‘Siku ya kwanza ilikuwa ngumu kwetu mwanangu, maana ilibidi
tutafute sehemu ya kujibanza, ili angalau tupate usingizi, mbu, wakawa wageni
wetu, baridi lilikuwa kali kweli …ukumbuke mimi ndio nilitoka kujifungua
kwahiyo bado nilikuwa na maumivu ya kujifungua.
Kama nilivyokuambia kuwa yule mtu niliyekuwa naye alikuwa
kava kofia pana, na mawani makubwa na alikuwa na mandevu mengi, kwahiyo
sikuweza kumgundua haraka kuwa ni nani, …lakini yeye nilihisi kuwa
alishanigundua hasa pale tulipoanza kuongea;
‘Unasema umejifungua mtoto,…mtoto gani ?’ akaniuliza.
‘Mtoto mwanaume….’nikamwambia.
‘Baba yake ni nani?’ akaniuliza huku akionyesha kuwa makini sana, lakini alikuwa haniangilii moja kwa moja, kama vile anaona aibu kuniangalia machoni.
‘Baba yake kamkataa, kasema hiyo mimba siyo yake…kwahiyo
…ndivyo ilivyokuwa,…’sikutaka kumuelezea zaidi, lakini alizidi kunidadisi
‘Unahisi ni kwanini aliikataa hiyo mimba ?’ akauliza.
‘Sijui,..labda aliogopa kuwajibika, maana mimi simjui
mwanaume yoyote zaidi yak wake yeye, na mungu wangu ni sahidi..’nikasema.
‘Oh, lakini kila mtu anapenda kusema hivyo, hata mwizi
akikamatwa, anaapa na kuapa kuwa mungu wak ni shahidi, huenda anahisi una
mahusiano na mtu mwingine..’akasema.
‘Hiyo ni shauri lake, ahisi anavyotaka yeye, lakini mimi
nina uhakika huo, kwasababu sikuwahi kuwa na mwanaume mwingine zaidi yake, yeye
ndiye aliyenifundisha hayo yote, sikuwa nayajua…’akasema mama
‘Sasa ukikutana naye tena utasemaje, …?’ akaniuliza.
‘Sina haja naye tena, …tatizo ni kuwa, nimemtelekeza
mwanangu,…sasa sijui itakuwaje?’ mama akaanza kulia.
‘Huo ni uzembe wako….utaondakaje umuache mtoto mchanga peke
yake, …sijawahi kusikia mama aliyejifungua karibuni akimuacha mtoto wake, wewe
ndio wa kwanza…..huna huruma na kichanga, hapana, lawama zote zitakushukia
wewe…’akasema huyo mwaname akionyesha kinilaumu kupita kiasi.
‘Sasa ndio unanilaumu mimi, ..isingelikuwa kuahangaika
kukuokoa wewe, nisingelifikwa na haya yote…lakini kweli ni kosa langu, sijui
kilisnishiak kitu gani, hadi nikaondoka pale, na kumuacha mwanangu,
…nitajilaumu sana, kama mwanangu atazurika kwa lolote lile..’akasema.
‘Nasikia mwanamke akijifungua anatakiwa kukandwa na maji ya
moto, sasa ni nani atakukanda?’ nikashangaa akiniuliza hivyo.
‘Sijui, na wala sijali tena…mimi hapa nilipo nataka nipate
nauli nirudi huko nilipomuacha mwanangu..’nikamwambia huyo jamaa.
‘Sawa ngoja kupambazuke tuone kazi gani tunaweza kuifanya
ili tupate nauli…’akasema. Hata hivyo nauli haikupatikana kirahisi hivyo, wiki
ikapita, mwezi ukaingia, na miezi ikawa inahesabika.
‘Ina maana hukuweza kumgundua kuwa ni nani?’ nikamuuliza
mama
********
‘Kila nilichokiona ni cha ajabu ni kwa huyu mwanaume ,
alikuwa akijaribu sana kutokuwa karibu na mimi au kuniangalia machoni;
‘Mbona unaonekana kunikwepa,….nakuona kama unaniogopa vile?’
nikamuuliza.
‘Sio hivyo, wewe umetoka kujifungua karibuni, na tunaishi
pamoja, lililo jema, ni kuhakikisha naishi na wewe kama vile inavyotakiwa,
tusije tukaingie kwenye mahusiano mengine…ilihali hatujakubaliana na hilo….’akasema
na mimi nikaona lina msingi, na nikakubaliana naye.
‘Lakini hata hivyo, hayo madevu yako huoni kuwa yanatisha,….hata
sura haijulini vyema, kwanini huyanyoi, au kuyaounguza, ….na hiyo miwani, mbona
ni ya jua, sijawahi kukuona ukiiondoa machoni, nahisi kuna jambo ndani yake….’nikamwambia.
‘Hapana sitaki kunyoa hiz ndevu kwasababu….mwenyewe unafahamu
kuwa ninatafutwa na polisi, sipendi kabisa wanifahamu mimi ni nani, huwezi
kujua, hawa watu wanaweza wakawa wametumwa huku……najua kabisa nikinyoa hizi
ndevu, polisi wakiniona watanitambua, ….’akasema, lakini nikamsisitiza kuwa
angalau ayapunguze, maana yalikuwa mengi sana, kiasi kwamba yalikuwa yakimziba
hata mdomo.
Kwa kumuonyesha kuwa nilikuwa nalifuatilia hilo, nikanunua
mashine ya kunyolea na wembe wake,…yeye akasema kwa wasiwasi
‘Nitayapunguza mwenyewe….’akasema, na kweli siku hiyo
akapunguza hizo ndevu kidogo, kiasi kwamba sura yake ilikuwa vile vile ya
kificho. Mimi akilini mwangu nilijua kabisa anafanya hivyo kwa ajili ya
kujilinda, ili asitambulikane, kwahiyo sikupenda kumshawishi zaidi, japokuwa
nilikuwa siyapendi yale madevu yake…alikuwa anatisha.
Siku moja alikunywa pombe akalewa sana,…na huwa akilewa
hivyo, anaishia kulala fofofo, …. mimi nikaona hapo ndio sehemu ya kumpatia…nitampunuza
hizo ndevu, angalau kidogo, , …nilipohakikisha kuwa kalala, nikachukua ile
mashine na kuanza kumnyoa kwasababu ya haraka haraka, na kwa vile nilifanya
hivyo kwa haraka bila kuwa na mpangilia maalumu, nikajikuta nimemnyoa vibaya,
sehemu nyingine ndevu zikawa zimekwesha kabisa,….ilikuwa kama mtu
aliyenyofolewa.
Alipoamuka asubuhi na kujiona alivyokuwa kanyofolewa ndevu
zake, na kuonekana kioja, ikabidi achukue ile mashine na kujinyoa mwenyewe
vizuri zaidi huku akilaani kweli kweli...
‘Hivi ni nani kanifanya hivyo, ni wewe tu najua umenifanya
hivi kwanini umenifanya hivi, ina maana hukunielewa, sasa itabisi niwe makini
zaidi,….sijui nitafanya nini wakiniona hawa maaskari’ akawa analaalmika kwa hasira.
‘Wewe hukumbuki ulipogombana na yule mtu, ….akakupiga na
kukuzidi nguvu, alichukua sijui chupa ile, na akawa anakukwangua nayo kwenye
midevu yako….…’nikamdanganya.
‘Sio kweli….ni wewe umenifanya hivi, na ole wake polisi
wanikamate, tutaenda wote jela…’akasema huku akimaliza kujinyoa, na alipogeuka
kuniangalia, , nikajikuta nikipigwa na bumbuwazi. Yeye akageuka kwa haraka na
kuchukua mawani yake ni kuivaa, lakini alikuwa kachelewa.
‘Hivi kumbe ni wewe…’nikamwambia.
‘Ndio ni mimi kwani nimekuwa nani tena, ….’akasema huku
akitaka kuondoka.
‘Yaani kujificha kwako kote no kudai kuwa unajificha na
polisi…kumbe ni wewe…oh..’nikajikuta nikisema huku mwili mzima ukinisisimuka
kwa hasira.
‘Oh kwani vipi….nimebadilika ehe, nimekuwa kijana….mrembo au
sio…?’ akageuka na kuniangalia huku
akicheka….akiwa na mawani yake usoni, sijui ni kweli kuwa hakufahamu nina maana
gani kumwambia vile.
Yeye , akageuka kwa haraka na kwenda mezani kulipokuwa na
karanga na kuanza kazi ya kufungwa karanga kwenye vimfuko, kwa ajili ya kwenda
kuuza, huo ulikuwa ni mmoja wa miradi yetu tuliokuwa tukiufanya.
‘Una urembo gani wewe, mnyama mkubwa wewe…mzandiki, msaliti
mkubwa wewe….’nikasema kwa hasira na hapo, akageuka na kuniangalia aliposikia
sauti yangu ya hasira na matusi ambayo hakuyatarajia kutoka kwangu.
‘Kwanini unanitukana?’ akaniuliza huku akiendelea kufunga
karanga. Kwa maisha tuliyokuwa tukiishi lugha kama hizo zilikuwa ni kitu cha
kawaida, nay eye alishazoea hizo lugha hiyo japokuwa mwanzoni alikuwa
akigombana na watu karibu kila siku…, kwani akatika kuhangaika kwetu, tulikuwa
tukikutana na matusi ya kila aina, kwahiyo matusi na kejeli ilikuwa sehemu ya maisha
yetu, tulijuja tukazoea. Naona pale aliposikia nkiyaporomsha matusi, alijifanya
hakujali, …..
‘Leo umegauka kuwa hao wauza unga,…ambao kila siku
wanajifunzia matusi kwangu,…mimi sasa sijali, waache watukane wanavyotaka,
lakini najua ni nini ninachokifanya…, mimi sijali, hayo ndio maisha yetu,
walalahoi, kinachonishanga ni kutukanwa na mtu ninayemthamini kama wewe…nimekukosea
nini mpenzi…’akasema.
‘Ningelikuwa mpenzi wako usingelinitelekeza kipindi kile…..,
na kunisusia uja ujazito na kudai kuwa mimba sio ya kwako…’nikamwambia na hapo
akajikuta akidondosha kile kimfuko cha karanga alichokuwa kakishika mkononi na
kunikodolea macho.
‘Oh, ina maana umeshanigundua….sasa nimekwisha, ….maana kama
wewe umenigundua, hao polisi nitawakwepaje….umeshaniweka ndani wewe….’akasema
akinigeukia huku akiwa kashika kidevu chake na kuivaa miwani yake haraka.
‘Ningeligundua kuwa ni wewe nisingelikuokoa kwenye ule mto ,
ningelikuachia ukafa na maji,…una bahati sana wewe, lakini hata hivyoo siwezi
kukusamehe kamwe kwa hayo uliyonitendea…kamwe sitaweza kukusamehe….’akasema mama
akinihadithia kisa cha maisha yake na huyo mwanaume.
‘Mimi nina uhakika umeshanisamehe,….. na ninashukuru kuwa
tumekutana tena, na mungu akijalia tutaishi pamoja kama mke na mume….hiyo ndio
ahadi yangu toka siku nyingi…..’akasema na kuniacha nibakie mdomo wazi,sikuamini
maneno yake, niliona ni kwa vile nimemfanyia mambo makubwa ambayo yalistahili
kutendewa watu wema, lakini sio mtu kama yeye…tulitulia kwa muda kila mmoja
akijifanya yuko bize na kufunga
karanga.
‘Mama nanihii, natumai umenisamehe au sio…?’ akauliza, tangu
siku alipogundua kuwa nina mtoto alikuwa kazoea kuniita hivyo; mama nanihii.
‘Kwa hayo uliyonitendea, siwezi kamwe kukusamehe, …..hakuna
ambaye angeliweza kukusamehe kwa ujeuri na unyama kama ule,…..wewe sio mtu wa
kusamehewa, ulichonifanyia ni unyama uliopitiliza….huoni kuwa wewe umekuwa
chanzo cha kuharibika maisha yangu, na sasa wewe umekuwa chanzo cha kunifanya
nimtelekeze mwanangu..’akasema akionyesha hasira usoni.
‘Nina uhakika mtoto yupo salama huko alipo….na nina uhakika
kuwa tutarudi tutamkuta akiwa salama….hilo nakuhakikishia, na nitafurahi sana
nikimuona mtoto wangu…ahsante sana kwa wema wako na kuvumilia mengi….’akasema
na kuinuka, akajinyosha huku akiwa kashika kiuno, alionekana kuchoka maana
alikuwa akifanya kazi nyingi za nguvu.
‘Sasa hivi unamuita mtoto wako,..hahahaha, eti nikimuona mtoto wangu….kweli nyie
wanaume mna visa, …wakati nina mimba ulinikana, sasa una uhakika mtoto yupo, na
unajua analelewa na watu wengine, huna majukumu naye,….unajigamba, ….`mtoto
wangu’….huna mtoto wewe, mtoto ni wa huyo unayemjua kuwa alinipa ule uja uzito…sio
wa kwako wewe umeshasahau kunifukuza na panga…eehe’mama akasema kwa hasira.
Yule mwanaume, kuona vile, akageuka na kusogea pembeni,
akachukua mfuko aliokuwa kaweka nguo zake na kutafuta kitu, baadaye akatoa
kiboksi, akakifungua, kilikuwa kiboksi kizuri, …kiboksi kidogo, akanisogelea na
kukifungua, na ndani yake kulikuwa na pete nzuri sana.
Akanisogelea hadi tukawa tumeangalia machoni, halafu akapiga
magoti, na huku amekifungua kile kiboski, akainua kichwa na kuniangalai
machoni, akasema;
‘Mama nanihii, naomba unikubalie ombi langu, nataka uwe mke
wangu…wa hii shida tunayoipata kwasasa na raha tutakayokuja kuipata baadaye
nina uhakika kuwa raha ipo mbele yetu,….’akasema huku akiniangalia kwa macho ya
huruma. Sikumjibu kitu, macho yangu yalikuwa kwenye ile pete, ilikuwa nzuri ya
bei mbaya, sikujua wapi alipoipatia….
‘Najua nilikukosea sana…….na nikuambie ukweli, siku ile
ulipoondoka pale, niliingiwa na huzuni kubwa sana, nilijuta sana kwa tendo
lile, nikawa ninalia kila siku ya mungu,….na nikuambie ukweli, kuwa kila siku,
kutoka siku ile. Nilikuwa nikikutafuta kila kona..na nikawa nalewa kupita
kiasi, kila nikikumbuka….na hata nilipopata zile pesa cha kwanza nilichofanya
ni kwenda kununua hii pete ya bei mbaya, kwa ajili yako….’akasema.
‘Siwezi kuamini hayo maneno yako’mama akamwambia huku
akigeuka pembeni kutaka kuondoka, lakini miguu ilikuwa minzito, akajikuta
amesimama pale pale, huku akiwa kageuka upande kuangalia sehemu nyingine.
‘Siku tukirudi jaribu kuulizia watu
wanaonofahamu,….watakuambia kila kitu, jinsi gani nilivyokuwa nikikuulizia,nikikutafuta
kila kona, amini hayo ninayokuambia …….nilifika hadi kwenu kukuulizia, kama
unabisha waulizie wazazi wako…...na cha ajabu nilimkuta mama yako akisikitika
sana…na yeye alikuwa akikutafuta…ilikuwa ni hasira tu waliyokuwa nayo hawakuwa
na dhamira ya kukufukuza moja kwa moja….’akasema.
‘Walinikataa wenyewe…kama walikuwa na dhamira hiyo au la….mimi
sijui…, ila lawama zangu hadi mwisho ni kwako wewe….kwenu nyie wanaume
mnaopenda kuwahadaa wanawake na mwisho wa siku mnakimbilia kuwatelekeza…eti
hamjui hio mimba, wakati kabisa, ulikuja kupanda mbegu kwangu….hiyo ni laana….’nikamwambia
huyo mwanaume.
‘Pole sana….kwangu mimi nakiri kosa, na ninaomba msamhana
nipo chini ya miguu yako, ila kwa wazazi wako,….ilikuwa ni wajibu wao
kukasirika, ….na kosa ni la kwangu mimi..nitajitahidi sana kwenda kuwaomba
msamaha….’akasema huyu mwanaume akionyesha kujuta kiukweli..
‘Wazazi wangu, wanalawama….wangelinipa muda, niweze
kuwaelezea vyema, maana ilibidi nifanye hivyo, kwani nilikuwa sijaongea na wewe….wao
walikimbilia kunifukuza….sasa sioni kwanini wahangaike kunitafuta tena….shauri
lao..na hata wewe ulinikataa, sasa kwa vile umesikia nina mtoto, na mtoto
mwenyewe mwanaume, unajifanya sasa unanipenda,…sizani kama nitaweza kulisahau
hilo…’akasema mama.
‘Najua hilo…lakini nakupenda sana mama Nanihii..nisamehe, na
pokea hii pete yangu ya uchumba, na ukitaka kesho tunakwenda kufunga
ndoa,….’akasema na mama akamgeukia huku akimwangalia kwa mashangao, hakuamini
hilo….
Nilifikiria sana na niliona hakuna jinsi, kwani hata hivyo,
nilikuwa nampenda sana huyo mwanaume, na siku aliponikataa, niliumia sana, na
moyoni nilikuwa nimeapa kutokuwa na mahusiano na mwanaume mwingine yoyote….
Na kweli kesho yake tukaenda kufunga ndoa,…..’akasema mama
huku akionyesha uso wa furaha…lakini baadaye ile furaha ikayeyuka na
kubadilisha sura yake na kuwa ya huzuni.
‘Tulipotoka kufunga ndoa ….tukawa tupo mitaani tumeshikana
mikono kwa raha zetu…tulijihisi tupo duniani nyingine, dunia ya wependanao,…..hatukujua,
kumbe kulikuwa na watu wanatufuatilia kwa nyuma, hatukujua hilo kabisa..na
mwenzangu alishajisahau.., mara hawo watu wakatupita, na walipokuwa mbele yetu,
wakatugeukia, na kipindi hicho jamaa yangu alishajisahau na kuvua miwani yake.
Wale watu wakasimama mbele yetu na mmoja akatoa kitambulisho
na kujitambulisha kuwa wao ni askari kanzu.
‘Mnataka nini ….?’ Akauliza mwenzangu akionyesha wasiwasi
‘Wewe ndiye Mtumwa…au sio?’ akauliza huyo askari, na kabla
mume wangu hajajibu kitu mwingine akatoa pingu,..
‘Ndiye yeye mkuu…..tulirejeshe home, rikajibu mashitaka…’akasema huyo askari mwingine na wakaanza
kumpiga mume wangu pale alipokataa kutii amri, na baadaye likaja gari aina ya
landrover, wakambeba mume wangu juu kwa juu ….na kumuingiza kwenye hilo gari, wakaondoka
naye.
Nilijaribu kufuatilia wapi walipompeleka, lakini kwa siku
hiyo sikufanikiwa na kesho yake, nikaenda kituo ambacho nilihisi kitaweza kuwa
na taarifa naye, kama walivyoniahidi, na hapo wakanimbia kuwa mume wangu
karudishwa huko nyumbani, kwenda kujibu mashitaka ya wizi, wa mamilioni ya
pesa.
‘Nikabakia peke yangu……’ akasema mama akionyesha masikitiko.
NB: Haya ndio hivyo, kwa shida tutafika….
WAZO LA LEO:
Linapotokea jambo hasa la misiba, au majanga, ajali nk, ambalo ni la
kusikitisha, kwanza tuliweke mikononi mwa muumba, kuwa yeye ndiye mweza wa
yote, na pili, tusikimbilie kunyosheana vidole, kabla hatujakuwa na ushahidi wa
chanzo cha janga hilo. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tunaonyesha hisia zetu,
zilizojificha…na kumbe huenda hata huyo tunayemnyoshea kidole hahusiki. Chuki
ni tabia ya ibilisi.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Very nice post. I simply stumbled upon your weblog and wanted to say that I've truly enjoyed surfing around your weblog posts. In any case I will be subscribing in your rss feed and I am hoping you write once more very soon!
Here is my website ... home Loans fresno
Post a Comment