Mjumbe alipokuja kwangu, alianza kwa kunisihi kuwa ni bora
nikaondoka hapo kwenye hiyo nyumba, ili wahusika waweze kukamilisha mambo yao
ya kuweka mali za marehemu kwenye umiliki wa kifamilia kwa muda, hadi hapo
mirathi na taratibu nyingine za kisheria zitakapotangazwa na kama kuna lolote
jingine, nilifikishe kwa wanafamilia, ili taratibu zote zifuatwe ikiwemo haki
ya mjane, na mimi hapo hapo nikamuuliza;
‘Mjumbe wewe ni kiongozi wetu wa eneo hili, sawa si sawa?’nikamuuliza
huku tukiwa tumesimama, sikutaka hata kumkaribisha kiti, na mkononi nilikuwa
nimeshikilia panga. Silaha yangu kubwa ilikuwa panga, na panga langu lilikuwa
refu na zito, likiwa na makali.
‘Ni sawa….’akanijibu huku akionyesha kuwa na wasiwasi,…
sijui ni kwasababu ya hilo swali, au panga nililoshika au alikuwa na wasi wasi
wa jambo jingine ambalo huenda hakulitaka litokee, na alikuwa akichelea
likitokea kunaweza kuharibu amani. Nilijua kabisa kaja na kundi la watu ,…japokuwa
wao hawakuonekana, walikuwa wanasubiria sehemu nyingine, mimi nilishajiandaa
kwa lolote lile, na nisingelikubali kutoka humo, labda wanitoe nikiwa
sijitambui, au maiti…’babu akawa anaongea kwa ujasiri.
‘Mjukuu wangu, mimi najiamini, inapofikia sehemu ya kudai
haki yangu siogopi kitu…, huwa siogopi, nafahamu kabisa yule anayefanya jambo la
dhuluma, moyo wake umetekwa na wasiwasi,..na hilo linamweka katika udhaifu wa
kujiamini, na hapo unapata mwanya wa kumshinda.
'Unajua mkuu wangu hata haya majambazi yanayokuja
kupora watu kwa silaha, wasingeliweza kufanya hivyo, kama tungelikuwa
tunajiamini, wao kwanza wanachofanya ni kuwaondolea hiyo hali ya kujiamini, na
kuwajengea hofu, na kwa udhaifu wetu, tunaogopa…japokuwa, kiubinadamu inahitaji
moyo, na ujasiri, kitu ambacho ni adimu kwa bina-adamu….’akasema babu.
`Mjukuu wangu, katika maisha yako, kumbuka mambo hayo,
kwanza kuhakikishia unasimama kwenye haki, na kuitenda haki, …uwe mkweli na
utende yaliyo kweli…usiwe mzembe, mvivu, kuwa wa kwanza kujituma kwa kila
jambo, ili upate baraka ya mwanzio, hayo yatakupa ufahamu wa kujiamini,…ni
lazima utajiamini, maana hutakuwa na wasiwasi,…
Nikamwangalai mjumbe kwa kumkazia macho, na kuendelea
kumuuliza maswali nikitaka kwanza kujue lengo lao, pili kujaribu kumuelimisha,
ili alainike na kuondokana na dhamira yao hiyo, nikamuuliza swali;
‘Kwahiyo wewe kama mjumbe, mambo yote ya eneo lako hili
yakitendeka unayaona, sawa si sawa?’ nikamuuliza mjumbe na yeye akanijibu huku
akinikazia macho kujionyesha kuwa haniogopi, na yeye kama mjumba ana mamlaka
yake.
‘Ni sawa kwa yale yaliyopo wazi, ambayo yanaonekana kwa upeo
wa macho na kusikia, kama yanafanyika ndani ya nyumba za watu, na kwa siri,
mimi sio mchawi, au mtalaamu wa kugundua mambo yaliyo siri kiasi hicho,….
siwezi kusema naweza kuyaona yote’akasema.
‘Na mimi nimeuliza hilo kwa yale mambo ambayo yapo wazi,
sijalenga mambo ya ndani ya nyumba, …na hatuzungumzii maswala ya gizani mjumbe…’nikamwambia
na yeye akasema;
‘Mimi najitahidi sana kuwa makini kwa kadri ya uwezo wangu,
na ikiwa ni pamoja na kuwapitia watu wangu, na pia kuhakikisha kuwa kila
kinachotendeka kwenye eneo langu nakifahamu….kwa ajili ya usalama na matakwa ya
eneo letu, ilimradi yapo ndani ya sheria, na kama yanakiuka sheria, sitasita
kuyafikisha kunakostahili, kama yanazidi uwezo wetu…’akasema.
Mjumbe wetu huyu namfahamu sana, huwa wakati mwingine ana
maneno mengi yasiyo na vitendo, na kujisifia kusiko na sababu, ni mwanasiasa
mwenye lugha ya kushawishi, lakini udhaifu wake ni kuwabeba wale wenye uwezo, ….nikamuuliza;
‘Na hata kukiwa na ujenzi wa nyumba, au maduka unakuwa
makini kufuatilia kuwa ni nani amejenga sawa au si sawa?’ nikamuuliza na hapo,
akatulia kama swali hilo limemgusa.
‘Ni sawa,…naweza kusema hivyo, kuwa kama kuna nyumba mpya inajengwa
naifuatilia, kwasababu ni sehemu ya nyumba zangu, kama ujuavyo mimi ni mjumbe
wa nyumba kumi, zikizidi nina haki ya kufahamu, ili serikali za mitaa ijue
hilo, japokuwa kisheria hilo lilihitajika kuwa mkazi wowote akijenga nyumba, au
muhusika ni lazima kuifahamisha serikali za mitaa kupitia kwa mjumbe wake,
lakini wengine hawafanyi hivyo, …ila kwa vile ni eneo langu, hata kama atakuwa
hakufuata sheria za kujitambulisha, nitafahamu kwani ujenzi haujifichi…’akasema.
‘Kwahiyo ilipojengwa hii nyumba, na duka, wewe uliiona kama
mjumbe na ulifahamishwa kisheria au sio?’ nikamuuliza.
‘Niliiona, japokuwa sikufahamishwa kisheria,…lakini kwa vile
nafahamu udhaifu wa watu wangu, nilijitahidi kukutana na huyu mwanamama, …na
nilifika hapa mara kwa mara kuingalia ikiendelea kujengwa na kama unavyojua ni
moja ya nyumba zilizojengwa kwa haraka na kwa kisasa zaidi….’akasema.
‘Na ulimfahamu vyema anayejenga hii nyumba ni nani, sawa si
sawa?’ nikamuuliza.
‘Nilimfahamu ndio…’akasema akionyeshwa kukerwa na maswali
yangu, na yeye kama kiongozi, alijiona kama namshushia hadhi yake, na hapo
alikuwa kwa dhamira yake nyingine na huenda hakuhitajia maelezo zaidi.
‘Ni nani aliyekuwa mjenzi wa hii nyumba?’ nikamuuliza na
hapo akaangalia nje kwa kupitia mlangoni, maana pale aliposimama, alikuwa
akiona nje, mimi sikuwa naona huko nje, kwani nilikuwa sehemu inayozuiwa na
mlango kwa ndani…na alivyoangalia nje ilikuwa, kama vile anataka kuhakikisha
kuwa hayo anayoongea hayasikiki.
‘Maswali yako bwana, mjenzi si fundi nani hii, aah, jina
lake nani vile, …’akasema akionyesha kwa hakuelewa hilo swali nilikuwa na maana
gani.
‘Sijaulizia fundi, …naulizia aliyejenga hiyo nyumba, ….ni
nani?’ nikauliza sikutaka kumfafanulia vyema nikiwa na maana yangu
‘Ohoo, tatizo lako unauliza maswali mengi kama polisi, au
wakili mahakamani, ….au wazee wa baraza, haya, kama ulikuwa na maana hiyo,
aliyejenga hiyo nyumba alikuwa Mama wa hii nyumba…’akasema.
‘Ukisema mama wa hii nyumba una maana gani?’ nikamuuliza ili
niwe na uhakika, japokuwa nilifahamu ana maana gani.
‘Unajua hapa hatutaki kuangalia kumbukumbu zilizopita, tunachohitajia
hapa kwa sasa ni sheria na taratibu zote za kimila…mimi nafahamu kabisa lengo
lako ni nini, hayo maswali yote, nafahamu msingi wake ni nini, lakini
nikufahamishe wazi, kuwa hapa, hatuangalii swala la kujenga na kusimamia ujenzi. Katika
nyumba kuna wajenzi, kuna wasimamizi,…na yoyote anaweza akafanya hivyo na bado
asiwe mumiliki halali wa hiyo nyumba, sijui unanielewa maana nakuona haupo
makini na sheria…’akasema mjumbe akionyesha kujiamini, na baadaye akaendelea
kuongea kwa kujikoga;
‘Unasikia sana, …tunapoangalia mumiliki wa nyumba,
tunasimamia kwenye sheria, maana hapo kuna maandishi…kuna stakabadhi za
umiliki, kisheria, ….hayo mzee ni mambo ya wasomi, sio enzi zenu za kuaminiana
kwa mdomo tu..siku hizi ni mambo ya karatasi, ….natumai umenielewa,…na kama
umenielewa au hukunielewa,…naomba sasa unisikilize na mimi, ili tunamalize kazi….’akasema
akionyeshea kwa vitendo kama vile kashika katarasi au hiyo hati miliki mkononi.
‘Mjumbe mimi ni mkazi wako, na nina haki ya kukuuliza ili
tuwe sambamba, na bado hatujamalizana, nakuona wewe unachukulia haya mambo kwa
haraka, ….na haraka haraka haina baraka, ….’nikasema na akanikatiza kwa kusema;
‘Sasa naona tusipotezeane muda kwa maswali yako ….hayo
yatahitajika baadaye kama ni lazima, muda ukifika…mimi hapa nimekuja kwa kazi
moja, ambayo kisheria, umekiuka,….na tumeliangalai hilo na wenzangu, tukaona ni
bora tufanye hivyo, na naomba wewe kama mzee mwenzagu unielewe….ili tusije
tukafikishana kubaya….na tumeishi vyema kwa muda mrefu, bila kuleteana utata,
na hili lisitufikishe huko,….hapa naona mzee mwenzangu umeteleza…’akasema huyo
mjumbe pale aliposikia watu wakiongea na kulalamika huko nje.
Sauti za watu zilisikika zikisema, ‘mjumbe mbona
unatupotezea muda, atoke nje huyo mtu…’
‘Mjumbe, ni kweli unayoongea kuwa kuna sheria, za maandishi…sijui
karatasi, hati miliki na mambo kama
hayo…., lakini ukumbuke kuwa sheria hizo
zinatokana na ushahidi wa vitendo, na watu siku hizi ni wajanja, hasa hawa wanaojifanya
ni wasomi… maana ukiwa msomo wa kweli, huwezi ukafanya hayo wanayofanya wao….’nikasema
huku nikiwa sibandui macho yangu kwake, japokuwa yeye alikuwa akiniangalia na
kugeuka huku na kule.
‘Vijana wetu hawo wanaojiita wasomi, wanaweza kutumia
karatasi na kalamu vibaya, bila kujua madhara yake baadaye,…imefikiwa wakati
sasa mwenye haki anadhulumu kwa kutumia karatasi na kalamu, kwa vile huyo mtu hajui
sheria,au hata kama anajua kidogo, lakini ulaghai unaweza ukapita chini kwa
chini , watu wakatafutwa, na hadaa ikatumika, na haki ya mtu ikapotea hivi
hivi, tumeyaona hayo mara ngapi yakitendeka…tena kwenye kaya zako mwenyewe…’nikamwambia
mjumbe.
‘Kama nilivyokuambia hayo kama yatakuwepo, tutayaangalia
kisheria, …na udhaifu huo upo, lakini mwisho wa siku tunakuja kusuluhisha,
yanakwisha, au sio…hata kama yalitokea kwangu, lakini mimi kama mjumbe,
nilijitahidi tukayaongea kwa heri, yakaisha, na ndivyo ninavyohitajia iwe
hivyo,…lakini kwa sasa….naona nikumbie wazi moja kwa moja, kuwa sisi watendaji
wakijiji, tumeonelea, ili kuleta sluhu ya hilo …. unahitajika utoke humu kwenye
hii nyumba, ili iwe mikononi mwa wahusika…’akasema.
‘Hawo wahusika ni akina nani?’ nikamuuliza huku nikiwa
najaribu kuangalia nje japokuwa sikuweza kuona huko nje, lakini kwa hisia
nikawa nawachora hawo waliomtuma, na hawo wahusika aliokuwa akiwamaanisha huyo
mjumbe, huenda wapo huko nje wanasubiria.
‘Ni familia ya merehemu, …wao ndio wahusika wa muda, ambao watahakikisha kuwa mali za
marehemu zipo kwenye usalama kabla swala la mirathi halijatangazwa, na wao
hawana nia mbaya, wanachohitajia ni kuwa mali zote zinazotambulikana kisheria
kuwa zilikuwa na za marehemu ziwe mikononi mwao ili baadaye kila mwenye haki
yake apate..’akasema mjumbe akiniangalia machoni, mimi hapo nikawa kimiya
kumsikiliza na hapo akapata mwanya wa kuongea zaidi, akasema;
‘ Kwa mfano marehemu alikuwa, na mtoto mdogo, ….na pia
alikuwa na mke, na walikuwa na mali zao, kwasasa, baada ya msiba, tunasema ule
`ubia’ tunaweza kutumia neno hilo, ingawaje linaweza lisiwe na maana ya moja
kwa moja,…`ubia’ nikiwa na maana makubaliano ya ndoa, mahusiano ya ndoa
yliyokutanisha watu wawili, wakapata mtoto, au watoto,…hayo sasa yamevunjika…’akatulia.
‘Kama huo ubia haupo tena, ni lazima kuwe na masuluhisho….ili
kuelewa ni vipi hatima ya baadaye, tukiangalia mke, mtoto na mali zao….na hivyo
vyote kimila, kisheria vinatakiwa visimamiwe, na watu waka karibu, ambao ni
familia…na familia hapo tuna maana, baba na mama, au ndugu wanaohusiana na hiyo
familia…’ akatulia kidogo.
‘Tukiangalia kwa hapa, wanaohusika sasa ni ndugu, kaka wa
marehemu, wao ndio wapo karibu na familia hii, maana wazazi wao hawapo….umenielewa
mzee mwenzangu?’ akauliza.
‘Nakuelewa sana,…na hilo silipingi kwa msingi huo…kama kweli
lina lengo jema,..’nikasema na hapo akatikisha kichwa akitabasamu ,
akijiaminisha kuwa huenda nimelainika kwa maneno yake, halafu akasema.
‘Kwa maelezo hayo, na kwa vile umenielewa,…ni kuwa basi,
mtoto, mke wa marehemu na mali yote, vite hivyo vinahitajika kuwa mikononi mwa
hiyo familia, na hilo nafahamu sana kuwa wewe unalijua vyema, hayo unayatambua
vyema mzee mwenzangu, tusitake tukosane kwa vitu vilivyo wazi…’akasema.
‘Mjumbe,…neno kukosana kwa sasa halipo,..ila mimi
nakushangaa wewe unalitamka sana, kuonyesha kuwa huenda umekuja kwa lengo hilo.
Mimi sihitaji shari, wala kukosana na mtu, maana baada ya arubaini ikiisha,
mimi nitakwenda kwangu, na kumuachia mwenye mali hizi …mali zake…sasa wewe
mjumbe naona unavutika kirahisi kufanya yale utakayokuja kujijutia baadaye…’nikaongea
kuhitimisha.
‘Mjumbe…..kwanini watu wanakuteka kiakili, ukasahau majukumu
yako, ukasahau ile busara yako…, ndio maana kwanza nilikuuliza ni nani
aliyejenga hii nyumba, ukasema ni mama wa hii nyumba, na aliijenga kuanzia
mwanzo hadi mwisho ukishuhuda wewe mwenyewe kwa macho yako, mumewe kipindi
hicho hakuwepo,…kwahiyo kivitendo na kihaki, hizi sio mali za urithi, ….labda
hapo tuliongee kivingine lakini sio mali zinazohitajika kuweka kwenye meza ya
urithi…sijui mjumbe hapo tupo pamoja…?’ nikamuuliza.
‘Tusirejeshe mazungumzo nyuma, hayo yatakuja baadaye, kama
kuna utata wowote, mimi sioni kama kuna tatizo hapo…kwani baadaye ndipo tutajua
hiki ni cha urithi, au sio cha urithi, wewe unafanya haya mambo yawe magumu,
yaonekane kuwa kuna tatizo,….hapa hakuna tatizo kila mtu anajua kuwa hivyo
inavyotakiwa iwe ndivyo ilivyo, sheria zipo wazi, na sisi ni viongozi,
tutahakikisha hilo linatendwa kisheria,…kama mali hii ni ya mjane, haipo kwenye
kundi la urithi, hilo tutakuja kulisimamia, na hapo huenda ikahitajika kwenda
mahakamani kama kutakuwepo na kutokukubaliana.. kwanini mzee mwenzangu hutaki
kunielewa’akasema.
‘Mjumbe, sijasema sitaki kukuelewa, nakuelewa sana, ndio
maana nikajaribu kukumbusha mambo ambayo ni muhimu sana,….nahisi , na hili
ndilo linanifanya mnione kuwa ni mtata. Nakuona kabisa kuwa wewe unafuta
matakwa ya watu ambao nia yao sio njema, kwani nawajua vyema hawo watu na
malengo yao, na nini wanakusudia kukifanya…na sio kihisia bali wao wenyewe
wamenihakikishia hivyo, kuwa wanataka kumiliki mali zote za marehemu na mjane
hana chake, hivi wewe mjumbe hayo yangetendeka kwa binti yako ungelikubali?’
niiamuuliza huku nikimwangalia na yeye akawa kama anakwepa kuniangalia machoni
moja kwa moja.
‘Mzee mwazangu, tusitake kupotezeana muda, mimi kama mjumbe
nitahakikisha kuwa haki ya kila mtu inatendeka, na ikishindikana tutalipeleka
hili swala mahakamani, na mimi kama mjumbe nitatoa ushahidi wangu, kama
nilivyoona, kama mjumbe, ….kwahiyo sioni tatizo lipo wapi, sheria zitamlinda
kila mtu bila kubagua …wewe toka kwenye hii nyumba ya watu, na kabidhi kila
kitu kwa wanafamilia ili kuepusha shari, maana wenyewe wanakuona kama mvamizi
wa mali za marehemu….’akasema mjumbe.
‘Mjumbe, kwanini unatekwa kimawazo na hawa watu…?’
nikamuuliza nikimwangalia kwa makini, na kabla hajajibu nikasema;
‘Mjumbe, kabla ya haya tulishawahi kuongea jinsi gani watu
wanavyokuja kuchukua mali za marehemu, na kuwatelekeza wajane na watoto wao, na
wewe ukaahidi kuwa hilo halitaweza kutokea kwenye kaya zako, ….unakumbuka
mjumbe?’ nikamuuliza na mjumbe akaangalia saa na kusikiliza kelele za watu
wakipiga ukelele kumuamrisha nitolewe nje.
‘Mjumbe nakukumbusha pia kuwa mke wangu ameuwawa ndani ya
kaya zako na kundi linalojifanya kuwa linapambana na wachawi,…na hukuchukua
hatua yoyote, na hilo lilikuwa moja ya ahadi zako kuwa utapambana na watu
wanaowazalilisha wazee kwa imani zao haba za kishirikina, unakumbuka hilo
wakati unapita nyumba hadi nyumba kuomba ujumbe wa nyumba kumi, wenzako wote
tulikataa hilo jukumu japokuwa tuna uwezi zaidi yako…?’ nikamwambia na hapo
nikawa kama nimemkasirisha.
‘Mjumbe siku tukio lilipotokea la kuvamiwa nyumba yangu,
niliitwa nikaambiwa kuwa unanihitaji, kwa vile mimi ni mmoja wa wazee wa kijiji,
na nilijituma kama kawaida yangu kuja kwako, kumbe ni uwongo, kumbe ilikuwa
mbinu ya kunitoa mimi kwenye nyumba ili watu hawo, wahalifu wafanye lile
walilokusudia, na huenda wewe ulishirikishwa maana kwanini siku hiyo ulitafuta
kisngizio cha kutokuwepo nyumbani, …huenda ulijitungia safari za ajabu ajabu
ili hilo tendo litokee, …ninakuonywa mjumbe, kuwa hayo yote sisi raia tunao-onewa
tunayaona….’nikasema.
‘Hayo ni dhana yako potofu ….ni mawazo yako haba, na hayana
ushahidi wowote, na hayahusiani na hili, mimi kama mjumbe nafuata sheria, wewe
hukustahili kuzuia hii nyumba, kwa vile huna haki yoyote, wenye haki hiyo ni
wanafamilia na kama mjane angelikuwepo hapo, labda angelikuwa na mamlaka hayo,
lakini sio wewe…mjane, mtoto wote wapo kwa familia husika kwanini hawi
hukuwazuia,…sasa hivi unakuja kuzuia mali….huoni hapo unakuwa mtata!’akasema
mjumbe
‘Mjumbe mimi nilikuwa naishi hapa na wanafamilia wa hii
nyumba, na walinikubali kama mzazi wao, na hata walifika kwako wakanitambulisha
kwako hivyo, na hata baada ya hujuma ya kumuua mke wangu na kuchoma nyumba
yangu ilipotokea mke wa marehemu alikuja kwako…oh, alikuelezea ulipofika hapa
kuwa mimi nitaishi naye kama baba yake…..je umeyasahau hayo?’ nikamuuliza.
‘Ndio aliniambia na pia alifika kwangu, hilo silikatai,
lakini hilo linahusiana vipi na hii nyumba na mali za marehemu?’ akauliza.
‘Ni kwasababu mimi kama mzazi wao, nina haki ya kuhakikisha
kuwa mali zao zinakuwa kwenye usalama hadi hapo arubaini itakapokwisha na hadi
hapo mumiliki halali wa mali hizi ikiwemo hii nyumba an duka watakapofika, na
yeye ndiye atajua ni nini cha kufanya…natimiza haki yangu kama mzazi, …na hili
uliangalie kwa macho mawili, kuwa hata wewe una watoto, linaweza likatokea
kwako, je utakaa kimiya, ukiona kuna watu wanataka kumdhulumu binti yako?’
nikamuuliza, na mara mlango ukafunguliwa kwa fujo, akaingia askari mgambo wa
kijiji na vijana wengine wakafuatia baadaye.
‘Mjumbe tumeingiwa na wasiwasi, ..tunaona huyu jamaa asije
akakufanya vibaya, …je tufanye kazi yetu, maana huyu jamaa ukienda naye kisiasa
hutamuweza, …tupe nafasi tumtoe nje, hata kama ana nguvu za giza, sisi
tutazimaliza…..’akasema mmoja wa vijana mwenye mwili uliotuna na mikono ilikuwa
imejaa misuli.
Nilimwangalia mjumbe kwa makini, nikusbiri kauli yake…ingawaje
nilijua hatakuwa na jipya, hapo nilikuwa kwenye vita ya kujihami, na panga
langu lilikuwa vyema mkononi, sikuwa nimewaangalia hawo watu, nikatulia.
‘Kwa mara ya mwisho nakuomba utoke humu ndani…’mjumbe
akasema, nikahema na kutabasamu nikasema;
‘Kama nilivyokuambai mjumbe, mimi nalinda mali za watoto
wangu, ….kama mlinzi halali, na kama mzazi wao sitaweza kutoka hapa hadi hapo
mama wa nyumba hii, ambaye ndiye ndiye mjenzi, ndiye mumiliki halali, aliyejenga kwa pesa
zake….’nikasema na kabla sijamaliza, hawo jamaa wakacheka kwa dharau, hata
mjumbe naye akaungana nao.
‘Mzee mwenzangu unajua mwanzo nilikuwa nakusikiliza tu, ili
kujua mawzo yako yamelenga wapi, hivi kweli unaamini kuwa huyo mwanamke
alijenga nyumba hii kwa pesa zake, …alikuwa akifanya kazi gani hadi akapata
hizo pesa, huwezi kujiuliza maswali kama hayo…Mzee mwanzangu hujajiuliza
maswali mengi kuhusiana na hili, na kutambua kuwa kuwa hizo pesa zilikuwa za
marehemu….!’akatulia huku akishika kichwa kwa kidole chake.
‘Huyo marehemu alizipata wapi hizo pesa, hebu na wewe
niambie, kwasababu marehemu tulikuwa tukiishi naye hapa siku zote, na
aliondoka, huko alipokwenda na hakukaa kwa muda mfupi na kureejshwa hapa ,
kukabiliana na mashitaka ya wizi,…..na akafungwa, na mnakumbuka akiwa
kifungoni, kulipita muda, na ndipo huyu binti, mwenye nyumba hii, akafika, toka
huko mjini…na kuanza ujenzi wa hii nyumba, sasa nimbieni huyu marehemu alipoletwa
hapa alikuja na hizo pesa, au aliwahi kuwaambia kuwa alimuachia mkewe pesa na
ndizo hizo alizokuja kujengea hii nyumba, au mnafikiria hivyo tu…?’
nikamuuliza.
‘Hayo maswala yalishamalizwa mahakamani, na walioibiwa pesa
zao, walishasamehe, lakini pesa hazikuwahi kurejeshwa, ina maana hizo pesa
zilikuwa wapi?’ akaniuliza, na wenzake waksema;
‘Alibakia nazo mkewe…’wakasema.
Mimi nikachekwa kwa dharau na kusema,;
’ Ama kweli jambo msilo lijua ni kama usiku wa giza, hivi mnakumbuka
kuwa huyu binti aliwahi kusakamwa kwa hilo kuwa haya maendeleo aliyoyaleta kwa
kujenga nyumba na miradi yake ni kutokana na hizo pesa za wizi, na wale
waliokuwa wameibiwa, wakafuatilia lakini baadaye walikuja kugundua kuwa sio
hizo pesa zao….kwanini hawakumshitaki huyo binti, kwa kupatikana na pesa za
wizi, kwanini hamjiulizi hilo…’nikawaambia.
‘Hahaha…sasa unataka kusema nini, huo ulikuwa ni ujanja wa
mwanamke, aliwahadaa tu, lakini kiukweli hizo pesa zilikuwa za mumewe….’akasema
mmoja wapo.
‘Mjumbe nilishakuambia ukianza kuongea na huyu mtu kisiasa
hutamuweza, sisi tunamfahamu sana, dawa yake ni kumtoa kwa nguvu…’akasema yule
jamaa aliyejazia kifua, na alionekana akitoa jasho la hamasa, akiwa na rungu
lake mkononi.
‘Naona tumefunga mjadala, nakuamrisha utoke humu ndani, na
unikabidhi ufungua wa nyumba na wa duka…’mjumbe akasema.
‘Mjumbe msimamo wangu umeshausikia sijabadili msimamo wangu,
sina zaidi la kusema…’nikasema
‘Narudia tena,….ili kuepusha shari tunakuomba, tunakuamrisha
utoke humu ndani na utukakabidhi ufungua za nyumba na duka…’akasema mjumbe ,
mimi nikaa kimiya, akawageukiwa wenzake na kuwaangalia kila mmoja kwa wakati
wake.
‘Kwa mamlaka niliyopewa na serikali ya mtaa, kuwa mtu
anapokuwa mkaidi kama huyu, tunaweza kumshawishi kwa njia nyingine iliyo salama
ili tuepushe shari, naombeni mmtoe huyu mtu, kwenye hii nyumba na mchukue
funguo ili tuzikadhi kwa wenyewe,…’akasema mjumbe na kutoka nje.
Hapo kazi ikaanza, sikukubali, na wao walikuja kutambua kuwa
mimi sio lele mama kama wanavyoniona kuwa ni mzee, kwani kwa dakika kumi tu,
wote walikuwa hoi…hakuna aliyeweza kunisogeza pale niliposimama.
‘Mjumbe huyu mtu ni mkaidi, inabidi tutumie nguvu…’akasema
mmoja wapo
‘Kama mumeshindwa, ngoja niwaongezee nguvu mpya…’akasema
mjumbe na wakaingia vijana wengine na jumla yao wakawa watu saba, na hawa
walioingia sasa hivi waliingia kwa shari, kwani walianza kunipiga na marungu
yao kwenye mabega na magotini, hapo wakanipandisha hasira.
Kila dakika ikipita mtu wao mmoja anadondoka chini,
hajitambui….niliwabana sana, lakini unajua tena uzee, na wao walikuwa wengi, na
sehemu ya tuliyokuwemo ilikuwa ni ndogo, usingeliweza kusogea huku na kule ili
kumkwepa adui,…na walipobakia wawili, wakiwa hoi wakipambana na mimi, wengine
wao walikuwa wamelala chini, wengine wakiwa wamepoteza fahamu,….
‘Na ukumbuke hapo, nilikuwa simkati mtu kwa panga,
nilichokuwa nikifanya nikuwaginga na sehemu ile isiyo na makali…na wale
waliozidiwa walikuwa hawana hamu na mimi, ila hawa wawili walikuwa bado wakaidi….nikawa
napambana nao, na wakati huo nilishapandisha zile hasira za kizamani, kwa
bahati mbaya mmojawapo aliyekuwa kadondoka chini, na nikijua kuwa kapoteza
fahamu, alisimama, bila mimi kumuona…
Nilichosikia ni kitu kama chuma kikigonga kichwani kwangu,
na begani nikasikia kisu kikizama upande wa
kulia karibu nakwapa, hapo nikajua wameniweza, maana maumivu yalikuwa
makali…. Nikaanza kuona vinyota, na
kudondoka chini, huku wakinishambulia kila mtu kwa silaha yake, na sikuweza
kujua nini kilitokea baadaye maana giza lilitanda usoni, nikapoteza fahamu….
NB: Haya niambieni nyie, mkikaa kimiya sawa, hakuna shida..
WAZO LA LEO:
Unapotaka kujua haki za watu, na kutetea haki za watu au pande mbili tofauti,
ni vyema ukasimama kati kati, na kusahau lolote la sehemu hizo mbili
zinazohasimiana, na hapo unahitajika kuwasikiliza wote kwa usawa bila kuingilia
kati, na ujaribu sana kutokusimamia upande wowote, hata kama wewe upande mmoja
unakugusa zaidi.
Kama una jukumu hilo la kusimamia haki, na ukatekwa na imani
za kutetea upande mmoja, ujue wewe ni mkosaji mkubwa sana, na kama kutatokea
uvunjifu wa amani, ujue wewe ndio chanzo, na utawajibika, sio hapa duniani tu,na
kesho kwa mwenyezimungu utaulizwa hilo.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Duh! nimesisimka na nimependa jinsi alivyokuwa akiwapiga kwa panga ...natumai atakuwa hajaumia hapo alivyopigwa na chuma ...nasubiri kwa hamu. Vile vile nimependa wazo la leo ningefurahi kama wengi wangesoma hapa. Ahsante pamoja daima.
Post a Comment