Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, July 17, 2013

WEMA HAUOZI-36


Wakili mwanadada alisimama na kwenda kufungua mlango, na mlango ulipofunguka akajikuta kama anashituka kuashiria kuwa aliyemuona hakutarajia kuonana naye, kwanza alitulia akawa anamuangalai huyo mtu kwa nje, na mimi pale nilipokuwa nimekaa, sikuweza kumtambua ni nani, maana huyo mtu aligonga mlango bila kutoa kauli ya hodi. Mimi kwa muda huo nilikuwa nikimalizia kuondoa vyombo tulivyokuwa tukitumia kupata chakula cha mchana…’akaendelea kunihadithia mama kuhusu maisha yake

‘Ni nani mbona umeduwaa, na hufungui mlango….?’ Nikamuuliza wakili mwanadada nilipoona katulia kimiya huku kashikilia mlango.

‘Oh karibu, ….’akasema wakil mwanadada na kugeuka kuja kukaa, na sekunde chache zikapita bila kumuona huyo mgeni aliyegonga mlango na kukaibishwa na wakili mwanadada. Nilipoona hivyo nikageuka kumwangalia wakili mwanadada usoni, kutaka kumuuliza tena ni nani huyo aliyegonga mlango na mbona haingii ndani. Na mara nikasikia sauti kutoka nje ikisema;

‘Shemeji nilipita tu hapa kidogo,kutaka kuwajulia hali, kwani siku mbili tatu sijaweza kufika huku, je mnaendeleaje hapa,….naona mna maongezi na wakili wako, sitaki kuwaharibia maongezi yenu …nitakuja kesho au siku nyingine…’sauti ya shemeji yangu, mwanasheria  wa familia ya marehemu mume wangu ikasikika kwa nje.

‘Sasa kwanini huingii ndani, ….?’ Nikamuuliza huyo shemeji maana sio kawaida yake kufanya hivyo.

‘Kwani kuna shida yoyote?’ akauliza akiwa bado yupo huko nje, na kauli hiyo ilinishangaza sana maana huwa hafany I hivyo, kawaida yake akifika hapa kwangu ni lazima aingie ndani, atujulie hali, acheze na mtoto kidogo, hata kama ana haraak vipi.

‘Kama umekuja kuangalia familia yako, utaijuaje inaendelea vipi, wakati umesimama nje, kuna kitu gani unakiogopa, mbona siku zote ukifika unaingia hadi ndani….?’ Nikamuuliza.

Na hapo akafungua mlango na kuingia ndani,kwanza  alisimama pale mlangoni kwa sekude chache, , na akaita jina la mtoto, ambaye alikuwa kapumzika ndani, nikamwambia kuwa mtoto amepumzika ndani hajambo, kwani huo ulikuwa muda wake wa kulala, na nisingelipenda kumuamusha.

‘Hamna shida shemeji, nilikuwa napita tu, unajua hii kesi inaniwia nzito sana, hata muda wa kuja kuwasalimia unakuwa haupatikani, na hili linaniumiza moyo wangu kuwa nimeshindwa kutimiza ahadi yangu….’akatulia kidgogo, halafu akageuka kidogo kumwangalia wakili mwanadada, na alitaka kusema jambo lakini akasita halafu akanigeukia na kusema;

‘Unajua shemeji, najikuta nikitetea watu ambao hawataki kuniambia ukweli, na kila siku ya kesi najikuta nikikutana namambo mapya ambayo, wao walikuwa wamenificha…sijui kwanini hawaniambii ukweli mapema, nakuwa na wakati mgumu sana…’akawa analalamika na sasa akasogea kwenye sofa na kukaa.

‘Sasa shemeji, ina maana wewe uliamua kuwatetea bila kujirizisha,…hukufanya uchunguzi kwanza kwa hayo waliyoshitakiwa nayo, maana huenda ukawa unatetea wahalifu…’nikasema na yeye akatabasamu kidogo huku akingalia huku akiwa kaweka mkono kwenye uso wake na kunyosha kidole kimoja juu kikiwa kwenye muelekeo wa pua.

‘Mimi kwanza kabisa niliamua kufanya hivyo kwa ajili ya familia yangu, ….lakini baadaye watu wakanijia kuwa wanahitaji niwatetee….nikaona kwa vile maswala yote yanafanana, basi hakuna shida, na kwa vile nina uhakika kuwa familia yangu haina makosa, na makosa yaliyotokea ni kwa vile walijumuishwa na watu wanaosadikiwa ni wahalifu, …kwa mtizamo wa maaskari, kama ujuavyo samaki mmoja akioza wote wanaonekena wameoza,nikawa, sina budi kufanya hivyo….’akatulia.

‘Na ulijirizisha kuwa kweli hawana hatia?’ nikamuuliza na yeye kwanza akageuka kumwangalia wakili mwanadada, na alipona wakili mwanadada katulia akisoma makabrasha yake, akasema;.

‘Kwa maelezo yao, ukiyasikiliza kwa makini hata bila ya kutafuta vielelezo, unaona kabisa hawana hatia,….ila kuna tatizo kubwa,….’akageuka tena kumwangalia wakili mwanadada, na huenda alitaka hayo anayoyaongea ayasikie huyo wakili mwanadada.

‘Wengi wamekuwa wakinishinikiza kuwa kaka yangu ndiye aliyekuwa akiwahimiza kufanya hayo waliyoshitakiwa nayo , hapo inaniwia vigumu sana, maana nikiwatetea wao, namshinikiza kaka kwenye hatia….ndio maana nakuwa na wakati mgumu sana..’akasema na akageuza uso kumwangalia wakili mwanadada kama vila anahitajia ushauri wake, lakini wakili mwanadada likuwa akiendelea vile vile na shughuli zake.

‘J e wewe unavyoona, ni kweli kuwa kaka yako alihusika na hayo yote….unaamini maneno yao waliyokuambia, je wana ushahidi wowote wa hizo kauli zao?’ nikamuuliza na mimin nikageuka kumwangalia wakili mwanadada, nikitaka kujua hilo swali ni sahihi, au naingilia kazi yake.

Wakili mwanadada, akawa kashika peni, na kuanza kuandika jambo kwenye karatasi yake sikujua anaandika mambo yake, au alikuwa akifuatilia hayo mazungumzo yetu,yeye  alionekana kama vile hayupo kabisa na hayo tunayoyazungumza.

‘Kwa upande mmoja, najikuta kukubali hivyo, maana haiwezekani watu zaidi ya watano waseme hivyo hivyo, na ukifuatalia maneno yao na baadhi ya ushahidi mbali mbali, unakuwa huna jinsi ya kumtetea kaka yangu…lakini nikichulia hali halisi, kwa jinsi ninavyomfahamu kaka, nashindwa kukubalina na hoja zao…….’akatulia.

‘Kwahiyo wewe unamtetea kaka yako kwa vile unamfahamu tabia yake, na matendo yake, ya nyuma jinsi mlivyokuwa mukishi naye toka utoto wako na yeye, kuwa ndiye aliyekulea  ulipokuwa mdogo…..na kwahiyo hawezi kufanya hayo wanayosema kayafanya….huoni kuwa huo ni udhaifu wa kulipa fadhila tu…?’ nikamuuliza.

‘Ndio hivyo, kaka, pamoja na ukali wake, lakini hapendi kabisa kumwaga damu ya mtu…na ni kitu ambacho alikuwa akituasa sana, aliwahi kuniambia kuwa yeye hata ukitokea ugomvi, wakawa wanagombana na mwenzake, atajitahidi sana ….asimtoe damu…..’akasema na mimi nikacheka kwa dharau.

‘Huniambii kitu kuhusu shemeji mkubwa, oh, marehemu…shemeji lakini siku ile ulishuhudia mwenye akitaka kuni….kunitoa roho,.’nikasema kwa kubabaika, maana nilikuwa sipendi kumuongea ubaya marehemu, pia sikutaka kusema haya kwa wakili mwanadada, kwani sikuwahi kumwambia na sikupendelea ajue jinsi gani ilivyotokea siku hiyo, na wakili mwanadada aliposikua hivyo akainua uso kuniangalia kwa udadisi.

‘Lakini shsmeji, siku ile kaka alikuwa akikutishia tu angekushika vile na kukuachilia, asingelikuumiza kabisa… na alihuzunika sana kwa kitendo kile, kwani aliniambia, alijikuta akifanya vile kutokana na hali iliyokuwa ikimkabili,…mambo mengi yalikuwa yakimzonga, na watu wengi walikuwa hawataki kumuelewa….’akasema mwanasheria.

‘Sawa, mimi nilishasahu, ile nilitaka kukupinga kauli yako, maana wanaume mkipandisha hasira mnaweza kufanya matendo bila kufikiria athari yake baadaye..’nikasema na  huku nikinyosha kitambaa, baada ya kumimina juizi na kuweka stuli, mbele ya shemeji,nikaweka gilasi ya juisi na kumkaribisha.

‘ Sasa shemeji, nikuulize, maana wewe ni mwanasheria, unaifahamu vyema sheri, kwa hali kama hiyo utafanyaje, maana watu wamekuomba uwatetee, na ukiwatetea kihalali kama ulivyodai,  ina maana unamwingiza ndugu yako kwenye hatia, japokuwa hayupo duniani , lakini bado haki yake inatakiwa kulindwa…?’ nikamuuliza.

Akageuka kumwangalia wakili mwanadada bila kujibu swali langu, na baadaye akaangalia juu, huku akijaribu kuficha uso wake, ambao ulishajaa huzuni, na hata macho yalishaanza kuonyesha dalili ya machozi. Nahisi swali hilo lilimkumbusha mbali na akawa anamuwaza ndugu yake, na baadaye akasema;

‘Hata sijui….maana inanisikitisha sana, kuona kuwa sasa kaka keshaondoka, na watu alokuwa akiwaamini, …sasa wanamsingizia mambo mengi ambayo, sikuzania kuwa wangelifanya hivyo kama angelikuwa hai….natamani nijitoe kuwatetea hawa watu, lakini, kwasasa siwezi tena ….’akatulia na mara akainuka na kutaka kuondoka, na mara wakili mwanadada akasema;

‘Wewe ni wakili na umesomea sheria, kwanini unakuwa mdhaifu, inapofikia kwenye familia yako, kwanini hutumii taaluma yako vyema, ili kurekebisha makosa, hata kama yamefanywa na familia yako, lakini kwa kufanya hivyo, utakuwa umeiweka jamii katika mstari unaotakiwa hata kama kwa kufanya hivyo itakuwa kinyume na matakwa ya familia yako?’ akauliza wakili mwanadada.

 Na mwanasheria ambaye alikuwa kasimama kutaka kuondoka, kusikia sauti ya mwanadada, akawa kama alitamani kuiskia, akarudi kukaa, hakusema kitu, alitulia kwa muda, na mara simu yake ikaita, akaichukua kwa haraka, kama vile alikuwa akiisubiria, akaiangalia kuona ni nani aliyempigia, na mara uso wake ukabadilika, na kuonyesha wasiwasi, akageuka kutuangalia, na kusimama, akasema samhanai kidogo akatoka nje.

Wakili mwanadada, akainuka kwa haraka, na kuwa kama anamfuatilia, akasimama mlangoni, akiwa kama anasikiliza ni nini huyo mwanasheria anaongea, …ilichukua dakika tano, halafu huyo mwanasheria, akafungua mlango, na kujikuta wakiangaliana uso kwa na wakili mwanadada. Wakili mwanadada aliwahiwa kabla hajarudi kukaa kwenye sehemu yake

‘Ulikuwa unasikiliza eeh, sikuhizi umegeuka kuwa mpelelezi, ..ulitaka kusikia ni nini ninaongea…sasa umesikia niambia umepata nini cha muhimu?’ akauliza kwa mshangao.

‘Nilikuwa nakuja kufunga mlango, nikidhania umeshaondoka….bahati na wewe ndio ukafungua mlangi, ndio huvyo tu, kwani una wasiwasi gani…’akajitetea wakili mwanadada.

‘Sizani kama ulikuwa na lengo hilo, sauti yako inakusuta, hujaozoea kuongopa…nakufahamu sana wewe, lakini nataka kukuambia jambo moja, ….’akasema akiwa kasimama na kuangalia pembeni, hakuwa akimwangalia wakili mwanadada moja kwa moja.

‘Mimi sifanyi haya kwa nia mbaya, kama unavyonifikiria wewe, kama kweli sheria ipo wazi, na kama kweli nimepata ushahidi wa kutosha kuwa hilo ninalolifanya sio sahihi, …..nisingeliweza kufanya hili ninalolifanya sasa hivi…’akasema na wakili mwanadada ambye alikuwa naye bado kasimama akawa kageuka kuniangali mimi huku akimpa mgongo huyo mwanasheria.

‘Sawa..mimi nimekuelewa,ila nazidi kukusisitizia kuwa usije ukasahau taaluma yako ya sheria kwa ajili ya kutetea familia, ambayo huenda ina makosa….sikulaumu kwa hilo, kwasaabbu nafahamu hali unayokabiliana nayo, upo kwenye wakati mgumu sana, lakini usije ukajitwika mzigo ambao mwisho wake utajikuta ukija kujijutia..’akasema wakili mwanadada.

‘Kwanini unasema hivyo?’ akauliza mwanasheria.

‘Nikuulize swali, na nataka unijibu kwa ukweli wako….?’ Akauliza wakili mwanadada.

‘Najua unataka kuniuliza ni nani niliyekuwa nikiongea naye kwenye simu, na najua unanitega kwa vile umeshasikia nikiongea …na unafahau kabisa nilikuwa naongea na nani…’akasema mwanasheria.

‘Je upo tayari kumtetea?’ akaulizwa.

‘Nani…?’ akauliza mwanasheria akimkazia macho wakili mwanadada, na wakili mwanadada akatabasamu na kukaa kimiya, na mwanasheria akijua huyo wakili mwanadada ana maana gani, akasema;

‘Nimemjibu kuwa nahitaji kwanza kusikiliza maelezo yake, na kama nikirizika nayo, nitamtetea , maana yeye ni mmoja wa ukoo wangu,japokuwa sio karibu kihivyo, ndio maana hata vikao vya kifamilia, wao hawahusiki sana, labda kama ni jambo kubwa la ukoo mzima,…mahusiano yetu yanatoka kwa mababu zetu, ….kwahiyo  kwa namna moja yeye ni ndugu yangu, nastahili kumsaidia …kama ikibidi…’akasema.

‘Kama ikibidi, hata kama ana makosa?’ akauliza wakili mwanadada huku akishika kichwa wa kidole, na hakuwa anamwangalia mwanasheria huyo. Na mwanasheria akashika kichwa kama anawaza jambo. Wakili mwanadada akaenda pale alipokaa huyo mwanasheria akapiga magoti karibu yake na kusema;

‘Sikiliza `mate’…kumbuka tulipotoka, kumbuka yale ya masomoni, unakumbuka siku moja tuliwahi kulijadili hili na wewe ukasema, wewe utasimamia kwenye sheria na haki, hata kama ni kupambana na ndugu yako wa tumbo, utafanya hivyo, ilimradi ukijua kuwa unachokitetea ni haki….unakumbuka….’akasema wakili mwanadada akiwa anamuonyeshea kwa mkono, lakini mwanasheria, akawa kama anamkwepa kumwangalia huyo mwanadada usoni, akawa kashika kichwa huku kaangalia pembeni.

‘Kwani sasa mimi nimefanya lipi la kukiuka hayo ya masomoni, …natimiza wajibu wangu, au ni kwa vile nawatetea ndugu zangu ndio maana unaona nafanya makosa?’ akauliza huku akiwa hamuangali wakili mwanadada, alikuwa vile vile kashika kichwa…ilikuwa kama watu wasiojuana kabisa.

‘Kwanini unaziba amsikio na macho, kwa kitu ambacho kipo wazi,…huyo uliyekuwa ukiongea naye huoni kama ana makosa…?’ akaulizwa.

‘Sizani kama ana makosa, kutoka na wadhifa alio nao, hawezi kufanya makosa hayo, labda kuwajibika tu kwa vile kiongozi unabeba lawama za kila mtu, hata kama kiongozi huyo hajui ni nini kilichotokea…na kama ana makosa nitamshauri ipasavyo iwe….’akasema na wakili mwanadada kusikia hivyo, akasimama na kurudi pale alipokuwa amekaa, huku akisema;

‘Na kama umemshauri akasisitiza kuwa umtetee, kwa vile anajua ukifanya hivyo unaweza ukacheza na sheria, kama mlivyozoea kufanya ili tu mtu aweze  kuingiza kipato…’akasema na mwanasheria akaonyesha kukerwa na kauli hiyo akasema;

‘Lini nimefanya hivyo…hizo shutuma zako hazina msingi, kwasababu  sifanyi hivyo kwa ajili ya kupata chochote, hawo ni ndugu zangu, ni raia wema kabisa, na wengi ni wa ukoo wangu, siwezi kudai hata senti moja kutoka kwao, mbona unanishutumu kwa jambo nisilowahi kulifanya..’akasema kwa hasira.

‘Samahani nimekosea usemi wangu kama umelewa hivyo, lakini lengo langu lilikuwa na maana ya ujumla, kuwa kuna mawakili wapo radhi, kufanya kazi zao hata kama yule wanayemtetea ana hatia, ..anafanya hivyo kwa ajili ya masilahi tu….sasa na wewe usije ukajiingiza huko,…nilikuwa na maana hiyo ya kukuasa…au nimekosea ?’akasema wakili mwanadada.

‘Mwanadada, usije ukaweka mambo yetu binafsi kwenye hii kesi, ….nakuomba sana….’akasema huku akimnyoshea kidole wakili mwanadada, na wakili mwanadada akawa katulia akiangalia kile kidole cha mwanasheria, na yule mwanasheria, akashusha mkono wake, halafu akaendelea kuongea kwa kusema;

‘Mimi nafanya haya kwa vile nawajibika na familia yangu, kama unavyoona….sifanyi haya kwa ubinafsi wangu, kama unavyoona, hivi sasa nimekabidhiwa uongozi wa familia, je kwa hali kama hiyo unafikiria ningelifanyaje, ….hebu niambie, au kwa vile huna uchungu na familia yangu, unataka mimi nikae kimiya, …eti niache kuisaidia familia niliyokabidhiwa na kuipa mgongo…hilo haliwezekani!’ akawa kama anauliza na kumwangalia wakili mwanadada, huku akiwa kama anasubiri kupata jibu, halafu akakuna kichwa mfululizo na kusema.

‘Hivi kwa ingelikuwa wewe, ungefanyaje…..eti,, kwa vile wanashukiwa kuwa wao wana makosa, nikae kimiya hata kujaribu kuwatetea, angalau waone nipo nao,kama wanashukiwa wana haki ya kujitetea na kupata mtu wa kuwatetea, na ndivyo ninavyofanya …..naona wewe unasema hivyo kwa vile haupo kwenye sehemu yangu,….na je kama wana makosa hayo makosa yapo wapi, upo wapi ushahidi wa makosa yao…mbona hutaki kunionyesha huo ukweli na ushahidi ili nisipoteze muda wa kuwatetea, wewe mwenyewe unanifahamu, kuwa nikugundua ukweli, nipo vipi…unao ushahidi…?.’akawa kama anauliza.

Wakili mwanadada, akatabasamu huku anatikisa kichwa, akainua kichwa na kumwangalia mwanasheria akasema;

‘Mimi nakuhakikishia kuwa hawo unaowatetea hasa huyo uliyetoka kuongea naye kwenye simu sasa hivi wana hatia…na nashangaa sana, ukisema ni mmoja wa ukoo wenu, …., na bado kadiriki, kumwanga damu ya ndugu yake….’akasema wakili mwanadada, na mwanasheria akashituka na kauli hiyo na kumwangalia mwanadada huyo kwa macho ya kushangaa, huku kayakodoa macho, kama vile haamini hicho alichosikia, akauliza.

‘Eti nini,…una maana gani kusema hivyo?’ akauliza huku akiinuka pale alipokuwa amekaa na kumsogelea mwanadada huyo, na simu ya wakili mwanadada ikaita, na huyo mwanadada kama vile anafahamu ni nani aliyempigia hiyo simu, akaichukua na kuitupia macho mara moja, halafu akasema;

‘Samahani kidogo nataka kuongea na simu, na nitaenda kuongelea nje…’ akasema na kuniangalia mimi mara moja, halafu akamgeukia huyo mwanasheria na kusema;

‘Kama unaondoka tutaonana mahakamani, nitakuthibitishia kila nilichokiongea hapa, na mengineyo kuwa mimi ndio nimesimamia kwenye haki na ukweli, na ili unione kuwa mimi nipo sahihi, lakini siwezi kukuonyesha hapa,..unaelewa ni kwanini nasema hivyo….samahani, ngoja nikapokee simu…’akasema wakili mwanadada, huku simu ikiendelea kuita.

‘Sikuelewe, ina maana umefikia hatua hiyo…kama kweli unafahamu jambo kama hilo halafu unanificha , jambo nzito kama hilo,…hutaki kuniambia ukweli, ..siamini, na kama hivyo , sizani kama tutakuja kungea vyema mimi na wewe….’akasema mwanasheria na wakili mwanadada akamtupia jicho, na akawa kama anatabsamu, halafu akatoka nje, na kuusindika ule mlango kwa nje, kuhakikisha kuwa amefungika vyema, naona aliogopa mwenzake asije akafanya kama alivyofanya yeye.

*****
Tulibakia mimi na shemeji yangu, na kwanza kulitawala ukimiya halafu akasema;

‘Hebu niambie shemeji, Mwanadada ana maana gani kusema hivyo?’ akaniuliza baada ya kupita ukimiya fulani, na hatukuweza kusikia sauti yoyote nje ya mwanadada akiongea na simu, inaonekana alikwenda mbali kidogo, au alikuwa akiongea kwa sauti ya chini.

‘Kuhusu nini, kuhusu kuwa familia yako unayoitetea ina makosa au kuhusu nini hasa maana hapa yameongelewa mengi..?’ nikauliza nikitaka kujua alikuwa kakusidia nini hasa.Na huyu mwanasherai akashika kichwa kuonyesha kuwaza jambo, na hilo jambo lilionekana kumkera sana, akasema huku akiwa kainama chini.

‘Hiyo kauli yake, kuwa kuna mtu wa ukoo wetu, …kuwa eti ndiye aliyehusika kumuua kaka yangu, maana mimi nilifuatlia kabisa kuhusu kifi cha kaka, ilionekana kaka kafa kwa shinikizo la damu, na hii nijuavyo, na nilishamkanya kaka mara nyingi, ni kutokana na hasira zake, …na pia inawezekana ikawa ni shinikizo kwa hali halisi aliyokuwa akikabiliana nayo,….sikuweza kulipinga hilo, maana kaka alishaanza kulalamika toka awali kuwa ana tatizo la shinikizo la damu…sasa haya ninayoyasikia kwa Mwanadada ni mapya kwangu…sijui kama ana ushahidi gani, na kwanini hataki kuniambia ukweli, kwa jambo nzito kama hilo…..’akasema mwanasheria.

‘Kwani kwa kauli hiyo ya wakili mwanadada, ana maanisha ni nani hasa aliyefanya hivyo, maana kaongea kwa ujumla ,mimi sikusikia akimtaja mtu,…. na huwezi ukathibitisha kuwa alikuwa akimuongelea mtu fulani kutokana na kauli yake…na jinsi alivyokuwa akiongea, labda kwa vile mnajuana, huenda wewe umegundua kuwa anamuelezea mtu fulani, au wewe unamfahamu huyo aliyekuwa akimuongelea?’ nikamuuliza.

‘Nina uhakika kuwa wakati naongea na simu , huyo wakili mwanadada, alikuwa kasimama hapo nyuma ya mlango,, akinisikiliza,…nilijua hilo,…lakini sikujali sana maana halikuwa na uzito, hata kama angelisikia, lakini hakuwa na haki ya kufanya hivyo…kwahiyo huyo niliyekuwa nikiongea naye, ndiye anayemnyoshea kidole kuwa huenda anahusika na kifo cha kaka…kitu ambacho hakiingii akilini kwangu, hata siku moja siwezi kuliwazia hilo…huyo hawezi kabisa, labda amtaje mtu mwingine, na hata hivyo, kaka kafa kifo cha kawaida…...’akasema.

‘Lakini dunia hii ina maajabu yake, umzanie kuwa siye, anaweza kuwa ndiye..na hasa kunapotokea makundi yenye msimamo mkali kama hilo liligundulikana hapa….wao wanasimamia katika mantiki yao, kuwa wanachofanya ni sahihi,…na huwezi kuwageuza katika itikadi yao hiyo…na pia kuna mambo ya kula amini, kuwa ni lazima hili lifanyike ili mambo yasonge mbele..ni makubaliano yenya msimamo mkali. Kama yeye alionekana ni kikwazo kwenye kundi, au angaliweza kutoa siri, sioni ajabu wakiamua kumuua…’nikasema.

‘Usije ukatekwa na tabia za huyo mwanadada….mimi nimegundua kitu, yeye kwasasa anatafuta umaarufu, wengi wanafanya hivyo, kuwa ili uweze kujulikana kwenye kazi zako, unahitajika kujitangaza, na kujitangaza kupo kwa njia mbali mbali…usione watu wanaweka mapicha yao kwenye mitandao, magezeti nk,  ukafikiria wana maana gani,…’akatulia kidogo, akiniangalia moja kwa moja usoni, na mimi nikamkwepa kuangaliana naye moja kwa moja usoni.

‘Kila mmoja ana malengo yake moyoni, …lakini shemeji kiukweli hayo yote kwa ujumla wake yanafanyia kwa malengo ya kutaka kujitangaza, au kutangaza hilo mtu alilolikusudia moyoni mwake,…japokuwa makusudio mengi yapo ndani ya muhusika mwenyewe…sasa huyu mwanadada, nahisi na ndivyo ilivyo,anatumia njia hii ya kujifanya anatetea watu, kwa minajili ya kujitangaza, wewe huoni kwa muda mfupi sasa jina lake linatajwa kila kona….?’akasema kama anauliza.

‘Mimi sikatai hilo la kijitangaza, lakini kujitangaza huko kuwe na lengo jema,…kama ulivyosema kuweka picha, …watu wengine wanaweka picha kwa malego mema, kuwa dhamira yao ni ya dhati kufikisha ujumbe fulani, na watu kama hao wanajiamini, kuwa hata wakijulikana hawama shaka….na halikadhalika, mwanadada, nia yake sio mbaya, hata kama anatumia hivyo kujitangaza, lakini anajitangaza kwa kutenda yale yaliyosahihi…na ndio maana hana wasiwasi, anajiamini….’nikasema.

‘Naona sasa wewe umeshatekwa na huyu dada eeh…unaanza kujitenga na familia ya mume wako, hata mwaka haujaisha umeshaanza kumsahau  mume wako, kwa ajili ya kumwezesha mwanadada kutimiza malengo yake….shemeji mimi ninachokifanya ni kwa ajili ya familia yetu, familia aliyotoka mumeo, familia ya mtoto wako, je hapo nina makosa gani?’ akawa kama anauliza.

‘Mbona unabadili muelekeo wa hoja yetu…mimi sijakupinga kabisa hilo la kuitetea  familia yako,…hapa tulikuwa tukimuongea mwanadada, kuwa wewe unaona anajitangaza, na kwahiyo na mimi namtetea yeye,..au sio, …lakini sijajitenga na familia yangu kwa kutizama mambo kwa usahihi wake,…tugeukiwa upende wa mwanadada,mimi nakuambia ukweli kuwa kwa kipindi kifupi nilichomfahamu yeye, ninakiri kuwa yeye kweli ni mtetezi wa haki…hilo nakuthibitishia na hilo litamtangaza sana….anastahiki kupongezwa, na mola atamsaidia ….’nikasema na mara wakili mwanadada akingia.

‘Jamani mimi nahitajika kikazi..tutaonana baadaye…’akasema huku akichukua mkoba wake na kuyaweka makabrasha yake ndani ya huo mkoba, akaniangalia mara moja, akatoa tabasamu kidogo, halafu bila ya kumwangalia mwanasheria akaanza kuelekea mlangoni. Mwanasheria, kuona mwanadada anaondoka akamkimbilia na kumshika mkono.

‘Hatujamalizana, …huwezi kuniacaah hewani, hebu niambie kuhusu kauli yako kuwa huyo niliyekwua nikiongea naye kwenye simu, anahusikaje na kifo cha kaka yangu , wakati kaka yangu kafariki kwa shinikizo la damu?’ akauliza na wakili mwanadada akamwangalia huku akitabasamu kwa dharau. Na mwaansheria akawa kamuachia huyo mwanadada mkono, na akawa anaangaliana uso kwa uso na huyo mwanadada, aliyegeuza kichwa tu.

‘Usitie shaka, hayo na mengine mengi utayapata mahakamani, kwasasa siwezi kukuambia jambo, maana sasa hivi tuwapinzani kuhusiana na hiyo kesi, siwezi kumwanga sera zangu kwako, ambazo natarajia zitakuwa silaha zangu kwenye ulingo wa mapambano,…lakini katika kuitetea haki…’akasema wakili mwanadada, na alipotaka kuondoka mwanasheria akamshika mkono kumzuia.

Wakili mwanadada, taratibu akashusha uso kuangalia ule mkono wa mwanasheria uliokuwa umemshika, na mwanasheria alipoona huyo mwanadada anauangalia mkono wake, ambao umeshika mkono wa mwanasheria, kama vile kafanya makosa kumshika, akauondoa mkono wake kwa haraka, na kufanya kama anaukung’uta mkono wake na akasema;

‘Samahani muheshimiwa wakili mwanadada…’ na wakili mwanadada akainua uso taratibu na kumwangalia usoni mwanasheria huyo, sasa hivi uso uliomwangalia mwanasheria huyu,  sio ule wa legelege, ulikuwa uso wa kazi, uso uliojaa ujasiri, ..na macho yasiyotetereka yakamwangalia moja kwa moja mwanasheria huyu, na mwanasheria naye akajitahidi kufanya hivyo hivyo, kwahiyo wakawa kama wapiganaji wawili waliokuwa wakitunishiana misuli. Mimi pale nikatabasamu …..

Wakili mwanadada akawa wa kwanza kuongea, na kwa sauti ya kijasiri akasema;

‘Tutaonana mahakamani…’
Lakini mwanasheria hakusema kitu, akabakia ameduwaa, bado akimwangalia wakili mwanadada ambaye alikuwa akitoka nje, na kuondoka, hata bila ya kuniaga.

NB, Haya naona sasa tutaingia kwenye kesi yenyewe baada ya utangulizi huo

WAZO LA LEO: Ushindani katika mambo mema unaruhusiwa, na wakati mnashindana, mnakuwa mahasimu , huku mkijua lengo lenu ni kutafuta muafaka, au maendeleo, kw kila mmoja kuonyesha ubora wa hoja zake…


Na baada ya kupatikana mshindi, inabidi nyote mrudi na kuwa kitu kimoja kwa kushikana mikono na kupongezana, huku mkiwekeza kwa lile mlolokuwa mkilipigania,..huu ndio ushandani wa haki, na  tunaweza kuuita vyovyote tupendavyo, lakini lengo ni kwa ajili ya mema, kwa manufaa ya jamii.

Ni mimi: emu-three

3 comments :

Unknown said...

Dah malipo ni hapahapa duniani na mungu ni wa wote milele, kila la heri mdada mwanasheria

Unknown said...

Dah malipo ni hapahapa duniani na mungu ni wa wote milele, kila la heri mdada mwanasheria

Rachel Siwa said...

Hongera sana ndugu wa mimi.. kazi nzuri sana sana...