Dini zipo nyingi, na madhehebu ndani ya kila dini ni mengi.
Ili kuleta umoja, na kuondoa sintofahamu, minung’uniko, ambayo ndio inachochea
mambo, mikutano kama hiyo wangejaribu kuwajumuisha viongozi wote wanaokubaliwa
na watu wao, ili kila mmoja atoe mawazo yake, na baadaye wazame kwenye imaniza
kweli za dini zao, ambazo ukichunguza kiukweli, zote zinahimiza amani, upendo,
haki sawa.
Mimi naamini kama
viongozi wa dini wakitumia imani zao vyema, wakazieneza kwa waumini wao kwa
hekima na busara, bila kuweka ubinafsi wa hisia zao, nchi hii itakuwa na amani,
kwa vile bado wananchi wetu wana mioyo ya kiimani, hawajagubikwa na imani za
chuki kihivyo. Na pia ukiangalia kiundani viongozi wa kisiasa pamoja ya jazba zao,
wakikutana na viongozi wao wa dini wanakubali ushauri wao, na wengine
wanazitumia hata kwenye kazi zao.
Kwa uoni wangu,
wakati sasa umefika, nchi kama hii yetu kuwa na baraza la viongozi wa dini Tanzania, ambapo humo watakuwepo
viongozi mbali mbali wa dini zote zilizopo nchini, bila kubagua, na viongozi
hawo wawe wanaokubalika na waumini zao, wasichaguliwe kisiasa, na hili baraza
liwe karibu na raisi, kama washauri wake kuhusu maswala yanayotokana na dini,
ili raisi asipotoshwe, kwani kuna taarifa nyingine zikifika kwake zinakuwa
zimeshachakachuliwa.
Baraza hili kila kukitokea tatizo wakutane, na sio kusubiri
tatizo tu, hapana pia wawe na vikao vya mara kwa mara kwa maslahi ya taifa. Pia
hii inaweza ikajenga hali ya kuzoeana kwa viongozi hawa wa dini, nah ii inakwena
moja kwa moja hadi kwa waumini wao, na viongozi hawa wakiwa karibukaribu,
wataweza hata kukosoana wenyewe kwa wenyewe, kuwa mwenzetu hapo umekosea, hebu
tuambie imani gani inataka hivyo unavyofanya wewe. Lakini pia ni kupeana ukweli
ili kila mmoja ajue dini ya mwenzake vyema.
Zamani baba wa taifa, J.K Nyerere,
alikuwa akikutana na wazee mara kwa mara, hii ina maana yake, kuna maswala
ambayo yanahitaji busara za wazee. Akiona ni muhimu, na huenda anataak kuchukua
hatua itakayoleta manung’uniko, kwanza anakwenda kuwaweka sawa wazee…kiukweli,
na kihekima, kuna maswala ambayo yanahitaji busara za wazee, hata kiongozi uwe
mzuri gani, bado kuna kukosea, na wazee wetu wanajua mengi, wanaweza wakakushauri
jambo, ambalo lingesaidia taifa,…sisi sasa wazee tunawageuak na kuwaita wachawi…..balaa
na laana
Kiukweli na kihali halisi kwa nchi yetu hii ambayo dini
inaheshimika dini imeteka akili za watu, japokuwa wengi hawazifahamu dini zao
vyema, na ndio udhaifu waliogundua
wenzetu na wanataka kuutumia udhaifu huo kutugawa, na hapa ndio utaona umuhimu
wa viongozi wa dini kuwa wanahitajika sana kutumiwa ili kujenga umoja, ili
kuzijenga imani za watu wakawa kitu kimoja, na pale tunapozungumzia utaifa
tuonekane watu wamoja, japokuwa kiimani
tunatofautiana. Raisi tumia baraza hili kupata ushauri, hawa ni watu wa hekima,
na wana nguvu sana kwa waumini wao, na nguvu zao ni za kimungu.
Wakati sasa umefika,
na ninarejea usemi wangu, kuwa kama kuna
kipindi tunatakiwa tuwe wamoja, ni kipindi kama HIKI, maana maadui zetu, wameshagundua
udhaifu wetu, kwanza tunatatizo la elimi(adui ujinga), na sio kuzarauliana,
lakini elimu inamsaidia mtu kuweza kupambanua mambo kwa uhakika zaidi, sisi
elimu yetu bado ipo chini, utasema mbona kuna nchi za wasomi mbona wanagombana.
Lakini elimi ninayoizungumzia hapa ni elimu ya utambuzi,…
Lakini kubwa zaidi tuna
udhaifi wa elimu ya dini, wakati tunajifanya tuwaumini, na hapo ndio watu hawa
wanapotupatia,wanatuperekesha kama bendera fuata upepo, lakini ukichunguza
sana, ni kwasababu waumini hawazijui dini zao vyema, na wanachokifanya ni
kuwafuata watu(viongozi wao) kama ndio dini zao, hili ni tatizo na ni udhaifu unatumiwa
kwetu, nah ii ni hatari.
Najingine kubwa kuliko ni hali mbaya ya kiuchumi, umasikini uliokithiri, ambao pia unachangiwa
na utofauti mkubwa wa walio nacho na wasio nacho, kwani adui yako muombee njaa.
Imefikia hali ambayo ile hali ya kusaidiana imeanza kuondoka, na ubinfasi
umetawala.
Mimi nina imani kuwa Taifa letu bado halijafikia kuitwa
masikini wa kutupwa, kwasabbu wapo matajiri, ambao bado wana imani zao za dini,
wakiamua, wanaweza wakatumia utajiri wao kuwekeza na kuwaajiri wale
wasiojiweza. Na hapo ndio maana nasema kama kuna wakati tunahitajika kuwa
pamoja ni sasa, kabla hatujaupanua huu wigo wa chuki, kwani utatoka kwenye
imani za dini, utakwenda kwa walio nacho na wasio na nacho, na ukichunguza
sana, nahisi watu hawachukiani kwasababu ya `dini’ zao, tuwe makini hapo,….sababu
kubwa ni hali mbaya uchumi, haki haipo,….watu wameshaanza kuhisi hivyo. Kuna
upendeleo unahisiwa, hili watu wanalalamika wanapuuzwa ….na hili litaondoka ,
pale watu tutakapowezeshana. Hebu tuliangalia hili nalo kiundani.
Wenye nacho wakumbukeni wasio nacho, timizeni kiukweli imani
zenu, ..imani za dini zinatutaka hivyo, tupendane, tusaidiane, tuhurumiane…sasa
nashangaa pale watu wanapotafuta njia ya kuwezeshwa wengine wanakataza, wakati
wao wana hiyo mianya, je kweli tuna upendo wa dhati hapo,…tuungane tujadilaine
hili na tutafute njia ya kusaidiana kwa upendo wa kweli.
Kama viongozi wa dini mtafarakisha watu, …tutakuwa na shaka
na imani zenu, kwani tujuavyo sisi waumini wa kawaida ni kuwa, imani zote za
dini zinafundisha upendo au sio?
Na pia kwa viongozi wa dini msimilikiwe na viongozi wa siasa,
hawo ni waumini wenu pia, kama mtamilikiwa na viongozi wa siasa tutakuwa na
mashaka na imani zenu, ina maana wao ndio wanawafundiha imani za dini, sio
kweli, na pia wameshatuambia kuwa wao kama wanasiasa mambo yao hayana dini,
kwanini mnatekwa na wao. …
Kwa hilo la viongozi wa dini kukutana hongereni sana, ila
boresheni kwa kuwaongeza viongozi wengine wa dini zote, ili mjenge usawa, umoja
na mshikamano wa imani zote.
WAZO LA LEO:
Dini, zinatufundisha amani na upendo, haki za kila eneo, na mshikamano pale
tunapokuwa na imani tofauti, je viongozi wa dini, mnafanya hivyo, na kama mnafundisha
kufarakana, hiyo ni imani gani. Je ni kweli ni kuwa udini ndio unasababisha
haya yote, nahisi tunahitaji kulichunguza hili zaidi, na hili mtalipata
mkikutana mara kwa mara na kwa kuwa karibu na waumini zenu.
Ni mimi:
emu-three
3 comments :
Hoja iliyokwenda shule-tatizo sehemu kama hizi hawafiki wao na udaku
safi kabisa kaka nakuunga mkono
Hoja iliyokwenda shule-tatizo sehemu kama hizi hawafiki wao na udaku
Post a Comment