nisiwe na haki wakati hiyo ninayodai ni jasho
langu, ni pesa yangu niliyojengea hiyoo nyumba na duka, na kama tatizo ni
kujenga kwenye eneo la familia, au eneo la marehemu mume wangu, lakini mimi pia
ni mwanafamilia, mimi ni mzazi wa mtoto ambaye mnamtambua kama mwanafamilia…’nikawa
najitetea lakini ilionekana kama mimi naleta siasa mpya kwenye familia.
‘Mizimu inakasirika mwanangu, kwingi cha hawo ndege, sijui
ni ndege au ni wadudu, kimeonekana kikitokea milimani, hiyo ni ishara mbaya,
hii inabashiria jambo baya limetokea,…na wengi wanahisi ni kwa vile wewe
unataka kumiliki mali kama mwanamke, unataka kumiliki kitu ambacho ni wanaume
tu wanastahili kumiliki, na pili wewe ulitakiwa urithiwe na mmoja wa
wanafamilia ukakataa kwa vile unajiona unajiweza….mwanangu mimi kama mama mkwe
wakp nakuomba ujirudi’akasema mama mkwe huku akiniangalia kwa wasiwasi, kama
vile mimi ni kitu cha kuogofya.
‘Nikuulize mama yangu, mfano hiyo familia isingelikuwepo,…hawo
wanaume wakunirithi wasingelikuwepo, mimi nilitakiwa niweje, nikae tu, au nisimame
barabarani niwe naomba,….?’ Akauliza.
‘Hayo ni mambo mengine, yanakubalika kama hali hiyo ipo,
lakini hali kama hiyo haipo, wanafamilia wapo, wanaume wa familia wapo, kwanini
ufikirie kitu ambacho hakipo,…nikuambia ukweli, wakati mwingine tusiwe na
kiburi cha ubinafsi, kumbuka unapoolewa unatakiwa utii amri za hapo ulipoolewa,
usilete mambo uliyokuja nayo…wazazi wako hawakukufunda kwa hilo, mimi sizani
kuwa hawakukuelezea, ni kiburi chako tu….’akasema huyo mama.
‘Mama sijakataa mambo ya kifamilia, sijapinga mambo ya
kifamilia, ila ninachotaka ni ile haki yangu, kama ulivyoona, sikutakiwa niseme
nyumba hiyo nimejenga kwa pesa zangu wakati kweli nilijenga kwa pesa zangu,
sasa imejulikana ukweli, kuwa nilijenga kwa pesa zangu, na nilijua kuwa nyie
kama akina mama, wanawake wenzangu mungeniunga mkono….’akamwangalia mama huyo
kwa macho ya huruma na mama huyo akatikisa kichwa kukataa.
‘Haki hiyo haipo….nielewe…haki ni yako na mume wako, na haki
hiyo umefungwa ndani ya mamlaka ya mume wako,….mbona ni kitu kidogo tu cha
kuelewa…..’akasema huyo mama akionyesha kukunja uso.
‘Mama hivi ni kweli,…unaamini hayo, hivi ni haki na kweli
kuwa sisi wanawake, hatutakiwi, kudai haki zetu hata kama ni haki yako
kiukweli, …mimi naona kuna walakini hapo, kama mzazi, baba wa watoto hayupo,ni
nani anastahili kuchukua nafasi yake, ….lakini hata hivyo, hapo sidai kitu cha
mtu,ninachodai ni kile change, je ni kweli kuwa mwanamke hastahili kumiliki
kilicho haki yake,…ndivyo mila inasema hivyo, sio kwamba ni mbinu za watu
wachache wanaotaka kunufaika na jasho la watu wengine….?’ Akauliza mwanamama.
‘Tatizo lako wewe ndio mnaojiita kizazi kipya, hatukuwezi…mbishi
na una kiburi, na tabia kama hiyo kwenye ndoa haifai, …haifai kabisa, sisi
wenzako tumeshaanza kukuogopa kuwa unatuletea vurugu kwenye familia, tangu
uolewe kwenye familia yetu, hatuna amani
, kila siku unaongelewa wewe, sasa hebu angalia mabalaa ya msiiba
inavyofululiza kwenye hii familia, hatujui itatokea nini tena huko, na mguu
wangu huu ulikuja kukupa taarifa nyingine mbaya…’akasema na mwanamama
akashituka
‘Taarifa gani tena hiyo mama, mungu wangu, isije ikawa ni
ile ndoto…’akasema huku akishika kichwa kuashiria wasiwasi.
‘Ndoto gani, ..unaonaeee, hiyo ndio mizimu imekasirika, na
inataka kutuadhibu, tunachoombea ni mtoto wetu huyo apone, lakini kama
hatapona, hatuna budu kuchukua hatua kubwa zaidi, ili mkosi huu uondoke kwenye
familia yetu…sisi akina mama wa familia itabidi tuingilie kati, maana
utatumalizia watoto na waume zetu.’akasema huyo mama
‘Lakini kuna nini mama, mbona umefika na mambo mara ya mzimu,mara sijui apone, kwani ni nani
anaumwa? ….’akauliza na kumwangalia mama huyo na mama huyo akawa kaangalai
pembeni kama vile anakwepa kumwambia huyo mama, kuashiria ni taarifa ya
kutisha.
‘Mama kuna nini, mbona hutaki kunielezea hiyo taarifa, kuna
nini , maana jana usiku niliota marehemu mume wangu kaja, akiwa amelowana damu,
na kuniamba kuwa niende nikampokee shemeji yangu kituoni…’akasema
‘Ndio hay o hayo, unaona mpaka unaletewa ishara na marehemu
mume wako lakini hutaki kuamini…damu maana yake ni nini, sio baalaa hilo…’akasema
huyo mama, akasema akimwangalia mwana mama kwa macho kama mtu aliyeona kitu cha
kuogofya.
‘Basi nikashangaa, na kumuuliza mume wangu,…marehemu, ….mbona
mwili wako umejaa damu, kuna nini kimekutokea, …yeye akawa hasemi na alikuwa
kasimama kwa mbele yangu, na nilipomuuliza hivyo, akainama kujiangalia,akawa
kama anajishangaa, na kusema, mmh, ina maana damu hizi kanipaka ndugu yangu, …akageuka
kurudi huko alipotoka, nikawa namuita ili anifahamishe zaidi lakini hakugeuka
akatoweka, na mimi nikashituka kutoka usingizini…’akasema mwanamama.
‘Hiyo ndoto mama…binti yangu, hiyo ina ishara mbaya, ni
mumeo alikutembelea kukupa ujumbe,…,kama angelikuwepo mtaalamu angekuagulia, angeitafsiri
vyema hiyo ndoto,….lakini mtaalamu katoweka, nasikia alikuja mahakamani, na baadaye
akasema anarudi kwa mizimu, I wanasema , kasema kuwa anatumikia kifungo kwa
kukiuka baadhi ya masharti,…sijui mimi siamini hayo, yule mtu ni mtaalamu
kweli, anasaidia watu, leo hii anasingiziwa ubaya….kama kuna kifungo, basi,
tunamuombea amalize hicho kifungo, ili aje kutusaidia…’akasema huyo mama.
‘Huyu mtaalamu alivunja masharti au alikuwa ni tapeli tu, hivi mama
kweli nyie mnamuamini huyo mtu, hamuoni kuwa ndio yeye aliyewapandikiza watu
fitina kuwa mama mkunga ni mchawi, wakati sio kweli, je hizo ndizo kazi zake,
hilo mumeliona, …'akasema na huyo mama akawa anamuangalia huyo mwanamama kwa macho ya dharau.
'Mama hebu jiulize ni mangapi aliyoyafanya ya hadaa ambayo hamjaambiwa,…Huyo atakuwa kahusikia
na mambo mengi mabaya, pale mahakamani alikwua akijikosha tu…mimi simwamini
hata chembe…’akasema mwanamama na yule mama akawa anamwangalia mwanamama kwa
mshangao, na akainuka haraka.
‘Wewe mtoto, mbona wataka kutuletea balaa, unaongea kitu
gani, hivi unamfahamu huyo mtaalamu, kila mnachoongea ndani, anakifahamu..hata
kama unateta na mume wako chumbani kwa siri, kesho yake anakujia na kuwaambia
yote mliyokuwa mkiongea wewe na mume wako…ole wako, ndio maana tunataka uondoke
kwenye hii familia, kwani utatuletea majanga…wewe sio mtu mwema, kabisa,….’akasema
‘Ndivyo mlivyopanga hivyo…ndivyo mnavyojidanganya ehe…?’
akauliza mwanamama.
‘Wewe kuondoka haijapitishwa bado,…tulikuwa tunasmubiria
huyo mwanasheria aje aitishe kikao, na sisi tutalitoa hilo hadharani, …lakini
sasa unaona, kwa vile huyo kawa kiongozi, na anaukaribu na wewe, mabala
yamemtokea, mkosi, …wewe mume hatakiwi akuguse,..sasa tunakuambia, kama
mwanasheria atafariki, basi, hatuna budi kufanya hivyo..tutakufukuza…’akasema
‘Kama mwanasheria atafariki, kwani vipi, kwani anaumwa….mbona
alikuwepo mahakamani akiwa na afya yake…?’ akauliza mwanamama kwa mshangao.
‘Mguu wangu huu ulikuja kwako kukupa hiyo taarifa, kuwa
mwanasheria kaletwa kutoka msituni akiwa hajitambui, kapigwa risasi, ….na hali
yake ni mbaya sana, na madakitari wanahangaika kujitahidi kama wanaweza kuokoa
uhai wake, lakini inavyosadikiwa ni kuwa keshafariki, hayo mengine ni kupoteza
muda tu na hiyo ndoto yako, mmh, naona ni hayo hayo..’akasema huyo mama na
mwanamama akashika kichwa, akakaa chini, akasimama ….
‘Yupo hospitali gani?’ akauliza mwanamama
‘Unauliza hospitali gani, itakusaidia nini wewe, wakati wewe
ndio mkosi wa familia, enenda huko ulipotoka, utuachie familia yetu, tangu
uolewe hapa umekuwa ni gubu, tatizo,nuksi, hujioni….tunakuomba sana, kabla
mambo hayajawa mabaya zaidi ufungashe uondoke..tuachie mjuukuu wangu maana huyo
ni damu yetu, mimi sitashindwa kumlea…wapo akina mama zake wadogo watamlea…’akasema
huyo mama, na mwanamama alikuwa hamsikilizi.
Mwanamama akawa anajiandaa kuondoka kwenda huko hospitalini
hakutaka kumsikiliza huyo mama tena, alikuwa anataka kwenda kujionea mwenyewe
au kusikia ni nini kimetokea kwa shemeji yake huyo.
‘Oh, samhanai mama, mimi inabidi niende huko hospitalini, ..’akasema
mwanamama
‘Nakuuliza ili ukafanye nini, …kwani wewe ni dakitari, wewe
ni mkosi tu, unachopeleka huko ni kilio, ambacho tunakisubiria muda wowote
kitatangazwa, na hiyo kesi yako itaahirishwa, na ukiendelea nayo tena, janga jingine
litatokea,…wewe mwanamke huna jema katika familia hii, ndio maana nimekuja
kukushauri kwa nia njema uondoke…’akasema huyo mama, na kabla hajamaliza mlango
ukagongwa.
Mwanamama akainuka haraka na kwenda kufungua mlango, na
macho yake yakatua kwa mwanadada aliyeonekana kuchafuka na nguo zina alama za
damu, alikuwa kachoka, na macho yake yalikuwa kama yamevimba, kama mtu
aliyekuwa akilia, ..
‘Kuna usalama huko?’ akuliza yule mama alipoona mwanadada
akiingia akiwa kachoka.
‘Usalama upo, msiwe na wasiwasi, sasa hivi mambo haya yanakwisha,….kila
jambo baya lina mwisho wake, cha muhimu ni sisi sasa kuungana kwa pamoja, na
kuwepo kesho kwa wingi mahakamani, lakini kwa jinsi ilivyo , huenda kesho kesi inaweza isifanyike….tumeshapeleka maombi, kwani
kuna mambo mengi ya kufuatailia, ikiwemo ushahidi mpya na muhimu uliopatikana
huko msituni..’akasema mwanadada akijipweteka kwenye sofa.
‘Ushahidi gani tena, kwani mwanasheria alipigwaje risasi na
huko msituni hakuhitajiki kutumiwa silaha?’ akauliza yule mama.
‘Yaliyotokea ni bahati mbaya, lakini ni katika kumkamata huyo mhalifu wetu, na mwanasheria alijitolea
mhanga, na ndipo ajali hiyo ikamkuta, lakini haikudhamiriwa iwe hivyo…’akasema
mwanadada akimwangalia huyo mama.
‘Yote hayo ndio mikosi yenyewe niliyokuwa nikimwambia huyu
mwenzako,… ndio maana nilikuwa namshauri huyu mwenzako, kabla hali haijawa
mbaya zaidi, yeye ni bora aondoke, atuachie maisha yetu ya amani, kwani tangu
afike kwenye hii familia ni mikosi…angalia hayo yanayotokea sasa..hamuoni hilo
jamani….’akaana kubwabwaja huyo mama, na mwanadada akamkatisha na kusema;
‘Wewe mama, huyu mwanamama, hana mkosi wowote, ingelikuwa
unaufahamu wa mbali ungelimshukuru sana huyu mwanamama,ungelikuwa una maono ya
mbali, ungesema asante mungu umetuletea nuru, huyo mwanamama ndiye nuru ya familia
yenu, kwani kutokana na yeye mtaweza kufahamu haki zenu, zilizokuwa zimeanza
kutekwa na mjanja mmoja…’akasema mwanadada.
‘Nakufahamu sana wewe, huwa unajiona umesoma, unajifanya
unafahamu sheria, sheria na mizimu wapi na wapi…wao wana sheria zao,….huwezi
kuwaangilia, …sikilizeni niwaambie, hamtafanikiwa kamwe….kwa mtaji huo mtaishia
kubaya…..’akasema huyo mama akiinuka kutaka kuondoka, na akawa kama kakumbuka
jambo, akauliza;
‘Na unasema huyo mwanasheria keshafariki au …ndio
mnajidanganya kuwa atapona kweli…nasikia alishakata kauli, wakati analetwa,
ilibakia kupewa maji tu…hawo madakitari wanachotaka ni ushahidi tu, ili kazi
yao ionekane…’akasema huyo mama, na mwanadada akamwangalia huyo mama kwa jicho
baya na kusema;
‘Wewe mama, ningeliongea vibaya kama usingelikuwa mama mkwe,
mama chunga sana mdomo wako, jaribu kuwa na hekima, jaribu kutuliza moyo wako,
na kuomba heri badala ya shari,…kumbuka japokuwa hujamzaa wewe lakini huyo ni
mwanao, hukustahili kuongea hivyo…kwanini unamuongelea mabaya,unajua mama
mabaya mengine tunajiumbia sisi wenyewe
bila kujua, huu sio wakati wa kuongea mambo kama hayo,….yule sasa hivi yupo
kwenye mikono ya madakitari, na wanafahamu kuwa anaweza akapona, tunachotakiwa
ni kumuombea apone,….’akasema mwanadada akijaribu kuzuia kutoa kilio.
‘Haya yetu macho, ila narejea kuwaonya, sisi ni akina mama
tunametoka mbali, na tunafahamu sana mambo ya hapa,, nyie mumekuja juzi juzi tu
hapa, hamjui vyema hii miji yetu hamjui mambo ya kimila, msipotulizana,
mtaishia kubaya…na ilivyo, mwenzenu huyu ana mkosi, ana nuksi, …’akasema
akianza kuondoka.
‘Sio kosa lako mama, ni kosa la elimu, ambayo imekuwa adimu
hapa kijijini, ni kosa la wajanja walioamua kutumia udhaifi wenu huo,
kuwapandikiza fitina na kuwajaza hofu. Watu hawo ni wabaya kuliko hata huyo
mchawi mnayemzania kuwa yupo, hakuna mchawi, mchawi ni nyinyi wenyewe…’akasema mwanadada na
yule mama akasimama akiwa kaweka mikono kiuononi.
‘Unasema nini wewe binti, hebu rudio huo usemi wako tena,
kuwa eti kuwa sisi ni wachawi,…’akasema huyo mama akiuma meno kwa hasira….
‘Mama naomba unielewe, labda
natumia lugha ngumu kwako ambayo unashindwa kunielewa, nasema hivi, hapa
kijijini hakuna uchawi, hakuna kulogana, hizo ni hisia mlizopandikizwa kiujanja
na huyo mnayemuita mtaalamu, ..kama ni mchawi , basi huyo mnayemuita mtalaamu, ndiye
anayestahili kuitwa mchawi,..huyo ndiye mchawi wenu’akasema mwanadada akiinuka
kutaka kwenda bafuni kuoga.
‘Mhh, nyie watoto nyie, …mbona mnaleta balaa, hizo kauli
zenu zinanitisha, na naona ni bora niondoke hapa haraka msije mkaniangaiza na
mimi, oooh, jamani kizazi hiki kina nini, hivi mnamfahamu nyema huyo mtaalamu,
au mnamsikia tu…?’ akawa kama anauliza na mwanadada akasema
‘Tunamfahamu sana, yeye ni jambazi, tapeli, na mwizi, na
kama ni mtu anayestahili kuitwa mchawi, basi huyo ndiye mchawi wa hiki kijiji,…..amekuwa
akiwatapeli, kuwahadaa, na kuwapuambza kiakili, na hilo tumalithibitisha na
yeye kakiri mwenyewe, na yupo tayari kuelezea kila kitu, mahakamani, maana za
mwizi ni arubaini, na mwisho wa ubaya ni fedheha tu,…’akasema mwanadada
akisimama na kumgeukia mwanamama, akasema
‘Mwanamama nakuomba ujitayarishe, tunakwenda hospitalini,
nasikia mgonjwa alipata fahamu kidogo, akaomba kuwa twende ana mazngumzo na
sisi, ni muhimu sana….’akasema na mwanamama ambaye bado alikuwa na mshituko
akasema;
‘Mimi sina cha kujiandaa zaidi, …nipo tayari twende….’akasema
‘Huyo anawaita kuwaaga…ndio safari hiyo, oh, mwanangu jamani…’akasema
na kujifanya analia, huku anaondoka
NB: Mbona hitimisho linakuwa mbali.
WAZO LA LEO:
Uwoga ni udhaifu wa akili, na ukitawalia na hisia hizi za uwoga, kuogopa, mambo
yasiyoonekana kama uchawi, na mamo kama hayo, utashindwa kufanya mambo ya
maendelea,wakati mwingine, kwa udhaifu huo, tunageuka kuwa wachawi wenyewe, na
kujiloga wenyewe, kwa kujiumbia matatizo, …..cha muhimu, ondoa hisia hasi, na
jenga muelekeo chanya, kuwa inawezekana, na nitafanikiwa…huku ukijibidisha
katika kutafuta mambo ya heri.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment