Maua akiwa na mama yake mdogo, aliona huo ndio wakati
muafaka wa kumdadisi mama yake mdogo kuhusu huo mzigo ambao alitakiwa aupate
kutoka kwa mama yake mdogo, kutokana na maagizo ya docta. Akamwangalia mama
yake mdogo ambaye alionekana akiongea na simu, na alipomaliza kuongea na simu,
Maua akauliza;
‘Ma-mdogo, Sasa huo mzigo upo wapi, na una nini ndani yake?’
akauliza Maua.
‘Mzigo gani huo….umeanza Maua, ….nimechoka na adha zako,
huniachi nikapumua,….?’ Akauliza mama mdogo akionyesha kukerwa.
‘Huo mzigo uliosema docta alikuambia unikabidhi….upo wapi
mama mdogo, najiuliza ulikuwa na nini ndani yake?’akasema Maua.
‘Sijui upo wapi…..na wala sijui kuna nini ndani yake, maana
mtu ambaye angelisaidia kujua ni nini kilichokuwepo, keshauliwa, lakini nina
uhakika kuwa kilichopo ndani yake kina thamani kubwa sana,…..ndio maana
sijakata tamaa, na sitaweza kabisa kuwakabidhi huo mzigo kwa polisi…’akasema mama mdogo.
‘Lakini umeambiwa kuwa ni mzigo wangu…au sio?’ akauliza Maua
akimwangalia mama yake mdogo, ambaye alikuwa kamgeuzia mgongo, na alipoona mama
yake hasemi kitu akasema;
‘Kama ni hivyo, huo ni mzigo wangu, nina haki ya kuupata, …nakuomba
mama unikabidhi huo mzigo..tusije tukafikishana mbali’akasema Maua.
‘Ni kukabidhi wewe,hahaha...ili ukauharibu, thubutu, hicho
ni kitu cha mwisho kukifanya…huu ndio mtaji wa mwisho kwa hawa watu, hapa
najiandaa , kesho naingia Arusha….oh,…’akasema na safari hii akashika kiuona,
lakini alikuwa vile vile akiwa kampa mgongo Maua, na baadaye akageuka na
kusema;
‘Nimekuambia, kwa vile inabidi ubakie na nyumba, vinginevyo,
ningeondoka taratibu, shaaaah, sikutaka ujue hiyo safari yangu…maana una
kiherehere, huna akili ya kujua maisha….sasa skiliza ni hivyo, kesho kimiya
kimiya….bomba hadi Arusha….’akasema mama mdogo huku akishika mdomoni kwa
kiganja cha mkono kuashiria kuwaza na kuziba mdomo wake.
‘Mama mdogo….unakwenda Arusha kufuta nini tena unakumbuka
huko ulishafukuzwa na uliambiwa ukionekana huko unaweza ukaishia jela, pia
ukumbuke hapa upo kwa dhamana….?’ akauliza Maua akiwa na wasiwasi na kauli ya
mama yake huyo mdogo, lakini akilini alikuwa akikumbuka maagizo ya Inspecta.
‘Huyu mtu tunamuachia
kwa dhamana, lakini kwa malengo maalumu, na wewe tunaomba utusaidie kazi moja,…utupe
habari katika mienendo yake…kila analofanya ambalo litatusaidia kutufikisha
kwenye masalio ya kundi hilo, utuambie…sio ombi, bali ni amri, usije ukajikuta
na wewe upo matatani kwa kuficha nyoka chumbani kwako…..
‘Eti unauliza Arusha kufuata nini….hahahaha….tatizo lako
umejaa ujinga akilini mwako,…siwezi kuishia patupu hapa, huko mimi nitakwenda
kwa siri na ole wako…narudia tena, na ole wako ufungue hilo domo lako kwa hawo
wanaojiita polisi…., ‘ akamnyoshea kidole Maua, na alipokishusha akasema;
‘Hata kama polisi wameniambia kuwa siwezi kusafiri, kwa vile
nipo nje kwa dhamana,….lakini mimi sio mtoto mdogo, mimi ni mtoto wa mjini,
nitakwenda shaaaapu!, Na hawataamni, siku inayofuata nipo hapa, tajiri… hawatajua
kabisa kuwa nilisafiri…’akasema mama mdogo akibenua mdomo na kutikisa kichw.
‘Mama mdogo, mimi siwezi kukubaliana na hilo, japokuwa sio
mimi niliyekuwekea dhamana, lakini mimi ninaweza kukamatwa kwa kutokutoa
taarifa kuwa umeondoka kwenda Arusha bila kibali cha hao polisi na kinyume cha
sheria…’akasema Maua.
‘Wewe fanya unalotaka…. , na hata siku moja siwezi
kukusikiliza unavyotaka wewe, kwanza wewe kama nani, wewe ni kula kulala tu…hapa
nahangaika kwa jili ya kula kwako, na hicho kimimba chako…..’akanyosha kidole
kwenye tumbo la Maua, halafu akamkazia macho Maua na kusema;
‘Kwanza sikiliza,…kwa vile huniskilizi mimi…. kwanza
umtafute huyo mwenye hicho kimimba haraka iwezekanavyo, maana huyo docta uliyesema
kuwa ndiye anayehusika keshaondoka, unasikia sana….sasa tafuta mtu mwingine wa
kumbambikia huo mzigo wako, maana kila mwanaume unayetaka kumbambikia anakufa…sijui
kuna nini na hicho kimimba chako….’akasema huku akitabasamu kinafiki
‘Hayo ni mawazo yako….’akasema Maua.
‘Sawa ni mawazo yangu, lakini natumai unanielewa….’akasema
huku akigeuka na kuanza kuondoka.
‘Mama mdogo, naomba usinisimange kwa hii mimba, maana wewe
ndiye uliyenifanyia haya yote, na kama nitawaelezea polisi haya yote
mliyonitendea, nina uhakika na wewe utakwenda jela…..’akasema Maua, na mama yake
mdogo akageuza kichwa kwa nyuma na kumwangalia kwa dharau.
‘Thubutu….wewe huoni, kwanini wamenitoa huko rumande kwa
haraka, kama wao wanajiamini kweli kwanini hawakuendelea kunishikilia, na
ninakuhakikishia kuwa kesi dhidi yangu itafutwa…unacheza na mtoto wa
mjini….’akasema huku akisonya.
‘Haya kama una ndugu yako huko polisi endelea na kujiamini kwako,
huwajui polisi, ehe, wamekuachia huku wanakuchunguza nyendo zako,… mimi simo
kabisa, niliyo nayo yananitosha…ila nataka unipe huo mzigo, ulioambiwa kuwa ni
wa kwangu ….’akasema Maua.
‘Utaupata hapo nikishika milioni zangu …..’akasema huku
akiondoka zake, akionyesha kukerwa kuendekea kuongea na Maua.
‘Naona hapa hakuna raha , na hutaki kunielewa…..naondoka
zangu, nikahangaike, nikirejea hapa sitaki kelele zako…unasikia sitaki kelele
zako, nimechooka…’akasema na kuondoka.
Mama mdogo alipotoka nje, Maua kwa haraka na yeye akatoka, akamwangalia
mama yake anapoelekea , na akafunga mlango na kuanza kumfuatilia kwa
nyuma,….Mama yake huyo hakuwa na wasiwasi kuwa kuna watu wanamfuatilia,
aliondoka hadi sehemu yake anayofanyia shughuli zake.
Maua kwa uficho naye akaingia na alimuona mama yake akiongea
na baadhi ya watu, baadaye, akaingia kwenye chumba, …..Maua akasubiri, na
ikapita kama dakika kumi, baadaye mama yake huyo akatoka, akiwa kashikilia
mkoba wake, kama kawaida.
Mama mdogo hakukaa sana hapo kwenye shughuli zake, akatoka
na kuingia kwenye bajaji, na Maua naye akatafuta bajaji na kumuelezea dereva
anaomba aifuatilie hiyo bajaji….
‘Wewe ni shushu nini….?’ Akauliza mwenye bajaji
‘Hayakuhusu, wewe fanya kazi yako,….’akasema Maua.
‘Sawa bosi, maana naona huyo mama anafuatiliwa na watu
wengi, sijui kalikoroga,..’akasema dereva wa hiyo bajaji.
‘Watu gani wanaomfuatilia?’ akauliza Maua.
‘Angalia kwa nyuma yetu, kuna watu wanamfuatilia, toka
jana,…mama huyo alipotoka rumande, kuna watu wanabadilishana, mimi mwenyewe
jana walinichukua nimfuatilie,….’akasema huyo dereva.
‘Ulimfuatilia mpaka wapi?’ akauliza Maua.
‘Hadi ….Sinza, …’akasema huyo dereva.
Mama akakumbuka kuwa Sinza ndipo, docta alipouliwa, na huko
ndipo mama mdogo alipeleka huko mzigo, na huenda ndipo alipokuwa ameuficha huo
mzigo wake. Wakaendelea kumfuatilia na
safari hii huyo mama akaelekea kituoni Ubungo.
‘Huyu mama inaonyesha anasafiri au kaja kukata tiketi, kama
unataka nikusaidia mimi naweza kwenda kukufanyia hiyo kazi, uniongeze nauli
kidogo…’akasema huyo dereva, na Maua akaona hakitaharibika kitu, akamuambia huyo
dereva afanye hivyo.
Baadaye huyo dereva alirudi, na kumwambia huyo mama kakata
tiketi ya kwenda Arusha, …na Maua akachukua simu yake na kuwasiliana na
Inspekta.
‘Oh, tulijua atafanya hivyo,….tunashukuru Maua kwa msaada
wako, ‘akasema Inspekta.
********
Maua aliporudi nyumbani, mama yake alikuwa bado hajarejea,
na akilini mawazo yakamjia, kuwa aingie chumbani kwa mama yake afanya
uchunguzi, huenda, huo mzigo anaosema mama yake upo humo humo ndani.
Alitafuta ufungua wa akiba, ambao, ambao mama yake hakufahamu
kuwa Maua anaufahamu ulipo, akafungua ndani na kuanza msako,….alitafuta kila
kona nyumba, lakini hakuona huo mzigo, na wakati keshakata tamaa, akakumbuka
kuangalia chini ya meza.
Humo ndani kulikuwa na meza, ambayo juu yake kulipangwa
vifaa vya mama huyo vya kujiremba, ilikuwa meza kubwa, na chini kulikuwa na
uwazi, japokuwa kulikuwa na mbao inaonyoesha kuwa meza hiyo in sehemu,
iliyopigiliwa tu, lakini haina droo ya kuvuta,
Akainua ile mbao ambayo iliwekezwa bila kupigiliwa, akaona
begi la safari, …akakumbuka ni begi la huyo mama la safari, kwaharaka akalitoa,
na kulifungua, akatoa nguo kwa uangalifu ili azijeshe kama zilivyo, na kwenye
moja ka khanga, akaona imefungiwa, kiti.
Akaikunjua ile khanga, na mara akaona bahasha kubwa,
iliyokuwa na kitu ndani, akaichukua ile bahasha na kutoa kile kitu
kilichokuwepo ndani akaona mkanda wa video, na juu yake umeandikwa;
‘Zindiko –Dar…’
Kwa haraka akachukua mkanda uliokuwa umekwa juu ya ile meza,
uliokuwa mbovu, akauweka kwenye khanga na kuifunga kama ilivyokuwa awali, na
kurejeshea nguo kama zilivyokuwa zimepangwa, akalirudishia lile begi, na kuweka
kama ilivyokuwa na akatoka nje, na kufunga mlango.
Wakati anageuka akasikia mama yake mdogo akiongea nje,…
‘Huyu maua kaenda wapi?’ akasikia akiulia na Maua hakusema kitu,
akaingia chumbani kwake, na kuhakikisha ameuificha huo mkanda sehemu ambayo
hakuna mtu anayeweza kuuona, halafu aakjilaza kitandani.
‘Wewe Maua..upo wapi,…?’ akaiskia mama yake akiita.
‘Nipo nimelala…’akasema.
‘Umelala…hicho kimimba chako kinakufanya ujione bosi, au
sio, hebu toka huku, nataka unifulie nguo zangu, ….’akasema na Maua akatoka
nje, na kukuta lundo la nguo linamsubiri kufua.
‘Nguo zote hizo za nini..kwani unasafiri karibuni?’ akauliza
Maua.
‘Wewe hayo hayakuhusu, fanya lile ninalokuagiza..’akasema
mama mdogo akitoa sabuni ya kufulia.
Maua akaendelea kufua, hadi alipomaliza na mama mdogo
akatoka na sfari zake za mitaani. Na Maua alipomaliza hiyo kazi akaingia ndani
ya kuuchukua ule mkanda, na kwenda kwa jirani yake mwenye runinga ya kuangalia
kanda za video.
‘Rafiki yangu kuna mkanda nataka kuuangali, lakini nataka
niwe peke yangu….’akasema.
‘Hakuna shida, kwani mimi mwenyewe natoka, nina safari
zangu, wewe ingia chumbani kwangu, angalia ukimaliza funga mlango, funguo
nitazikuta kwako…’akaambiwa.
Maua alipohakikisha huyo rafiki yake kaondoka, akauweka huo
mkanda kwenye hiyo runinga na kuanza kuuangalia…..
********
Ilikuwa siku ambayo hataweza kuisahahu maishani, lakini hakutarajia
kuwa ndivyo ilivyokuwa siku hiyo, kwani mengi alishaanza kuyasahau,….na bahati
mbaya wakai mkanda huo ukiendelea hakuwa n fahamu, kwahiyo hakuweza kuyaona
yote aliyofanyiwa siku hiyo. Hata ule mkanda ulipofika mwishoni, alikuwa bado hajazidukana.
Maua alipozindukana alikuta ule mkanda umeshajizima, na kwa
haraka bila kufikiria zaidi akautoa huo mkanda wa video na kuondoka zake.
Alipofika nyumbani, akachukua kibiriti na mafuta ya taa, na
kuumwagia ule mkanda, akahakikisha umekuwa majivu, na yale majivu akayazoa, na
kwenda kuyazika chini, kuhakikisha kuwa hakuna kitakachoonekena baada ya
hapo….akaingia ndani na kwenda kulala,… na akiwa ndotoni akamuona;
********
‘Niambie ukweli wewe ndiye uliyenipa ujauzito huu?’ Maua
akauliza, na yule mtu aliyekuwa kalala kitandani akawa anajaribu kuinua mkono,
huku akiwa kanyosha kidole kuashiria jambo nyuma yake,lakini hakuweza….., na hapo
Maua akahisi huenda yupo mtu mwingine nyuma yake, akageuka hwa kuangalia,
lakini kichwa hakikuweza kugeuka chote, lakini alihisi kuwa kweli yupo mtu, na
hupo Maua akasikia sauti ya huyo mtu aliyekuwa nyuma yake akisema;
‘Nisamehe Maua, sikujua yote yalikwenda kiibilisibilisi…….naomba
unisamehe nisiendelee kupata taabu…’huyo mtu aliyekuwa nyuma yake akasema, na
Maua alijaribu kugeuza kichwa ili amwangali vyema, na kuiona sura yake lakini
hakuweza kumuona, akaona ni bora aulize;
‘Kwani wewe ni nani, …?’ akauliza Maua.
‘Mimi ni miongoni mwa wafu wanateseka, kwa matendo maovu
tuliyowahi kuyafanya duniani…’ile sauto ikasema, Maua alijaribu kuitafuta hiyo
sauti ni ya nani, lakini hakuweza kugundua, ilionekana kuwa akili yake imezuiwa
kumgundua ni nani, na ile sauti ikaendelea kusema;
‘Huku sote majina yotu ni sawa...na haina haja kunijua kwa
jina la kidunia…., ila ujue kuwa huku ndipo kule kulipoelezewa, na huku haki
haipotei, kwani kila jambo ulilotenda limenakiliwa liwe baya au jema, yote
utayakuta yamehifadhiwa….. , hata kama lilitendelea chini ya udongo, lakini
kama ulilitenda ukiwa hai, na ukalitenda hilo jambo kwa utashi wako, ujue kuwa
limeonekana na kunakiliwa …..
‘Kwahiyo ….Maua, ..binti….ya….ya…..nakuomba unisamehe…’sauti
hiyo ikasema na hayo maneno mengine hayakuweza kusikika, kwani kulikuwa na
sauti ya uvumi wa upepo, ukiwa mkali, na ulikuwa kama unayapeperusha hayo
maneno….
‘Nitakusameheje, na mimi sikujui, na wala sijui kosa
ulilonitendea, je kwanini ukaniita hivyo, na hisi kama unanifahamu
vyema,….kwani wewe ni nani …?’akauliza Maua.
‘Ukweli upo kwenye kanda ya video, kama uliiangalia vyema
kila kitu kilikuwa kikionekana humo.....’Na mara sauti ikasikika mbele yake
ikiita jina lake, na hapo akamkumbuka yule mtu aliyekuwa akiongea naye ambaye
alikuwa kalala kitandani….lakini kabla hajageuza kichwa na kumwangalia mara
akazindukana kutoka kwenye usingizi,….
Alipozindukana, alijiona kama anaelea hewani, akili ilikuwa
kama imesimama, na akawa anaangali huku na kule kuhakikisha yupo wapi, na
akajikuta akiongea peke yake na kusema;
‘Ina maana ule mkanda wa video ulikuwa na kila kitu…oh,
mbona nimeuchoma moto, kabla sijauona huo ukweli wote…’akasema akiinuka pale
kitandani, huku bado akijiuliza ile ndoto ina maana gani, lakini alijikuta
kichwa kikimuuama sana…akakimbilia kutafuta dawa ya maumivi ya kichwa…. Na mara
akasikia sauti ya mama yake mdogo ikiita;
********
‘Wewe Maua, bado umelala, mimi naondoka , kama
nilivyokuelezea, mtu akikuuliza mwambie nipo kwenye shughuli zangu…’akasema na
Maua akataka kusema jambo, lakini mama yake alishaondoka.
Maua akaamuka na kumpigia simu inspekta wa polisi ambaye
alimwambia kuwa wanamfuatilia kwa nyuma, kwani huenda akawafikisha kwenye
masalia ya hilo kundi;
‘Na haja yetu kwasasa ni kupta huo mkanda wa video, ambao
tunahisi una siri nyingi sana, na thamani yake ni kubwa sana, ndio maana kundi
nzima lilikuwa likuusaka huo mkanda….’akasema Inspekta.
‘Mimi sina uhakika na huo mkanda…’akasema Maua na inspketa
akamkatisha na kusema;
‘Usijali, sisi tuna usahidi kuwa anao mkanda, ….ambao
anatarajia kupata pesa nyingi kwa mzee, lakini huko Arusha anatarajia kukutana
na masalia ya hilo kundi, …tutawanasa wote na sheria itafuata mkondo
wake…..’akasema Inspketa.
Na alipomaliza kuongea na Inspekta, mara simu ya mama yake
ikaita, na akapoipokea na kuanza kuongea na mama yake;
‘Maua hawa mabinti wamefika hapa kwangu ,wanakuhutajia ufike
huko Arusha kwa ajili ya baba, yao, …mimi nimewaambia hilo halitawezekana, wao
wameniomba hadi kunipigia magoti, na wamesema hata nisema chochote
ninachokitaka wao wapo tayari kutoa…’akasema mama yake.
‘Mama hawa watu nimewachukia bila maelezo na kama ningelikuwa
na uwezo, ningewalipua wote kwa bomu…’akasema Maua.
‘Kwani imekuwaje?’ akauliza mama yake
‘Mama hawa watu ni wanyama, unakumbuka Tajiri alisema nifike
kwa docta , kuwa yeye ndio atanielezea ni nani aliyenipa uja uzito…’akasema
‘Si nimeskia kuwa docta kauwawa?’ akauliza mama yake
‘Ndio kauwawa, lakini kuna ushahidi ulioachwa….na hapo
nimegundia ni nani aliyenipa huo uja uzito, na …sijui mama nifanyeje?’ akasema
Maua.
‘Ni nani?’ akauliza mama yake.
‘Mama …naogopa hata kukuambia maana, wewe mwenyewe
hutakubaliana naye…’akasema Maua.
‘Mwanangu mbona unanitisha kwani ni nani huyo je mnaishi
naye huko?’ akauliza mama.
‘Mama …..hapa nilipo nawaza jinsi gani ya kufanya, japokuwa
sikuweza kuuangalia huo mkanda wa video wote, kwasababu ulipofikia sehemu hiyo
ya kuzalilishwa, niliishiwa nguvu, na kupoteza fahamu na nilipozindukana,
naliuchukua huo mkanda na kuuharibu…..’akasema.
‘Sasa kama umeuharibu, utapatia wapi huo usahidi ….?’
Akauliza mama yake.
‘Mimi nilipoona kule kuzalilishwa, sikuweza kuvumilia tena,
lakini kama ni shahidi…..wao walionifanyia hivyo wanajua na mungu
atawalipilizia. Mimi mwanzoni niliamua kuchukua hatua ya kupambana nao lakini…..tatizo
ni wewe, ambaye umenikataza nisiwakaribie..’akasema Maua
‘Una maana gani kusema hivyo?’ akauliza.
‘Kwasababu ulishaniasa, kuwa niskanyage mguu wangu kwao,
huwataki kabisa hawo watu…’akasema.
‘Mwanangu wewe nilikulea bila baba yako wa kukuzaa, na sioni
kwanini nishinde kumlea mjukuu wangu, wewe kama utaona huwezi kumlea niletee huyo
mjukuu wangu, ….lakini sitaki ufike kwenye hiyo familia, japokuwa walifika hapa
na kunipigia magoti….kuwa eti baba yao akikuona huenda akapona…’akasema mama.
‘Mama mimi nisingeliogopa kufika huko, kwani wanastahili
kuwajibika kwa hilo…lakini huenda nikashindwa kuvumilia nikikumbuka hayo
matendo niliyoyaona kwenye huo mkanda….ni bora nivute subira hadi hapo
nitakapojifungua….’ akasema Maua.
‘Mwanangu, uliwahi kuniulizia kuhusu baba yako, na kwa
bahati mbaya hatukuweza kufanikiwa kwa hilo, lakini mimi niliwahi kwenda na
kumuona familia ya huyo aliyesababisha maisha yangu kufikia hapa nilipo.
Japokuwa
sikuwa na uhakika na hilo…., ila safari hii nilipofika kijijini, nilifanya
utafiti na kweli NA mwanangu, …habari nilizozipata zilinielezea
ukweli…’akatulia.
‘Kwahiyo baba yangu yupo wapi, au ndio keshakufa kama
ulivyokuwa ukiniambia toka utotoni,…..?’ akauliza Maua.
‘Baba yako ….alishakufa moyoni mwangu, lakini bado alikuwa
hai kivyake…..na mungu alivyo wa ajabu, aliamua kunionyesha maiti yake, kabla
hajakwenda kuzikwa…na siku ile nilipomuona sikuwa na uhakika wa moja kwa moja
kuwa ndio yeye,….sasa hivi nimeamini kuwa ndiyo yeye..kweli hayupo hai tena…’akasema
Mama Maua.
‘Oh, kwahiyo kumbe ni kweli alishafariki dunia, na uliweza
kugundua alizikiwa wapi, na ni nani huyo?’ akauliza Maua.
‘Mwanangu, …..nilitaka kukuficha hilo, kwani sikupenda ujue
kabisa kuwa baba yako alikuwa ni nani, japokuwa nilikuhadithia kwenye kisa cha
maisha yangu, lakini sikupenda uje uonane naye..kwanza wa nini wakati
alishafariki kwenye moyo wangu…’akasema mama yake.
‘Lakini ni haki yangu kumfahamu …’akasema Maua.
‘Ili iweje….lakini kwa hali inavyokwenda nahisi unaweza
ukajikuta uniingia kwenye familia hiyo hiyo aambayo kwangu nilishaitoa moyoni,
na nisingelipenda mtoto wangu akaingia kwenye familia hiyo tena…’akasema mama
Maua.
‘Mama maisha hayo ni ya kizamani kuwa eti sitaki familia
yangu iolewe an familia fulani , au ukoo fulani au kabila fulani,…..siku hizi
kuoana ni maelewano,…labda kuwe na sababu nyingine ya kimsingi…’akasema Maua.
‘Nasema hivyo kwasababu ipo sababu ya kimsingi, na mimi
ndiye niliyekulea na kwa taabu,….nisingelipeda baada ya uvumilivu wote huo,
mateso na taaabu zije zikuandame na wewe …..hapana mwanangu, nakuomba tena
sana, sitapenda kabisa urejee kwenye hiyo familia…’akasema mama Maua.
‘Una maana baba yangu anatokana na familia ya …huyo mzee,
….ina maana ….mbona mama sikuelewei, naomba uniabie ukweli….’akasema Maua.
‘Ndio baba ayko anatokana na hiyo familia ya huyo
mzee….’akasema mama na kumfanya Maua aanze kujisikia vibaya..
‘Maua…Maua….’simu ikawa anaita,lakini akili ya Maua ilikuwa
imeganda, haikuwa inasikia hiyo sauti, kwani kumbukumbu za ule mkanda zilikuwa
zikimcheza akilini…akawa anaapa kimoyomoyo, kuwa wote waliomfanyia hivyo,
atawalipilzia kisasi…lakini hakujua ni kisasi cha namna gani….
‘Mama hivi ni nani huyo baba yangu…?’ akauliza Maua akiwa
anaanza kulia.
‘Wewe unaanza kulia,….hujamsikia baba yako ni nani, je mimi niliyetendewa hivyo,
nilijiskiaje,…..’akasema mama yake.
‘Huoni hata mimi wamenitendea kile kile walichokkutendea
wewe..na kwanini tuwaachie watuzalilishe kiasi hicho’akasema Maua.
‘Ndio maana naona ni bora ukaachana nao,….kama ni adhabu,
wameshaipata….japokuwa wana utajiri, lakini hawajawahi kuishi kwa
raha…..’akasema Mama Maua.
‘Mama naomba uniambie baba yangu ni nani…’ akatulia
akisubiri na alipoona mama yake hasemi kitu, akasema kwa ukali;
‘Mama, …utaniambia au huniambii, maana naona mwisho wake simu
hii itakatika, na nishindwe kumfahamu vyema huyo baba yangu, je huyo baba yangu
ni mzee, au …..?’ akauliza akiwa kakunja uso.
‘Baba yako sio huyo mzee, …baba yako ni Tajiri….’akasema
mama Maua.
‘Mama, eti…unasema ni..ni..nani …..Tajiri. Una maana huyo
Tajiri marehemu, haiwezekani mama, haiwezekani mama, mungu wangu nitafanya nini
mimi mama, jamani ni mkosi gani huu tena, mama..oh,….ohooooh….’Maua hakuweza kuvumilia,
kichwa kikawa kinamuuma, na kiza kikatanda usoni, na ghafla aakshikwa na
kizunguzungu,akadondoka chini na kupoteza fahamu.
‘Maua….Maua…..’mama yake akawa anaita kwenye simu, ….lakini
hakuna aliyemuitikia….
********
HITIMISHO:
‘Baada ya hapo niliamua kuharibu mawasiliano yote na watu wanaonifahamu,akiwemo
mama yangu….mzee na mabinti zake, niliona ni vyema nibebe jukumu hili peke
yangu hadi hapo nitakapojifungua. Baada ya hapo ..sijui itakuwaje….
‘Mama mdogo alipotoka
kifungo cha mwezi mmoja, ambapo alikuja kuachiliwa baadaya kukosekana ushaidi
wa moja kwa moja wa kumuhusisha na hilo kundi.., hasira zote alizielekeza
kwangu na kunifanya mimi ndiye mfanyakazi wake wa nyumbani. Sikujali, niliamua
kuwa hivyo, nikijua kuwa yote hayo yana mwisho, na kunitendea kwake hivyo, sio
kosa lake, ni kosa la roho yake mbaya….
Yote hayo
sikujali,..niliona ni bora nikae kwake hadi hapo nitakapojifungua huyo mtoto,
huenda huyo mtoto akawa ndio faraja yangu…na huenda baada ya hapo nitakuwa na
maamuzi yaliyosahihi….hata hivyo …sijui kama ni uamauzi sahihi, sikuwa na
uhakika na uamuzi huo….’akasema Maua huku akijilazimisha kutabasamu
Nilimwangalia huyu
binti kwa macho ya huruma, nikitamani aendelee na kisa hicho, kwani kilikuwa
bado na maswali mengi, na huyu binti aliponiona hivyo akasema;
`Ndio maana siku ile
uliponikuta pale nje, nikiwa nimejikunyata, (rejea mwanzo wa kisa hiki hapa)..nilikuwa
nikiwaza maisha yangu ya mbeleni yatakuwaje, je ina maana taabu, mashaka ,na madhila
ya duniani, yanayotokana na historia ya kizazi changu(kizalia)? , je nifanyeje
ili kuondoakana na hicho kizalia?....’
‘Nilisakamwa na
mawazo mengi, kwani hata mama mdogo ambaye nilimuona kama ndiye aliyeniingiza
kwenye shida hizi hakuwa na msaada kwangu zaidi ya kunilaumu kuwa mimi ndiye
nilimkosesha mamilioni ya hela, sasa je niendelee kuteseka kuwa mtumwa wake, au
niende kwa hao walioamua kuizalilisha familia yangu..? sikutaka kabisa mama
yangu mzazi ahusikane na haya….
‘Bado kuna maswala ya
kijamii, je nikiamua kumuendea huyo mzee, na kuwa naye, kama anavyotaka, jamii itanielewaje,je mama atakuwa radhi na
mimi, kwani yeye alishanikanya kwenda huko, na kama mama yangu namuheshimu
sana, ukizingatia jinsi gani alivyonilea kwa shida? …..’ akatulia kidogo, na
baadaye Maua akasema
‘Kwakweli hapa nipo
njia panda…sijui hata nichukua uamuzi gani….’Maua akashika kichwa kwa
masikitiko, huku akiniangalia, kuashiria kuwa huenda anahitaji ushauri au
nasaha, kuniangalia kwangu mimi, kakuangalia na wewe, je wewe ungamshauri nini.
Maua akatulia,huku
akiwa kashika kichwa, akainama chini , na alipoinua kichwa chake machozi
yalikuwa yametanda machoni mwake, na kusema.
‘Hicho ndicho kisa changu walimwengu….’
%%%% MWISHO.%%%%
NB Nawashukuruni sana wale wote tuliokuwa pamoja kuanzia
mwanzo wa kisa hiki hadi hapa kilipofikia, natumai ujumbe wa kisa hiki umefika,
japo kulikuwa na mengi ya kuendeleza, lakini inabidi kisa kiishe ili kiingie
kingine….
Huenda kuna makosa ya hapa na pale au kutokurizika kwa hili
na lile, kama binadamu siwezi kuyaepuka hayo, ….nawaomba tusameheane kwa hilo,
na kama una maoni usisite kunitumia kwa e-mail yangu:
miram3.com@gmail.com.
Mwisho wa kisa ni mwanzo wa kisa kingine. Japokuwa kwa sasa
nipo kwenye mitihani ya kimaisha, lakini
tutajitahid tuwe pamoja…Tuombeane heri…
WAZO LA LEO:
Tunapoishi na watoto wa wenzetu, tuwatendee wema sawa sawa , kama
tunavyowatendea watoto wetu, kwani wao ni haki yao, na wewe ni mzazi kama huyo mzazi
wa huyo mtoto unayeishi naye. Na ili tuweze kufikiria hilo, kumbuka machungu ya
uzazi, ulioupata kwa mtoto wako, ukumbuke kuwa na uchngu huo huo aliupata mwenzako
…kwali hali hiyo sote tu wazazi na kama wazazi basi sote tuna jukumu la kulea
tukikumbuka kuwa;
Uchungu wa mwana
aujuaye ni mzaziNi mimi:
emu-three
1 comment :
Kaka asante kwa kisa kizuri. Nimekuwa nikifatilia hadithi zako katika blog yako. Nimejifunza mengi, nimeburudika sana. Mungu akutie nguvu uendelee kutoa hadithi nyingi.
Ndimi msomaji
Elinasa
Post a Comment