Wakili mwanadada
alisimama na kwenda kufungua mlango, na mlango ulipofunguka akajikuta kama
anashituka kuashiria kuwa aliyemuona hakutarajia kuonana naye, kwanza alitulia
akawa anamuangalai huyo mtu kwa nje, na mimi pale nilipokuwa nimekaa, sikuweza
kumtambua ni nani, maana huyo mtu aligonga mlango bila kutoa kauli ya hodi.
Mimi kwa muda huo nilikuwa nikimalizia kuondoa vyombo tulivyokuwa tukitumia kupata
chakula cha mchana…’akaendelea kunihadithia mama kuhusu maisha yake
‘Ni nani mbona umeduwaa, na hufungui mlango….?’ Nikamuuliza
wakili mwanadada nilipoona katulia kimiya huku kashikilia mlango.
‘Oh karibu, ….’akasema wakil mwanadada na kugeuka kuja
kukaa, na sekunde chache zikapita bila kumuona huyo mgeni aliyegonga mlango na
kukaibishwa na wakili mwanadada. Nilipoona hivyo nikageuka kumwangalia wakili
mwanadada usoni, kutaka kumuuliza tena ni nani huyo aliyegonga mlango na mbona
haingii ndani. Na mara nikasikia sauti kutoka nje ikisema;
‘Shemeji nilipita tu hapa kidogo,kutaka kuwajulia hali,
kwani siku mbili tatu sijaweza kufika huku, je mnaendeleaje hapa,….naona mna
maongezi na wakili wako, sitaki kuwaharibia maongezi yenu …nitakuja kesho au
siku nyingine…’sauti ya shemeji yangu, mwanasheria wa familia ya marehemu mume wangu ikasikika
kwa nje.
‘Sasa kwanini huingii ndani, ….?’ Nikamuuliza huyo shemeji
maana sio kawaida yake kufanya hivyo.
‘Kwani kuna shida yoyote?’ akauliza akiwa bado yupo huko
nje, na kauli hiyo ilinishangaza sana maana huwa hafany I hivyo, kawaida yake
akifika hapa kwangu ni lazima aingie ndani, atujulie hali, acheze na mtoto
kidogo, hata kama ana haraak vipi.
‘Kama umekuja kuangalia familia yako, utaijuaje inaendelea
vipi, wakati umesimama nje, kuna kitu gani unakiogopa, mbona siku zote ukifika
unaingia hadi ndani….?’ Nikamuuliza.
Na hapo akafungua mlango na kuingia ndani,kwanza alisimama pale mlangoni kwa sekude chache, ,
na akaita jina la mtoto, ambaye alikuwa kapumzika ndani, nikamwambia kuwa mtoto
amepumzika ndani hajambo, kwani huo ulikuwa muda wake wa kulala, na
nisingelipenda kumuamusha.
‘Hamna shida shemeji, nilikuwa napita tu, unajua hii kesi
inaniwia nzito sana, hata muda wa kuja kuwasalimia unakuwa haupatikani, na hili
linaniumiza moyo wangu kuwa nimeshindwa kutimiza ahadi yangu….’akatulia
kidgogo, halafu akageuka kidogo kumwangalia wakili mwanadada, na alitaka kusema
jambo lakini akasita halafu akanigeukia na kusema;
‘Unajua shemeji, najikuta nikitetea watu ambao hawataki
kuniambia ukweli, na kila siku ya kesi najikuta nikikutana namambo mapya
ambayo, wao walikuwa wamenificha…sijui kwanini hawaniambii ukweli mapema,
nakuwa na wakati mgumu sana…’akawa analalamika na sasa akasogea kwenye sofa na
kukaa.
‘Sasa shemeji, ina maana wewe uliamua kuwatetea bila
kujirizisha,…hukufanya uchunguzi kwanza kwa hayo waliyoshitakiwa nayo, maana huenda
ukawa unatetea wahalifu…’nikasema na yeye akatabasamu kidogo huku akingalia
huku akiwa kaweka mkono kwenye uso wake na kunyosha kidole kimoja juu kikiwa
kwenye muelekeo wa pua.
‘Mimi kwanza kabisa niliamua kufanya hivyo kwa ajili ya
familia yangu, ….lakini baadaye watu wakanijia kuwa wanahitaji
niwatetee….nikaona kwa vile maswala yote yanafanana, basi hakuna shida, na kwa
vile nina uhakika kuwa familia yangu haina makosa, na makosa yaliyotokea ni kwa
vile walijumuishwa na watu wanaosadikiwa ni wahalifu, …kwa mtizamo wa maaskari,
kama ujuavyo samaki mmoja akioza wote wanaonekena wameoza,nikawa, sina budi
kufanya hivyo….’akatulia.
‘Na ulijirizisha kuwa kweli hawana hatia?’ nikamuuliza na
yeye kwanza akageuka kumwangalia wakili mwanadada, na alipona wakili mwanadada
katulia akisoma makabrasha yake, akasema;.
‘Kwa maelezo yao, ukiyasikiliza kwa makini hata bila ya
kutafuta vielelezo, unaona kabisa hawana hatia,….ila kuna tatizo kubwa,….’akageuka
tena kumwangalia wakili mwanadada, na huenda alitaka hayo anayoyaongea ayasikie
huyo wakili mwanadada.
‘Wengi wamekuwa wakinishinikiza kuwa kaka yangu ndiye
aliyekuwa akiwahimiza kufanya hayo waliyoshitakiwa nayo , hapo inaniwia vigumu
sana, maana nikiwatetea wao, namshinikiza kaka kwenye hatia….ndio maana nakuwa
na wakati mgumu sana..’akasema na akageuza uso kumwangalia wakili mwanadada
kama vila anahitajia ushauri wake, lakini wakili mwanadada likuwa akiendelea
vile vile na shughuli zake.
‘J e wewe unavyoona, ni kweli kuwa kaka yako alihusika na
hayo yote….unaamini maneno yao waliyokuambia, je wana ushahidi wowote wa hizo
kauli zao?’ nikamuuliza na mimin nikageuka kumwangalia wakili mwanadada,
nikitaka kujua hilo swali ni sahihi, au naingilia kazi yake.
Wakili mwanadada, akawa kashika peni, na kuanza kuandika jambo
kwenye karatasi yake sikujua anaandika mambo yake, au alikuwa akifuatilia hayo
mazungumzo yetu,yeye alionekana kama vile
hayupo kabisa na hayo tunayoyazungumza.
‘Kwa upande mmoja, najikuta kukubali hivyo, maana
haiwezekani watu zaidi ya watano waseme hivyo hivyo, na ukifuatalia maneno yao
na baadhi ya ushahidi mbali mbali, unakuwa huna jinsi ya kumtetea kaka yangu…lakini
nikichulia hali halisi, kwa jinsi ninavyomfahamu kaka, nashindwa kukubalina na
hoja zao…….’akatulia.
‘Kwahiyo wewe unamtetea kaka yako kwa vile unamfahamu tabia
yake, na matendo yake, ya nyuma jinsi mlivyokuwa mukishi naye toka utoto wako
na yeye, kuwa ndiye aliyekulea ulipokuwa
mdogo…..na kwahiyo hawezi kufanya hayo wanayosema kayafanya….huoni kuwa huo ni
udhaifu wa kulipa fadhila tu…?’ nikamuuliza.
‘Ndio hivyo, kaka, pamoja na ukali wake, lakini hapendi
kabisa kumwaga damu ya mtu…na ni kitu ambacho alikuwa akituasa sana, aliwahi
kuniambia kuwa yeye hata ukitokea ugomvi, wakawa wanagombana na mwenzake,
atajitahidi sana ….asimtoe damu…..’akasema na mimi nikacheka kwa dharau.
‘Huniambii kitu kuhusu shemeji mkubwa, oh, marehemu…shemeji lakini siku ile ulishuhudia mwenye
akitaka kuni….kunitoa roho,.’nikasema kwa kubabaika, maana nilikuwa sipendi kumuongea ubaya marehemu, pia sikutaka kusema haya kwa wakili mwanadada, kwani
sikuwahi kumwambia na sikupendelea ajue jinsi gani ilivyotokea siku hiyo, na
wakili mwanadada aliposikua hivyo akainua uso kuniangalia kwa udadisi.
‘Lakini shsmeji, siku ile kaka alikuwa akikutishia tu
angekushika vile na kukuachilia, asingelikuumiza kabisa… na alihuzunika sana
kwa kitendo kile, kwani aliniambia, alijikuta akifanya vile kutokana na hali
iliyokuwa ikimkabili,…mambo mengi yalikuwa yakimzonga, na watu wengi walikuwa
hawataki kumuelewa….’akasema mwanasheria.
‘Sawa, mimi nilishasahu, ile nilitaka kukupinga kauli yako,
maana wanaume mkipandisha hasira mnaweza kufanya matendo bila kufikiria athari
yake baadaye..’nikasema na huku
nikinyosha kitambaa, baada ya kumimina juizi na kuweka stuli, mbele ya
shemeji,nikaweka gilasi ya juisi na kumkaribisha.
‘ Sasa shemeji, nikuulize, maana wewe ni mwanasheria,
unaifahamu vyema sheri, kwa hali kama hiyo utafanyaje, maana watu wamekuomba
uwatetee, na ukiwatetea kihalali kama ulivyodai, ina maana unamwingiza ndugu yako kwenye hatia,
japokuwa hayupo duniani , lakini bado haki yake inatakiwa kulindwa…?’ nikamuuliza.
Akageuka kumwangalia wakili mwanadada bila kujibu swali
langu, na baadaye akaangalia juu, huku akijaribu kuficha uso wake, ambao
ulishajaa huzuni, na hata macho yalishaanza kuonyesha dalili ya machozi. Nahisi
swali hilo lilimkumbusha mbali na akawa anamuwaza ndugu yake, na baadaye
akasema;
‘Hata sijui….maana inanisikitisha sana, kuona kuwa sasa kaka
keshaondoka, na watu alokuwa akiwaamini, …sasa wanamsingizia mambo mengi
ambayo, sikuzania kuwa wangelifanya hivyo kama angelikuwa hai….natamani nijitoe
kuwatetea hawa watu, lakini, kwasasa siwezi tena ….’akatulia na mara akainuka
na kutaka kuondoka, na mara wakili mwanadada akasema;
‘Wewe ni wakili na umesomea sheria, kwanini unakuwa mdhaifu,
inapofikia kwenye familia yako, kwanini hutumii taaluma yako vyema, ili
kurekebisha makosa, hata kama yamefanywa na familia yako, lakini kwa kufanya
hivyo, utakuwa umeiweka jamii katika mstari unaotakiwa hata kama kwa kufanya
hivyo itakuwa kinyume na matakwa ya familia yako?’ akauliza wakili mwanadada.
Na mwanasheria ambaye
alikuwa kasimama kutaka kuondoka, kusikia sauti ya mwanadada, akawa kama
alitamani kuiskia, akarudi kukaa, hakusema kitu, alitulia kwa muda, na mara
simu yake ikaita, akaichukua kwa haraka, kama vile alikuwa akiisubiria,
akaiangalia kuona ni nani aliyempigia, na mara uso wake ukabadilika, na
kuonyesha wasiwasi, akageuka kutuangalia, na kusimama, akasema samhanai kidogo akatoka
nje.
Wakili mwanadada, akainuka kwa haraka, na kuwa kama
anamfuatilia, akasimama mlangoni, akiwa kama anasikiliza ni nini huyo mwanasheria
anaongea, …ilichukua dakika tano, halafu huyo mwanasheria, akafungua mlango, na
kujikuta wakiangaliana uso kwa na wakili mwanadada. Wakili mwanadada aliwahiwa
kabla hajarudi kukaa kwenye sehemu yake
‘Ulikuwa unasikiliza eeh, sikuhizi umegeuka kuwa mpelelezi,
..ulitaka kusikia ni nini ninaongea…sasa umesikia niambia umepata nini cha
muhimu?’ akauliza kwa mshangao.
‘Nilikuwa nakuja kufunga mlango, nikidhania umeshaondoka….bahati
na wewe ndio ukafungua mlangi, ndio huvyo tu, kwani una wasiwasi gani…’akajitetea
wakili mwanadada.
‘Sizani kama ulikuwa na lengo hilo, sauti yako inakusuta,
hujaozoea kuongopa…nakufahamu sana wewe, lakini nataka kukuambia jambo moja, ….’akasema
akiwa kasimama na kuangalia pembeni, hakuwa akimwangalia wakili mwanadada moja kwa
moja.
‘Mimi sifanyi haya kwa nia mbaya, kama unavyonifikiria wewe,
kama kweli sheria ipo wazi, na kama kweli nimepata ushahidi wa kutosha kuwa
hilo ninalolifanya sio sahihi, …..nisingeliweza kufanya hili ninalolifanya sasa
hivi…’akasema na wakili mwanadada ambye alikuwa naye bado kasimama akawa
kageuka kuniangali mimi huku akimpa mgongo huyo mwanasheria.
‘Sawa..mimi nimekuelewa,ila nazidi kukusisitizia kuwa usije
ukasahau taaluma yako ya sheria kwa ajili ya kutetea familia, ambayo huenda ina
makosa….sikulaumu kwa hilo, kwasaabbu nafahamu hali unayokabiliana nayo, upo
kwenye wakati mgumu sana, lakini usije ukajitwika mzigo ambao mwisho wake
utajikuta ukija kujijutia..’akasema wakili mwanadada.
‘Kwanini unasema hivyo?’ akauliza mwanasheria.
‘Nikuulize swali, na nataka unijibu kwa ukweli wako….?’
Akauliza wakili mwanadada.
‘Najua unataka kuniuliza ni nani niliyekuwa nikiongea naye
kwenye simu, na najua unanitega kwa vile umeshasikia nikiongea …na unafahau
kabisa nilikuwa naongea na nani…’akasema mwanasheria.
‘Je upo tayari kumtetea?’ akaulizwa.
‘Nani…?’ akauliza mwanasheria akimkazia macho wakili
mwanadada, na wakili mwanadada akatabasamu na kukaa kimiya, na mwanasheria
akijua huyo wakili mwanadada ana maana gani, akasema;
‘Nimemjibu kuwa nahitaji kwanza kusikiliza maelezo yake, na
kama nikirizika nayo, nitamtetea , maana yeye ni mmoja wa ukoo wangu,japokuwa
sio karibu kihivyo, ndio maana hata vikao vya kifamilia, wao hawahusiki sana,
labda kama ni jambo kubwa la ukoo mzima,…mahusiano yetu yanatoka kwa mababu zetu,
….kwahiyo kwa namna moja yeye ni ndugu
yangu, nastahili kumsaidia …kama ikibidi…’akasema.
‘Kama ikibidi, hata kama ana makosa?’ akauliza wakili
mwanadada huku akishika kichwa wa kidole, na hakuwa anamwangalia mwanasheria
huyo. Na mwanasheria akashika kichwa kama anawaza jambo. Wakili mwanadada
akaenda pale alipokaa huyo mwanasheria akapiga magoti karibu yake na kusema;
‘Sikiliza `mate’…kumbuka tulipotoka, kumbuka yale ya
masomoni, unakumbuka siku moja tuliwahi kulijadili hili na wewe ukasema, wewe utasimamia
kwenye sheria na haki, hata kama ni kupambana na ndugu yako wa tumbo, utafanya
hivyo, ilimradi ukijua kuwa unachokitetea ni haki….unakumbuka….’akasema wakili
mwanadada akiwa anamuonyeshea kwa mkono, lakini mwanasheria, akawa kama
anamkwepa kumwangalia huyo mwanadada usoni, akawa kashika kichwa huku kaangalia
pembeni.
‘Kwani sasa mimi nimefanya lipi la kukiuka hayo ya masomoni,
…natimiza wajibu wangu, au ni kwa vile nawatetea ndugu zangu ndio maana unaona
nafanya makosa?’ akauliza huku akiwa hamuangali wakili mwanadada, alikuwa vile
vile kashika kichwa…ilikuwa kama watu wasiojuana kabisa.
‘Kwanini unaziba amsikio na macho, kwa kitu ambacho kipo
wazi,…huyo uliyekuwa ukiongea naye huoni kama ana makosa…?’ akaulizwa.
‘Sizani kama ana makosa, kutoka na wadhifa alio nao, hawezi
kufanya makosa hayo, labda kuwajibika tu kwa vile kiongozi unabeba lawama za
kila mtu, hata kama kiongozi huyo hajui ni nini kilichotokea…na kama ana makosa
nitamshauri ipasavyo iwe….’akasema na wakili mwanadada kusikia hivyo, akasimama
na kurudi pale alipokuwa amekaa, huku akisema;
‘Na kama umemshauri akasisitiza kuwa umtetee, kwa vile
anajua ukifanya hivyo unaweza ukacheza na sheria, kama mlivyozoea kufanya ili
tu mtu aweze kuingiza kipato…’akasema na
mwanasheria akaonyesha kukerwa na kauli hiyo akasema;
‘Lini nimefanya hivyo…hizo shutuma zako hazina msingi,
kwasababu sifanyi hivyo kwa ajili ya
kupata chochote, hawo ni ndugu zangu, ni raia wema kabisa, na wengi ni wa ukoo
wangu, siwezi kudai hata senti moja kutoka kwao, mbona unanishutumu kwa jambo
nisilowahi kulifanya..’akasema kwa hasira.
‘Samahani nimekosea usemi wangu kama umelewa hivyo, lakini
lengo langu lilikuwa na maana ya ujumla, kuwa kuna mawakili wapo radhi, kufanya
kazi zao hata kama yule wanayemtetea ana hatia, ..anafanya hivyo kwa ajili ya
masilahi tu….sasa na wewe usije ukajiingiza huko,…nilikuwa na maana hiyo ya
kukuasa…au nimekosea ?’akasema wakili mwanadada.
‘Mwanadada, usije ukaweka mambo yetu binafsi kwenye hii
kesi, ….nakuomba sana….’akasema huku akimnyoshea kidole wakili mwanadada, na
wakili mwanadada akawa katulia akiangalia kile kidole cha mwanasheria, na yule
mwanasheria, akashusha mkono wake, halafu akaendelea kuongea kwa kusema;
‘Mimi nafanya haya kwa vile nawajibika na familia yangu,
kama unavyoona….sifanyi haya kwa ubinafsi wangu, kama unavyoona, hivi sasa
nimekabidhiwa uongozi wa familia, je kwa hali kama hiyo unafikiria
ningelifanyaje, ….hebu niambie, au kwa vile huna uchungu na familia yangu,
unataka mimi nikae kimiya, …eti niache kuisaidia familia niliyokabidhiwa na kuipa
mgongo…hilo haliwezekani!’ akawa kama anauliza na kumwangalia wakili mwanadada,
huku akiwa kama anasubiri kupata jibu, halafu akakuna kichwa mfululizo na
kusema.
‘Hivi kwa ingelikuwa wewe, ungefanyaje…..eti,, kwa vile wanashukiwa
kuwa wao wana makosa, nikae kimiya hata kujaribu kuwatetea, angalau waone nipo
nao,kama wanashukiwa wana haki ya kujitetea na kupata mtu wa kuwatetea, na
ndivyo ninavyofanya …..naona wewe unasema hivyo kwa vile haupo kwenye sehemu
yangu,….na je kama wana makosa hayo makosa yapo wapi, upo wapi ushahidi wa
makosa yao…mbona hutaki kunionyesha huo ukweli na ushahidi ili nisipoteze muda
wa kuwatetea, wewe mwenyewe unanifahamu, kuwa nikugundua ukweli, nipo vipi…unao
ushahidi…?.’akawa kama anauliza.
Wakili mwanadada, akatabasamu huku anatikisa kichwa, akainua
kichwa na kumwangalia mwanasheria akasema;
‘Mimi nakuhakikishia kuwa hawo unaowatetea hasa huyo
uliyetoka kuongea naye kwenye simu sasa hivi wana hatia…na nashangaa sana,
ukisema ni mmoja wa ukoo wenu, …., na bado kadiriki, kumwanga damu ya ndugu
yake….’akasema wakili mwanadada, na mwanasheria akashituka na kauli hiyo na kumwangalia
mwanadada huyo kwa macho ya kushangaa, huku kayakodoa macho, kama vile haamini
hicho alichosikia, akauliza.
‘Eti nini,…una maana gani kusema hivyo?’ akauliza huku akiinuka
pale alipokuwa amekaa na kumsogelea mwanadada huyo, na simu ya wakili mwanadada
ikaita, na huyo mwanadada kama vile anafahamu ni nani aliyempigia hiyo simu, akaichukua
na kuitupia macho mara moja, halafu akasema;
‘Samahani kidogo nataka kuongea na simu, na nitaenda
kuongelea nje…’ akasema na kuniangalia mimi mara moja, halafu akamgeukia huyo
mwanasheria na kusema;
‘Kama unaondoka tutaonana mahakamani, nitakuthibitishia kila
nilichokiongea hapa, na mengineyo kuwa mimi ndio nimesimamia kwenye haki na
ukweli, na ili unione kuwa mimi nipo sahihi, lakini siwezi kukuonyesha
hapa,..unaelewa ni kwanini nasema hivyo….samahani, ngoja nikapokee simu…’akasema
wakili mwanadada, huku simu ikiendelea kuita.
‘Sikuelewe, ina maana umefikia hatua hiyo…kama kweli
unafahamu jambo kama hilo halafu unanificha , jambo nzito kama hilo,…hutaki
kuniambia ukweli, ..siamini, na kama hivyo , sizani kama tutakuja kungea vyema mimi
na wewe….’akasema mwanasheria na wakili mwanadada akamtupia jicho, na akawa
kama anatabsamu, halafu akatoka nje, na kuusindika ule mlango kwa nje, kuhakikisha
kuwa amefungika vyema, naona aliogopa mwenzake asije akafanya kama alivyofanya
yeye.
*****
Tulibakia mimi na shemeji yangu, na kwanza kulitawala
ukimiya halafu akasema;
‘Hebu niambie shemeji, Mwanadada ana maana gani kusema
hivyo?’ akaniuliza baada ya kupita ukimiya fulani, na hatukuweza kusikia sauti
yoyote nje ya mwanadada akiongea na simu, inaonekana alikwenda mbali kidogo, au
alikuwa akiongea kwa sauti ya chini.
‘Kuhusu nini, kuhusu kuwa familia yako unayoitetea ina
makosa au kuhusu nini hasa maana hapa yameongelewa mengi..?’ nikauliza nikitaka
kujua alikuwa kakusidia nini hasa.Na huyu mwanasherai akashika kichwa kuonyesha
kuwaza jambo, na hilo jambo lilionekana kumkera sana, akasema huku akiwa
kainama chini.
‘Hiyo kauli yake, kuwa kuna mtu wa ukoo wetu, …kuwa eti ndiye
aliyehusika kumuua kaka yangu, maana mimi nilifuatlia kabisa kuhusu kifi cha
kaka, ilionekana kaka kafa kwa shinikizo la damu, na hii nijuavyo, na
nilishamkanya kaka mara nyingi, ni kutokana na hasira zake, …na pia inawezekana
ikawa ni shinikizo kwa hali halisi aliyokuwa akikabiliana nayo,….sikuweza
kulipinga hilo, maana kaka alishaanza kulalamika toka awali kuwa ana tatizo la
shinikizo la damu…sasa haya ninayoyasikia kwa Mwanadada ni mapya kwangu…sijui
kama ana ushahidi gani, na kwanini hataki kuniambia ukweli, kwa jambo nzito
kama hilo…..’akasema mwanasheria.
‘Kwani kwa kauli hiyo ya wakili mwanadada, ana maanisha ni
nani hasa aliyefanya hivyo, maana kaongea kwa ujumla ,mimi sikusikia akimtaja
mtu,…. na huwezi ukathibitisha kuwa alikuwa akimuongelea mtu fulani kutokana na
kauli yake…na jinsi alivyokuwa akiongea, labda kwa vile mnajuana, huenda wewe
umegundua kuwa anamuelezea mtu fulani, au wewe unamfahamu huyo aliyekuwa
akimuongelea?’ nikamuuliza.
‘Nina uhakika kuwa wakati naongea na simu , huyo wakili
mwanadada, alikuwa kasimama hapo nyuma ya mlango,, akinisikiliza,…nilijua
hilo,…lakini sikujali sana maana halikuwa na uzito, hata kama angelisikia,
lakini hakuwa na haki ya kufanya hivyo…kwahiyo huyo niliyekuwa nikiongea naye,
ndiye anayemnyoshea kidole kuwa huenda anahusika na kifo cha kaka…kitu ambacho
hakiingii akilini kwangu, hata siku moja siwezi kuliwazia hilo…huyo hawezi
kabisa, labda amtaje mtu mwingine, na hata hivyo, kaka kafa kifo cha kawaida…...’akasema.
‘Lakini dunia hii ina maajabu yake, umzanie kuwa siye,
anaweza kuwa ndiye..na hasa kunapotokea makundi yenye msimamo mkali kama hilo
liligundulikana hapa….wao wanasimamia katika mantiki yao, kuwa wanachofanya ni
sahihi,…na huwezi kuwageuza katika itikadi yao hiyo…na pia kuna mambo ya kula
amini, kuwa ni lazima hili lifanyike ili mambo yasonge mbele..ni makubaliano
yenya msimamo mkali. Kama yeye alionekana ni kikwazo kwenye kundi, au
angaliweza kutoa siri, sioni ajabu wakiamua kumuua…’nikasema.
‘Usije ukatekwa na tabia za huyo mwanadada….mimi nimegundua
kitu, yeye kwasasa anatafuta umaarufu, wengi wanafanya hivyo, kuwa ili uweze
kujulikana kwenye kazi zako, unahitajika kujitangaza, na kujitangaza kupo kwa njia
mbali mbali…usione watu wanaweka mapicha yao kwenye mitandao, magezeti nk, ukafikiria wana maana gani,…’akatulia kidogo,
akiniangalia moja kwa moja usoni, na mimi nikamkwepa kuangaliana naye moja kwa
moja usoni.
‘Kila mmoja ana malengo yake moyoni, …lakini shemeji
kiukweli hayo yote kwa ujumla wake yanafanyia kwa malengo ya kutaka
kujitangaza, au kutangaza hilo mtu alilolikusudia moyoni mwake,…japokuwa makusudio
mengi yapo ndani ya muhusika mwenyewe…sasa huyu mwanadada, nahisi na ndivyo
ilivyo,anatumia njia hii ya kujifanya anatetea watu, kwa minajili ya
kujitangaza, wewe huoni kwa muda mfupi sasa jina lake linatajwa kila kona….?’akasema
kama anauliza.
‘Mimi sikatai hilo la kijitangaza, lakini kujitangaza huko
kuwe na lengo jema,…kama ulivyosema kuweka picha, …watu wengine wanaweka picha
kwa malego mema, kuwa dhamira yao ni ya dhati kufikisha ujumbe fulani, na watu
kama hao wanajiamini, kuwa hata wakijulikana hawama shaka….na halikadhalika,
mwanadada, nia yake sio mbaya, hata kama anatumia hivyo kujitangaza, lakini
anajitangaza kwa kutenda yale yaliyosahihi…na ndio maana hana wasiwasi,
anajiamini….’nikasema.
‘Naona sasa wewe umeshatekwa na huyu dada eeh…unaanza
kujitenga na familia ya mume wako, hata mwaka haujaisha umeshaanza kumsahau mume wako, kwa ajili ya kumwezesha mwanadada
kutimiza malengo yake….shemeji mimi ninachokifanya ni kwa ajili ya familia yetu,
familia aliyotoka mumeo, familia ya mtoto wako, je hapo nina makosa gani?’
akawa kama anauliza.
‘Mbona unabadili muelekeo wa hoja yetu…mimi sijakupinga
kabisa hilo la kuitetea familia
yako,…hapa tulikuwa tukimuongea mwanadada, kuwa wewe unaona anajitangaza, na
kwahiyo na mimi namtetea yeye,..au sio, …lakini sijajitenga na familia yangu
kwa kutizama mambo kwa usahihi wake,…tugeukiwa upende wa mwanadada,mimi
nakuambia ukweli kuwa kwa kipindi kifupi nilichomfahamu yeye, ninakiri kuwa
yeye kweli ni mtetezi wa haki…hilo nakuthibitishia na hilo litamtangaza sana….anastahiki
kupongezwa, na mola atamsaidia ….’nikasema na mara wakili mwanadada akingia.
‘Jamani mimi nahitajika kikazi..tutaonana baadaye…’akasema
huku akichukua mkoba wake na kuyaweka makabrasha yake ndani ya huo mkoba,
akaniangalia mara moja, akatoa tabasamu kidogo, halafu bila ya kumwangalia
mwanasheria akaanza kuelekea mlangoni. Mwanasheria, kuona mwanadada anaondoka
akamkimbilia na kumshika mkono.
‘Hatujamalizana, …huwezi kuniacaah hewani, hebu niambie
kuhusu kauli yako kuwa huyo niliyekwua nikiongea naye kwenye simu, anahusikaje
na kifo cha kaka yangu , wakati kaka yangu kafariki kwa shinikizo la damu?’
akauliza na wakili mwanadada akamwangalia huku akitabasamu kwa dharau. Na
mwaansheria akawa kamuachia huyo mwanadada mkono, na akawa anaangaliana uso kwa
uso na huyo mwanadada, aliyegeuza kichwa tu.
‘Usitie shaka, hayo na mengine mengi utayapata mahakamani,
kwasasa siwezi kukuambia jambo, maana sasa hivi tuwapinzani kuhusiana na hiyo
kesi, siwezi kumwanga sera zangu kwako, ambazo natarajia zitakuwa silaha zangu
kwenye ulingo wa mapambano,…lakini katika kuitetea haki…’akasema wakili
mwanadada, na alipotaka kuondoka mwanasheria akamshika mkono kumzuia.
Wakili mwanadada, taratibu akashusha uso kuangalia ule mkono
wa mwanasheria uliokuwa umemshika, na mwanasheria alipoona huyo mwanadada
anauangalia mkono wake, ambao umeshika mkono wa mwanasheria, kama vile kafanya
makosa kumshika, akauondoa mkono wake kwa haraka, na kufanya kama anaukung’uta
mkono wake na akasema;
‘Samahani muheshimiwa wakili mwanadada…’ na wakili mwanadada
akainua uso taratibu na kumwangalia usoni mwanasheria huyo, sasa hivi uso
uliomwangalia mwanasheria huyu, sio ule
wa legelege, ulikuwa uso wa kazi, uso uliojaa ujasiri, ..na macho
yasiyotetereka yakamwangalia moja kwa moja mwanasheria huyu, na mwanasheria
naye akajitahidi kufanya hivyo hivyo, kwahiyo wakawa kama wapiganaji wawili
waliokuwa wakitunishiana misuli. Mimi pale nikatabasamu …..
Wakili mwanadada akawa wa kwanza kuongea, na kwa sauti ya
kijasiri akasema;
‘Tutaonana mahakamani…’
Lakini mwanasheria hakusema kitu, akabakia ameduwaa, bado
akimwangalia wakili mwanadada ambaye alikuwa akitoka nje, na kuondoka, hata
bila ya kuniaga.
NB, Haya naona sasa tutaingia kwenye kesi yenyewe baada ya
utangulizi huo
WAZO LA LEO: Ushindani katika mambo mema unaruhusiwa, na
wakati mnashindana, mnakuwa mahasimu , huku mkijua lengo lenu ni kutafuta
muafaka, au maendeleo, kw kila mmoja kuonyesha ubora wa hoja zake…
Na baada ya kupatikana mshindi, inabidi nyote mrudi na kuwa
kitu kimoja kwa kushikana mikono na kupongezana, huku mkiwekeza kwa lile mlolokuwa
mkilipigania,..huu ndio ushandani wa haki, na
tunaweza kuuita vyovyote tupendavyo, lakini lengo ni kwa ajili ya mema,
kwa manufaa ya jamii.
Ni mimi:
emu-three
3 comments :
Dah malipo ni hapahapa duniani na mungu ni wa wote milele, kila la heri mdada mwanasheria
Dah malipo ni hapahapa duniani na mungu ni wa wote milele, kila la heri mdada mwanasheria
Hongera sana ndugu wa mimi.. kazi nzuri sana sana...
Post a Comment