Kama ilivyotarajiwa na wengi kesi hiyo haikuwa nzuri kwangu,
na wanasema wahenga, siku njema huonekana kuanzia asubuhi, na mimi siku hiyo
nilishaanza kuiona kuwa haitakuwa na jema kwangu. Akili yangu ilikuwa haitulii,
na moyoni nilikuwa na wasiwasi,…
Nilipokuwa tayari nimeshajiandaa mara simu yangu ikaita, ….nikashituka
utafikiri sijawahi kusikia huo mlio kabla, nikaitoa hiyo simu kwenye mkoba
wangu, na kuangalia mpigaji ni nani, alikuwa ni nesi, huyu nesi nilimuomba awe
karibu na baba yangu wa kufikia, nilimuomba awe akimhudumia baba yangu huyo,na
kama kuna tatizo lolote aweza kuniarifu kwa haraka,…
Baba yangu huyo wa kufikia bado alikuwa kalazwa, mkono wake
ulikuwa umefungwa mhogo(POP),na sehemu ile aliyochomwa kisu, ilikuwa imeshonwa,
lakini alikuwa akidai ubavuni, alikuwa akipata maumivu makali, kwahiyo wakawa
wamempiga picha ya X-ray, na walikuwa wakisubiria matokeao yeka, na kutokana na
hiyo hali, bado alikuwa amelazwa hapo hospitalini. Tulitarajia kuwa huenda wiki
hii angeliruhusiwa, lakini dakitari akashauri kuwa abakia siku mbili zaidi
akisuburia majibu ya vipimo alivyochukuliwa.
Nikaichukua simu yangu kwenye mkoba, kwani nilishaiweka
ndani ya mkobwa wangu, tayari kwa safari ya kuelekea mahamani. Nikasubiri kama
huyo nesi anabipu, au anapiga, na nilipoona simu inaendelea kuita,nikaamua
kuipokea, nilihisi mapigo ya moyo yakiongezeka, kwa wasiwasi, nikaanza kuhisi
vinginevyo, …na hisioo hizo zikanifanya nikae kwenye kiti wakati naiweka hiyo
simu hewani.
‘Halooh,…’nikasema kwa sauti ya mashaka.
‘Ni mimi nesi hapa napiga simu kutoka hospitali ya
mkoa,….’akasema.
Huyo nesi alisema
jana usiku mgonjwa hali yake haikuwa nzuri, ..lakini leo asubuhi kidogo mgonjwa
ana nafuu, ila kaagiza kuwa ananihitaji mimi niende tukaonane naye kwa haraka
sana.
‘Nesi ningelikuja maana sijui kwanini ananihtajia hivyo ,
lakini nahitajika mahakamani, leo ndio siku yetu ya kesi yangu..’nikasema na
Nesi akasema atajaribu kumweka sana.
‘Kwani unamuonaje…yupo katika hali mbaya kiasi gani?’
nikamuuliza.
‘Usiku ndio ilikuwa na hali mbaya sana, joto lilikuwa kali
sana mwilini, na kwa vile tulishachukua vipimo vya damu, na picha ya x-ray tutaangalia
tatizo nini, huenda ni malaria au inawezekana ni athari za ndani kwa ndani, kwa
hivi sasa joto halipo tena, na halalamiki kusikia maumivu tena, sasa hivi
anasema vyote vimatulia…kwahiyo hali yake sio mbaya sana, lakini ilibidi
nifikishe ujumbe wake kwako maana kasisitiza kweli…’akasema
‘Basi tutaangalia jinsi gani tutakavyojipanga, na nashukuru
sana nesi….’nikasema.
‘Usijali, tupo pamoja, nakutakia kilalaheri…’akasema huyo
nezi.
Baadaye niliongea na
wazazi wangu, ikabidi tugawane, nikamwambia baba yangu mzazi ni bora yeye
apitie huko kwa mgonjwa akaone kuna tatizo gani, halafu yeye akitoka huko
tukutane mahakamani, kwani na yeye anaweza kuhitajika kama shahidi. Kwakweli
moyo wangu haukuwa na amani tena, kila mara nilikuwa nikijiuliza kwanini baba
yangu huyo ananihtaji kwa haraka kiasi hicho, kuna nini, je ni kutokana na
kuumwa kwake, au kuna jambo jingine ….
Au kuna jambo jingine linalohusiana na hiyo kesi, kwani
alikuwa anafahamu fika kuwa siku hiyo ndio siku ya kesi yangu, na alishanipa
baraka zake,…..sasa kuna nini…. nikawa najiuliza maswali mengi bila kupata
majibu.
*********
Tuliingia mahakamani na kesi ikaanza, kwasababu sikuwa na
wakili, ilibidi nisimame mwenyewe kujielezea, na niliposimama watu walikuwa wametulia,
wakinitizama kwa shauku, nilishangaa kuona watu wengi hapo mahakamani, sikujua
ni kwasababu ya kesi yangu au wamekuja kwa kesi nyingine, sikujali hilo,
nikajipa moyo na kuanza kutoa maelezo yangu, na baada ya kumaliza maelezo yangu,
sikutaka kuongea mengi sana, nilifupisha kadri ya uwezo wangu,…
Hakimu akauliza kuwa nina uthibitisho wowote au shahidi
yoyote, kuthibitisha maelezo yangu, nikasema kwasasa sina……
Nikafikia mwisho wa maelezo yangu na hakimu akaruhusu
maswali, na aliyeanza kuja kuniuliza maswali alikuwa yule yule mwanasheria wa familia
ya mume wangu.
Kwakweli maswali yake yalinifanya watu wanione mimi ni
tapeli, niliyejitungia mwenyewe mbinu za kupata nyumba, na duka,….na baadaye
nikahitajika kutoa mashahidi na ushahidi nikawa sina. Zamu yangu ikaisha, na
ikaja zamu ya washitakiwa,…kwakweli walikuwa wamejiandaa na kwa vile walikuwa
na mtu anayefahamu ni nini anachokifanya, nikaishiwa nguvu na kukata tamaa kabisa.
Huyo mwanasheria wa familia, ambaye alisimama kwa niaba ya
familia, alianzia mbali, na kwa kujiamini, na akafikia sehemu akasema;
‘Muheshimiwa hakimu, mimi ni ndugu wa marehemu, na nilikuwa
nikifika mara kwa mara nyumbani, na kipindi alipofungwa, nilikuwa masomoni nje
ya nchi, kwahiyo sikuweza kuja kuona ni nini hasa kilitokea, na kama
ningelikuwepo, natumai ukweli halisi ungejulikana mapema, kwani ukweli huo
ulikuja kujulikana wakati keshatumikia kifungo…...’akatulia na kumwangalia
hakimu ambaye alikwa akindika kitu kwenye makabrasha yake.
‘Ndugu hakimu, ndugu yangu huyo alipotoka kifungoni, alikuwa
mgonjwa, na baada ya uchunguzi akapatikana kuwa kaambukizwa kifua kikuu, …na akaanza
matibabu, lakini hali yake ilizidi kuzorota, kama unavyojua kuwa ugonjwa huo
ili dawa zifanye kazi vyema unahitajika kufuata masharti , ikiwemo kutokunywa
pombe na kuvuta sigara. Lakini kutokana na hali ya msongo wa mawazo,na kukosa
mshauri wa karibu, akawa anavunja hayo masharti, na dawa zikawa hazifanyi kazi
yake ipasavyo. Mimi kipindi hicho nilikuwa nimesharudi, kwahiyo nikafika kuonana
naye….
‘Kwakweli hali yake ilikuwa ya kusikitisha, maana inavyoonekana,
pamoja na kuwa alishagunduliwa tatizo ni
nini, lakini kuna mambo mengi alihitajika kutendewa, kama vile kupewa ushauri
nasaha, kupata lishe bora na ukarimu,…..kwa udadisi wa haraka, sisi kama
wnafamilia tuligundua kuwa hakuwa akipata mambo hayo ipaavyo, maana unaweza
ukakaa na mgonjwa usijue kumliwaza, na badala yake ukatumia lugha ya ukali,
shuruti na kukatisha tamaa. Ndugu yangu huyo kwa ahli aliyokuwa nayo, na
kutokana na mitihani aliyokuwa nayo, alihitaji ushauri nasaha ikiwemo lishe
….’akatulia.
‘Basi tulishauriana jinsi gani ya kumsaidia, na tukaonana
naye ili kumpa ushauri wetu, lakini mwenzetu huyo hakukubaliana na wazo letu
moja kwa moja, kama mume alihitaji kuongea na mkewe…lakini tulipokutana naye
baadaye, tulishangaa akisema hawezi kuondoka kwake na kuitelekeza familia yake.
Lakini hata hivyo sisi kama ndugu ilibidi tupate njia nyingine mabadala,
tukashauriana kuwa mmojawetu awe pale nyumbani kwa marehemu,ili kutoa msaada wa
karibu, na hapo tukamchagua mmoja wa ndugu zetu, …..mdogo wetu wa kike, ili awe
anafika na kutoa huduma zinastahili.
‘Siku moja, nilifika tena kuja kuwaona, mara nyingi
ninapofika yeye huja kwenye makao ya familia yetu, kwa kaka yetu mkubwa, siku
hiyo aliniambia kuwa anahitaji msaada wangu, nikamuuliza msaada wa nini,
akasema kuwa wao sasa hivi wana nyumba na duka, na amejitahidi hadi hivyo
vimemilikishwa kwa jina lake, lakini bado hana uhakika na usalama wa mali hizo
kwa baadaye..
‘Kwa baadaye kwa vipi, bro, maana umeshamilikisha, hapo
huhitajii kuingiwa na wasi wasi tena…’nikamwambia, na yeye akasema;
‘Kama unavyoona hali yangu, sitarajii kuishi muda mrefu
tena,….maisha yangu yalimalizikia jela, na yaliyotokea yamenivunja nguvu na
sina raha….kwahiyo naona kuna haja ya kufanya jambo kwa ajili ya mtoto wangu…’akasema
hivyo
‘Nikajaribu kumliwaza, maana alivyokuwa akiongea, ilionyesha
kuwa keshakata tamaa ya kuishi, kwani alikuwa kama anatoa usia, wa jinsi gani mali
yake itakavyogawanywa, na alitaka hayo niyaweke kisheria, basi mimi nikamwambia
kama ni hilo halina shida, kwanza inabidi yeye mwenyewe aandike kwa mkono wake,
aweke na sahihi, halafu nitamtafuta mwanasheria kuja kusimamia, sikutaka mimi
nifanya kila kitu
‘Siki hiyo sikulichukulia maanani, nikaondoka, na siku
kadhaa,akanipigia simu kuwa keshaandika kila kitu, nimlete huyo mwanasheria, na
sikutaka kumvunja nguvu, nikamtafuta mwanasheria, tukafika naye, akatuonesha
hiyo barua aliyoandika, ambayo ilielezea jinsi gani anataka mali yake iwe kama
akifariki.
‘Ndugu hakimu, mimi niliona ajabu kubwa, maana mali yote
aliindikisha kwangu, na msaidizi wake awe ni mdogo wangu wa kike, nikamuuliza, kwanini anafanya hivyo, wakati
ana mke na mtoto…..’akasema;
‘Mila zetu mume akifariki, ndugu anaruhusiwa kumrithi mjane,
na wewe nimekuona unafaa kumrithi mke wangu,…kwa vile wewe hujaoa, na pia mke
wangu bado kijana, mtaweza kuishi naye bila wasiwasi, kwahiyo wewe utasimama
badaa yangu,….sihitaji kumwandikisha mke wangu, ….ni kama mimi nilivyo, mbona
kila kitu nimeandikisha kwa jina langu,…mke sijamuandikisha, kwahiyo itakuwa
hivyo hivyo kwako, na nakuomba usije ukamtupa mke wangu,….na pili wewe ni
mwanasheria, unaweza ukazilinda mali zetu…kwa ajili ya familia yangu, nakuamini
sana ndugu yangu’akasema huku akimwangalia hakimu.
‘Ndugu yangu haya uliyoyaandika na mambo mazito, je uliwahi
kuongea na mke wako?’ nikamuuliza.
‘Mke wangu sijaongea naye kiundani, hata hivyo, nimjuavyo
mimi hatakubali , najua yeye ana msimamo wake, na nikimwambia haya anaweza
akachanganyikiwa akashindwa kufanya shughuli zake, ambazo zinatusaidia kuishi,
kwahiyo akasema kama litatokea lolote,..hatuombei hivyo, lakini mimi mwenyewe
najiona, kila siku nakufa….nakuomba wewe ndugu yangu uwe ni msimamizi wa mali
yangu, na sio msimamizi tu, lakini uwe m- miliki kwa niaba yangu, maana wewe
ndio mimi….’akasema
‘Kwakweli muheshimiwa wakili, nilikataa mbele yake,
sikukubali kubeba mzigo huo mnzito, ..kwasababu hayo yalikuwa msimamo wake,
hajamshirikisha mkewe….’akasema na kutulia.
‘Lakini pia nilikuwa an sababu nyingine kubwa ya msingi ya
kukataa…, kwasababu nilishasikia uvumi kuwa mali hiyo , yaani nyumba na duka,
vilijengwa na mkewe, na mkewe aliwahi kusema kuwa alijenga na pesa aliyopata
kutokana na ushindi wa promosheni ya moja ya kampuni za simu. Hilo nililiona
linaweza kuleta utata baadaye.
‘Uvumi huo tuliwahi kuongea naye kabla, na aliniomba
nifuatilie huko mjini, nione kuwa kweli aliwahi kupata hizo pesa, na nilijaribu
kufanya hivyo, na muda alioniita, nilikuwa sijafanikisha huo uchunguzi, kwahiyo
ombi lake, nikaliweka pembeni kwanza, ….Nilimwambia wazi, kwasasa sitaweza
kukubali hadi hapo nitakapokamilisha uchunguzi wangu kuhakikisha kuwa kweli
hayo anayozungumza mkewe ni ya kweli.
Niliporudi Dar, ikabidi nilifanyie kazi hilo swala, na
nikawa nafika ofisi za kampuni hiyo, ambayo shemeji yangu, yaani mke wa
marahemu anadai kuwa ndipo aliposhidia hiyo proimosheni. Ofisi hiyo haikuwepo
hapo tena, na hata jina la kampuni hiyo halikuwepo tena, ila kwa vile
nilifahamu kuwa kampuni hiyo zamani ilikuwa naitwa hivyo na baadaye ilikuja
kuabdili jina na kuitwa kampuni nyingine, na ilikuwa na wamiliki wengine kabisa
na hata wafanyakazi waliokuwepo kipindi hicho hawapo tena.
Ilikuwa kazi kweli kutafuta ukweli wa hilo …kuwa kweli
shemeji aliwahi kushinda, na je kulikuwa na kumbukumbu zozote zinazothibitisha
hilo…nikafuatilia..kwakeli muheshimiwa hakimu , sikuweza kuona ushahidi wowote
kuwa yeye aliwahi kupata huo ushindi, ….na hata jina alke halikuwepo katika
orodha ya watu walioshinda kwa tarehe hizo alizozitaja,….’akatulia.
‘Mimi kuona hivyo, nikawa na mashaka na shemeji, kuwa kama
ameweza kutunga uwongo kama huo, inawezekana pia akafanya lolote kwa ndugu
yetu, kwahiyo nikarudi , na kuonega na familia, na sikuongea na ndugu yangu
huyo marehemu kuhusiana na hilo, maana ningelimwambia huenda ingelisababisha
ugomvi kwenye hiyo familia,….mimi na kaka zangu tukajadiliana kama wanafamilia,
inabidi tumsaidie ndugu yetu, ili kuona usalama wake na afya yake pia.
‘Kwa upande wa afya yake hatukuwa na wasiwasi tena, kwani ndugu
yetu tuliyemtuma awe anamsaidia, alikuwa akifanya hivyo kwa karibu sana, na
dawa na matunzo mengi tuliyatoa kwa kupitia kwake, na ilifikia hadi akaonyesha
mafanikio mazuri,…
Lakini tatizo ilikuwa , pamoja na kuwa ndugu yetu yupo pale,
lakini hawezi kuingilia maisha ya ndani ya wanandoa, na aliona kabisa, jinsi
gani kaka yetu huyo marehemu alivyokuwa akigombana mara kwa mara na mkewe,…na
ikitokea hivyo, yeye, yaani marehemu anakimbilia kunywa pombe na kuvuta sigara,
vitu ambavyo ni sumu kwake….’akatulia na kumwangalia hakimu.
‘Hapo tukawa na mtihani mkubwa, je tufanyeje,…maana hatuwezi
kumchukua ndugu yetu tukaishi naye, ikabidi tuwe tunamuelelekeza ndugu yetu,
yaani mdogo wetu jinsi gani ya kufanya, kuwa kwa mfano akiona kuna ugomvi,
ajaribu kuingilia kati, na kumuondoa ndugu yetu mbali, ili asizidi kuchanganyikiwa..
‘Lakini mume na mkewe,….huwezi kuwatenganisha, …na
kilichokuja kutushangaza ni kuona ndugu yetu anakuwa kama kachanganyikiwa maana
alifikia hatua sasa akifanya kila anachoambiwa na mke wake, …na tunaweza
tukamshauri jambo, akakubali, lakini akifika kwa mke wake, anabadilika, na
ilionyesha wazi kuwa kuna tatizo kubwa sana, na huenda limefanywa hivyo kwa
malengo fulani….na kila ndugu yetu huyo alionekana mwingi wa mawazo, na yeye
mwenyewe alidai kuwa ili kuondokana na hayo mawazo, ndio maana alikuwa akikimbilia
kulewa, na kuvuta sigara, kitu ambacho kilizidi kumathiri kiafya…
‘Alipozidiwa sana, tuliamua kama wanafamilia kufanya kila
iwezekanavyo tumchukue tukae naye, ili tuweze kumuhudumia wenyewe na
kuhakikisha anafuata masharti yote, na matibabu muhimu kwakweli hali yake
ilikuwa mbaya sana, na tunasikitika kuwa uamuzi huo ulifika kipindi
tumeshachelewa….
‘Na utaona ajabu, siku huyo ambayo tuliamua kwenda kumchukua
kwa nguvu,hata mke wake hakuwepo nyumbani, fikiria mgonjwa kama huyo, wewe kama
mke, kama kweli unamjali mwenzako, usingeliweza kuondoka na kumuacha kitandani,
hajala, hajasaidia kuogoshwa, maana ilifikia hatua kila kitu kinafanyika hapo
hapo kitandani, ,……hali yake ilikuwa ya kusikitisha, na alipofika kwetu,
haikuchukua muda akafariki ….tukampoteza ndugu yetu…’akasema kwa uchungu.
******
Mimi pale nilipokuwa nimekaa, huku nasikiliza maelezo ya
huyo mwanafamilia, niliingiwa na hasira, machungu na kama isingelikuwa
kuheshimu sheria za mahakama, ningelifika pale mbele nimzabe kibao huyo mtu na
kumshushua kuwa ni mwongo mkubwa,... Sikuamini kuwa msomi kama huyo angeliweza
kunitunga uwongo kiasi hicho,…sikuamini, yaani ina maana wema wangu wote
niliufanya kwa mume wangu haukutambulikana…wangelijua jinsi gani nilivyokuwa
nikiteseka na mume wangu, wasingelisema hayo, lakini ni nani atathibistiha hayo…
Nilijikuta nikitoa machozi kama maji,…. na hata muda wa
maswali ulipofika sikujua niulize nini, hata hivyo nikajitahidi na kusimama na kwa
hasira nikamuuliza;
‘Kama unadai hizo pesa sio za ushindi wa shindano hilo la
promosheni, je pesa hizo zilipatikana wapi, na ni nani alijenga hiyo nyumba?’
nikamuuliza kwa hasira.
‘Ndugu yetu alituambia kuwa katika shughuli zake mbalimbali,
aliweza kupata pesa nyingi, kwani walikuwa wakihangaika hadi huko milimani
kutafuta madini, kwahiyo…kama ni biashara ya madini, huwa inatokea mtu akapata
bahati na kupata pesa nyingi tu, yeye sio wa kwanza, wapo wengi hapa kijijini
wamefanikiwa kwa hilo.
‘Yeye akawa miongoni mwa waliofanikiwa, na alipopata
pesa,aliamua kwenda kuwekeza Dar, na alisema siku alipopata hizo pesa marafiki
zake wakawa wanamundama wakitaka kumpora hizo pesa, basi akawa anaishi kwa
mashaka kwa kujificha,…hakuwa na usalama. Na siku alipoamua kuondoka hapo
kijijini ndio siku mliokutana naye na mkaondoka kwa siri,…….
‘Kwasababu alikuwa akikuamini sana, hakuwa na shaka na wewe,
na uliweza kuona wapi alipokuwa kaweka peza zake, aliweka pesa hizo kwenye
mkoba ambao alikuwa habanduki nao mkononi, na mtu pekee aliyekuwa anajua kuwa
ana pesa ni wewe. Aliniambia kuwa mlipofika Dar, zile pesa zikawa hazionekani…na
aliniambia akiwa na uhakika akisema;
‘Ndugu yangu sio
rahisi mtu kuja kuzichukua hizo pesa, kwani nilikuwa nimezifunga vyema, kama
nguo, na kuziweka kwenye mkoba, na huyu mtu aliyefanya hivyo, atakuwa anafahamu
kuwa hapo niliweka pesa, na hakuna mwingine zaidi ya mke wangu…..’
‘Pesa zangu hizo
nimezipata kwa shida, ..na nikikumbuka hilo, akili yangu haikai vyema,
inanisikitisha sana, kwani ndio ulikuwa mtaji wangu wa maisha, na sasa
wamenifunga, sina maisha tena, …..pesa zangu zimeibiwa, sitaki hata kuishi…’ndivyo
alivyokuwa akiniambia akiw keshakata tamaa.
‘Kwa maneno haya unaweza kuona jinsi gani kuibiwa kwa hizo
pesa kulivyomtesa ndugu yangu, na ana uhakika mtu pekee ambaye angeliweza
kumuibia hizo pesa kwa jinsi alivyokuwa kazificha ni mke wake….’akasema na
kumgeukia hakimu, na huku akiendelea kusema;
‘ Ndio maana tunaamini kuwa pesa ulizojengea nyumba ni hizo
pesa ulizochukua kutoka kwa ndugu yangu…’akasema.
‘Mimi nilijua wasomi sio waongo, …..na sitakuamini tena
katika maisha yangu….’sina cha kuuliza tena muheshimiwa hakimu…’nikasema na
kuanza kulia, sikuwa na nguvu ya kuongea, sikuamini kuwa huyo mtu anaweza
kunifanyia hivyo nikarudi na kukaa.
**********
Hakimu alipouliza ushahidi kwa upande wao,wakawa nao, kila
kitu kikiwa kimejitosheleza kuthibitisha maelezo yake, hakimu alionekana
kuniangalia kwa mshaka sana, ndivyo nilivyokuwa nikiwaza hivyo, kuwa hata
hakimu aliniona mimi kama tapeli, basi baadaye hakimu alisema kuwa mimi
mshitakiwa anhitajika kuleta ushahidi na vithibitisho kwenye siku iliyopangwa
kusikilizwa tena hiyo kesi, na baada ya hapo, itasubiriwa siku ya hukumu
Siku hiyo,… kila mtu
pale ndani alioniona mimi kama tapeli fulani, hata sikuweza kuwaangali watu
machoni, maana wengi, nilihisi walikuwa wakiniangalia kwa jicho baya, na hisia
mbaya dhidi yangu, nikainama na kutoka nje, huku wakinifuatilia kwa akribu
wazazi wangu.
Tulipotoka nje ya mahakama, yule mwanasheria wa familia
akaja kuongea namimi, kwanza sikutaka hata kumwangalia, lakini baadaye niliona
sio ubinadamu, nikataka kujua anahitaji nini kutoka kwangu, nikamskiliza;
‘Shemeji usituone kuwa labda hatukupendi,….sisi tunakupenda
sana na hili tuliona lifanyike ili ujirizishe mwenyewe, kiukweli kama ulivyoona,
hukuwa na hoja ya kudai hiyo nyumba kuwa ni yako, na mimi niliongea wazi yale
aliyoniambia ndugu yangu, je unafikiria mimi ningelifanya nini kama ndugu yangu
kaniambia haya yote, nikae kimiya, ndio huenda ningelikaa kimiya kama
ungelitulia tukakubaliana. Lakini wewe hutaki, hutaki hata kunisikiliza….’akasema
‘Nyumba ni ya kwangu, duka ni la kwangu nimejenga kwa jasho
langu, kama mumeamua kunidhulumu, sawa,..lakini bado nitaendelea kuvipigania
hadi hatua ya mwisho…’nikamwambia.
‘Shameji kwanini unasema hivyo, …usijihangaishe kwa kupoteza
muda wako bure, kwa kukata rufaa, ujue ukishindwa huko mbele, kuna gharama
utahitajika kuzilipa, na pia kwanini tufike huko, mimi naona kwa vile umeshaona
uhakika wa jambo lenyewe lilivyo, tuongee tukubaliane……kwasababu huna ushahidi
wowote, ni nani atakuamini kwa hayo unayoyasema wakati huna hata kitu kimoja
cha kuthibitisha hivyo….shemeji achana nayo, tushirikiane tu,….’akasema
akiniangalia moja kwa moja usoni.
`Mhhh…’ halafu nikamnyaa, nikaangalai pembeni, huku nimeweka
mkono kiunoni, utafikiri nimeshashinda kesi, na yeye akawa bado ananiangalia,
halafu akasema;
‘ Shemeji mimi nakuhakikishia kama kweli ungelikuwa na kitu
cha kunishawishi kuwa hivyo vitu ni vyako, nisingelichukua hiyo hatua
niliyoichukua,…nilifanya hivyo baada ya kujirizisha, na kuona kuwa kweli hayo
aliyoniambia ndugu yangu yana ukweli…..sasa kama unayo ushahidi wowote, au kuna
njia yoyote ya kukuamini, kuwa hayo unayoyasema ni kweli, nionyeshe, mimi
mwenyewe nitahakikisha kuwa vyote hivyo vinaandikishwa kwa jina lako,
…’akaniambia.
‘Usitake kujitakasa hapa kwangu mnafiki mkbwa wewe, ….huna
lolote, mwongo mkubwa wewe, nyie ndio mnaotumia elimu yenu vibaya, umefanya
hivyo, kwa vile ulifahamu kuwa ushahidi niliokuwa nao, haupo tena…..mtu una
elimu yako badala ya kujitahidi upate vya jasho lako mnakimbilia mbali za
wenzenu,….hamtafanikia abadani’nikasema kwa hasira na kanza kuondoka.
‘Shameji tafadhali nisikilize kidogo, mimi nipo tayari
kukusaidia, na hata kama hiyo nyumba na duka utahitajia niandikishe kwa jina
lako ninaweza kuwashawishi ndugu zangu, tukafanya hivyo,lakini hilo sio rahisi
kihivyo, ….nikupe siri moja, ili ufanikiwe hilo kwanza unahitajika ukubali kuwa
mwanafamilia,…na ufuate kama alivyoagiza na ndugu yangu….mimi nipo tayari…..shemeji…’akasema
na niligeuka na kumwangalia kwa macho yaliyojaa hasira.
‘Hilo la kujizalilisha kwenu,…ndivyo mnavyotaka,…?’
nikamuuliza, lakini sikumpa nafasi ya kutoa jibu nikasema;
‘Hata siku moja sitafanya hivyo…..kama ndio lengo lenu,
mumenoa, tutapambana huko huko mahakamani…..’nikasema na yeye akaniangalia huku
akitabasamu, hakuonyesha wasiwasi, ….alikuwa akijiamini kupita maelezo, na mimi
nikageuka na kuondoka zangu
Tulipofika nyumbani, wazazi wangu wakaniuliza tufanyeje,
kwani ilivyo, japokuwa hukumu bado,lakini inaonyesha wazo kuwa kesi
tumeshindwa, kwahiyo tutafute jinsi gani ya kufanya…..na hapo nikawaambia, kama
tutashindwa hapo inabidi tukate rufaa, kwasababu ninachodai ni haki yangu…
‘Hata kama tukikata rufaa, tutapatia wapi huo ushahidi, ….huoni
kuwa huko tutakwenda kupoteza muda bure, na tutahitajika kulipa gharama?’
Akauliza mama.
‘Inabidi kwanza kuhangaike kutafuta huo ushahidi, kama kuna
nyaraka zozote, …na kama tunaweza kumtumia mtu akajaribu kuzitafuta hizo
nyaraka kwenye hiyo familia, nahisi kama waliiziba wao, na huenda ni huyo wifi
yako, mliyekuwa mkiishi naye …’akasema baba.
‘Sina uhakika sana na hilo, nahisi waliziiba kipindi hicho
nilipokuwa kwenye msiba, lakini wote hawo lao moja, hata huyu mchumba wa huyo
mwanasheria wao, simuamini, na yeye alifika hapa jana, akajifanya kuwa anataka
kunisaidia, nahisi hawa watu wanakuja kwa lengo la kupata taarifa, mwisho wa
siku wanatuangamiza….’nikasema.
‘Cha mhumi ni kukata kabisa mguu nao kwa kutokuwa na
mawasiliano nao, kama wakija ni wageni wakaribishe lakini chunga ulimi wako,
usiwe na maongezi yanayohusiana nah ii kesi, na kama ikiwezekana usiwakaribishe
ndani, achana nao kabisa….wote lao ni moja..’akasema mama.
‘Mimi nina wazo jingine, unajua kuna usemi usemao, adui yako
mpende, …usemi huu una hekima kubwa sana, sisi hawa tuwe nao pamoja, na hao hao
ndio tutawatumia kupata taarifa. Na nina wazo ambalo sijui kama binti yangu
utakubaliana nalo…’akasema na kuniangalia kwa mashaka.
‘Wazo gani?’ nikamuuliza.
‘Huyo mwanasheria wao, anaonyesha kabisa kuwa amekupenda,
sasa unaweza kumtumia huyo huyo ukayamaliza haya yote, kwa njia kubwa mbili,
kwanza kwa kukubali kweli yeye akurithi uwe mume wake, na hapo utakuwa
umekipata kila kitu…ni akili kichwani mwako, lakini pia kuna njia ya pili,
ambapo unaweza kujifanya wewe ni mpenzi wake, na ukaweza kumshawishi hadi akabadili
hati za nyumba na duka….sikufundishi vibaya mwanangu, lakini hizo njia pia
zinaweza kutumika, kwa wakati kama huu ambapo, tupo vitani….au wenzangu
mnasemaje?’ akasema baba.
‘Baba….hapana, mimi njia zote hizo kwangu zisiziafiki maana ni za kuhadaa, ….kwanza
baba mimi sipendi kuolewa kwenye hiyo familia tena, kama ni lazima ifanyika
hivyo, na baba moyo wangu hautaki tena kuolewa, kabisaa…nataka niishi na
mwanangu tu……hata hivyo, mimi ninachodai ni haki yangu , na ninataka haki yangu
niipate kwa halali, sio kwa mbinu za kuhadaa….’nikasema.
‘Mimi kihalali nakubalina na hiyo hali, kihalali,…akini kwa
hali kama hii, najiuliza kwa vipi, maana mahamani wanahitaji ushahidi, ..na
sisi hatuna aina yoyote ya ushahidi, wala amshahidi ambao ni muhumi…na tunavyohisi
ni kuwa ushahidi upo kwa hawo hawo maadui zetu….’akasema baba.
‘Mwanangu,…wakati mwingine unahitajika kutumia mbinu za
kiujanja kama hizo, …mimi siwezi kuiona ni hadaa, ni medali za kivita,…ilimradi
tu, usiwe na nia mbaya…vinginevyo, basi tena mwanangu sisi wazazi wako tupo, na
sasa tupo tayari kuishi na wewe bila shaka…’akasema baba na kabla hajamaliza
mlango ukagongwa na hodi ikasikika.
Ilikuwa ni sauti ya kike, …ya yule mchumba wa wakili…
NB: Je itakuwaje? Ndio hivyo, …..tunajikongoja, ipo siku
tutaweza….wengi wananishauri nikamilishe vitabu,….mambo magumu! Hata hivyo tupo
pamoja,
WAZO LA LEO: Hivi
ni lazima kudanganya ili kupata haki yako, haki ni haki haipatikani kwa ujanja,
kwa kufanya hivyo ni sawa na kufua shati jeupe kwa maji machafu.
Ni mimi:
emu-three
5 comments :
lol! kaz kweli kweli! haya ngoja tuone itakuwaje il akweli haki haipatikani kwa ujanja ujanja lazima kuwa straigth!
kisa kinakolea na kusisimua safi sana...nasubiri
Hello! I could have sworn I've been to this blog before but after looking at many of the articles I realized it's
new to me. Regardless, I'm certainly delighted I found it and I'll be book-marking it and checking back often!
my blog post ... how much is an e cig
Thanks designed for sharing such a fastidious idea, article is pleasant,
thats why i have read it entirely
My web-site :: electronic cigarrettes
fantastic put up, very informative. I ponder why the other experts of this sector don't realize this. You must continue your writing. I am confident, you've a great readers' base already!
Look at my page e cig brands
Post a Comment