Mwanadada aliendelea
kumsimulia mama yangu , mama ambaye ndiye aliyekuwa akimsimulia mwanae, jinsi
maisha yake yalivyokuwa, na jinsi gani alivyoweza kupambana kuitetea haki yake
ambayo kama angekaa kimiya, angekosa kila kitu kutokana na dhuluma ya watu
wachache. Hata hivyo mama yake alisema yote hayo yalitokana na wema, wema
uliotokana na mtendo mema ambayo ndiyo ylioyomuwezesha hadi kuweza kuwashinda waovu na dhuluma zao…
Tuendelee na kisa chetu, tukiwa bado tupo msituni, na
mwanadada na mwanadada akiwa na kundi lake, na ukumbuke kuwa yule muongozaji
anayeufahamu huo msitu na miiko yake, alishasema kuwa yeye anaondoka, kwani
kazi aliyotumwa kuifanya alishaikamilisha, je waliobakia wataweza kuikamilisha
hiyo kazi,………
‘Hatukuweza kumshawishi yule muongozaji wetu msafara, na
ikabidi yeye aondoke…japokuwa bado tulikua tukimuhitajia sana…..’akasema
mwanadada.
‘Mimi ningelifurahia niendelee nanyi hadi mwisho, lakini
kutokana na masharti niliyopewa, mimi siruhusiwi tena kuendelea zaidi ya hapo,
kwahiyo endeleeni wenyewe na kama mtanihitajia kutoa ushahidi mahakamani nipo tayari wakati
wowote….’akasema huku akiondoka.
‘Jamani tusipoteze muda, kazi iliyopo mbele yetu kwa sasa ni
kuhakikisha huyu mtu anakamatwa, akiwa hai, ….na kama mlivyosikia, huku
haturuhusiwi kutumia silaha, milio ya risasi hairuhusiwi huku msituni, sijui
ndani ya hilo….’akasema mwanadada.
‘Lakini hakusema ndani ya handaki, kasema huku nje…tukimfuta
huko ndani ikibidi tunaweza kutumia , lakini sio muhimu….’akasema mwanasheria,
na mwanadada akamtizama kwa mashaka, na yule mkuu akatikisha kichwa kama
kusikitika.
Kwa vile ule waya wa Antenna ulishakatwa, ambao tulikuwa na
wasiwasi kuwa ndio unaopeleka mawasiliano huko, ndani tulikuwa hatuna wasiwasi
tena, na kwa muda huo tulikuw tukisubiria kikosi kingine cha mkuu ambacho
walitengana nacho katika kugawana majukumu, na haikupita muda kikosi hicho
kikafika na hapo tukawa na uhakika kuwa hata kama jamaa ana kikosi huko ndani
hatatuweza.
‘Mikakati ikaanza ya
jinsi ya kuingia ndani ya hilo shimo kwa nia ya kumvamia mtaalamu, na sasa hatukuwa
na lile lengo la awali la kuonana naye kwa ajili ya kuthibitisha zile sumu,
sasa tulikuwa tunamuhitajia kama mshukiwa muhimu wa kesi yetu iliyokuwa bado
mahakamani, ambayo kesho yake inahitajika kuendelea….
‘Mkuu, utaongoza kikosi chetu na mimi nitakuwa msaidizi
wako..’akasema mwanadada.
‘Hamna shida, …’akasema huyo mkuu, na hakuacha kumwngalia
mwanasheria wa familia, na uvumilivu wake ukafika kikomo, akamshika mwanadada
mkono na kusogea naye mbali kidogo na kuanza kuteta naye, akauliza;
‘Na huyu mtu naye kafuata nini?’ akauliza akimuashiria
mwanasheria wa familia ya marehemu mume wangu, na mwanadada hakutaka kuuliza
kuwa anamuulizia nani alishajua anachoulizia akasema
‘Huyu mwanasheria ehe….yeye kasema ameamua kujiunga na sisi
baada ya kugundua ukweli,….’akasema mwanadada.
‘Mimi bado simwamini, angalia hali ilivyo, kila unayemwamini
unakuja kugundua kuwa ni mmoja wao, na anaongea kwa nia ya kujisafisha tu…sasa
mimi nashangaa kweli baada ya yote bado unamwaini huyu mtu….!’akasema mkuu huyo
akimwangalia mwanasheria kwa macho ya uficho.
‘Mimi naona tusiwe na mashaka naye, ….’akasema mwanadada.
‘Mwanadada, ninakuambia ukweli hawa watu hawaaminiki, wanaweza kujigeuza kama
kinyonga, ilimradi wapate wanachokitaka, na kwa vile sasa maji yameshawafika
shingoni, …..ndio maana wanaamua kufanya hivyo, ….kuwa makini, walichokifanya
kwa binti yangu sizani kama nitakuwa na amani na watu kama hawa, unafahamu kuwa
binti yangu katoweka tena….’akasema akionyesha uso wa huzuni.
‘Unasema kweli…!?’ akauliza mwanadada kwa mshangao.
‘Katoweka kiajabu na hatujui tutamtafutia wapi, na yule
kijana aliyekuwa ni rafiki yake, hali yake ilizidi kuwa mbaya sana, na wakati
tupo huku, nikasikia binti yangu katoweka kijabu na mara wakasema hali ya huyo
kijana rafiki yake imebadilika ghafla na kuwa krejea kwenye hali yake ya
kawaida, wanasema hajambo kabisa, …..sasa sijui, kuna nini , na je kuna
uhusiano wowote wa kupotea kwa binti yangu na hiyo hali yake…’akasema.
‘Unafikiri kuumwa kwa huyo kijana na kurejea kwa hali hiyo
na hatimaye kupotea kwa huyo kijana kunatokana na hawa watu?’ akauliza.
‘Ndivyo walivyosema hawo watu wanaomshughulikia huyo kijana,
na wanadai kuwa tusipohangaika kumshughulikia huyo binti, kesho ndio siku ya
mwisho, hatutaweza kumpata tena, na baada ya hapo kunaweza kutokea makubwa
zaidi….’ Akasema huyo mkuu kwa masikitiko.
‘Sasa wewe unasemaje?’ akauliza mwanadada akiwa kapagawa.
‘Mimi nina imani kuwa hawataweza kumzuru binti yangu, na
kama ndio hawo, …na kama ni mambo yao ya kishirikina, mimi nitapambana nao kwa
silaha….na nitahakikisha wote wanaohusika wanakwenda jela au nawamaliza
kabisa….’akasema akikunja uso kwa hasira na kumshika mwanadada warejee kwa
wenzao.
‘Ila nasema hivi huyu mtu usimwamini, asishirikishwe kwenye
kazi zetu…’akasema huyo mkuu.
‘Sijamuamini moja kwa moja, ila kwa vile ninamfahamu, sizani
kama anaweza kutusaliti, mimi namfahamu sana, mara nyingi ni mbishi, lakini ukweli
ukidhihiri, akagundua kuwa kweli ana makosa, hachelewi
kukiri,….ninakuhakikishia hilo, hataweza kutusaliti, lakini sio kwamba nimemkubalia
moja kwa moja kuwa nasi….’akasema mwanadada.
‘Usije ukarubuniwa kwa vile alikuwa mchumba wako, tunapokuwa
kwenye kazi kama hizi, mapenzi unayasahau kabisa…kama ningekuwa mdhaifi kiasi
hicho mimi nisingelwieza kuja kuendelea na haya mambo, fikiria binti yangu
kipenzi, ……hapana, nakuomba sana usije ukafanya makosa….’akasema huyo mkuu.
‘Usijali mkuu…..’akasema mwanadada huku akimtizama
mwanasheria ambaye alikuwa akiongea na watu wa usalama kama vile ni mmoja wa
kundi lao la kumkamata huyo mtaalamu.
‘Wasiwasi wangu ni kuwa nyie akina mama ni wepesi sana
kutekwa na mapenzi mkajisahau, unajua mwanadad mapenzi yanaweza kuwa sumu, na
kujikuta kazi yote tuliyofanya inakuwa ni kazi bure, hawa watu ni wajanja
sana…sijawahi kukutana na watu wajanja kama hawa….’akasema huyo mkuu huku
akimwangalia mwansheria ambaye alikuwa katulia upande wa pili, akisubiri na
wenzake ni nini kitafuata baada ya hapo.
Mwanadada akapiga makofi, kuwaashiria watu waliopo hapo
wakusanyike mahali pamoja, ili waweze kupanga jinsi gani ya kufanya, na
walipokusanyika, mwanadada akasema;
‘Mimi sio mtaalamu sana wa kuongoza mapigano haya ya moja
kwa moja, sisi utaalamu wetu ni kwenye ulingo wa mahakama,….japokuwa sio kwamba
siwezi kazi hii, ila kwa vile yupo mkuu, mtaalamu wa mambo haya, siwezi
kujifanya naweza, zaidi yake,… kwahiyo , inabidi mimi nikae pembeni tuongozwe
na mtaalamu wetu huyu, mkuu wa kituo chetu katika idara ya upelelezi, natumai
tutamtii ili tuweze kukamilisha kazi iliyopo mbele yetui, karibu mkuu…’akasema
mwanadada.
Mkuu hakupoteza muda, akaanza kuelekeza jinis gani ya
kufanya, na kila mmoja akampa kazi yake ya kufanya, na ilipofika kwa
mwanasheria, akasita na kusema;
‘Mhh, nashindwa kukupa jukumu, …mwanasheria maana wewe haupo
uapnde wetu, sina uhakika na ujio wako, ila nakuonya kama una lolote dhidi
yetu, bora urejee huko kwenu, maana sitakusamehe , na nitahakikisha nachukua
sheria mkononi mwangu kwani kundi lenu ni baya sana…’akasema
‘Kama huniamini mkuu, mimi nitalinda huku nje, msiwe na
shaka na mimi nafahamu unajisikiaje,..hata mimi ningelikuwa upande wenu huenda
ningejisikia hivyo hivyo, …..ila kama mtanihitajia niingie huko ndani nipo
tayari, lakini naomba sana mtu huyu asitoroke, na akitoka nje, nitakula naye
sahani moja,…’akasema huku akikunja uso kwa hasira.
‘Tuna watu wa kutosha, wewe tusubirie huku nje, na
tunakukanya kama ulivyosikia eneo hili
halihitajii kutumia risasi, sasa usije ukatumia mbinu za kumuua huyu mtu, kama
atatuponyoka ili asiweze kutoa ushahidi, utabeba hilo jukumu, utakuwa wewe
ndiye mshukuwa mkuu …..’akasema huyo mkuu.
‘Msiwe na shaka na hilo, nalielewa sana….’akasema huku
akionyesha kukerwa na alipoona kuwa
hataweza kuruhusiwa kuingia ndani akasema;
‘Na mkuu ninaomba sana muhakikishe mwanadada hadhuriki…..akidhurika
na lolote na mimi sitakusamehe kwa hilo….’akasema na kumwangalia mwanadada kwa
macho ya upendo.
‘Hahaha..leo hii unayasema hayo….umeshachelewa mpendwa....’akasema mwanadada akigeuka
kuelekea pale walipoona jamaa akifungua ule mlango, na wanzake akiwemo huyo
mkuu wakamfuata na kushirikiana kwa pamoja kuyasogeza yale majani yaliyokuwa
yametambaa na kutengeneza kitu kama mkeka, na kumbe kwa chini, kulikuwa na huo mfuniko,
wakasogeza yale majani na kukuta ule mfuniko.
‘Haya jamani kazi imeanza akasema mkuu, …na yeye akawa wa
kwanza kuingia baada ya kufunua ule mfuniko, na akafuataiwa na mwanadada….na maskari
wengine wa usalama wakaingia, alibakia askari mmoja wa usalama, ..
‘Wewe kwanini umebakia nje..?’ mwanasheria akamuuliza
akimwangalia kwa mashaka.
‘Mimi nahitajika kulinda huku nje…kwanza kwanini unaniuliza wakati
wewe umeshaambiwa kuwa huhusiki….?’akasema huyo askari kwa hasira, na
mwanasheria akatabasamu na hakupenda kuendelea kubishana naye, akasogea
kichakani na kujificha huku macho yake hayabanduki kwenye ule mlango wa lile
pango.
Yule askari wa usalama, naye akasogea upande mwingine, na
alipoona yupo peke yake, akatoa simu na kuanza kuwasiliana …..
**********
‘Tulipoingia ndani ya hilo pango,….ambalo linaelekea chini
kidogo kama shimo,…na kwa pale juu, kulitengenezwa vyema kabisa, kiasi kwamba
hata mvua ikinyesha maji hayaendi chini,ule mfuniko hauruhusu maji kuingia na
kwa pembeni kuna mzunguko wa kuwezesha maji yasituame hapo na kuleta madhara…na
shimo hilo lilichimwa sio kwa kwenda chini moka kwa moja, lilikuwa likienda upande upande, huku
linaelekea chini kwa mahesabu ya aina yake…
Kwa pembeni mwa hilo shimo, kulikuwa na sehemu kubwa , kama
kichemba, ambapo pikipiki na baiskeli vilikuwa vimewekwa na kufungwa na
minyororo, na kushikanishwa na waya ambao inaonekana ni kwa ajili ya tahadhari,
kama mtu akigusa tu,kunatokea ishara kwa ndani au mtu huyo hurushwa na umeme.
‘Mtu asiguse huyo mnyororo au hiyo baskeli na pikipiki,
inaonekana imetegeshewa….’akasema huyo mkuu,
Ilivyotenegenezwa ilikuwa kama ngazi, kuwa unashuka kidogo
kwenda chini, halafu unatembea kidogo kwenda mbele, ni kama ngazi, ilikuwa
imejengwa vizuri, kama vile imesakafiwa, lakini ni kwa udongo wa mfinyazi….kila
mmoja alishangaa ustadi uliotumika humo ndani, hata hivyo kila mmoja alikuwa
akitembea kwa tahadhari akijua ni hatari gani iliyopo mbele yao….
‘Tuliifuata ile ngazi kwa uangalifu, na kwa vile sio
mtereremko, hatukuweza kupata shida, na tulipofika mbele kidogo kwa pembeni
kulikuwa na mlango, uliotengenezwa kwa mbao, na kuzungushiwa nondo, ni mlango uliotengenezwa
kama suara kwa ufundi wa aina yake, na kupambwa kwa maua, na haukuwa umefungwa
kwa ndani, kwani tulipojaribu kuusukuma ulifunguka kwa kwenda juu, nakuacha
nafasi na baada ya muda kidogo hujifunga tena,
‘Hakikisheni hamuachi alama za vidole,….’akasema yule mkuu
wa upelelezi, na kila mmoja alihakikisha kuwa amevaa soksi za mikononi kwa
ajili ya kuzuia alama zao za vidole, na kila mmoja alikuwa na silaha tayari
mkonono kama ni lazima kuitumia
‘Japokuwa tumeambiwa huku hakutakiwi kutumia silaha, lakini tupo ndani ya shimo,
kama itakuwa ni lazima, hatusita kuitumia silaha , kisichotakiwa ni nje, maana
hawo mizimu hawapendi milipuko…milio ya bunduki ndiyo iliyowafukuza uraiani,
historia inasema watu hawa walikimbia vita, walikimbia milio ya bunduki,…...’akasema
huyo mkuu, na wamadada akawa anachunguza kwa macho huku na kule hakuwa akisema
neno, aliitikia kwa kichwa tu.
‘Nilikuwa na mawazo mengi kichwani kwa muda huo, na
ungeniuliza unawaza nini kwa wakati ule nisingeliweza kukuambia,…..ilikuwa kama
kichwa kimelindukana vitu vingi na vyote vinatakiwa kufanyika na muda
hautoshi…..’akasema mwanadada.
Wakafungua tena ule mlango na kwa haraka wakaingia ndani na kujikuta
kwenye chumba kama cha mapokezi, sehemu zote kulikuwa na mwanga, kwani kulikuwa
na taa zimewekeza ukutani, huwezi kuziona kwa jinsi zilivyowekwa kwa ustadi, na
mwanga wakekufanya chumba hicho kiwe kama mchana,….wakaangaza huku na kule, na
kwa chini, kulikuwa na busati,…
‘Mbona hakuna mlango?’ akauliza mmoja wa maaskari akiangalia
huku na kule
‘Tumia akili bwana…’akasema huyu mkuu na kuinua lile busati,
na hapo wakaona mlango wa chini huu haukuwa wa duara, ulikuwa wa mapana na
marefu yanayolingana, na kulikuwa na kitasa kilichowea na kuchimbiwa ndani
kulingana na ule mlango, na juu yake kuna kimbao, kiasi kwamba usingeliweza kuwa
kuna kitsa kama hicho, ni mpaka ukibenua kile kimlango,…. Wakafungua kile
kitasa kwa taratibu na ule mlango ukajisogeza bila kutoa sauti na kukaonekana
ngazi za kwenda chini, wakashuka kwa taratibu..
Na hapo wakajikuta kwenye chumba kipana kama ukumbi, kukiwa
na meza na viti, na viti vilikuwa vimekwa juu ya meza kuashiria kuwa
kumefungwa, kama wafanyavyo kwenye maukumbi na kulikuwa na mlango moja tu wa
ulioonekana mbele yao
Kote kuikuwa na taa za umeme, zilizowekwa ukutani kiufundi, kiasi
kwamba, huwezi kujua kuwa kuna taa zipo ukutani,na ilionekana kama vile upo nje….kwakweli
ujenzi huo utakuwa umegharimu pesa nyingi sana na utaalamu wa aina yake.
‘Kuweni makini,huenda huyo jamaa yupo tayari anatusubiri kwa
silaha,na inaonekana hayupo peke yake…’akasema mkuu, na wote wakawa makini na
silaha zao zikiwa tayari mikononi, kama zitahitajika kutumiwa, na mkuu
akafungua ule mlango na ulipokuwa wazi, yeye akapenya kwa haraka na kuangaza
huku na kule, na alipoona kuna usalama akawaashiria waingie waingie, hapo kulilikuwa
na taa zilizofifia mwanga, ..ni za rangi, isiyojulikana kuwa ni rangi.
Chumba hicho hakikuwa kipana sana, lakini kilikuwa ni ofisi,
ikiwa na kila kitu cha kiofisini komputa, mafaili,na simu ya mkononi na mashine
iliyoonekana ndiyo inayoongoza kila kitu hapo ndani, kwani kulikuwa na screen
kubwa ikiwa ukutani na kwa muda huo ilikuwa haionyeshi kitu, huenda ni kutokana
na vile tuslihakata ule waya wa kusaidia kuona nje. Kwa pembeni yake kulikuwa
na milango, ilikuwa milango miwili inayoashiria kuwa ni vyumba vingine ..
Mkuu akamuashiria mwanadada kuwa yeye na watu wawili waingie
chumba kimojawapo nay eye na watu wawili wafungue mlango mwingine, mwanadada
akakubali kwa kichwa, akiwa na silaha yake tayari mkononi, akashika kitasa cha
ule mlango, na kwa taratibu akakinyonga kile kitasa, na mlango ukafunguka, kilikuwa
chumba cha kulala, kitanda na kila kitu kama ilivyo chumba cha kawaida, na pale
kitandani kulikuwa na watu wawili wamelala mwanamke na mwanamume..
Yule mwanaume alikuwa kalala kifudifudi, tumbo chini, huku
mkono mmoja umeshikilia chupa ya kilevi, na mkono huo ulikuwa umening’inia
pembeni mwa kitanda, na chupa ile ilikuwa kwenye stuli, japokuwa mkono ulikuwa
umeshukilia ile chupa, kama vile hataki mtu kuichukua,…..
Pembeni yake, kwa ukutani alikuwa kalala mwanadada, ni binti
mdogo tu,akiwa kalala huku kaangalia juu huku mikono imeweka kichwani kama mto,
na alionekana kama analia….kwa kutoa machozi sio kwa sauti…
Yule msichana alikuwa ndiye wa kwanza kushituka kuwa kuna watu wamefungua
mlango, na alipowaona hawo watu, kwanza
litaka kupanua mdomo kupiga kelele, lakini mwanadada akamuashiria anyamaze, na
yule mwanadada akatulia kimiya japokuwa alikuwa kainua kichwa, na ywele zake
nyingi, alizokuwa kaziachia zilikuwa zimemfunika uso,na kubakisa sehemu za
macho….na isingelikuwa rahisi kumgundua huyo binti ni naki kwa muda ule, na
wote pale mawazo yao yalikuwa kwa huyo mtu aliyelala hapo kitandani.
Yule mwanaume alionekana alikuwa kalewa, au kalala kweli,
maana kilichokuwa kikisikika ni mihemo ya ya mtu aliyelala, na kama kitu
kinamkaba, kwahiyo mara kwa mara akawa kama anakohoa, na ilionekana dhahiri ni
kutokana na jinsi alivyoalala …,na kwa jinsi alivyoshikilia ile chupa ya ya
pombe inaonyesha kuwa ni muhimu sana
kwake, kuliko kitu kingine.
Mwanadada na watu wake wakaingia wakiwa na tahadhari na
mmoja alikwa tayari ana pingu mkononi, taayri kwa kumfunga, na bastola zao
mkononi, wakamsogelea huyo jamaa pale
alipolala…
Yule mtu kwanza alitikisika na kuwa kama anakoroma kuashiria
kuwa alikuwa kalala, na akatulia kimiya, na mwanadada akamuashiria yule msichana
kuinuka na wakati huyo msicahan anainuka pale kitandani, yule mtu kama mshale
alijibinua na aliposimama alikuwa kashikilia bastola mbili mkononi, na
kujibanza kwenye ukuta, akiwa tayari kwa mapambano.
‘Upo chini ya ulinzi…mtaalamu, usijaribu kufanya
lolote..’akasema mwanadada.
‘Ni nani unamuita mtaalamu, mimi sio mtaalamu, mtaalamu wa
kitu gani….na kwanini nipo chini ya ulinzi,…na kwanini mnaingilia maisha ya
watu….?’ akauliza huyu jamaa akiwa kashikilia bastola akiieleekeza huku na
kule, na kwa mbele yake alikuwepo yule msichana akitetemeka kwa uwoga na yule
askari usalama naye akiwa kashikilia bastola yake, akiwa anamwangalia kwa
makini huyo mtu.
‘Kila jambo lina mwisho wake, yote uliyoyafanya sasa yamefika
mwisho wake, weka silaha yako chini na jisalimishe ili tuyamalize haya mambo
kwa amani, hakustahili kumwaga damu tena na hasa eneo hili, kama unavyofahamu kuwa
huku hakutakiwi kutumiwa silaha… mtaalamu…’akasema mwanadada.
Yule jamaa kwanza alishikwa na butwaa, lakini kwa haraka
akajibadili na kuondoa hiyo hali ya kushangaa machoni mwake, na kusema;
‘Ohoo, kumbe, mnataka sharieeh, ok, kwangu mimi haina
tofauti, …nipo tayari kufa, …’akasema huku akiniangalia kwa mchao yaliyojaa
hasira. Na kwa haraka akapiga hatua moja mbele kumkaribia yule msichana.
‘Tatizo lako hunijui mimi, wewe mwanamke mimi sio huyo
unayemuita mtaalamu….kwanza kwa usalama
wenu tokeni kama mlivyokuja, ….sitasita kuitumia hii silaha, maana
mumeniingilia nyumbani kwangu….’akasema huku akiwa keshakiweka kidole sehemu ya
kufyatulia risasi.
‘Sikiliza….’akasema mwanadada na yule mtu akaelekeza hiyo
bastola kwa mwanadada kama anataka kuifyatua, na yule askari wa usalama akawa
anataka kujibu mashambulizi lakini mwanadada akamuasiria asifanye hivyo.
‘Kwanini mnanivamia kama mhalafu, mbona mnaingilia maisha ya
watu, nina kosa gani mimi, au kwa vile mnaona ninaishi huku …mapangoni, haya ni
maisha yangu niliyojichagulia mwenyewe,…..?’ akasema huyo mtu huku akimwangalia
yule mtu wa usalama kwa jicho la kujiiba, na ghafla akamdaka yule msichana
aliyekuwa karibu yake na kumshikilia huku akiwa kamlenga bastola kichwani.
‘Usijifanye hamnazo, sisi tumeshagundua janja
yako….ulipokuwa mahakamani ukitoa ushahidi kuna sehemu uliteleze mimi
nikafuatilia, na kugundua mengi kukuhusu wewe….kujibadili kwako, sio tatizo,
kuna mambo mengi yameshafichukuliwa , kama kweli huna hatia, una haki ya
kujitetea mahakamani, na haki itakulinda….’akasema mwanadada
‘Kama hamtatoka hapa au kuniruhusu mimi kutoka hapa
ninammaliza huyu binti…mimi sihitaji kwenda mahakamani, sheria ninayo mwenyewe,
ndio maana naishi huku, sitaki shida na watu, …lakini kama mnanitaka shari,
sitasita kufanya lolote kujihami….’akasema na kumvuta yule msichana , na yule
msichana akawa mbele yake, huku akiwa kamzungushia mikono yenye bastola na
kuelekeza moja kwa mwanadada na nyingine kwa yule askari usalama.
‘Sikiliza ndugu yetu, mimi kuja kwangu hapa sio kwa shari,
na ulionyesha moja wa kushirikiana na mimi, na nahitajika kulipa fadhila
nitajitahidi kukutetea kadri niwezavyo…’akasema mwanadada na huyo mtu akacheka
kwa dharau.
‘Tatizo wewe mwanamke huelewei unaongea na nani, …nimeshakuambia
kuwa mimi ninasihi kwa sheri zangu, sihitaji huruma ya mtu, sihitaji kusaidiwa,
…ninajua ni nini ninachokifanya, na ni nini mwisho wa yote, siogopi kufa, kufa
nilishaandikiwa mapema….’akasema na kumsogeza huyo msicha kifuani kwake, na
huyo msichana akawa analalamika kwa maumivu.
‘Muachie huyo msichana aende zake, kama kweli unajiamini,
kama kweli huogopi kufa, kwanini uwahukumu wengine wasio na hatia…..’akasema
mwanadada.
‘Sikilizeni msinipoteza muda, akafyatua risasi iliyopiga
ukutani , na hapo mwanadada akafahamu kuwa huyo jamaa hatanii, na mawazoni
mwake, alitaka kufanya lolote, na yule jamaa, akaiweka bastola moja mfukono kwa
haraka na akawa an mkono mmoja upo hutu, akamshika yule msichna vizuri na
kusema mnamfahamu vyema huyu binti ni nani?’ akauliza huyu mtu.
Na mwanadada akamwangalia yule binti kwa makini, kwani
nywele zilizokuwa zimetimuliwa zilikuwa zimemfuniko usoni, na aliposema hivyo
yule mtu, akamfunua zile nywele yule binti eneo la usoni na hapo mwanadada
akaweza kumuona vyema yule binti.
‘Wewe binti umefuata nini huku?’ akauliza mwanadada kwa
mshangao.
‘Sijui nimefikaje huku….’akasema huyo binti akiangalia huku
na kule, na mara mkuu wa kituo katika kitengo cha upelelezi akaingia na kikundi
chake na kusimama katikati ya mlango, na kumfanya yule mtu kuonekana kupagawa
kwa wasiwasi, hakutarajia hilo tukio, alijua kuwa anapambana na hawo watu
waliopo ndani, ….lakini kuna cha zaidi kilichomfanya hadi aonekane kuwa na
wasiwasi kuliko kawaida ahasa alipomuona huyu mkuu
Hata hivyo, hakumuachikia yule binti, na wakati huo yule
binti nywele zilikuwa zimemfunika kama mwanzo, sasa akawa anamsukuma yule binti
asogee mbele, na yeye akatembe hatua chache kukaribia kwenye mlango, nahisi
alishafahamu kuwa watu hawo hawawezi kutumia silaha zao, kwahiyo hakujali tena,
akamsukuma yule binti atembee kuelekea
kule kule aliposimama huyo mkuu.
Mkuu alipoingia alikuwa kashikilia bastola yake mkononi, na
macho yake yalikuwa kwa huyo mtu, tayari kwa lolote lile na alipomkuta huyo mtu
kashikilia bastola akiwa kaikandamiza shingoni kwa huyo msichana, akasita
lakini hakuacha kuuilekeze bastola yake kwa huyo mtu, na kwa muda huo akili
yake ilikuwa kwa huyo mtu, hakuwa na haja ya kumwangalia huyo msichana ni nani,
Ni pale macho yake, yalipotua kwa huyo msichana,kwanza
alimtizama kwa mashaka, halafu akawa kama kaduwaa, na baadaye akasema kwa
mshangao
‘Binti yangu ….’akasema mkuu huku akiwa kaduwaa, hakuamini
macho yake.
Na hiyo ndiyo nafasi aliyokuwa akiihitajia huyo mtu, kwani
kwa haraka,alimsukuma yule binti, na yule binti kwa vile hakutajia hilo tendo,
alikwenda moja kwa moja na kugongana na baba yake, na wote wakaserereka chini,
na wakati huyo mkuu ana jizoa zoa, yule mtu akawapita na kuwasukuma wote wawii
kwa pamoja na kuwafanya wawe wamelaliana, na hapo akawapita kwa haraka, na mkuu
alishindwa kufanya lolote kwani binti yake alikuwa kamlalia,
Mwanadada na maaskari wengine, walikuwa wakijaribu kumwahi
huyo jamaa, lakini huyo jamaa alikuwa mwepesi ajabu, kwani hayo yote aliyafanya
kwa muda mfupi, na keshatoka mle ndani. Na mwanadada akawa anatoa amri kwa watu
waliopo nje wahakikisha wanamshika huyo mtu, asitoroke, na mara wakasikia milio
ya bastola na vilio vya watu vikasikika kuashiria maumivu .
‘Oh, mambo yameshaharibika….’akasema mwanadada, na yule mkuu
akasema kwa suati
‘Msimuua, tunamuhitaji akiwa hai…..’alisema huku akiinuka na
kuelekea huko nje, na wote wakajikuta wapo mlangoni, na mlango ulikuwa ni
mdogo, inahitajika atoke mtu mmoja mmoja.
Mwanadada na mkuu, na maaskari wengine,wakatoka kwa haraka
kuelekea sehemu hiyo ambapo milio ya risasi ilisikika, wakiwa na bastola zao
mkononi, lakini walikuwa wamechelewa, kwani eneo la nje ya la hapo ofisini, waliwakuta askari wao wawili wakiwa wamelala
chini, huku wakivuja, damu, na wengine walikuwa wakifukuzana na huyu jamaa huku wakijibizana kwa bastola…
NB: Je miiko itavumilika, kuwa silaha zisitumike, hasa kwa
mtu kama huyo, ….Je kumdhibiti muhalafu wa namna hiyo inahitajika nini, zaidi
ya kutumia nguvu, ….
WAZO LA LEO:
Matendo mabaya yakikithiri, mioyo huota sugu, na ubinadamu hutoweka kabisa. Wanadamu
huwa kama wanyama, huruma na upendo hutoweka, chuki visasi na husuda inauwa na
hulka…amani hakuna tena.Swali la kujiuliza ni nini faida yake, wakati kila
mmoja njia ni hiyo hiyo ya umauti, kwanini tusiwe wema, na dunia ikawa ni
kisiwa cha amani.
***********
Maombi: Pendekeza blog hii kuingia kwenye mashindano ya best blog awards kwa kuandika email na kutuma
kwa
``tanzanianblogawards@gmail.com’’
Kwenye subject unaandika diary yangu (
http://miram3.blogspot.com/) na kwenye maelezo unaandika hivi;
Naipendekeza blog hii ya diary yangu (http://miram3.blogspot.com/ kwenye kipengele cha;
Best Creative Writing Blog
Best Educational Blog
Best General Blog
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment