Baada ya kumaliza maelezo yangu, ya awali nikaingia kwenye
hoja yangu, ambayo nilianzia pale tulipofika Dar, na mume wangu alipogundua
kuwa kaibiwa pesa zote alizokuwa nazo, na jinsi gani tulivyohangaika na maisha
magumu, maana hatukuwa na pesa, tukaanza kuomba vibarua huku na kule na
tulipopata pesa kidogo, tukaanza kufanya biashara ndogo ndogo za kuuza karanga,
na ubuyu…
‘Kama hizo pesa mnazodai zingelikuwepo, kwanini tungeishi
maisha hayo ya taabu, ….sio maisha rahisi kama mnavyohisi, ….’nikawaambia
Nikaendelea kuwaelezea jinsi tulivyofikia hatua ya kufunga
ndoa, na tukio zima la kukamatwa kwa mume wangu, ambalo lilitokea pindi tu
tulipotoka kufunga ndoa, nikawaelezea jinsi gani alivyoniacha katika hali
ngumu…..
‘Hata hivyo sikukata tamaa,nikaanza kuhangaika nikiwa peke
yangu, kwa kuendeleza zile biashara nilizokuwa nikizifanya alipokuwepo mume
wangu. Nilihangaika, na kukutana na mitihani mingi, ikiwemo ya kupambana na
wanaume walitoka kunibaka…..yalikuwa maisha ya shida …taabu na hatari’nikaendelea
kuwahadithia, na watu walikuwa kimiya, na wengi waliona kama kisa cha
kufikirika.
‘Kuna muda nilifanikiwa nikaweza kupata pesa za kuniwezesha
kupata nauli ya kurejea nyumbani, na siku hiyo nikajiandaa kabisa kuwa kesho
yake naondoka, wezi wakaniingilia na kuzichukua pesa zote, nikabakia mikono
mitupu,….hebu fikirieni hiyo, pesa yenyewe ya kuingiliwa na majambazi ilikuwa
pesa gani, na kama hiyo pesa ingelikuwepo, kweli majambazi wangeiacha,….walitafuta
na kukuta hizo pesa kidogo wakaondoka zao….hapo ina maana nilitakiwa kuanza
maisha upya, na je ningelianzaje wakati pesa zote wameshazichukua…
‘Haya ninayowahadithia ndio maisha niliyokutana nayo Dar,
sio rahisi kama watu mnavyokisia kuwa ukifika pale utaweza kupata kazi kirahisi
na kujiwezesha,..sio rahisi kihivyo, maana hata kazi za ufanyakazi wa ndani wa kulea watoto na kuosha vyombo….haipatikani
kirahisi, japokuwa mnasikia kila sikuwa watu wanakuja huku kuulizia wafanyakazi
wa ndani, inakuwa vigumu ukiwepo pale, kwani watakuaminije kuwa wewe sio hawo
matapeli wa mjini..’nikainua uso kuwaangalia, na wote walikuwa wamenikodolea
macho wakisikiliza maelezo yangu.
‘Kwahiyo mimi pale nikaanzia na biashara ndogo ya zile
karanga zilizobakia, …bahati nzuri walipokosa pesa , hawakuhangaika kuchukua
karanga kidogo nilizokuwa nazo na ubuyu, na ndizo hizo nilianza nazo,japokuwa
zilikuwa kidogo sana, nahazingeliweza kunisaidia kitu, ukumbuke nilikuwa naishi
kwenye nyumba ya kupanga, chumba …na siku za kulipia kodi zilikaribia, na
mwenye nyumba akija, kama huna kodi unaondoka, ….anaingiza mtu mwingine siku
hiyo hiyo…
‘Ili niishi hapo, ilibidi kwanza nihangaike ipate hiyo kodi,
kwahiyo nikaanza kuhangaika mitaani, kuuza hizo karanga, na kujichanganya kwa
mama Ntilie, ambao waliweza kunipa kazi ya usafi, na hata kubeba mizigo ambayo
niliweza kuibeba, ya wale wanaonunua vitu sokoni, na wanahitajia kubebewa hadi
kwenye magari yao au hata nyumbani kwao….’nikatulia kidogo.
‘Kwakweli ilikuwa kazi nzito, na nilikuwa nachoka kupita
maelezio, ilifikia muda sasa, nikaona sitaweza …nikaanza kuingiwa na tamaa,
kuwa labda na mimi nijiingize kwenye biashara haramu za ukahaba, lakini moyo
wangu ulikataa kata kata…
‘Nikajiuliza nitawezaje kuishi, nitapata wapi kodi ya
nyumba, na siku zinakaribia za kulipa hiyo kodi, nikasema nitajitahidi hivyo
hivyo, na sitakata tamaa, nikadunduliza, hadi siku ya kulipa kodi ilipofikia
nikawa na kiasi hicho taslimu…..
Siku hiyo niliyoweza kulipia kodi ya mwezi mmoja, na
kubakiwa bila hata senti moja ya akiba zaidi ya karanga na ubuyu ambazo
nilizinuunua kwa ajili ya kuuza kesho yake, nilikuwa sina hata pesa ya
kununulia maji ya kunywa na sikujua nitakula nini…san asana nilitafuta punje
chache za karanga, ilimradi siku iweze kwenda….na hutaamini, kuna muda na mimi
nilichakura majalalani , ili angalau nipata masalia….na hili nililifanya wakati
natafuta chupa za plastiki, kwa ajili ya kuuza. Nilichopata, nilikwenda
kukipasha moto, …siku ikaenda…’nikasema na nilipogeuka kumwangalia mama yangu
nikamuona machozi yanatiririka usoni.
‘Siku hiyo baada ya kulipa kodi na kubakiwa bila senti moja,
nilijilaumu kwanini ile pesa nisingeliitumia kama nauli….lakini
moyoni,nilijiuliza , kama ningeliitumia kama nauli na kurejea huku, bado
ningelikuwa sina kitu, na sikutaka kuja kuwasumbua wazazi wangu ,…na mtoto
wangu nitamlea vipi, nikaona kilicho bora nikuhangaika, nipate chochote,
angalau pesa ya maziwa …..’hapo nikatulia.
‘Nikajipa moyo kuwa mimi kama mzazi, sina jinsi, lazima
nihangaike,….ili nipate pesa ya kumlea mwanangu, na ikibidi niweze kufuatilia
kesi ya mume wangu, kwani nilijua nina dhima kwake. Kwakeli siku ile sitaweza
kuisahau maishani….’nikakohoa kulainisha koo.
‘Siku ambayo nilianza kuhisi hali ilivyo kuwa ngumu mbele
yangu, na kweli hapo nilianza kuona umuhimu wa kuwa na mwenzangu, yeye alikuwa
ni mwanaume na ilikuwa rahisi kwake kujichanganya kwenye kazi ngumu, na
kupambana na wanaume wenzake, na akitoka hapo sio haba, tuliweza kupata visenti
kidogo tukaongezea mtaji wetu. Lakini hakuwepo tena, ..na sikuwa an ndugu
anayenifahamu, majirani zangu, ambao ni wapangaji wenzangu, walikuwa na
shughuli zao…na maisha yao hayakuwa tofauti nay a kwangu….hapo nilimkumbuka sana
mume wangu na kuanza hata kulia ….
‘Lakini nikajiuliza hata nikikesha kwa kulia, itasaidia
nini, cha muhimu ni kujituma, ili nipate nauli,kwahiyo hapo lengo likawa
kutafuta nauli, ikifikia tu, naondoka, ….’nikajipa moyo
`Usiku ule ulikuwa mgumu sana kwangu sikuweza kulala, nikaona
muda huo baada ya kumaliza kuzifunga zile karanga na ubuyu, niutumie pia
kumuomba mungu…siku zote nilikuwa namuomba mungu, lakini siku ile ilikuwa
tofauti,….niliomba nikijua kuwa sasa hali yangu imefikia kubaya….’hapo
nikajikuta machozi yakinilenga lenga, nikiikumbuka hiyo siku.
‘ Kweli sikujua muda gani usingizi ulinishika, maana
nilikuwa nikimuomba mungu kwa hali niliyoifahamu, na nilikumbuka wazazi wangu
walivyonifundisha, wazazi wangu wa kunizaa, na wazazi wangu wa kufikia ambao
siku zote walikuwa wakiniambia kuwa, kumbuka kumuomba mungu wako, kwanza kwa
kutubu madhambi yako, maana kila siku sisi ni watendani wa mdhambi, mengine
hayakwepeki,….na waliniambia kuwa kila ikifika usiku omba msamaha kwa yale
mabaya uliyoyafanya, halfu baadaye unaomba kwa kuyakumbuka mema yote
uliyoyafanya…hayo mema, ndio yatakupa baraka….
‘Nakumbuka sana wazazi wangu walivyoniambia kuwa yale mema
uliyoyafanya yatakuwa ndio kiyoo chako cha kukumulikia njia ya mfanikio,..ndio
maana inatakiwa katika maisha yako kujitahidi kutenda mema, na ujibidishe
kuytafuta matendo mema, hata ikibidi kujitolea, ….ndio maana inapotokea jambo
la kufanya usitegee, uwe wa kwanza kujituma, kujitolea, ili uweza kuyapata hayo
mema..
‘Kujituma kwa kutenda mema hakuji hivihivi, hii tabia
huanzia toka utotoni, na hili nisingelifanya na kufanikiwa kama nisingelipata
msingi mwema kutoka kwa wazazi wangu wa kunizaa na huyo wa kufikia ambaye nashangaa
kusikia kuwa mnamuona kama mtu mwema mbaya, …..mimi kama ndugu yenu
nawahakikishia kuwa huyo mzee ni mtu mwema sana na muadilifu wa kweli,…na kama
mngelimsikiliza msingalifika hapo na kusigishana na yeye, nasikia kuwa
mumefikia hadi kupigana na yeye, na sijui hali yake kwa hivi sasa ipoje….masikini baba wa watu…’nikasema na
kushika shavu.
‘Ndugu zanguni, ninachotaka kuwambia ni kuwa, isingelikuwa
hawa wazazi kujitolea kunilea katika maadili mema, kunifundisha kujituma,
nisingeliweza kuishi maisha maisha niliyokutana nayo Dar, huenda ningejiingiza
kwenye biashara ya ukahaba, maana nilifikia hatua siku inapita bila kuonja kitu
zaidi ya kutafuta tembe chache za karanga, huku natembea umbali mrefu kutafuta
wateja wa karanga,…wengine wananunua, wengine wananiibia wengine
wananisimanga,…lakini yote hayo hayakunikatisha tamaa….’nilirejea kuwaelezea
maelezo hayo kwa msisitizo.
`Siku nyingine nilikuwa nikununua ndizi Kariakoo za kuiva,
kwa wale wanaouza nje, na mimi natembea mitaani nikiwa nimeongeza faida yangu, …sikuchagua
biashara tena, iwe ndizi au embe …ilimradi napaat faida kidogo…
‘Mola hamtupi mja
wake, maombi yangu yalikubaliwa, na sikuamini siku nilipopigiwa simu kuwa
nimeshinda katika moja ya promosheni za matangazo ya kampuni za simu, …na
waliponitajia hicho kiwango nilichoshinda niliona kama wananitania, lakini
kweli nilishinda na kukabidhiwa kitita cha pesa,…na ndicho hicho
kilichoniwezesha kuja huku na kujenga nyumba na hilo duka …..’hapo nikasikia
watu wakiguna.
‘Kwahiyo nduguzanguni samahanini sana kwa maelezo hayo
marefu, lakini nia na lengo langu ni-ili muwe na ufahamu kwa kina, …..najua
wengine hawaamini haya, hata mimi sikuwa naamini kuwa mtu anaweza kushinda na
kulipwa pesa zote hizo. Ni bahati, na bahati ilikuwa yangu siku ile, na yote
haya yalitokea kwa kudra za mungu…’nikatulia na nilimuona mwenyekiti
akitabasamu, tabasamu la dharau, na nikamuona akiinuka na kumsogelea yule mdogo
wake mwanasheria na kumnobg’oneza kitu
Mimi nikawa nimetulia sikuwa na la kuongea zaidi,
nikasubiri, mwenyekiti atasema nini, na baada ya wao kuteta kwa muda, nikamuona
mwenyekiti akisimama, na kuelekea pale alipokuwa kakaa mzee, yaani baba yao
mdogo, yule aliyeonga mwanzoni, na wakateta kwa muda, halafu akareeja pale
alipokuwa amekaa , akakohoa;
‘Samahanini kidogo kwa kuwapotezea muda, nilikuwa nateta
kidogo…shemeji sijui kama umemaliza maelezo yao, au bado….naona umenyamza,
endelea, tunakusikiliza ..mimi nilikuwa nateta na wazangu, maana kuna mambo
mengine unaogoa kuyaongea mpaka usikie wenzako wanasema nini, hekima ina
masharti yake, usijione wewe ni kiongozi, ukazani kila utakaloongea lina hekima….na
kwa vile nina wenzangu, nilihitajia hekima zao kidogo…’ Akasema na kuniangaliai
na mimi nilikuwa nimetulia kimiya.
‘Natumai umemaliza
….’akasema mwenyekiti, na mimi nikasema kwa sauti ya kinyonge ;
‘Nimemaliza ndugu zangu, nawasikiliza nyie mtasemaje
kuhusiana na hilo kosa lililofanyika, siwezi kuwalaumu, maana sio jambo rahisi
kukubalika mpaka ujione umeshinda,…..ni kweli nilishinda na nikazipata hizo
pesa , na ndizo zilizojenga hiyo nyumba na duka…..natumai mumenielewa, ….na
kama kosa lilifanyika, basi tulirekebishe, …..’nikasema na kutulia.
‘Sawa shemeji tumekusikia na ombi lako limefika mbele ya
kikao, na mimi kama mwenyekiti siwezi nikasema lolote kwasasa, mimi ni kama
kiongozi wa kusimamia hiki kikao, na ni vyema kila mmoja akachangia kuhusiana
na hoja hii, na kabla sijamkaribisha mzee wetu atoe ufafanuzi kidogo,
ningeliomba, mwanasheria wetu akuhoji kidogo, kutokana na maelezi yako hayo…’akasema
mwenyekiti na yule shemeji, mwanasheria, akasimama …
‘Mimi ni kijana naomba nisimame, na kutokana na nilivyozoea
huko mahakamani, huwa tukiongea tunakuwa tumesimama, …’akasema na baadaye
akanigeukia na kuniangalia usoni, akatabasamu na kugeuka kumwangalia
mwenyekiti….
‘Ndugu mwenyekiti, ….kwanza nilitaka kujua,hili ni ombi toka
kwa ndugu yetu, mwanafamilia, au ni lalamiko?’ akauliza huku akishika kichwa.
‘Naomba umuulize muhusika mwenyewe..’akasema mwenyekiti.
‘Ninalalamika..kuwa nimetendewa isivyo haki…sio ombi, huwezi
kuomba haki yako’nikasema kwa sauti.
‘Haya kama ni hivyo,naomba nikuulize swali moja, ili kuweza
kuweka maelezo yako sawa, je ulipopewa hizo pesa, ulitangazwa kwenye vyombo vya
habari, maana mimi nijuavyo, hawa watu wakitoa mashandano kama hayo wanayoyaita
promosheni, wanatangaza kwenye vyombo vya habari, …’akasema na kutoa ufafanuzi.
‘Ni kweli waliniambia ndivyo kuwa watanikabidhi hizo pesa
kwenye shughuli waliyoiandaa, lakini mimi niliwaomba, kutokana na dharura
niliyo nayo, kuwa nahitajika kuja kusimamia kesi ya mume wangu, na nikawaambia
kuwa kuna wagonjwa, kuna mtoto wangu, ananihtaji,…na hali ngumu niliyo nayo,….ningeliomba
nisiwepo kwenye hiyo shughuli…. pia nikawaambai kuwa wakinitangaza kwa hali
ninavyoijua hizo pesa zitaishia mikononi mwa watu…’nikasema na mwenyekiti
akacheka, na kunyosha mikono yakuonyesha kuwa hakuna kitu.
‘Samhani sana shemeji, ….nikisema hivyo, kuwa nina mashaka
na maelezo yako hayo sizani kisheria kama yanaweza kukubaliwa, maana ilivyo,wao
wana msharti yao, na huwa wanatoa hizo promosheni kwa nia ya
kujitangaza,…kwenye mashandano yao kuna maneno wanasema, `na msharti
kuzingatiwa…’ yana maana yake kisheria,..sasa shemeji yetu, iweje wewe wa
kufanyie tofauti na wengine, ..?’ akaniuliza.
‘Ni kweli walinikatalia kata kata kuwa hawataweza kunipa
hizo pesa hadi kwenye hiyo shughuli waliyoiandaa….mimi nikawaambia kama ni
hivyo, basi sihitaji pesa zao maana najua sitaweza kuzitumia kama
wakinitangaza….’nikasema, watu wakaguna kuonyesha kuwa nilichoongea ni uwongo
wa kujitungia.
‘Kwani kitu gani ulichokuwa ukikiogopa kuwa ukitangazwa
kitatokea, utaibiwa au….?’ Akauliza huyo mwanasheria.
‘Mume wangu alikuwa jela kwasababu ya kushitakiwa kwa kuiba
pesa, wewe huoni mimi kama mke wake, wangelinihisi kuwa hizo pesa ni hizo alizokuwa
kaiba mume wangu, wangelikuja kudai hizo pesa na sikuwa na muda wa kuanza
kupambana na hawo watu, lengo na nia yangu ni kumpigania mume wangu atoke,…,na
hata hivyo, mtu akiumwa na nyoka, akiguswa na unyasi ni lazima atashituka, mimi
nilishaibiwa,, kwahiyo nilikuwa na uwoga wa kuibiwa….’nikasema.
‘Hiyo shemeji sio sababu ya msingi ya kuweza kuwaabdili hawo
watu wakufanyie tofauti, kwasbabu hayo mashindano ya lengo maalumu, hawatoi
kama sadaka…..sizani…hebu tuambie ilikuwaje mpaja wao wakufanyie tofauti,
haiingii akilini, ailikuwaje shemeji?’ akauliza.
‘Niliwaomba mtu mwingine asimame badili yangu na mimi
nitamlipa…’nikasema na watu wakacheka, na huyo shemeji mwanasheria akasema;
‘Hiyo sasa mpya, ….shemeji mimi nafahamu sana hizo
promosheni na lengo lao kubwa ni kujitangaza, na pesa hizo ni yingi,
wasingeliweza kukubali kufanya kama ulivyotaka wewe….ina maana basi ulihinga,
kwa lugha rahisi, kitu ambacho hakiwezekani..’akasema.
‘Kama hamuamini basi…..kama mnataka basi ,naomba twende huko
Dar, nina imani watathibitsha hilo….’nikasema.
‘Shemeji, sio kwamba nakupinga kwa nia ya kukupinga, hilo
nililisikia, na nikalifanyia uchunguzi, ..kiukweli sikuweza kuliona jina lako
kwenye hiyo promosheni, kweli kulikuwa na mshindi wa namna hiyo, lakini jina
lako halipo pale, na bahati mbaya, mitambo yao ya kipindi hicho iliharibiwa na
virusi,….lakini hata hivyo, bado walikuwa na namna nyingine za kupata hiyo
taarifa, kuna picha za tukio hilo, mawasiliano
ya simu….,wewe haupo ‘akasema na mimi nikamkatisha.
‘Nimekuambia, niliwaomba kwa hiyo dharura, sasa picha yangu
ingelionekana vipi….kama hamuniamini kuwa kweli nishinda mimi sijali,…lakini
kwanza kwanini hamjiulizi kuwa wale waliokuja kudai mwanzoni kuwa hizo pesa
nilizojengea ni za wizi, mbona walishindwa kunipeleka mahakamani, wao wenyewe walikuja
kufutilia na baadaye wakaona ni kweli na kuachana na hayo madai yao…?’
nikawauliza.
‘Shameji, ….hayo yote nilifuatilia,….niliwauliza….wakasema
waliona hakuna haja tena ya kuhangaika, …kwani walipofika huko kwenye ofisi za
simu uliposema ulishinda, walijikuta wakipewa tarehe, njoo kesho njoo kesho, na
ukumbuke kuwa kampuni hiyo ilishabadilika mara nyingi, leo inaitwa jina hili
kesho lile,...kwahiyo waliokuwepo awali hawapo tena….hata hivyo. Kumbukumbu
muhimu hazipotei….hakuna jina lako…kabisaa’akasema huyo wakili.
‘Mimi nimeshawaambia kama hamuniamni, sijali, mimi
sitakubali kwa hilo, kwani nyumba na duka vyote hivyo nimejenga kwa pesa zangu,
…nitavipigania hadi hatua ya mwisho,…’nikasema kwa hasira. Na mwenyekiti
aliposikia hivyo akaingilia kati.
‘Shemeji, nilitaka usikie sheria inasemaje juu ya hilo,
maana hata mimi niliposikia hivyo niliingiwa na mashaka,….hatukuwahi kusikia
jina lako likitajwa kuwa wewe umeshinda pesa kama hizo, ina maana wote siku
hiyo hatujaliwa kusikiliza redio na kuangalia runinga….hilo ndilo lililotufanya
tusiamini kuwa pesa hizo ulizipata kwa bahati nasibu, ni jingine ni kauli ya
mume wako na maandishi yake mwenyewe, …kama unayahitaji tutakuonyesha,
….’akasema mwenyekiti.
‘Hiyo sio kweli, maandishi mumeyatunga wenyewe….hakuna kitu
kama hicho..,nawafahamu sana huenda mlimuhadaa, ili mwisho wa siku ionekane
hivyo…na hapa mtakuwa mkimsingizia marehemu kwa vile hayupo…’nikasema kwa
hasira.
‘Mimi niliongea na ,mume wako akiwa bado mzima, na alisema
hizo pesa huenda wewe ndiye uliyemuibia wakati mnafika Dar, ukazificha,….maana
muda wote mlikuwa wote wawili, haiwezekani ule mkoba umtoke mikononi, na wakati
yeye alikuwa kaushikilia mikononi….’
Aliniambia mpaka leo hajui jinsi gani huo mkoba ulivyomtoka
hadi hizo pesa zikachukuliwa, mtu ambaye angeliweza kufanya hivyo ni wewe….maana
mlikuwa pamoja, na alikuamini….kwahiyo wewe ulipopata huo mwanya, ukaziiba, na
alipokamatwa, na ukaona umepata nafasi ya kudanganya,….’akasema mwenyekiti kwa
kujiamini, na nilipotaka kujitetea akaonyesha mkono wa kunituliza, kuwa
hajamaliza, akasema;
‘Ndio maana ukasingizia kuwa ulishinda kwenye hiyo bahati
nasibu…na ndugu yetu, alisema kuwa kwa vile wewe ndio umezichukua na kuzifanyia
jambo la maana, bsi haina shida, ila akasema ni lazima ahakikishe kuwa nyumba
na hilo duka zinakuwa katika jina lake, ndio maana akapigania hadi ukakubali
kuandikisha jina lake ….’akasema mwenyekiti, na kunifanya nibakie siamini
maneno haya, kwani niliwahi kukorofishana na mume wangu akayazungumza hayo,
lakini baadaye nilimuelewesha mume wangu hadi akakubali…
‘Nahisi mliongea naye kipindi kile alichokuwa akilewa sana,….tukawa
hatuelewani, na kipindi hicho tulikuwa hatuelewani kwsaabau ya ulevu wake, na
nahisi ndipo mlipomshawishio hadi akanishawishi nikakubali kuandikisha jina
lake….mimi nilikubali kwasababu ni mume wangu, na huenda ndipo mlipomrubuni
hadi akakubali kuwaandikia hayo maandishi mnayodai kuwa aliyaandika yeye na
kuweka sahihi yake…..’nikasema.
‘Kama ulijenga kwa pesa yako tunavyokujuwa wewe,
usingelikubali kuandikisha jina la mume wako kwenye hati ya nyumba an duka, …..kwanini
usingesema kuwa muandikishe kuwa mumejenga kwa kushirikiana, ina maana kwako
hakuwa na uzito, kwani pesa zilikuwa ni za kwake…?’ akasema mwenyekiti.
‘Nyie mnadai kuwa pesa hizo zilizojenga hiyo nyumba ni za
wizi , kama kweli alindika hizo nyaraka za kuhalalisha kuwa nyumba hiyo ni yake
kutokana na hizo pesa mnazodai kuwa ni hizo za wizi, na kama ni kweli mbona hamkuwaambia
wenyewe, walioibiwa ili waje wataifishe hiyo nyumba na duka..?’ nikawauliza na
watu wakacheka.
‘Hilo lipo kwenye ajenda yetu ya mwisho, ajenda ya
kukushukuru kwa kuweza kumfichia mume wako, …na juhudu za ziada ulizozifanya
hadi ukaweza kujenga hiyo nyumba, …..ni dhuluma ndio lakini kwa namna nyingine
imewezesha kuwepo na nyumba nzuri kwenye familia yetu , hilo tulitaka baadaye
tukupongeze, na kama ikibidi tungelitafuta njia ya kuliweka sana, na …hatua
iliyofanyika ya kuiandikisha kwa jina la mtu mwingine ni moja ya kuhakikisha kuwa
mali hizo hazichukuliwi tena….’akasema mwenyekiti.
‘Haya mengine hatukutaka kuyasema ni siri zetu za
ndani….maana kama tumefanikiwa kwa kiasi hicho, tukapata nyumba na duka,
hatuwezi kuanza kuchunguza kuku kala nini,….eti,…’ akawa kama anauliza na
baadaye akasema
‘Sisi tunachoangalia ni nyama…au sio…! Nyama ni hiyo nyumba
na duka, na iliyobakia kwetu ni kusaidia juhudi za mwenzetu, aliyefanikiwa hadi
ikapatikana hiyo nyumba, tusikubali ichukuliwe tena, itakuwa ni aibu kwetu…’
akawa anapunguza sauti, kwani huwa akiongea sauti yake ni nzito na kusikika.
‘Kwahiyo sisi tuliliongelea hili , tukaona ili lisilete
utata, tulinyamazie hivi hivi, …wasije wakasikia wenyewe na kuanza kuleta
balaa, ingawaje mwanasheria wa familia keshaliweka sawa,…katu hataweza kudai
kuwa pesa iliyojenga hiyo nyumba na duka imetokana na pesa ya wizi, ushahidi
upo wapi….hatutakubali hilo abadani,….’akawa anaongea kwa sauti ya chinichini
ili eti asisikiwe.
‘Hizi zilizojenga hiyo nyumba, hazikutokana na pesa mnayodai
ni ya wizi,….nyumba hiyo nimejenga kwa pesa yangu,nieleweni ndugu zanguni ….’ Nikasema
kwa sauti, hadi mwenyekiti akaniangalia kwa mshangao. Sikumjali, nikasema;
‘Mbona hamunielewi ndugu zanguni,….kama ni hivyo, kwakweli
mimi sitakubali,….hiyo nyumba ni yangu, na kama mlipanga kufanya hivyo, mkifikiria
kuwa nyumba hiyo imejengwa kwa pesa za urithi, mlikosea, na nawaambi, msiwe na
haja ya kuogopa, kuwa hawo watu watakuja kudai eti hizo pesa zilikuwa zao
zilizoibiwa, hizo pesa ni za kwangu, zilitokana na huo ushindi wa promosheni ….’nikasema
kwa sauti kubwa.
‘Hebu punguza sauti shemeji, hatupo kwenye ugomvi hapa…tumekusikia
hayo maelezo yako, kiukweli, siyo ya kweli, umejitungia, ili kuhalalisha hilo…tunashukuru
sana kuwa ulionyesha juhudi za kuweza kujenga hiyo nyumba, ….kweli tunashukuru
sana, ….’akasema mwenyekiti.
‘Naona sasa mnanitafuta ubaya,…mimi sikubaliani kabisa,…na
kama mumeshikilia maamuzi yenu hayo mimi nitachukua hatua nyingine,… nitafika
mahakamani kudai haki yangu…’nikasema na hapo yule mwanasheria akanyosha mkono,
na mwenyekiti akamruhusu.
‘Shemeji hapo kazungumza la maana sana, …kama mtu anaona
katendewa kinyume na sheria, na anahitaji haki yake, sehemu muhimu ni
mahakamani..mimi nashauri, ili aweze kuitetea haki yake vyema, tumpe nafasi
hiyo ya kwenda mahakami, na kama atathibistiha hivyo, basi tutabadilisha kila
kitu, na kuweka jina lake….’akasema huyo mwanasheria.
‘Na kama utafanya hivyo,basi atakuwa umeisaliti
familia….maana kama familia haya tulitakiwa tuyaongea humu ndani na kuyamaliza,
lakini yakitoka nje, na kwenda mhakamani,…hapo wewe sio mwenzetu….hebu
tujiulize hapo unamshitaki nani,?’ akauliza mwenyekiti akionyesha kukasirika.
‘Mimi nimetoa malalamiko yangu kwenu, mumeyapinga, na nyote
mpo kitu kimoja, sasa unafikiria haki yangu nitaipata wapi….mnataka nitulie
wakati najua kabisa kuwa hiyo ni haki yangu,…hapana, mimi nitaipigania haki
yangu hadi hatua ya mwisho, …na nawaambia ukweli,…nyumba na duka ni mali yangu,
sikubaliani na chochote, hata kama udugu utavunjika kwa hilo, kwa vile najua ninachokitetea
ni haki yangu…’nikasema na hapo kikao kikaanza kuvurugika.
‘Sikiliza wewe mwanamke….nimekuvumilia sana…na nimekuambia
haina haja ya kupandisha sauti juu, na sikiliza kwa makini, sisi tunajua nini
tulikifanya, na tulitarajia kuwa ungelikuwa na ushahidi mpya, ambao
ungetusaidia, lakini kumbe ni hayo maelezo yako…sasa sikiliza kwa makini, nyumba
ile sio mali yako, na duka ..huo ndio uamuzi wa kikao hiki,….kama una jingine,
sema, kama una ushaidi mwingine tunauhitajia,..vinginevyo, tunakuomba uheshimu
kikao na viongozi wako, maana wao walifanya haya kwa nia
njema,…’akasema
mwenyekiti, na watu wakamshangilia.
‘Mwenyekiti, mimi sitakubaliana na hilo..’nikasema na
mwenyekiti akaniamurisha ninyamaze.
Wazazi wangu waliomba waongee kidogo, lakini hawakuruhusiwa,
na walipoona kikao kinakwenda hali ya kutokuelewana, wakanishauri tuondoke, na
wazee wakutane walijadili hilo swala kwa undani, lakini wao kama familia
walishikilia msimamo wao kuwa kamwe hawatakubali kuachia mali ya mtoto wao kuandikishwa
kwa mtu mwingine,
‘Kama ni hivyo mimi nitachukua hatua nyingine, nitakwenda
mahakamani…’nikasema.
‘Ukifanya hivyo, ….ujue kuwa umejitenga na familia hii, na
sio kwamba tunaogopa kwa hatua hiyo, lakini kwa hatua kama hiyo ya kuishitaki
familia, inaonyesha kuwa haupo ndani ya familia….’akasema mwenyekiti .
‘Sawa, mimi nifanya hivyo kwa nia njema, ili haki yangu
ipatikane…na kama itafanya niachane na familia kwa ajili ya hilo, samahanini
sana, mtanisamehe kwa hilo,…’nikasema na kuinuka kuondoka, na wazazi wangu wakainuka
na kunifuata nyuma na yule mwanasheria, akasema;,
‘Basi hakuna shida, tutakutana mahakamani…’.
NB: Haya je mnasemaje kuhusu maamuzi ya huyu mwanamama?
WAZO LA LEO:
Wakati mwingine haki inaweza ikawa ngumu kupatikana kwa majadiliano ya
kifamilia, na wakati mwingine wanafamilia wanaweza wakawa hawamtendei haki
mwanafamilia mwenzao, kwasababu ya mila na desturi, na mila nyingi na desturi
zinawatenga akina mama, kuwa wao kama wanawake hawana haki ya kutetea haki zao,
na utakuta haki hzi ni za msingi na za kweli. Zipo haki zao zinajulikana kisheria na kidini,
lakini wanashindwa kuzitetea,au kupewa nafasi ya kuzitetea . Kitu cha kufahamu
ni kuwa haki ni kwa kila mtu awe mwanamke au mwanaume kila mmoja anastahili
apewe haki yake.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment