Wakati uchunguzi wa polisi ukikamilika kuhusiana na kadhia
nzima ya genge la wauza madawa ya kulevya na wala mlungula(blackmailer), na
kesi za maujaii zilizotokana na maswala hayo. Maua alipata mwanya wa kwenda
kuonana na mama yake mdogo ambaye bado alikuwa kashikiliwa kuisaidia polisi, na
alipofika hapo alimkuta akiwa mnyonge sana;
‘Mama vipi, unaumwa, au ni hali ya jela?’ akauliza.
‘Jela nani kafungwa jela, hawa wameniweka rumande, na
nitatoka muda sio mrefu na nikitoka hapa nawafungulia mashitaka kwa kunipotezea
muda wangu bure….’akasema kwa sauti kubwa.
‘Mama mdogo, kwanini unaongea hivyo, unataka kila mtu
akusikie huoni unajiharibia ….’akalalamika Maua.
‘Kwanini niogope kuongea kwa sauti, ..nitaongea hivyo hivyo
kwa vile ninajiamini kuwa sina hatia, ….’akasema kwa sauto ile ile.
Baadaye Maua alikwenda kuonana na mkuu wa upelelezi ili
kujua hatima ya dhamana ya mama yake, na huko ndio akapata maelezo ambayo
hakuyatarajia;
‘Maua nilikuwa mbioni kuja kuonana na wewe, baada ya kuongea
na mama yako na kukubaliana kuwa yupo tayari kushirikiana na sisi,…..kwa
ujumala kundi nzima la hawa wauza madawa na wala mlungula, lilokuwa na makao
yake pale Mererai tumelisambaratisha, lakini kuna matawi yake, …..ambayo
tunataak kuhakikisha na yenyewe yanakufa….’akatulia.
‘Katika uchunguzi wetu, tumegundua kuwa mama yako mdogo
alikuwa akitumika hapa Dar, kuunganisha mambo yao ….alikuwa kama mtumishi wa
kutafuta mabinti, ambao walitumika kukam ilisha kazi zao…’
‘Na tulikuja kugundua kuwa hata wewe ulikuwa mmoja wa
mabinti walioingizwa kwenye kukamlisha kazi zao hizo, lakini tulikosa ushahisi
wa moja kwa moja,….na tulikuwa mbioni kuoanana na wewe ili utusaidie kwa
hilo…..’akamwangalia Maua.
‘Mimi nitawasaidia kwa vipi?’ akauliza Maua.
‘Ni rahisi tu, …kinachohitajika ni kuelezea walichokufanyia
hawa watu, na ni nani, na kama kuna njia yoyote ya ushahidi,….kwani tuligundua
kuwa walikuwa na utaratibi wa kuweka kumbukumbu za video, video ambazo walikuwa
wakiwatumia wahanga wao, je wewe hawakuwahi kukutumia kanda za vide?’
akaulizwa.
‘Hata kama walinitumia nisingeliweza kuowaonyesha, kwasababu
ni mambo machafu….sitaki hata kusimulia…’akasema Maua akionyesha hasira nz
huzuni.
‘Pole sana…na nia yetu sio kuwadhalilisha na hizo kanda za
video, kwani kuna utaratibu wa kimahakama ambao utalinda heshimz zenu,
hatutazionyesha hadharani, ila zitatusaidia kama vielelezo, ili haki
itenedeke….’akasema huyo mkuu.
‘Nisingeliweza kuziweka kanda hizo, na popote
nitakapozipatanitazichoma moto….’akasema Maua.
‘Kwahiyo unasema kuwa waliwahi kukuumia hizi kanda, kwa yale
waliyokufanyia?’ akauliza.
‘Mhh, ni kweli walifanya hivyo, lakini ….’akatulia.
‘Maua najua jinsi gani unavyojisikia, lakini ni vyema
tukasaidiana na hili, ili haki yako ipatikane, na walihusika waadhibiwe…’akasema.
‘Wameshakufa, wataadhibiwa kaburini….’akasema Maua.
‘Hawo ni baadhi, tuna uhakika kuwa kulikuwa na kundi kubwa
la watu, hata kama viongozi wao wameshakufa, lakini wale wote waliohusika ni
lazima wafikishwe mahakamani ili iwe ni fundisho kwa wengine…’akaambiwa.
‘Sasa mimi nitawajuaje?’ akauliza Maua.
‘Kama tungelipata hizo kanda, tungelijua jinsi gani ya
kufuatilia…na ndio maana bado tunamshikilia mama yako mdogo kwani tunahisi anao
ushahidi kama huo..’akasema huyo mpelelezi.
‘Mimi kwakweli sijui, maana mama yangu mdogo ana mambo yake
na hapendi kuingiliwa, mimi sina uhakika na hilo, ila ninachojua, ni kama
mlivyosema, kuwa kuna watu kwasababu ya shida walijikuta wakiingizwa kwenye
kufanikisha matakwa ya hawo wahalifu, na mama mdogo naye alijikuta kwenye huo
mkumbo…’akasema Maua.
‘Kama mama yako mdogo angelikubali kushirikiana na sisi,
kesi yake ingelikuwa ndogo,…tungemshirikisha kama watu waliojitolea kuisaidia
polisi, na kimahakama angeliweza kusamehewa, kwani kwa mtindo huo atakuwa kakiri kosa, kuwa alishirikishwa
bila kujua, na pili kaisaidia serikali kuhakikisha hawo watu
wanakamatwa..’akaambiwa.
‘Sasa mnataka mimi nifanyeje?’ akauliza Maua.
‘Mshawishi mama yako mdogo, ….sisi tuna mbinu nyingi za
kushawishi, lakini hatupendi kufikia hatua hiyo kwa mama kama huyo, lakini
ikibidi tutafanya hivyo, ….sasa kabla hatujafikia huko hebu jaribu kuongea naye
mshawishi, …..’akaambiwa.
‘Mimi sizani kama ninaweza kumshawishi mama mdogo,
ninamfahamu sana,…yeye ukitaka kumpata uwe na pesa,…pesa kwakwe ndio kishawishi
kikubwa…’akasema Maua.
‘Oh,…sawa wewe kaongee naye kwanza, sisi tutajua jinsi gani
ya kufanya, ahsante sana kwa ushiriukiano wako’akasema huyo mkuu.
******
‘Siku nilipofika kwa docta na kuongea naye, aliniambia yote
yaliyotokea siku ile ulipobebeshwa hiyo mimba…’akasema mama mdogo baada ya
kuachiwa kwa dhamana, na kukubali kushirikiana na polisi.
‘Ilikuwaje ?’ akauliza Maua kwa shauku.
‘Sijui kilichokuwa kimetendeka huko ndani, na wala sikuwa
ninafahamu kuwa docta alikuwepo siku hiyo….’akasema mama mdogo
‘Sasa ulijuaje?’ akauliza Maua.
‘Nilipofika kwa docta nikiwa na mzigo, mzigo ambao thamani
yake ni milioni ishirini na tano, …nilimwambia kuwa ili aupate huo mzigo wake,
inabidi tugawane, hizo milioni, au tukubaliane jinsi gani ya kugawana…’akasema mama
mdogo na kumfanya Maua atabasamu, na huku akimwangalia mama mdogo kwa macho ya
kumshangaa.
‘Wewe tatizo lako hujaamuka, hujui hawa watu
walikuwaje,…mimi nilikuja kugundua kuwa hizo ndio kazi zao, wanachokifanya ni kuwarubuni
watu, na baadaye wanachukua picha zao mbaya kwa ajili ya kuwatishia kuwa
wasipotoa pesa wanazipelekea hizo picha sehemu ambayo inaweza kumharibia huyo
mtu maisha yake…na wanachagua sehemu ambayo kweli wakizipeleka kama ni bosi,
ubosi unaondoka, na kama ni mwanandoa, ….ndoa inaharibika, maana wanaweza hata
kuupeleka huo mkanda kwa wakwe zako….’akatulia.
‘Maua unisamehe sana kwa hilo,…japokuwa nitakulaumu kwa
kutokutoa ushirikiano, maana sasa hivi tungelikuwa matajiri….’akasema huku
akibenua uso kwa hisia za kukata tamaa.
‘Hata hivyo sikupenda kukuingiza kwenye uchafu huo, lakini
nilikuwa na hali mbaya kipesa, na nikaona wewe ungelinisaidia kwa hilo, ndio
maana nilikuingiza huko….lakini kwa mitego, kuhakikisha kuwa ninakuwepo kila
hatua, ili wasije wakakufanya vibaya…wao waliniambia kuwa wanahitaji binti
mdogo, ambaye hajaguswa, nikaona wewe ni dili…’akatulia.
‘Kwa muda ule nilichokuwa nimejali zaidi ni pesa….’akasema
huku akionyesha vidole kuashiria pesa.
‘Sijui walijuaje kuwa nakulinda, na walitaka waniondoe
kinamna… walichofanya ni kunilewesha sana , ili nisipate muda wa kuwa karibu
nawe, kwani nilipanga kuwa kila hatua nitakuwa karibu nawe, ili wasije
wakakudhuru,…mimi nakujali sana, wewe hujui tu, ilitokea bahati mbaya….’akasema
akimwangalia tumboni.
‘Japokuwa kwa sasa utakula jeuri yako, maana hatuna pesa, na
wewe una huo mzigo, ….hapa nyumbani kwangu, nakuambi aukweli, wewe sasa utageuka
kuwa mfanyakazi wangu wa nyumbani….’akasema akikunja uso kwa hasira.
Maua hakusema neno akasubiria mama mdogo aendelee na maelezo
yake, akisubiria kusikia kile alichokihitajia. Mama mdogo alipoona Maua hasemi
kitu akaendelea na maelezo yake.
‘Siku ile wakaniwekea madawa kwenye kilevi
nikapitiliza….nlipoamuka nilijikuta nipo chooni…hawana adabu hawa watu,
walinificha chooni…..’akasema.
‘Nilijuta sana, na nilipoongea na Tajiri siku nyingine,
akanijia juu kwa ukali, siunajua tabia yake…..ni mkali sana kwa wafanyakazi
wake….japokuwa kwako wewe alikuwa akinywea….ole wake angelikuwepo hai, nina
uhakika pesa ingemtoka…safari hii nilijipanga vyema…’akasema.
‘Basi siku ile nikaenda kwa docta…..’mama mdogo akawa
anaelezea huku akikumbuka jinsi ilivyokuwa siku hiyo alipokwenda kwa docta.
********
‘Una shida gani mama yangu,…maana huku ni nyumbani sio
hospitalini?’ akauliza docta.
‘Shida yangu ni ndogo tu, ukikubali kushirikiana name, la
sivyo,…shida hiyo inaweza kuwa kubwa , na huenda ikakuharibia kazi yako, na
hata kukupeleka jela…’akasema mama mdogo.
Docta akakumbuka ile simu aliyopokea, japokuwa haikuwa na
sauti ya kueleweka vyema, lakini ilikuwa ni
sauti ya mwanamke. Akahisi huenda
ni huyu mwanamama, na alipomchunguza vyema akakumbuka kuwa aliwahi kuonana naye
kabla;
‘Mama ninahitajika kujiandaa, niwahi kazini,…sema
kilichokuleta, …’akasema docta.
‘Hiyo kazi yako inaweza ikapotea kama usiponisikiliza mimi,
hili nililokuja nalo ni jambo muhimu kuliko hta hiyo kazi yako, ndio maana
nikawahi asubuhi na mapema kabla hujatoka…’akasema mama mdogo.
‘Jambo gani, elezea ili nielewe tusipotezeane muda..’akasema
docta huku akishikilia taulo yake aliyokuwa kaifunga kiunoni, ilionekana ndogo
kwa muda mfupi.
‘Ni hivi, mimi nina mzigo wako,…na nikisema mzigo,
usijifanye hufahamu….na nilivyoupata hilo halikuhusu, ninachotaka ni kupata
nusu ya hizo pesa, tunagawana,….la sivyo, mimi huo mzigo naupeleka
polisi..’akasema.
‘Mzigo gani huo…..mimi sina mzigo wowote uliopotea,….kwahiyo
fanya upendavyo, na naomba utoke hapa kwangu haraka…’akasema docta.
‘Kwani mzigo wako,…wa kanda za video, uliokuwa ukiutafuta,
niliuchukua mimi, na …thamani yake ni milioni ishirini na tano…kama unauhitaji,
sawa, nipe zangu kumi, basi nitakureejshea kama huuhitaji basi, ngoja
nikawakabidhi polisi….’akasema na kuinuka kuondoka.
‘Subiri….’akasema docta.
‘Unafahamu ni nini kilichopo humo ndani?’ akauliza docta.
‘Hiyo haiinuhusu, nifahamu nisifahamu, cha muhimu kwangu ni
pesa,…’akasema mama mdogo.
‘Wewe mwanamke unoata…Mimi nitazipata wapi pesa nyingi kama
hizo….hebu jaribu kufikiria mwenyewe, hata kama nina hospitali, lakini pesa
unazodai ni nyingi sana….’akasema docta.
‘Unajua wapi kwa kuzipata, kwa kukusaidia ni kuwa mimi nipo
tayari kwenda huko ulipotarajia kuzipata, na lazimz zitapatikana, ….’akasema
mama mdogo.
‘Wapi huko unapohisi zitapatikana?’ akauliza docta.
‘Wewe usinifanye mimi mtoto mdogo, usifikirie kuwa nimekuja
hapa kwa kubahatisha, ninajua kila kitu, ninajua jisni gani mlivyokuwa mkifanya
na akina Tajiri, na huyo Malaya wake…sasa kabla hawajakuwahi, maana ninajua
wapo mbioni kuja kwako, tuwawahi mapema,…kesho kukicha tunaingia basi hadi
Arusha, mzee yule ana pesa za kumwanga…’akasema na docta akajikuta akishikwa na
butwaa.
‘Wewe umajuaje yote hayo, kwanza wewe ni nani….?’ Akauliza
‘Tatizo lenu nyie, mnajifanya wasomi,…lakini sisi tusioenda
shule tuna akili zaidi yenu tatizo ni kuwa hatukubahatika kupata hizo nafasi,
kama tungelibahatika, tungelikuwa zaidi yenu…..sasa sikiliza, tusipoteze muda,
tafuta upenyo tuondoke…..’akasema.
‘Mama hilo halitawezekana…nikuambia ukweli, hapo nje kuna
maaskari, jana walifika hapa kwangu wakachunguza, na kupekea kila mahali ,
walikuwa wakitafuta vtu kama hivyo…lakini walikuta hakuan kitu, kwani mimi
nilishaharibu kila kitu, …’akasema docta.
‘Afadhali nimeuwahi huo mzigo, maana ungelikuwepo na wenyewe
ungeliuharibu, tukakosa pesa, au huo mzigo ulikuwa umeuweka pembeni kwa ajili
ya kupata hizo pesa?’ akauliza mama mdogo.
‘Nakuhakikishia kuwa kama ungelikuwepo ungelikuwa ni wa
kwanza kuharibiwa, …hilo sasa hivi ni kaa la moto, ..ni bomu, wala mimi
siuhitaji tena huo mzigo, kama wewe unajiamini, endelea kukaa huo mzigo, na endelea kuwa na
mawazo hayo yaliyopitwa na wakati,…, lakini mimi simo kabisa, nimeshatubu, na
nahisi nipo mweupe, nasubiri kwenda mbinguni….ila kilichokuwa kikinisumbua ni
huo mzigo maana, haujaharibiwa, na ni vyema, ukafika kwa mlengwa kwanza….naomba
tafadhali uharibu au vinginevyo ufikishe kwa mwenyewe anayestahili kuwa nao, na
nina uhakika akiuona atauharibu mwenyewe,….’akasema docta.
‘Sawa hakuna shinda, najua polisi wanauhitaji sana huu
mzigo,….na wao wataamua kuuharibu au la, ngoja niwapelekee..’akasema huyo mama.
‘Kwanini uwapelekee polisi,…ili kuondoa utata, na watu
kuletewa matatizo, mimi naona ni vyema ukaharibiwa kabisa,….maana kuwepo kwake,
hakutakusaidia wewe, ila utakuwezesha wewe kuonekana kuwa ualikuwa unahusika,
na matokeo yake ni wewe kwenda jela, kwani ni vielelezo vinavyohitajika na
polisi….mimi nimeshawaambia kuwa sina kitu chochote, na wamehakikisha,
….’akasema docta.
‘Sawa, kama wamehakikisha basi ngoja niwapelekee….na wao
watajua unamuhusu nani, na nani kautengeneza na kwa ajili gani,….natumai wao
watanishukuru sana…’akasema huku akiondoka.
‘Wewe mama hebu tulia kidogo, …tafadhali nakuomba kitu
kimoja,…mimi sina pesa unazozihitajia, na sitaweza kwenda kwa huyo unayehisi
kuwa anaweza kuzitoa hizo pesa, mimi
nakushari ni bora tukauharibu, au vinginevyo, naomba umpelekee Maua,….’aliposema
Maua akanyamaza kwa muda kama aliyekumbuka jambo, halafu akasema;
‘Nakuomba tafadhali usiupeleke polisi..Tajiri mwenyewe,
aliniagiza kuwa niuharibu…lakini sikuweza kupata nafasi ya kufanya
hivyo…’akasema Docta
‘Tajiri eeh, unaona kumbe mambo yapo wazi,….sasa kwanini
Tajiri alikuambia uuharibu?’ akauliza na Docta akawa akawa anamwangali yule
mama kwa macho yaliyojaa wasiwasi kwani kumbukumbu za mazungumzo yake na
Tajiri, yalikuwa yakimjia kichwani, na kuwa kama ndoto iliyopita, …kwani kumbe
yalikuwa ni maongezi yake ya mwisho na mtu waliyeshibana sana….
*********
‘Tajiri, habari za siku nyingi, vipi maendeleo ya huko, …?’
akauliza kwenye simu, huku akiwa kaweka kumputa yake mbele, alijua kuwa kuna
kazi anatakiwa kuifanya na huyo bosi wake kwenye kazi hizo za kudurufu kanda za
video.
‘Sikiliza docta , hali iliyopo sasa hivi ni mbaya sana,
polisi wamecharuka, na hawakamatiki kwa chochote kile, hawataki pesa…., hapa
ninapoongea Malikia yupo jela…sasa sikiliza, kuna jambo kubwa nimeligundua, na
najua wewe una nakala za zile video zetu….’akasema.
‘Nakala kama ipi, au ya tukio la wapi?’ Docta akauliza
akifungua nakala za video zilizopita.
‘Lile tukio la kafara, lililofanyiaka Dar, …..najua bado una
nakala yake,….ninachotaka ni kuwa, utengeneza nakala nyingine tofauti na ile ya
mwanzo, nah ii ya sasa hivi, hakikisa mimi unaniondoa kabisa, …wabakie wahusika
wengine, …sawa, na ukishamaliza, ifute kabisa hiyo kazi kwenye komputa yako,….’akasema
na kutulia, halafu akaongezea kusema;
‘Kutokana na hali ilivyo, futa kazi nyingine zote zinazotoakana na mambo
yetu,…..,kwani unaweza ukaingiliwa na polisi wakati wowote…ukawa hatiani’akaambiwa.
‘Kuna nini kimetokea,….?’ Akauliza docta akiwa na wasiwasi
‘Polisi wameshagundua mengi, na ninachoogopa ni kuwa malikia
anaweza kufanya lolote, hata kama akiwa jela, nataka akitoka, akukute huna
ushahidi wowote, kwani alivyo anaweza akatugeuka,…kama anaona akifanya hivyo
yeye ataokoka…natuma unanielewa?’ akauliza.
‘Ni kweli yule mama haaminiki, …nitafanya hivyo bosi, lakini
…..’akataka kusema kitu.
‘Najua unataka kusema nini.…hilo nitafanyia kazi, najua hiyo
kazi ulihitaji milioni tano, au sio…ni pesa nyingi sana, lakini kwetu sisi ni
pesa kidogo, kwani hiyo kazi tukimpelekea mteja…., tungelikusanya zaidi ya
shilingi milioni ishirni na tano…kama angelikuwa mtu tumemkusudia, ….na hayo
yalikuwa mahesabu ya malikia, alipotaka kuzipata hizo pesa kwa mzee…., kwasasa
kazi hiyo haina maana kwetu, kwani ni nani atatupa hizo pesa…siwezi kwenda
kumdai mzee, ….’akasema.
‘Lakini mzee bado yupo, unaweza ukatumia watu ukazipata hizo
pesa, sio kwamba nakushauri ufanye hivyo, hapana,nasema tu, kuwa kama mtu unatamaa ya pesa ungeliweza kuzipata kwa
mzee mwenyewe ….’akasema docta.
‘Ndio mzee bado yupo, lakini ukumbuke mabinti zake
wamesharudi, na wanataka kujishughulisha kwenye miradi ya baba yao,…kwa sasa
hivi wanahitajia malipo yote ysilipwe mpaka wao wakahakiki, japokuwa kisheria
Wakili bado ana haki ya kuidhinisha malipo maana hakuna barua yoyote iliyotumwa
benki kumuondoa yeye…’akasema.
‘Sasa unataka nifanyeje kwenye huo mkanda?’ akauliza.
‘Ukishautengeneza kama nilivyokulekeza , na kuniondoa mimi kabisa,
wakabakia wahusika wengine, hapo mimi sitajulikana kabisa kuwa nilikuwepo,na
hata kama nilikuwepo, lakini sikuhusika
kwenye tendo lenyewe,…atabakia huyo muhusika mwingine, ambaye yupo
tayari kubeba dhamana zote,…kwa huyo binti….’akasema.
‘Mimi nilikuwa nahisi ni kwa ajili ya kupata pesa kwa mzee,
kumbe ni kwa ajili ya huyo binti, …..kwa vipi tena imekuwa hivyo eeh?....Maana
tangu mwanzoni uliniambia kuwa huyo ndiye anayekufaa, au sio , anayekufaa…kuwa
mke wako, kuna nini kimetokea ambacho mimi sikijui?’ akauliza docta.
‘Hayo yaache kama yalivyo, maana ….hapa nilipo natamani
dunia ipasuke nizame ndani yake, lakini yote ni maisha, na ….kwa vile , kuna
huwo uwezekano,. ….naomba ufanye hivyo, kwani tukio zima limeharibu mpangilio
wangu wa kimaisha…yaani hata sijui kama nitaweza kusahau hilo ,….na huenda yote
yametokea kama adhabu kwangu….maana hii njia ya kutafuta utajiri, naona
unanitumbukiza kwenye kina cha moto….najihisi kuwa wakala wa ibilisi…’akasema.
‘Una maana gani kusema hivyo,mbona unaonekana kama vile kuna
jambo kubwa umeligundua, na nakushauri, uwe makini na hayo mawazo, unaweza
ukajikuta ukipatwa na mshituko wa moyo, usiwazie kihivyo, kama limetokea jambo,
tafuta ufumbuzi, na ulitatue, usiliweke kichwani ….kwani kuna nini mzee wa
mapesa, ….?’ Huyo docta akauliza na kabla Tajiri hajajibu, huyo docta akasema;
‘Mimi kwakweli, nilishawaambia kuwa hayo mnayoyafanya ipo
siku mtakuja kujijutia, japokuwa mumeniingiza kinamna, lakini moyo wangu haupo
radhi na haya yote,…..kwanza imeniumiza sana,pale mnapochukua mabinti wa watu
wadogo wasio na hatia kwenye mambo yenu….lakini hamjachelewa, acheni, tubuni,
…na tafuteni njia nyingine ya kuishi…..’akasema docta.
‘Unajua docta unaongea hivyo, kwa kuwa hukuingia ndani
kabisa ya haya mambo,….natamani nifanye hivyo, lakini..oh,…..nimekuwa kama
nimenaswa kwenye ulimbo wa haya yote. Kwa ujumla yote hayo niliyafanya, na moja
ya masharti ya zindiko….tungelifanyeje, ….’akasema Tajirikujitetea.
‘Hapana,hayo ni mambo yakishetani, kwani zindiko ni lazima,
kwani wanaofanikiwa wanafanya hayo, hebu angalia hawo wazungu wanafanya hizo
biashara, ina maana na wao wana mazindiko ya kizungu, hakuna kitu kama hicho,
mimi kama mtu wako wa karibu nakushauri uachane kabisa na mambo hayo….’ Akasema
docta.
‘Nimekuelewa docta…..’akasema Tajiri, lakini kauli yake
ilikuwa ikiashiria unyonge fulani, na dota akaona hapo ndipo sehemu ya kumpa
vipande vyake huyo jamaa , akasema;
‘Angalia kama hilo mnaloliita eti ni zindiko, hilo la Dar, ambalo
unataka tulichakuchue….huyo binti emeniuma sana, kwani hafanani kabisa na
kutendewa hayo mliyoyatenda….sijui kama mtasamehewa kwa hilo,….sio halali
kabisa,……’akasema.
‘Lakini docta,….mimi sikujua wewe ulifika hapo na mzee, na
mliyoyafanya sikuwa nayajua,kama nisingeliuona huo mkanda wa video,nisingelijua
kuwa mlifika na sikuwa ooh, tuyaache hayo maana yananiuma sana, sikujua kuwa
najiumiza mwenyewe…ooh, docta naona hayo tuyaache….’akasema Tajiri.
‘Sawa tutayaacha ila nataak nikuweke sawa, maana sikuwa
nimepata muda wa kukuelezea vyema ilivyokuwa siku hiyo, huenda ukaniona na mimi
nilikuwa mmoja wa hayo mambo yenu, …’akasema docta.
‘Kwahiyo unataka kusemaje…?’ akauliza Tajiri.
‘Kama nilivyokuwa nimekuambia…japokuwa sikuwa
nimekufafanulia vyema …ni kuwa, hayo maelekezo niliyapata kutoka kwa Malikia,
na kama sikosei lengo na nia yake,ilikuwa kukuzuia wewe usije ukawa na uhusiano
wa karibu na huyo binti, kwani kama sikosei, alishaambiwa na watu wake,kuwa
wewe upo mbioni kumfanya huyo binti kuwa mchumba wako….’akasema docta.
‘Docta acha hayo maelezo yako….sipendi kuyasikia….kwasababu
mwanzoni sikuwa naelewa hivyo…’akasema Tajiri.
‘Ndio hivyo Tajiri, mimi nataka kukufafanulia tu…kuwa watu
wake ndio huenda waliokuwekea kilevi,ili uzidiwe na ushindwe kufanya lolote kwa
huyo binti…ingawaje wewe ulisema unahisi Malikia kuna mchezo kakufanyia ili
usiwe na nguvu, ukikutana na watu asiowataka….lakini siku ile ilikuwa ni lazima
zindiko lifanyike au sio, na watu waliokubalika kwenye hilo mnaloliita zindiko wewe
na mzee…..bila nyie nguvu ya huo ushirikina wenu usingelifanya kazi au sio?’akasema
docta.
‘Oh,.. unajua docta sasa naanza kuelewa….huyu
mwanamke,…ndiye kaniingiza kwenye haya yote, bila yeye sizani kama ningeliinga
kwenye dhambi hii kubwa….sasa nitahakikisha ama zake ama zangu…’akasema Tajiri
kwa hasira.
‘Hilo wewe na malikia nii sawa na pwagu na pwaguzi, ….ila
ninalotaka kuliweka sawa na hiloo tukio la siku ile, ili uelewe kuwa mimi
sikupendelea hayo, kwani aliponielezea Malikia kuwa Wewe na mzee, ndio pekee
mliostahili kulifanikisha hilo na wewe hutaweza kufanya lolote, akanishauri
nimchukue mzee…’akasema.
‘Lakini mzee alishaniachia kila kitu…’akasema Tajiri na
kukatiza maelezo yake.
‘Ndio kwa maelezo ya malikia kutoka kwa shangazi yako,
aliambiwa …unakumbuka shangazi yako, yaani mke wa mzee, ndiye anayejua zaidi
mambo hayo kwa vile yeye ndiye aliyemuingiza mumewe kwenye shughuli
hizo..’akasema docta.
‘Hayo nayafahamu sana…’akasema Tajiri.
‘Sasa malikia aliongea an huyu mama, ndio huyo mama
akamuelekeza njia mbadala kuwa wanaoweza kufanikisha hilo ni wewe na mzee, hilo
halifutiki mpaka mkutane tena na huyo mtaalamu ambaye kwa sasa hajulikani
alipo,..sawa si sawa?’ akauliza docta.
‘Hilo ni sawa….’akasema Tajiri.
‘Na ukumbuke siku ile, nilikuwa na mzee huku Dar, kwasababu
alitaka nimfanyie upasuaji kwa ajili ya kumrejeshea hali yake ya kumuwezesha
mbegu kubebesha mimba tena…’akasema docta.
‘Oh,….mbona hukuniambia hilo docta…oh, sasa kumbe mambo
yatajiweka sawa,…Kwahiyo ina maana kumbe uliwahi kumrejesha mzee uzazi wake…mambo sasa yamejiweka sawa…’akasema
Tjiri akionyesha hali ya furaha.
‘Unakumbuka wazo la kumfanyia huyo mzee huo upasuaji ,
lilitoka kwa mkewe, kuwa ili mumewe asije akawa na watoto wan je, basi afanyiwe
huo upasuaji, lakini ionekanae kuwa ni kwa ajili ya fya yake, na hata mwenyewe,
…mzee asijuie hilo, ….na kweli mzee alijua kuwa anafanyiwa huoo upasuaji kwa
ajili ya afya yake,….’akasema docta.
‘Kwahiyo na wewe kumbe umehusika..huwezi kukwepa hilo?’
akasema Tajiri.
‘Oh, siwezi kuhusika…kwa kipindi kile niliona ni jambo la
busara, kama kila kipindi huyo mzee alitakiwa kutafutiwa mwadada…kwa ajili ya
hilo zindiko, huoni uwezekano wa kuwa na watoto wan je ungelikuwa mkubwa…..?’
akawa kama anauliza.
‘Ok, sasa niambie ina maana ulimrejesha mzee, kwenye hali
yake,na ikafanikiwa?’ akauliza Tajiri.
‘Kwanini isifanikiwe, ni upasuaji mdogo tu….,na siku ile nilipopata
simu ya malikia kuwa wewe hutaweza kufanya lolote siku hiyo, na hilo zindiko ni muhimu kwenu, nikaona
mzee,akapate mazoezi… na malikia kwa vile alikuwa akijua nipo na mzee huku, na
japokuwa hakujua kuwa mzee yupo huku kwa upasuaji huo…yeye akanisahuri nimshinikize
mzee mpaka akubaliane na hilo tendo….’akasema docta.
‘Lakini mbona….hizo dawa za malikia,…..hazikufanya kazi….kama
ilivyokuwa siku nyingine,maana nilipoamuka, sikuwa na hali kama ile
iliyonifanya ninywe pombe …..kwa hasira,niliposhindwa kufanya kile nilichokuwa
nimekitamani kukifanya siku nyingi….nilikimbilia kulewa na nilipoamuka..oh,
sitaki hata kukumbuka…?’ Akasema Tajiri na kutulia kimiya.
‘Hayo mimi sijui,….kama nisingeliuona huo mkanda,
nisingelijau kilichotokea baadaye,….maana mimi niliondoka na mzee…hata hivyoo
kuhusu hizo dawa kama unahisi alikuwekea malikia ungelimuuliza yeye….huenda
nguvu za dawa yake aliyokuwekea ilikuwa imeisha muda wake, ndio maana
alinisisitizia nihakikishe wewe huamuki hadi asubuhi….’akasema docta.
‘Ulitakiwa ufanyeje….?’ Akauliza Tajiri kwa hasira, na kabla
docta hajajibu akaendelea kuuliza
‘Kwanini sasa hukufanya hivyo…kwani ingelisaidia
mengi….aheri ungelifanay hivyo, kwanini hukufanya hivyo?’ akawa aanuliza Tajiri
kuonyesha kusikitika.
‘Sikuwa na muda huo, mzee, alikuwa katahayari baada ya hilo
tukio, akaniomba turejee kwake,ilionyesha kukerwa sana na tukio hilo kwani
aliniambai kuwa yeye alishajitoa kwenye mambo hayo, ila alifanya ….oh, eti kwa
vile nilimshauri mimi, hakujua kuwa mimi nilimshauri hivyoo kutokana na Malikia….na
kesho yake tukarudi Arusha haraka, kwahiyo wengi hawakujua kuwa mzee, alikuwepo
hapo, kama isingelikuwa huo mkanda wa video kuonyesha hilo tukio…..’akasema.
‘Docta, sasa hapo mpango wangu utafanyika vyema, …..fanya
kama nilivyokuambia,….vinginevyo nahitajika kufanya jambo ambalo huenda
sitaliweza…’akasema Tajiri.
‘Kwanini sasa unakata kufanya hivyo, una wasiwasi kuwa huyo
binti atakushitaki kwakutumia huo ushahidi?’ akauliza docta.
‘Hapana,….kuna mengine zaidi ya hayo….naombe usiyachimbue
zaidi…kwani vinginevyo natakiwa niende hapo alipozaliwa huyo binti, yakaanyike
mambo ya kutakasa, huko nikakutane na watu wa msituni, watanisaidia….nani
atajipeka kwenye mdomo wa simba…..oh, tuyaache kama yalivyo.’akasemaTajiri
‘Kwanini sasa yafanyike hayo yote, ….kwani siku zote
mnafanya hivyo, kwanini hilo tukio liwe tofauti, na ama kwa mzee wako
yaliyotokea sio kwa nia mbaya,ilikuwa ni kwaajili yakufanikisha hilo mnaloliita
zindiko….na najua baadaya hapo,hakupendelea tena….’akasema docta
‘Ungelijua yaliyotokea huku…, usingelisema hivyo…nilikuwa
karibu nikosane na mzee…lakini kumbe ni
kwa maslahi yangu, sikujua kabisa…..kuwa hali hiyo itakuja kunisaidia
baadaye….oh, we acha tu…na hapa tumeshachelewa, ….nilitakiwa kwenda hukoo
kijijini niende kwenye hilo posi alipozaliwa huyo binti, vinginevyo…mabalaa
yatatokea, ikiwemo vifo….’akasema Tajiri.
‘Oh, achana na imani hizo….wewe sasa angalia muelekeo
mwingine,…hata hivyo nikuulize, kuna nini kinaendela kati yako na mzee, ina
maana mnamgombea huyo kimwana au sio?’ akasema docta kwa mzaha na kucheka.
‘We acha tu, ….sitaki hata kukumbuka…natamani,dunia ipasuke
nizame….. lakini nahisi yote yalitokea ili iwe heri kwangu, kati yangu na mzee
na….fanya hivyo, hakikisha unaondoa kila kitu kuhusu mimi, na mimi huku nitajua
la kufanya,….sipendi kabisa nionekane nilikuwepo kwenye hilo tukio, ….na huo
utakuwa msimamo wangu hadi kifo, ….vyovyote iwavyo, nataka iwe hivyo… ni heri
isijulikane hivyo, ….na safari ya kwenda huko msituni, ….sijui kama itawezekana
kwa sasa….lakini ni muhimu..’ Akasema.
‘Sawa bosi….hiyo safari yako ya msituni, naona unaisema
sana, kuna zindiko jingine tena au kuna nini zaidi….sawa naona hilo hutaki
kuniambia, ila nakuuliza kuhusu hii kazi yako ,nikashamaliza nifanye nini? ’akauliza
docta.
‘Hiyo nakala utampa Maua….pale nitakapokuarifu ufanye hivyo,
au kama kutakuja kutokea lolote maana haya mambo sasa yananitisha, nakuomba
umpe hiyo kazi Maua, ili ajikoshe moyo wake, huo utamsaidia kama ushahidi
wake….sina zaidi, tutaongea ukikamlisha hiyo kazi…’akasema na kukata simu.
Docta alitafuta hiyo kazi kwenye komputa yake, na
kuitengeneza kwanza kama ilivyokuwa, na kutoa nakala moja,….
‘Hii nakala nitaiweka kama akiba…huenda milioni ishirini na
tano nikazihitaji….’akasema na kuiweka ile nakala kwenye sehemu yake maalumu,
halafu akaanza kuitengeneza hiyo kazi kama alivyotaka Tajiri, na alipokuwa
karibu kuimalizia hiyo kazi, komputa yake ghafla ikasimama,…na akahindwa
kuimalizia hiyo kazi kwa kuiweka kwenye CD’s.
‘Oh, mbona ilikuwa karibu nimalize….’akasema na mara simu
yake ikaita kuwa anahitajika kazini kwake;
‘Hii kazi nitakuja kuifanya baadaye….’ Akasema na
haikuwezekana kuifanya hiyo kazi tena, kwani kesho yake alisikia kuwa Tajiri
keshaiaga dunia.
******
Docta akahisi kuwa
kasikia mlango ukifunguliwa, na akafunga taulo lake vyema kiuoni, na kugeuka
kuangalia mlangoni.
‘Nahisi hawo ni polisi, kama umekuja na huo mzigo, tafuta
sehemu ukaufiche, ….tafadhali, sitaki waje wauone upo hapa kwangu…’akasema na
mama mdogo akageuka kuangalia mlangoni, na mara mlango ukafunguliwa kwa kasi,
akaingoa mtu aliyekuwa kajifunika uso mzima na kubakiza macho, akiwa na bastola
mkononi..
Mama mdogo, akanyosha mikono juu kwa haraka kujisalimisha,a
, huku akitetemeka, na kabla hajasema kitu , yule mtu akaielekeza ile bastola
kwanza kwa mama mdogo, na mama mdogo, akashika kichwa kama analinda kichwa
chake kisipasuliwe na risasi, na alikaa hivyo kwa muda,….., hata pale
aliposikia sauti ya mtu akilia kwa
maumivu, bado aliendelea kukaa
vile vile, akiogopa kuondoa
mikono au kumwangalia huyo mtu ….
Kukawa kimiya, na mama mdogo , akainua kichwa kwa pole pole
akiangalia mlangoni,….hakukuwa na mtu tena,…hakuamini, kuwa amepona, akajikagua..na
alipoona yupo salama, akageuka kumwangalia docta, ….Docta alikuwa kalala kwenye
sakafu huku kashikilia kifuani,…damu zikiwa zinamvuja,…
‘Oh, ….hawa watu hawana maana ina maana wamemuua docta…..ina
maana mamilioni ndio sitayapata tena..hapana mimi sikubali …’akasema
akimwangalia docta aliyekuwa akigugumia kwa maumivu.
`Sasa hili ni balaa….’ Akasema mama mdogo, na kugeuka kutaka
kuondoka, na sauti ya docta akiomba msaada ilisikia, na mwisho akasikia sauti
iliyoashiria kukata -tamaa ikasema;
‘Ta-fadh-li, ha-ri-bu
ka-bi-sa huo mka-nda,..p-le-ase…au
m-pe Ma-ua ooooh’ ilikuwa sauti ya mwisho wa docta, na mara akatulia kimiya….
Mama mdogo ambaye
alikuwa kashikwa na butwaa, akishindwa kuondoka,na hakujua afanye nini kwa
wakati ule,…..alipoona docta katulia kimiya, akamtupia jicho kwa haraka, na
bila kumsogelea, akageuka kuondoka,….
Alitembea hatua
tatu…halafu akili ikawa inamtuma kufanya jambo jingine, na hapo kwa haraka
akaangaza mle ndani kama kuna kitu anachoweza kuondoka nacho,…. lakini kabla
hajalisogelea kabati, ambalo alihisi anaweza kupata kitu, akasikia sauti ya mlango
wa getini ikiashiria kufunguliwa , akajua kuna mtu kaingia…
‘Oh,…mbona sasa huu ni mkosi,…ina maana nitaondoka hapa hata
bila senti…’akasema huku akikimbilia mlangoni, na kweli akasikia mtu akifungua
mlango wa hiyo nyumba, akajificha, hadi huyo mtu alipoingia ndani….alikuwa
mwanadada, akiwa kavalia nguo za
kutokea, na alionekana mrembo, na mmamdogo akahisi huyo atakuwa mfanyakazi wa
hapo,….
Huyo mwanadada alipoingia ndani kwanza kabisa alielekea chumba
chake cha kubadilishia nguo, hakuingia moja kwa moja kusalimia kwa bosi wake,
na hii ilimsaidia mama mdogo, kutoka pale alipojificha bila kuonekana na huyo
mwanadada
Mama mdogo alipoona huyo mwanadada haonekani tena, yupo huko
ndani kwenye chumba ambacho alihisi nisehemu anapobadilishia nguo,yeye kwa haraka akatoka pale alipojificha na
kuelekea nje, hakusubiri, ….akakimbilia kwenye geti la nje, na alipofungua geti
tu, yowe likasikika toka ndani ya hiyo
nyumba, ….yeye hakutaka kugeuka…alichojua yeye ni kuhakikisha anaondoka kabisa
eneo hilo…..
NB: Nimekuwa sipo hewani karibu wiki sasa, sababu ya mambo yaliyojuu ya
uwezo wangu, likiwemo la ukosefu wa mtandao, na umeme…tuwiane radhi maana sikuwa na jinsi nyingine, hizi ni sehemu mbili kwa pamoja, nimefanya hivyo nikichelea kupata tatizo jingine kama hilo….natumai sehemu ijayo huenda ikawa ndio mwisho wa kisa hiki, …..
WAZO LA LEO:
Yaliyopita ni sawa na ndoto,…kunapopambazuka au ukiamuka ndoto hiyo imekwisha.
Hatahivyo matendo yetu yaliyopita yawe ni dira, kama nuru ya jua …. yanayotuonyeshea
muelekeo wa kimaisha, kama matendo hayo yalikuwa ni mabaya, jisahihishe kwa
kutenda mema, na kama yalikuwa ni mema, yawekeze kwenye msimamo wako wa kimaisha.
No comments :
Post a Comment