Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, April 16, 2013

Uchungu wa mwana Aujuaye ni mzazi-83 hitimisho 3



    ‘Mama mdogo kwani ilikuwaje?’ akauliza Maua pale alipomtembelea mama yake mdogo ambaye bado alikuwa kashikiliwa na polisi.

‘Ilikuwaje, …?’ akamwangalia Maua kwa zarau, halafu akageuka kuangalia kule aliposimama askari polisi aliyekuwa kwenye zamu.

‘Hawa watu hawanifahamu vyema, nimewaambia wasipoangalia mimi nitakwenda moja kwa moja kwa bosi wao, ….hawewezi kunishikilia hapa kama muuaji, kama wameshindwa kumkamata huyo muuaji, waseme,…hawajui kazi,….kabisa’akasema kwa sauti ili yule askari amsikie, lakini yule askari hakugeuka kuwaangalia.

‘Sikiliza Maua , nakutuma uende kwa mkuu wa polisi, umwambie ni mimi nimekutuma, yule tunafahamiana sana,….na ole wao, ..hawa wote watapoteza ajira zao..’akaendelea kuongea kwa sauti, na mara akaja mkuu wa hicho kituo.

‘Afadhali umekuja mkuu, natumai wewe sasa tutaelewana, maana hawa askari wako wadogo, hawanifahamu vyema, ….’akasema mama mdogo, huku Maua akiwa anamwangalia mama yake mdogo kama vile mtu anayemuangalia mchekeshaji wa filamu.

Yule mkuu wa hicho kituo akaamrisha Mama mdogo afikishwe kwenye ofisi yake, na hapo mahojiano yakaanza.

‘Unajua hii ni kesi ya mauaji, na tungelifurahia kama tungelipata msaada wenu, ili tumkamate muuaji haraka iwezekanavyo’akasema huyo mkuu.

‘Ina maana bado hamjamkamata huyo muuaji,…kweli nyie mnajua kazi yenu vyema….oh, hawo vijana wako hawajui kazi vyema, …,ingelikuwa ni mimi, sizani kama huyo muuaji angelimaliza siku…usinione hivi, mimi nafahamu kila kazi…’akasema mama mdogo akiwa kashika kiuno.

‘Sawa kabisa, ..hivyo ndivyo nataka, mtu aliyetayari kuisaidia na polisi ili muuaji apatikane, nahisi sasa utaonyesha huo ujasiri wako wa kujua kila kazi, na hapa tunatarajia utatusaidia ili tumpate huyo muuji, na kwa kuanzia tunaomba utuambie ukweli ilivyokuwa, je ni nini kilikupeleka kwa Docta, …?’akaulizwa.

‘Hayo maswali nimeshaulizwa mara nyingi, na sioni kwanini niulizwe tena na tena, kwani hayatasaidia lolote, kwani kwenda kwangu kuonana na docta, ni kawaida, ….yule ni dakitari na mimi ni mgonjwa, kuna ubaya wa mgonjwa kumuona docta, unaona…..kwa vile yeye ni dakitari, na pia nilikuwa nafahamiana naye siku nyingi, …sioni kuwa hilo swali lina umuhimu wowote’akageuka kumwangalia Maua.

‘Katika kumbukumbu za video iliyochukuliwa ilionyesha kuwa ulikuwa na mzigo, uliokuwa kwenye bahasha , ukitaka kumkabidhi, docta, na hapo ndipo akatokea muuaji na kumpiga docta risasi, huoni kuwa huo mzigo, ndio ulikuwa chanzo cha yote hayo?’ akaulizwa.

‘Hilo swali nimeshalijibu,….ule mzigo ulikuwa ni wa docta, hauhusiani kabisa na hayo mauaji, nina uhakika, na hilo,….na hata hivyo, huyo docta mwenyewe alisema nimkabidhi Maua,…’akatulia na kumuangalia Maua, na Maua akashituka kusikia hivyo.

‘Mzigo gani huo mama?’ akauliza Maua kwa wasiwasi.

‘Haya hayakuhusu…tulia nimalizane na hawa watu…’akasema mama mdogo huku akimwangalia yule askari

‘Ni mzigo gani huo, mbona hujamkabidhi Maua mzigo wake?’ akaulizwa yule askari polisi

‘Nitamkabidhije, wakati nyie mumeshanikamata…nitamkabidhi mkiniachia, haina shida,…’akasema na mara simu ya yule askari ikaita, na haraka akaipokea na kusikiliza kwa muda mrefu bila kusema neno, na baadaye akasema;

‘Kwahiyo mumemkamata?’ akauliza, na kusikiliza tena kwa muda, halafu akasema,;

‘Sawa mfikisheni hospitali lakini kwa ulinzi mkali, na hiyo miili ipo katika hali gani?’ akauliza na kuskiliza tena kwa makini, halafu akageuka kumwangalia mama mdogo wa Maua, huku anasikiliza hiyo simu, na baadaye akamaliza kuongea na simu, akasema;

‘Hatimaye muuaji keshakamatwa,..na wakati anafuatiliwa kulitokea majibishano ya risasi, na kujeruhiwa, ila hali yake inaendelea vyema , na tunashukuru kuwa keshakubali kuisadia polisi….’akasema mkuu huyo.

‘Kwahiyo tunaweza kuondoka..?’ akauliza mama mdogo huku akiinuka kuondoka.

‘Binti yako anaweza kuondoka, ….ila wewe bado tuna maswali hujatupatia majibu yake, na usipoyajibu kama vyema kama inavyotakiwa , unaweza ukahusishwa na hilo kundi,…..japokuwa wahusika wakuu wote wameshakmatwa, lakini inasemakana lilikuwa kundi kubwa,….likiwa na watu wengi, na huenda wewe ulikuwa mmojawapo’akasema huyo askari.

‘Wahusika wakubwa kama akina nani…..mbona siwaelewi?’ akauliza mama mdogo.

‘Utawafahamu pindi utakapoziona hizo maiti mbili..’akasema huyo askari.

‘Maiti mbili,..hapana sitaki kuona tena maiti…..mbona mnanitia mkosi, huyo docta kauliwa mbele yangu, nimeogopa na kuogopa,…sasa tena mnataka kunionyesha maiti nyingine, hapana mimi sitaki kabisa….’akasema.

‘Ni lazima ukaione hii miili, kwa ajili ya uchunguzi wetu, na nakuhakikishia usiposema ukweli, sasa hivi utawekwa ndani, ..utapelekewa segerea…ukiwa miongoni mwa hilo kundi, na huenda ukabeba dhambi zote za hilo kundi..’akasema huyo mkuu, na kumfanya mama mdogo, kumwangalia kwa woga.

‘Mnipeleke Segerea kwa kosa gani, na siwezi kwenda huko kuchungulia maiti..mbona mnanitaka niwe naota usiku,…..’akalalamika, lakini polisi kwa sababu zao walizozijua wao wakamchukua hadi hapo zilipohifadhiwa hizo maiti.

Mama mdogo alipofikisha hapo, akaulizwa;

‘Je unawafahamu hawa maiti?’ akaulizwa

‘Siwafahamu kabisa…, na wala sijawahi kukutana nao…..oh, ,,,,’akageuka pembeni , hakutaka kuwaangalia tena wale maiti, na akaulizwa hilo swali mara tatu,

‘Kwanini mnaniuliza swali hilo mara kwa mara ina maana hamniamini , kama hamniamini iulizeni hiyo maiti, itawaambia ukweli…’akasema huku akiangalia kwa jicho ka kujiiba, akionyesha wasiwasi mwingi.

‘Sawa, sisi tumekuleta hapa makusudi, ili kupima ukweli wako, na kwa kauli yako inatufanya tukushikile hadi hapo uchunguzi utakapokamlika…..’akaambiwa.

‘Kwanini mnishikilie, kwani mimi ndiye niliyewaua, wameuwawa kwa ujinga wao wenyewe, …..’akatulia.

‘Umejuaje kuwa wameuwawa kwa ujinga wao wenyewe?’ akaulizwa.

‘Hawa waatu wanaonekana ni majambazi,…’akasema na baadaye akaja askari mmoja, na kuongea na yule mkuu wa kituo, na walipomaliza kuongea akasema;

‘Nashukuru mwenzetu wa huko Arusha ambaye anaishughulikia hii kesi amaeshawasili, ….

                                                ****

‘Hawa watu tumekuwa tukiwatafuta kwa muda, na tulijua lazima watakuwa na mtandao mpana, na jinsi ilivyo, na ushahidi uliopatikana inaonyesha lengo lao ilikuwa kuchukua hizo pesa za mzee, na kusafiri nchi za jirani, lakini hawakuelewana…wameshachukua pesa nyingi kwa matajiri mbalimbli, ilionekana kuwa ilikuwa sehemu yao ya mwisho ya kukusanya pesa kwa kutumia vitisho vyao vya aknda za video walizozitengeneza…..’akasema askari mpelelezi toka Arusha.

‘Huyu jamaa ambaye alimuua Docta, baada ya kukubali kusema ukweli, alituelezea kuwa yeye alipewa pesa na wakili, akamuue Docta, na baadaye akirudi atamaliziwa pesa yake, lakini alipokaribia eneo hilo, akasikia milio ya risasi, na kwa uwoga, akataka kukimbia.

‘Lakini kwa vile alishamtoroka mtu wetu ambaye alikuwa akimfuailia kwa nyuma, akaona akirudi nyuma ni lazima atakutana na huyo mtu, akaona ni vyema kwanza atafute sehemu nzuri ya kujificha na sehemu aliyoiona ni hapo hapo kwenye hilo jengo, kwahiyo akaingia humo ndani…

‘Baadaye alipoona kupo kimiya akaamua kuwafuatilia watu wake,a mbao walikuwa wamejificha chini ya hilo jengo. Jengo hilo lilikuwa bado jipiya , na lilikuwa na vyumba vya chini kwa chini, na hapo ndipo palikuwa na makao ya hawa watu.

Watu wetu waliokuwa wakifuatilia wakafika kwenye eneo hilo, hawakuwa na uhakika kuwa kuna watu wanaishi humo ndani, na kumbe na wao walisikia huo mlio wa risasi, kwahiyo wakaamua kuingia …

Wakati wanaingia , mmoja wa watu wetu akamuona huyo muuaji wa docta, akitembea kuelekea vyumba vya chini kwa kupitia kwenye ngazi, wakamfuatilia, hadi alipofika kwenye hivyo vyumba walipojificha hawo jamaa, akagonga…

Mlango haukufungulia, na yule jamaa akafungua mlango, na watu wetu wakasubiri kwa nje, ..baadaye huyo jamaa akatoka akionekana kuwa na wasiwasi, huku akiwa na begi mkononi, na hapo wakamuwahi, na hakukubali kwani alikuwa na silaha mkononi, akaanza kujibishana na watu wetu, na watu wetu wakamjeruhi…

Watu wetu waliungia mle na kukuta hizo maiti mbili, ambazo baada  ya uchunguzi iligudulikana kuwa waliuwana wenyewe, …na hata tulipomhoji huyo muuaji wa docta, alikiri kuwafahamu hawo watu kuwa walikuwa ni mabosi wake na ndio waliomtuma kumuua docta.

‘Ndani ya lile bgi kuna ushahidi mwingi tu, zikiwemo kanda za video, ambazo zinaonyesha jinsi gani walivyokuwa wakifanya kazi zao, kuchukua mapicha mabaya na kuwatishia watu, kuwa wasipowalipa pesa watazionyesha hizo picha hadharani, na hata huyo muuaji wa docta, alikiri kuwa yeye ndiye waliyekuwa wakimtumia kupelekea hizo kanda kwa watu mbali mbali waliokuwa wamewakusudia..

‘Kwa hapa Dar, hawakuwa na watu maalumu kwa kazi zao hizo,…kuachilia docta, ambaye tulikuja kugundua kuwa yeye, alishirikishwa katika utaalamu wa kuzitengeza hizo kanda za video kwa vile wanavyotaka wao hawo watu. Ukiangalia vyema, watu waliokuja kushirikiana nao, ni kwa kuingizwa bila kujua ni nini kinachoendelea kwenye kundi hilo kwahiyo hakuna anayefahamu zaidi.

‘Kwahiyo hizi maiti mbili ni za viongozi wa kundi, ….’akahitimisha ripoti ya huyo mpelelezi kutoka Arusha

‘Ambao ni Wakili , na huyo mwanadada anayejulikana kama Malikia wa Mererani…

                                              ********

‘Mama mdogo ameshikiliwa na polisi, na tunatarajia kuwa ataachiwa na aliniambia kuwa ana mzigo wangu aliopewa na docta, ….nahisi huo ndio utakuwa na siri iliyojificha ya huu uja uzito wangu….’akasema Maua akiongea na mama yake kwenye simu.

‘Mwanangu , wewe kubali kuwa huyo mtoto ni wako, na baba yake hayupo, ili kuepusha shari, mimi ninaweza kumchukua huyo mjukuu wangu pindi ukijifungua, nitamlea kama nilivyokulea wewe…’akasema mama mtu.

‘Mama usiwe na wasiwasi na mimi, ninajua nini ninachokitafuta, najua sitashindwa kumlea huyu mtoto nikijifungua, lakini kwanini tuwe kimia na watu kama hawa, maana wamenitendea mimi leo, kesho watamtendea mtu mwingine, ….hiyo sio haki..’akasema Maua.

‘Ukitafuta haki mwanangu utaumia, haki ni ngumu kuipata kwa watu wenye pesa, ….wao wanajua kila mbinu, haki utaipata kwa mungu peke yake, wewe muachie mungu, atakusaidia, angalia maisha yangu niliyopitia, kama ningeitafuta hiyo haki ningelikuwa wapi sasa hivi, yote nilimuachia mungu, ndio maana unaniona badoo nipo hivi….’akasema mama yake.

‘Mama nikuulize kwani huyo mke wa mzee aliondoka vipi hapo nyumbani kwake, kwasababu tulipoondoka pale alisema kuwa kesharudiana na mume wake, ilikuwaje tena?’ akauliza.

‘Mwanangu ndio maana nakuomba uachane na hiyo familia, kwani kilichotokea pale ni mungu kumdhihirisha mnafiki mbele za watu, kuwa jinsi mtu anavyoonekana sivyo alivyo kwenye nafasi yake…’akasema mama Maua.

‘Watoto wale baada ya kumuamini mama yao, wakawa wanaondoka kwenye shughuli zao, kwasabbu ilibidi wachukua majukumu ya mzee, ya kuendesha miradi yao, kwahiyo muda mwingi walikuwa maofisini, …’akaendelea kuhadithia mama mtu….

                             ****

Mke wa mzee aliinama huku akiwaza, alijiona kama mfungwa, kwa jinsi alivyokuwa akimuhudumia mumewe, mwanzoni libidi ajitume, ili kuwaonyesha watoto wake kuwa anamjali mume wake, akawa anamhudumia vyema, …

‘Hii kazi itanishinda siwezi kuwa yaya wa kumhudumia huyu mzee….’akawa analalamika kimo moyo.

‘Mama unaonaje tukimtafuta yaya, au nesi ambaye tutamlipa awe anamhudumia mzee?’ wakamuuliza wale mabinti.

‘Yaya au nesi wa nini, mimi nitakuwa nafanya nini, ..nahitajia kumhudmia mume wangu, huu ndio wakati wangu wa kumuonyesha kuwa mimi sipo mbaya kwake..’akasema kinafiki.

‘Haya mama, tunashukuru kusikia hivyo, na natumai hata baba akipona, atakupenda sana’wakasema na yeye akacheka  kimoyo momoyo akasema;

‘Haponi huyu,…hii ndio safari yake ya mwisho,…’akaguna na kugeuka kumwangalia yule mzee, ambaye alikuwa kakodoa macho akimwangalia mkewe, chuki ilikuwa waziwazi usoni mwake, na akwa anatoa sauti ile il, akisema kwa shida;

‘Maua…mmmaua’akasema.

‘Maua Maua, nenda kayachume nje kama una uwezo..’akasema kwa hasira na kipindi hicho mabinti walishatoka nje. Akamsogelea mumewe na kwa haraka akachomoa mipira inayomsaidia kupumua, na kwa ila haraka akawa kachomoa na mpira wa kumsaidia kukojoa na mkoja ukawa unatoka kitandani

‘Aaah, unaona balaa tupu, utakaa na mkojo wako mapaka kukauke…’akasema na kutoka nje. Baadaye binti mmoja akaingia na akahisi baba yake akihangaika pale kitandani alipolazwa, akamsogelea, na alishangaa kuona mpira ya kumsaidia kumupumia imetolewa, kwa haraka akamuita docta.

‘Oh,..mbona hizi mipira zimechomolewa, hamuoni kuwa mtamuua baba yenu kabla ya muda wake?’ akauliza docta..

‘Mamama…huyu mama kaenda wapi maana yeye ndiye alibakia na mgonjwa….’akasema huyo binti.

‘Inaonekena kuna mtu kaziondoa hizi mipira za kumsaidia mgonjwa, na hii inaonyesha kuwa huyu aliyefanya hivi kafanya makusudi…mna bahati hali ya mgonjwa ilikuwa sio mbaya, na...baadaye tutaziondoa hizi mipira hazitahitajika tena....’akasema docta akimalizia kazi yake ya kuirejeshea hiyo mipira.

‘Hakuna mtu mwingine aliyebakia na mgonjwa zaidi ya mama…’akasema huyo binti.

‘Naombeni muwe makini, …sipendi kuwagombanisha na mama yenu, lakini kwa hali kama hii, na kama yeye ndiye aliyemtoa huyu mzee hii mipira, hastahili kukaa na mgonjwa, tafuteni mtu mwingine…na kama isngelikuwa ni mama yenu, ningewashauri muwaite polisi wafanye uchunguzi, maana huu sasa ni uuaji...’akasema docta.

‘Sawa Docta, tunashukuru,…kwani haiwezekana ikawa mgonja kajiondoa mwenyewe?’akasema kama anauliza.

'Haiwezekani, hii ni mtu kaiondoa, tena aliiondoa kwa fujo, huoni kamjeruhi na mgonjwa....hapana haiwezekani mgonjwa akaweza kujiondoa mwenyewe hii mipira...'akasema huku akiendelea na kazi yake

Akajaribu kumtafuta mama yake, lakini hakumuona hapo nyumbani, kumbe mama yake alikuwa keshaingia mitaani, na kumuacha mzee peke yake, Yule binti, akaanza kumuhudumia baba yake, na dada yake aliporudi, ikabidi amuelezee tukio lililotokea.

‘Dada hivi mama kaenda wapi?’ akauliza

‘Kaenda wapi, si tulimuacha haka,akisema anamhudumia baba’akasema mwenzake.

‘Hayupo, na inaonekana kaondoka muda mrefu’akasema mwenzake.

‘Oh, jamani mama, kwanini anafanay hivi, sisi tukimshauri tumtafute mtu amasaidie hataki, …na ilihali anajau fika hataweza kumsaidia mgonjwa, mama hawezi kutulia sehemu moja,anajidanganya tu….’akasema huyo binti mwingine.

‘Maua….mm-le-te…Maua…..ooh, aMaua…’Mzee akawa anasema hivyo, na alionekana yupo kwenye hali mbaya sana, na docta akawaomba watoke nje, ili aweze kufanya kazi yake kwa nafasi, na wale mabinti wakatoka nje, na kuanza kuongea mambo yao.

‘Dada mimi naona baba kweli anamuhitaji Maua….’akasema binti mmojawapo mdogo mtu.

‘Hata mimi nilikuwa na wazo hilo, lakini tutampata wapi, na ukumbuke waliondoka hapa kwa kashifa, sizani kuwa watakubali kurudi hapa tena’akasema.

‘Kashfa ni ya yule mama yake mdogo, sisi tumtafute, na tumwambie aje peke yake, huenda kuja kwake kutasaidia mengi’akasema mdogo mtu.

‘Haya mimi nitapitia kule dukani kwa mama yake, huwa nasikia anakuja mara moja moja, na nikimkosa nitaacha ujumbe, …namba zao za simu haziptatikani tena, naona wote waliamua kubadili namba zao za simu’akasema huyo dada mtu.

‘Na lile swala la benki limeishia wapi?’akauliza.

‘Niliwaambia wazizuie akaunti zote za mzee,….wasitoe pesa hadi hapo tutakapoweka mambo vizuri, nashukuru kuwa hakuna pesa iliyotolewa zaidi ya zile za mwanzo,….kwahiyo benki wana taarifa hizo, na wameshawaondoa Tajiri, na wakili kama waidhinishaji, … natumai hilo litakuwa limefanyika,….nitalifuatilia leo kwa wakili wetu…’akasema dada mtu.

‘Kuna nyaraka wanazihitajia , ….nimezitafuta kwenye makabati ya mzee sizioni, nahisi atakuwa aliondoka nazo yule wakili ….au malikia, na sijui waliingia muda gani na kuzichukua, …..’akasema mdogo mtu na mara simu yake ikalia.

‘Oh, inspecta …..’akasema huku akimwangalia dada yake.

‘Ongea naye tu…’akasema dada yake.

‘Halooh, inspketa nipe habari,…’akasema na kutulia kwa muda akimsikiliza Inspekta akiongea,…… na baadaye akaondoa simu sikioni na kumgeukia dada yake, akionyesha tabasamu mdomoni.

‘Nikuambie kitu, japokuwa sivyo tulivyotaka,… lakini imetokea, hivyo, wanasema ukiua kwa upanga na wewe utauwawa kwa upanga, ukitenda ubaya na wewe utalipwa ubaya…’akasema mdogo mtu.

‘Na wewe siku hizi umekuwa mswahili, mtunga mashahiri, au umegauka kuwa bongo fleva…’akasema dada mtu.

‘Wale wahalifu wamekamatwa…..’akasema mdogo mtu huku akikunja uso kuonyesha hasira na watu hawo.

*****

Dada mtu akamwangalia mdogo wake kwa muda akisubiri, amalizie sentensi yake aliyoiongea na baada ya kumuona yupo kimiya akauliza;

‘Wale wahalifu akina nani hao?’ akauliza dada mtu akiwa hana uhakika na hicho anachokiwazia yeye kichwani.

‘Wakili na malikia,…..’akasema mdogo mtu, akikunjua uso kuondoa hasira alizokuwa nazo, na kutabasamu, na dada yake akafungua nyusi za macho kuonyesha mshangao, akatabasamu pia na kusema;.

‘Oh, mungu mkubwa…kwahiyo sasa hawo polisi wahakikishe kuwa hawo wahalifu hawatoroki tena,..’akasema dada mtu.

‘Hawewezi kutoroka tena,…. kwasababu wameshajihukumu wenyewe, ndio maana nikakuambia kuwa kila mtenda mabaya, atalipwa kwa ubaya, na ukiua kwa upanda na wewe utauwawa kwa upanga, na damu ya mtu haipotei bure…..’akasema mdogo mtu.

‘Una maana gani kusema hivyo….?’akauliza dada mtu.

‘Kilichotokea ni kuwa, kumbe walipoondoka hapa walikwenda kujificha Dar, na huko walimwendea docta, yule docta wa mzee. Kumbe yule docta wa mzee alikuwa akijua siri nyingi, na kwa uchunguzi wa polisi, kumbe hata yule docta alikuwa miongoni mwa kundi hilo, …lakini kwa shinikizo’akasema.

‘Unasema kweli..kwa shinikizo kwa vipi?’ akauliza dada mtu kwa mshangao.

‘Ndivyo walivyogundua polisi kutokana na ushahidi wa kanda za video walizozipata kwenye mkoba uliokamatwa ukiwa na hivyo vitu. Kumbe docta, alikuwa na ujuzi mwingine wa mambo ya kutengeneza vido, mitandao na program zake…, ‘

‘Kwahiyo kundi likaamua kumtumia yeye, na kwa vile alikuwa karibu na mzee, walijua kuwa angeliweza kusaidia sana kuwezesha hizo kanda kuchukua kumbukumbu muhimu, ….yeye akawa mtu wa kutengeneza zile kanda za video kwa ajili ya kubalackmail watu, na wanadai kuwa alishinikizwa na malikia kwa mtindo huo huo, wa kufanyiwa `blackmail’  kuwa usipotufanyia kazi zetu na wewe tutatoa siri zako’akasema mdogo mtu.

Mai..mai mai…God’ kwahiyo kumbe na yeye alikuwa ana kashifa zake, …na wao wakazipata, na wakazitumia hizo kashafa kumnasa, na yeye bila kufikiria sana, akawa mtumwa wao….oh, kwanini hakuwaambia polisi, ndio ujinga unaofanywa na hawa watu..’akasema dada mtu.

‘Polisi…kwa muda ule….mmmh, Malikia, alikuwa keshaiweka polisi ya hapa mkononi,  siunamfahamu malikia alivyo, na docta alikuja kugundua kuwa hakuna mtu wa kumwamini hata akishitaki,…’ akasema 
huyo binti.

‘Malikia alikuwa mjanja, kwa mtindo huo huo wa kupandikizia kashifa,aliuetenda kwa watendaji wa kituo cha polisi, na wao wakajikuta wapo kwenye mtandao wake, …siunakumbuak yule mkuu wa kituo, alivyohamishwa, walishagundua kuwa huyo mtu hataweza kufanya kazi yake vyema akiwepo eneo hilo, na ndio maana wakaamua kumuhamisha,..nasikia wametupa huko mikoa ya mbali,…’akasema.

‘Huyu mkuu mpya alipokuja ndio akayafichua yote hayo..na malikia hakuweza kuivana naye, maana yeye ndiye aliyekuwa akiwarubuni hawo wakuu, na kuwanasa kwa urembo wake, na mwisho wa siku wanaingia kwenye mitego yake….’akasema mdogo mtu ambaye kwenye kazi za mzee wao, alikuwa akishiriki kwenye vitengo vya sheria, na masoko.

‘Oh, kwahiyo ina maana wote wamekamatwa, ….na..unasema imekuwaje,…?’ akauliza.

‘Basi polisi walipogundua kuwa wapo Dar , wakatuma kikosi chao kwa kificho, hakuna aliyejua kuwa kikosi kipo huko kikifuatilia kwa  karibu,….kikosi hicho kilikuwa kikimfuatalia kila mtu waliyemshuku, na kweli mtego huo ukazaa matunda…’akasema.

‘Wakanaswa kwenye jengo ambalo walikuwa wamejificha, na wakasubiri wakati muafaka, na kama ilivyotegemewa …..hawa watu wakawa hawaaminiani, kosa walilofanya ni kuwa hawakumfuatilia mtu mmoja aliyekuwa katumwa na kiongozi wao, ….hawakuwa makini naye, kwani huyo mtu alikuwa hafahamiki vyema, …..’akatulia.

‘Mtu huyo akaenda kumuaa docta..na kumbe docta angelikuwa hai mambo mengi ya hilo kundu yangeligundulikana…’akatulia.

‘Oh, kwanini hawakumshuku docta mapema, mimi nilishaingiwa na wasiwasi, naye maana kipindi fulani nilikuwa nikimpigia simu kumuulizia maswala ya mzee,. Majibu yake yalikuwa yakinipa wasiwasi, moyoni mwangu nikaanza kumuhisi vibaya, unakumbuka nilivyokuambia kipindi kile….’akasema dada yake.

‘Ndio hivyo,nakumbuka, lakini kwa kipindi kile nilikuwa siamini kuwa huyo docta anaweza kuwa mbaya kiasi hicho …’akasema mdogo mtu.

‘Kwasababu walijua kuwa yeye anafahamu siri kubwa, walimtuma mtu kwenda  kumuua…na siri aliyokuwa akiijua amekwenda nayo, kwani hawakubahatisha kupata chochote kwake….’akasema.

‘Sasa waligunduaje kuwa huyo docta alikuwa ndani ya kundi?’ akauliza.

‘Kwenye vitu walivyovikuta kwenye begi,….kuna mkoba, ambao kulikuwa na nyaraka za mzee, …nahisi humo kutakuwepo pia na zile nyaraka za benki tunazozitafuta, itabidi tuwaulize polisi, maana zinahitajika sana. Kwenye huo mkoba kulika na kanda za video, ambazo zinaonyesha, mambo mengi, ikiwemo hiyo ya kashafa ya docta…’akasema.

‘Na cha ajabu huyo muuaji akaamua kuisaidia polisi …maana aliona hana cha kupoteza, waliokuwa wakiogopewa hawapo tena…’akasema.

‘Ni kweli, maana inavyoonekana Malikia na Wakili ndio walikuwa viongozi wakubwa, kama walishaingia mikononi mwa polisi , basi nani wakuogopwa tena’akasema dada mtu.

‘Waliingia mikononi mwa polisi wakiwa wafu…’akasema mdogo mtu.

‘Oh, ina maana polisi waliwaua….kwanini wasingeliwakamata wakiwa hai, ili wahukumiwe na kusota jela….au kunyongwa,….ili kila mtu aone kuwa haki imetendeka?’ akuliza dada mtu akikunja uso kwa hasira.

‘Walijiua wenyewe,….waliuana wenyewe, inavyoonekana kwa uchunguzi wa polisi ni kuwa walikuwa hawaaminiani, na katika kunyang’anyana hizo nyaraka, na vitabu vya beni walivyoondokana navyo, wakapigana risasi…kwahiyo muosha kaoshwa’akasema mdogo mtu.

‘Oh, masikini malikia,….na kutamba kote kule, sasa kaishia kaburini…kwa njia ile ile aliyokuwa akiwafanyia wenzake….’akasema dada mtu.

‘Kila mtu ataishia huko…kaburini, au sio…, ila cha kuomba ni kuishia kaburini ukiwa na matendo mema, sio kama walivyoishia wao…..’akasema mdogo mtu

‘Kweli muosha huoshwa..’wakasema na kutulia pale mlango ulipofunguliwa na mama yao aakaingia huku akionyesha uso wa wasiwasi, akawaangalia wale mabinti, kama vile anasubiri kuambiwa jambo, na dada mtu akauliza;.

‘Mama ulikwenda wapi?’.

‘Niliitwa na polisi..kwani kuna nini kimetokea..?’akauliza huku akigeuza uso kuangalia chumba alichokuwa kalala mzee wao.

'Mama kwa usalama wako tunakuomba undoke humu ndani, rudi kijijini ukakae huko huko...hadi hali itakapokuwa shwari, vinginevyo utaishia jela...'akasema dada mtu.

'Huyo mtu alishajifia.....'akasema na akafunga mdomo pale docta alipotoka, na wote wakageuka kumwangalia kusikia atasema nini

NB: Oh, kumbe bado kidogo, …nilitarajia kukimaliza hiki kisa leo, lakini bado kuna maswali meni yanahitajia majibu, tuwe na subira.

WAZO LA LEO: Ukitenda mabaya ujue mwisho wake utalipwa mabaya, usitarajie kuwa utachuma kile usichokifanyia kazi, wengi wanaota ndoto za namna hiyo, na kujiingiza kwenye matendo mabaya, ili kupata utajiri wa haraka. Tukumbuke kuwa mwisho wa ubaya ni ubaya,….ukiua kwa upanga na wewe utakufa kwa upanga.


Ni mimi: emu-three

1 comment :

Yasinta Ngonyani said...

Hakika Mikono yako Mungu alipata muda wa ziada kuiumba..Kazi nzuri sana ndugu yangu..Tupo Pamoja.