Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, May 16, 2013

WEMA HAUOZI-8



Siku hiyo niliamua kwenda kuitembelea iliyokuwa nyumba ya huyo mtaalamu, ilikuwa imeteketea yote kwa moto, na hakikubakia hata  kitu kimoja, …yalikuwa ni majivu matupu yaliyokuwa yamebakia. Na kwa vile nyumba za kijijini nyingi zilijengwa kwa miti, zikakandikwa kwa udongo na kuezekwa kwa makuti, moto ukishika, inaungua haraka sana.

Siku zilizofuata kukawa kunanyesha mvua, nilipopita pale siku nyingine niliona yale majivu yote yamegendamana kwenye ardhi kama vile kumpigwa sakafu ya udongo ulaya…na baada ya siku tatu, majani yakaanza kuota kuzunguka lile eneo. Ilikuwa ajabu kabisa, maana pale kati kati, palibakia hivyo hivyo bila kuota majani, huku pembeni yake majani na miti vikiota kwa kasi ya ajabu.

Wiki kadhaa zikapita, na watu walianza kulalamika kuwa wakipita eneo hilo, wanasikia kama sauti za watu wakiongea na kukipiga ukulele, au kunatoka sauti zisizofahamika vyema.

‘Hiyo ni mizmu ya huyo mtalaamu, nini ….?’watu wakawa wanaulizana

‘Kama ni mizumu yake, je haitaweza kutuathiri na sisi?’ mmoja akauliza

‘Inabidi tuwaone wazee wanaojua mambo hayo, maana eneo hili sasa halipitiki…mimi mwenyewe nilipia jioni jioni nikasikia kama watu wanaongea, na vyombo vikigongana, na mara nikasikia kama sauti ya kilio cha mtoto mdogo…’akasema jamaa mmoja, na watu wakamwangalia wakiwa na wasiwasi.

‘Kama ni hivyo, kuna jambo….ni heri tuhangaike, kwanza ni bora tuwaone wazee wa hapa kijijini,….’wengine wakashauri hivyo, na wengine wakapuuzia, na kweli baadhi yao, waliwaendea wazee na kuomba ushauri, na wazee walipoulizwa, walisema bila kuficha;

‘Inaonekana huyu mwenzetu alikuwa na mambo mengine ambayo sio ya kawaida. Tunakubali kuwa alipewa karama ya utibabu, lakini yeye alichanganya hayo na mambo mengine yasiyo ya halali, na hayo mnayoyasikias ni mambo yake mabaya….’akasema mzee mmoja.

‘Na yanahitajika kuondolewa haraka eneo hilo kwani lipo kwenye himaya za makazi yetu, mmiliki wake hayupo, ni nani wa kuyadhibiti hayo madude, hatujui yanakula nini, au yanafanywaje ili yasihangaike kwenye makazi ya watu wengine au kusambaa kwenye njia tunazopita…’akasema mzee mwingine.

‘Na kama ni madude,…., yanaweza yakawakumba watu na kuleta athari…na nahisi huenda kuna jambo linaweza kutokea kama hatutafanya juhudi za haraka..’akasema mzee mwingine

‘Sasa wazee wetu tufanyeje?’ akaulizwa.

‘Inabidi watu wafunge safari kwenda huko milimani na kuwapata watu wanajua mambo hayo….kwa hapa kwetu mtu tuliyekuwa tukimtegemea ndio huyo mtaalamu, sasa keshaondoka. …’akasema mzee.

‘Na ninavyo mimi kaondoka kwa mabaya, tofauti na enzi zetu, kwani mtu kama huyo alitakiwa kuwa muadilifu,… lakini mlimuonaje maisha yake yalivyokuwa,…yeye tamaa ilimzidi akakiuka masharti ya kazi kama hiyo…’akasema mzee mwingine.

‘Mimi niliwahi kumkanya, …lakini aliniona mbaya, tukawa hatusalimiani,…na ilionekana wazi kuwa mambo yake mengine alikuwa akifanya kwa maslahi yake, …sio wote aliokuwa akisema ni wachawi,walikuwa ni wachawi, wengine aliwasingizia pale alipoona wanaingilia maslahi yake….sasa hatuju ni kwanini hili limetokea, lakini nahisi ni mabaya yake ndiyo yaliyomuangamizai…’akasema huyo mzee.

Watu wakaanza kutishika , na kuogopa kabisa kupita eneo hilo, wakijua wanaweza kukumbwa na hayo waliyokuja kujua kuwa ni mashetani ya huyo mzee. Wazee nao wakahangaika hadi kwenda huko milimani, na waliporejea walisema hawakuweza kufanikiwa, kwani inavyoonesha ni kuwa walishachelewa, iliyobakia ni kusubiria tu.

‘Cha muhimu eneo hilo litengwe kabisa….’akashauri huyo mzee, na kweli eneo hilo likawa nje ya mipaka ya wanakijiji, ndio maana hadi leo unaliona hilo eneo likiwa limebakia msitu, na ukiingia ndani ya huo msitu, kuna sehemu ipo pakavu kabisa…..ndio asili ya jina hilo la mzimuni….’babu yake akasema.

********

Niliendelea kukumbuka yale aliyoniahdithia babu, ambayo mengine mama hakuweza kunihadithia a, huenda aliogopa kunisimulia, nisije nikatishika, ….nikakumbuka jinsi babu alivyosema siku ile alipokuwa akinihadithia;

‘Mimi nikarejea nyumbani kwa mama yako nikisubiria nyumba yangu ijengwe, na ndoto zile mbaya za kutisha zikawa zimepotea kabisa,…hata hivyo sikuweza kuwa na amani, bado nilikuwa nikimuwaza mke wangu, na jinsi gani ya kuwapata hawo waliomfanyia hivyo.

Kulianza kutokea maajabu hapo kijijini, kila siku kulizuka jambo la kustaajabisha, na mambo hayo yalionekana kufanana. Vijana walianza kufa ovyo, na vifo vyao, kama nilivyosema awali, vilikuwa vya aina moja…nikajua ubaya umeanza kulipizwa….

‘Hawa inasadikiwa ndio waliokuwa vijana wa mtaalamu, hawa ndio huyo mtalaamu alikuwa akiwatuma kufanya mauaji kwa wale wanaosadakiwa kuwa ni wachawi…na kufuatilia mambo yake.’watu wakawa wanasema.

Hawo vijana, mmoja mmoja akawa anashikwa na kitu kama mshituko, halafu anakuwa kama kachanganyika, au kupandisha mashetani, na kuanza kukimbia ovyo. Alipoanza wa kwanza, watu walizania huenda ni hayo mabangi wanayopenda kutumia vijana, lakini alipofuatia wa pili , watatu , wanne, na wote wanajulikana ni nani, watu wakahisi kuna jambo.

Na cha ajbu zaidi wote walitaabika na hali hiyo ya kuchanganyikiwa, na mwisho wake wanakutwa wamekufa eneo hilo hilo la huyo mtaalamu, mmoja baada ya mwingine. Na siku ya kwanza ya kufariki kwa kijana huyo, ndugu na jamaa wakafika kumtoa pale alipofarikia, na kumpeka nyumbani kwako, lakini ikashindikana, kwani watu walijikuta wakizungukwa na nyuki wengi.

‘Chomeni moto , hawo nyuki wataondoka,…..’mmoja akasema, lakini hakuna aliyeweza kusogea pale, na kila ukiletwa hapo karibu, unazimika.

‘Hili sio la kawaida, inabidi tukawaulize wazee….’mmoja, akasema na wakafuatilia, huko kwa wazee wanajua mambo hayo.

‘Huyo mzikeni eneo hilo hilo,…’akashauri huyo mzee, Na kweli walipoanza kuchimba makaburi, wale nyuki wakawa wanazunguka hewani, hadi walipomaliza kumzika, na nyuki wale wakaanza kuwashambulia, kuashiriwa kuwa waondoke haraka, …

Haikupita siku mbili, hali kama ile ikamtokea kijana mwingine, na yaliyotokea kwa mwenzake ilikuwa hivyo hivyo, na huyo naye wakamzika eneo hilo hilo.

‘Wazee wetu sasa hili ni balaa gani maana vijana wetu wanamalizika…..?’ wakina mama wakauliza.

‘Haya matukio yanaoenekana ni dhuluma ilietendwa na hawo vijana, na inavyoonekana, hawa vijana walikuwa wafuasi wa huyo mtaalamu, kwahiyo waliotendewa hizo dhuluma, walilalamika, na huenda wengine walikwenda kuomboleza kuwa hawow aliofanya hivyo mabaya yawakute….’wakasema hawo wazee.

‘Sasa tufanyeje, maana hali kama hii hatujawahi kukutana nayo?’ wakauliza.

‘Kwanza ni hawo wanahusika kukubali makosa yao, na kwenda kutubu hayo makosa yao kwa hawo waliodhulumiwa, swali kubwa hapa ni je wanajua makosa yao, na hawo waliotendewa hivyo bado wapo hai, kama hawapo hai, ….hatuna la kufanya’wakasema hawo wazee.

‘Oh, sasa tutafanyeje….?’ Wakina mama wenye vijana ambao wanafahamu kuwa vijana wao walikuwa na mafungamano na huyo mtaalamu wakaanza kulalamika na kuhaha huku na kule kutafuta jinsi gani ya kuweza kulikwepa hilo janga.

‘Ubaya unapotendwa, watu wanajionea ni kawaida, na hujiona kama wao ni washindi , lakini unashindwa kufahamu kuwa tunaowatendea huo ubaya ni binadamu kama sisi….wanaumia, na kujiskia uchungu kama sisi, basi dhuluma hiyo haitaisha hivi hivi, mpaka na nyie msikie uchungu kama wao walivyosikia….’akasema huyo mzee.

‘Lakini sisi tulikuwa hatujui,….tulikuwa tukimfuata huyo mtaalamu, kama unavyojua kuwa yeye watu wote walikuwa wakimuamini kwa kila anachoongea….’wakasema hawo watu.

‘Sasa kama mlikuwa mkimwamni kwa kila kitu,….mkasahau kuwa kuna mungu, inabidi mumtafute huyo mtaalamu, …..hakuna la kufanya kwa sasa…’wakasema hawo wazee.

‘Hatuwezii kwenda huko milima kwa watu wema wakatusaidia?’ wakauliza.

‘Wema wao sio wa kudaidia wadhalimu, kwani wakisaidia wadhalimu na wao watakuwa kama wamedhulumu, …hebu fikiria unapomsaidia mwenye makosa, ni nini hukumu yake kisheria,…ni kuwa na wewe unashitakiwa kama msaidizi wa mtenda makosa…’akasema huyo mzee.

‘Wazee tunaomba msaada wenu, nyie ndio wazee wetu, na huenda mambo kama haya yaliwahi kutoeka huko nyuma, je ilipotokea hivi mlifanya nini..?’ wakauliza.

‘Kuna mambo ya kimila yalifanyika, kuna matambiko,….lakini bado kulikuwa na jukumu la kujua kosa na nani waliofanya hivyo, na kwa nani….enzi zetu, watu walikuwa wakweli, kama walitenda kosa, walikiri, na wakatubu makosa hayo kwa waliotendewa…je nyie mnaweza kufanya hivyo?’ akauliza

‘Sisi wazazi tunaweza kufanya hivyo kwa niaba ya watoto wetu..’wakasema hawo wazazi.

‘Hapana, makosa kama hayo yanatakiwa mtu mwenyewe akutubu, …na asichelewe kabla adhabu haijaanza..hivi sasa naona kama mumeshachelewa…..’akasema huyo mzee, na mara sauti ya ukulele unaoashiria masiba, ukasikika kule kule eneo la mzimuni, …

 ‘Je ndio kisasi kimeanza, na ni mbinu gani watatumia, ili kuondokana na janga hilo..?

*****

Mume wangu alianza kuzidiwa, kifua kile hakikutaka kupona, na ikafikia hadi kurudishwa hospitalini na kulazwa, lakini hali yake haikuweza kutengamaa, na ikafikia muda wakashauri arejeshwe nyumbani tu, na hapo tukajua kuwa madakitari wameona uwezekano wake wa kupona haupo tena.

Tukahangaika na tiba mbadala, na ikawa inasaidia kwa muda, lakini baadaye hali yake iliendelea kuwa tete. Na kilichokuwa kikimzidishia zaidi ni kutokana na kutokupenda masharti, Mume wangu alikuwa mbishi sana wa kufuata masharti.

‘Mume wangu huoni kuwa kwa kutokufuata masharti, kama ulivyoelekezwa na dakitari unajiua wewe mwenyewe…’nikawa namwambia mume wangu ambaye kwa muda huo alikuwa kashikilia sigara mkononi.

‘Wangapi wamekufa , hata bila kuumwa,…hata bila kuvuta sigara, hata bila kunywa pombe...kama ni kufa nitakufa tu, … tusisingizie kuwa zifuati masharti, siku yako ukifika uwe umafuta masharti, au hujafuata utakufa tu….kwanza hebu niambie nimekiuka masharti gani ..maana wewe unanifuata futa sana…nikifa una shida gani, nyumba unayo, mtoto unaye…kwanza ndio vizuri umpate mume mwingine asiyeumwa….’akawa anaongea kwa hasira na ilionyesha kabisa kama vile kakata tamaa na kuchanganyikiwa.

‘Umeambiwa usinywe pombe, usivute sigara, lakini wewe hutaki kuviacha hivyo vitu, …huoni hiyo ni sumu ya afya yako…na mume wangu kuumwa ni mitihani ambayo inakufanya umkumbuke mungu wako, ukiumwa, jaribu kutuliza kichwa, achana nay ale yasiyofaa, ili mola wako akusikilize…hayo ya mume mwingine ni mawazo yako, …..’nikamwambia nikiwa namwangalia kwa macho ya huruma.

‘Mimi pombe siachi, sigara nimepunguza kidogooo, japo tatu kwa siku sio mbaya, inanisaidia kuondoa mawazo…..kama nikufa nitakufa tu, kwanza hebu niache….maana walionifunga wameharibu maisha yangu…natafuta mtu wa kuondoka naye, siwezi kukubali kuondoka hivi hivi….yote haya wameyataka hawo wabaya wangu ili nifungwe na hatimaye nipate haya magonjwa mabaya...’akawa analalamika

‘Sasa kwanini wewe uliiba pesa za watu, hujui kuwa wizi ni mbaya, unaweza ukaiba ukaona umeshinda, ukasahau kuwa kwa kumuibia hiyo mtu, umemkwaza sana, huenda pesa hiyo ilitakiwa kumsaidia kwenye matibabu, kula watoto….wewe ukazichukua kulewea….yeye unafikiri atafanya nini, kama anakujua atakufunga tu, na kama hakujui, basi atakushitakia kwa mungu, atakuwa akiomba kwa mola wake,…na hayo ndio malipizo yake…’nikamwambia mume wangu.

‘Wangapi wanaiba bwana, na wanafanikiwa…mimi sio wa kwanza kuiba, sema tu, bahati haikuwa yangu, kwanza ilibidi nifanye hivyo, nimewatumikia miaka mingi, hawanijali, Napata shida, naomba angalau mkopo hawanipi, nikapa ile nafasi, kwanini nisiitumia, sema mjanja mwingine akaniwahi,..huyo mtu ana bahati kweli, maana kapata bila jasho, na matokea yake naumia mimi, sawa…’akashika shavu huku akiiangalai ile sigara ambayo alikuwa hajaiwasha.

‘Mume wangu nakupenda sana, nasikitika kukuona kwenye hiyo hali, kwa kukuonyesha kuwa nakupenda, nyumba nimeandika kwa jina lako kama ulivyotaka….sasa ukifa nyumba itabakia na nani…’nikamsogelea na kumshika begani.

‘Mhh, eti unanipenda, kama ungelikuwa unanipenda tangia mwanzo, usingelipinga na mimi nilipokuambai uandike jina langu, hata hivyo, mimi sitaishi sana, nyumba hiyo itabakia mikononi mwako, lakini nikiwa hai angalau nifaidi heshima yangu….kwasabbau ungeliandika jina lako, ningelizarauliwa….’akasema huku bado akiwa anaiangalia ile sigara.

‘Basi tupa hiyo sigara, maana ukiivuta utaanza kukohoa hapo, hadi utoe vyote ulivyokula….achana na hizo sigara na pombe, ili dawa unazotumia zifanye kazi…’nikamwambia.

‘Umeanza kuniuzi….huku kuumwa, sio mimi wa kwanza, wapo wameumwa kaba yangu, wakapona, na wengine wakafa, sio ajabu mimi nikifa au nikipona,…’akawa anasema huku akianza kukohoa kidogo, na mara akafululiza kukohoa.

‘Tatizo lako wewe ni mbishi sana,…..’nikamwambia mume wangu, ambaye kwa hasira alisimama na kuanza kuondoka. Imekuwa ni kawaida yake, kwani kila ukijaribu kumshauri jambo, mnaishia kwenye malumbano, na akiona umemshinda kwa hoja, anachokimbilia yeye ni kuondoka, kwenda kulewa…ikabidi niwatafute marafiki zake wanakunywa naye wajaribu kumshauri, lakini haikusaidia kitu, akawa ndio anazidi kunywa pombe, kuvita sigara, na mwili ukazidi kuisha,…….

Kuna kipindi kulitokea ubishi wa nyumba tuliyojenga, yeye kwa vile ni mwanaume, alitaka tuandikishe nyumba hiyo kwa jina lake, mimi sikukubali nilijua kuwa nilijenga kwa pesa yangu,..malumbano haya yalileta mgongano mkubwa, mwishowe niliona haina haja ya kulumbana nay eye ndio, nikakubalia nyumba hiyo ikaandikishwa kwa jina lake, nikijua kuwa nyumba hiyo ni yetu wote wawili na mimi nampenda mume wangu.

Baada ya yeye kuondoka, akaja rafikii yangu, tukawa tunaongea hili na lile kubadilishana mawazo, na baadaye akauliza;

‘Nimemuona mume wako akielekea sehemu yake…’ akasema akionyeshea mkono mdomoni kuashiria kuwa mume wangu kaenda sehemu yake anapopenda kwenda kunya pombe.

‘Wala mimi sijui kuwa kaelekea huko….’nikasema nikijifanya kuwa sijui.

‘Lakini kwanini mwanaume huyo hasikii,….ni mbishi sana, namfahamu sana huyu mume wako, kwa ubishi namtolea kofia,….lakini hata hivyo ubishi mwingine hauna maana, haoni kuwa huko kulewa kutamuondoa duniani kabla ya siku zake….’akasema huyo rafiki yangu.

‘Nimesema wee nimechoka…..naona nimuache kama alivyo, maana mwishowe tutagombana, tuihie kushikana, na bahati mbaya nimsukume, iwe ndio kisa cha umauti wake….niambiwe ooh, umemuua mume wako, maana nyie watu hamna dogo…’nikasema kwa utani.

‘Lakini….rafiki twende mbele turudi nyuma,…. hayo aliyo nayo mume wako sio bure…’akasema huku akishika kichwa na kuangalai juu, halafu akaniangalia na kusema;

‘Tatizo lako nikukushauri jambo unachukulia ni mzaha,huyo mwanaume wako usipoangalia utamkosa hivi hivi…na inavyoonyesha huyo aliyemfanyizia, kafanya kazi kweli kweli…maana kakufanya hata na wewe usiwe na akili ya kumgangaikia,….nakuambia ukweli, muda sio mrefu huyo ataondoka….’akasema huku akinikazia macho, sikusema kitu, na alipoona hivyo akasema;

‘Na haya yote ni uchawi wa huyo mwanamama wenu, hamjaushughulia, ….unakumbuka alivyokuambia yule mtaalamu, …wewe ukapuuzia, ….mtoto hajambo sasa, lakini akianza kuumwa na yeye mtatafuatana, sasa hivi ni zamu ya mumeo…..hangaikeni, huyo mwanamama, kaondoka lakini mtaondoka naye,….alikuwa mwanga kiukweli kweli…nawaambia ukweli, huyo atawamaliza wote..’akasema huyo rafiki yangu.

‘Ondoka na mdomo wako mbaya, labda kama wewe ndio mwanga, na unataka kutuondoa, umejuaje yote hayo, kama huhusiki na kumsingizia mama wa watu, ….kwanza wewe bado hujachoka na hayo maneno yako,…umesikia ni kitu gani kinachowapata sasa hivi hawo vijana walioshiriki kuchoma nyumba ya mama huyo na wengine wasio na hatia…?’ nikamuuliza rafiki yangu.

‘Hayo ni maneno ya watu,hawo vijana wamebwia unga wao, na mabangi yamewapanda kichwani, sasa kwa kuwatetea wanasema hivyo, yule mtaalamu mimi namwaminia, hawezi akasema uwongo…mama yako alikuwa mwanga….tena mwanga kweli….’akasema na kukatiza maneno yake, akatulia kama mtu aliyenyamazishwa na jambo la hatari….

Mimi nikamwangalia, na kugundua kuwa alikuwa akiangalia kwa nyuma yangu,…macho yamemtoka na kiwa mdomo upo wazi,… nikageuza kichwa kuangalia ni kitu gani kimemfanya anyamaze vile na kuduwaa kama mtu aliyeona kitu cha kuogofya….na mara macho yangu yakakutana na babu yako;

‘Ba-ba-ba kumbe umerudi, karibu….’nikasema kwa kigugumizi,huku nikiwa nimetahayari, kwani alichosema rafiki yangu ni lazima kakiskia babu yako, na hata mimi sikupenda hiyo kauli yake, lakini sikutaka kuleta migongano kwa watu hawa, nikavunga ili babu yako alainike….lakini

‘Mwambie huyo rafiki yako, mwanga ni yeye mwenyewe,…akome kabisa kumuita mke wangu mwanga..hawa ndio waliopandikiza chuki na fitina….. na leo nataka athibitishe hiyo kauli yake la sivyo nitaufunga huo mdomo wake….’akasema babu na rafiki yangu akainuka kwa haraka akitaka kukimbia, na ghafla akadondoka chini……..na kuanza kujinyonga nyinga, na baadaye akatulia kimiya.

‘Oh, hili sasa ni balaa …..’nikasema, na mara ikasikika hodi , na sauti iliyosikika ilinifanya moyo wangu ulipukwe kwa woga, …..nikageuka kumwamgalia babu yako, aliyekuwa bado kasimama kwa hasira, akiwa hajali ni kilichotokea na wala hakujali huyo aliyepiga hodi ni nani.
Aliyepiga hodi alikuwa ni mume wa huyo rafiki yangu, ambaye alikuwa kalala sakafuni, kimiya, ikiashiria kuwa kapoteza fahamu…

NB: Naona kisa kinasua sua….tatizo jembe hili ninalotumia lina matatizo, mtandao umegoma, sasa inabidi nitafute njia mbadala. Cha kuazima hakisitiri uchi,…

WAZO LA LEO: Tuogopeni sana uzushi, kwani neno moja la uzushi wenye nia mbaya linaweza kuwa baya zaidi ya bomu…uzushi ni sumu ya amani. Watu siku hizi tunaona ni jambo la kawaida kusema uwongo, na kuzua mambo yasiyo na ukweli, eti ili kumzalilisha mpinzani wako, eti ili kumfanya mtu fulani asifanikiwe, eti ili,….. kujiimarisha kwenye masilahi haya ya kidunia yenye muda mfupi tu.

 Jamani, jamani uwongo, uzushi, ufitinishaji, ni mambo mabaya sana katika maisha yetu, lakini sisi tumeona kuwa ni dili, ilimradi tunafanikiwa katika maslahi yetu…huo ni unafiki, tuyaepukeni mambo haya, ili tusiwe wanafiki.




Ni mimi: emu-three

2 comments :

Rachel Siwa said...

Mhhh. .Ndugu wa mimi kweli umebarikiwa. ..kisa kinagusa sana. Mungu azidi kubariki kazi za mikono yako. ...kweli wema hauozi. .Pamoja sana!

Anonymous said...

Actually no matter if someone doesn't be aware of after that its up
to other people that they will help, so here it occurs.