Mama aliendelea
kunihadithia maisha yake kwa kusema
Mgeni aliyegonga mlango alipoingia tulitupiana macho na
wazazi wangu tukikumbuka maongezi yetu yaliyopita, na baba hakusita kuonyesha
hisia zake kwa kunionyeshea ishara kuwa niwe makini, na mimi nikageuka
kumwangalia mgeni nikichelea asije akamuona baba yangu alipokuwa akinionyesha
hiyo ishara…
‘Karibu mgeni,….’nikasema nikimuonyeshea huyo mgeni kukaa
kwenye kiti, nikitarajia kuwa atasema
kuwa hatakaa ana haraka, lakini haikuwa hivyo, kwani mgeni, alisogea pale
kwenye kiti na kukaa na kabla hajafanya hivyo, aliwageukia wazazi kwa adabu, na
kuanza kuwasiliama mmoja mmoja nikatulia hadi walipomaliza kusalimiana, na
baadaye nikamuuliza mgeni nimpe chochote, ikiwa ni sehemu ya kumchokoza ili
nisikie akisema amekuja mara moja anaondoka….
‘Hapana nashukuru sana, mimi nimepitia tu hapa, kwani
sikuwepo kwenye kesi, na niliyoyasikia kwa wenzangu yaliniuma sana, na yamezidi
kunitonesha moyo wangu…nikaona nije tuongee, na tuone ni jinsi gani tutaweza
kusaidiana,kama tulivyoongea siku ile…’akasema na mama akanionyesha ishara kuwa
niwe makini.
‘Ndivyo ilivyo, yote namwachia mungu….’nikasema nikisita
kuongea sana.
‘Mimi nilijua mapema, kuwa itakuwa hivyo kama nilivyongea na
wewe siku ile, ni hii sio kwmba labda unaonewa, hapana, yote ni kwa vile huna
ushahidi wowote wa kulinda hoja yako, itamuwia vigumu hakimu kukupatia haki
yako kwa hali kama hiyo, na ukiangalia wenzako walikuwa wamejiandaa kwa kila
kitu..’akasema.
‘Lakini haki ya mtu haiendi bure, hata kama watashinikiza na kupata mali ya dhuluma,
ipo siku itawatokea puani, mimi nina imani kuwa haki ya mtu haiendi bure….’akasema
baba.
‘Mzazi wangu, hizo ni imani za kujipa moyo, na bora kuwa na
imani hiyo ila wenzako hawayaangalii hayo….na imani kama hiyo hata wao wanayo,
kuwa kila mtu akipata kapata kwa uwezo wa mungu na ni haki yake kupata, hata
kama kadhulumu, wanakuambia kwanza kupata, mengine ni majaliwa…kwahiyo ukiomba
omba ukiwa na wewe unajituma na kujisaidia, usilale huku unaomba upate chakula,
…kweli utakipata, hapana ni mpaka utoke, ukitafute…ukiomba wakati mwenzako
keshapata, inakuwa kama dua la kuku kwa mwewe….’akasema.
‘Sasa kama tutakuwa tunafanya hivyo, yaani dunia ikiwa ni ya
kudhulumiana, kuwa yule mjanja ndiye mshindi hata kama sio haki yake, unafikiri
kutakuwa na amani kweli, maana kama mimi nimeshindwa na nina uhakika kuwa hiyo
ni mali yangu..kwa vile tu sina huo unaoitwa ushahidi kutokana na uchakachuaji
wa ujanja, huoni kuwa ninaweza kufanya lolote….’akasema mama.
‘Mama,….wenzako wamesimamia kwenye sheria, ina maana lolote
utakalolifanya litakuja kukuleta matatizo baadaye, maana sheria itawalinda, …cha
muhimu wewe ni kujipanga, na kuhangaika kutafuta ushahidi, maana upo,
haiwezekani ufanya jambo, kusiwepo na ushahidi, cha muhimu ni kujaribu kutafuta
wale wanaojua sheria, …wao mawakili, hawa ukiwaeleze ajinsi ilivyokuwa, watajua
jinsi ganii ya kusaidia.’akasema.
‘Lakini hayo yanahitaji pesa,….huwezi kumtafuta wakili, aje
ajitoee, , yeye kwake hiyo ni ajira, ….na ukiangalai kesi hii ilivyokaa, inawezekana
kabisa, wameshauharibu ushaidi uliopo wa kutusaidia , mimi naona sheria hizo
zimewekwa ili kuwasaidia wenye nacho ni sheria za kutetea dhuluma, kama sheria
ndio hivyo, basi haina haja ya kwenda mahakamani…’akasema baba.
‘Tatizo sio mahakama, tatizo ni wewe unayedai haki yako, je
una viambatishi vya kuhakikisha kuwa hiyo ni haki yako,…nakupa mfano mdogo tu
wa maisha yetu, wengi tunapokwenda kununua vitu madukani, hadai kupata
stakabadhi , kitu ambacho ni haki yako, kwahiyo hata likitokea tatizo huwezi
kwenda kulalamika kuthibitisha kuwa wewe ndiye uliyenunua hicho kifaa
mahali hapo…lakini kama ungelikuwa na
stakabadhi, huwezi kudhulumiwa, huo unakuwa ni ushahidi wako,….ni vitu unaviona
ni vidogo, kama hakuna tatizo, lakini kukitokea tatizo utauona umuhimu
wake….’akasema.
‘Kwahiyo una maana nikinunua majani sukari, hivi vitu vidogo
vidogo tunavyonunua kila siku nahitajika kupewa stakabadhi, ..huoni ni kupoteza
muda, na hata hivyo hawo wenye maduka nao watakuwa na muda gani wa kukuandikia
hiyo staakbadhi, pipi, stakabadhi, majani, stakabadhi….watu wenyewe hata
kuandika ni shida…..’akasema mama.
‘Ni muhimu kufanya hivyo, kama umenunua vitu vidogo vidogo
vingi, vyote hivyo vinaandikwa kweney staakbadhi moja, ndivyo ilivyo, maana hiyo
pia inawasaidia watu wa ushuru, wakija kwenye maduka, wanahitaji kuangalia hizo
stakabadhi, kwa ajili ya malipo ya kodi, kwahiyo, kitu kama hicho kina manufaa
sio kwako tu, lakini pia kwa maendelea ya taifa letu….ni taratibu ambazo
tunazizarau kwa vile labda hatujakuwa na utaratibu mzuri na tabia hiyo ya
kuweka kumbukumbuku, lakini kukiwepo na utaratibu mnzuri, na sisi wateja,
walaji tukawa makini kwa hilo,….kutakuwa hakuna matatizo tena, na wote tutakuwa
tunaijenga nchi yetu….’akasema.
‘Sasa sisi watu wa chini, watu wa huku kijijini tutajuaje
hayo,na elimu yetu ni ya chini ya mwembe, ukiangalia hata hizo stakabadhi
wameandika kwa kiingereza…wakati sisi lugha yetu ni ya Kiswahili, wengine hata
hicho Kiswahili ni shida kwao wanajua lugha zao za asili,…..huonio kuwa hayo
mambo yamewekwa kuwalinda wajanja…?’ akasema baba.
‘Ni kweli tatizo ni elimu, na huenda hilo la ukosefu wa elimu
limefanywa makusidi ili werevu wapate kufaidika na wasio soma wapate
kudhulumiwa,….unafikiri kama tungekuwa na wakili, kweli kesi kama hiii tungelishindwa,
n kwakuwa hatuna wakili, hatuna pesa za kumpata wakili, na elimu yetu ya
kutambua ni nini tufenye ..basi tena..’akasema mama.
‘Wazazi wangu,….mimi sijakubali kushindwa, hata kama sina
hiyo elimu inayotakiwa, lakini nina elimu yangu ya asili ya kutambua kuwa hili
ni jema au hili ni baya, nina elimu ya kutambua kuwa hii ni haki au hii sio haki
yangu, tatizo ni jinis gani ya kumshawishi mtu mwingine kuwa ninachodai ni haki
yangu, kwa vile nafsi za wengi zimejaa ubinafsi na dhuluma….’nikasema na huyu
mgeni wangu akawa anatuangalia kila mmoja akitoa maoni yake na kama kawaida
yake macho yake yalijaa huruma,….inaonekana hiyo ndio tabia yake.
‘Ndugu yangu, wazazi wangu, kama nilivyowaambia kuwa huenda
sisi wenyewe ndio tunachangia haya yote, na hii itawafanya hawo werevu
kuwachukulia haki zenu. Kwasababu watu wengi hawataki kujua kuwa haki japokuwa
ipo, lakini inahitjia kuipigania, sio kila kitu kinakuja kama mvua, na hata
mvua ukiwa umeharibu vyanzo vyake, itaadimika. Kwanini hatujiuliza kuwa, kuna
tatizo gani tukifuata utaratibu, ….’akatulia akiwa kaangalia chini.
‘Ni kwanini tunazarau
kufuata utaratibu wa mambo mengine ambayo yapo wazi, mimi sioni kwanini mtu usidai
kitu kama stakabadhi….au upo ndani ya daladala unalipa nauli hudai tiketi
yako,…baadaye linatokea tatizo unashindwa kudai haki yako..haya ni mambo mdogo
tu yasiyohitajia elimu kubwaa…jamani hali ilivyo sasa,tunahitaji tubadilike.
….’akasema huyo wakili sote mle ndani tukawa tumetulia kumsikiliza.
‘Sasa mimi nimekuja, pamoja na hayo, lakini kama
nilivyoongea na ndugu yangu huyu, nilimuelezea kuwa nitajitahidi kutafuta
uwezekano wa kumsaidia, lakini kama ujuavyo, mimi nipo ndani ya hiyo familia,
hata hivyo, mimi ni mwanasheria, kama mwanasheria nihitajika kutumia ujuzi
wangu huo kuhakikisha sheria inatekelezwa, kwa haki, ……….’akatulia kidogo.
‘Mimi niliporudi Dar, nlijaribu kufuatilia tena kule kwenye
hiyo kampuni, nilihangaiak sana, nia na lengoo langu, lilikuwa kama inawezekana
kumpata huyo aliyekuwa mkuu wa hicho kitengo wakati huo, na japokuwa waliweza
kumpata, …lakini ikawa vigumu kwa huyo mtu, kusema lolote, kwa vile kumbukumbu
zote zilibakia humo humo kwenye hiyo kampuni, hakuondoka nazo…hata hivyo,
nilimuomba afanye kila iwezekanavyo, awaombe wenye hiyo kampuni, atoe msaada
wake…’akatulia.
‘Tatizo ni kuwa mtu anapoondoka kwenye kampuni husika ,
haruhusiwi tena kufanya lolote kwenye hiyo kampuni, na ukizingatia kuwa huyo
mtu alikuwa ameshaajiriwa kwenye kampuni nyingi, asimu kibiashara na hiyo
kampuni tunayoizungumzia….’akatulia
‘Ndio maana narudi pale pale, kuwa unapofanya jambo la
kibiashara, kulipa pesa au kupokea pesa, huwa mara nyingi unahitajika kuwa na
stakabadhi na kampunii kubwa kama hiyo , isingeliweza kutoa pesa nyingi kama
hizi bila kuwa na kumbukumbu za malipo….na hilo ndilo limenipa hamasa ya
kufuatilia…’akatulia.
‘Sasa cha ajabu…..nilichokiona ni kuwa kwenye kumbukumbu
hizo jina lako halikuwepo….ni kwanini?’ akauliza.
‘Kama nilivyokuambia,…nilihitaji nipate hizo pesa, kwa
haraka, na niliwaomba, wafanye iwezekanavyo, ili nipata hizo pesa, hata kwa
kusimamiwa na mtu mwingine…sikujali mambo ya stakabadhi..na hata nilipopewa
hiyo stakabadhi, sikujali kuangalia ni nini kilichonadikwa….mawazo hayo sikuwa
nayo…sasa hivi ndio wazo hilo linanijia,….kwakweli sikumbuki, kuangalia jina kwenye
hiyo stakabadhi kama kweli liliandikwa langu au….sikumbuki kabisa…’nikasema.
‘Lakini ulipewa stakabadhi ya kuonyesha kuwa umepoeka pesa….?’
Akauliza.
‘Ndio nilipata….na nikaja nayo, na hiyo pamoja na kumbukumbu
nyingine walizonipa nilihifadhi kwenye mkoba wangu, ambao ni mkuukuu…niliuweka
kwenye kabati, na vitambulisho vyangu vya kupigia kura…lakini havipo tena,…’nikasema.
‘Hapo ndipo nahisi kuna jambo limejificha ndani yake….maana
hata nilipokutana na huyo jamaa, na nilipomwelezea hilo, nilimuona akisita, na
hata alipokumbuka, alikuwa hapendi kabisa kunisaidia,…nahisi kuna kitu
kimefanyika,….lakini sijakata tamaa, kwani baada ya kuona hivyo, ikanibidi
niwasiliane na vyombo vya usalama, ili wafanya uchunguzi…’huyo mwanadada
akatulia.
‘Oh, wanaweza kukubali kufanya uchunguzi kwa tukio kama
hilo?’ baba akauliza.
‘Ndio kazi yao….lakini unahitajika uonyeshe dhamira ya kweli
kwao,…mimi ni wakili, na mawakili wanakuwa na dhamana kisheria, kwahiyo
nilipowaambia , waliona kuwa lina umuhimu, hata hivyo yupo mwanausalama mmoja
naelewana naye, amekubali kulivalia njuga…’akasema.
‘Oh,ndugu yangu nitashukuru sana, lakini nitawalipa nini,
maana hali yenyewe unavyoiona, sina mbele wala nyuma, hata duka ambalo
nililitegemea, siwezi kufanya lolote tena, …..limefungwa eti kwa vile lipo
kwenye migogoro, …’nikasema.
‘Hiyo haiwezi kukuzuia kufanya biashara yako, kwa vile ndio
sehemu inayokupatia riziki, ….kwa vile nimeamua kukusaidia kutokana na jinsi
mambo yalivyojitokeza, nitajitahidi upewe kiabli cha kufanya biashara…’akasema.
‘Huoni ukifanya hivyo, utakuwa umeisaliti familia yako?’
nikumuuliza.
‘Usijali….imebidi iwe hivyo, maana mwenzangu hanielewi, yeye
kaweka ufamilia mbele, na kuiweka sheria nyuma…hilo tumeshindwa kukubaliana ,
na hata uchumba wetu umeshaingia doa…sijui kwanini…labda, akini hilo tuliache
kwanza.’akasema na kuonyesha uchungu fulani kwa kukunja uso..
‘Ina maana wewe na mchumba wako hamuelewani tena?’
nikamuuliza.
Akainama na kuangalia chini, baadaye akawa kama kajishitukia
na kuniangalia machoni, na hapo akaniuliza ;
‘Nikuulize swali, na naomba unijibu kwa usahihi, maana
nimeshaamua kukusaidia, na kwa ajili hiyo, huenda uchumba wangu na mwenzangu
ukaisha…japokuwa oh,…., lakini niliyoyasikia yamenikera sana, sijawa na uhakika
wa moja kwa moja, ila sikio halina kizuizi, ….napenda nikuulize swali muhimu
sana…’akatulia huku akiwa ameniangalia machoni.
‘Uliza tu mpendwa…’ aliyesema hivyo alikuwa ni mama, mimi
nilikuwa nimeduwa, uwoga ulikuwa umeshaanza kuniingia sijui kwanini...
‘Je kama ni lazima ili tuweze kufanikiwa kwa hili, kama
kutakosekana huo ushahidi ninaoutafuta ambao ni muhimu sana….na ikabidi
tutafute njia nyingine, na njia zipo nyingi za kutafuta haki yako, na nyingine
sio za moja kwa moja, lakini lengo ni kutafauta njia ya kupata haki yako.
Mimi niliwaza sana wazo hili, nikaona nisiwe machoyo, maana
hata hivyo, naona mambo yameshaharibika,….kuna njia moja iliyobakia ambayo ni
kujitoa muhanga , hata kama hupendi, lakini inabidi, ili tuweze kushinda, …..’akatulia
huku akionyesha ujasiri fulani.
‘Nasema hivyo, kwa vile nimeamua kukusaidia na hii ni njia
nyingine mbadala ya kupata ushahidi na kupata haki yako,..hii ni njia ya
kupitia kukubali kurithiwa….nazungumza hili kwa vile nina ushidi kuwa kama
utakubali, tunaweza kuvipata hivyo vitu…na ikibidi, itakuwa njia nyingina ya kupata
ushaidi tunaouhitajia, unaweza kukubaliana na wazo hili?’ akauliza na kunifanya
nishituke, yeye akawa nusu anatabasamu, nusu haeleweki, lakini alionyesha kuniangalia kwa shauku
Sauti yake ilionyesha udhabiti, kuashiria kuwa alikuwa na
uhakika na alichokisema, …na kwasaabbu hiyo nikawa na wasiwasi kuwa huenda wazo
hili likawa na uzito mkubwa,….sikutarajia kuwa hata huyu mwanadada mwanasheria
angelikuja na wazo kama hili…kichwani nikawa namuomba mungu anipe wasaa wa
kutoa jibu, litakalokidhi haja, na isiwe jibu linataliniweka kubaya.
Nikawageukiwa wazazi wangu, ambao na wao mwanzoni walinipa wazo hilo…
Baba na mama wakaniangalia, kila mmoja akiwa shauku ya
kusikia kauli yangu, sikurizika na macho yao, nikaona wao wanaweza wakakubalina
na wazo hili hata kunishinikiza nikubali kurithiwa, ….na hapo nikajaribu
kumvuta huyo anayehitahika kunirithi, je niatweza kishi naye, je nafsi yangu ipo razi naye,….je kweli nampenda..
‘Nilishangaa kwanini kila ninapokutana na huyo jamaa, nafsi
yangu inakuwa kwenye hisia zisizo za kawaida, siwezi kuziita kuwa ni kupenda,
hapana, sijawazia jamboo kama hilo, ila kila nilipobahatika kuonana naye moyo
wangu ulikuwa ukienda mbio….lakini baada ya siku ya ile kesi, moyo wangu
ulishaingia kutu, ila hali ya ya moyo kwenda mbio ilibadilika na kuwa chuki,…..na
kama ningelikuwa na uwezo wa kufanya jambo, baya, basi nisingelisita kufanya
hivyo kwa mtu kama huyu.
‘Nikageuza macho yangu na kumwangalia huyo mwanadada, ambaye
alikuwa kaniangalia moja kwa moja machoni, ….lakini cha ajabu macho yetu
yalipokutana kwa sasa nilichokiona machoni kwake ni ukungu wa machozi,
yaliyokuwa yakitaka kutoka,…na alipoona hivyo, akachukua leso yake na kujifanya
anajifuta usoni, kumbe alikuwa na nia ya kuiondoa ile hali machoni mwake, mimi
bia kujijua zaidi nikajikuta niongea hivi ….
‘Hapana , siwezi kukubali kurithiwa, kamwe, hata kama kwa
kufanya hivyo, kungesaidia kufanikiwa kupata haki yangu, ..kamwe….sitaweza
kudai haki kwa kuuza utu wangu…..’nikasema na upande wa pili wa wazazi wangu ,
nikawasikia wakipumua,lakini sikupenda kuwageukiwa, macho yangu yalikuwa
yanamtizama huyo mwanadada, na akacheka kidogo, kicheko cha kuonyesha
kushangaa, halafu akawa kama hataki kuniangalia machoni, akasema;
‘Ahsante sana,…..’ Sikuelewa kwanini kasema Ahsante…nilijaribu
kumwanmgalia machoni, lakini hakunipa mwanya huo, akainuka na kuanza kuondoka, bila
kusema kwaheri, na alipofika mlangoni, akawageukiwa wazazi wangu akasema;
‘Hongera wazazi wangu,……kweli mnajua kulea, ….’halafu
akanigeukia na kusema;
‘Tutakutana mahakamani..’akasema huku akianiangalia kwa
macho makavu, ambayo usingeliweza kujua ana nia gani, ya amani au ya shari…akaondoka.
NB: Ndivyo ilivyokuwa je, itakuwaje..?
WAZO LA LEO: Hali
jinsi inavyozidi kuwa ngumu, kila mmoja anajaribu kupata, kwa njia nyingi, na
nyingine zisizo za halali. Na kwa hali hii , ule utofauti wa walionacho na
wasio kuwa-nacho unazidi kuwa mkubwa, ubinadamu unakuwa ni jambo adimu, watu
wapo tayari kudhulumu, kudanganya, kuhonga, ilimradi wapate, na wakipata wanatafuta mwanya wa kuhalalisha kipato chao hata kwa kutumia maandiko
matakatifu, swali langu ni kuwa je
tunamdanganya nani….
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
duh!leo nimepata kkitu baada ya kusoma kisa hiki..big up sana...
Post a Comment