‘Kwahiyo kumbe ni kweli kuwa utajiri wa huo mzee
ulifungamana na mambo ya kishirikina, japokuwa yeye hakupendelea hayo mambo?’
akauliza Maua, akiwa leo kavalia kitamaduni zaidi, na docta alitabasamu, huku akimwangalia juu chini.
‘Mimi sina uhakika sana na hilo, japokuwa nilijaribu kufanya
utafiti wangu, lakini siweza kupata ushahidi kamili, ..ni kama bahati nasibu,
maana kuna wengine walifanya hayo mambo na hawakufanikiwa, …na kwa imani hizi
hizo….’akasema Docta.
‘Sawa naombe uendelee na maelezo yako, japokuwa sijaweza
kufahamu ni kwanini unielezee hayo yote wakati mimi nahitaji kutambua jambo
moja tu kutoka kwako, au ni wewe uliyenifanya hivyo, na hapa unajaribu kuvuta
muda….?’ Akauliza Maua akijiangalai tumboni.
‘Je kama ni mimi upo tayari kuishi na mimi,…lakini sio kwa
ndoa, maana mimi nina ndoa yangu tayari?’ akauliza huyo docta.
‘Kama unajua una ndoa yako..kwanini ukafanya yale
yanayokwenda kinyume cha ndoa, maana ulivunja miiko ya ndoa ?’ akauliza Maua.
‘Hayo tuyaache kwanza Maua, turejee kwenye maelezo yangu,
….umeniuliza kwanini nakuhadithia hayo yote, jibu ni kuwa Tajiri alipenda
nikuelezee haya yote, kwa vile yanaweza kukusaidia kama ikibidi ….’akasema.
‘Haya niambie ulimsaidiaje huyo Mzee, na kama ulivyosikia
kwa watu kuwa huenda mke wake ndiye aliyemfanya hivyo kwa kuma madawa ya
kumpumbaza…wengine huita limbwata?’ akauliza Maua.
‘Huenda ni mambo ya kishirikiana, mimi hayo sio fani yangu,
mimi nilijaribu kumsaidia kutokana na fani yangu, kuna rafiki yake mmoja, yeye
alimsaidia kwa njia hizo za kienyeji, na bahati , sasa sina uhakika kwa hayo
aliyofanyiwa huko alipokwenda na huyo rafiki yake, ila mimi nilimsaidia
kitaalamu,..nijuavyo mimi na kweli akaanza kurejea katika hali yake ya kawaida,
Cha ajabu ambacho sijakielewa vyema japokuwa kwa imani za
watu wanasema hivyo…huyu mzee…akatokea kumchukia sana mkewe, ….alimchukia kama
nini sijui, hebu jaribu kuwaza, watu waliokuwa wanapendana kama pete na kidole,
na ghafla watu hawo wachukiane kama paka na chui…watu wakawa wanasema zile ni dawa
za mkewe zimeisha nguvu, …’akatulia kidogo na kucheka.
‘Yaani walisema mkewe alimwekea dawa za kumfanya awe hivyo,
awe hajitambui na anachofikiria ni kukaa nyumbani na kufuata yale anayotaka
mkewe tu, ..na kumbe hizo dawa zina masharti yake, na ukiyavunja, zinakurejea
na kuwa kinyume chake,…huyo mwanadada akavunja masharti, na hizo dawa
zikabadili muelekeo,…badala ya upendo ukawa ni chuki….wanadai kuwa ile dawa
aliyowekewa iliisha nguvu na ikiiisha nguvu ndivyo inavyokuwa hivyo….mume akawa
hampendi tena huyo mwanamke, ….chuki, hasira…
‘Nakusimulia yote hayo, ni ili uelewe kuwa hilo lililokupata
wewe sio jambo la bahati mbaya ni kitu kilichopangwa…kilianzia mbali….lakini
kwa namna ambayo sio kwa kukukusdia wewe, ila ni kwa yoyote ambaye angeliingia
kwenye mtego wao ndio maana Tajiri, akaniambia nikusimulie na mimi ili uwe na
uhakika na hayo aliyowahi kukusimulia…’akasema pale alipoona Maua, akipiga
miayo.
‘Siku moja huyu shemeji,….kama nilivyozoea kumuita,
akanijia,…nikajua ana jambo, maana alionyesha wasiwasi na huzuni, kwanza
niliwazia kuwa huenda mumewe kashikwa na maradhi mengine mabaya, au yeye
mwenyewe kaambukizwa, lakini aliyonielezea, yalikuwa kinyume chake, na yalinitia
wasiwasi sana…’akatulia huku akishika shavu.
‘Sikupenda ……, lakini kwa vile nilimuheshimu na sikupenda
kumuumiza, ikabidi nimsikilize amalizie hoja yake, na mwishowe akaniambia;
‘Shemeji, najua wewe ni mdogo sana kwangu…na hili ninalotaka
kukuelezea huenda usilielewe na huenda katika fani yako ukaona kama
nakuingilia, lakini naomba sana msaada wako….’akaniambia.
‘Shemeji mambo hayo ni magumu sana kwangu, …’nikajitetea,
lakini hakukubali, akaendelea kunishinikiza, na sijui kwanini baadaye nilikuja
kukubaliana naye, inakuwa kama vile ana kitu cha ushawishi chenye nguvu
sana…..’akatulia
‘Mume wangu kama unavyomuona, amekuwa muhuni sana, yeye na
wanawake,..na sasa kawa mlevi…pombe wanawake na yeye….sasa hili linanitia
wasiwasi,…’akasema
‘Kwanini likutie wasiwasi……wakati hata wewe ndio tabia yako,
….naona kama nyote mumekuata, na kwani ameanza leo?’ nikamuuliza.
‘Sio hivyo, mume wangu anaumwa, lakini anaogopa hata kuja
kutibiwa, anaona aibu, ….na amekuwa akinunua dawa kienyeji, sasa naona
keshafikia hatua mbaya..’akaniambia.
‘Anaumwa nini, na kwanini haji kuniona?’ nikamuuliza.
‘Ana magonjwa sehemu zake za siri…’akasema.
‘Mwambie aje,…hayo yanatibika, asicheleweshe kwani
akichelewesha anaweza akapata madhara makubwa, na huenda akapatwa na magonjwa
mengine mabaya,…ukumbuke sasa hivi kuna ukimwi…’nikamwambia.
‘Nimemshauri yote hayo, lakini hataki, na kaniambia nisije
nikamwambia mtu…atakuwa akinunua dawa na kutumia’akasema.
‘Sasa unataka mimi nifanyeje?’ nikamuuliza.
‘Nitamshauri aje kwako, na wewe tumia mbinu zako za
kidakitari, kumshawishi…, mpime damu, na wakati wa kumpa majibu, mwambie
umegundua kuwa ana matatizo mengine…ambayo ni hatari zaidi,…nafikiri hapo
utakuwa umempata….’akasema huyo dada.
‘Na jambo jingine…ili kumdhibiti, naomba umfanyie upasuaji
wa kumzuia kabisa asizae….’akaniambia.
‘Kwa vipi, hilo la kumzuia asizae ni makubaliano yenu, na
mimi kama dakitari siwezi kuingilia maswala hayo ya ndoa…’nikasema.
‘Nakuomba ufanye hivyo…maana huyu mume wangu anaweza akaniletea
watoto wa nje…’akasema na kunisisitiza sana, na kipindi hicho hali yao ya
kiuchumi ilikuwa juu….pesa kwao ilikuwa sio shida.
Kwa vile nilikuwa nimeelewana sana na huyu dada, nikafanya
hivyo, lakini nilifanya hivyo baadaya kumshauri sana huyo mzee, na yeye kwa
vile alikuwa keshakata tamaa na ugonjwa aliokuwa nao, ambao ulishamuathiri
sana, kwa kuchelewa kutibiwa, akawa anakubaliana na kile nilichomshauri, na
ndipo nikamfanyia huo upasuaji ….
Akawa hawezi kubebesha mimba, ila angeliweza kufanya hivyo,
kama ningelimfanyia upasuaji huo na kurekebisha njia zake za uzazi, ni upasuaji
wa kawaida tu unajulikana. …..Tukawa
tumezoeana kwa mapana na hadi kuwa dakitari wake.
‘Kwahiyo ni kweli kumbe mzee hana uzazi….?’ Akauliza Maua.
‘Sijasema hivyo Maua….uzazi anao, ila tulisimamisha tu kwa
muda, ndio maana nikaanza kukuelezea hayo kwa kirefu….’akasema Docta.
‘Na hayo maelezo yote yanahusianaje na huu uja uzito
niliokuwa nao?’ akauliza Maua.
********
Kama nilivyokuwambia kuwa Tajiri, tulikuwa naye..kwahiyo
namfahamu toka huko utotoni, na ndoto yake ya kuwa tajiri alikuwa nayo toka
shuleni, …na hakupenda kusoma sana. Mimi nilifaulu na kwenda sekondari, hadi
chuoni, na nikaja kukutana naye hapo Arusha, akiwa na Malikia,…
‘Dakitari, bora nimekuona, maana nilikuwa nakuhitaji
sana…’akanimabi.
‘Jambo gani,….mkuu’ nikamuuliza, kipindi hicho alikuwa
hajajulikana kwa jina la Tajiri.
‘Mimi nataka kuelewana na mjomba wangu, na wewe nimekuona
upo karibu sana naye,…sijui nitumie njia gani?’ akaniuliza.
‘Yule ni mjomba wako…kwanini usielewane naye?’ nikamuuliza.
‘Tatizo ni mkewe……’akaniambia,….na tukawa tunakutana mara
kwa mara, na mimi nilimshawishi sana huyo mzee, hadi akaamua kuwa karibu na
Tajiri,….kwahiyo utaona jinsi gani nilivyokuwa karibu na hawa watu.
‘Kumbe japokuwa nilikuwa nimehusika sana kumshawishi mzee,
kuwa karibu na mpwa, wake, kumbe nyuma ya haya yote alikuwepo Malikia, na
hakuataka nijuane naye mapema, alikuwa akikutana na mimi pale tu anapoumwa.
Kuna kipindi nilikwama sana, kimaisha, kulitokea tatizo huko
kazini, tukasimamishwa nikawa sina mbele wala nyuma, …na mara akatokea Malikia;
‘Docta, mimi nakufahamu sana, utalaamu wako sitaki upotee
bure, mimi kwa sasa nina pesa nyingi tu, nitakusaidia mtaji, ufungue dispensary
yako, na utakachopata utakuwa ukinirejeshea deni, sio lazima leo,…’akaniambia,
na sikuamini kwani kweli alifanya hivyo, nikafungua zahanati yangu, na kwa vile
nilikuwa najulikana sana, nikawa Napata wateja hadi ikawa zahanati kubwa.
Kila nilipokutana na Malikia, ili kumrejeshea deni lake,
japokuwa kwa kidogo kidogo, yeye alikataa, akasema ipo siku atahitajia
kurejeshewa sio lazima iwe pesa, sikumuelewa, ….
‘Alikuwa mpenzi wako?’ akauliza Maua.
‘Nilishakuambia Malkia hana mpenzi…yeye mpenzi ni pale akiwa
na shida na wewe,….’akasema docta.
‘Siku moja akanipigia simu, ..na kuniambia kuwa atakuwa
akileta kazi zake kwa ajili ya kuziweka kwenye CD, mimi pamoja na udakitari,
lakini nilikuwa nimesomea mambo ya komputa, kwahiyo nilikuwa najua jinsi gani
ya kuziweka kazi kwenye CD, kutengeneza video za harusi…kwahiyo
sikumkatalia….’akasema.
‘Nikawa mara kwa mara ananiletea kazi zake….ambazo nyingi,
zilikuwa za watu alizozichukua kwa siri, zilikuwa ….oh, hazifai kwa jamii…mimi
niliogopa sana, lakini sikuweza kumkatalia…’akasema docta.
‘Kazi gani hizo?’ akauliza Maua.
‘Huyu mwanadada,a likuwa akichukua picha za watu, ambazo ni
za aibu, na huniomba nifute baadhi ya mambo, na kuyaweka kinamna …ni utaalamu
ambao nilikuwa naufahamu sana, sikupendelea hiyo kazi ukizingatia kuwa mimi ni
dakitari, na mambo kama hayo yakija kugundulika ningeliweza kupoteza kazi yangu…Lakini
nilikuwa sina ujanja wa kumkatalia, ….kwahiyo nikawa mmoja wa wasiri wake
wakubwa..’akasema docta.
`Siku zilivyozidi kwenda ndio jinsi alivyozidi kuniletea
kazi za hatari …yeye alikuwa haogopi kabisa, ikawa ni sehemu yake ya kupata
pesa kutoka kwa matajiri, ….alikuwa haogopi kabisa’akatulia.
`Alipoingia kwa mzee kwa mgongo wa Tajiri…akawa sasa
ananiletea kazi za Tajiri, kila tajiri anapokwenda mahali ni lazima awatumie
vijana wake kumletea kumbukumbu za kila alichokifanya, ….alisema ni kwa ajili ya
kumlinda Tajiri, …lakini sio kweli…..
‘Malikia kama alivyokuwa mke wa Mzee, walikuwa na tabia ya
kuamini sana mambo ya kishirikina, na sio wao tu,…kwa uchunguzi wangu nilikuja
kugundua kuwa wengi waliojiingiza kwenye biashara ya madini, walikuwa wakiamini
sana mambo hayo….
`Kwahiyo hawa watu walikuwa wakifanya mambo yao kila
mara,…na nilikuwa nayafahamu hayo kwa kanda za video walizokuwa wakiniletea
kuzihakiki na kuziweka kwa jinsi wanavyotaka wao,…sikuwa napenda kuzihifadhi
hizo kazi, maana niliogopa kuwa ipo siku wanaweza wakanivamia polisi nikajikuta
kwenye matatizo, ungeliona hizo kanda, ungeliogopa, …
‘Sasa kwanini ukakubaliana na kazi hizo za hatari?’ akauliza
Maua.
‘Malikia ni mwanamke anayejua mbinu nyingi sana,…pamoja na
kuwa yeye ndiye aliyeniinua wakati nikiwa nikiwa na shida, lakini alijua kuwa
akiniambia nimfanyie kazi zake kama hizo ningelikataa, kwahiyo aliweza kunitega
katika mambo mengine,….na kunitishia kuwa nisipomsadia kwenye kazi zake
atanilipua na sitaweza kufanya kazi zangu za udakitari tena….’akasema huyo
dakitari
‘Mambo gani hayo mengine?’ akauliza Malikia akimwangalia
huyo dakitari kwa macho ya wasiwasi.
‘Mhhh, tatizo lako unahoji sana….wewe huko sio pakukuelezea,
tuendelee na lile lililokuleta….’akasema docta na huku akiangalia saa yake
*********
`Tajiri na Malikia walikuwa na urafiki wa pwagu na pwaguzi,
kwani kuna siku wanakosana kabisa, lakini baadaye unawakuta wakiwa
wamelewana….na yote ni kwasababu ya utajiri wa mzee. Malikia alifahamu bila
Tajiri asingeliweza kupata kile alichokitaka kwa Mzee, kwahiyo alikuwa akiuma
na kupuliza. Kuna kipindi ambacho Tajiri alikuwa akisafiri sana kuja huku Dar,
na ikagundulikana kuwa keshampata msichana mwingine....
‘Unaweza kusema huenda Malikia alikuwa kaingiwa wivu,…ni
kweli ilionekana hivyo, lakini kwa mpangilia wa Malikia, alitaka ifikiea hatua
ya yeye kufunga ndoa na Tajiri, na kwa vile alishafanya mipango, na kumshawishi
Tajiri hadi akawa kaandikishwa kama mtoto wa mzee, kwahiyo alikuwa na haki ya
kumiliki…
Sasa zikaanza safari za Dar,…huko Tajiri akakutana na
kimwana mpya, akawa keshampenda, na hili lilikuwa kinyume na makubaliano yao na
Tajiri. Na Tajiri hakufahamu kuwa katika wale watu anaoandamana nao, kuna watu
waliopandikizwa na Malikia kwa kazi maalumu.
‘Hawa watu wakaleta taarifa kuwa kimwana aliyekutana na Tajiri,
sio tu kwa mambo yao ya kishirikina, bali anatakiwa kuwa mke wa Tajiri, na Malikia
aliposikia hivyo, akaweka pingamizi za safari za Dar, lakini Tajiri akakaidi, ….hili
lilimshitua sana Malikia kwani ndiye aliyekuwa akiratibu hizo safari, akaona
kuna umuhimu wa kumtambua huyo msichana…’akatulia
`Msichana gani huyo?’ akauliza Maua.
‘Maua…’akasema Docta, akiwa kaangalia pembeni, alitamka hilo
jina kama vile hamfahamu huyo anayemtaja jina ni huyo aliyekaa mbele yake.
‘Oh, kumbe ni mimi…’akasema Maua.
‘Mimi mwanzoni nilikuwa sikujui,..na sikuwa nakufahamu
vyema,… hadi nilipokutana nawe kule Arusha…na pale nilipoongea na Tajiri, …ndio
kumbukumbu za nyuma zikanijia, hata kwenye picha zako kwenye video, hazikuwa
zimekunyesha vyema….’akasema.
‘Uliongea na Tajiri kuhusu mimi?’ akauliza Maua.
‘Ndio , alipogundua kuwa hataweza kuishi, alinipigia simu,
akaniomba sana….niongee na wewe…na nikuelezee yote,…’akatulia na kuangalia saa
yake na mara simu yake ikailia, akaiangalia kwa makini, na baadaye akaipokea.
‘Kwani wewe ni nani?’ akauliza huku akiwa kakunja uso, na
akionekana kuwa na wasiwasi
‘Unasema unao mzigo wangu, ….kwahiyo unasemaje?’ akauliza.
‘Huo mzigo wanautafuta polisi ,…jana walikuja wakitafuta
ushahidi kwahiyo kama unao, ni bora uulete , vingenavyo umekalia bomu….’akasema
na kuinuka kwenye kiti, na alionekana kuwa na wasiwasi sana.
‘Mimi siwezi kujadiliana na hilo,….shauri lako….’akakata
simu kwa hasira.
‘Ni nani huyo?’ akauliza Maua huku akitabasamu. Na docta akakaa kwenye kiti,
na baadaye akainuka, akawa akionekana hana amani, akasogea pale alipokaa Maua,
na akawa kama anataka kuondoka.
‘Sasa unakwenda wapi docta….?’ Akauliza Maua.
‘Mambo yameheribika….’akasema huku akiangalia huku na kule.
‘Kwahiyo unasemaje?’ akauliza Maua.
Na kabla hajatulia mlango kagongwa, na mhudumu wake
akamsogelea akawa anamnong’oneza, lakini Maua alimsikia anavyoongea;
‘Wamekuja askari, …’akasema huyo mhudumu.
WAZO LA LEO: Kila aliyejuu ya mti , akumbuke kuwa alitoka chinini shinani, ....tusijisahau, tukajiona tumefika, huku juu kwenye kunahitaji uangalifu, jinsi gani ya kukaa, usije ukaanguka, ..Tatizo wengine wakiwa juu wanajisahau, na kuanza kuwatemea mate waliochini. Kwa vyovyote iwavyo ujue ipo siku utashuka!
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
Kisa kinanoga kwelikweli nimesoma kufikia hapa ..."Kwahiyo unasemaje?’ akauliza Maua.
Na kabla hajatulia mlango kagongwa, na mhudumu wake akamsogelea akawa anamnong’oneza, lakini Maua alimsikia anavyoongea;
‘Wamekuja askari, …’akasema huyo mhudumu."...nikasema aahhh mbona utamu ulikuwa unazidi eti ndo mwisho mpaka kesho tena....wazo la leo nimelipenda sana...Ahsante
'Mpaka kesho tena..' mpendwa wangu, kesho ni jmosi, labda niende internet cafe,
Nashkuru kwa moyo wako huo wa kujitahidi kuwa pamoja na karibu kila mwanablog, maana kila ninapotembelea nakuona umepiga hodi, Huo ndio ujirani mwema, na huo ndio upendo wa zati.
Napendekeza uwe mwanamblog wa mwaka, unasemaje?
Post a Comment