Kipindi cha msiba wa baba yako, nilikuwa nina wakati mgumu
sana, na siku zote nilizokuwa hapo kwenye msiba kwa shemeji , yaani kaka wa
mume wangu sikuwa najitambua. Nilikuwa hapo kimwili, lakini akili, ilikuwa siyo
yangu, nilikuwa kama nimepooza mwili mzima, akili ilikuwa kama imeganda, siwezi
kufikiri zaidi, na kwa hali kama hii mwili ulikuwa hauna mawasiliano na ubongo,
hata kutembea ikawa shida, …ilibidi kuwa na mtu wa kunishikilia kila nilipotaka
kwenda haja…nikawa mtu wa kulala, na skutamani kula kabisa.
‘Huyu sasa ni mgonjwa, ….tusipoangalia tutaita msiba
mwingine sasa hivi….’akasema huyo wifi aliyekuwa akinisaidia . Huyu wifi yangu,
alikuwa ndugu yao wa kike, na kidogo tulikuwa tukielewana, na mara kwa mara
wakati kaka yake yupo hai, alikuwa na tabia ya kunitembelea, japokuwa baadaye
nilianza kumuogopa, kwani alikuwa kama mpelelezi wao, anachukua mambo yetu na
kuyapeleka kwenye familia yao.
Kwa sababu ya mazoea, hayo nilikuwa karibu naye
kuliko ndugu zake wengine, na hata kwenye huu msiba, yeye alikuwa karibu na
mimi, na hata alijitolea kuja hapo nilipotengwa na kushinda na mimi, hakuruhusiwa
kukaa sana, na hata hivyo kwa hali ya kawaida ilikuwa inachosha, palikuwa sio
mahali pa kukaa muda mrefu.
Wifi yangu huyu ndiye aliyekuwa akiniletea chakula, maji, na
hata kunisaidia kwenda haja na shughuli nyingine, na hakuata msaada, lakini
siku zilivyozidi kwenda na yeye akajikuta anachoka, akaanza kulalamika kwa
ndugu zake wengine, hasa kaka yao mkubwa ambaye alionekana kama kiongozi wa
familia yao yote.
‘Huyo sio mgonjwa bwana , …..wakati mwingine ni kujidekeza,
hata hivyo, hiyo tunaweza kusema ni hali ya akwaida ukipatwa na mshituko kama
huo, na inahitajia uwezo wako binafsi kujituma, na ili hilo liondoke,
alihitajia kulia, akilia kwa haja, hali hiyo itatengamaa…..muacheni kama alivyo….muda
utafika atabadilika, akizidi sana, sisi tutajua nini cha kufanya….’akasema huyo
shemeji mkubwa.
Huyo shemeji mkubwa, sikumpenda hata kumwangalia, maana mimi
na yeye damu zetu hazikuendana kabisa, na kila niliposikia sauti yake, nilihisi
mwili ukichemka kwa hasira, na wakati mwingine, nilimuhisi vibaya, kuwa huenda
yeye alitaka mume wangu aje kwake, ili asipate huduma muhimu afe haraka.
Sikumpenda kabisa….na hatuelewani hadi leo.
‘Sasa tufanyeje….maana hata mimi nimechoka, sitaweza kukaa
naye siku zote, na hivi kaka arubaini imebakia siku ngapi?’ akauliza huyo wifi.
Huyo wifi yangu alikuwa kipenzi chao, na alionekana kuwajulia na kuishi
kutokana na mtu mwenyewe, na ndio maana nikawa makini naye sana, japokuwa
nilizoeana naye.
‘Leo ni siku ya ishirini, zimebakia siku kumi, vumilia tu
mdogo wangu,…baada ya hapo, utakuwa huru, na mjane ataamua mwenyewe kuwa anataka
kwenda wapi, ama kwao, au atabakia pale kwenye nyumba ya marehemu, hadi hapo
atakapopata mume mwingine, , kama atakubalia kukaa hapo na kukubalina na
msharti ya familia hatuwezi kumfukuza …..’sauti ya shemeji mkubwa ikasema.
Moyoni nikawa najiuliza hayo masharti ni yapi, maana kama niyakurithiwa mimi siwezi
kukubali…
‘Lakini mimi nijuavyo, wifi ndiye aliyesimamia ujenzi wa
hiyo nyumba mpaka inakamilika, kipindi kaka marehemu yupo jela…yeye alipotoka
nyumba ilikuwa imeshakamilika na yeye kwa vile ni fundi, akawa anafanya
marekebisho ya hapa na pale, lakini aliyeijenga ni wifi.’sautii ya wifi ikasema
na kunifanya nitege sikio vizuri.
‘Wewe, acha kidomo domo chako, hayo hayakuhusu, na nikusikie
tena ukiongea hayo maneno, …..hata kama alisimamia ujenzi, pesa zilitoka kwa
nani na huo ulikuwa ni wajibu wake, maana mwenzake alijitolea hadi kupelekwa
jela, sasa yeye angekaa tu….yoyote yule angelifanya hilo alilolifanya,
vinginevyo angelikuwa ni mnyonyajii tu…wewe kwa akili yakol pesa hizo za ujenzi
zilitoka wapi?’ akauliza shemeji.
‘Wanasema ndio hizo pesa alizoiba kaka…..’akasema wifi.
‘Aliiba…! wewe ulikuwepo akiziiba, nyie hayo maneno ya
kujiropokea yatawapeleka pabaya…unajuaje kuwa aliziiba, na kama aliziiba,
kwanini wahusika baadaye wakaamua kumsamehe….walifanya hivyo baadaya kuona
hawana ushahidi, walioiba walikuja kugundulika baadaye….huyu ndugu yetu
walimpachika tu, na kwa vile alikuwa na tamaa, akajiingiza kichwa kichwa,
lakini ….tuyaache hayo, ila nakukanya, tena usikie hili ninalokuambia, achana
na tabia ya kuropka ovyo, itakuponza…’akasema huyo kama mkubwa.
‘Kaka naye bwana, yamekuwa hayo,..hapa sisi tunaongea tu,
siwezi kuyaongea hayo kwa watu wengine, mimi niliongea tu, kama nilivyosikia,
au hutaki tena niwe ninakuambia wanayosema watu…kama ni hivyo siongei tena hayo
mambo….’akasema huyo wifi.
‘Ukiongea tena,…maneno kama haya, yakasikika kwa wabaya
wetu,… ina maana hata hayo aliyokuachia ndugu yako hutayapata tena, sasa hivi
lile duka ni lako,…utaliendeleza, tutakuongezea mtaji, na hutakuwa na shida
tena, unakumbuka jinsi kaka yalko alivyokuwa akikupenda, ndio maana kakuachia
duka, ….hebu fikiria upendwe vipi….tulizana, tusikilize sisi kaka zako, utaishi
maisha ya rana na utapata mume ambaye hutapata shida….tutahakikisha kuwa mume
atakaye kuoa anakufaa, ndio maana sijawakubalai wale wote waliotaka kukuoa,
nawafahamu sana, wewe tulia, nisikilize mimi…’akasema kaka mtu.
‘Nashukuru sana kaka kwa kunijali, na kwakweli nina machungu
sana, kwa kuondoka kaka yangu….ina maana sitaweza kumuona tena,…..na ule ulevi
wake,….unajua kaka, kaka yetu yule, hata alewe vipi, akiniona mimi,
atatulia,…na atanipa kila ninachokitaka, ndio maana hakusita kuniachia hilo
duka kama urithi,…huko alipo najua atakuwa peponi kwa wema wake huo…’akasema
wifi.
Kauli hiyo iliniweka njia panda, ina maana kweli mume wangu aliandikisha
vitu vyangu, ….japokuwa vilikuwa vyetu, lakini nyumba duka, nilijenga kwa pesa
yangu, ….alitakiwa kushirikiana na mimi kabala hajafikia hayo maamuzi,
haiwezekani, hapo kuna kitu kimejificha, lakini nitajuaje hayo, na kwanini
wanajiamini hivyo…..
Hayo yote nilikuwa nayasikia kama ndoto, japokuwa nilikuwa
macho, na kuna wakati usingizi ulikuwa ukinijia na nikisikia sauti yao
wakiongea, usingizi unakuwa wa mang’amung’amu, nawasikia kama vile wanaongelea
kwenye sikio langu,…na baadaye nikipitiwa na usingizi wa kweli, na nilipokuwa
kwenye usingizi wa kweli nikawa naota, kwanza ilianza kama watu wanaongea, na
baadaye ikasikika sauti ya mtu ninayemjua, niliposikia sautu hiyo, nikashituka,
na nilitaka kama kukimbia, lakini nipo usingizini, sauti hiyo ilinifanya
nishituke, nahisi ni kwa vile ubongo ulishakubali hali halisi kuwa mume wangu
keshafariki, kwahiyo ukisikia sauti yake, ni lazima ushituke, ilikuwa ikisema
kwa sauti ya mwangwi:
‘Nilikuambia mke
wangu….kwa hali kama ilivyokuwa, nisingeliweza kupona…nikakuambia mke wangu unahitajika
tubadili hiyo hati haraka, kabla hali haijakuwa mbaya, sasa umechelewa,
‘Mke wangu nilijua
kabisa kuwa nimetenda vibaya, kuandikisha mali yote kwa jina langu, najua
ulikubali kwa vile ulikuwa uannipenda, ..je huoni kuwa nitateseka kwa kosa
hilo,…kwani sasa nimeshakufa na watu wakiona hizo hati zikiwa na jina langu, hawatakuamini
tena, watakusumbua, hasa ndugu zangu, nawafahamu sana …nawafahamu sana ndugu
zangu kwa ubinfsi wao,
'Mke wangu….nilikuambia kuwa ufanye hima-hima, kubadili hizo hati
nikiwa badi hai, sasa umechelewa mke wangu, Napata taabu kwasababu hiyo mke
wangu.….’sauti ikasikia kichwani mwangu
na muda huo kichwa kilikuwa kikiuma sana japo nipo usingizini.
Nikashika kichwa nikiwa ndani ya usungizi, na kutamani
kupiga ukulele, na nilitamani niwaambie hawo watu wengine wanaoongea wanyamaze,
kwani sauto zilikuwa zikiingiliana, na nilishindwa nimsikilize nani, kulikuwa
na sauti za watu wengine, na hapo hapo kuna sauti hiyo inayokuja kama mwangwi ,
ambayo ni sauti ya mume wangu…ile sauti ya mwangwi ikawa inaendelea kuongea;
‘Mke wangu,….nilikuambia
ukumbuke kubadili hati ya nyumba, mke wangu nilikusisitizia kuwa ufuatilia
kubadilisha hati za mali zetu ikiwemo nyumba na duka, ilikuwa ni muhimu sana….sasa
mke wangu umechelewa, mke wangu umechelewa…., nilikuambia ukumbuke kubadili hizo
ili usipate taabu…sasa umechelewa, sasa umechelewa…,…mke wangu kwanini sasa
unaona, kwanini sasa…..umechelewa, sas mke wangu umechelewa…..’ Haya maneno
yakawa yanajirudia rudia kichwani kwangu, mpaka yakawa kama yanapandana pandana.
Hata sikuelewa ni kitu gani, kichwa kikawa kinaniuma, na nikahisi mwili ukiwa
sio wangu tena….na hapo nikapiga ukulele wa nguvu. Nikainuka na kusimama,
sikujua nipo wapi, sikujijua tena mimi ni nani,kwani kilichotokea hapo, ilikuwa
ni vurugu, na sikuelewa ni nini kiliendelea baadaye…
Nilizindukana siku ya pili yake asubuhi na mapema,
nikajikuta nipo peke yangu, nimefungwa kamba miguuni na mikononi, nikajaribu
kujifungua lakini sikuweza kabisa, walikuwa wamenifunga kama kuni, nimenyooka
moja kwa moja, na kwa muda huo mdomo, koo vilikuwa vimekaua kabisa, nilikuwa na kiu, na sikuona mtu wa kunisaidia,
nikaanza kujitikisa tikisa ili kama kuna mtu karibu aje kunisadia, lakini
walivyonifunga ilikuwa vigumu sana, nikawa najiviringisha hapo chini,
Nilikaa katika hali hiyo , nikiteseka kwa maumivi mwilini,
kuchoka, kiu, maumivu ya zile kamba ambazo zilionyesha kabisa kukaza na hata
sehemu zile zilizopita kamba zilionyesha kuvimba, na niliona ajabu kuhisi hata
njaa, maaan muda nilikuwa sili chakula, wakiniletea chakula naonja tu nakusema
sijisiki kula, na waoo hawakuwa na ushawishi wa kunifanya nile….nilikaa katika
hali ile kwa muda mrefu hadi watu walipoanza kuamuka na bahati mtu mmoja akaja
kuchungulia pale nilipolala, alichungulia kwa wasiwasi, akiogopa;
‘Sijui kama huyu mtu kazindukana, maana mimi naogopa hata
kuingia, na muda mrefu hajala, anaweza akafa kwa njaa….’ilikuwa sauti ya kike
‘Usije ukaingia humo ndani, akikurupuka hapo ndani anaweza
akakata kamba zote, na kubadilika kuwa mbogo, na akifanikiwa kuchomoka humo
ndani akakimbia, hamtapata tena, atakimbia hadi kwenye mto, au ziwa, au bahari
azame moja kwa moja, naona kakumbwa na shetani, kwani hiyo sauti ni ya kiume,
na huyo ni jini mwanaume anayeitwa jinni makata….’ikasema suti ya kike, sikujua
ni ya mwanamke gani.
‘Hiyo sauti ya kiume inafanana na sauti ya mdogo wangu, huyo
marehemu…’ikasema sauti ya mwanaume.
‘Ndio ilivyo, mara nyingi hawa mashetani wakiwaingi wanadamu
wanakuja na sura, sauti na umbo tofauti na kwa yule mtu mnayemfahamu , hasa wale
marehemu. Na huyo ni kaigiza sauti ya mume wake, kuleta ujumbe fulani.
‘Sasa atakaa hivi mpaka lini…?’ ilikuwa ile sauti ya kike ikiuliza.
‘Subirini kidogo, hiyo dawa ifanye kazi, …na cha muhimu, ni
kutokumkubusha lolote litakalomuathiri kiakili…kwa sasa, , na kama mlivyomsikia
kuna mambo aliagiziwa na mumewe, akiwa hai, na huenda huyo mjane hakuwahi
kuyatimiza, ….kama kuna mambo aliagizwa na mumewe, inabidi ayatimize, la sivyo
hali hio itakuwa ikimtokea mara kwa mara….’sauti ya kike ikasema.
‘Kuna lolote mnalolijua zaidi ambalo mkewe alitakiwa kulifanya
na mumewe lakini hakuweza kulitekeleza, au hayo yalikuwa siri ya watu
wawili,….naweza kulitafuta, lakini sioni haja kwasasa, kama mnalifahamu ni bora
mkalifuatilia…nyie mnaweza mkalitekeleza kwa niaba yake’akasema huyo mwanamke
mgeni
‘Hakuna , tujuavyo sisi hakuna, maana mimi nilikuwa na
marehemu hadi anakata roho, hakuwahi kuniambia jambo zaidi ya kuwa tuitunze
familia yake…., kwahiyo hayo aliyoropka, nahisi ni hisia zake kutaka mambo yawe
hivyo anavyotaka yeye…na sisi kama wanafamilia hatuwezi kukubaliana nayo maana
tulikuwa na marehemu hadi anakata roho, zaidi ni yale ya kawaida ambayo
tutakwenda kuyatekeleza,na mengi ya hayo tulikwisha kubaliana na marehemu akiwa
mzima, haiwezekani aje kuyasema baadaye….' akatulia na kuwa kama anawaza jambo fulani.
'Labda kama aliyasema kwa shinikizo,
maana huyo mwanamke na watu anaoishi nao, sio wa kawaida, inawezekana
walimfanay watakavyo ili afuate masharti yao, na hilo tuliliona, ando maana
tukawahi kumchukua mdogo wetu mapema….’sauti ya kiume ikasema…nahisi alikuwa
shemeji mkubwa.
‘Sasa nyie mnataka mimi nifanye nini, …maana huo ndio
ukweli,…..na ukweli mwingine huenda anaujua mke wake vizuri kuliko hata nyie, …je
tumsubiri, ili tuje tumuulize, au tumreejshe huyo makata aongee mwenyewe, ili
atumabie ni kitu gani anahitajia,…..’akauliza sauti ya kike.
‘Hapana, hatuwezi kuvumilia hiyo hali tena, fanya vinginevyo
unavyoona wewe , ilimradi huyo shetani aondoke…’sauti ya kike ikasema.
‘Lakini kama mnataka iwe tofauti, kunahitajika mambo mengi,
makafara ya kuchinja, mlete, ngombe, kondoo na mbuzi wa rangi tofauti…..na ili
kumtoa huyo shetani kichwani mwake, inabidi haya yakafanyikie baharini, na
….hili ni hatari, maana anaweza akatuzidi nguvu, akakimbilia baharini, na
kupotea moja kwa moja….lakini tukifanya kama tulivyoagizwa, hiyo ni kazi ndogo
sana, maana hiy ndio fani yangu…’akasema hiyo sauti ya kike.
‘Sisi tunaomba ufanye kila iwezekanavyo, hali hii
iondoke,…na kama ikishindikana basi , ni bora tumpeleke kwao, japokuwa nasikia
kwao hawaelewani….Huyu mwanamke ni mkorofi kweli, hebu fikiria tangu afike hapa
toka huko alipokuwa kakimbilia, nasikia hana habari kabisa na familia yake,
…mama yake anahangaika lakini yeye hamjali, baba yake ndio kabisa, nasikia
hawaongei,…sasa hicho kiburi hatuwezi kukivumilia kwenye familia yetu, sisi
tutakiondoa au vinginevyo aondoke….’sauti ya kiume ikasema.
Nilishangaa sana kusikia hivyo, kuwa mimi sielewani na
familia yangu, kwani mimi na familia
yangu, yaani baba na mama yangu tulishamaliza mfarakano wetu, na nilikuwa mara
kwa mara nakwenda kuwatembelea japokuwa baba alikuwa bado ana hasira na mimi,
lakini sio kiasi cha kununiana, na mara moja moja alikuwa akinitembelea, na
tulikuwa tukiongea vizuri tu.
Kitu ambacho nilikuwa na uhakika nacho ni kuwa Baba alikuwa
hampendi mume wangu, kwani anadai kuwa ni jambazi, na jambazi hawezi kuishi na
mtoto wake. Na kila anapofika akimkuta yupo, hakai, anasalimia juu kwa juu na
kuondoka, ….Mara nikasikia huyu mwanamke akisema;
‘Sawa mimi nawasikiliza nyie, lakini je baba yake huyu
binti, huyo baba mnayesema aiansihi naye, mumeongea naye , maana hapa kuna kazi
tunahitajika tukaifanye ndani ya hiyo nyumba ya marehemu, ….na kuzunguka miradi
yote ya marehemu ili kuondoa
yaliyofungwa humo, na kuyazindika ili yasiingiliwe na mtu mwingine tena?’
Akauliza.
‘Yule sio baba yake, yule mzee hana familia, yeye kwa upweke
wake, maana mke wake aliuwawa kwa vile ni mchawi….yeye akona sehemu ya
kujisitiri ni kwa mdogo wangu, sasa mdogo wangu hayupo, na sisi hatuwezi
kumsitiri, maana hatuelewani naye, …kwa mtaji huo hana jinsi yeye atakwenda
kuishi kwenye nyumba yake, ….japokuwa haijamalizika….’ikasema sauti ya kiume
‘Sasa kwanini hataki kuondoka…?’ sauti ya kike ikauliza
‘Sisi tunamshangaa, kwani aliyasema hayo mbele yangu, ….na
kasema hawezi kutoka hapo kwenye hiyo nyumba ya marehemu, hadi hapo
kitakapoeleweka, akisisitizia kuwa nyumba hiyo na mali zote ni za mjane,….huyu
mtu ana akili kweli, toka lini mali ikawa ay mke, mbona hazungumzii watoto. Mke
ataolewa, na mume mwingine kwenye ukoo mwingine tofauti, ina maana hiyo mali
tapelekwa huko, na hawo watoto wa marehemu watabakia na nini….ndio maana
tunahitajai kuilinda kwa ajili ya mtoto wa mrehemu, kwani kuna leo na
kesho…mimi yule nimemwambia kuwa kwangu kwangu kafika…simuogopi hata siku moja,
mzee mwenyewe kajichokea, …..anatafuta mada
kesi’sauti ikasema, alikuwa ni shemeji mkubwa.
‘Huyo anahitaji kuwekwa sawa, ni kazi ndogo kwangu,
nitamlegeza viungo vyake, na mwishowe atalainika, mtaweza kufanya lolote
mnalolitaka, maana inavyoonekana ana ulinzi mkali,…lakini mimi nitausambaratisha,….hilo
niachieni mimi, nitaona jinsi nitakavyofanya, kwahiyo yeye ndio yupo kwenye
hiyo nyumba peke yake si ndio,?’ akauliza.
‘Yupo na hataki kutoka, na hataki mtu kuingia kule…nahisi
yale waliyomfanyia mdogo wangu wamemfanyia na huyo mzee, ndio maana huyo mzee
anakuwa upande wa huyo mjane sana, mpaka anasahau kabisa mambo ya kimila,
mwenyewe alishawekwa sawa na mkewe, na isingelikwua watu kumuua, kijiji hiki
kingeharibika kwa mambo yake…..hutaamini, yale yaliyotakiwa kufanyika baaada ya
msiba, anayapinga, eti yamepitwa na wakati….huyu mzee balaa kweli, anataka
kutuletea nuksi kwenya familia yetu…..watu kama hawa tukiwakumbatia
watakiharibu kijiji chetu..’akasema.
‘Sasa vyovyote iwavyo, kuna mambo yanahitajika kufanyika
ndani ya hiyo nyumba,….kuondoa hiyo mikosi, kuondoa hayo mazinduko yaliyowekwa,na
kama kuna lolote lilifanyika, liondolewe, ……na hayo ni lazima yafanyike, ndani ya hiyo
nyumba, … sasa niambieni tutafanyaje kama bado huyo jamaa yupo humo ndani, na je
yupo tayari kuturuhusu tufanye mambo yetu, hata kama akiwemo humo ndani?….na
kama unavyosema kuwa anazuia watu wasiingie, huyo mtu huenda keshajua ni kitu
gani kinakuja mbele yake…maana inavyoonekana ana mambo yake…mimi hapa namuona
na watu wengine, hayupo peke yake kama mnavyodai…?’ akawa kama anauliza.
‘Sisi chakufanya, ….kwanza tumeshamuona mjumbe, na sijui
kama mjumbe ataweza kumshawishi, maana hata mjumbe mwenyewe anamuogopa huyo
jamaa, mimi sijui wanamuogopea nini yule mzee, unasikia mtalaamu, huyo mzee
hana lolote, …kama alikuwa na miguvu, ni hizo enzi zake, kwa hivi sasa keshajichokea,….njaa
na shida vime mmaliza kabisa,…. hawezi kabisa kupambana na vijana….lakini
tunamuheshimu tu, …sasa la kufanya tutamuitia polisi,…ili tusionekane wakorofi,
kuwa tumejichukulia sheria mkononi..’akasema na kuangalia nje.
‘Fanyeni hivyo haraka….’ikasema hiyo sauti ya kike, huku
akipiga chafya mfulululizo.
‘Tutafanya hivyo mtaalamu kwa vile tuna sababu muhimu, kuwa
anang’ang’ania mali ambayo sio yake,…..mimi mwenyewe nilishaongea na polisi, na
tumewaonyesha nyaraka zote muhimu, na wao wametushauri kuwa, kiutaratibu kwanza
ni muhimu tumwambie mjumbe, na kama mjumbe akishindwa kumtoa, sisi tutafika na
kumshika kwa kosa la kuingilia vitu vya watu, na hilo kosa ni sawa na kuvamia
mali za watu…polisi watafika tu, kwani yupo jamaa nafahamiana naye, nimeongea
naye na yeye kasema hivyo hivyo kuwa huyo jamaa ni mkorofi tu, lakini cha
muhimu kwanza nikuongea na mjumbe. …’akasema.
‘Na mumeshafanya hivyo…yaani mumeshaongea na mjumbe?’
akauliza huyo mwanamama.
‘Mjumbe naye tumeshamuelezea na kumweka sawa,…hana shida,
ila hakutaka tutumie nguvu, yeye mwenyewe kasema atakwenda kuongea naye na huyo
mzee, na nimefika kwake kujua wameonega nini, lakini hayupo, mkewe kasema
mjumbe aliondoka asubuhi hajarudi…’akasema.
‘Sawa fanyeni hivyo, muondoeni hapo kwenye hiyo nyumba kwa
njia yoyote isiyoleta vurugu, maana serikali inaweza ikatuweka pabaya kuwa
tumevunja sheria, na haya mambo yetu hayathaminiki kwenye serikali, japokuwa
watu wake, viongozi wakubwa wanakuja kwangu kuomba niwafanyie mamb hay ohayo
wnayosema hawayaamini….na ni vyema tufuate sheria, ili tuweze kufanya mambo
yetu kwa haraka na kwa amani….’ikasema hiyo sauti ya mwanake ambayo ilikuwa
ngeni kwangu.
Nilivyosikia hivyo, nikaona kumbe jambo jema nikujifanya
kuwa sielewi kitu, hadi hapo arubaini itakapokwisha, na hapo nitajua jinsi gani
ya kufanya,…kwani sikujua wana kitu gani cha kuwafanya wajiamini kupita kiasi,
na je nyaraka hizo wamezipata wapi,….hapo nikakumbuak siku ile nlipofika na
kukuta vitu vimevurugwa vurugwa, huenda walikuwa wakitafuta hati za nyumba na
duka…sikukumbuka kuviangalai vitu hivyo….mungu wangu ina maana
walivichukua,….mbona itakuwa kazi..
Na nilipofikiria hivyo, mara nikasikia sauti ya mume wangu
kwenye ubing ikisema;
‘Mke wangu,….nilikuambia
ukumbuke kubadili hati ya nyumba, mke wangu nilikusisitizia kuwa ufuatilia
kubadilisha hati za mali zetu ikiwemo nyumba na duka, ilikuwa ni muhimu
sana….sasa umechelewa….’
Sikubali, na sijachelewa, nitapigania kile kilicho change
hadi hatua ya mwisho…’nikajikuta nikisema kwa suti ndigo, na akili yangu
ikamkumbuka huyo baba yangu wa kufikia, kuwa wanaweza kumfanya lolote baya mzee
wa watu, na nisingelikubali hilo litokee, kama nikuumizana tuumizane wenyewe,
huyo mzee wa watu keshaumia tayari, wanataka nini tena kwake…
Mara nikasikia watu wakija upande wangu, nikafumba macho
haraka na kujifanaya bado nimelala..
‘Huyu keshazindukana lakini bado hajawa tayari, , …nitampa
hizi dawa, ili akizindukana vyema asiwe na nguvu tena, na wengine muanze hiyo
mikakati ya kuhakikisha huyo jamaa anaondoka kwenye hiyo nyumba,…’akasema, na sauti
yake ikakatishwa na sauti nyingene zilizotoka huko nje, ilikuwa ni sauti ya
kilio kuashiria kuwa kuna mtu mgeni kafika, na anajitambulisha kuwa kaja kutoa
pole. Huwa akija mgeni, huja na kilio, na baadaye anatulia , na kuanza
kusalimia, kwahiyo huyo aliyefika inaonekana hakuwepo toka awali msiba
ulipotokea ,ni mgeni….
‘Oh …tumekusubiri sana, …maana uliondoka mapema sana,
hatutakulaumu maana kazi za watu zina umuhimu wake, lakini najua umeweza
kulifuatilia lile swala letu , kwani hilo ni sehemu ya mambo ya msiba, na lina
umuhimu wake, hebu nipe taarifa, umefikia wapi?’ akaulizwa.
‘Hayo na mambo mdogo bro, tumeshayamaliza, kwa vile kaka
aliweka saini yake..kabla hajafariki, na alifanya hivyo akiwa na fahamu zake
timamu, haikuwa na shida,…,maana kubadili umiliki wa nyumba au eneo achilia
mbali usumbufu, lakini ni gharama kubwa sana, …asilimia kumi ya thamani ya
nyumba unatakiwa kuwalipa watu wasiohusika kabisa….inachukuliwa, na hapo
hujafanya lolote, hujauza hiyo nyumba au….kwahiyo kuna vipengele vyake vingi,
lakini kwa vile sisi wenyewe tunajuana…..tulisaidiana.
Kilachosaidia ni kuwa
kila kitu kilikuwa kimejieleza kisheria, basi hakuna shaka,…tumeshalimaliza
hilo iliyobakia ni utekelezaji tu’sauti ikasema.
‘Mambo si hayo, najua kwako kila kitu kitakwenda shwari,
maana hatutaki kuonekana hatufuati sheria,…na sasa umefika, …au sio,..na kabla
hujaondoka tena hakikisha kila kitu kimekuwa sawa kisheria….
‘Kama utaondoka karibuni,…uhakikishe umekutana na viongozi
wa serikali na kuthibitisha haya yote kwao, ili wasije wakatuona sisi ni wababaishaji,
na kuanzia sasa tunakukabidhi hilo swaia,la, ni lako….familia hiyo ni yako, mtoto
huyo ni wako, kama mama yake hatapenda kukaa na wewe, basi yeye tutamruhusu
aondoke, lakini mtoto haondoki, maana hiyo ni damu yetu, na huo ndio mshiko
wetu kisheria na kimila ….’ikasema shemeji mkubwa.
‘Hilo halina shida, ….mimi nitaweza kuishi nao bila shaka,
kwanza nina likizo ndefu kidogo, naweka mambo yangu sawa, kama mnavyoona
nimekuja na….na mwenzangu, yeye ni mwanasheria pia…tulikuwa naye huko chuoni
japokuwa nilimtangulia, na tukaona kuwa tunaweza tukaishi pamoja, mategemeo
yetu ni kuishi kama mke na mume.’akatulia
kidogo, akimgeukia mwenzake ambaye alikuwa katulia akiangalia chini.
‘Kwahiyo unasema huyu ni shemeji yangu…oh, hiyo kama
umeitamka kama una mashaka vile, kama hutamuweza mimi ananifaa sana huyu..!’
akasema kaka mtu, ikawa kama utani, wakacheka, nay eye akaendelea kuongea kwa
kusema;
‘Safi kabisa, maana famiia yenu itakuwa ya wanasheria, na
tunawahitajai sana kwenye familia yetu kongwe, maana tukiwa na watu kama nyie,
tuna uhakika hakitaharibika kitu, karibu sana shemeji…..japokuwa kama kaka
mkubwa, hilo neno shemeji halijabarikiwa, nahitajia mjitambulishe rasmi,kwa
wakati muafaka, sio siku kama ya leo, bado tupo kwenye maombolezo ….na kwa vile
sasa hivi mumekuja kwa ajili ya kumalizia msiba, siwezi kumlaumu sana bwana
mdogo , karibuni sana….!’ Akasema huyo kaka mkubwa
‘Ndio bro, sisi tumeshakaribia,…ndio yeye, ni mtarajiwa
wangu, nataka tufunge ndoa haraka iwezekanavyo , ila huu msiba ndio umekwamisha
hayo tuliyokuwa tumekubaliana,…nimakuja anye, ili na yeye afike kutoa rambi
rambi zake, kama mlivyoona kuwa keshaitoa kwa taratibu zetu, kwanza kulia, pili
sasa anhitajika kumuona mjane, na ndugu wengine….sijamleta rasmi, naomba hilo
mlifahamu, msije mkanipiga faini ya kutokufuata utaratibu’akasema.
‘Sawa hayo ni ya baadaye, tutayamaliza muda ukifika, sasa
hivi ndio tupo kwenye kumalizia maombolezo, na mimi kwa hivi sasa jukumu kubwa
lililopo mbele yangu lilikuwa hilo, la kuhakikisha kuwa kila kitu cha marehemu
tumekiweka katika, maana haya mambo yakitokea, wajanja wanakuwa wengi,..’akakohoa
kidogo, halafu akasema;
‘Dunia sasa imebadilika, wanawake wa sasa sio wale wa
zamani, enzi hizo ikitokea msiba kama huu, wanawake wenyewe wanajua taratibu
zao, hatupati shida, lakini siku hizi mume akifa, famiia ya kikeni, kwa
marehemu, wanakuja kuvamia….sasa hili inabidi sisi tunaojali mila na taraibu
tulifungie kibwebwe…’ akatulia na kukohoa tena, halafu akaendelea kusema
‘Eeeh,…bwana mdogo, na shemeji, cha muhimu na hayo majukumu yao
bwana mdogo, aliyokuachia ndugu yako, hakikisha unayatimiza ipasavyo, na usione
haya, maana ndugu yako alikuamini sana,…mimi kama kaka mkubwa nitakuwa kama
mshauri tu…nasimamia pale nitakapoona unakwama,…au sio japokuwa sijasoma,
lakini huniwezi kwa mambo ya kimila na uongozi, hapa ni jembe, wazazi wenyewe
walinivulai kofia….’kaka mkubwa akasema.
‘Kwani huyo shemeji yupo wapi?’ akauliza huyo mgeni, na hapo
nikajua muda wowote wanaweza kuingia, na nafsi yangu ilitamani sana kumuona
huyo mdogo wa hawa ndugu zangu, maana kila mara ,mume wangu alikuwa akimtaja
sana, kuwa ni msomi,mstaarabu, mpole na sifa nyingi ….sikuwahi kuonana naye kabla
ana kwa ana….
‘Shameji yako yupo kwenye sehemu yake ya maombolezo,
unahitaji kumuona sasa hivi?’ akaulizwa.
‘Ndio ni muhimu sana, maana kama nimekabidhiwa hiyo familia,
ni lazima nijue afya yake,….. na mtoto yupo wapi?’ akauliza.
‘Yupo na wenzake wanacheza, mtoto hana shida kabisa…kwa umri
wake, hawezi kujua ni kitu gani kimetokea, na hatutaki ajisikia hivyo….basi
karibu huko alipowekwa shemeji yako’wakasema na mara wakaingia pale
nilipolazwa.
‘Mbona mumemfunga hivi?’ akauliza huyu mgeni. Alikuwa
mvulana mtanashaji, na hakuonekana mdogo au mkubwa sana, tofauti na jinsi
walivyokuwa wakimsimulia, na alivalia kiofisini, kwani hawa watu wa sheria
wanapenda sana kuvai tai, ….akaniagalia kwa muda mrefu, na mimi nilikuwa
nimefungua macho kidogo, na baadaye nikayafunga, sikuyafungua kabisa, lakini
nilihisi bado ananitizama.
‘Alipandisha mashetani, akawa anaongea sauti ya mume wake,
ilikuwa kivumbi hapa, ndio tukamuita mtaalamu akayaweka sawa, …lakini kasema
kwa hivi sasa tunaweza kumfungua’sauti ikasema na mara nikasikia mtu
akinifungua hizi kamba, nikatulia hadi wakamaliza kunifungua, na nilishi mikono
milaini ikiniinua na kunikalisha. Sijui kwanini maana hiyo mikono ilipokutana
na mwili wangu nilihisi mwili mzima ukinisisimuka, nikafungua macho.
‘Oh, pole sana shemeji,…naomba ujitahidi kuyahimili haya ,
ni mipango ya mweneyzimungu, …..na wote ni watarajiwa, ujaribu kuyasahau japo
hayasahauliki, ….usijiweke katika hali ambayo utakuja kuumia, ukumbuke kuwa
yupo mtoto anakuhitajia sana, ….na sote tuna machungu kama wewe….na…’akawa
anaongea huku akiwa bado kaweka mikono yake shingoni, kunisaidia nikae vyema.
Sikusema kitu, nilimwangalia mara moja, nikakwepesha amcho
yangu na kuwa nimeangalia chini, lakini kila mara nijaribu kugeuza macho yangu
na kuangalia naye…alikuwa mdogo kwangu, kwahiyo nilimuona kama mdogo wangu, ila
kuna hali ailiniingia ambayo sikuweza kuitambua kwa wakati ule.
Nikajitahidi ni kukaa vyema, na baadaye akaingia wifi yangu
ambaye nilimzoe, nilipomuona nikamuonyesha ishara kuwa nina kiu, na wifi yangu
akaelewa, maana kuishi naye hapo, nimekuwa nikiongea naye kama mtu mwenye udhaifu
wa kuongea, …wifi akaligundua hilo akatoka kwenda kuniletea maji, niliyanywa
kama ng’ombe mwenye kiu ya muda mrefu…
Niliyanywa yale maji yote na, nikaomba niongezwe mengine, na
baadaye nikapatiwa chakula kidogo, nilikula kwa kujilazimisha, ili nisije nikazimia
kwa njaa, kwani nilikuwa sijisikii kula kabisa na baadaye usingizi ukanijia,
lakini kabla ya kupitiwa na usingizi ulionijia kwa kasi, nilisikia shemeji mkubwa
akisema;
‘Tumefanikiwa kumtoa huyo jamaa kwenye nyumba, lakini baada
ya kupambana na kikosi chetu kwa muda mrefu, ameumia vibaya sana,…anaweza hata
asiishi, lakini polisi wamemshikilia kama mleta vurugu…’
‘Oh, kwanini mumemuumiza,
ina maana imefikia hatua hiyo yakuumizana, ….lakini nyie mliniambia kuwa
huyo sio baba yao, sasa kwanini aingilie mambo yasiyomuhusu, ….’ Akamgeukia huyo
mchumba wake akionyesha kutahayari, kama vile hayo yanayoongelewa hapo
yanamzalilisha kama mwanasheria, na alipomuona mchumba wake akiwa na uso wa
huzuni, akiwa habandui macho yake kuniangalia mimi, akasema;
‘Mimi nahisi huyo atakuwa na sababu kubwa, ambayo mimi
siijui,… lakini kama hana sababu ni ubishi tu, na kama anahitajia kupambana na
mimi tutapambana naye….’akasema huku anatikisa kichwa na alipogeuka kumwangalia
mchumba wake, alishangaa kumuona akitoa machozi na baadaye yule mchumba wake akasema;
‘I cant believe this…’
akiwa na maana haamini hayo anayoyaona na kuyasikia.
Na mimi mwili ukawa hauna nguvu tena, usingizi, au kupotewa
na fahamu kukanijia na kuzama kwenye giza…
*******
NB: Ni kazi kweli kweli kufanya mambo haya kwenye mazingiraj
magumu ninayokabiliana nayo, lakini nitajitahidi hadi nifikishe ujumbe wa kisa
hiki kama tukio lilivyotokea.
WAZO LA LEO:
Ukiona haki inapindishwa, ukiona haki inavunjwa itetee, ama kwa mikono yako,au
kwa kukemea, au kama umeshindwa, basi ikatae moyoni. Usisubiri hadi hayo wanayotendewa wenzako yafike
kwako ndio uanze kupiga ukulele, maana leo kwa mwenzako kesho ni kwako. Ulewe
kuwa wavunja haki hawachagui mlango wa kuingia.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment