‘Niambe ukweli, kuna
nini kimetokea ….? Nikauliza. Babu yako akanisogelea na kunishika , na machoni
hakuweza kuvumilia, machozi yakaanza kumtoka.Nikajua ni msiba, je ni wa mume
wangu au kuna ndugu yangu mwingine. Lakini mume wangu hali yake ilishaanza kuwa
nzuri, niliongea naye usiku akionyesha kupona…haiwezkeni, sio yeye….’nikawa najipa
matumaini.
Mara yule mwanaume
aliyeingia na babu, bila kuvuta, au kusubiri, akasema;
‘Mume wako hayupo
duniani….’akasema huyo mtu, ambaye ni kaka mkubwa wa mume wangu. Nilimwangalia
kama vile sijasikia vyema, nikatoa jicho, kumwangalia kama vile simuoni vyema,
nikapanua masikio, nisikie vyema, lakini hakurudia, alikuwa akiniangalia, bila
kupepesa macho.
Nikajau hicho
nilichosikia ni kweli, mume wangu hayupo duniani, hapo akili ikaanza kuliingiza
hilo tukio, na mwili ukaanza kulegezwa, hapo sikuweza tena kuvumilia, nilimfuata
yule shemeji, nikaanza kumparura kwa makucha, huku nikisema
‘Nyie ndio mumemua mume
wangu….mumemchukua hapa akiwa keshaanza kupona na kwenda kummalizia,huko kwenu
kwanini mlimchukua, wakati alisema kama ni kufa anataka afie kwenye nyumba yake
….’ Lakini jinsi muda ulivyokwenda, nilijikuta nguvu zinaisha hata kuinua mkono
ikawa shida, na hapo hapo nilishuka chini kwanza taratib, halafu mwili
ukadondoka kwa kishindo sakafuni.
Wakati nadondoka,,
yule shemeji aliona hiyo dalili ya mimi kuishiwa na nguvu na kuwa asiponishika nitadondoka, lakini...., hakutaka hata kunishika, na kwa mbali nilimuona
babu yako akivua hatua kuja kunidaka, lakini alikuwa kachelewa,….nikadondoka
sakafuni na kupoteza fahamu…..’ Mama akamalizia sehemu hiyo.
Na hapo nikakumbuka
babu alivyoendelezea sehemu hii kwani yaliyotokea baadaye mama hakuwa na
taarifa nayo.hata alipozindukana, hakuweza kuongea hadi siku kumi zilipopita,
alikuwa kama bubu…
********
Mjukuu wangu, kufiwa kusikie kwa wenzako, lakini ikitokea
kwako ndipo utajua uchungu wake, …ukisikia kwa wenzako utakwenda na kusema;`yote ni mapenzi ya mungu..’ utaondoka,
lakini sasa ni wewe umefiwa, ...halafu aliyefariki ni yule ulikuwa naye karibu,....manakula naye, mnashinda naye, mnalala naye....patamu hapo....na machungu yanazidishwa zaidi kutoka kwa watu wanakuja kwako,...'babu akatulia kidogo.
'Unajua kila mtu ana silika zake, na kila mmoja anakuja kwa
hisia zake, na wengine hawana elimu ya kumliwaza mtu, na wengine hawajui kutoa pole
isiyorejesha hisia nyuma kwa mfiwa ambayo itaweza kumuongezea machungu...' babu akaendelea kuongea.
Basi ilikuwa kazi kubwa sana, na nilimuonea huruma sana mama
yako, maana mila zetu zinatambulikana, mke akifiwa anakuwa kama mtu asiye na thamani tena, anaanza kuteswa, ....mimi nakuita kuteswa, kwani yanayofanyika sio mambo ya kungwana, jinsi
anavyotengwa, sehemu anayolala, na jinsi gani anatendewa, anakuwa kama yeye ni
mkosi fulani, uliosababisha hicho kifo, na hayo anayotendewa ni kama adhabu fulani, nilijua kuwa akizindukana,
alihitajika kuwa na mtu wa karibu anayemjali,…lakini haikuwezekana, maana alishachukuliwa na huko atakuwa ugenini, nyumbani kwa
shemeji yake.
Katika familia hiyo, shemeji huyo ambaye ndiye kaka mkubwa,
walikuwa hawaivani kabisa na mama yako na mdogo wake, na siku zote, alikuwa akisema kuwa mdogo wake,
anaumwa kwasababu ya huyo mkewe. Na anateseka kwa vile hataki kuwa karibu na familia yao, kajietenga, hasikii..., alifikia hadi kusema mama yako ndiye
kamuambukiza baba yako huo ugonjwa, au vitu kama hivyo.
Walifikia hadi …..kusema kuna mkono wa mtu....., lakini maneno yake yalielekea
hivyo, kuwa mama yako kuna dawa kamuwekea mumewe, …au tuseme kamloga, lakini
alikuwa akikwepa kauli hiyo,ya kusema kalogwa na alisema;
‘Hawa wanawake hamuwajui, huenda alitafuta dawa, akiwa na
lengo, a kumweka sawa mumewe, na bila kujua madhara yake, akamuumiza mumewe,
hamuoni, kwanini haponi, mbona wengine wanaumwa ugonjwa huo mbona
wanapona….’akawa anasema.
‘Mimi nikiweza kumtoa mdogo wangu kwenye makucha ya huyo
mwanamke, nitahakikisha mdogo wangu hamrejei tena huyo mwanamke…hafai kabisa
kwenye ukoo wetu…’akawa anasema kwa watu.
Kwakweli kama ningelielewa hilo, kama ningelikuwa na mtu wa
kunisaidia, ningelimchukua mama yako na kuhakikisha kila anayekuja kumpa pole nampa somo kwanza ni kwa jinsi gani atakavyongea, lakini haikuwa rahisi hivyo.
‘Kwanza kitu cha ajabu ni pale huyo kaka wa marehemu
alipokuja kutoa taarifa, hakutumia busara, alikuwa kama anaongea na mtu baki,
hakujua kuwa anaongea na mke wa marehemu, mke ambaye ni ubavu wa mwenzake, ina maana ubavu ulioondoka ni ubavu
wa huyo mjane, sasa haupo tena, kwahiyo mwenzake hana nguvu za kujishikilia,
anahitajia msaada, na msaada utatoka wapi, kama wanandugu ndio hawo, wanaotaka
kumtelekeza.
‘Hili nililiona kwa vile lilinitokea na mimi, alipofariki
mke wangu, nilikuwa kama nimekatwa upande mmoja wa mwili, nikawa sina nguvu
kabisa, ….sasa fikiria mimi mwanaume, na tunajitapa kuwa wanaume kidogo tuna
ustahimilivu,….hebu geukia upande wa mama yako uhisi hali aliyokuwa nayo.
Wakati nimesimama karibu na mama yako nilijua kuwa lolote
linaweza kutokea , kwahiyo nilikuwa nipo tayari kumsaidia, lakini alivyochomoka
na kumwendea shemeji yake, na kuanza kumpiga makofi, akisema kuwa wao ndio
waliomuua, nilijikuta nimeshikwa na bumbuwazi.
Na alipoishiwa nguvu na kudndoka, nilikuwa ndio
nimezindukana kiakili, na hata niliposogea pale walipokuwa wamesimama, nilikuwa
nimechelewa, kwani mama yako aliodondoka chini, bila ya msaada wowote, shemeji
yake alikuwa akimwangalia tu….Nilitamani nimzabe kibao, lakini nikajua kuwa
haya yeye yupo kwenye machungu, maana yeye ni ndugu wa damu, ana machungu yake
kumpoteza ndugu yake.
‘Hivi wewe unashindwa hata kumshika, huoni alivyodondoka
angeliweza kuumia namna hiyo….’nikasema.
‘Ningelifanya nini hapo, …nai aisiye na amchungu ya kufiwa,
au kwa vile anajua kesho na keshokutwa atapata mume mwingine, sasa mimi
nitampata wapi ndugu mwingine ……mimi nina machungu zaidi yake, lakini siwezi
kufanya anavyofanya yeye….achana naye bwana…’akasema huku akiangalia huku na
huku, akiikagua nyumba kwa macho.
‘Sasa taratibu zitakuwaje, maana hapa ni nyumbani kwa
marehemu, na ingelikuwa bora maiti ikaletwa hapa nyumbani kwake?’ nikamuuliza.
‘Hayo ni mambo yetu, tumeshayajadili, nilikuwa tu niwape
taarifa kuwa kuanzia sasa kila kitu cha marehemu kitakuwa kwenye mikono ya
familia anayotoka, na mimi kama kaka mkubwa natakiwa kufuatilia na kuhakikisha
mambo yote yanakwenda kutokana na taratibu za mila na desturi zetu…’akasema
‘Hilo halina shaka, na nijuavyo, taratibu za mila nyingi za
hapa kwetu, hasa za misiba hazitofautiani sana, na mke ana nafasi yake, kwa
mumewe, sio kwa vile mumewe kaondoka, ndio aachwe pembeni, na sehemu ya
marehemu ni muhimu sana, na mwili wa marehemu unahitajika kuhifadhiwa hapo hadi
dakika ya mwisho…’nikamwambia.
‘Hayo ni ya kwako, sisi kama familia, tunaheshimu sana
utawala, ….katika familia yoyote, kama mkubwa ana heshima yake, na kila jambo
linahitajika kufanyikia kwake,…hilo la kuwa mwili uwekwe kwenye nyumba yake,
kwetu halipo, mambo yote yanafanyikiwa kwa kaka mkubwa, au sehemu ya familia
alipotoka marehemu….’akasema huku akiendelea kuikagua ile nyumba.
‘Kama mama na baba wangelikuwepo, tungelienda kwao, kwani
hata uwe mkubwa vipi, bado wao ni wazazi wetu, lakini hawapo, mimi kama kaka
mkubwa ndiye nasimama badala yao…kwahiyo mambo yote yatafanyikia kwangu, na taratibi zote
zitafanyikiwa kwangu,…na huyu mjane, tunaondoka naye, ili akafuate taratibu
zote zinazomstahiki. Na kila kitu cha marehemu,…..kinatakiwa kikabidhiwe
kwangu, ili tujua hatima yake….taratibu zote zitafuatwa…’akasema huku
akiendelea kuikagua hiyo nyumba kwa macho.
‘Sawa ….kwa vile tupo kwenye msiba, sihitajiki kulumbana
sana, ila mnatakiwa muwe waangaliafu kwa hilo, msije mkaingiza maswala ya
tamaa, kwenye mali za watu, hamjui wenyewe walichuma vipi, kwahiyo vyovyote
itakavyo kuwa, mimi nasimama kama mzazi wao, na kwa vile nimaishi nao, na
walinitambua kama mzazi wao, ….nayafahamu sana mambo yao…’nikasema.
‘Sikatai, …hilo silipingi mzee wangu, kila kitu
kitafikiriwa, na wewe utashirikishwa kila hatua, kwa kutoa mawazo, tunakutambua
sana, na tunashukuru sana kwa mchango wako mkubwa kwenye hii familia, lakini
mambo ya familia yetu yanakuwa mbele, hatuwezi tukavuruga taratibu za familia
kwa ajili ya kuwaridhisha watu wengine….tunakuomba ulijue hilo, na tunakuomba
uheshimu taratibu zetu, maana hatujawahi kuja kuwaingilia kwenye taratibu
zenu….au tuna uhasama na wewe…sizani, ni mambo ya kawaida, ambayo kuanzia sasa
mimi kama kaka mtu nitahakikisha hayo yamekwisha…’akasema na kumwangalia mama
yako ambaye bado alikuwa kalala sakafuni.
‘Huyu watakuja kumchukua wenzao, na ingelifaa wafike haraka
wambebe, ili akizindukana ajikute kwenye sehemu yake…siunajua taratibi zilivyo,kuwa
mke akifiwa anajengewa sehemu yake maalumu, …atakaa hapo hadi siku arubaini zitakapoisha,
hataki kulala kwenye starehe, anatakiwa aonyeshe uchungu, analala kwenye mkeka,
na katika hali ya taabu, tutasema hivyo, lakini ndivyo ilivyo, kwasaabbu
mwenzake anakwenda wapi, …si kwenye udongo, sasa yeye anatakiwa aiihisi ile
hali,….hayo yanajulikana au sio mzee?’ akawa kama ananiuliza.
‘Hayo mambo mengine ni ya kutesana tu, hayana msingi wowote,
hayajaandikiwa hata kwenye vitabu vya dini,,…hilo tumekuwa tukilipiga vita sana,
haiwezekani, mtu atengwe, ajengewe kibanda cha ovyo, alale kwenye udongo,
…yaani mtu kafiwa, ana machungu na bado mnataka kumtesa, …..huko sikumuongezea
uchungu…jaribuni kuwa waungwana….’nikasema kwa hasira.
‘Mzee, mbona unavunja mila na desturi, sisi hayo tumeyakuta,
na wewe uliyakuta,…kwanini sisi tuwe wa kwanza kuyavunja,…kama unayavunja wewe,
sio mimi…mimi nimelelewa kimila na nitazifuata mila zetu moja baadaya jingine,
na hili ni amri, niisingelipenda uliingilie hili na mengine tutakayoyafanya, ..mjane
bado yupo kwenye himaya yetu,hadi hapo itakapomalizika arubaini, na kutoka hapo
ndio tutaangalia taratibu nyingine, natumai mzee hutatuingilia kwa hilo…’akasema
huku akianza kutembea mle ndani.
‘Nakuona unaikagua hii nyumba ….kama vile ndio mara ya
kwanza kuingia humu, vipi kulikoni, au ndio mtu akifa, basi kila mtu anamezea
mate mali za watu…wacheni hiyo jamani, ..wakati wanahangaika mlikuwa hampo, sasa
mmoja keshaondoka mnaanza kupiga mahesabu kichwani,….hii nyumba….’kabla
hajasema wakina mama wakafika.
‘Haya mchukueni huyo mwenzenu, na kama inawezekana mbebeni
akiwa hivyo hivyo, msihangaike kumzidua, atazindukana kwenye kibanda
chake…’akasema huyo kama mtu, huku akipuuza yale niliyomwambia, maana sasa
likuwa kiingia chumba baada ya chumba akikagua .
‘Lazima nitimize wajibu wangu kama kaka mkubwa, lazima nijue
mali za marehemu ili wasije watu wakazifanyia ubadhirifu, na mzee, nitafurahi
sana ukitoa mchango wako, wa kunisaidia kuzitambua mali zote, ambazo huenda
hata mimi sizijui….’akasema huku akiwa kashika karatasi.
‘Nafikiri huu sio wakati wake…hapo nakuona, unakimbilia mali
badala ya msiba, hiki ni kipindi cha msiba, ni kipindi cha mashituko, inahitajika
watu tuomboleze, sio muda wa kupigiana mahesabu ya mali ya marehemu, …hata
hivyo wenyewe walishajipanga, mke wa marehemu anajua kila kitu, na anajua ni
nini afanye…nyumba hii ni ya kwake…’nikasema.
‘Ndio ni ya kwake…ni ya ndugu yangu hilo halina shaka,….mke
yupo tu, kesho anaweza kwenda kuolewa shemu nyingine, lakini nyumba inabakia
kuwa mali ya familia, na kwa vile wana mtoto mmoja, huyo atakuwa chini ya
himaya yetu, …kama familia tutamlea, kama familia tutamiliki mali yote ya
marehemu, na muda ukifika …mtoto akikua, tunamkabidhi mali yake…kwa hivi sasa
mtoto wake ni mdogo sana, hajui lolote, hapo unasema nini…..mama yake hana
mamlaka tena…ni kama ndugu zetu wa kike,….wapo, na siku yoyote wataolewa, na
kwenda kwa waume zao….’akasema
Sikutaka kubisha naye sana, maana ulikuwa sio wakati wake,
lakini niliahidi moyoni,kuwa mimi kama mzazi nitapigania mali za hawa wanangu
hadi tone la mwisho…
‘Kwahiyo mzee, tunaomba ushirikiano wa kututajia mali zote
za marehemu, ili nikawakilishe kwa wanafamilia, ili tujue taratibu nyingine
zitakuwaje, ….na kuanzia sasa hivi, hii nyumba tutaifunga, na haitatumika hadi
arubaini ikiisha, na wewe kwa vile umebahatika kuishi hapa, una sahemu yako, ya
kutoa mawazo…ila kwa vile nyumba yako ipo karibu kuisha, ni bora uende ukakae
hapo kwako, ili tuwe na nafasi ya kufanya mambo yetu kifamilia,,…’akasema
akiniangalia kwa jicho la kujiiba, akihisi kuwa nitasema kitu.
‘Hayo tutakuja kuyaaongelea, kama nilivyosema nyumba hii
inajulikana ni nani kaijenga,…..lakini naona hayo sio wakati wake muafaka, na
sina cha kushirikiana na nyie, maana kila kitu kilishawekwa sawa, kati ya
marehemu na mkewe, na mtu wa kumuuliza ni mkewe, na hilo huwezi kulifanya muda
kama huu, tusbiri muda ukifika tutaliweka sawa…mimi ndio ushauri
wangu…’nikasema.
‘Huwezi ukaacha mali zikae bila usalama, ni lazima kila kitu
kiwekwe katika usalama, na kuwe na utaratibu, huku mambo mengine yakiendelea,
hivi watu wakija na kuiba, au kudai hiki ni changu, mimi kama kaka mkubwa
nitasemaje…ni lazima nianze kuchukua hatamu, pale mdogo wangu alipoishia, na
hili halitakiwi kusubiri…vipi mzee, mbona unakuwa kama umezaliwa leo….’akasema
na kauli hiyo ilinichefua, kwani alikuwa akitamka kwa kejeli huku akizungusha
macho huku na kule kutizama kila kona ya nyumba.
‘Kijana, usione kuwa umekuwa….mimi nimekuona ukizaliwa, …leo
hii unaota mapemba, halafu unaota mapembe kwenye jasho la watu,…hivi nyie watu
mtabadilika lini, hangaikeni kutafuta vya jasho lenu, msisubiri wenzenu
wahangaike, halafu wakifa mnakimbilia kumiliki, …mtalaanika….nawaambia ukweli,
mali yote iliyopo hapa ni mali ya mke wa marehemu na mwanae, na mimi baba yako
nitailinda kwa nguvu zangu zote….’nikasema na jamaa huyo akaniangalia kwa jicha
la kushangaa.
‘Mzee, toka lini ukawa mzazi wa hawa watu, wewe tunajua
kabisa huna mtoto, hukuwahi kuzaa, na kama ulizaa, bahati haikuwa yako, hayo ni
mapenzi ya mungu…lakini kwanini udandie yale yasioyokuhusu, leo hii unaingilia
watoto wa wenzako, na kujifanya wewe ni mzazi wao, mzee, jiheshimu, na sisi
tutakuheshimu…sitaki kabisa kuvunjiana heshima na wewe, na kama huwezi
kutusaidia kwa hilo, basi ondoka…acha mambo ya watu wenye familia na wanaojua
taratibu za kifamilia…haya hayakuhudu, wewe ni wa kutoa mawazo tu, na ukitoa
mawazo sio lazima yote yatakubaliwa….’akasema, na hapo nikashindwa kuvumilia.
‘Kijana naona hatutaelewana, na hili sio muda wake, wewe
ondoka humu ndani…, ila nasema, kuanzia sasa kila kilichopo humu ni mali ya mke
wa marehemu,…wakati hawa watu wanahngaika haaukuwepo, mimi nilikuwa nao, naijua
familia toka jiwe linawekwa, toka ….huyu binti alipotelekezwa, nimemlea
mwenyewe, hadi alipokutana na huyo mwenzake, kwahiyo huwezi kunidanganya
lolote,….mimi waliniheshimu kama mzazi wao, na waliniomba niwalinda kama baba
anavyowalinda watoto wake, na hilo nitahakikisha nalifanya, hadi hapo
nitakapoingia kaburini.
‘Mzee ….mzeee….’akawa anaita mzee, mzee bila kusema neno, na
mimi nikaendelea kuongea;
‘Niliahidi mbele yako, na sasa naahidi mbele yako, kuwa nitawalinda,
na nitalinda mali yako usiku na mchana, hadi hapo muafaka utakapopatikana, na
kama kuna mtu anataka shari , basi mimi nipo tayari kupambana na yeye….kama ni
kwa shari ama ni kwa heri, basi hilo tutalijua wakati ukifika, kwasasa sio muda
wake….’nikasema na kulichezesha panga langu hewani
‘Mhh, naona sasa mzee unatingisha kiberiti….ngoja
nikalichukue jeshi langu, maana siku nyingi nimekuwa nikilitaka hilo hili
litokee, nipambane na wewe,….wewe mzee, umekuwa ukiwaharibu sawa hawa watu,
ndugu yangu alikuwa mbali kabisa na familia yao, kwasababu yako…mkewe akaota
mapembe, haheshimu mila na desturi za familia yetu, hili ni kwasababu yako,
tumejitahidi lakini tulikuja kugundua kuwa wewe ndio kikwazo…’ akaninyoshea
kidole.
‘Sasa muda wa kuliweka hili sawa umefika, utapambana na mimi,
mzee, utapambana na mimi…’ akawa napiga piga kifua, na mimi nikawa namuangalia
tu, akasogea akionyesha kutaka kuondoka, na akaendelea kuongea kwa majigambo;
‘Lakini kwanza ngoja nikalifikishe hili kwenye familia, ili
wasije wakaoa nimechukua sheria mikononi mwangu…mimi mzee sikuogopi wewe kabisa,
nasikia kuwa una nguvu za ziada,…mimi siogopi, uchawi, siogopi ubabe
wako,….kama una hizo nguvu za ziada, hebu nikuulize mkeo wako yupo
wapi…’akasema huku keshafika mlangoni, akionyesha kujihami ….alimpomtaja mke
wangu sikuweza kuvumilia, nikamfuata na panga likiwa juu…
NB: Haya yapo kwenye jamii zetu, tukio hili ni kielelezo
kidogo tu ndani ya jamii, tusaidieni ili tuweze kufikisha ujumbe huu
WAZO LA LEO:
Wanapohangaiaka wawili, yaani mke na mume, mnawaona, wakifanikiwa mnawaona,
lakini anapokufa mmoja kati ya wanndoa hawa hasa mume, akamuacha mke,
tunayasahau haya yote, na kwenda kuwadhulumu wanafamilia hao.Tumuogope mungu, haki
yao tuwape, kamwe tusiwadhulumu mayatima, wajane maana haya ndiyo yanayochangia
kuleta laana kwenye hii dunia.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Either employed by hackers, or by a suspicious spouse
or parent, a Keylogger for Mac at hand, you will be checking
with them.
Also visit my web site: keyloggers
Post a Comment