Siku hiyo niliamua kwenda kuitembelea iliyokuwa nyumba ya
huyo mtaalamu, ilikuwa imeteketea yote kwa moto, na hakikubakia hata kitu kimoja, …yalikuwa ni majivu matupu
yaliyokuwa yamebakia. Na kwa vile nyumba za kijijini nyingi zilijengwa kwa
miti, zikakandikwa kwa udongo na kuezekwa kwa makuti, moto ukishika, inaungua
haraka sana.
Siku zilizofuata kukawa kunanyesha mvua, nilipopita pale
siku nyingine niliona yale majivu yote yamegendamana kwenye ardhi kama vile
kumpigwa sakafu ya udongo ulaya…na baada ya siku tatu, majani yakaanza kuota
kuzunguka lile eneo. Ilikuwa ajabu kabisa, maana pale kati kati, palibakia hivyo
hivyo bila kuota majani, huku pembeni yake majani na miti vikiota kwa kasi ya
ajabu.
Wiki kadhaa zikapita, na watu walianza kulalamika kuwa
wakipita eneo hilo, wanasikia kama sauti za watu wakiongea na kukipiga ukulele,
au kunatoka sauti zisizofahamika vyema.
‘Hiyo ni mizmu ya huyo mtalaamu, nini ….?’watu wakawa
wanaulizana
‘Kama ni mizumu yake, je haitaweza kutuathiri na sisi?’
mmoja akauliza
‘Inabidi tuwaone wazee wanaojua mambo hayo, maana eneo hili
sasa halipitiki…mimi mwenyewe nilipia jioni jioni nikasikia kama watu
wanaongea, na vyombo vikigongana, na mara nikasikia kama sauti ya kilio cha
mtoto mdogo…’akasema jamaa mmoja, na watu wakamwangalia wakiwa na wasiwasi.
‘Kama ni hivyo, kuna jambo….ni heri tuhangaike, kwanza ni
bora tuwaone wazee wa hapa kijijini,….’wengine wakashauri hivyo, na wengine
wakapuuzia, na kweli baadhi yao, waliwaendea wazee na kuomba ushauri, na wazee
walipoulizwa, walisema bila kuficha;
‘Inaonekana huyu mwenzetu alikuwa na mambo mengine ambayo sio
ya kawaida. Tunakubali kuwa alipewa karama ya utibabu, lakini yeye alichanganya
hayo na mambo mengine yasiyo ya halali, na hayo mnayoyasikias ni mambo yake
mabaya….’akasema mzee mmoja.
‘Na yanahitajika kuondolewa haraka eneo hilo kwani lipo
kwenye himaya za makazi yetu, mmiliki wake hayupo, ni nani wa kuyadhibiti hayo
madude, hatujui yanakula nini, au yanafanywaje ili yasihangaike kwenye makazi
ya watu wengine au kusambaa kwenye njia tunazopita…’akasema mzee mwingine.
‘Na kama ni madude,…., yanaweza yakawakumba watu na kuleta
athari…na nahisi huenda kuna jambo linaweza kutokea kama hatutafanya juhudi za
haraka..’akasema mzee mwingine
‘Sasa wazee wetu tufanyeje?’ akaulizwa.
‘Inabidi watu wafunge safari kwenda huko milimani na
kuwapata watu wanajua mambo hayo….kwa hapa kwetu mtu tuliyekuwa tukimtegemea
ndio huyo mtaalamu, sasa keshaondoka.
…’akasema mzee.
‘Na ninavyo mimi kaondoka kwa mabaya, tofauti na enzi zetu,
kwani mtu kama huyo alitakiwa kuwa muadilifu,… lakini mlimuonaje maisha yake
yalivyokuwa,…yeye tamaa ilimzidi akakiuka masharti ya kazi kama hiyo…’akasema
mzee mwingine.
‘Mimi niliwahi kumkanya, …lakini aliniona mbaya, tukawa
hatusalimiani,…na ilionekana wazi kuwa mambo yake mengine alikuwa akifanya kwa
maslahi yake, …sio wote aliokuwa akisema ni wachawi,walikuwa ni wachawi,
wengine aliwasingizia pale alipoona wanaingilia maslahi yake….sasa hatuju ni
kwanini hili limetokea, lakini nahisi ni mabaya yake ndiyo yaliyomuangamizai…’akasema
huyo mzee.
Watu wakaanza kutishika , na kuogopa kabisa kupita eneo
hilo, wakijua wanaweza kukumbwa na hayo waliyokuja kujua kuwa ni mashetani ya
huyo mzee. Wazee nao wakahangaika hadi kwenda huko milimani, na waliporejea
walisema hawakuweza kufanikiwa, kwani inavyoonesha ni kuwa walishachelewa,
iliyobakia ni kusubiria tu.
‘Cha muhimu eneo hilo litengwe kabisa….’akashauri huyo mzee,
na kweli eneo hilo likawa nje ya mipaka ya wanakijiji, ndio maana hadi leo unaliona
hilo eneo likiwa limebakia msitu, na ukiingia ndani ya huo msitu, kuna sehemu
ipo pakavu kabisa…..ndio asili ya jina hilo la mzimuni….’babu yake akasema.
********
Niliendelea kukumbuka
yale aliyoniahdithia babu, ambayo mengine mama hakuweza kunihadithia a, huenda
aliogopa kunisimulia, nisije nikatishika, ….nikakumbuka jinsi babu alivyosema
siku ile alipokuwa akinihadithia;
‘Mimi nikarejea nyumbani kwa mama yako nikisubiria nyumba
yangu ijengwe, na ndoto zile mbaya za kutisha zikawa zimepotea kabisa,…hata
hivyo sikuweza kuwa na amani, bado nilikuwa nikimuwaza mke wangu, na jinsi gani
ya kuwapata hawo waliomfanyia hivyo.
Kulianza kutokea maajabu hapo kijijini, kila siku kulizuka
jambo la kustaajabisha, na mambo hayo yalionekana kufanana. Vijana walianza
kufa ovyo, na vifo vyao, kama nilivyosema awali, vilikuwa vya aina moja…nikajua
ubaya umeanza kulipizwa….
‘Hawa inasadikiwa ndio waliokuwa vijana wa mtaalamu, hawa
ndio huyo mtalaamu alikuwa akiwatuma kufanya mauaji kwa wale wanaosadakiwa kuwa
ni wachawi…na kufuatilia mambo yake.’watu wakawa wanasema.
Hawo vijana, mmoja mmoja akawa anashikwa na kitu kama
mshituko, halafu anakuwa kama kachanganyika, au kupandisha mashetani, na kuanza
kukimbia ovyo. Alipoanza wa kwanza, watu walizania huenda ni hayo mabangi
wanayopenda kutumia vijana, lakini alipofuatia wa pili , watatu , wanne, na
wote wanajulikana ni nani, watu wakahisi kuna jambo.
Na cha ajbu zaidi wote walitaabika na hali hiyo ya
kuchanganyikiwa, na mwisho wake wanakutwa wamekufa eneo hilo hilo la huyo
mtaalamu, mmoja baada ya mwingine. Na siku ya kwanza ya kufariki kwa kijana
huyo, ndugu na jamaa wakafika kumtoa pale alipofarikia, na kumpeka nyumbani
kwako, lakini ikashindikana, kwani watu walijikuta wakizungukwa na nyuki wengi.
‘Chomeni moto , hawo nyuki wataondoka,…..’mmoja akasema,
lakini hakuna aliyeweza kusogea pale, na kila ukiletwa hapo karibu, unazimika.
‘Hili sio la kawaida, inabidi tukawaulize wazee….’mmoja,
akasema na wakafuatilia, huko kwa wazee wanajua mambo hayo.
‘Huyo mzikeni eneo hilo hilo,…’akashauri huyo mzee, Na kweli
walipoanza kuchimba makaburi, wale nyuki wakawa wanazunguka hewani, hadi
walipomaliza kumzika, na nyuki wale wakaanza kuwashambulia, kuashiriwa kuwa
waondoke haraka, …
Haikupita siku mbili, hali kama ile ikamtokea kijana
mwingine, na yaliyotokea kwa mwenzake ilikuwa hivyo hivyo, na huyo naye
wakamzika eneo hilo hilo.
‘Wazee wetu sasa hili ni balaa gani maana vijana wetu
wanamalizika…..?’ wakina mama wakauliza.
‘Haya matukio yanaoenekana ni dhuluma ilietendwa na hawo
vijana, na inavyoonekana, hawa vijana walikuwa wafuasi wa huyo mtaalamu,
kwahiyo waliotendewa hizo dhuluma, walilalamika, na huenda wengine walikwenda
kuomboleza kuwa hawow aliofanya hivyo mabaya yawakute….’wakasema hawo wazee.
‘Sasa tufanyeje, maana hali kama hii hatujawahi kukutana
nayo?’ wakauliza.
‘Kwanza ni hawo wanahusika kukubali makosa yao, na kwenda
kutubu hayo makosa yao kwa hawo waliodhulumiwa, swali kubwa hapa ni je wanajua
makosa yao, na hawo waliotendewa hivyo bado wapo hai, kama hawapo hai, ….hatuna
la kufanya’wakasema hawo wazee.
‘Oh, sasa tutafanyeje….?’ Wakina mama wenye vijana ambao
wanafahamu kuwa vijana wao walikuwa na mafungamano na huyo mtaalamu wakaanza
kulalamika na kuhaha huku na kule kutafuta jinsi gani ya kuweza kulikwepa hilo
janga.
‘Ubaya unapotendwa, watu wanajionea ni kawaida, na hujiona
kama wao ni washindi , lakini unashindwa kufahamu kuwa tunaowatendea huo ubaya
ni binadamu kama sisi….wanaumia, na kujiskia uchungu kama sisi, basi dhuluma
hiyo haitaisha hivi hivi, mpaka na nyie msikie uchungu kama wao
walivyosikia….’akasema huyo mzee.
‘Lakini sisi tulikuwa hatujui,….tulikuwa tukimfuata huyo
mtaalamu, kama unavyojua kuwa yeye watu wote walikuwa wakimuamini kwa kila
anachoongea….’wakasema hawo watu.
‘Sasa kama mlikuwa mkimwamni kwa kila kitu,….mkasahau kuwa
kuna mungu, inabidi mumtafute huyo mtaalamu, …..hakuna la kufanya kwa
sasa…’wakasema hawo wazee.
‘Hatuwezii kwenda huko milima kwa watu wema wakatusaidia?’
wakauliza.
‘Wema wao sio wa kudaidia wadhalimu, kwani wakisaidia
wadhalimu na wao watakuwa kama wamedhulumu, …hebu fikiria unapomsaidia mwenye
makosa, ni nini hukumu yake kisheria,…ni kuwa na wewe unashitakiwa kama
msaidizi wa mtenda makosa…’akasema huyo mzee.
‘Wazee tunaomba msaada wenu, nyie ndio wazee wetu, na huenda
mambo kama haya yaliwahi kutoeka huko nyuma, je ilipotokea hivi mlifanya
nini..?’ wakauliza.
‘Kuna mambo ya kimila yalifanyika, kuna matambiko,….lakini
bado kulikuwa na jukumu la kujua kosa na nani waliofanya hivyo, na kwa
nani….enzi zetu, watu walikuwa wakweli, kama walitenda kosa, walikiri, na
wakatubu makosa hayo kwa waliotendewa…je nyie mnaweza kufanya hivyo?’ akauliza
‘Sisi wazazi tunaweza kufanya hivyo kwa niaba ya watoto
wetu..’wakasema hawo wazazi.
‘Hapana, makosa kama hayo yanatakiwa mtu mwenyewe akutubu,
…na asichelewe kabla adhabu haijaanza..hivi sasa naona kama
mumeshachelewa…..’akasema huyo mzee, na mara sauti ya ukulele unaoashiria
masiba, ukasikika kule kule eneo la mzimuni, …
‘Je ndio kisasi
kimeanza, na ni mbinu gani watatumia, ili kuondokana na janga hilo..?
*****
Mume wangu alianza kuzidiwa, kifua kile hakikutaka kupona,
na ikafikia hadi kurudishwa hospitalini na kulazwa, lakini hali yake haikuweza
kutengamaa, na ikafikia muda wakashauri arejeshwe nyumbani tu, na hapo tukajua
kuwa madakitari wameona uwezekano wake wa kupona haupo tena.
Tukahangaika na tiba mbadala, na ikawa inasaidia kwa muda,
lakini baadaye hali yake iliendelea kuwa tete. Na kilichokuwa kikimzidishia
zaidi ni kutokana na kutokupenda masharti, Mume wangu alikuwa mbishi sana wa
kufuata masharti.
‘Mume wangu huoni kuwa kwa kutokufuata masharti, kama
ulivyoelekezwa na dakitari unajiua wewe mwenyewe…’nikawa namwambia mume wangu
ambaye kwa muda huo alikuwa kashikilia sigara mkononi.
‘Wangapi wamekufa , hata bila kuumwa,…hata bila kuvuta
sigara, hata bila kunywa pombe...kama ni kufa nitakufa tu, … tusisingizie kuwa
zifuati masharti, siku yako ukifika uwe umafuta masharti, au hujafuata utakufa
tu….kwanza hebu niambie nimekiuka masharti gani ..maana wewe unanifuata futa
sana…nikifa una shida gani, nyumba unayo, mtoto unaye…kwanza ndio vizuri umpate
mume mwingine asiyeumwa….’akawa anaongea kwa hasira na ilionyesha kabisa kama
vile kakata tamaa na kuchanganyikiwa.
‘Umeambiwa usinywe pombe, usivute sigara, lakini wewe hutaki
kuviacha hivyo vitu, …huoni hiyo ni sumu ya afya yako…na mume wangu kuumwa ni
mitihani ambayo inakufanya umkumbuke mungu wako, ukiumwa, jaribu kutuliza
kichwa, achana nay ale yasiyofaa, ili mola wako akusikilize…hayo ya mume
mwingine ni mawazo yako, …..’nikamwambia nikiwa namwangalia kwa macho ya huruma.
‘Mimi pombe siachi, sigara nimepunguza kidogooo, japo tatu
kwa siku sio mbaya, inanisaidia kuondoa mawazo…..kama nikufa nitakufa tu, kwanza
hebu niache….maana walionifunga wameharibu maisha yangu…natafuta mtu wa
kuondoka naye, siwezi kukubali kuondoka hivi hivi….yote haya wameyataka hawo
wabaya wangu ili nifungwe na hatimaye nipate haya magonjwa mabaya...’akawa
analalamika
‘Sasa kwanini wewe uliiba pesa za watu, hujui kuwa wizi ni
mbaya, unaweza ukaiba ukaona umeshinda, ukasahau kuwa kwa kumuibia hiyo mtu,
umemkwaza sana, huenda pesa hiyo ilitakiwa kumsaidia kwenye matibabu, kula
watoto….wewe ukazichukua kulewea….yeye unafikiri atafanya nini, kama anakujua
atakufunga tu, na kama hakujui, basi atakushitakia kwa mungu, atakuwa akiomba
kwa mola wake,…na hayo ndio malipizo yake…’nikamwambia mume wangu.
‘Wangapi wanaiba bwana, na wanafanikiwa…mimi sio wa kwanza
kuiba, sema tu, bahati haikuwa yangu, kwanza ilibidi nifanye hivyo,
nimewatumikia miaka mingi, hawanijali, Napata shida, naomba angalau mkopo
hawanipi, nikapa ile nafasi, kwanini nisiitumia, sema mjanja mwingine
akaniwahi,..huyo mtu ana bahati kweli, maana kapata bila jasho, na matokea yake
naumia mimi, sawa…’akashika shavu huku akiiangalai ile sigara ambayo alikuwa
hajaiwasha.
‘Mume wangu nakupenda sana, nasikitika kukuona kwenye hiyo
hali, kwa kukuonyesha kuwa nakupenda, nyumba nimeandika kwa jina lako kama
ulivyotaka….sasa ukifa nyumba itabakia na nani…’nikamsogelea na kumshika
begani.
‘Mhh, eti unanipenda, kama ungelikuwa unanipenda tangia
mwanzo, usingelipinga na mimi nilipokuambai uandike jina langu, hata hivyo,
mimi sitaishi sana, nyumba hiyo itabakia mikononi mwako, lakini nikiwa hai
angalau nifaidi heshima yangu….kwasabbau ungeliandika jina lako,
ningelizarauliwa….’akasema huku bado akiwa anaiangalia ile sigara.
‘Basi tupa hiyo sigara, maana ukiivuta utaanza kukohoa hapo,
hadi utoe vyote ulivyokula….achana na hizo sigara na pombe, ili dawa unazotumia
zifanye kazi…’nikamwambia.
‘Umeanza kuniuzi….huku kuumwa, sio mimi wa kwanza, wapo
wameumwa kaba yangu, wakapona, na wengine wakafa, sio ajabu mimi nikifa au
nikipona,…’akawa anasema huku akianza kukohoa kidogo, na mara akafululiza kukohoa.
‘Tatizo lako wewe ni mbishi sana,…..’nikamwambia mume wangu,
ambaye kwa hasira alisimama na kuanza kuondoka. Imekuwa ni kawaida yake, kwani
kila ukijaribu kumshauri jambo, mnaishia kwenye malumbano, na akiona umemshinda
kwa hoja, anachokimbilia yeye ni kuondoka, kwenda kulewa…ikabidi niwatafute
marafiki zake wanakunywa naye wajaribu kumshauri, lakini haikusaidia kitu,
akawa ndio anazidi kunywa pombe, kuvita sigara, na mwili ukazidi kuisha,…….
Kuna kipindi kulitokea ubishi wa nyumba tuliyojenga, yeye
kwa vile ni mwanaume, alitaka tuandikishe nyumba hiyo kwa jina lake, mimi
sikukubali nilijua kuwa nilijenga kwa pesa yangu,..malumbano haya yalileta
mgongano mkubwa, mwishowe niliona haina haja ya kulumbana nay eye ndio,
nikakubalia nyumba hiyo ikaandikishwa kwa jina lake, nikijua kuwa nyumba hiyo
ni yetu wote wawili na mimi nampenda mume wangu.
Baada ya yeye kuondoka, akaja rafikii yangu, tukawa
tunaongea hili na lile kubadilishana mawazo, na baadaye akauliza;
‘Nimemuona mume wako akielekea sehemu yake…’ akasema
akionyeshea mkono mdomoni kuashiria kuwa mume wangu kaenda sehemu yake
anapopenda kwenda kunya pombe.
‘Wala mimi sijui kuwa kaelekea huko….’nikasema nikijifanya
kuwa sijui.
‘Lakini kwanini mwanaume huyo hasikii,….ni mbishi sana,
namfahamu sana huyu mume wako, kwa ubishi namtolea kofia,….lakini hata hivyo
ubishi mwingine hauna maana, haoni kuwa huko kulewa kutamuondoa duniani kabla
ya siku zake….’akasema huyo rafiki yangu.
‘Nimesema wee nimechoka…..naona nimuache kama alivyo, maana
mwishowe tutagombana, tuihie kushikana, na bahati mbaya nimsukume, iwe ndio
kisa cha umauti wake….niambiwe ooh, umemuua mume wako, maana nyie watu hamna
dogo…’nikasema kwa utani.
‘Lakini….rafiki twende mbele turudi nyuma,…. hayo aliyo nayo
mume wako sio bure…’akasema huku akishika kichwa na kuangalai juu, halafu
akaniangalia na kusema;
‘Tatizo lako nikukushauri jambo unachukulia ni mzaha,huyo
mwanaume wako usipoangalia utamkosa hivi hivi…na inavyoonyesha huyo
aliyemfanyizia, kafanya kazi kweli kweli…maana kakufanya hata na wewe usiwe na
akili ya kumgangaikia,….nakuambia ukweli, muda sio mrefu huyo
ataondoka….’akasema huku akinikazia macho, sikusema kitu, na alipoona hivyo
akasema;
‘Na haya yote ni uchawi wa huyo mwanamama wenu, hamjaushughulia,
….unakumbuka alivyokuambia yule mtaalamu, …wewe ukapuuzia, ….mtoto hajambo
sasa, lakini akianza kuumwa na yeye mtatafuatana, sasa hivi ni zamu ya
mumeo…..hangaikeni, huyo mwanamama, kaondoka lakini mtaondoka naye,….alikuwa
mwanga kiukweli kweli…nawaambia ukweli, huyo atawamaliza wote..’akasema huyo
rafiki yangu.
‘Ondoka na mdomo wako mbaya, labda kama wewe ndio mwanga, na
unataka kutuondoa, umejuaje yote hayo, kama huhusiki na kumsingizia mama wa
watu, ….kwanza wewe bado hujachoka na hayo maneno yako,…umesikia ni kitu gani
kinachowapata sasa hivi hawo vijana walioshiriki kuchoma nyumba ya mama huyo na
wengine wasio na hatia…?’ nikamuuliza rafiki yangu.
‘Hayo ni maneno ya watu,hawo vijana wamebwia unga wao, na
mabangi yamewapanda kichwani, sasa kwa kuwatetea wanasema hivyo, yule mtaalamu
mimi namwaminia, hawezi akasema uwongo…mama yako alikuwa mwanga….tena mwanga
kweli….’akasema na kukatiza maneno yake, akatulia kama mtu aliyenyamazishwa na
jambo la hatari….
Mimi nikamwangalia, na kugundua kuwa alikuwa akiangalia kwa
nyuma yangu,…macho yamemtoka na kiwa mdomo upo wazi,… nikageuza kichwa kuangalia
ni kitu gani kimemfanya anyamaze vile na kuduwaa kama mtu aliyeona kitu cha
kuogofya….na mara macho yangu yakakutana na babu yako;
‘Ba-ba-ba kumbe umerudi, karibu….’nikasema kwa kigugumizi,huku
nikiwa nimetahayari, kwani alichosema rafiki yangu ni lazima kakiskia babu
yako, na hata mimi sikupenda hiyo kauli yake, lakini sikutaka kuleta migongano
kwa watu hawa, nikavunga ili babu yako alainike….lakini
‘Mwambie huyo rafiki yako, mwanga ni yeye mwenyewe,…akome
kabisa kumuita mke wangu mwanga..hawa ndio waliopandikiza chuki na fitina….. na
leo nataka athibitishe hiyo kauli yake la sivyo nitaufunga huo mdomo
wake….’akasema babu na rafiki yangu akainuka kwa haraka akitaka kukimbia, na
ghafla akadondoka chini……..na kuanza kujinyonga nyinga, na baadaye akatulia
kimiya.
‘Oh, hili sasa ni balaa …..’nikasema, na mara ikasikika hodi
, na sauti iliyosikika ilinifanya moyo wangu ulipukwe kwa woga, …..nikageuka
kumwamgalia babu yako, aliyekuwa bado kasimama kwa hasira, akiwa hajali ni
kilichotokea na wala hakujali huyo aliyepiga hodi ni nani.
Aliyepiga hodi alikuwa ni mume wa huyo rafiki yangu, ambaye
alikuwa kalala sakafuni, kimiya, ikiashiria kuwa kapoteza fahamu…
NB: Naona kisa kinasua sua….tatizo jembe hili ninalotumia
lina matatizo, mtandao umegoma, sasa inabidi nitafute njia mbadala. Cha kuazima
hakisitiri uchi,…
WAZO LA LEO: Tuogopeni
sana uzushi, kwani neno moja la uzushi wenye nia mbaya linaweza kuwa baya zaidi
ya bomu…uzushi ni sumu ya amani. Watu siku hizi tunaona ni jambo la kawaida
kusema uwongo, na kuzua mambo yasiyo na ukweli, eti ili kumzalilisha mpinzani
wako, eti ili kumfanya mtu fulani asifanikiwe, eti ili,….. kujiimarisha kwenye
masilahi haya ya kidunia yenye muda mfupi tu.
Jamani, jamani uwongo,
uzushi, ufitinishaji, ni mambo mabaya sana katika maisha yetu, lakini sisi
tumeona kuwa ni dili, ilimradi tunafanikiwa katika maslahi yetu…huo ni unafiki,
tuyaepukeni mambo haya, ili tusiwe wanafiki.
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
Mhhh. .Ndugu wa mimi kweli umebarikiwa. ..kisa kinagusa sana. Mungu azidi kubariki kazi za mikono yako. ...kweli wema hauozi. .Pamoja sana!
Actually no matter if someone doesn't be aware of after that its up
to other people that they will help, so here it occurs.
Post a Comment