Yule mzee alifungua macho, akijaribu kuyalazimisha, lakini dawa
zilishaanza kufanya kazi, na kwa mujibu wa dakitari, akishazitumia hizo dawa hakutakiwa
kusumbuliwa tena…, sasa huyo aliyeingia ni nani, na anakumbuka kabisa,
alimwambia docta wake akitoka, awaambie wafanyakazi wake, wasimruhusu mtu
yoyote kuingia ndani….kutokana maagizo yake mwenyewe.
‘Huyu atakuwa huyu mwanamke…mapepe, simpendi huyu mwanamke, …acha
tu, …mjomba wangu nimemwambia huyo sio mke wa kuoa, …lakini hasikii, ooh, ndio
kupenda huko…shauri lake…’akawa anawaza huku bado akijaribu kufungua macho.
Alikumbuka kusikia sauti za watu wakijibishana, na mwanzoni
alijua kuwa huenda alikuwa ni huyo dokitari wake akiwaelekeza wafanyakazi wake
kuwa wasimruhusu mtu kuingia humo ndani…..
Na alipoona mlango ukifunguliwa….akahisi huenda ni docta wake
karudi tena,..lakini cha ajabu aliona taswira ya mtu mwingine akiingia, na
japokuwa alikuwa akimuona na mawingu machoni, lakini alijua kabisa huyo alikuwa
ni mwanamke…kwa jinsi alivyovaa…hapo, akaguna, akijua ni yule mwanamke asiyependa
kuonana naye,….mchumba wa mjomba wake.
Siku za karibuni mwanamke huyo ametokea kubadilika, na
amekuwa akiingia humo hajali, ….hamjali, na wala hajali masharti ya dakitari,
kuwa yeye hatakiwi kusmbuliwa na mambo mengine ya kimaisha,, kwa hali aliyo
nayo anastahili kupumziahs kichwa chake, lakini akiingia huyo mwanamke, anakuwa
kama vile anataka kuhakikisha yeye haponi, na ikibidi afe….
Mwanzoni huyu mwanamke alikuwa mpole, akawa anamnyenyekea
utafikiri mtu wa dini, na kwa tabia hiyo aliyoionyesha mwanzoni, mzee huyo akamwamini
na kumpenda sana, na hata alifikia kumshauri mjomba wake , amuoe huyo mwanamke,
kwani angeliweza kumsadia katika shughuli zao za kibiashara. Lakini siku moja
akamjia rafiki yake wa karibu akamuonya kuhusu mwanake.
*********
‘Rafiki yangu, najua hutaki kuingiliwa mambo yako, lakini
hili sitaweza kulivumilia, maana mwisho wa siku ukiharibikiwa, halafu nije
nikuambie kuwa nilikuwa nalijua hilo utanilaumu sana….’akasema rafiki yake.
‘Umeshaanza, ..mimi nilishakuambia mambo yangu …hasa maisha
yangu ya ndani sitaki mtu wa kuniingilia, ..hilo nimewaambia hata wazazi wangu,
ndugu zangu wote, na wamelielewa, japokuwa ni kwa shingo upande…sembuse wewe
rafiki tu…’akasema huyo mzee.
‘Hilo nitakuambia hata kama ukinikasirikia, lakini ni vyema
nikuambia tu,..maana najua hatima yake ni nini….na nashindwa imekuwaje, siku
hizi hufuatilii mambo yako …ulikuwa ni lazima uchunguze jambo kabla
hujakubaliana nalo…sasa iweje,….’akasisitiza huyo jamaa na kutulia pale
mwenzake alipoonyesha kukerekwa.
‘Kwanza ni jambo gani hilo….usiwe mtu wa kufumba fumba, …ni
jambo gani hilo na linamhusu nani?’ akauliza huyo mzee pale alipoona huyo jamaa
akisisitiza.
‘Ni kuhusu huyu mwanamke ambaye ni rafiki wa kijana wako, ….mchumba
wa mjomba wako’akasema huyo jamaa
‘Ehe, ehe….nilijua tu watu wataanza kuchonga maneno, …kwanini
hamuniachi nikapumua, na maisha yangu….mumechonga maneno hadi mke wangu
kaondoka,…sasa na huyo naye…huyo ni rafiki wa mjomba wangu, na mimi sipendi
kuingilia maisha yake..hasa hayo ya kindani kiasi hicho…’akasema huyo mzee.
‘Wewe ni mjomba mtu,.na kiutamaduni, na mila za kiafrika,
mtu anayestahili kuingilia mambo kama hayo ni mjomba, au shangazi..au kwa vile
unajiafanya mzungu, ndio maana hata mila zetu unazisahau…!’akasema huyo jamaa
akionyesha kushangaa.
‘Haya nayajua….achana nayo,…haya sema ni jambo gani maana
wewe ni sasa umegauka kuwa mwanasiasa, ongea lililokujia, maana mambo yetu ya
kibiashara huyaoni ya maana,..umeanza mambo ya mitaani na kuchunguza nani kala
nini na anaishi na nani, umeanza wapi hiyo tabia…unajua tumekuwa marafiki wa
siku nyingi kutokana na tabia zetu kuivana, tabia yako haipo mbali na tabia
yangu…’akatulia akimwangalia rafiki yake huyo .
‘Na kuuliza unamfahamu vyema huyo mwanamke?’ akauliza huyu
rafiki yake
‘Nani,…una maana huyo anyejiita Malikia wa Mererani,….aah,kwa
ujumla simfahamu vyema….sina kumbukumbu za kumtambua, nahisi ni hawa wasichana
waliotoka huko kijijini, …aliniambia kuwa kwao ni huko huko kwetu,
nilipozaliwa, japokuwa ni vijiji tofauti…’akasema huku akianza kuingiwa na hamasa
za kumjua huyo binti.
‘Ina maana umesahau….unakumbuka siku zile mke wako alipoanza
kukujia juu, akidai kuwa huenda una mwanamke wa nje, umesahau, ….?’ Akauliza huyo
jamaa.
‘Yale yalikuwa maneno na hisia za mke wangu, lakini ….’akatulia
kuwaza.
‘Kipindi kile tunakwena kujirusha kwenye ile hoteli ya
kitalii, hukumbuki msichana mmoja aliyekuwa akijileta kwako mara kwa mara..na
wewe kwa vile ulishamshiba mkeo, hukumjali…na kwa vile pia ulikuwa na ile
nyumba ndogo, nyingine, ukawa hutizami nyuma wale mbele…’akaambiwa.
‘Aaah, hayo yalishapita bwana, nyumba ndogo nyumba ndogo…yule
mwanamke sitaki hata kumkumbuka, ameniweka mahali pabaya sana…sijui kama
nitamsamehe..’akasema.
‘Mkeo au hiyo nyumba ndogo?’ akauliza huyo rafiki yake.
‘Aaah, mke wangu achana naye…tunazungumzia hiyo nyumba ndogo…’akasema
huyo mzee.
‘Hiyo nyumba ndogo….najua huachi kuiwaza,….sawa tuachane
nayo au sio…’akasema na kutulia.
‘Ndio na wala sihitaji kujua nini kuhusu yeye…’akasema huyo
mzee.
‘Kweli inabidi umsahau kabisa, kwani nasikia yupo ulaya na aliwahi
kurudi mwaka jana na huyo mume wake, hutaamini, huwezi kujua kuwa ni
mwenzetu,..kabadilika kabisa, na kwa ile sura yake nyeupe, na nywele
alivyoziweka, huwezi amini kuwa ni muafrika….kampata mume tajiri , na alivyo
mjanja, kawainua ndugu zake, na familia yao, toka walivyokuwa awali, na sasa
kila mmoja nyumbani kwao ana gari, nyumba, kitega uchumi…..’akasema huyo jamaa
‘Hayo yote nayafahamu….lakini ipo siku atanikumbuka,…’akasema
huyo mzee.
‘Hilo ni dua la kuku,…halimpati mwewe..yule mwanadada ni
kichwa, anajua kutafuta maisha na kuwezesha, kimahesabu,..hasaidii tu, bali
anawezesha watu kujiajiri, …katoa misaada kwao, kwa lengo la kujiendeleza, …yule
kama ungelimpata wewe sasa hivi tungelikuwa tunaongea mengine…’akasema huyo
jamaa.
‘Tatizo lako, unataka kuniumiza moyo wangu bure tu, maana
hali imeshakuwa hivyo, unataka mimi sasa nifanye nini….alinikataa kwasababu
nina mke mwingine, na masharti yake, yalikuwa nimuache mke wangu wa kwanza
nimuoe yeye…na haikuwezekana kwa haraka vile….’akasema huyo mzee huku
akisononkena moyoni.
‘Lakini mimi nilikushauri kuwa uangalie mbele, na ujaribu
kuwapima hawo wanawake wawili…huyo mke wako wa kwanza, hana jingine zaidi kua
kutumia, kudai, na kuharibu…hajaweza kukusaidia lolote,….angali jinsi
alivyokuweka kwenye maisha magumu, hafundishiki yule…yeye ni kujitanua ,
kujionyesha na …kwakweli mimi sikumpenda awe na wewe, ndio maana nikakushauri
uachane naye, umchukue huyo …ukanipuuza’akasema.
‘Ok…yamepita, na …sihitaji tena, maelezo ya hayo maisha
yangu ya nyuma hayana maana kwangu, hakuna jinsi ya kuyarejesha, na hivi sasa
sitaki kuiharibu familia yangu tena,..najua makosa yangu, na nililenga kuwa kwa
vile yule ni mama watoto wangu, ingefikia muda angelitulia,na kubadilika….lakini
hajawahi kunisikiliza, na baya zaidi kawaambukiza hadi watoto wangu…’akasema
kwa huzuni.
‘Lakini kuhusu watoto wako usijali, mtoto kwa mzazi,….ni
mtoto tu, hata kama wapo upande wa mama ipo siku watakureja…..na kukumbuka
fadhila zako….’akasema huyo jamaa.
‘Mhh, hilo naliwazia sana….na najaribu kutumia lugha ya
hekima nikiongea nao, lakini naona kama vile, mama yao kawapika na wakapikika,
wanajua kuwa mimi ni mbaya kwa mama yao, kwasababu ya nyumba ndogo, na nyumba
ndogo yenyewe imeshaota mabawa…’akasema.
‘Kwahiyo huna mawasiliano na watoto wako tena, …?’ akauliza
huyo jamaa.
‘Mawasiliano nao mpaka niwapigie mimi simu, na ukiwapigia
simu, inakuwa kama unawakera…..na wale wawili ambo nilijua ni majemba ya
familia, wameoa wazungu, …na unakumbuka walipofika mwaka jana hapa, hawakutaka
kabisa kukaka kwao, wamefikia hotelini, na kuondokea huko huko…haya na hawa
mabinti zangu wawili, ….’akatulia kidogo akionyesha kusikitika.
‘Kwani wamemaliza kusoma, si uliniambia bado wapo chuo kikuu…huko
ulaya?’ akauliza.
‘Wameshamaliza na wamepata kazi huko huko Ulaya, na wao sio
wale mabinti ninaowafahamu tena….wao wanasisitiza kuwa mimi ninaendekeza nyumba
ndogo, simjali mama yao..na kwahiyo na wao hawatakuwa upande wangu….’akasema.
‘Sikiliza mwenzagu kwa mtaji huo, nakushauri, nenda kwa mkeo
ukampgie magoti, maana kuna leo na kesho, utaumwa humu ndani ukose wa kukupa
maji….hasa kwa maisha yetu tunayoishi….ambayo ndugu ambao wanahisi hizi mali
tumeziapata kirahisi na wanakuja kuchuma, utafikiri matunda yamejiotea…hawataweza
kukusaidia pindi hali ikija kuwa mbaya….unaweza ukawa mgonjwa….’akasema huyo jamaa
yake.
‘Ninakwenda kumpigia mgoti kwa lipi..hebu nielewe, mimi
sijamfukuza, na wala sijamfanyia kosa lolote, nilichojaribu ni kudhibiti
matumizi yake,…yeye anapenda kutumia pesa bila mpangilio, sherehe kila muda,
yeye kiguu na njia na shughuli zisizoisha…., hivi kweli kwa maisha kama hayo
tunaweza kusonga mbele..hapana, mimi siweze kwenda kumpigia magoti..’akasema
huyo mzee.
‘Hilo sitaweza kukushauri zaidi, najua itafikia muda
utakwenda tu,..maana kukaa peke yako ndani ya jumba la kifahari kama hili haina
raha yoyote..basi kama umeamua hivyo….tafuta nyumba ndogo nyingine iwe
inakuondoa mawazo…au nikusaidie kutafuta….’akamshauri .
‘Nimeshakuwa mzee bwana,…nyumba ndogo, …nitapata wapi ambaye
atanikubali na uzee huu, …san asana nyumba ndogo itaishia kunipeleka kaburini
muda sio wangu,…’akasema na wakawa wanacheka..
‘Haya niambie kuhusu mazungumzo yale ya mwanzoni kuhusu huyo
mwanamke..’akasema.
‘Nani…?’ akauliza huyo jamaa.
‘Wewe mwanzoni ulikuwa unataka kunielezea kuhusu nini?’
akauliza huyo mzee.
‘Ohh, kuhusu Malikia wa Mererani..ngoja nikae vyema….halafu
nikuulize, nasikia huyo mjomba wako alipokuwa huko Dar, aliwahi kumpata mrembo
mwingine….nasikia huyo ni mrembo kweli…na ana tabia njema…., unamfahamu?’
akauliza huyo jamaa.
‘Hata ...nitamfahamu vipi, wakati nasikia anaishi huko Dar…’akasema
‘Mimi nimemfahamu kwa jina , sijamjua vyema, ni nani na anatokea wapi, ila jina lake anaitwa Maua…ni Maua kweli…..
*********
‘…Maana kukaa peke
yako ndani ya jumba la kifahari kama hili haina raha yoyote..basi tafuta nyumba
ndogo nyingine iwe inakuondoa mawazo’ Mawazo hayo yalitinga kichwani
haraka, pale alipoona mwanamke akifungua mlango, na pale alipothibitisha kuwa
huyo aliyeingia sio yule mwanamke ambaye keshagundua mengi kuhusiana ma maisha
yake.
‘Wewe ni nani, na kwanini unaingia bila hodi,….’akajitahidi
kufumbua macho na kuangalia vyema, na macho yake yalipomuona vyema yule
mwanamke,… hata zile nguvu za dawa zikapungua na akaweza kujitutumua na kuinua
kichwa kidogo.
Akili, ushaiwishi wa nafsi ukauteka ubongo wake, na
akajikuta akimuwaza mkewe..kwanza akili ilimkumbuka mkewe, lakini baadaye akili
ikatekwa an yumba ndogo yake…na kila alipojaribu kuyaondoa hayo mawazo
hakuweza, alichokiona mbele…na kitu kilichougusa moyo wake, akajikuta akipitisha
ulimi mdomoni, na akameza mate kulainisha koo, akajitutumua na kukaa vyema,
sasa macho yakafunguka japo kwa shida na kumuona huyo mwanamke aliyeingia.
Kwanza kutokana na mchanganyiko wa nguvu za dawa, na mawazo
yaliyokuwa yakiuteka ubongo wake, akili yake ilishindwa kufikiri kwa muda,
akajikuta akiweweseka mdomoni, akishindwa aseme nini, na baadaye akaweza
kutamka maneno haya..
‘Wewe ndiye mwanamke uliyetumwa na rafiki yangu…nashukuru
sana …maana…’akahisi uzito wa macho ukimjia tena.
‘Samahani sana mzee wangu, nimeambiwa na docta kuwa nisikusumbue
kwa vile umeshakunywa dawa, lakini nikamuomba nije nikuona tu, hata kama upo
usingizi ili niijue sura yako, ili kama nikikutana na wewe baadaye niweze
kukufahamu…’akasema huyo mwanadada.
‘Njoo ukae hapa pembenii ya kitanda, ili niweze kuisikia
sauti yako vyema, ….maana ukiongea kwa mbali, nahisi kama sauti nyingi, ….wimbo
mzuri…oh, kama wewe ndiye aliyekuchagua rafiki yangu uje, ….basi kafanya kazi
nzuri sana…namshukuru sana, unafaa kabisa kuwa na mimi..usiogope,njoo ukae…’akasema
huku akijaribu kuzuia ile hali ya usingizi.
Maua hakuelewa huyo mzee ana maana gani, yeye alijua kuwa
huenda huyo mzee, anazungumzia kuhusu Tajiri, kuwa huenda keshamtambulisha,
kwake, kwahiyo amerizika na kwa jinsi alivyomuona,
Maua kabla hajasogea pale kitandani akawa anahisi joto,
akaona ni vyema aondoe ile khanga aliyokuwa kajitanda….
Mzee akamtupia jicho,…na nguvu ya jabu, ikamjia, nguvu ya
dawa ikawa imepungua kwa kiasi kikubwa kwenye akili yake, akajiinua na kukaa
vyema kitandani, ..akabakia kumwangali yule mwanamke,
‘Oh…kumbe sio mwanamke,
ni mwanadada mrembo…’akatabsamu huku akiendelea kumwangalia, na wakati huo Maua
alikuwa akiikunja ile khanga yake na kuiweka kwenye meza….
‘Kweli rafiki yangu anajua kunichagulia..mtu anayenifaa…huyu
atanifaa sana, japokuwa simfahamu vyema, lakini kaweza kuiteka nfasi yangu kwa
muda mfupi, sijui atanikubali na uzee wangu huu, hata akikubali japokuwa
kunihudumia inatosha tu,…na kama ikiwezekana, sitapoteza muda, mimi nitamuoa,
kwa gharama yoyote ile…’akawa anawaza akilini mwake.
‘Mzee wangu naona nisikusumbue, kwani unahitajika kupumzika,
ili dawa ifanye kazi…na samahanii sana kwa jinsi nilivyokuja bila taarifa , na
bila hodi,…sikukusudia kuja kukusumbua…’akasema huyo mwanamke.
‘Ungelijua kwa jinsi gani ninavyojiskia sasa hivi,
usingelisema hayo..sasa hivi najiona mtu mpya,…kama vile wewe ndiye dawa, kuja
kwako, imekuwa tiba…jinsi nilivyokuwa nikijiskia sasa hivi sijisikii tena, na
cha ajabu hata nguvu za dawa zimekwisha,…ajabu kabisa..kweli rafiki yangu ananijali…haya
kwanza nipe maji nilainishe koo, maana hizi dawa zinakausha koo kweli kweli…’akasema
Maua akageuka upande wa pili akaona gilasi na jagi la maji,
akachukua ile gilasi, na kuchukua kitambaa cheupe kilichokuwepo, akaifuta ile
gialsi vyema, akamimina maji, na kumsogelea yule mzee..na kila hatua aliyokuwa
akiifanya, yule mzee alikuwa akiifuatilia na kujiskia raha ya ajabu.
‘Nakushukuru sana mungu….hatimaye nimepata tiba…’akajikuta
akisema.
Maua akamsogelea yule mzee, huku akishangaa na kauli hiyi,
hakujali,..akasogea na gilasi ikiwa mkononi, na sasa akawa ananyosha mkono
kumkabidhi yule mzee gilasi iliyokuwa imejaa maji, yule mzee, akajaribu kuinua
mkono, mkono wake,ukawa kama unatetemeka….na yule mwanamke alipoona hivyo,
akakaa kwenye kitanda, na kumsogelea yule mzee, ili aweze kumnywesha…..
Mara ghafla mlango ukafunguliwa…na mwanamke mfanyakazi wa
humo ndani akaingia…akionekana kuwa na wasiwasi..kwanza ilionekana kuwa hajui
kuwa kuna mtu zaidi ya yule mzee, kwahiyo alikuwa kama hana habari na zaidi ya
kuangalia huku na huku kuona kuwa kunahitajika chchote cha kufanya, lakini…alipotupa
macho pale kwenye lile sofa ambalo lipo kama kitandani….akamuona yule mwanamke
akiwa karibu kumywesha maji yule mzee….akashikwa na mshituko….
Kwani aliinua mikono na kushika mdomo, kama anataka kupiga
yowe…, lakini sauti haikutoka, akaona haitoshi…akakimbilia pale walipokaa hawa
watu wawili na kwa haraka akapiga ile gilasi iliyokuwa karibu na mdomo wa yule
mzee, na yale maji yakamwangaika, kwenye
lile sofa….
‘Ooooh, ninii wewe unafanya nini……’ akasema yule mzee,
akijitutumua kuinuka kuyakwepa yake maji yaimlowanishe…
‘Usinywe hayo maji yana sumu…’akasema yule mwanamke
mfanyakazi wa humo.
NB: Niendelee nisiendelee………….
WAZO LA LEO:
Uhalisia wa kibinadamu upo, na hata kama tutajitahidi vipi kuuondoa, bado
mwisho wa siku tutaishia kujiumiza wenyewe…japokuwa wapo waliojaliwa kuwa na uwezo
wa huo wa kuhimili, na kudhibiti nafsi zao lakini walio wengi hawana uwezo huo.Upendo wa kweli hasa, NDOA-
kuishi mke na mume ni moja ya uhalisia huo, wazo langu la leo ni kuwashauri -kwa wale waliojaliwa, ni vyema
tukaingia kwenye ndoa.
1 comment :
Emu-three,kila nikijaribu kupitia blogu yako huwa najiuliza swali moja je unapata wapi muda wa kuandika hizi simulizi? kwa maana wewe kama binadamu mwingine lazima unapaswa kuwa na majukumu kama vile kazi,familia na mambo mengine ya jamii. Je unao mpango wowote wa kuandika series ya vitabu vya simulizi zako hizi toka mwanzo hadi mwisho?
Post a Comment