‘Ni nani wewe….’akasema Maua, na kugeuka haraka kuangalia
nyuma yake, na kujikuta wakiangaliana na mama yake mdogo,
‘Umejuaje kuwa nipo hapa ?’ Maua akamuuliza mama yake mdogo kwa
mshangao. Mama yake mdogo alikuwa akiangalia barabarani, akiwa anaangalia gari
la yule dakitari likiondoka.
‘Milioni mia mbili, ….hebu fikiria pesa kama hiyo ukiishika
mkononi, umasikini wote bai-bai,….Unaona, hii ndio dunia..ujanja kupata sio
kuwahi,….’akasema huku akiangalia juu, kama vile anawaza jambo fulani.
‘Nimekuuliza ulijuaje kuwa nipo hapa na huyu Dakitari?’
akauliza tena Maua.
‘Hiyo sio kazi yako, ….’akasema huku akiondoka, na wala
hakujali kumsubiri Maua. Na Maua akamfuatili kwa nyuma hadi walipofika
nyumbani.
‘Mimi nakushangaa, naona umekuwa mtu wa kunifuatilia kama
kivuli, …..’akasema Maua.
‘Mimi sijakufuatilia wewe….nilikuwa nafuatilia mambo yangu,
wewe endelea na gumzo lako na huyo dakitari wako, ….mimi sina muda
huo…’akasema.
‘Mama , unajua haya yote yametokea kwa sababu yako,..na
usikimbilie kunilaumu, kwani usingeliniingiza kwenye mambo yenu nisingelifikia
hapa…..’akasema Maua.
‘Acha visingizio….ushamba wako ndio umefikisha hapo, na
usinitupie lawama mimi kamwe, usipojifunza kwa hilo, usitegemee kuwa kuna
mwalimu wa kukufundisha,…’akasema mama mdogo.
‘Sawa nashukuru….sizani kama ungelikuwa umenizaa
ungelinifanyia haya,…’akasema Maua kwa uchungu.
‘Tatizo lako umeshahu kuwa nilikutoa kwenye umasikini, na
kutokana na mimi mama yako ana nyumba, hayo yote hamuyaoni….’akasema huyo mama.
‘Yote hayo yamefanyika kwa mgongo wangu, mimi ndiye
nimeumizwa, hadi haya yote yakapatikana..’akasema Maua.
‘Na utaumia zaidi…..’akasema mama mdogo huku akijiangalia
kwenye kiyoo.
‘Sawa..ipo siku nitakipa..na mtajuta wote mlionifanyia
haya…’akasema Maua
‘Haya endelea na usafi, maana leo ulinitegea, fua nguo,
ukimaliza, pika,….mimi nakwenda kuhangaika, bila kuhangaika, hatuwezi
kula…..wewe na hicho kimimba chako, jipweteka hapa nyumbani, mwisho wa siku
utakula jeuri yako…..maana sasa hivi si unaringa, ngoja, ifikie muda wa
kujifungua, ndipo hapo utakaponiona mimi ni nani’akasema.
‘Una maana gani kusema hivyo?’ akauliza Maua.
‘Utanielewa tu…mimi sio mtu wa kulea mmba za watu,
…nilishakuambia mtafute mume wa kuilea hiyo mimba, hutaki, ukakimbilia kumuona
dakitari, haya kakusaidia nini…?’ akauliza na kama vile kakumbuka kitu akasema;
‘Lakini sio mbaya, …nimefurahi kwamba kanifunua akili,..milioni
ishirini…na ngapi vile…’akasema huku akionyesha kufurahi na kuondoka zake, na
Maua kwa shida akawa anafanya hizo kazi za nyumbani.
*****
‘Maua umefika,samhanai kwa kuchelewa, na naona hapa
tutaongea bila kusumbulia….’akasema docta huku akifunga mlango, na Maua akakaa
kwenye kiti bila hata ya kukaribishwa, akasubiri Dakitari akae, huku akili yake
ikiwa inawaza mambo mengi.
‘Docta, mimi sioni kwanini tuwe na mazungumzo marefu, kwani
sizani hilo linahitajia kuongea, kama kwelii unamfahamu , au unafahamu ni nani
aliyenipa huu ujauzito niambie ukweli nijua ni wewe au kuna mtu mwingine, …?’
akauliza Maua na docta akamwangalia na kutaabsamu.
‘Tulia mpendwa,…kwa hali ilivyo…nasita hata kukuambia
ukweli, japokuwa nilimuahidi Tajiri kufanya hivyo…’akasema.
‘Kwanini docta…na najua kuwa unafahamu yote vinginevyo
Tajiri asingelinielekeza nije kwako’akasema Maua akionyesha kukaat tamaa.
‘Kama niliyokuambia kuwa mimi ni dakiatari wa familia ya
Mzee, na kwa vile nilikuwa nikimuhudumia Mzee, basi nikawa dakitari wa familia
nzima,….kila kukitokea tatizo, la ugonjwa, wakawa wananiita mimi…na bahati
niliyo nayo, sikusomea udakitari tu…..’akaanza kulezea.
‘Mzee, alianza matatizo yake, kitambo, na mimi nilijaribu
kumuelekeza jinsi gani ya kuweza kuyakwepa hayo yanayoweza kumletea madhara,
lakini mzee yule alikuwa mbishi sana,….Nilimwambia ili asiumie zaidi kwanza asiwe
anabishana na mkewe, kwani chanzo cha matatizo yao kilianzia kwenye
kutokuelewana kati yake na mkewe…’akatulia.
‘Maua nikuelezee ukweli, …ndoa ni nusu ya maisha ya mtu,
ukishaoa, ujue kuwa kila kitu ni kimeshinikizwa kwenye ndoa, hata kuwaza, ….mawazo
yako yote hayawezi kuwaza bila kuifikiria ndoa yako, vinginevyo unajiadanganya….’akasema
na kumwangalia Maua.
‘ Mzee, alikuwa kajenga utaratibu wake ….na hata baada ya
kuona alikuwa kaweka mipango yake, kuwa mambo yake, hasa ya kikazi, kibishara
ni yake binafsi na mkewe ni mshauri tu, hakupenda kumshirikisha moja kwa moja…na
chochoko zilianzia hapo….’akasema.
‘Katika maisha kuna kupanda na kushuka, ilifikia mahali
akakwama, mkewe akamshauri,….na alimshauri
kwenye mambo ya kishirkina,….wakati
huo, alikuwa hana matatizo ya kiafya, kwahiyo kujuana kwetu hakukuwa kama
ilivyokuja kuwa baadaye….’akakohoa kidogo kama kusafisha koo.
‘Mzee, akakubali, na wakafanya waliyoyafanya, na sina
uhakika kuwa hayo waliyoyafanya ndiyo yaliyowasaidia,..hadi kufikia hatua hiyo….kama
alivyoniambai mkewe….kuwa utajiri wote ulitokana na imani hiyo….’akatulia.
Maisha yakawanyookea, biashara ikapanuka, wakafungua
kampuni, na hata kuwa na wafanyakazi, na pesa ikaanza kufanya mambo yake. Mzee,
enzi hizo sio mzee, ni Tajiri…jina tajiri, lilikuwa jina la mzee, kipindi
hicho,japokuwa halikuwa jina la kujulikana kama alivyokuja kulitumia mpwa wake…akawa
sio mwenzetu. ..’akatulia.
Pesa, utajiri, usipouweza kuumiliki unaweza ukakuharibu,
…mzee kipindi hicho hakuwa na wazo hilo, akawa anatumia, na huenda ndio ulikuwa
muda wake, ili kujionyesha, basi akina dada hakucheza nao mbali, na hili likawa
limemkwaza sana mkewe, …wivu, na ….ni kawaida kwenye ndoa….wakawa wanakwazana. Basi
siku moja mkewe akadondoka kwa shinikizo la moyo….
********
Siku mkewe
alipodondoka ilikuwa ni siku ya sherehe za kuzaliwa mmoja wa binti zao, na mume
akaaga kuwa anatoka kidogo, sijui ilikuwaje, mke akashituka na kuanza
kuwafuatilia. Ni kweli kumbe mumewe alikuwa kaagana na mwanamke ….kwenye nyumba
ya wageni.
Mkewe akafika kwenye eneo la tukio, na akamfuma mumewe, …,
akiwa na mwanamke, na mwanamke huyo alikuwa rafiki kipenzi cha huyo mkewe,
hakuamini, na akili, ikishindwa kuhimili, mapigo ya moyo yakaongezeka, na
matokea yake ni kudondoka na kupoteza fahamu….’ Akaangalia saa yake na baaadaye
akamwangalia Maua.
‘Maua usione huu mwili, …kitu kidogo tu, kinaweza kikaharibu
mpangilio wote wa mwili, na ukawa sio yule mtu wa jana, huyo mama akawa mgonjwa
sana, …ikabidi huyo mwanadada alatwe hospitalini nilipokuwa nafanyia kazi
kipindi hicho…, kipindi hicho huyo mwanadada anawaka kweli mrembo, japokuwa
alishazaa watoto watatu….
Na ndipo nilipoanza kuzoeana na mke wa mzee, kwani alipofika
hapo hospitalini, nikawa mimi ndio namtibia, na akawa kila mara akijisikia
vibaya ananiita mimi, …na kipindi hicho sijawa mzoefu sana, na kufikia kiwango
cha dakitari bingwa.
‘Nilimchukulia huyo mama , kama sehemu ya utafiti wa kazi
yangu, nikawa karibu naye, na nikawa nikimdadidisi, kujua undani wa matatizo
yao…. nikagundua kuwa ana mawazo sana, na mawazo hayo yalitokana na ndoa yake…wivu..chuki,
na alikuwa tayari kulipiza kisasi…. Nilimshauri sana,…kuwa ajaribu kuhimili
hayo yaliyopo mbele yake, kwani yana mwisho, na asipojitahidi hivyo, ataumia,
na wenzake watachukua nafasi yake… nashukuru alinielewa, japokuwa kila mara
alikuwa akiniambia;
'Wewe bado mdogo, hujui uchungu wa kuchukuliwa mume,
….’aliniambia na nilimuelewa ana maana gani, na nikajaribu nijuavyo
kumuelimisha, japokuwa nilikuwa mdogo, ….lakini baadaye akatulia na tukawa kama
marafiki.
‘Huyu mwanadada, kipindi hajaolewa alikuwa rafiki ya kaka
yangu, na kipindi hicho alitakiwa
kuolewa na kaka yangu, lakini haikuwezekana, kwani mzee, alimuwahi na kumuacha
kaka yangu akiteseka kwa mawazo, kwani kaka alimpenda sana huyo mwanamama….mimi
nilikuwa mdogo, na nilimuonea huruma sana kaka yangu,…sikutarajia kuwa
nitafanikiwa kuwa karibu na huyu msalati wa kaka yangu.
Kaka yangu alipomkosa huyu mwanadada, alikosa raha sana, ….unajua kaka yangu alimpenda sana huyo mwanadada hadi kupeana pete za uchumba, na ilibakia kidogo tu wafunge
ndoa,…siku wakati wanasubiri hiyo ndoa, ndio huyu mwanadada akapotea ghafla, na kila wakienda kuulizia nyumbani kwao, hawatoi jibu lililo sahihi, kuonyesha kuwa walikuwa njama moja.
Kaka akawa mgonjwa…..hali halali......
Mapenzi hayana siri, kwani, baadaye tukasikia kuwa wamefunga ndoa na huyo mzee, na
wanaishi naye…kaka aliumia,…unajua kuumia, …akawa kama mgonjwa, …mimi nilikuwa
nampenda sana kaka yangu huyu, nikawa sichezi mbali na yeye, na ule utoto,
..nikimuona kaka yangu alivyobadilika, kakonda kama mgonjwa wa ugonjwa usio
pona…nilikuwa nalia…na ilifikia hatua naapiza kuwa siku nikimuona huyo
aliyemfanyia kaka yangu hivyo, cha moto akakiona….
‘Na yeye nitahakikisha anapata taabu….na kukonda kama
alivyomfanyia kaka yangu…’nikamwambia mama, na mama kipindi hicho anaumwa,
akaniambia;
‘Mwanangu ukitaka maisha yako yawe mazuri, usipende kulipiza
visasi…hata mtu akikufanyia ubaya gani, wewe uwe mwema kwake…’akasema mama. Na
baadaye niliposikia kuwa mama kafariki, na chanzo ni hay ohayo….’akatulia na
alionekana kama anajiwa na machozi, lakini akajikaza kiume na kusema;
‘Hawa watu walihamia Arusha muda mrefu, na kutokana na
historia ya familia yao, watu wengi waliamini kuwa wana tabia hiyo ya
kishirikina…mimi siamini sana mambo hayo, …na hata wazazi hawakupendezewa pale
kaka alipoamua kumuoa huyo mwanamke, kwa
imani hizo hizo…na ilipotokea hivyo..kuwa huyo mwanamke kakimbilia kwa mwanaume
mwingine.., kwao wao walishukuru sana…
Ghafla nikajikuta nipo na hawa watu tena…sikuyajali ya kale,
na kwa vile nimeshakuwa mtu mzima, mwenye taaluma, nikajipotezea hayo na
kuganga yalikuwepo mbele yangu. Na hata nilipokutana na huyu mwanadada
nilimtambua kwa jina la shemeji na tukawa tunaitana hivyo…nilikuwa na hasira
naye, kwa jinsi alivyomfanyia kaka yangu, lakini kwa vile yalishapita,
sikuyatilia maanani sana.
*******
Tabia haina dawa, na ukiingiza ubongo wako kwenye imani,
unaweza ukajikuta ukiwa mtumwa,…na huenda kama sio mtafiti, ukajikuta
unajiumiza mwenyewe, kwa imani ambazo huenda hata sio za kweli…na ndivyo
ilivyokuwa kwa huyu mwanadada.
Alipoletwa kwangu nikamtibia na kumpa ushauri nasaha,
alikuwa akiitikia tu,..lakini alikuwa na lake moyoni,….kwani alipopona, alimua
kutumia njia nyingine alizojua yeye…..nafikiri alipokutana na wazazi , kwani
aliamua kwenda kupumzika huko kijijini kwao,..huenda wazazi au marafiki walimshauri hivyo, au ni kutokana na maamuzi
yake, au hizo imani za mapokeo bila kufikiria akazifuata….na akawa kama
analipiza kisasi, kwani aliporudi toka nyumbani kwao, akabadilika…
Ndivyo maisha ya ndoa yalivyo…..mama huyo aliporejea mjini,
alikuja kwa namna ya pekee kabisa, ile hali aliyokuwa nayo, ka kujifunga
makanga, kujifunika, ikawa haipo tena…mavazi yakabadilika, …muonekano ukawa sio
ule tuliokuwa tukiufahamu,….akawa mtoto wa mjini….kaamua na yeye kujirusha na
wanaume wengine.
Alipokuwa huko kijijini, alikutana na kaka yangu, na watu
walifikia kusema kuwa huenda, aliamua kumrejea aliyekuwa mpenzi wake wa zamani,
yaani kaka yangu…sina uhakika sana na hilo. Lakini ni tatizo lilozindua hisia
zilizokuwa zimeshaanza kupoa, na ilionekana kama huyo mwanamke alikuwa an nia
mbaya na familia yetu.
Kaka yangu alikaa muda mrefu bila kuoa,…akisononeka….na mama
yangu akawa hana raha,...na kutokana na hilo, mama akashikwa na ugonjwa
..uliompelekea kupooza upande mmoja na hakukaa sana akafariki dunia...mama nilimpenda sana..oh, kipindi hicho bado nasoma, naletewa taarifa kama hiyo niliumia sana…niliporejea
nyumbani na kuhadithia hayo…niliumia sana, nilitaka kwenda kwenye hiyo familia kufanya jambo baya, lakini wakanizuia….'akatulia akiwa kakunja uso.
'Anyway...yote yakapita, nikarejea masomoni....na hata nilipoondoka hapo nikawa nimerejesha moyo nyuma na kusema yote hayo ni
mapenzi ya mungu....na yana mwisho wake...'akainama na kuwa kama anaomba
Na kipindi huyo mwanadada alipofika huko, alimkuta kaka ndio
kaoa mke mwingine , baada ya kuachana na mke aliyekuwa naye awali….mke huyo
aliyemuoa alikuwa na sifa zote za mke mwema, na wengi tulitarajia kuwa wataweza kuishi na kaka vyema,
lakini cha ajabu, kaka alipomuona huyu mwanadada, akamuacha mkewe…na kuanza
kutembea na huyu mwanadada…niliumia sana nilivyosikia hivyo.
Kaka hakujua kuwa mwenzake anayafanya hayo kwa hasira za
kulipiza kisasi kwa mumewe….anadanganyika, na wengine wakasema huyo mwanamke
kamuwekea dawa kaka yangu ili awe naye, lakini sio kwa mapenzi ya nzati…kaka
akawa kama mtumwa fulani wa huyo mwanadada..huwezi kusema kitu….wazazi wakawa
hawana raha….yote hayo nilikuja kuhadithiwa …’akatulia na kulionekana chuki
usoni na baadaye akasema
‘Tayaache hayo…tuendelee na ya kwetu….’akasema na kushika
kichwa na alionekana kama anawaza jambo, halafu akasema;.
‘Baadaye huyu mama akamuacha kaka kwenye mataa, akamrejea
mume wake huku Arusha, akiwa sio yule mama tuliyemjua kabla, aliamua kubadilika
sana,…, akawa mtu wa starehe kupitiliza, analewa na kutembea na waume za watu
bila aibu…ikawa na aheri ya mume wake…na ghafla kukatokea jambo lilozua gumzo
kwa watu, maana mume wake nay eye alibadilika ghafla, ……’akatulia kidogo.
Mume wake akawa kama mjinga fulani, habanduki nyumbani,
….akawa hatoki, akitoka, anakuwa kama anajiiba, hata watu wakaanza kusema kuwa
huyo mwanamama, kamtengeneza mumewe, kipindi hicho ni mwanadada, japokuwa alikuwa
keshazaa, lakini alikuwa msichana mrembo….na wanaume waroho wakawa wanasogelea
kila kukicha.
Hali ya mzee, ikawa ya mashaka, kwani alikuwa kama mtu
anayetumia madawa ya kulevya,….zezeta , ikabidi afikishwe hospitalini, na mimi
nikawa karibu naye, ….na tukawa tumezoeana sana, japokuwa ni mkubwa sana kwangu,
lakini kama alivyokuwa mkewe tukajenga urafiki wa karibu, na ndipo akaanza
kunielezea maisha yake, nikamjua na yeye vyema, kama nilivyomfahamu mkewe….
Nikawa nimeijua hii familia kama vile nimezaliwa ndani
yake..na moyo wangu ukawa unanihimiza nitimize lile lengo langu la utotoni…kulipiza
kisasi …..na huku moyo mwingine ukinikanya kuwa hayo hayana faida kwangu…..nikajikuta
kwenye njia panda…
NB: Imenibidi niandike sehemu hii ndogo kwa shida,..ndio
maisha,…na sasa tumesikia nauli hizo zinapanda…mbona kazi, ..kufa hatufi ila cha moto
tutakiona. Usitarajie mwenye shibe akamjali mwenye njaa, watatezi wetu,
viongozi wetu, hawawezi kamwe kujua shida zenu,…wao wana shibe, ndio wawekezaji
wa usafiri, unatarajia nini.
Naomba….tusichoke kuendelea na hiki kisa, kwani ni visa
vyenye mafunzo, na kila sehemu ina ajenda ya kuelimisha jambo fulani…na tuna
imani kuwa tukimalizana na huyu docta, tunaingia kwenye hitimisho.
WAZO LA LEO: Tuwe
makini kwa vijana wetu hasa wanapofikia ule umri wa `vishawishi’ tujaribu
kujenga tabia ya kuwaweka karibu na kusikiliza matatizo yao, kwani muda huo
unaweza ukawa mgumu kwao, na wasipopata msaada wa hekima, inawezekana ikawa ni
chanzo cha kuharibikiwa katika maisha yao.
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
Hakika hapa pazuri na pananoga..ilausiwe sana kwenye njia panda...wala hatuchoki tupo pamoja...
Ndugu wa mimi naona Kazi inapamba mto..MUNGU azidi kukusimamia na kubariki kazi za mikono yako!!
Pamoja sana Ndugu wamimi...
Post a Comment