Hata nilipofika kwa Dar, sikuweza kualala…., kwani akili
yangu ilikuwa imechoka kwa kuwaza, na ikizingatia kuwa sikufanikiwa kwa kile
kilichotufanya tufunge safari hadi Arusha. Na tumerudi Dar, mikono mitupu, na
kugeuzwa mfanyakazi wa ndani, huku mama mdogo akinilaumu mimi kuwa ndiye niliyefanya
mambo yasifanikiwe.
‘Sasa unaona tumerudi huku Dar, na umasikini wetu, ….mfadhili
mkuu, keshafaraiki, na hapa sina mbele wala nyuma,….hivi wewe angalia, kama
nisingelifanya yale maarifa tukapata hivi vijisenti vya kuanzia biashara yetu,
unafikiri ungelikula nini wewe….unalalamika kazi nyingi, sijui nini….’mama
madogo akawa ananisimanga.
‘Kwani mimi nimefanya nini kibaya….ni kweli kazi zimenia
nyingi, na hapa nilipo najisikia vibaya….’akajitetea Maua.
‘Kwani umefanya nini
kibaya….unadiriki kusema hivyo….’akashika kiuno na kumwangalia Maua kwa
hasira.
‘Hebu niambie, mimi ndiye niliyekupa huo ujauzito, …eti unajisikia
vibaya, siumejitakia mwenyewe,….wewe ukijiskia vibaya, ni shauri lako, hiyo
ndio raha yake..hehehe…unalo hilo, mimi siyo niliyekupa hiyo mimba, na
usinilaumu kwa lolote lile….ulitakiwa ugangamale, usikubali kuondoka
kule….’akasema mama mdogo.
‘Nibaki kule, wakati wewe umegeuka kuwa tapeli, huoni kama
tungeling’ang’ania kuaka kule ungeishia jela, na kutuingiza kwenye matatizo na
sisi, ….na mama yangu angeliingizwa kwenye matatizo yasiyomuhusu…..’akasema
Maua.
‘Ushamab wenu tu, mimi, wesingeliweza, maana kila kitu
nilikifanya nikiwa na uhakika nacho,….yale yote niliyafanay nikijua kuwa kuna
kukamatwa na polisi, lakini nilijua mwisho wa siku wataniachia, na ndipo
ningeliweza kuwabana wale watu…wewe unajua fika kuwa familia inayohusika ipo
pale, na ilistahili kuwajibika…nyie watu bwana, sijui mumezaliwa wapi….’akasema
mama kwa hasira.
‘Familia ipo, lakini sio wao walionipa huo uja uzito, na
kama mambo yalivyokuwa, hata huyo Tajiri mwenyewe alikana kabisa kuwa sio yeye
aliyenipa hupo ujauzito, sasa kwanini tuwabebeshe mzigo ambao sio wa kwao.
‘Hivi wewe una akili kweli….huyo Tajiri, mlikuwa naye huko
chumbani, …ni nani mwingine anayestahili kubeba huo mzigo….kama sio yeye, mimi
nakumbuka kabisa mliondoka naye na kuingia chumbani.., labda wewe mwenyewe
unamfahamu mwanaume mwingine, uniambie mapema niende kumshikiza mzigo
wake,…..’akasema.
‘Mimi sijui mtu mwingine, …nyie ndio mnaojua, kwasaabbu
mlininywesha madawa nikawa sijitambui,…’akajitetea Maua.
‘Kama hujui mtu mwingine, basi ni hawo hawo…na sitavumilia,…ni
lazima turudi huko huko, na safari hii tukirudi,….hakuna cha kulaza damu.
Mumeniharibia mpango wango wote, siku ile kama mambo yangelikwenda vyema,
…’akatikisa kichwa.
‘Kwani ilikuwaje mama mdogo, mpaka ukafanya vile?’ akauliza
Maua.
‘Wala usinikumbushe,….maana, aaah, yule askari moja
anajifanya sheria yote yake,….na kama isingekuwa yule mzee, ningeliswekwa
ndani……walibeba juu kwa juuu hadi polisi, nikatupwa rumande…..’akaanza
kuelezea.
*****
‘Mnanikamata kwa kosa gani….’, nikawauliza
‘Kwa kosa la utapeli, umedanganya kuwa unadaiwa pesa za
hoteli, kumbe sio kweli, …..mzee wa watu akatoa pesa nyingi….tunahitaji hizo
pesa haraka.’akasema huyo askari.
‘Mimi sijafanya hivyo , yote hayo ni uzushi, kama mnabisha
twendeni kwa huyo mzee, mkamuulize vyema, haya yite ni fitina tu, ili, hawa watu
wasiwajibike….’akasema mama mdogo.
‘Hebu tuambie ukweli,ukisema ukweli, sisi tutakuachia, hizo
pesa zipo wapi?’ akauliza huyo askari, akinifanya ,mimi mtoto mdogo,
nikamwambia.
‘Pesa gani hizo unazoulizia….mbona mimi siwaelewi?’
nikamuuliza kwa kushangaa.
‘Afande hawa ni watoto wa bongo, tusipowafundiaha adabu
hawawezii kusema ukweli….’akasema askari mmoja, nikijua ana maana
gani,…nikamgeukia na kusema;
‘Hivi nyie, mnajau sheria kweli…hamuwezi kunisingizia makosa
kama hamna ushahidi nao,nitawashitaki kwa kunizalilisha, kwanza, nitawafungulia
mashitaki kwa kutaka kunibaka….’nikasema na wale maaskari wakaangua kicheko.
‘Unaona afande, huyo ni mtoto wa bongo…..’akasema huyo
askari, na yule aaskri, akaniangalia kwa makini, na kuniuliza.
‘Hebu niambia ni nini kusudio lenu la kuja hapa Arusha?’
akaniuliza.
‘Kamuulize Tajiri, yeye ndiye alituchukua hadi akatuleta
hapa Arusha, kama isingelikuwa yeye tusingelikuwa hapa Arusha’akasema mama
mdogo.
‘Tutamuulizaje marehemu, au hufahamu kuwa Tajiri ni
marehemu’akasema huyo askari.
‘Basi kama ni marehemu, …..muulizei mjomba wake, wote hawo
watakuwa wanafahamu vyema, na nina imani
kuwa mzee, asingeliependa mambo yake yaongelewe ovyo….’akasema mama mdogo.
‘Hebu niambie, wewe na malikia mlijuana vipi?’akauliza huyo
askari.
‘Mimi na malikia, huyo malikia ndio nani, maana mimi namjua
malikia wa Uingereza, sasa huyo malikia mwingine wa Tanzania ndio nani?’
akauliza kwa mshangao.
‘Kuna binti mmoja aliyejulikana kama Malikia wa Mererani, na
…inasemakana mlikuwa mkikutana naye mara kwa mara…..’akasema huyo askari.
‘Inasemakana…ina maana hayo ni maneno ya kusikia,…huna
uhakika nayo, mimi niaweza kusema simjui mtu kama huyo, kama mna ushahidi wa
hilo nendeni mahakamani..’akasema mama mdogo. Na mara akaja askari mmoja na
kuongea na yule afande.
Yule afande akamwangalia mama mdogo kwa hasira, na baadaye
akaondoka, na yule askari aliyefika ambaye cheo chake kilionekana ni kikubwa
ziadi ya yule aaksri wa mwanzi, akamsogelea Mama mdogo, na kusema;
‘Mzee, kasema uachiwe na maswala yenu mtayamaliza huko
nyumbani, lakini nakuonya kuwa tabia hiyo sio nzuri, na nakuhakikishia safari
nyingine hutapata huo msamaha,. ….na kesho tusiwaone hapa Arusha, maana kuwepo
kwenu hapa kunatutua mashaka….’akasea huyo askari.
‘Mimi ni raia wa Tanzania, hakuna sheria ya nchi inayomzuia
raia yoyote kuwepo kokote kwenye nchi…nina haki kama raia wengine, kama nina
kosa, nipelekeni mahakamani…’akasema mama mdogo kwa nyodo.
‘Mahakamani utafika tu,…hilo kama unalihitajia, ….’akasema
na kukatisha pale simu yake ilipoita, akasema;
‘Sawa tumeshamuachaia, mnahaitaji aje huko?’ akauliza.
Wameshakata tiketi ya kesho, basi itakuwa vyema,…mama
tunakuhakikishia kesho hiyo watasindikizwa na askari, na tutahakikisha
wanaondoka na basi la kwanza, …mapemza iwezekanavyo….’akasema huyo askari.
‘Ina maana aliyebadili muda wetu wa kuondoka ni mama, mke wa
mzee,….?’ Akauliza Maua.
‘Ndiye huyo huyo….alikuwa na hasira ya pesa yake,……’akasema
mama mdogo.
‘Sasa pesa yake ulichukua ya nini?’ akauliza Maua.
‘Mimi nilitaka nichukue pesa ya kila mmojawapo anayejiweka
kimbele mbele …yeye alijifanay ndiye mwenye mamlaka ya mali ya mzee, sasa
nilitaka kumuonyesha kuwa sisi ni wajanja zaidi, …..na yeye ndiye aliyetilia
utambi kuwa mimi nikamatwe…’akasema mama mdogo.
‘Kwahiyo ulimdai hiyo pesa, au
yeye alikupa tu kwa kukuhurumia?’ akauliza .
‘Tuliingia naye makubaliano, kuwa
nisiwe shahidi kuwa wewe una uja uzito wa mzee, …kwasababu yeye kasikia kuwa
mimba uliyo nayo ni ya mzee, kwahiyo kama itabidi kwenda mahakamani au nikulizwa
na polsi, niseme kuwa sio kweli, ….na pili, nihakikishe kuwa tunaondoka pale
Arusha iwezekanavyo…mimi nikamwambia yote yanawezekana, ..lakini ni lazima kwa
thamani …’akasema.
‘Thamani ya nini..?’ akaniuliza
kama haelewi, na mimi nikamuonyeshea kwa vidole,….kuwa ni thamani ya pesa, na
akaniuliza kiasi gani, nikamwambia, kwa kuanzia tu nataka kamilioni kamoja,
akamaka kwa hasira,
‘Mama huoni kuwa hilo unalotaka
mimi nifanye ni jambo kubwa sana, kukataa ujauzito,..na kumuondolewa huyo mzee,
hiyo aibu, huoni kuwa mzee, ayaadhirika kwa kuonekana kuwa ana mamimba ya binti
mdogo kama yule,. Na huoni kuwa binti yule ni mrembo, akifika kwa huyo mzee,
utakosa kila kitu…’akatulia mama mdogo.
‘Halafu ikawaje?’ akauliza Maua.
‘Ikawaje, mama maneno yale
yakamtia wivu,..akajikuta akiingiza mkono kwenye pochi lake, na akatoka laki
tano….’alaipozitoa, nikwambia kuwa ile sio pesa saan sana itakuwa ni nauli tu,
lakini nikiitwa mahakamani sitaweza kufanga mdomo wangu.
‘Sina pesa hapa…kesho nitakuleta
hiyo pesa nyingine na ole wako ukinihadaa, nitakufanya ndondocha…’akasema na
mimi nikacheka kwa dharau ni kasema;
‘Mtoto wa mjani halogwi..kama ni
kuwafanya ndondocha kawafanye hawo washamba wenzako…mimi ni mtoto wa mjini.’akasema
huku yule mwanamama akimwangalia mama mdogo kwa mashaka, wakati Mama mdogo
alikuwa akizifutika zile laki tano kwenye pochi lake.
‘Sasa kwanini akasema kuwa
umemuhadaa?’ akauliza Maua.
‘Alikuja kugundua kuwa mimba hiyo
inawezekana isiwe ya mume wake,……na hapo akagundua kuwa nimemuhadaa, ….’akasema
mama mdogo.
‘Lakini mama mdogo, kama huu
ujauzito sio wa Tajiri, ni nani mwingine anahusika na huu ujauzito?’ akauliza
Maua.
‘Unaniuliza mimi tena…hilo
utalijua mwenyewe, na naomba , umtafute mume wa hiyo mimba, haraka la sivyo,
….ohooo…mimba hiyo itageuka kuwa kitega uchumi kwa wenzako jambo ambalo mimi
sitakubaliana nalo….’akasema huyo mama mdogo akisahau kuwa yote aliyesababisha
hayo ni yeye, nikainama chini nilizuia machozi, nikasema;
‘Na mimi ni lazima nimpate huyo
mtu, hata ikibidi kurudi huko Arusha nitarudi, hadi nimpate huyo aliyenipa huu
ujazito, na nikimpata…sijui,…..hasira zote zitaishia kwake..’akasema Maua.
‘Ukimpata huyo mtu kwanza faini,
….milioni tano,…pili,utaishi na yeye hadi ujifungue, na kila mwezi nitakuwa
nafika kama mzazi kuchukua pesa….’akasema mama mdogo kwa uroho wake.
‘Ni mpaka nikimpata…., ila ni
lazima nitampate, japokuwa nipo tayari kumlea mwanangu mwenyewe ikibidi, lakini
ni lazima nimfahamu huyo mtu, aliyenifanya nitaabike hivi, kwani taabu
ninayoipata…ajuaye ni mungu peke yake…., hali ninayoisikia, siwezi hata
kumsimulia mtu,….najua nikimuona huyo dakitari…nitapata majibu yote’akasema
Maua.
‘Dakitari…!?.....hivi huyo
dakitari ni yupi huyo maana kila mara wewe na mama yako mnamtaja huyo dakitari,
badala ya kuangalia watu wenye pesa, mnamtafuta dakitari,…mimi
siwaelewi…..dakitari gani huyo….?’ akauliza mama mdogo kwa mshangao.
‘Lazima nionane na huyo dakitari,
la sivyo nisingelirudi huku Dar, haraka kiasi hiki ….safari ya kurudi huku,
….ni kwa ajili yake,…na natumai nikikutana na huyo dakitari nitakuwa nimepata
jibu la fumbo hili….’akasema Maua akiwa kakunja uso akihisi maumivu ya tumbo.
‘Huenda ndio yeye aliyefanya vitu
vyake..hahaha..unalo hilo..’akasema mama mdogo akicheka na kuondoka kwenda
kwenye shughuli zake.
**********
‘Ninaomba kumuona dakitari mmiliki wa hii hospitali’akasema
Maua. Maua akiwa peke yake, hakutaka kuja na mama yake mdogo, kwani alijua
akiwa naye hataweza kupata ukweli wote aliokusudia.
‘Oh, ndio yule anataka kuondoka…’akasema binti wa mapokezi
akionyeshea kwa kidole kwenye maegesho ya gari, na Maua akageuza kichwa
kuangalia huko anapoonyeshea huyo dada wa mapokezi, na kule kulikuwa na jamaa
akiwa kavalia suti akitaka kuingia kwenye gari. Maua kwa haraka akamkimbilia na
kumuwahi kabla hajaingia kwenye gari lake;
‘Mimi ni Maua nimekuja hapa kutokana na maagizo kutoka kwa Tajiri…’akasema
Maua na kumfanya yule dakitari ageuka kwa haraka kumwangalia Maua na kugeuka
haraka kuangalia kwenye gari lake.
‘Oh, ….sizani kuwa nina muda wa kuongea….’Yule dakitari
akaguna na kusema, na huku akiwa kashikilia mlango wa gari lake, hakutaka
kumwangalia Maua akasema
‘Unasema Tajiri,….Tajiri yupi huyo?’ akawa anauliza kama
vila yupo kwenye mshangao.
‘Tajiri wa Arusha….’akasema Maua akiwa anajaribu kutafuta
mwanya wa kumwangalia yule dakitari, lakini yule dakitari, hakugeuka, na badala
yake akafungua mlango wa nyuma wa lile gari lake, halafu bila kumgeukia Maua,
na akasema;
‘Nina haraka sana, ..lakini kama ulitumwa na huyo mtu,
nahisi kuna jambo la muhimu sana, ingia ndani ya gari, tutaongea humo ndani ya
gari, nikiwa naendesha, nitahakikisha kuwa unafika nyumbani kwako..’akasema
huyo dakitari, na alipohakikisha kuwa Maua kaingia ndani ya gari, akafunga
mlango , halafu na yeye akaingia mbele.
Maua alihisi kuwa yule dakitari anamkwepa kumwangalia usoni,
….inaonekana hakutana Maua amwangalie moja kwa moja usoni, kwani hata
alipoingia ndani gari, kwa haraka alitoa miwani mikubwa akavaa usoni, halafu
akageuka nyuma kumwangalia Maua akasema;
‘Umesema wewe ni nani?’akauliza akiwa kamwangalia Maua.
‘Mimi naitwa Maua, na nahisi kama niliwahi kuonana na wewe
kabla …..’akasema Maua akimwangalia yule dakitari, lakini kutokana na ile
miwani hakuweza kumtambua vyema.
‘Inawezekana maana mimi kama dakitari nakutana na watu
wengi, unahisi ulionana na mimi wapi?’ akauliza huyo dakitari huku akigeuka
kuangalia mbele, na kuanza kuendesha gari.
‘Sina uhakika…kama ungelivua hiyo miwani, ingekuwa rahisi
kwangu mimi kukutambua vyema…’akasema Maua, na yule dakitari, akawa kama vile
hakusikia hilo ombi la Maua la kuvua miwani, akasema;
‘Haya niambie wewe na Tajiri mpoje?’ akauliza huyo dakitari
kwa sauti ya upole
‘Mimi na Tajiri, tumejuana kwasababu aliwahi kuniajiri
kwenye ofisi yake hapa Dar, …na sasa ni marehemu…’akasema Maua.
‘Kwahiyo hadi anafariki wewe ulikuwa mfanyakazi wake kama
sikosei, au?’ akauliza huyo dakitari.
‘Tunaweza kusema hivyo….’akasema Maua, akiwa na shaka ya
kuelezea kile alichohitajia kumuelezea huyo dakitari.
‘Kwahiyo hata kipindi Tajiri anafariki ulikuwa hapa hapa
Dar, …?’ akauliza.
‘Hapana nilikuwa na marehemu huko huko Arusha…’akasema Maua
na akamfanya yule dakitari ageuke na kumwangalia Maua , halafu akageuka
kuendelea kuendesha gari, akawa kimiya kwa muda, halafu akafika sehemu yenye
mgahawa akasimamisha gari, …akateremka na kumfungulia Maua, akasema;
‘Nahisi nimeshakufahamu….na kwa vile huko ninapokwenda
nahitaji haraka na nina mambo ya kuwaza, nitashindwa kuendesha huku naongea,
….tunaweza kuongea hapa mgahawani, kama hayo mazungumzo hayatakuwa marefu…’akasema
‘Hata mimi nahisi nakufahamu lakini sina uhakika…’akasema
Maua huku akiweka nguo yake vyema iliyojikunja wakati akiwa amekaa ndani ya
hilo gari, akawa anajaribu kumwangalia yule dakitari, lakini hakuweza kuwa na
uhakika na hisia zake.
‘Inawezekana, hebu tukae hapa kidogo, maana nikiondoka hapa
nafika kuwajibika….unajua tena kazi zetu,…huwa hatuhitaji maongezi marefu… nina
miadi ya kuonana na wateja wangu, naomba uongee moja kwa moja, ili tusipoteze
muda, …’akasema huyo dakitari
‘Kipindi Tajiri, akiwa katika hali mbaya, alinielekeza nije
nikuone wewe, akisema kuwa wewe ndiye utakayeweza kuni…..’hapo Maua akasita .
Yule dakitari akamwangalia Maua, halafu akasema;
‘Ni kuhusuiana na jambo gani, maana mimi mwenyewe nasita
kusema lolote, …maana sijakufahamu vyema, japo nina hisia kuwa nakufahamu,…..watu
wanafanana…..ungeniambia ukweli wewe ni nani kwa Tajiri, ili tuweze kuongea
vyema, na tusipoteze muda’akasema huyo Dakitari.
‘Mimi naitwa Maua…sijui kama uliwahi kulisikia hilo
jina,….na kama hujawahi basi ndio jina langu, na kama nilivyokuambia nilikuwa
mfanyakazi wa Tajiri… na bahati mbaya tukaingia kwenye mahusiano na yeye, na
akanipa ujauzito wake, lakini….’akatulia.
‘Oh, nimeshakuelewa, …unasema ulikuwa na mahusiano na yeye,
kama wapenzi kama sikosei,….’akasema na kumwangalia Maua . Maua akawa katizama
chini kama vile anaona aibu kumwangalia yule dakitari moja kwa moja.
‘Usijali, hayo ni mambo ya gawaida, na kwa Tajiri siwezi
kushangaa….’akasema dakitari.
‘Kwahiyo mnafahamiana sana na Tajiri?’ akauliza Maua.
‘Kutokana na kazi yangu..nafamiana na watu wengi….na huyo ni
mmojawapo….
‘Kwahiyo ndio wewe niliyekutana nawe kwa Mzee, nikakupa kadi
yangu?’ akauliza na Maua akainua uso na kuangaliana na yule dakitari ambaye kwa
muda huo alikuwa keshaivua ile miwani yake, na kuishikilia mkononi, kama vile
anaisafisha.
‘Oh, ndio wewe kumbe…unajua ulivyokuwa umevaa hiyo miwani
nilikuwa sijakutambua, na siku ile sikuwapata muda wa kukuangalai
vyema,….’akasema Maua.
‘Ndio mimi, …..mimi dakitari wa mzee wa siku nyingi, na
namfahamu sana yule mzee, kama alivyokuwa wakili wake, sisi tulikulia pamoja
huko kijijini, japokuwa mimi nilikuwa mdogo kwao, na bahati nzuri tukajikuta
tukiingia kwenye mahusiano ya kikazi….’akasema huyo dakitari.
‘Lakini…..sio kuhusu Mzee…’akataka kuongea Maua, kuwa
hakufika hapo kwa ajili ya mzee.
‘Huwezi kuongea maswala ya Tajiri bila kumuhusisha mzee,
kwasababu Tajiri alikuwa sehemu yam zee, na ndiye aliyekuwa mtendaji wake mkuu,
japokuwa kiundani kulikuwa na mambo yaliyokuwa yakiendelea kinyuma na matakwa
yam zee….’akasema huyo dakitari.
‘Alinielezea Tajiri, na sikuamini kuwa mtu kama yule
angelifanya hivyo, ila mimi naamini ni kwasababu ya Malikia…..’akasema Maua.
‘Malikia….mmh’akasema huyo dakitari na kuguna.
‘Inaonekena Malikia ni mtu muhimu sana, na anajulikana
sana?’ akauliza Maua.
‘Ni mwanamke asiyeleweka, na tusema ni mjanja kupita kiasi,
lakini ujanja wake ni kibinafsi zaidi, …..yeye aliweza kufanya lolote ili
kupata anachokihitajia hata ikibidi kuua. Mwanzoni sikuwa namfahamu vyema,
lakini nilipokuja kupewa taarifa zake na kuja kukutana naye mwenyewe ana kwa
ana, ….’akatulia nakuangalia saa yake.
‘Sawa , hata mimi nimeshamfahamu….’akasema Maua akichelea
kuwa hataweza kuongea yale yaliyomleta.
‘Maua, najua kuna jambo kubwa sana tunahitajia kuliongea,
lakini nahisi muda hautatosha maana nahitajika kuwajibika, sasa…wewe njoo kesho
pale hospitalini kwangu, …ukifika nitajua wapo tutakaa na kuongea kwa mapana,
hilo unalolihitajia linahitajia umakini ….’akasema huyo dakitari akiinuka kuongea.
‘Lakini dakitari, halihitajii maelezo marefu…ninachotaka
kujua ni kumtambua aliyeniap huu uja uzito, maana….’akasita Maua pale dakitari
alipomwangalia.
‘Maua ….ninaweza kusema hata mimi sijui ni nani aliyekupa
huo ujauzito, mpaka nifanya utafiti wa kina, na kwa vile mimi sikuwa nafahamu
kuwa kweli imetoeka hivyo, sikuwa nimelitilia maanani ….kwahiyo nahitajia muda
wa kukusanya vielelezo,….’akasema huyo dakitari, akiangalia saa yake.
‘Docta ni nani aliyenipa huu ujazito?’ akauliza Maua kwa
hasira.
‘Kwahiyo unahisi ni nani….kuwa ni mimi….?’ Akauliza huyo
dakitari kwa mashaka.
‘Inawezekana, ….maana kwanini ujifiche macho..na sasa
unachelea kunielezea ukweli…nahisi mlikuwa na njama zenu…sasa kama usiponiambia
ukweli, nikitoka hapa kituo cha kwanza ni polisi,….’akasema Maua
‘Utakwenda kusema nini, kuwa ulibakwa au?’ akauliza dakitari
akivaa miwani yake , huku akiangalia huku na kule kuonyesha wasiwasi.
‘Ndio, na wewe ukitumia udakitari wako, mkaniwekea
madawa…..’akasema Maua.
‘Maua, …sitaki nikuambia jambo hilo juu kwa juu, kwanza
itanibidi niwasiliane na wote waliohusika ili tuliweke sawa,
vinginevyo,…utakuwa ukipigwa dana dana…kama Tajiri kasema sio yeye, …kakutuma
kwangu, ….huenda kuja kwako hapa ulifahamu kuwa mimi ndiye niliyekupa huo
ujauzito…na mimi nasema …sio mimi mwenye huo uja uzito wako…kama unataka ukweli
ufanye subira, lakini kama unataka haraka, nenda kamuulize aliyekuwa wakili wa
mzee….’akasema huyo daktari na kuanza kuondoka.
‘Tatizo lenu hamnijui,…ngoja niende polisi, huko ndio ukweli
utajulikana,…..’akasema Maua akiiunuka kuondoka.
‘Maua hilo halihitajii polisi…utakuwa unajiahangaisha
bure…ushahidi wote nilikuwa nao mimi, ….lakini nahisi Malikia
keshauwahi…kwahiyo wacha nitafute mbinu za kukubaliana na yeye, ….kwani mimi
ndiye niliyebeba dhamana….’akasema kwa sauti ndogo.
‘Malikia aliwezaje kuuchukua kwako, kwani alikimbilia huku
Dar, alipokuwa akitafutwa na polisi?’ akauliza Maua.
‘Apofika hapa sikujua anatafutwa na polisi, na kwa ujanja
wake, akaweza kukaa kwangu siku hiyo, akiwa na mpenzi wake…?’ akasema Dakitari.
‘Na mpenzi wake yupo tena?’ akauliza Maua.
‘Haya mambo usitake kuyauliza sana,….Malikia ana wapenzi
wengi, na kila mmoja alikuwa na jukumu lake, na huyo aliye naye kwa sasa tunaweza kusema ndiye waliyeshibana zaidi, na
ndiye msiri mkubwa kwake,…..’akasema dakitari.
‘Kwahiyo Tajiri, alikuwa sio mpenzi wake?’ akauliza Maua.
‘Tajiri alikuwa mpenzi wake kwa ajili ya jukumu kubwa la
kumuwezesha Malikia kuingia kwenye miliki ya Mzee, …na alipofanikiwa akawa
ndiye muendeshaji wa shughuli zote, nyuma ya Tajiri, Tajiri pale alikuwa kama
tarishi…mzee hakulijua hilo….’akasema dakitari.
‘Kwanini sasa hukumwambia mzee…..?’ akauliza Maua.
‘Wewe humjui mzee, yule mzee, akimwamini mtu , huwezi
kumbadili, mpaka litokee jambo ka uwazi, litakapothibitisha vinginevyo…mimi
niliwahi kumwambia kuwa awe makini na huyo binti, lakini kwa kipindi kile
hakupenda kabisa kunisikiliza, …’akasema dakitari.
‘Na hata huyo mpenzi wake Malikia ulikuwa ukijua ubaya wake
kwa mzee, na mzee hakuweza kukusikiliza, au na wewe ulikuwa kwenye chambo cha
Malikia?’ akauliza Maua na kumfanya dakitari atabasamu, akasema.
‘Huyo mpenzi wa Malikia, sikuweza kumfahamu mapenda kuwa ni
mshiriki wa kumwangamiza mzee,…usingeliweza kumfahamu , na hata mzee,
asingeliweza kumfahamu,….hadi hatua ya mwisho, aliposikia wakiongea akiwa
kapoteza fahamu, na bahati alizindukana nila wao kujua na kuyasikia hayo
waliyokuwa wakiongea….’akatulia.
‘Ni kweli hayo unayoyaongea?’ akauliza Maua.
‘Huo ndio ukweli…huenda wengi wakahisi kuwa na mimi nilikuwa
mmoja wa watu waliokuwa wakimuhadaa mzee, huku wakitumia utajiri wake, lakini
sivyo hivyo, na kawaida yangu huwa sipendi umbeya….niliyoyagundua kama
yalistahili kumuelezea mzee, nilimshauri, lakini mzee hakusunisikiliza, na mimi
nikaona sina haja ya kujiingiza zaidi,….’akasema.
‘Kwahiyo ulipoona kuwa mambo yanazidi kuwa mabaya ukaamua
kukimbilia huku Dar, au sio?’ akauliza Maua.
‘Maua wewe ulifaa kuwa mpelelezi, mbona maswali yako
yanakuwa kama ya askari kanzu’akasema dakitari.
‘Kwani una wasiwasi na askari kanzu?’ akauliza Maua.
‘Kwanini niwe na wasiwasi..?’ akauliza.
‘Nakuona…matendo yako yanadhihirisha hilo..’akasema Maua.
‘Matendo kama yapi?’ akauliza dakitari akimwangalia Maua.
‘Kama hayo….ya kuvaa miwani kuogopa nisikutamabue kwa
haraka, …na …na’akasita kuendelea kuongea.
‘Maua hayo niliyayafanya makusidi, niliposikia jina lako
nikahisi nakufahamu, lakini sikutaka wewe unifahamu mapema, kabla sijakufamu
wewe…ndio maana nikavaa hiyo miwani, lakini sio kwa nia mbaya. Na hivi sasa
natakiwa niwe makini kwa kila jambo la hawa watu, kwani ni wahalifu,
wanatafutwa na polisi, na wameshachukua ushahidi muhimu….’akasema na kutulia.
‘Je umeshawahi kuwasiliana na polisi kuhusiana na ushahidi
huo?’ akauliza Maua.
‘Ushahidi huo kwasasa hauwahusu polisi, ni maswala ya ndani
ya watu binafsi, lakini kama ingelifikia hatua polisi wanauhitaji…..nisingesita
kuwakabidhi, lakini kwa kibalia cha wenyewe..’akasema dakitari.
‘Kibali cha wenyewe akina nani?’ akauliza Maua.
‘Tajiri na mzee wake…’akasema huyo dakitari.
‘Umesema huo ushahidi umechukuliwa na Malikia, na….huo
ushaidi unahusiana vipi na huu uja uzito wangu?’ akauliza Maua.
‘Tajiri alikuwa na tabia ye kurekodi matukio yake yote, na
baadaye huyapitia na kuondoa sehemu zile zisitakiwa,…..kabla hajawakilisha kwa
Malikia, na mimi ndiye niliyemshauri hivyo., kwani kama nilivyokuambia,….kila
kitu alichokuwa akikifanya Tajiri, kilitokana na Malikia, …na walianza
kusigishana pale Tajiri alipokutana na wewe, na akawa anafanya manbo kinyume na
makubaliano…’akasita.
‘Wewe yote hayo uliyajulia wapi?’ akauliza.
‘Maua,…..kweli sasa naanza kukushuku vibaya, hayo maswali
yako sio mema,..lakini sijali, ila ninachoweza kukuambia ni kuwa Tajiri, mimi
na ….huyo mpenzi wa Malikia, tulikuwa marafiki wa siku nyingi….ingawaje, kila
mmoja alikwa na siri yake moyoni..’akasema.
‘Na huenda wote mlikuwa wapenzi wa Malikia?’ akasema Maua
kama anauliza.
‘Kwa malikia lolote liliwezekana, na ndio maana alipokwama ….alikimbilia
kwangu, lakini mimi nilishamfahamu vyema, kuwa alivyo, hata rafiki wa kudumu,
rafiki kwake ni wakati pale anapohitajia msaada, akishaupata hana faida na wewe
tena…walipofika hapa, niliwashitukia, na walipogundua kuwa ninaweza kuwaarifu
polisi, wakatoroka usiku….’akasema.
‘Wakatoroka na huo ushaidi?’ akauliza
‘Nahisi ndio wao wameuchukua,…maana hakuna mtu mwingine
angelikuwa na hamasa nao’akasema.
‘Wewe uligundua lini kuwa huo ushahidi haupo?’ akauliza.
‘Jana…niliposikia kuwa hali ya mzee ni mbaya, na
nilipokwenda kuangalis sehemu nilipoweka huo ushahidi nikakuta kabati lipo
wazi, na hakuna mtu anaweza kingie huko…..ni mara ya kwanza kutokea hivyo…’akasema.
‘Sasa utafanyaje kuupata huo ushahidi na una umuhimu gani
kwangu, maana mimi ninachohitaji ni kumjua huyo aliyenifanay hivi,…na kwanini….sihitajiii
ushahidi wowote’akasema Maua.
‘Unahitajia ushaidi, maana nikikuambia kwa mdomo hutaamini,
na ….huenda usiaminike kwa hilo kwa yoyote yule, na mimi nahitajia kuwa makini
kwa kila jambo, ili mwisho wa siku nisije nikaingia lawamani….ukumbuke huyo
mtoto akizaliwa atahitajai kumfahamu baba yake, au sio? Akauliza huyo dakitari.
.Kwani huo ushihidi una muhusu ni nini Malikia, na je
ukiuhitajia kwake, unahisi atasema nini, maana yeye anatafutwa na polisi na
kama ana vitu kama hivyo, vitadhihirisha kuwa yeye ndiye alikuwa nyuma ya mambo
yote hayo…unahisi kwanini kauchukua huo ushahidi?’ akauliza Maua.
‘Malikia alipanag kila jambo kwa manufaa ya baadaye….anachohitajia
hapo kwasasa ni pesa…’akasema dakitari.
‘Kwanini ni pesa, na ni kiasi gani?’ akauliza Maua akionyeha
uso wa kukasirika.
‘Yule bado anahitaji pesa kwa mzee…..ni kiasi gani, siwezi
kusema inawezakana ni zaidi ya milioni mia mbili…sina uhakika…’akasema huyo
dakitari akiondoka.
‘Eti nini…..milioni mia mbili,….oh?’ akasema Maua, na
alipogeuka kwa haraka kutaka kumkimbilia Dakitari, akajikuta akishikwa began a mtu,
akageuka haraka kwa hasira,……;
NB: Tumerudi tena ulingoni.
WAZO LA LEO:
Unapoaminika na kupewa siri ya mtu , inabidi uitunze, kwani hiyo ni dhamana ya
watu, vinginevyo ungelikataa moja kwa moja kwa huyo mliyekubaliana naye. Na pia tuwe makini kukubali kubeba dhamana hizo, tukijua kuwa nyingine ni mzigo usiobebeka
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment