Baada ya kuona kuwa kweli wanafamilia wale wamezamiria
kuchukua haki yangu, nikaona njia bora ni kwenda mahakamani, lakini kabla ya
hayo yote, ilibidi nikae na wazazi wangu tuone jinsi gani tutasaidiana kwa
hilo. Wazazi wangu walipinga sana wazo hilo, wakidai kuwa tutajenga uadui
mkubwa na hiyo familia, ….
‘Mwanangu acha kama ilivyo, mungu atakusaidia utapata
nyingine na utajenga nyumba nyingine waacahe wachukue,…’akasema mama.
‘Hapana, hilo sio wazo jema, …tukiwaachia hawa watu
watatuona sisi ni wajinga, ushauri mzuri, tukafungue kesi,….’akasema baba.
Kikao hicho kiliisha bila maafikiano, na mimi kesho yake,
nikaenda kumuona baba wa kufikia ambaye alikuwa bado mgonjwa, nilimkuta akiwa
na nafuu kidogo, kwani walimvunja mkono, na kumchoma kisu sehemu ya ubavuni,
bahati nzuri kisu hicho hakikuingia ndani sana,.
‘Baba mimi pamoja na kuja kukuona, pia ningelipenda
kukuarifu kuwa nimeamua kwenda mahakamani kutetea haki yangu…’nikamwambia.
‘Mimi nipo pamoja na wewe, na namuomba mungu siku hiyo ya
kesi niweze kufika mahakani ili nitaoe ushahidi wangu…’akaniambia, na mimi
nikashukuru kuwa angalau nina watu wapo nyuma yangu.
Na kweli nikaenda mahakama ya mwanzo kufungua kesi, na kesi
ikapangwa tarehe ya kusikilizwa, na washitakiwa wakapelekewa barua ya kuitwa
mahakamani. Na kipindi hicho huyu wanayemuita mwanasheria wa familia, hakuwepo,
ikabidi wamtumie ujumbe wa haraka ili afike.
Na siku kabla ya kesi, akaja kunitembelea mchumba wa huyo
wanayemuita mwanasheria wa familia, nilishangaa, kwani toka siku niliposema
nitakwenda mahakamani kudai haki yangu, nilikuwa kama nimetengwa na hiyo familia
ya mume wangu, na wanafamilia wote waliambiwa kuwa atakayeonekana yupo upande
wangu basi yeye sio mwanandugu. Kwahiyo ndugu wote wa upande wa mume wangu
walikuwa maadui zangu
‘Karibu ndani….’nikamkaribisha huyo mwanadada, nikiwa na
mashaka na ujio huo, yeye hakuonekana kuwa na wasiwasi wowote, aliingia ndani
ya kukaa kwenye kiti. Na baada ya kusalimiana tukaanza kuongea.
‘Ahsante kwa kunikaribisha, nimekuja mara moja tu, kama
unavyojua, kuwa hakuna anayeruhusiwa kuja huku kwako,kwasababu wewe umeshaamua
kujitenga na hiyo familia…..sikutakiwa kuja huku, na ujio huu hakuna anyefahamu
kuwa nimekuja kwako….ndio mimi ni mwanafamilia hiyo japokuwa hatujafunga ndoa
na huyo mchumba wangu, lakini wanachokifanya sio kizuri, kwani kila mmoja ana
haki ya kudai na kutafuta haki yake….’akaanza kujieleza.
‘Sasa kwanini umefika hapa kwangu na kujiweka katika uhasama
na familia yako, huoni kuwa unajitafutia mfarakano na jamaa zako….au
wamekutuma?’ nikauliza
‘Nimekuja kwa ridhaa yangu mwenyewe, na wala sikutumwa….niliaga
kuwa nakwenda sokoni, nikaona nikupitie mara moja,…kwanza kwa vile hili swala
limenigusa sana kama mwanamke….nikuambie ukweli, nimekuwa nikijisikia vibaya
sana, ….tangu siku ile nilipokuona umewekwa kwenye kile kichumba na ile hali,
…moyo wangu hakuwa na amani, na nimekuwa sijisikii vyema, na ninaweza kukuambia
kuwa hata ule moyo wa kuolewa huku kwenu, umepungua…’akasema .
‘Ndio mila zetu, hatuwezi kuzikwepa,…na ukiolewa kwenye
familia zetu mambo kama hayo yakitokea huwezi kuyakwepa,..sisi tunaliona ni
jambo la kawaida maana tumelikuta lipo, na sio kuwa mimi ni kwanza kutendewa
vile, ….ni kawaida za mila zetu. Lakini hata hivyo huwezi kukataa kuolewa eti
kwa vile utafanyiwa mambo kama hayo, …pamoja na hayo, kuna mambo mengine mazuri..’nikasema.
‘Hapana, mimi ni wakili, na naheshimu sana mila na desturi
zetu za Kiafrika, na naheshimu sana taratibu za kidini, lakini kuna haya ya
kimila, ambayo hayana mshiko wa kidini, ni mambo ambayo wazee wetu waliyabuni,
pengine kwasababu zao, huenda enzi hizo yalifaa, lakini kadri siku
zinavyokwenda yanakutwa hayana maana tena,…’ akasema huku akiweka mguu mmoja
juu ya mwingine.
‘Ukiangalia kiafya, na kiutu, hayana maana yoyote,
nikutesana tu. Mambo mengina kama hayo
tunahitajika kuyaondoa au kuyarekebisha yawe katika mfumo unaokubalika, kwani
kuna ubaya gani hata kama ni kuweka mahali tofauti, lakini kuwe na hadhi, namna
ile utaishia kushikwa na maradhi, kama malaria…najua ni ngumu sana hasa kwa
wazee wetu, lakini sisi wenyewe tunaweza kuyapigania na kuyasahihisha, kama
tutakuwa na umoja..’akasema.
‘Wewe unasema hivyo kwa vile huajaolewa ndani ya hizi familia…ukiolewa
mwenyewe utajikuta ukiyafuata yote, vinginevyo jamii, na familia ile uliyoolewa
watakutenga, ..na kwa vile unampenda mume wako, inabidi ukubali yote, hata
hivyo kwa jinsi nilivyokuwa nikijisikia, siweza kuhisi chochote, kuwa labda
naumia,…hapa, akii yangu muda wote ilikuwa haipo....’nikamwambia huku
akiniangalia kwa macho yaliyojaa mshangao.
‘Kama nilivyokuambia najua ni vigumu sana kubadili haya na mengine yasiyofaa…..na
huenda itachukua muda, lakini mabadiliko hayo yanatakiwa yaanza kuanzia kwetu,
kwanza tukubali kuwa kuna mambo hayafai, na wanaoweza kuyaanzisha ni sisi
wenyewe, tunaoumia, …tutaanza kidogo kidogo,….na lakini kama sisi tunaoumia
tutanyamaza na kusema hiyo ndio kawaida, wao hawawezi kujua mateso
tunayoyapata,..hebu nikuulize hivi mwnaume akifiwa na mke wake anafanyiwa kama
mnavyofanyiwa wanawake?’ akaniuliza.
‘Hapana, wanaume hawafanyiwi hivyo..hayo ni mambo ya
wanawake, na kama ulivyoona, hata wasimamizi ni wanawake wenyewe, wao ndio
wanajua kipi kifanyike na kwa utaratibu gani….’nikasema.
‘Unaona, ….kwani mwanaume yeye hajisikii machungu kama
aliyokuwa nayo mwanamke, anapofiwa na mkewe. Mimi hapo naona kuna kasoro,….wewe
huoni hilo?’ akaniuliza.
‘Kama nilivyokuambia, haya yalikuwepo, na sisi tumeyakuta,.
..hata kama utaona hivyo, kuwa hakuna usawa, ….mimi kama mwanamke nitasema
nini, ‘nikasema kwa unyonge.
‘Ni sawa huenda kwa namna fulani mwanamke anatakiwa kuwa na
huzuni zaidi ya mwanaume kwa vile yeye atakuwa aliyepungukiwa na kitu kikubwa
sana katika maisha yake,…na ukizingatia kuwa mtu huna kazi, wewe ulikuwa mama
wa nyumbani, ..’akasema, na kutulia kidogo na baadaye akasema;
‘Huenda waliona kuwa, kwa kufanya hivyo, ndivyo itaonekana
kweli kuwa mwanamke ana huzuni kubwa kuliko mwanaume…lakini hebu tuangalie
kidni hivi kweli dini inaruhusu mambo hayo,..kweli dini inasema mwanamke
ajengewe kilinga kama kile, anatengwa na aishi kwenye mazingira magumu kama
hayo?’akauliza huku akiwa kakunja uso wa kusikitika.
‘Hayo maswali ungeliwauliza wazee,na hayo ni ya kimila zaidi
hayahusiani na dini, mimi sina jibu lake …. samahani sio kwamba nakufukuza, …. …mimi kwasasa ninajiandaa kwaajili ya kesi
yangu kesho, nisingelipenda kuumiza kichwa change kwa mambo mengine…’nikasema.
‘Mpendwa nalifahamu hilo, na ndio sababu ya kukupitia, ….lengo
langu kubwa ni kwa ajili ya hiyo kesi, lakini niliona nianzie kwenye mambo
hayo, maana kesi yako, pia ineonekana imegibikwa na taratibu nzima za mila za
kuwazulumu wanawake haki zai, ….’akatulia kidogo huku akiangalia saa yake.
‘Na nimekuulizia upande wa dini unasemaje,…kwani mimi
naogopa sana kuingilia maswala yanagusana na imani za dini,……mimi najua kabisa
dini haijasema hivyo, …kuna taratibu nzuri tu za dini, lakini watu hawataki
kuzisoma na kuzijua, wanachofuatilia kwa karibu ni hizi taratibu za kimila,
ambazo nyingine zinapingwa vikali na imani za dini….’ Akashika kichwa kwa mkono mmoja, ukiwa kwenye shavu, na kuniangalia kwa huruma, kiasi kwamba sipenda ile hali, ya kunihurumia vile..baadaye akasema;
‘Mimi nijuavyo ni kuwa mwanamke kweli anatakiwa akae siku
arubaini akiomboleza, hiyo ni kawaida,..lakini sio kwa kutengwa, na kufanyiwa
hayo niliyoona ukifanyiwa….na hili sasa limekwenda mbali zaidi, unaona, sasa
kwa vile wanawake wenyewe hatkusoma, hata hiyo dini yenyewe hatuijui, …tunafuata
yale wanaume wetu wanayopenda, na sasa kama unavyoona wanakunyang’anya hata ile
haki yako…’akasema.
‘Je na wewe unaamini kuwa hawa watu wameninyang’anya haki
yangu, au na wewe upo upande wa familia kuwa hiyo sio haki yangu?’ nikamuuliza.
‘Mimi ni mwanasheria, na mwanasheia, anasimamia upande wa
sheria, kutokana na ushahidi uliopo, huwezi ukadai haki kwa kuongea tu…kwasasa
hivi siwezi nikajibu hilo swali, japokuwa ukiliangalia kwa undani, na ushahidi
uliopatikana, inaonekana wazi kuwa huna haki….nazungumzia kisheria ilivyo,
nikivaa kiatu cha hakimu….’akasema huku akisita.
‘Nilijua tu….wamekutuma ili uje ujue undani wangu, au sio?’ nikawa kama namuuliza na yeye akawa
ananiangalia kwa macho ya huruma;
‘Kwahiyo naomba uondoke, maana hutanisaidia lolote….umekipata
ulichokitaka, nenda kawaambie, wenzako, na mume wako anahitajia sana haya
maelezo yangu, ili yamsaidie kuitetea familia yake’nikasema.
‘Nimekuja kukusaidia, kama upo tayari, sisemi kuwa nitakuwa
wakili wako,…hapana, siwezi kufanya hivyo,…kutokana na hali ilivyo, ila naweza
kukupa msaada wa kimawazo ili ikiwezekana uweze kutetea haki yako
kisheria…’akasema.
‘Mawazo kama yapi, na wakati kila kitu nilikwisha kielezea
pale mbele yenu kwenye kile kikao na nyie, mkasema maelezo yangu hayana mshiko
kisheria, ni ya kutungwa …mimi ninauhakika na nililolisema, na kama kweli
mahakama zipo kwa ajili ya kutetea haki, basi mimi nina imani kuwa nitaipata
haki yangu…’nikasema.
‘Mahakama zipo kuhakikisha kuwa haki inapatikana, lakini
mahakama haiwezi kwenda kinyume na ushahidi,….ushahidi ndio nguzo kubwa ya
kuipeleka haki kwa mlengwa,….sasa hebu niambie una ushahidi gani zaidi ya yale
maelezo yako…., kwa mfano,una viambatishi gani kuwa ulilipwa hizo pesa na hizo
kampuni zilizokulipa hizo pesa, na je una shahidi yoyote, anayeweza
kulithibitisha hilo, mfano ulishawahi kuwasiliana na hiyo kampuni iliyokulipa hizo
pesa ikakubali kukusimamia kwa hilo?’ akaniuliza.
‘Ushahidi wote niliokuwa nao, siuoni tena, inavyoonekana
wakati nipo kwenye msiba, waliingia watu humu ndani na kuchukua kila kitu
ambacho kingenisaidia kwenye hiyo kesi..na hiyo kampuni nilijaribu kuwapigia
simu, kuwaomba wanisaidie kwa hilo , lakini wamesema, kwenye kumbukumbu zao
hakuna jina langu, na hii inanipa wasiwasi kuwa huenda, umefanyika mpango wa
kuharibu ushahidi wote….’nikasema.
‘Hakuna aliyefanya hivyo, kama ni huyo mchumba wangu,
nakuhakikishia kuwa hajafanya hivyo, maana wakati anafuatilia, nilikuwa naye,
na kampuni hiyo walitafuta hizo kumbukumbu tukiwa na yeye, hakuna jina lako….na
wafanyakazi waliokuwepo kipindi hicho, hawapo tena, …hapo inakuwa vigumu sana’akasema
na kushika kidevu huku akionyesha kuwaza sana.
'Na namba ya simu uliyoshindia hiyo promosheni ndio hii
inayotumia kwa sasa?’ akaniuliza.
‘Hapana hii ni simu nyingine na namba tofauti, na ile namba
sikuwahi kuisajili, ila hii ya sasa nimeshaisajili,….. ile simu yangu ya mwanzo
iliibiwa wakati nipo kwenye biashara zangu, na sikuirudishia tena ile kadi
yake, maana nilikuwa na kadi za mitandao mingine, ….na hata namba yake
nimeisahau kabisa…..unajua sikutilia maanani sana kuhusiana na hilo, maana
sikufahamu kuwa haya yatakuja kutokea, ningelifahamu kuwa kuna jambo kama hili,
ningelihifadhi kila kitu…’nikasema.
‘Sasa huko mahakamani utakwenda kusema nini…maana ushahidi
na mshahidi ndio mambo muhimu , najua kabisa baada ya maelezo yako watakuuliza
ushahidi na mashahidi, na vyote hivyo huna , unafikiria wao watakuamini
vipi…naona kwenda kwako mahakamani umekurupuka bila kujipanga vyema,…lakini kwa
vile umeshafikisha mahakamani basi tuone itakuwaje, lakini kwa sasa sizani kama
utashinda hii kesi….’akasema.
‘Mimi ninachopigania ni haki yangu, na kama mahakama ipo kwa
ajili ya kutetea haki za watu, mimi bado nina imani kuwa nitashinda, nitaelezea
kila kitu, na wao kama kweli ni waadilifu nina imani kuwa wataniamini, …’nikasema
na yule mwanadada akaniangalia kwa jicho lile lile linaloonyesha huruma.
‘Hivi niambie, sasa mimi ningelifanyeje, nikae kimiya kwa
vile sina hayo yanayohitajika…hapana sitakaa kimiya, nitajitahidi kupigania
hadi hatua ya mwisho, mungu atanisaidia maana ninachopigania ni haki
yangu…’nikasema na huyo mwanadada akaniangalia kwa makini na baadaye akasema;
‘Nashindwa nikusaidie vipi, …maana huelewi sheria ilivyo,
….na sio kosa lako,…hili ni tatizo kubwa hasa kwa sisi wanawake, wengi
hatujasoma, na hata wale waliosoma, hawatoi mchango mkubwa kuwasaidia wenzao
angalau na wao wakasoma wakaijua haki yao,na hapo ndipo tunapojikuta tukinyanyasika kila siku… 'akasema huku akiwa kashikilia shavu, kuonyesha huzuni.
'Ohh, ningelisema niwe wakili wako ili
niweze kukutetea, lakini hakuna wakili atakayekubali kesi isiyo na ushahidi,
….hii kesi yako ina utata, na ukisikiliza maelezo yako, yanakuwa kama ni ya
kubuni au kuyatunga kwa jaili ya kupata mali…’akasema.
‘Kama huamini basi, wewe ondoka, nahisi wamekutuma ili
kunichimba,..haya umesikia kila kitu nenda kawaambie, ….lakini mimi najua mungu
atanisaidia tu…’nikasema kwa hasira.
‘Nimeshakuamba kuwa mimi sijatumwa na mtu….Nimekuja kwa ridhaa
yangu mwenyewe, na sijakata tamaa kukusaidia, nitajitahidi kukusaidia kadri
niwezavyo, maana lengo na mdhumuni yangu nikutumia elimu niliyoipata kwa ajili
ya kwasaidia wanawake, …..na sijakuwa mzoefu sana wa kazi hii, lakini lengo na
nia yangu ni kufanya hivyo, na kila mara ninapotembelea vijijini nakutana na
mambo mengi ambayo, yananipa uchungu sana, na kunifanya nijione msalati kama
nitakaa kimiya…..’akasema huku akisimama kuondoka.
‘Nataka nianzie mahali…nimeshafanya kesi chache lakini kesi
hizo zilikuwa za kiofisi, sijajiweka sawa kuwa wakili wa kujitegemea, sijawahi
kufanya kesi yakutetea akina mama,….nyingi ni za wafanyakzi kudai haki zao, au
mwajiri kutetea haki yake,…sasa naona muda umefika kugeukia upande huo, nataka
nianze kufanya hivyo…., ngoja nifike nyumba, nitulize kichwa, ninaweza kuja
kukutembelea hata kama ni usiku, kama nitakuwa na wazo linaloweza kukusaidia….kwaheri,
….. lakini kwa kesho nina uhakika hutaweza kushinda hiyo kesi, …huna ushahidi,
utamshawishi vipi hakimu….lakini usikate tamaa, vyovyote itakavyokuwa ujue nipo
pamoja na wewe…’akasema.
‘Wewe nenda kwa watu wako, waambie kuwa mimi nitaipigania
haki yangu,…hata kama nikishindwa hiyo kesi ya kesho nitakata rufaa hadi
mahakamu ya juu, na ikishindikana huko, …nita…nita….’nikashindwa kutamka neno
nililokusudia kulisema, na huyu mwanadada akawa ananiangalia kwa macho ya
huruma, na alipoona nasita kusema hilo neno, akasema.
‘Usijali, tupo pamoja,….nimekuelewa mpendwa,….’akasema na
kuondoka.
NB: Je wewe ungemsaidiaje huyu mwanamke?
WAZO LA LEO:
Imekuwa ni kawaida kufanya mambo mengi bila kuwa na kumbukumbu, ikiwemo kuuza
na kununua badhaa , au kukopeshana bila kuwa na maandishi yoyote au ushahidi wa
watu, hili ni kosa kubwa sana, na huwezi kujua ni nini kitatokea baadaye.
Tujenge tabia ya kudai stakabadhi kila tunaponunua, na kwa wafanyabishara
tujenge tabia ya kuweka kumbukumbu za kimahesabu katika biashara zetu…na pia
tukumbuke kuandikishana pale tunapokopeshana au kupeana pesa, kwa ajili ya
kumbukumbu za baadaye, kwani bashara
bila daftari, hupotea bila habari
Ni mimi:
emu-three
4 comments :
kweli nimesoma nikapata mawazo mengi ila ninataka nifuatilie mpaka nione mwisho je ulienda mahakamani na yule mwolewa pamoja alikusaidiaje hapo baadae ,tupo pamoja
Tunga vitabu kaka unalaza damu wenzako wanatumia jasho lako hata bila ahsante
Aisee!Kama uko juu ila fanya biashara ya vitabu kaka..ni mimi www,swahiliabroad.blogspot.com
Nawashukuruni sana wapendwa na mumenipa faraja, kuonyesha kuwa kumbe ninachoandika kinafaa hasa katika jamii yetu hii. Ni kweli kama ningelifanikiwa kutunga vitabu ingelikuwa ni vyema, sana, ....gharama , muda na vitendea kazi imekuwa ni kikwazo kwangu, kuna kipindi niliwaza kuwa huenda nikapata mdhamini, lkn kumbe nayo hiyo ni kazii ya aina yake. Hata hivyo sijakata tamaa, tupo pamoja
Post a Comment