Hapa mwanadada
anaelezea jinsi ilivyokuwa baada ya kuingia kwenye msitu, ulikuwa msitu mnzito,
uliojaa wadudu, wanyama na hisia za kutisha, na wengi huwa hawapendi kuingia
ndani ya msitu huo au kusimulia habari zake kutokana na historia yake, kuwa
kulikuwa na vita nyuma na watu wakakimbilia hapo, kujificha na wengi wakapotea humo
kabisa.
‘Huku kuna mambo mengi ya kutisha, historia inatuambia
mababu zetu waliokimbia vita, au wale waliokimbia kodi walikuja kujificha huku,
na kujenga mahandaki, …kama mnavyoona haya ni mahandaki, zilikuwa nyumba za
mababu zetu…..’akawa anasimulia huyo jamaa ambaye ndiye kiongozi wa msafara
akionyesha baadhi ya mashimi yaliyokuwa yameanza kujifukia.
‘Mimi mwenyewe nilizaliwa huku, kabla wazazi wangu
hawajahama, na kukimbilia huko uraiani, wazazi wangu wanasema walikuwa
wakionywa kuwa wasije wakahama na kwenda huko uraiani, waliambiwa kuwa wakihama
huku na kuja kuishi huko uraiona tutauliwa, kwani watu wa huko ni wakatatili,
wauwaji …lakini vijana hawakusikia wakati huo wazazi wangu walikuwa bado
vijana, wanatoroka mmoja mmoja, na kubakia
wazee….’akaendelea kusimulia.
‘Wazee wakabakia bila watu wa kuwasaidia wakawa wanajifia
ndani ya mahandaki, hadi kizazi hicho kikapotea kabisa na ndio maana
inasadakiwa kuwa kwenye mahadaki hayo kuna mizimu, mizimu hiyo ndio hawo mababu
waliojifia wenyewe wakiogopa kutoka nje….’akasema.
‘Kwa mfano kule tulipotoka, wale sio wanadamu wa
kawaida…’akasema na hapo mwanadada akaona aulize.
‘Lakini mbona wanaongea kama sisi…’
‘Ndio wanaweza kujigeuza hivyo, ..lakini hawana maisha kama
yetu,…na niwaambie ukweli wapo mizimu wazuri na wabaya,hawo sasa hivi ni
mashetani,…sio watu kama wale tuliokuwa tukiwajua, ukikumbana na hayo
mashetani, yanaweza kukuzuru kama ni yale yenye tabia chafu…’akasema huku
akiendelea kunyunyuzia vitu kama unga kila walipopita…na kuzuia upepo, ambao
ulikuwa ukija, na kuondoka,na baadaye akatulia na kuangalia huku na kule,
akatikisa kichwa na kusema;
‘Huku sasa hakuendeki, naona mambo magumu,…sijui tumepotea,au
haturuhusiwi kuendelea mbele, naona ujuzi wangu wa zidi ya hapa sina, lakini
twendeni,…..’akasema yule mtu huku akijitahidi kuuzuia ule upepo na usinge
wake, na akiwa kama kashikilia kitu kizito mkononi mwake,
‘Sasa tufanyeje?’ akauliza mwanadada alipoona yule mtu
anakuwa kama kabeba mzigo mzito, misuli imemtuna na jasho linamtoka
‘Sijui…sikuwa nimefikiria hili kabla, nilijua ni jambo
rahisi sana kwa vile niliwahi kuishi huku nikiwa mtoto mchanga, na nahisi kuwa
wakioniona wanaweza kunikumbuka na kunionea huruma maana ni damu yao….hata
hivyo, nina imani kuwa hawataweza kutuzuru, tusonge mbele kidogo…tukikwama
basi,hakuna jinsi itabidi turejee huko tulipotoka…’akasema
‘Kwahiyo, ina maana wao wanakufahamu wewe…kwanini usiongee
nao?’ akauliza mwanasheria
‘Wananifahamu, nay a kuwa damu ni nzito kuliko maji,…lakini
nahisi damu, nahisi ubaya mbeleni, kuna kitu ambacho sio cha akwaida,kilitendeka,
sijui ni miongoni mwetu, au….hapa sasa inahitajika…maombi ya ziada, na kama
kuna mmoja wetu ana damu ya mtu, kama kuna mtu mbaya bora aondoke…’akasema huyo
mtu, na mara ule upepo ukatulia, na huyo mtu akaangalia tena huku na kule;
‘Naona mababu wametusikiliza kilio chetu, haya twendeni
haraka kabla huo upepo haujarudi tena, huo sio upepo, kama mnavyohisi, ni kundi
la mizimu, limekuja kutuangalia sisi ni nani, na wamegundua kuwa sisi sio watu
wabaya, …hata kama yupo mwenye ubaya, sio mbaya wa kutishia amani yao.’akasema
‘Kwanini tusilimalize hilo kundu kwa risasi?’ akasema mmoja
wa watu waliokuwepo kwenye huo msafara.
‘Usije ukajaribu kitu kama hicho…huoni wamegundua dhamira
yetu, ndio maana wameondoka, kwanza walikuwa wanatupima, kama tutafanya
fujo….wakagundua kuwa hatuna ubaya, ila nahisi kuna kitu kibaya kipo maeneo
haya….’akasema huyo mtu na walipofika mbele, wakaona msitu umefunga kote.
Kulikuwa na aina ya mimea iliyoota kama kamba, ikatanda kama
nyavu, kiasi kwamba huwezi hata kupitisha mkono, na aina ya miti yenye miba
mikali ilikuwa imesheni kila kona, hapo yule mtu akawa anahangaika huku na
kule, kutafuta upenyo, lakini kulikuwa hakuna hata sehemu ya kuingiza mkono.
‘Tukiweza kupita hapa, basi tumeshafanikiwa…tutakuwa
tumeingia sehemu ya watu wa zamani ambao ni wema, wanaweza kutusaidia’akasema
‘Basi tufyeke?’ akauliza mmoja wa watu waliokuwepo
‘Panga halikati hapa..wewe unaona ni majani lakini ni zaidi
ya majani, …’akasema huyo mtu, na hapo hapo akatoa kitu kama unga na kuanza
kunyunyuzia kuzunguka yale majani, na mara ukatokea moshi, ukatanda hewani, na
ghafla kukatokea kitu kama mngurumo, au radi,…ilikuwa kali mpaka watu wakawa
wanaziba masikio
Ule mngurumo ulipokwisha, mara yalemajani yakawa kama
yanasogea, kama vile mtu anafungua mlango, na kukawa kunatokea barabara,
inayoelekea mbele,..
‘Sasa tunaingia miji ya watu,….tuwe makini, usikanyage kitu,
usiokote chochote, ….tembea kunifua mimi ninavyotembea…’akasema huyo mtu
akinyata na kuruka pale alipoona kitu, na sisi tukawa tunafanya hivyo…’akawa
anaendelea kusimulia mwanadada,akimsimulia mama yangu ambaye alikuja
kunisimulia hiki kisa ninachowahadithia….
Na wote wakawa wanamfuatia nyuma,…. nyuma hatua kwa hatua
hadi wakatokea kwenye mapango,…mapango hayo yalikuwa mengi, na ilionyesha kama
nyumba za watu, kwani sehemu ya kuingilia ilikuwa kama inatumika, …
‘Kazi iliyobakia ni kulitafuta pango letu…’akasema na kuanza
kunyunyuzia tena ule unga unga, na alipomaliza kukatokea sauti za kama watu
wanaongea , sauti nyingi kisai kwamba huwezi kujua wanachoongea ni nini, lakini
hakuna mtu aliyeonekana, na huyo mtu akasema
‘Hodi waungwana, tumekuja, sisi ni wageni wa mtu wetu,
anayeitwa mtalaamu, je tumemkuta?’ akauliza na zile sauti zikanyamaza na mara
kwenye moja ya pango, kukatokea mtu wa ajabu, uso wake ulikuwa kama upo kwenye
giza, yanaonekana macho tu na na kumeta meta kama anawaka moto….
Yule mtu alikuwa kashikilia fimbo ndefu nyembamba, na akawa kasimama tu,na uso ukawa anafunikwa
unafunuka, na macho yakawa yanatuangalia , kama vile yanatusoma ndani ya mioyo
yetu, akaonyesha ishara, ambayo
hatukuijua ile huyu muongozaji wetu akatuabia kuwa tumeambiwa tumfuate, na wote
wakafanya hivyo, hadi pale kwenye mlango wa lile pango,….na yule mtu, au uso wa
mtu , kwani kiwiliwili kilikuwa hakionekani, akaonyesha ishara, na huyo
muongozaji akasema tumeambiwa tuvue viatu, na wakafanya hivyo na kubakia miguu
mitupu, na halafu akaonyesha ishara ya kuwa waendelee kumfuata kuingia ndani ya
lile pango.
Mwanadada, anasema walijikuta wakiingia kwenye hilo pango,
na kulikuwa na kitu kama milango mingimingi, na mlango mmoja ukafunguliwa, na
hapo wakajikuta wapo kwenye sehemu kama chumba kikubwa kiasi……ilikuwa ni nyumba
iliyonakishiwa na udongo, kama vile ukuta uliowekwa maru maru…..za rangi mbali
mbali….na kwa mbele yao kulikuwa na milango mingi na hawakujua kitafuata nini
baadaye
Mara ikatokea fimbo, ilikuwa ya yulee mtu akaelekea kwenye
mlango mmojawapo uliokuwa mbele yao, na ile fimbo ikagusa na ule mlango
ukafungua, na yule mtu wao muendeshaji wa huo msafara, akawaambia wameambiwa
waingie na walipoingia wakajikuta kwenye
eneo pana kama ukumbi, ukumbi usio na viti wala meza, lakii cha ajabu kulikuwa
na harufu za vyakula kama hotelini.
Walipogeuka nyuma hawakuona mtu , na ile sura iliyokuwa
ikiwaongoza, yenye fimbo haipo tena, wakatulia na mara wakasikia sauti ikisema
‘Karibuni wageni…tuwasaidie nini’sauti ikasikika bila
kuonekana mtu
Mwanadada akasema kwa jinsi alivyokuwa kachoka alitamani kusema
anahitaji chakula na maji lakini akasita, akikumbuka kuwa walipewa tahadhari ya
kutokushika chochote mpaka watakapopewa maagizo, na yule mtu waliyeongozana
naye, kapiga magoti na kusema
‘Waungwana tuna shida, tunamtafuta mtu wetu anajulikana kama
mtaalamu, …
‘Mtaalamu,..huyu mtu sio mtu wa huku kwetu, …hatumjui’hiyo
sauti ikasema na kukapita kitambo kidogo.
‘Lakini katuambia yupo huku, akiwa kwenye mateso kwa
madhambi aliyoyafanya….’akasema huyo muongozaji wetu.
‘Hatuwezi kumkaribisha mtu kama huyo huku kwetu, mtu huyo
anaonekana ni mchafu, mikono yake imejaa damu,….huyo atakuwa anaishi sehamu
nyingine za walio hai,..lakini sio huku kwa wafu wasio na mdhambi…’akasema hiyo
sauti.
‘Tunaomba utusaidie, ili tuweze kumpata’akasema huyo mtu.
‘Nendeni na n jia ileee, mtafika sehemu
alipojificha,…’akasema na mara ikaonekana kitu kama njia, na ile sauti
hakusikika tena, na akina mwanadada na wenzake wakabakia wenyewe, na yule mtu
wao muongozaji, akasema
‘Twendeni….’na wote wakafuata ile njia na haikuchukua muda,
wakajikuta wapo nje kabisa ya hayo mapango, na kujikuta kwenye nyika, sehemu ya
kawaida, na hata walipogeuka nyuma hawakuona kitu zaidi ya yale majani
yaliyojitanda kama nyavu.
Mara kwa mbali wakasikia kitu kama mngurumo wa pikipiki, na
wote wakaambiwa wajifiche, na ile pikipiki, ilipofika pale walipokuwa
wamesimama mwanzoni, yule mwendeshaji akashuka na kuvua kofia, hapo ikasimama
kwa muda, kama anawaza jambo, akaangalia
huku na kule, na alipohakikisha kuwa yupo peke yake, akainama na akainua majani,
yale majani yalikuwa kama mkeka uliotandazwa, na chini yake kulikuwa na mfuniko
kama ile ya matanki makubwa, kumbe pale kulikuwa na mlango, na mara yule mtu
akalisogelea lile pikipiki lake na kulisogeza hadi kwenye ule mlango, akawa
analiigiza lile pikipiki, na alipomaliza kuliingiza yeye mwenyewe akaingia.
Na yale majani yakawa yanavutika kidogo kidogo hadi
yakafunika eneo lote na kuwa kama kawaida, huwezi kujua kuwa kuna kiu kama
hicho…
‘Mumeona, ….hapo ndipo anapojificha mtu wetu…’akasema huyu muongozaji.
‘Lakini yule ni nani?’ akauliza mwanasheria
‘Hahahahaha..ina maana mumeshamsahau mtu wenu , yule ndiye
mtaalamu, ..keshajibadili, ..kuanzia siku alipoondoka pale mahakamani,
alijibadili, kwa kuvua yale manguo aliyokuwa akivaa, na ngozi ya kichwani ambayo
ilikuwa na ndevu ndefu…sasa hivi anafanana na ……’akasema na kusita kidogo
‘Anafanana na kiongozi wa kijiji…’akasema mwanadada, na wote
wakageuka kumwangalia mwanadadam na mwanadada akasema
‘Nyie hamukumwangalia vyema alipovua lile kofia, kwa vile
mlikuwa mkiogopa, mimi nimeweza kumwangalia sura yake, anafanana kabisa na
kiongozi wa kijiji, utafikiri mapacha…’akasema mwanadada.
‘Kwani hawa watu wawili ni mapacha?’ akauliza mwanasheria.
‘Hapana sio mapacha, lakini ilitokea kufanana sana, kila
mmoja ana mama yake, ila baba yao ni mmoja, na kila mmoja kachukua tabia ya
mama yake…’akasema huyo mtu wao.
‘Sasa tufanyeje?’ akauliza mwanadada.
‘Kwanza na ni muhimu, huku hakuruhusiwi kupigana kwa risasi,
milio ya bunduki hairuhusiwi eneo hili,…kwahiyo kinachotakiwa na kutafuta njia
za kumkamata, sina uhakika huko ndani kupoje, …’akasema huyo mtu.
‘Sio kama huko tulipotoka..?’ akauliza mmoja wa watu wa
usalama.
‘Hapana, kule uliona kulivyokuwa, kule sio kwa
kawaida,..yale ni makaburi….’akasema na watu wakashangaa, nay eye hakusema
jambo jingine akawa ananyunyuzia unga
unga hewani, na baadaye katulia.
‘Hapa sio eneo la mizumu….na eneo la kawaida, tu, kwahiyo
mtu wetu anaishi maisha ya kawaida
tu….’akasema
‘Tufungue tuingie….’akasema mmoja wa watu wa usalama..
‘Subirini….’akasema mwanadada alipoona ishara kwenye simu
yake, na ilikuwa ni meseji, ikimwambia kuwa mtaalamu haonekani kawapotea watu
wake.
Na yeye akawajibu kwa ujumbe wa maneno kuwa wameshaona wapi
anajificha, na anahitaji msaada wa maaskari
‘Tuelekeze wapi mlipo, tupo na askari wa kutosha,…’ujumbe wa maneno
ukasema na mwanadada akamsogela yule mtu wao na kumuuliza hapo walipo ni wapi
‘Waambie tupo milimani,kwenye mapango ya watu wa kale,
wakifika waache mapikipiki yao kwenye mwanzo wa milima, hakuhitajiki kelele za
mingurumo au milio ya bunduki, na wafuate njia ya kale, watafika sehemu ambayo
tutawapa ishara, na watatuona wapi tulipo…’akasema na mwanadada akaandika
ujumbe
‘Mbona tupo karibu na sehemu hiyo…’ujumbe ukasema na
mwanadada akamwambia huyo mtu wao
‘Basi waambie wasubiri, ….’akasema na hapo akatoa ule usinge
wake na kuunyosha juu, na kupuliza mwanzo kwa nyuma kule anaposhika, na yale
manyoya ya ule usinge yakawa kama yanapepea angani..
‘Waambie waangalia hewani, wataona kitu kama mshale na
waufuate huo mshale unaoelekea angani…’akasema na mwanadada akaandika hivyo..
‘Sasa tuwasubiri wenzetu, na nina shaka, huenda huyu mtu
keshatuona…’akasema huyo muongozaji
‘Kwa vipi?’ akauliza mwanadada, na yule mtu akawa anaangalia
huku na kule, na kwa mbele akaona mtu mkubwa, na kusema
‘Baadhi waende kwenye ule mti wachunguze kuna nini, hayo
mnayajua nyie, sio utaalamu wangu…’ akasema na watu wawili wa usalama wakafanya
hivyo, na mmoja akarejea na kusema;
‘Kuna waya wa antenna, na juu uliokwenda juu kabisa kileleni
mwa huo mti, na mwisho wake kuna antenna ….inayofanya kazi, …’akasema
‘Mnaona hayo ni mambo yenu, kama mnajua jinsi ya kuizima
fanyeni hivyo haraka…’akasema na yule mtu akatoa simu yake na kuandika ujumbe
kumuelekeza mwenzake aliyemuacha huko, na baadaye ukaja ujumbe kuwa haiwezi
kuzimwa, labda ukatwe ule waya.
‘Anasema kwa juu huwezi kuizima, labda tukate huo
waya…’akasema
‘Basi fanyeni hivyo haraka…’akasema huku akiendelea kungalia
huku na kule
Yule mwanausalama anaondoka kumfuata mwenzake, baadaye walirudi
wote wawili na kusema waliona huo waya ukiwa umetoka ardhini, wakaufuatilia ,
na kukuta kweli huo waya umezama kwenda chini, na hata walipojaribu kuuvuta
haukuweza kuvutika….basi wakaukata.
‘Kama hakuna kitu kingine kama hicho, tutakuwa salama ,
hataweza kutuona, maana hana nguvu za misimu tena, huyo keshatengwa, anatumia
ujuzi wake wa kiaskari…’akasema
‘Kwani mtaalamu ni askari..?’ akauliza mwanasheria.
‘Ndio alikuwa askari, aliyeasi, na kufukuzwa, na aliporejea
akawa karibu sana na babu yake, na babu yake, upande wa mama yake, na huyoo
babu yake, ni mtu wa huku milimani, wakamuombea apewe mikoba, na ndipo
alipoapata huo ujuzi, japokuwa mizimu ilikuwa imeshaundua kuwa sio mtu mwema, …
‘Sasa kwanini walimpa hiyo mikoba?’ wakauliza
‘Ni ili iwe mitihani kwetu…ili haya yatokee, ili mjue kuwa
sio kila mtu anayeshi kwenye wema ni mwema,yeye ni chui aliyevaa ngozi ya
kondoo….mtakuja kumjua baadaye, ni ni mjnaja kweli kweli…’akasema huyo mtu.
‘Wewe umemfahamuje?’ akaulizwa.
‘Pamoja an kumfahamu katika hali ya kawaida, maana alikuwa
ni rafiki yangu kipindi tunatafuta dawa, tulikutana huku huku milimani, mimi
nahangaiaka na dawa na yeye halidhalika, tukapimana ubavu..maana haya mambo
yetu mkikutana ni lazima kupimana …tukagunduana kuwa sote ni watu wa njia
moja…’akasema
‘Tukawa tunakutana mara kwa mara…nilikuja kugundua kuwa
mwenzangu ana tamaa, …tamaa za ujana, na mimi sikuwa an tamaa hiyo, tulianza
kukosana, na kila mmoja akawa na maisha yake, na mimi nilihama kijiji hiki na
kwenda kuishi kijiji cha jirani, sikujua ni nini kilitokea, hadi
nilipoelelekezwa na mizmu…’akasema
‘Ulielekezwa kufanya nini?’ akauliza.
‘Kuja kumsaidia mama mkunga…’akasema
‘Kwa vipi?’ akauliza
‘Mama mkunga alitakiwa auwawe, kabisa, lakini haikuwa hivyo,
aliokoka kwenye ule moto,.na maji yaliyomwagika kutoka kwenye mtungi, maji yale
alikuwa akiweka kwa ajili ya kunywa, maji yale mara kwa mara alikuwa akiwapa
watoto mayatima, yalikuw aya baridi sana,…’akatulia.
‘Baraka za wema huo, zikawa zimejiweka kwenye ule mtungi, na
siku hiyo alipofikwa na janga hilo, baraka zile, ndizo zikatokea, na ule mtungi
ulipopasuka yale maji yalikuwa ya baridi sana, yakapooza ule moto, na kupunguza
ukali wake….’akatulia.
‘Kwahiyo kote kulizunguka moto, isipokuwa pale alipolala,
kwani yale maji yalikuwa yametiririka kumzunguka, …na alipozindukana akatembea
hadi msituni na huko akakutana na mimi, nikamweka hizo dawa, na majeraha
yakapona…’akasema.
‘Ngoja ngoja …mbona huyo mtalaamu alisema ni yeye alifanya
hivyo, akambeba na kumpelea porini…’akauliza mwanasheria.
‘Mengi aliyoyasema pale yana ukweli, kiasi fulani, lakini
aliyapanga yawe hivyo…ni kweli alifika akamuona akiwa kalala pale kwenye maji
machafu, aliyaona kama maji machafu, na alipomwangalia aliona kama
ameshakufa,…akaondoka’akasema huyo mtu.
‘Hatujakuelewa bado…’akasema
‘Huwezi kuelewa kwa ujanja wa huyo mtu, ambaye alikuja
kugundua baadaye kuwa huyo mama hajafa, na ni kipindi mizumu imeshaanza
kumsumbua, na alipouliza ni kwanini mizimu inamtenga akaambiwa, na hapo akaja
na uwongo huwo, alishagundua kuwa huyo mama yupo hai, na huyo mama hajui ni
nani aliyemtibia hayo majeraha yake…’akasema huyo mtu.
‘Kwahiyo hata huyu mama hajui kuwa ni wewe uliyemtibia?’
akaulizwa
‘Anafahamu…ila nilimwambia asiseme lolote kuhusu hayo
yaliyotokea hadi muda muafaka ukifika, atakuaj kwuasimulia mwenyewe yote hayo
mkimsimisha kutoa ushahidi…’akasema huyo mtu.
Mara sauti zikasikika na huyo mtu akatoa ishara kuwa
wajifiche, na baadaye wakatokea watu wa mkuu wa kituo idara ya upelelezi, na
walipofika pale wakawa wamesimama wakihangaika kutafuta wapi walipokuwa wakina
dada.
‘Tupo huku….’akasema huyu mtu wao, na wale watu walikuwa
tayari wametoa silaha kwa kujihami, na mwanadada akatokea, na wote wakakutana,
na hapo mipango ya kuingia ndani ya hilo shimo au pango ikapangwa,
‘Hatuna uhakika huko ndani kuna nini, je ana silaha, je, ana
watu wengine…’akasema mwanadada.
‘Silaha anaweza kuwa nazo, lakini anafahamu taratibu za huu
msitu, hataweza kuzitumia, anaweza kutumia silaha nyingine, kama sumu, ..amabzo
zinaweza kuwapofua, zipo kama tindikali, …ni hatari zaidi ya hizo
silaha,…’akasema huyo mtu wao.
‘Sasa tufanyeje…’akauliza mwanasheria.
‘Hiyo ni kazi yenu, hayo ni mambo yenu, mimi nimeshamaliza
kazi yangu,…naweza kuondoka…’akasema huyo mtu na mwanadada akasema
‘Hapana usiondoke tunakuhitajia sana, na nakuomba uwepo
mahakamani kutoa ushahidi…’akasema mwanadada.
‘Mimi utaalamu wangu unaishia hapa,…zaidi ya hapo, nitakuwa
nawadanganya, mambo ya silaha, na utaalamu wa antenna ni amabo yenu ya
kisasa…’akasema huyo mtu.
‘Tunakuomba tu uwe nasi, maana tukiwa na wewe , kwenye huu
msitu tunajisi amani, au kuna tatizo jingine linaliweza kukufanya usiwepo?’
akaulizwa.
‘Mizimu hainiruhusu kuingilia mambo ya huyu jamaa ,
nimeruhusiwa kisai hicho, …na baada ay hapo nahitajika kurejea kwangu, kama
mtanihitajia zaidi mtakuja kijijini kwangu, na jinsi ya kutoka hapa hamtapata
shida tena,…mtaongozwa vyema kabisa, msiwe an shaka, ila nawaomba msitumie
silaha, …’akasema na akawa anajiandaa kuondoka.
NB: JE ni nini kitatokea.
WAZO LA LEO: Kuna
historia ya mababu zetu, kuna historia ya misitu ya ajabu iliyogubikwa na
maelezo mengi ya kusisimua, hivi haya yanaachwa yapotee hivi hivi....historia na visa vyake vinasisimua kwa ajili ya kumbukumbu za vizazi vetu..
Je kuna
wanahistoria wameshafanya tafiti hizi, na kuweka kumbukumbu hizi za kale. Historia
itatusuta pale tutakapobakia na historia za akina Kali Petre na akina Vasco Dagama,
wakati huku wetu walikuwepo akina Mkwawa, Mangi. Nk, pia walikuwepo mababu zetu
waliokuwa na fani za kila aina…tusiwe watumwa hata wa kihistoria, tusikubali kuwa tegemezi
kwa kila kitu, Jamani hata historia yetu tunahitajia wafadhili kutoka nje, .....
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Buenas Sólo querÃa decirte que algunas de las imágenes no se cargan adecuadamente.
He probado en tres navegadores diferentes y todos muestran los mismos resultados .
Feel free to visit my web-site ... skineart.com
Post a Comment