‘Dereve wado wado,….
juu kwa juu….hapa kuna mtiti, lakini mbayu wayu ni wengi, ….’ Hii ni sauti ya
kondakta wa mabasi yatokayo Msasani hadi gongolamboto, ni kawaida yao ya
kutokusimama kituoni, kwani abiria wao ni wengi, na hawana haja ya kupiga debe,
…na kwa vile kuna wanafunzi, na hawawataki wanafunzi waingie kwenye mabasi yao,
…..wanachofanya wao ni kuendesha basi huku abiria mmoja akidandia….ni hatari
Kwa hali kama hiyo ya `juu kwa juu…’ wanaoweza kudandika
hayo mabasi wengi ni vijana, wazee na akina mama hupata shida sana,…na
inawalazimu wapande hayo mabasi wakati yakipita kwenda Gongolamboto na
kuwalazimu walipe nauli ya kwenda huko na kurudi nalo, nauli mara mbili,
wakisema buku haina chenji, …huu mtindo wa kulipa nauli mara mbili wanauita
`kegeuza nalo’…hiyo pesa haiendi kwa mwenye basi.
Hayo ndo maisha ya asubuhi na jioni ya wakazi wa eneo
hili,..ili uwahi kibaruani, au kuwahi kwenda kuhangaika kutafuta riziki yako na
huenda ili uipate inabidi kuelekea maeneo hayo ya mbali na, inakubidi uamuke asubuhi
sana, muda wa alifajiri asubuhi , na unarudi saa tatu usiku,au zaidi…..kiasi
kwamba kwako unapoishi, unajiona upo mgeni kila siku.
Haya ndio maisha yetu, hata hapo utakapoilipia haki yako
bado kuna adha nyingine,…hii ni adha ya foleni, hutaamini, mtu anaweza akafika
Morogoro kutoka Dar, lakini yule wa kutoka gongolamboto hadi Msasani
hajafika….wenye mamlaka hili hawalioni, wanachoona ni gharama zao zirejeshwe,
lakini zirejeshwe na nani,….mbona anyesababisha haya habebeswhi mzigo,
anayebebeshwa huo mzigo ni abiria, mlaji, mwananchi wa kawaida….
**********
‘Juu kwa juu, ndio maisha yetu siku hizi, kila jambo, lazima
liwe hivyo….juu kwa juu, hata biashara, au makubaliano ya biashara maofisini,
bila `cha juu’ hutajafanikiwa, ‘juu kwa juu’….ukiona mabosi au watu wa kitengo
cha mauzo, wakifukuzia jambo, unaweza ukazania kuwa hawa watu wanawajibika
kweli kweli…. , kwa manufaa ya kampuni yao, lakini ukiuliza zaidi utagundua
kuwa ndani ya hicho wanachokifukuzia kuna `cha juu chao’ ….
Hata siku hizi ukienda hospitali, ili mgonjwa wako atibiwe
haraka, lazima uwe na cha juu kwa mfukuziaji, muwezeshe yule unayeona
atafanikisha hilo jambo lako, ili faili lifike kwa dakitari haraka, na kama
mgonjwa wako kalazwa, docta aweze kumtembelea mara kwa mara…ukitaka iwe hivyo,
mkono wako usiwe mnzito,…..toa cha juu, hayo ndio maisha yanatotuzunguka, kama
huna basi cha moto utakiona.
Hata ukienda kimtaifa, angalia kwanini mataifa makubwa
yanavamia sehemu, yakijifanya yanatetea hicho kinachoitwa `haki za binadamu’ na
hata kukimbilia kupiga vita nchi fulani, wakisingizia hili au lile, chunguza
rasilimali za hiyo nchi, kama sio mafuta ni madini, yanayofukuziwa….ni nini
hicho kama sio cha juu kwa ajili ya manufaa ya hawo wanaoitwa `bwana wakubwa’
Pia angalia hawo wakuu wan chi, wakiwa wanatembelea mataifa fulani, mara kwa mara , sio bure, `kuna cha juu chao huko…’
Kama unabisha angalia mataifa yenye uwezo wao, yanayomiliki
hizo silaha za maangamizi, hawagusi, ni mazungumzo kwa kwenda mbele,…wanaogopa
au kwa vile hakuna maslahi….tunarudi kule kule, ni kwa vile huenda hakuna `cha
juu….’
********
Wakati nayawaza haya, nikamkumbuka babu yangu akituasa hasa
pale anapotuona tunahamanika na jambo fulani, au akituona tunagombea kitu
kidogo, au kubishania jambo fulani…ubishi kidogo unatupelekea hadi kutukanana,
au hata kushikana mashati,…lakini ni nini yote haya, huenda kwa utoto wetu
tulikuwa tukifanya hivyo tukiwa ni `watoto..’
Sisi wakati huo kwa utoto wetu, tulikuwa tukibishana bila
kuelewa athari za mambo hayo, na wakati mwingine ni kwa ajili tu ya kukwepa
kuwajibika, au kutafuta sababu ya kutegeana, kila mmoja akimtupia mwenzake
lawama kuwa yeye ndiye anayestahili kufanya. Na hili sio la utotoni tu, angalia
maisha yetu ya kila siku yalivyo, watu wataanzisha mjadala usio na tija, ambao
utakwenda hadi kurushiana maneno mabaya…tujiulize ili iweje,….je baada ya
ubishi huo kuna faida au hasara, au ni njia ya kupoteza muda tu.
Kwa wengine hayo kwao ni faida, ….lakini huenda wengine
wanafanya hivyo, ili mwisho wa siku litokee ambalo huenda lilipangwa liwe
hivyo,..swali kubwa hapa ni je hayo yote yanafanyika kwa maslahi ya nani….jibu
unalo mwenyewe….turudi kwa babu
‘Wajukuu zangu, kama mngelijuwa thamani ya kujitolea katu
msingalitegeana, msingelipoteza muda kwa kubishana jambo lisilo na manufaa, au
kutukanana, ….hizi lugha zisizo na busara, hazitawasaidia, sana sana, ni kuwapa manufaa majirani na wapiti njia…
‘Wajukuu zangu, kama
mngelijua athari ya kupupia, kugombea kile kidogo mlichojaliwa nacho, badala ya
kugawana sawa, au kwa haki, …..au kutaka ziada au hicho kinachoitwa cha juu,…nawaambia
ukweli mngelijua madhara yake, hata siku moja msingelipenda kurudia hayo mnayoyafanya ambayo
mwisho wake sio mwema, …hayo ya kula au kupata jambo bila kufikiria uhalali
wake…ni hatari, sio kwa afya zenu tu, bali pia kwa amani na utulivu
wenu….’akasema na sisi tukawa tumesimama tukiangaliana.
‘Wajukuu zangu hebu sogeeni hapa niwape mambo
yajayo….’akasema babu.
************
Ikabidi ile fuko, kuzozana na kutupiana vijembe, ikaisha na
sote tukamfuata babu, na wale wasiokubali kushindwa wakaanza kulalamika na
kusema;
‘Babu naye bwana, badala ya kutupigia hadithi, unataka
kutuambia mambo yajayo…mambo yajayo yanatuhusu nini, wakati sisi ni taifa la
leo….’akalalamika kaka yetu.
‘Wewe unajua nini, ujinga tu umekujaa kichwani…..ubishi tu,
twende kwanza tukamsikilize babu….’akasema ndugu yetu mwingine.
‘Unaona huyu ananitukana, ananiambia mimi ni
mjinga,….’akalalamika kaka.
‘Kama anakuambia wewe ni mjinga, basi mwambie yeye mwerevu
wa wajinga….’akasema babu na kutufanya tuangaliane tena huku tukimsogelea. Hasa
sisi tunaomjua babu, kuwa akiwaitia jambo….kuna jambo….tena sio la hivi hivi,
japokuwa kwa muda ule tuliona sio la muhimu sana, lakini sasa tunaona umuhimu
wake…na kila akizungumza jambo mwisho wa siku atatoa kisa kizuri…ambacho
baadaye nimegundua kuwa ni hazina kubwa ya maisha yetu.
‘Sikilizeni wajukuu zangu, maisha ya kuhamanika, na
kutamani, hata kile kisichokuwa chako, ni hatari, ni sawa na kujaza gunia, vitu
vingi kwa wakati mmoja bila kujali kuwa vingine vitaharibika au kuharibu vingine,…je
unaweza ukachanganya magarage , unga, mahindi kwenye gunia moja….’akatulia
kidogo kutafakari jambo.
‘Ngoja niwape siri ya kufanikiwa katika maisha, …’akasema na
kutulia.
‘Kuna mambo muhimu katika maisha na ukiiyajulia hayo,
hutahaangaika kamwe, na moyo wako utakuwa umejaa lulu ya utajiri, wa `kinaa’
moyo wa kurizka kutokana na kile ulichojaliwa nacho,…wewe utajiona tajiri,
kuliko yule mwenye magari na majumba, na ukichunguza ndani yake hana raha
kabisa….’akasema babu.
‘Haiwezekani babu,
ina maana gani sasa kuitwa tajiri, uwe na mipesa, magari, nyumba na kila kitu
cha kifahari, na bado usiwe na raha?’ akauliza ndugu yetu mmoja ambaye ni
mdadisi sana.
‘Kwasababu utajiri wake, aliupata kwa kupupia, aliupata kwa
kulimbikiza vya halali na visivyo vya halali, mali yake ina jasho la watu,
ambalo lipo mikononi mwake, na jasho hilo kwa vile ni la watu linamuandama , na
matokeo yake, ndio hayo,….moyo wake hautulii,….kwa kelele za waru wakidai haki
yao japoukuwa hawapo hapo,….
‘Hawa watu wana shida kweli, kwa jinsi walivyojijengea
maisha yake, hawawezi hata kukumbuka hilo, kuwa utajiri wake, una ziada za
watu, na wangelikumbuka hilo, wakazitoa hizo ziada za watu, wasingepaat shida,
kamwe…wangeliishi kwa raha mstarehe…..lakini wapi, maisha yao yamejaa pupa na
kuhamanika na hicho cha ziada (juu kwa juu), …ndio maisha hayo, kama ya
kukimbilia dala dala kama huwezi kudandia unaachwa na basi….’akasema babu na kutulia.
Tulicheka, kwa kipindi kile tulikuwa hatujui alikuwa na
maana gani na ni nini msingi wa maneno yake hayo,…nimekuja kuyagundua hivi sasa
katika maisha halisi….babu huyo akaendelea kusema;
‘Niwaambia siri moja ya maisha ….siri ya jinsi ya kufanikiwa
katika maisha yenu ya baadaye,….?’ akatuuliza na sisi tukasema
‘Tuambie babu..ili tuwe matajiri, kama akina…..’ tukaangaliana
tukitaka kuwataja matajiri tunaowafahamu. Babu akatabasamu na kutuangalia kila
mmoja kwa zamu yake, na baadaye akasema
‘Mfano umepita njiani ukaona mwiba, upo kati kati ya
barabara, utafanyaje?’ akatuuliza babu.
‘Nitauruka huo mwiba , na kuendelea na safari zangu….’akasema
kaka yangu kwa kujiamini
‘Mimi babu, nitausogeza pembeni ili usinichome, nipite, ili
niwahi nisije nikachelewa kama nimetumwa, kwasabbu ukichelewa
utachapwa…’akasema mwingine na mwingine akatoa hoja yake na mwingine na mwingine,
na babau alipotuona tumeishiwa na hoja akasema;
‘Unaona hapo kila mmoja anachojali ni yeye, ubinafsi wake …ili
apite…., hajali mwenziwe anayekuja nyuma, hajali kuwa kuna wenye matatizo ya
macho hawataona huo mwiba, hajali kuwa wapo watoto, hata watoto wake, au jamaa
zake wanaweza kupita hapo na wakaukanyaga bila kuuona huo mwiba….
‘Ndivyo maisha yetu yalivyo, kila mtu anataka apate,
afaidike zaidi,….hata maofisini, bosi anataak zaidi nna zaidi, anajilimbikizia
marupurupu, akiona hayo ni haki yake, …..wewe au yule anachojali ni kufanya
jambo kwa manufaa yake, kama mfano huo wa mwiba, kila mmoja anajojali na
kuangalia jinsi gani afanye ili awahi afike huko anapotka kwenda….
‘Ndio dunia yetu ya sasa hakuna anayejali kuwa huenda yeye
anahitaji kufanya jambo, ili na mwenzake apate, hebu fikiria kila mmoja
angekuwa na mwamko huo, kuwa afanye jambo ili na mwenzake apate dunia
ingekuwaje, lakini hata hivyo tukumbuke kuwa…..kuna watu wengine wanastahili
kupata riziki zao kwa kupitia watu wengine…
‘Hilo hatuwezi kulijua kamwe, kwasabbau ya ubinfasi wetu na
uchoyo wetu, hatutaki kuzitoa hizo
riziki , hatutaki kujitolea,... hebu niambieni wagonjwa, mayatima, na
wasiojiweza riziki zao zinapatika wapi kama sio kwa kupitia kwa watu
wengine….sio hao tu, hata wale wanaojiweza, wengine wanastahili kupata kwa
kupitia wengine, huo ni mpango wa muumba, sisi hatuwezi kuujua…..
‘Tunatakiwa tujitolee, tusitegeane, ili tuweze kuwekeza
kwenye riziki zetu, na tukifanya hivyo, tutapata , tutafaidiki, sote na mioyo
yetu itakuwa na amani……’akaendelea babu….na maelezo yake
*******
Nilipokumbuka hiyo kauli ya babu ya `kujitolea kwa ajili ya
watu wengine’ nikamkumbuka jamaa mmoja wakati tukiwa shuleni.Jamaa huyo alikuwa
akipenda kujitolea sana, hadi tukamuita jina la `Valmeti,(majina ya matrekta
)na kwa sasa tunapenda kuwaita watu wa namna hiyo kwa majina `majembe’…..hilo ni jembe
Jamaa yangu huyo, alikuwa akipenda kujitolea na kuwa mbele
kwa kila jambo la kujitolea, tofauti na
wengine, kama ujuavyo `utoto’ na hulka
ya utoto, wengi hupenda kutegeana kwenye kazi zozote. Lakini mwenzetu huyu,
hata siku moja hakupenda kabisa kutegea, akiona mnasita kufanya jambo fulani,
yeye husema’`ngoja nifanye mimi, niachieni nifanye mimi….’
‘Valimenti hilo…’basi tunamshangilia, na yeye bila hiyana, atavua shati lake la shule na
kubakia kifua wazi, na atalifanya jambo hilo huku wenzake tupo nyuma tukimwangalia
na kukonyezana, na hata kuelekeza,
`fanya hivi, sogeza kule,….na wengine hata
kumuona ni `mjinga au anajipendekeza vile’ lakini kumbe mwenzetu alikuwa na siri
yake, siri iliyojaa hekima ndani yake, na hekima hiyo aliipata toka kwa usia wa
babu yake.
Tatizo hivi sasa, hatuwajali wazee, babu zetu na bibi zetu,
….watu wanawageuza babu na bibi, kuwa sio wanadamu wanostahili kuishi, na wengi
wakiwaona wazee hawa, na mabadiliko ya miili yao ya macho, au mkunyazi kwenye
nyuso zao hukimbilia kuwaita `wachawi..’ vigagula…ni kama vile watu wa dar
walivyo sasa hivi, wakiona paka wanampiga mawe na kuwafukuza, ukiwauliza
kwanini, utasikiwa wakisema
‘Wanga hawo….’
‘Jamani toka lini paka akawa mwanga,…ni utaalamu gani huo wa
kisayansi, uliowawezesha hawo wachawi wakaweza kumgeuka mtu , au wao kugeuka kuwa
paka, kama ni hivyo, mbona tungekuwa matajiri, maana mnaweza kujigeuza vyovyote
mtakavyo, na kwa mtindo huo mnaweza kuingie popote, na kama tuna uwezo huo kwanini
tusiwe matajiri…..au uchawi hauna mema, hautaki mtu kuwa tajiri
Sasa imefika hatua wazee wetu, hazina ya hekima, baraka ya
dunia, tunawaita wazee hawa `vigagula, wachawi, tunawafananisha na hawo paka, ….wanga,
wala nyama za watu….tunajisahau kuwa , ni swala la muda tu, kesho na kesho
kutwa, na wewe utakuwa kama huyohuyo babu au bibi….na wewe ni mwanga , kigagula
au mchawi mtarajiwa, au sio.
*********
‘Mjukuu wangu, unaona
maisha tuliyoishi, huna baba, baba yako alikukana, akasema wewe sio mtoto wake,
kampa mama yako uja uzito, na baadaye akadai kuwa sio yeye peke yake aliyekuwa
na urafiki na mama yako,… huenda mimba hiyo sio yake, na hata ulipozaliwa
hakutaka kabisa kukulea…lakini baadaye akaja kuishi na mama yako…..’Babu akawa
anamsumilia mjukuu wake na huyu
mjukuu wake ndiye aliyekuwa akinisimulia hiki kisa….
Tuanze kisa hiki ambacho tutakiita tenda wema uende zako au
wema hauozi..
NB: Nilipatwa na misiba ya wapendwa wangu, shemeji yangu, na
mtoto wa mdogo wangu, misiba hii ilifuatana, kwahiyo nimekuwa nipo sipo ndani ya diary yangu, Yote mapenzi ya mungu. Na mungu akipenda tutakuja na kisa hiki cha WEMA HAUZI,…
WAZO LA LEO:
Uchungu wa matatizo hauelezeki, yule aliyepatwa na hayo matatizo ndiye anayeweza kujua ni kiasi
gani uchungu huo ulivyo. Tujaliane hasa mwenza anapokuwa kwenye matatizo,
ya ugonjwa, au misiba, kwani hayo yanamkuta kila mtu.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Duh..kaaaazi kwelikweli nasubiri kwa hamu hiki kisa..Tupo pamoja ndugu wangu,,
Post a Comment