Maua alifuata njia aliyoelekezwa, na alijaribu kuwa mwangalifu
asigundulikane kuwa yeye ni nani na anapokwenda ni wapi, na kila mara akili
yake ilitekwa na kauli za kejeli za yule mwanadada;
‘Hahahahaha…huoni hata
aibu, ..ninajua yote, na bahati nzuri, nilipata ushahidi, ….nikaona, jinsi
ulivyokuwa ukifanya, ulivyo kuwa ukitingisha, unavua nguo mbele ya wanaume,
wanakushika shika huku na kule….ni aibu mtoto wa kijijini kwetu kufanya uchafu
kama huo, ….
Maneno hayo kila yakimjia akilini, alijiona akipandwa na
hasira, na hapo alitakiwa kutuliza kichwa na kuifukuza hiyo hali, kwani
alishaambiwa ili aweze kuishinda hiyo hali, ahakikishe anaidhibiti hasira yake,
na kukiwazia kitu kwa muda mrefu….
‘Oh, ….kwanini nashindwa kuvumilia…’akawa anajilaumu pale
kichwa kilipoanza kumuuma, akatafuta sehemu akasimama kwa muda huku akijaribu
kutuliza akili, na alipoona hali haitulii, akaona ni bora ajipake yale mafuta yake
haraka, ..akatoa kile kichupa na kuyanusa yale mafuta puani,….kichwa kikawa
kama kimemwagiwa maji ya baridi, …akawa kama hana chocna baadaye akili ikatulia
na hote kichwani, na karibu ashikwe na usingizi….
‘Hapana nina haraka sitakiwi kulala hapa….’akasema na kuendelea
na safari yake.
Alipofika mitaa hiyo waliyoelekezwa, mitaa ambayo kuna nyumba
kubwa kubwa za kifahari, huku akili yake ikijaribu kukumbuka yale maelekezo
waliyopewa,..
‘Ukifika hapo, angalia mitaa yenye maduka mengi,…kwenye
barabara kuu ya mabasi, angali kulia kwako, kuna nyumba moja ipo tofauti, wa
jinsi ilivyopakwa rangi, imapakwa fito mbili za njano na kijani, unaweza kuiona
kwambali, ukiikaribia huwezei kuona kwa ndani tena kwani vile imezungushiwa
ukuta mkubwa,….ukifika hapo gonga kengele, …’huyo jamaa yao akawa anawaelekeza.
‘Kuna walinzi?’ akauliza mama mdogo.
‘Ndio wapo, tajiri kama huyo, asiwe na mlinzi,…japokuwa
kawapunguza, lakini kwa sasa yupo mlinzi mmoja tu…..muda wote analala, hana cha
kufanya…’akasema huyo jamaa yao.
‘Hawezi kutuzuia kuingia…..?’ wakauliza.
‘Hapo ni akili yenu wenyewe….maana mimi sina mazoea na hawo
watu, …nilimuuliza jamaa mmoja aliwahi kufanya akzi humo, amesema ukifika hapo,
unachotakiwa kusema ni kuwa wewe ni mfanyakazi wa Tajiri, umeleta mzigo wake,….’akatulia
akiwaza jambo.
‘Na kwa vila nyie ni akina mama,…na inategemea
mtaavyovaa..mvae kiheshima, ili msitiliwe mashaka,…nina imani atawaruhusu tu kuingia,
na ukishaingia ndani, nenda kwa haraka hadi kwenye jengo, na ukigonga mlango
unaweza kukutana na dakitari anayemuuguza huyo mzee, kwasababu nilisikia hali
ya huyo mzee ilikuwa mbaya….’akatulia tena.
‘Kama hayupo huyo dakitari, utawakuta wafanyakazi wa ndani
wao hawana lolote la kumzuia mtu…wewe ingia na unapoingia ndani ya hiyo nyumba,
utajikuta kwenye ukumbi, kuna viti vya kifahari, maua, mapambo, ukiwa mgeni
unaweza kuzubaa kuangalia jinis kulivyopendeza…’akageuka huku na huku kama
anaangalia.
‘Wewe si umesema hujawahi kufika humo ndani…?’ akauliza
Maua.
‘Hayo ni ya kuhadithiwa na huyo mlinzi aliyewahi kufanya
kazi humo, anasema kuna pendeza sana, sasa kushoto, kuna varanda, inakwenda mbele,….unaifuata
hadi mwisho wake, ambapo, utakuta mlango wa kushoto na kulia…fungua mlango wa
kulia….sijui hapo mnanielewa…?’ akasema huyo jamaa.
‘Tunakuelewa…muhimu ni kuingi ndani…’akasema Maua.
‘Sawa….huo mlngo wa kulia, ukifungua unajikuta tena kwenye
ukumbi, sio mkubwa sana…lakini nasikia hapo ndio kamaliza kila kitu , utafikiri
upo peponi..na mara nyingi huyo mzee anajipumzisha hapo, kuna sofa lake kubwa …lipo
kama bembea, karibu yake kuna bwawa…baridiii, na ndege wanaruka huku na kule,…samaki…yaani
we acha tu….’akasema huyu jamaa utafikiri aliwahi kufika humo ndani.
‘Hana mke?’ akauliza Maua
‘Mke wake walikorofishana akarudi kwao,….hawa matajiri wana
mambo wewe, unaweza ukawaona mitaani au mabarabarani na mgari yao ya kifahari, ukafikiri
wana raha,..sio wote wenye bahati kama hiyo, yeye na mkewe walikuwa wakiishi
kama paka na chui,hawana maelewano kabisa…wanawake wengine hawana maana, maana
pale mungu akupe nini, lakini nasikia alikuwa hatosheki….kila mara sherehe,
mara anataka kusafiri nje ya nchi…yaani alikuwa akimuendesha puta huyo mzee, ….hadi
basi….’aksema huyo jamaa yao ambaye aliombwa kuwasaidia.
‘Kwahiyo kumbe, huwezi kuzuiwa kuingia, au hawo wafanyakazi
hawawezi kumzuia mtu asionane na huyo mzee na watoto wake je, kwani hana watoto,…?’
akauliza.
‘Mara nyingi hakuna anayefika fika humo,…kutokana na tabia
zao za kujiona,… na kebehi zao, wao wanadai wanaishi kizungu, na kwahiyo maisha
yao ni ya upweke, …maana kama hutembelewi na ndugu, au jamaa zako, na eti ukitaka
kwenda kwake mpaka uwe na ahadi naye, ni maisha gani hayo kama sio upweke,….’akawa
kama anauliza.
‘Mungu sasa anamueleleza, watoto wote wapo ulaya, wanaishi
huko, hawataki hata kurudi, japokuwa wamesikia baba yao anaumwa, kisa, kwa vile
haishi vyema na mama yao…’akasema huyo jamaa.
‘Sasa unaona, hivi sasa anaumwa,…ndugu na jamaa hawana
habari naye, kwani wanadai kuwa huyo jamaa alipokuwa mzima alikuwa hajali ndugu
zake au jamaa….yeye alimjali mke wake, na watoto wake tu, kwahiyo awaite watoto
wake, waje wamsaidie…’
‘Kwahiyo kwasasa ninani anayemuuguza?’ akauliza mama mdogo.
‘Ni huyu mwanamke aliyepagawa, na mjomba wake,….yaani huyo
anayeitwa Tajiri, ….na hata hivyo huyo mwanamke, nasikia hana kauli nzuri na
huyo mzee, hawaelewani, ….nasikia huyo mwanamke, anajipendekeza tu kwa huyo
mzee, kujifanya anajali na kumuuguza, na anafanya hivyo ili tu apate mali, ili
arithi mali ya huyo mzee, na zaidi alikuwa akishinikiza aolewe na huyo
anayeitwa Tajiri…’akasema
‘Kwani huyo Tajiri sio ndio jina lake?’ akauliza Maua.
‘Ndivyo tunavyomjua hivyo kwa jina hilo, huenda ana jina
jingine, lakini wengi tunamfahamu kwa jina hilo…la Tajiri, …nilimuuliza huyo
mlinzi swali kama hilo akasema hata yeye hajui jina jingine….’akasema huyo
jamaa yao.
‘Mimi nitaenda ….nina hamu sana ya kuonana na huyo mzee, …’akasema
mama mdogo.
‘Hapana mama nitaenda mimi,kwa vile yote haya yananihusu
mimi, na wewe ubakie hapa, ili wajue kuwa bado tupo humu ndani, na hata huyo
Tajiri akija akukute humu ndani’akasema
Maua.
‘Acha mimi niende, nahisi huyo mzee ana pesa nyingi…lazima
nikamtoe pesa kidogo…na huyo ni mzee, anahitaji kuonana na watu wazima,
wanaojua taratibu ….na wewe huwezi kumtoa pesa,….’akasema mama mdogo.
‘Hapana mama ..huyo anahitaji kuonana na mimi, …wewe
utabakia hapa, najua ukienda huko utakwenda kudai pesa, na kuleta aibu tu….mama
hiyo tabia sio tabia njema watu wanatufikiri vibaya, ….’akalalamika Maua.
‘Wewe bado mdogo, kula kulalatu…..hujui tukirudi bongo,
tunahitajiwa kodi ya nyumba..tunahitaji kuendeleza ile biashara yetu,kwa hivi
sasa mtaji umeguduka,….unafikiria pesa tutapata wapi, kama sikutumia ujanja
ujanja….’akasema mama mdogo.
‘Mimi hayo maisha siyawezi….huko kwa huyo mzee, nitakwenda
mwenyewe, wewe bakia humu..’akasema Maua.
‘Tuahidiane, kuwa ukienda huko utakuja na pesa, na zote
utanikabidhi mimi, kama ukikubali hilo, mimi sina shida….’akasema mama mdogo, akiigiza
laafudhi za huko.
‘Mimi siendi kutafuta pesa, siendi kufanya kazi huko…utapataje
pesa bila kuzifanyia kazi’akasema Maua.
‘Kwani unakwenda kufanya kazi au unachohitajiwa ni kutumia
akili kidogo, wakati mwingine inabidi ufanye hivyo kwasababu utajiri wao
mwingine umepitia kwenye migongo yetu, na walistahili wakipata huo utajiri,
watuinue na sisi angalu kidogo, lakini hawataki…,’akasema mama mdogo.
‘Hayo ni mawazo yako..’akasema Maua.
‘Hivi wewe utajifunza lini akili ya kutafuta pesa…hakikisha
ukija hapa una pesa…’akasema mama mdogo kwa hasira.
Maua alimwangalia mama yake mdogo kwa macho ya kutommaliza, akachukua khanga moja na kujifunga kiunoni na
nyingine, akajitanda kichwani na kubakiwa na sehemu ndogo ya uso, alionekana
kama akina mama wa maeneo ya huko, ….na alipomwangalia mama yake mdogo, mama
yake mdogo akamnyoshea kidole cha gumba, kumpongeza;
‘Hapo umefanya itakiwavyo, ole wako uvurunde, halafu uje
bila pesa...’ Mama mdogo akasema , Maua hakusema kitu, akatoka na kuanza
kufuatilia njia kama wavyoelekezwa.
NB: Muda umewisha tukijaliwa tena kesho
WAZO LA LEO: Raha,
shida, huzuni, upweke, yote ni majaliwa ya
mwanadamu. Sio matajiri wote wana raka, kama tunavyofikiria,…. unaweza ukawa
tajiri na bado ukajikuta ukiwa huna raha, na unaweza ukawa masikini ukawa na
raha kulio hata huyo tajiri. Cha muhimu, ni kurizika, kujipa moyo, kuwa na
subira, ….na hali uliyojaliwa nayo.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment