Hauchi hauchi kukapambazuka, mama yako akafikia muda wa kujifungua…lakini hakuwa makini na tarehe hizo
Siku alipofikwa na machungu alikuwa, akifanya kazi ya kibarua kwa jamaa mmoja wa kihindi kama mfanyakazi wa ndani, na kwa vila alihitajika kufanya kazi hiyo ili apate chochote, na kuwekeza kwa ajili ya uzazi wake, akawa anajitahidi tu, kwa shida, masimango, na kudharauliwa, na hata kunyanyapaliwa, hakujali,… hata pale dalili za machungu ya kujifungua yalipojitokeza, hakujali….hakujua…maana dalili kama hizo zilikuwa zikimjia na kuondoka kabla...
Siku hiyo ilikuwa tofauti, machungu yalikuwa makubwa sana….hakuweza kuvumilia,…na akajikuta kizunguzungu kikimtanda machoni na ghafula akaanguka…. na bosi wake aliyekuwa karibu naye akamsogelea na kuanza kumtimba mateke huku akimsimanga;
‘Vewe mvivu sana, yaani sijui kwanini mume wangu amekung’ang’ania uendelee kufanya kazi hapa kwangu akijua Vewe ni mja mzito….hebu amuka huko….’akasema huyo mama.
Mama yako alijaribu kuinuka lakini hakuweza, kiuona kilikuwa kimekaza kweli kweli, maumivu yalikuwa sio ya kawaida, …hakuweza kuamuka, na alipojitahidi akajikuta akizidiwa na kudondoka, akatulia kimiya…..yule mama alipoona hivyo akajua mama yako amekwishakufa, akamuita mlinzi wake na kumuamrisha mama yako atolewe humo ndani.
‘Mama Bosi, sasa nitampeleka wapi,….huyu mtu, naona kama keshakufa?’ akauliza yule mlinzi.
‘Kamtupeni Popote pale lakini isiwe hapa nyumbani kwangu, kamtupe huko majalalani alipokuwa akiishi, ….’akasema huyo mama.
Basi yule mlinzi, akamuita mwenzake wakambeba huyo mama, na wazo lao kubwa likawa kwenda kumpeleka hospitalini, lakini wakiwa njiani wakakumbuka jambo.
‘Unamfahamu huyu mwanamke, je unawakumbuka ndugu zake, maana huu ni msala,…?’ akauliza.
‘Huyu mwanamke, nasikia aliwahi kufukuzwa kwao,….kwahiyo hatuwezi kumrejesha kwao au kwa jamaa yao yoyote, ….tunachotakiwa ni kufanya kama alivyosema bosi..tukamtupe maporini…’akasema mwenzake.
‘Hapana huo sio ubinadamu….mimi nina wazo, twende kwenye nyumba yoyote yenye mwanamke mtu mzima. Natumai yeye atajua la kufanya …’akasema na wote wakakubaliana na wazo hilo, wakaenda hadi kwenye nyumba moja wanayoifahamu kuwa anaishi mwanamke mtu mzima, na kumweka hapo kwenye kibaraza, na kuondoka zao.
Bahati nzuri, siku huyo bibi yako, alikuwa kaenda kwa jirani, kulikuwa na shughuli, na alichelewa kurudi mimi, nilikuwa nimejipumzikia ndani, nikapitiwa na usingizi, sikuwa najua kuwa kuna mtu katupwa hapo nje, kwenye kibaraza cha nyumba.
Bibi yako wakati anarudi ndio akamuona mtu kalala hapo kibarazani kwake…. Kwanza aliogopa akijua kuwa ni maiti, ……akapita hadi ndani na kuniamusha…na mimi kwa haraka nikatoka nje kuangalia.
‘Nilimkagua huyo mtu, yaani mama yako, na nikagundua kuwa hajafa, …
‘Huyu mtu hajafa,…..sasa tufanyeje….?’ Nikamuuliza.
‘Inabidi tuwaite majirani na mjumbe….maana hapa tunaweza tukazua kesi..’akasema bibi yako, na mara mama yako akazindukana, na kutaka kuinuka, na sisi tukamsaidia akaweza kukaa vyema. Tukamhoji ni kitu gani kimemsibu, na wakati anajaribu kuelezea, uchungu ukamshika,…
‘Huo sasa ni uchungu,…na hospitali hapa ni mbali, mpaka kukodi baiskeli….’akasema bibi.
Nilipita kwa majiani, lakini wengi wa akina mama walikuwa bado kwenye hiyo shughuli, sana sana niliowakuta ni akina baba, ambao wasingeliweza kumsaidia bibi yako kwenye mambo ya kumzalisha mama yako…kama ikibidi, kwani bibi yako alikuwa anafahamu mambo ya ukunga.
‘Nawaombeni tu, mnisaidie tukampeleke hospitali….’nikawaambia hawo majirani akina baba, na wakafika wawili, lakini tulikuwa tumechelewa, kwani tulipofika tulimkuta bibi yako akiwa kakashika kachanga.
‘Oh, amejifungua salama….’akasema bibi yako.
‘Hivyo ndivyo ulivyozaliwa mjukuu wangu, ….’akasema babu huku akitabasamu.
********
Babu alipofika hapo kwenye akili yangu, nikawa namsikiliza mama aendelee kuanzia hapo, ili kuthibitisha hayo, na ukumbuke kuwa wakatii huo mama alikuwa akiendelea kuongea, mama akasema;.
‘Mwanangu hata sijui jinsi gani nilivyokuzaa ninachokumbuka ni machungu,….machungu ambayo nilitamani roho itoke nikapumzike,…nilikumbuka siku nilipowahi kufika kiliniki , ilikuwa mara moja tu, na yule nesi alinielekeza mambo mengi, ya kufuata, lakini sikuwahi kuyafuata kabisa…sikuwa na muda huo, muda wote ulikuwa wa kuganga njaa, kuilea mimba…..oh.
Basi, hata uchungu uliponifika sikujua ndio muda umefika wa kukuzaa, …ulikuwa uachungu ambao sikuwahi kuupata kabla…. kitu cha mwisho kukisikia ni sauti yako ukilia, nikajua kweli sasa nimekuzaa na upo salama, na hapo hapo, nikapoteza fahamu.
Nilipoamuka ilikuwa ni usiku, niligeuka na kukuona umelezwa karibu yangu, ikiwa ni giza, …unajua tena nyumba za kwetu, hakuna umeme, taa ni kibatali, na taa ilishazimika kwa kukosa mafuta, nikainuka na kukuangalia kwenye giza,..sikuweza kuiona sura yako ya uchanga…
Nikahisi vikono vyako vidogo vikinishika…., hapo akili haikuwa yangu tena…..nilijikuta nikipandwa na hasira za machungu, hasira za kutelekezwa, hasira za kunyanyaswa na matajiri,…lakini vile vimkono vyako, vikanifanya moyoo uone huruma, nikalala vyema na kukunyonyesha na kuhakikisha kuwa umeshiba,…
Halafi kitu kikawa kimenizinga akilini, maana sikujua nini ninachokifanya kwa wakati ule, nikainuka kitandani, kwa shida,maumivu, kuchoka,..yaliniandama, lakini sikujali hayo, nikajikakamua na kutoka nje.
Nikatoka, nje, na kupata kibaridi cha usiku, sikujua naenda wapi, …miguu yangu ikawa anatembea tu, kwa kunyata….nikiyumba, ..nikatembea , nikatambea, hadi karibu na mto. Nilipofika hapo, nikahisi kiu, nikaamua kuinama na kupata maji..
Mara macho yangu yakahisi mtu amelala, ufukweni, nusu ndani ya maji, mwanzoni nilizania ni mamba, lakini huu mto haujawahi kuwa na mamba, nikajikuta nikimsogelea, na nilipomfikia, nikainama….alikuwa ni mwanaume…nashangaa sikuogopa, nikaweka kidole kwenye shingo ya huyo mtu kuangalia mapigo ya moyo, nikakuta bado yupo hai.
Nikajikakamua nikamvua nje ya maji, …..na hapo nilikuwa hoi, kwasababu ya kutumia nguvu nyingi kumtoa huyo mtu, …nikakaa pembeni yake, na kwasababu ya kuchoka, maumivu,…nikajikuta nimeshikwa na usingizi, ….na mwili wangu ukawa umelalia kifuani mwa huyu jamaa…..
‘Wewe amuka haraka,….tuondoke hapa, polisi wananitafuta…’ilikuwa sauti iliyoniamusha. Kulikuwa bado na kiza, lakini ilionyesha kuwa ni alifajiri.
‘Kwani wewe ni nani?’ nikamuuliza huku nikiingiwa na wasiwasi.
‘Usijali,..ilimradi wewe umeniokoa …basi utakuwa rafiki yangu…tuondoke haraka, hapa nilipo nina pesa nyingi,….lakini natafutwa na polisi, siwezi kuwapa hizi pesa, tumehangaiak pamoja, lakini wenzangu wanataka kunidhulumu, sikubali….najua hawo wenzangu wakinikamata wataniua, nab ado polisi nao wanatutafuta….sikubali kwenda jela….’akasema huyo jamaa. Ilikuwa bado giza, na sikuweza kumtambua vyema ni nani huyo mtu…alikuwa kiongea kuonyesha kuwa bado amelewa.
Ni mimi: emu-three
No comments :
Post a Comment