Ilikuwa siku ya kesi, wakati tunasubiriana, tuliwahi mapema
sana, na kukaa kwenye viti vilivyokuwa nje, huku tukiongea hili na lile.
Pembeni yangu alikuwepo, baba yangu wa kufikia, akiwa na mkongoja wake, alikuwa
kauinamia japokuwa alikuwa amekaa kwenye benchi, tulilokuwa tumekalia. Tuliomba
kuingia mapema, na tukaruhusiwa.
Nilimwangalai baba yangu huyu wa kufikia, na kugundua kuwa
mwingi wa mawazo, nikataka kumdadisi nijue zaidi, kama ni mawazo tu, au anaumwa.
‘Baba vipi upo powa kweli…?’ nikamuuliza. Yeye akainua
kichwa na kuniangalia, na macho yake yalionekana kama alikuwa amesinzia, kwanza
akatabasamu, na baadaye akasema;
‘Nipo powa,…usiwe na shaka na mimi, unajua unapofikia umri
kama huu wangu, huhitaji, mambo mengi ya kuwaza, lakini haya yanayotokea sasa,
yanakulazimisha kuwaza sana…..lakini najua mwisho wake umefika…najua sitakufa
mpaka hili lipate ufumbuzi wake, namuomba sana mungu iwe hivyo…’akasema na
kugeuka kuangalia pembeni yake, ambapo walikuwepo wazazi wangu, na baba yangu
mzazi akasema;
‘Lakini kwa ujumla kesi hii ni ngumu na yenye historia ya
kipekee, maana hawa watu wamejiandaa kweli, kila kona wamejaribu kuweka
vizingiti, na leo nasikia wameagiza wakili mwingine kuja kusaidia …’akasema
baba.
‘Hata walete mawakili wa kimataifa, hawataweza kuvuka huu
mto wenye mamba walio na njaa ya kudhulumiwa, maana ukweli upo dhahiri, na
penye ukweli uwongo hujitenga,…mimi nakuhakikishia, wataumbuka, na wataenda
jela, labda litokee la kutokea, maana hawa watu hawatabiriki..na jana …’akasita
kidogo, na mimi nikaingiwa na wasiwasi na kauli yake hiyo.
‘Na jana vipi baba , mbona watutisha…?’ nikamuuliza.
‘Jana nimeota ndoto mbaya sana, sijui ina maana
gani…’akasema baba huyo wa kufikia.
‘Ndoto ni ndoto tu wewe mwanaume, inaweza ikawa ni ndoto tu,
ni kama bahati nasibu, ukicheza huwezi kujiaaminisha kushinda, ikitokea
kushinda ni bahati yako….’akasema mama akimwangalia huyo baba kwa macho ya
kumshangaa.
‘Ni kweli, lakini ndoto zangu za namna hiyo, zinaashiria
jambo, na sio kwamba nina wasiwasi sana, hapana, ila nahisi kuna kitu
kitatokea, moyo wangu haujatulia, kabisa…sijui, tuombe mungu isiwe hivyo,…naomba
isije ikaathiri hii kesi…mungu ni mkubwa, hakutatokea kitu kibaya’akasema baba
wa kufikia, na mimi nikavutika kujua ni ndoto gani hiyo aliyoota huyu baba hadi
imuwekwe kwenye wasi wasi kama huo..
‘Kwani baba uliota ndoto gani?’ nikamuuliza. Na yeye kwanza
akawa kama anatabasamu ili kutuondoa wasiwasi, na akasema;
‘Huwezi kuielezea kiundani sana, maana ndoto kama hizi zinakuwa
za marue rue…, lakini nakumbuka, kulikuwa na kitu kama mapigano,…ya kutoana
damu, na watu wakaumizana, sana, na sina uhakika ni nani, lakini ni mmoja wetu,
akawa kaumizwa, na wao pia kidogo, watu wakawa wanambeba mtu wetu,a u watu
wetu, hapo sina uhakika sana, na kupelekwa hospitalini….sikumbuki mengine,
lakini ilikuwa ya kujirudia rudia, kama vile napewa ujumbe fulani’akatulia.
‘Mmoja wetu….?’ Nikauliza nikiwaangalia wazazi wangu
‘Ni mmoja wetu, katika kundi letu, hakuweza kutambulikana
vyema, lakini ni kama kiongozi, kitu kama hicho…na huyu akasababisha tushindwe
kwenda hayo mapigani, baada ya kuumia,
mapigani yakasimama ili hawo walioumia wapelekwe hospitalini,….halafu nakumbuka
kwa mbali nilisikia sauti ya hakimu akiita majina yetu, kuwa tunahitaji tuingie
ndani,..
'Lakini ndoto bwana, ilionekana tupo mbali, na wakati huo nikawa nahangaika kuwakusanya watu
wetu tuharakishe kuondoka, lakini kila mmoja, alikiwa kwenye pilika pilika na
kupambana na hawo watu waliokuwa wametuvamia,… unaona, yaani ni ndoto isiyo na
mpangilio maalumu, lakini ndoto kama hizo kwangu, zinaashiria kitu, sio bure,
tuombe mungu tu…iwe salama.’akasema.
‘Lakini mbona tumeshafika mahakamani , kwahiyo hiyo ni ndoto
tu….haina ukweli…’nikasema.
‘Ni kweli na hilo ndilo linanipa tumaini, maana ile ndoto,
ilionyesha kuwa hilo tukio lilitokea kabla hatujafika mahakamani….tukawa
tunachelewa kufika mahakamani na hakimu anaita majina yetu….’akasema baba huyo
wa kufikia.
‘Wakati mwingine ndoto ni ishara ya tukio fulani, na wakati
mwingine ndoto ni kutokana na mawazo yaliyokuzonga siku hiyo au siku za nyuma,
na hatutakiwi kuzitilia maanani sana, maana ukizifuatilia unaweza usifanye
mambo yako mengina ukiogopa ulichokiota na ni mwanzo wa kuingia kwenye shiriki,
tumuombe mungu na kumwamini yeye, kuwa lolote litatokea kwa matakwa yake,…..’akasema
baba yangu mzazi.
Tulikaa kimiya kidogo, tukiwazia hiyo ndoto ya baba wa
kufikia, na baadaye mama akauliza;
‘Hivi wakili mwanadada hakulala kwako?’ akauliza mama.
‘Alilala kwangu lakini aliondoka asubuhi sana, akisema kuna
mambo anayafuatilia, lakini aliahidi kuwahi , kwani yeye ndiye atakayeongoza
jopo la mawakili leo, kwa vile alisema watu muhimu aliokuwa akiwahitaji
wakamatwe wameshakamatwa…’nikasema.
‘Ina maana watu wote wanaoshukiwa wamekamatwa?’ akauliza
mama.
‘Ndivyo alivyoniambia wakili mwanadada, sina uhakika zaidi,
unajua sasa hivi mambo mengi hataki kuyasema, anasema ni vyema tukajua hayo
yanayojulikana na mengine yatajulikana huko mahaamani…’nikasema.
‘Na kweli safari hii, wamejitahidi kuficha mambo mengi, na
mambo mengi unayasikia ndani ya mahakama, nafikiri wanaogopa sana wapindani
kusikia mambo yao, na kwa vile hawana uhakika ni nani wakumuamini tena…’akasema
baba.
‘Wenzetu hawa , wana masikio makubwa, na kila mnaloongea
linawafikia, na ndio maana wameamua kutowaelezea watu, kuhusu mipango yao, na
ushahidi wao, hata kama wanawaamini vipi. Mimi mwenyewe mengi siyajui,
…’akasema baba wa kufikia.
‘Haiwezekani, kwanini usiyajue na wewe ni mmoja wa
wanaoshitaki, au kulalamika,…..usitufiche mzee mwanzangu…’akasema baba huku
akionyesha mshangao.
‘Kiukweli sijui, zaidi ya yale ninayoyajua mimi….wakili
mwanadada amekuwa msiri sana..anasema ni bora iwe hivyo, kwa ajili ya manufaa
yetu, na pia aliongeza kusema kuwa pia ni kwa ajili ya usalama wetu….’akasema
baba wa kufikia.
‘Basi kama ni hivyo hakijaharibika kitu, sisi tupo pamoja
naye, tunafahamu kuwa anafanya hayo kwa nia njema…’akasema mama.
‘Ni kweli tumuombee azidi kuwa na moyo huo na mungu ampe
afya na guvu, ili tuweze kuvuka mtihani huu…’akazema baba na mama akaitikia
‘Amini…..
*********
Wakati tupo tukiendelea kusubiri, mara likaja gari la mwanasheria, na wakati huo
geti al kuingia magari lilikuwa bado limefungwa, kwahiyo alisimama nje kwenye
barabara, kando kando ya barabara, alikuwa na baadhi ya watu wake, gari lake
liliposimama, watu wake wakateremka lakini huyo mwanasheria aliendelea kubakia
ndani ya hilo gari lake, huenda alisubiri geti likifunguliwa aingie na gari
lake.
Jamaa zake walipoteremka, yeye akashusha kiyoo, na sisi
tuliokuwa ndani kwenye viti tuliweza kumuona vyema, kwani pale tulipokuwa
tumekaa, tulikuwa kwa juu kidogo na barabarani kupo chini, kuna kitu kama
bonde. Nilipomuangalia , niligundua kuwa alikuwa kavalia nguo zake, suti ya vipande vitatu kama kawaida yake.
Kwanza aliinua uso kidogo kuangalia nje, halafu akainama kama anachukua kitu
kwa chini, na alipoinuka, alionekana ameshika karatasi, akawa anaisoma, na
kuandika andika …mimi na wenzangu tulikuwa kimiya, na kila mmoja alikuwa
akimwangalia yeye.
Mwanasheri huyu, mwili wake ulikuwa umepungua kidogo, huenda ni
kwasababu ya haya matukio mazima, na huenda na kwasababu ya mawazo yake binafsi
na mchumba wake, japokuwa yeye mwenyewe alisema, hasumbuki sana kumwazia
mchumba wake, kwani walishamalizana, kitu a,mbacho mimi sikukubaliana nacho…..
Akiwa ndani ya hilo gari, hakuinua uso wake tena, kuwaangalia
watu, alionekana kushughulika na jambo kwenye makabrasha yake, na sisi wakati
huo tulikuwa tunaongea hili na lile na wapiga picha na waandishi mbalimbali
walionekana hapa na pale, walionekana wakichukua picha za matukio na wengine
kuchukua kanda za video, kwa ajili ya matangazo yao. Ilikuwa ni kesi kubwa….
Kwa mbali tukaliona gari la wakili mwanadada likija, kwa
mwendo wa taratibu, na baadaye likapinda kona kama kutaka kuingia eneo la
mahakama, kwasababu ya msonagamao wa watu halikuingia moja kwa moja, likawa
limesimama kando ya barabara, na huenda mwanadada huyo alitaka ateremke kwanza,
na hilo gari lije liingie baadaye au ni kwa vile geti la kuingiza magari
lilikuwa bado limefungwa, sijui kwanini walikuwa hawajalifungua hilo geti.
Kwa haraka nikamtupa macho mwanasheria, ambaye
naye kama watu wengine, alipoona gari la mwanadada likiwa limesimama kando ya
gari lake, akainua kichwa na kuangalia hilo gari. Kila mtu alifanya hivyo…
Kwakweli walifika watu wengi siku hiyo, nab ado walikuwa
wakimiminika, na wengi wao, ilionyesha kuwa walifika kwa minajili ya kuwaona
hawa wanasheria kutokana na sifa zao hususani huyo wakili mwanadada, na hii
ilidhirisha wazi, kwani gari hilo lilipofika tu, watu wakaanza kulisogelea ili
wamuone vyema huyo mwanadada akitoka kwenye hilo gari.
Hapo waandishi wa habari,
wapiga picha wakawa wanalisogelea hilo gari, ili wapate picha nzuri na hapo maaskari
wakawa na kazi ya ziada ya kuwazuia watu, na sisi tukawa tunaangalia tu jinsi
gani watu wanavyopata taabu , kwani pale tulipokuwa tumekaa, tulikuwa tunaona
matendo yote kwa usahihi wake.
Kweli mwanadada huyu alikuwa keshajijenga jina…
‘Huyu dada ni jembe….’alisikika askari mmoja aliyekuwa kando
yetu, akiangalia usalama kwa uapande wa ndani.
‘Tena jembe ulaya…..’akasema askari mwingine.
‘Tukiwa na watu kama hawa, hakika tasinia hii ya wanasheria,
itafika mbali,…tutakuwa hatuna shida, maana ukiwa na kesi yako tu unauhakika wa
kutetewa….lakini yote haya yanahitaji pesa, kama huna pesa, unafikiri unaweza
kumpata mtu kama huyo?’ akasema mtu mmoja aliyekuwa kakaa nasi tukisubiri
kuingie ndani ya ukumbi wa mahakama, alikuwa kama anauliza.
‘Sasa hawa wanaotetewa wana pesa gani….kama unavyoona huyu
mwanadada ni kama kajitolea upande wa serikali,…sizani kama analipwa na hawo
watu, kwanza kesi yenyewe ni ya serkali kuwashitaki hawo watu, kama angelikuwa
anawatetea washitakiwa, basi, hapo tungelisema kuwa watamlipa pesa nyingi hawo
washitakiwa….’akasema jamaa mwingine.
‘Mhh, lakini kesi hii ingelipendeza zaidi kama huyo
mwanadada angelitetea washitakiwa, kesi hii ingenoga sana…unaonaje hilo?’akasema
jamaa mwingine.
‘Lakini wewe huoni, mimi naona ni kama vile anawatetea
washitakiwa, hasa wale walioshitakiwa kama wakosaji, lakini hawana makosa, ni
makosa ya kujumuishwa tu, na kwa upande mwingine, anawafichua wale wanastahili
kuwepo kwenye hii kesi,…maana kama ulivyoona kuna wahusika wakuu, lakini
hawajatambulikana vyema kwa ajili ya ujanja wao….’akasema jamaa huyo mwingine.
‘Swali langu ni hili, je, wamekamatwa wote, maana nilisikia
kuna watu huko kwenye hicho kijiji, hawakamatiki, wakifika majumbani kwao,
wanakuta paka …mtu hayupo,, ukikutana naye njiani, anatoweka, baadaye unamuona
yulee, keshafika mbali…..’akasema jamaa mmoja ambaye alionekana ni muhudumu,
kwani alikuwa kashika ufagio, na yeye akijumuika na watu wengine kuangalia
yanayotokea huko nje.
‘Hayo ni maneno ya watu
bwana, wewe unaamini mambo hayo?’ akasema askari usalama.
‘Ndivyo tulivyosikia, …..’akasema huyu jamaa.
‘Maneno ya kusikia yanakolezwa na uwongo, kwa lengo maalumu,
ni propaganda potofu tu, hazina ukweli, …hawo ambao walichelewa kukamatwa,
walikuwa na sababu zao, …huenda hata hawo maaskari, au watu wa usalama,
walikuwa wakifuatlia jambo fulani, kuhusiana na hawo watu. Ni mbinu za
kiuslama, nyie hamuwezi kuyajua hayo….’akasema huyo askari aliyekuwa akiangalia
usalama kwa eneo la ndani.
‘Lakini kwa ujumla kesi hi ni ngumu, na ikiisha itaweza
kuleta mabadiliko makubwa…’akasema mama mmoja aliyekuwa kasimama na mkoba wake,
na yeye akijaribu kuangalia huko nje ya geti.
‘Ni kweli, huenda na sisi tukapumua…’akasema mama mwingine.
‘Kinachotakiwa ni kumuunga mkono, hasa huyo wakili
mwanadada, maana yupo kwa ajili ya wanyonge, na hata akihitaji mchango wa
kipesa, mimi nitajitolea, nitauza kuku wangu, ili nipate pesa ya kumpa…’akasema
mama mwingine akiashiria ana biashara ya kuku.
Ni kweli umaarufu wa huyu mwanadada, ulikuwa umefika mbali,
watu kutoka vijiji vya mali walifika kuhudhuria hiyo kesi,…mimi nikageuka
kuangalia kule alipokuwa mwanasheria, ambaye kwasasa alikuwa amefungua mlango
wa gari lake kutoka nje na wapiga picha wakawa wanampiga picha, lakini wengi
walikuwa wamekwenda upande ule alipokuwa wakili mwanadada.
Kwa mbali tukaona gari ikija, kwa mwendo wa kasi kidogo,
ilionekana muendeshaji alikuwa ana haraka kama vile anakimbizwa, lakini cha
ajabu, gari lile lilikuwa likija kwa kasi huku linayumba yumba, na mimi kwa
akili yangu ya haraka, nikazania huenda huyo mwendeshaji atakuwa amelewa. Kwakweli
uendashaji ule haukubaliki, ikizingatia
kuwa kulikuwa na mkusanyiko wa watu, ambao waliokuwa wakiruka barabara kuelekea
upande mmoja wa barabara huku na kule,
na wengi sasa walikuwa wakiliendea gari la wakili mwanadada.
Kwa kipindi hicho wakili mwanadada alikuwa naye kaamua
kutoka nje, baada ya kuona geti la kuingiza magari linachelewa kufunguliwa, na
kama kawaida yake alikuwa kavaa mawani meusi, yanayoziba macho yake, akaivua na
kuiweka ndani ya gari lake, akageuka kuangalia upende walipokuwa waandishi, ambao
na wao hawakuwa na mawazo na hilo gari linalokuja kwa kasi…
Wakati huyo mwanadada anateremka, hakuwa na wasiwasi, kwahiyo mawazo yake yalikuwa kama
yakuuliza kwanini geti halifunguliwi, kwahiyo akawa anangalai muelekeo wa geti,
na kuupa mgongo usawa wa barabarani, ambapo ndipo gari hilo lilikuwa likija kwa
kasi, na hata hivyo sehemu alipokuwa kaegesha gari lake, ni sehemu salama, ni
upande ambao magari hayawezi kufika, labda kama yanataka kuegeshwa kama
alivyofanya yeye,kwahiyo hakuwa na mawazo ya kuangalia gari hilo lililokuwa
linakuja kwa kasi.
Ajabu! Gari lile lilitoka upande wake na kuelekea pale
liliposimama gari la wakili mwanadada, kwanza tulijua kuwa linakwenda
kuegeshwa, kama walivyofanya mawakili hawa, lakini ule mwendo ulikuwa sio wa
kuegesha gari, ulikuwa ni wa kasi, na gari lile lilikuwa likienda moja kwa moja
pale aliposimama wakili mwanadada ambaye alishatoka nje ya gari lake, na akawa kama
anajinyosha kidogo kwa kuweka mikono yake mbele ikiwa imekunja ngumi, ….
Alikuwa hana ile miwani yake, kuonyesha kuwa alishaivua na
kuiacha kwenye gari, na safari hii alikuwa kaziachia nywele zake kumzunguka na
ulimbwende wake ulizihiri pale alipogeukiwa watu kuwaangalia, na picha nyingi
zikawa zinapigwa.
Kila mtu aliyeliona hilo gari, linavyoelekea pale aliposimama
mwanadada, alishikwa na butwaa, maana gari lile lilikuwa likimwenda mwanadada
huyo kwa mwendo kasi, likionyesha dhahiri kuwa na lengo la kumgonga huyo
mwakili mwanadada, na wakili mwanadada likuwa hajawazia hiyo hatari, kwani
aligeuka kule gari linapotokea akiwa na uso wake wa ujasiri, na wakati huo
alikuwa kavua miwani.
Lakini alipogundua kuwa kuna hatari, kwanza akashikwa na butwaa, na haraka akiwa na
mshangao, akawa anataka kuruka, kulikwepa hilo gari, gari lililokuwa likimjia, kwani
alishahisi yupo hatarini, na gari hilo lilikuwa likimuelekea na pale
aliposimama, hakukuwa na nafasi nzuri ya kulikwepa,..alichofanya ni kuinua
mikono juu, kama vile anaomba mungu, na huku, akijitahidi kuruka pembeni, na
mara gari hilo likawa limeshamfikia….
Mlio wa bhaaa, ukasikika….
Watu walipiga mayowe, na wengine kufumba macho, na
walipofumbua waliona wakili mwanadada kalala chini, akiwa anatokwa na damu, na pembeni
yake alikuwa kalala mwanasheria,…gari lake upande mmoja ukiwa umebonyea na
mlangoo kung’oka kabisa….
‘Kimbiza hilo gari…’sauti ya askari ikasema na mmoja wa
maaskari akiwa kwenye pikipiki akaanza kulifukuza lile gari ambalo lilikuwa
limeshafika mbali kidogo, lakini tujuavyo mwendo wa pikipki za kijeshi , ni
lazima ataweza kulifikia hilo gari, kabla halijapotea na huenda huyo muhusika
akakamatwa kama hakutakuwa na kizuizi kingine.
‘Kuna usalama hapo….?’aliuliza mmoja wa maaskari wa hapo.
‘Kuna ajali mkuu…..’akasema askari mwingine.
‘Ajali ilikuwaje…?’ akauliza tena, na watu wa usalama wakawa
wanashughulika kuwazuia watu waliokuwa wakimiminika kuangalia wale watu wawili
waliokuwa wamelala chini, na aliyeonekana na yupo katika hali mbaya ni wakili
mwanadada, maana damu zilikuwa zikimtoka….lakini mwanasheria alionekana
kupoteza fahamu, au kushikwa na mfadhaiko wa muda , hakuwa akitokwa damu.
Tukio lilivyouwa wengi, walijikuta wakifumba macho ili
wasione, maana ilionyesha dhahiri lengo la huyo muedhaji gari, na kila mtu
alijua ni ajali mbaya itatokea, na matokea yake ni kukosa kuona jinsi gani
ilivyokuwa, hata mimi nilifumba macho kuogopa kuona tukio hilo, maana ….mmh,
ilitisha, na nikainuka haraka pale nilipokuwa nimekaa na kukimbilia na wazazi
wangu nao wakifanya hivyo hivyo.
‘Kwani ilikuwaje….?’ Akauliza mzee mmoja.
‘Nafikiri huyo mwenye gari, ametumwa kumuua wakili
mwanadada….’akasema jamaa mmoja.
‘Sasa imekuwaje..?’ akauliza mwingine.
‘Naona mwanasheria alipoona hivyo, alijitolea muhanga kwenda
kumuokoa wakili mwanadada , na wote wakagongwa na hilo gari,sasa hatujui athari
yake ikoje, lakini gari halikuweza kuwakanyaga zaidi ya kuwagonga na kutupwa
pembeni ….’akasema huyo mtu.
‘Kwanini wafenye hivyo, wangekuja wanigonge mimi, kuliko
kumgonga huyu mtetezi wa wanyonge…’akasema mzee mmoja.
‘Naona maaskari wanazuia watu, na hapa hakukaliki tena, tutafukuzwa, bora
tujitahidi tuingie ndani…’akasema mtu mmoja akijaribu kuingia ndani, na huyo
mzee naye akijitosa kufanya hivyo, kujaribu kuingia ndani, lakini haikuwa
rahisi, maaaskari wakawa wanawafukuza watu wote waondoke.
‘Jamani, hatutaki watu eneo hili la mahakama, rudini nyuma
na ondokeni kabisa eneo hili, na wale wanaohitajiwa wataitwa …’akasema askari,
lakini watu walikuwa kama hawamsikii, kila mtu alikuwa akijaribu kutafuta njia
ay kuingie eneo hilo la mahakama.
Mara gari la wagonjwa likafika, na hapo watu ambao hawakuona
tukio lilivyokuwa wakajua kuna tatizo, huenda, kweli gari hilo lililowagonga
wanasheria hawo litakuwa limeleta ajali mbaya, na wale watu wawili wakaonekana
wakiingizwa ndani ya hilo gari, wakiwa wamebebwa kwenye vitanda maalumu, huku
wakiendelea kufanyiwa huduma ya kwanza, na shuka zao zikionekana kulowana damu.
Kwakweli ilibidi kesi ilibidi iahirishwe, maana mawakili
muhimu walikuwa ndio hawo …na
haikujulikana hali zao zikoje,lakini jinisi ilivyoonekana hali zao zilikuwa
mbaya, …..
`Kesi imeahirishwa,..mtatangaziwa siku ya kesi hiyo baadaye...
’ tangazo likatolewa
Watu wengi hawakutaka hata kusikiliza, walipanda magari
kuelekea huko hspitalini walipopelekwa hawo wahanga wa hiyo ajali iliyoonyeshwa
ni ya kupangwa….
NB: Je itakuwaje….
WAZO LA LEO:
Huwezi kuizua haki kwa dhuluma, huwezi kutumia nguvu kupambana na haki, kwani
haki wakati wote ipo juu ya dhuluma, na mwisho wa dhuluma ni kuzalilika tu.
Ni mimi:
emu-three
3 comments :
Mmh, jamani mbona hivyo tena mungu amnusuru mwanasheria mdada ili atetee wanyonge. Na imani atapona na kuwakomesha hao waliopanga kumuua.
Mmh, jamani mbona hivyo tena mungu amnusuru mwanasheria mdada ili atetee wanyonge. Na imani atapona na kuwakomesha hao waliopanga kumuua.
Great!
Post a Comment