Maua na mama yake, walibakia wameduwaa, kwani kwa
makubaliano yao na Tajiri, ilikuwa wasionane na mtu yoyote, zaidi yake;
‘Nawataka mkae humu ndani hadi nirudi, hakuna kutoka, na sitaki
muonane na mtu yoyote, au kumpigia simu mtu yoyote kuwa mpo kwenye hii hoteli, …mimi
tu ndiye ninayejua na hata walinzi wangu hawajui, ….mnasikia?’ akasema Tajiri.
‘Kwanini ufanye hivyo, kwani sisi ni wafungwa?’ akalalamika
Maua.
‘Nina maana yangu kubwa, ….nitakuja kuwaambia baadaye ni
kwanini, na nataka watu wajue kuwa nimeshakuona, nikishafunga ndoa, maana watu
walishanichukulia kuwa mimi siwezi kuoa tena, …kwahiyo msitoke,na wala
msimfungulie yoyote zaidi yangu, kila kitu kitaletwa humu, nimeshatoa maagizo
kwa wahudumu wa hii hoteli, wakitaka kuja kuleta huduma watawapigia simu..’akasema
Tajiri.
‘Sisi hatuna shida, ..usije ukatutelekeza humu ndani…’akasema
mama mdogo.
‘Siwezi kufanya hivyo, nilijitambulisha kwa meneja wa hii
hoteli mbele yenu, na nikalipa kial kitu mbele yenu, kwanini nifanye ubaya
huo..mimi sitarudi nyuma kwa hili, nimeamua kwa Maua atakuwa mke wangu….ingawaje
yeye hataki, …’akasema Tajiri.
‘Hajakataa bwana, siunajau sisi wanawake, lazima kwanza
turinge…..’akasema mama mdogo.
‘Mimi nimesema ni makubaliano ya kuilea hii mimba, yote
mengine ni baada ya kuonana na mama yangu, …’akasema Maua huku akionyesha
kujiskia vibaya.
‘Kapumzikeni, ….na chochote mnachohitaji agizeni, pigeni
simu hiyo hapo mezani, manabonyeza namba moja tu…`moja’….atakuitikia muhudumu,
na kukuliza nini shida yako, na atakutimizia mara moja, bili kila kitu ni juu
yangu, sawa….’akasema na kuondoka.
*******
Huyu mgeni ni nani,
na anatoka wapi…wakabakia kujiuliza akili mwao
‘Labda ametumwa na Tajiri..’akasema mama mdogo.
‘Hilo jina uliwahi kulisikia ? ‘ Maua akawa kama anauliza
huku akigonga gonga kisgino sakafuni.
‘Malikia ….nakumbuka kama nimewahi kulisikia kutoka kwa
walinzi wake..’akasema Maua.
‘Malikia wa Mererani,…hilo sio jina lake, hiyo ni sifa ya
huyo mtu, kijikweza…., acha aje, tutapambana naye, awe malikia sisi tutakuwa
wafalme..’akasema mama mdogo, na kabla hajamaliza mlango ukagongwa, na hata
kabla hawajasema karibu mlango ukafunguliwa…
‘Ina maana hukufunga na ufunguo…’akasema mama mdogo
akionyesha mshangao
‘Mbona nilifunga na ufunguo…’akasema Maua naye akiwa kaduwaa
kwa mshangao.
‘Msiwe na wasiwasi, nimefungua mimi mwenyewe….’akasema
mwanadada mmoja akiwa kasimama kati kati ya mlango, huku akiwa kainua ufunguo
juu, kuonyesha kuwa , yeye ndiye aliyefungua huo mlango.
‘Sasa ni utaratibu gani huo, wa kuingia kwenye vyumba vya
watu, bila idhini yao,….hio sio taratibu nzuri, na tutalalamika kwenye utawala
wa hii hoteli, kwanini wanatufanyia hivyo…..’akasema mama mdogo.
‘Utawala ndio mimi…kama ni kulalamika ulalamike kwangu,….ni
kweli sio taratibu njema kuingia kama nilivyoingia mimi, lakini kuna sababu za
msingi, na hazina haja ya nyie kuzifahamu, kwanza nauliza Maua ndio nani?’
akauliza huku akiwaangalia mmoja mmoja.
Mama mdogo na binti yake, wakawa wanaangaliana, na kila
mmoja akimtegea mwenzake ajibu yeye, na kabla hawajafungua midomo yao, yule
mwanadada akaingia ndani na kurudishia mlango, akawasogelea na kuanza kuwakagua
kama vile mwalimu anavyowakagua watoto, usafi kwa uangalia kuanzia nywele hadi
miguuni,…hakuwagusa, alikuwa akiwakagua kwa macho.
‘Sikilizeni, kwa kuwaangalia tu, nimegundua kitu….mimi
nimeishi na watu wengi, na nikikutana na mtu kwa mara ya kwanza tu, ninaweza
kumjua udhaifu wake, na nyie, nimeshawajua udhaifu wenu, hasa wewe mama…sasa
sikilizeni,…’akasema huku akifungua pochi lake.
‘Pesa hizi hapa, najua mna shida ya pesa, hizi hapa, ni pesa
zitakazowatosha kwa nauli, na mtaji wa biashara zenu, …najua kabisa huko Dar,
mlikuwa na vibiashara vyenu, na mnahitaji mtaji wa kuviendeleza, ..mimi
najitolea, ..’akawa kazishika zile pesa mkono akizichezesha chezesha….na mama
mdogo akawa anaziangalia huku akizifuatilia kwa macho, jinsi zinavyoshushwa na
kupandishwa.
‘Nani kakuambia tunahitaji nauli?’ akauliza Maua huku akiwa
haziangalii zile pesa, …alikuwa moja kwa moja anatizamana uso kwa uso na huyo
mwanadada.
‘Ndio wewe eeh, …eti unaitwa Maua,…toka lini msichana kama
wewe ukaitwa Maua, ..hukustahili kupewa jina kama hilo….’akamsogelea na
kunyosha mkono wake, hadi kwenye shavu la Maua, na akaanza kupitisha kidole
kwenye shavu la Maua , na Maua alipoona hivyo akainua mkono wake na kukisukuma
hicho kidole pembeni.
‘Hilo halikuhusu, niitwe Maua, au niitwe nani, haikuhusu,
kama isivyo nihusu kwa wewe kuitwa Malikia, wakati huna hadhi ya huo umalikia…eti
Malikia wa Mererani’akasema Maua bila kujali, na mama yake akamgeukia, na
baadaye akaziangalia zile pesa zilizopo mkononi mwa huyo mwanadada.
‘Maua, mimi sikuja hapa kwa shari,…kama ningekuja kwa hivyo,
nisingeliingia humu ndani peke yangu, huwa sihangaiki kutumia mikono yangu,
kwani wapo watu wanaishi, na kulipwa kwa kazi hiyo…nimekuja kwa nia njema,
labda kwanza nijitambulishe kwenu, kwani nyie naona ni wakuja, hamnijua vyema
kuwa mimi ni nani…’akatoa kadi yenye picha yake,..
‘Hii hapa ni kadi yangu, inaonyesha kuwa mimi ni mkurugenzi
wa kampuni kubwa ya madini..kule Mererani, na zaidi ya hapo, wakazi, wa eno
hili wamenitunuku, na kunipa cheo cha umalikia,..kwa uzuri , urembo,
utanashati..haiba,….na kila unalilowazia kwa msichana mrembo, ninalo mimi,
…hebu jiangalie wewe, na mimi, hivi kweli tunaweza kukaa meza moja
kushindanishwa…ndio maana ya jina hilo sikujipa mwenyewe….’akawa anamwangalia
Maua kwa dharau.
‘Kwanza kwani hayo yote yametoka wapi?’ akauliza Maua, huku
akikunja uso wa kushangaa na hasira.
‘Wewe na huyo sijui ni nani wako, mnajua kwanini naongea
hivyo…na kama huoni umuhimu wa haya ninayoongea basi, ili kuepusha shari, na
kwa manufaa yako chukua pesa hizo, muondoke, rudini huko Bongo, mkauze mama
ntilie yenu, au ….maandazi,….’akawa kama anainua mikono na kujishika kifuani,
kama kuomba….’ Halafu akazirusha zile pesa mbele yao, zikatua miguuni kwa Maua
na Maua akainua mgu wake, na kusimama pembeni
‘Hayo ni maisha yetu hayakuhusu….na hatuajsema tunahitaji
pesa zako, ….na kwa kazi gani tuliyo kufanyia, …au wewe una udugu gani na sisi…chukua
pesa zako na rudi huko ulipotoka…’akasema Maua huku akisukuma kwa mguu zile
pesa zielekee aliposimama Malikia.
‘Ndio ni maisha yenu sio….?’ Akasema Malikia akitabasamu
kinafiki, huku akitembea huku na kule.
‘Ndio maisha yenu, ya kuchukua mabwana wa watu,…mnajiremba muonekanae kama wazungu, au sio,.ndio tabia
yenu, ya kutafuta pesa kwa kujiuza, mnafikiri mimi siwajui,….nina ushahidi
mkubwa sana, lakini sihitaji kufika huko, kwani hayo mliyo nayo ni makubwa
sana,..nawashauri tena kwa moy mkunjufu, rudini huko mliko toka,…na kama
ikiwezekana, msirudi kabisa…’akasema huku akitembea hatua ndogo ndogo kuondoka.
‘Chukua pesa zako ondoka nazo, kwani hatuzihitaji, na kwa
taarifa yako, hakuna mtu hapa aliyechukua bwana wa mtu, huyo unayesema ni bwana
wako, alikuja mwenyewe huko Dar, na kuni…..baka, ninaweza kusema hivyo, maana
alitenda tendo hilo bila ya rizaa yangu….’
‘Hahahahaha…huoni hata aibu, ..ninajua yote, na bahati
nzuri, nilipata ushahidi, ….nikaona, jinsi ulivyokuwa ukifanya, ulivyo kuwa ukitingisha,
unavua nguo mbele ya wanaume, wanakushika shika huku na kule….ni aibu mtoto wa
kijijini kwetu kufanya uchafu kama huo….mimi nilimshauri, huyo bwana, aziharibi
hizo kanda za video haraka, natumai amefanya hivyo….’akatulia pale alipomuona
Maua akitetemeka.
Mama mdogo alipoona hivyo, akafungua mkoba wake na kutafuta
kichupa, lakini hakukiweza kukipata kwa haraka,…Maua akabadilika, na kuanza
kutetemeka,…akaanza kunguruma kama simba, na sauti iliyotoka hapo, ilimfanya
hata mama Mdogo, adondoshe ule mkoba na kugeuka kutaka kukimbia….
‘Wewe mwanamke unakimbia wapi, ….unamuachia nani huyu
shetani wako…’akasema Malikia, huku akiuchukua ule mkoba wa mama mdogo, na
kumimina kila kitu kilichokuwepo mle ndani, na kile kichupa kikadondoka
‘Hii ndio dawa yake?’ akauliza Malikia huku akiwa na
wasiwasi, kwani wakati huo Maua alishamfiki,a na alipomuangalia machoni,
akajikuta akitoa jicho la uwoga….
‘Ndio mnyunyuzie haraka hayo mafuta…’akasema mama mdogo,
akiwa keshafika mlangoni, na kabla hajamaliza kuongea, Maua alishamuwahi
Malikia, akamshika na kumuinua juu, …akamzungusha hewani, halafu aakmrudisha
chini kwa taratibu…
‘Haya niambie ni nani kakuchukulia bwana wako….?’ Sauti nzito
ya kiume, ikiwa na mkoromo ikatoka
‘Ni…..hapana….nisamehe….’Malikia akawa anaongea kwa kutetemeka,
na wakati huo, mama mdogo, alishafika na kukiokota kile kichupa, kwani kilisha
mtoka Malikia na kudondoka sakafuni,….kwa haraka akakifungua kile kichupa na
kutoa mafuta, akamwangia Maua kichwani….
Yale mafuta yalipodondokea kwenye kichwa cha Maua ilikuwa
kama mtu aliyempiga Maua kichwani na kitu kizito, kwani aliyumba na kupepesuka
na hapo hapo akadondoka chini.
Malikia akiwa bado na wasiwasi, akaangalia mlangoni, akijiandaa
kukimbia, akageuka na kumwangalia Maua pale alipolala, na baadaye akamwangalia
mama Mdogo, akasogea na kukichukua kile kichupa na kumwagaia tena Maua yale
mafuta, halafu akamrudishia Mama mdogo kichupa chake, na haraka akainua simu
yake na kuwapigia watu wake, haikuchukua muda mlango ukafunguka, wakaingia
jamaa wawili , ambao ilionyesha kuwa ni walinzi wake.
‘Nyie mlikuwa wapi, wakati huyu shetani, anataka kuniua….mwanamke
hatari kweli huyu, kama nisingelikuwa mtu wa mazoezi, angelishinda, lakini
mnaona kalala skafuni chali haniwezi kabisa mimi….hakuna shida,…’akawa
anajiweka vyema, na kujirekebisha nguo yake, ambayo ilikunja.
‘Bosi hatukusikia kelele yoyote, je kuna tatizo….?’akasema
mlinzi wake,
‘Hakuna tatizo, ….ngoja nimalizane nao, …msiondoke hapo
mlangoni, …’akasema na kuzifuata zile pesa ambazo zilikuwa bado pale chini, na
kwa muda huo mama mdogo alikuwa naye anazifuata.
‘We mwanamke, najua unapenda sana pesa…wewe ni mroho mkubwa
wa pesa, sasa sikiliza, kweli hizi pesa nitakuachia, …lakini …narudia tena,
lakini,….ikifika jioni nisiwaone, hapa, …kuna usafiri wa muda huu, nendeni
mkakate tiketi, muondoke haraka….vinginevyo, sijui,….’akawa anaanza kuondoka,
lakini baadaye akageuka kumwangalia Maua.
‘Lakini mbona tumeshaelewana na Tajiri, kuwa atakuja na
tutamalizana….’akaanza kulalamika mama mdogo.
‘Nikuuliza kitu, hizo pesa umezichukua kwa kazi gani,
umefanya nini mpaka nikulipe pesa nyingi kiasi hicho….wewe mama, tamaa yako
itakupoza, ….ifanyie kazi hiyo pesa..’akamgeukia Maua ambaye ilionyesha anajitingisha
kuonyesha kuwa kazindukana.
‘Ninawashauri kwa nia
njema, rudini huko mlikotoka, ..ni kwa manufaa yenu, …nawashauri kwa nia njema
kwa vile tunatoka kijiji kimoja, ….vinginevyo, nisingelihangaika, ningelijua ni
nini cha kufanya,…’akasema Malikia.
‘Tutaondoka pindi tukionana na Tajiri…’akasema mama mdogo
huku akizifutika zile pesa kwenye pochi yake, na Malikia akawa anamuangalai kwa
dharau.
‘Nina imani kuwa Tajiri hana uwezo wa kuwasaidia kwa hilo…na
mjomba wake anaumwa sana, ndio maana kashindwa kufika hapa, ….na yote hayo ni
sababau ya pesa, ..hizo pesa unazozifutika kwenye kipochi chako ,….zitakutokea
puani….narudia tena kwa manufaa yenu,
ondokeni rudini huko mlipotoka, msije mkajijutia…’akawa keshafika mlangoni.
‘Hatuwezi kuondoka mpaka kieleweke, isingelikuwa huo uja
uzito, tusingelijali..tungeliondoka na wala tuisngelifika huku….’akasema mama
mdogo, na Malikia akawa kama kashikwa na umeme, akageuka mzima mzima
kuwaangalia wanawake hawo wawili,….akasema kwa kushangaa.
‘Whaaat….unasema
nini, uja uzito, ni nani kampa mimba nani?’ akauliza kwa ukali.
‘Nilifikiri unafahamu….’akasema mama mdogo.
‘Huyu unayesema ni bwana wako, ndiye aliyenipa mimi ujauzito
baada ya kunibaka, najua hizo kanda za video zitawadanganya, lakini kiukweli,
hayo yote yalifanyika bila ya rizaa, yangu, nahisi walininywesha dawa, za
kunipumbaza…mungu mwenyewe ndiye anajua hayo…na ipo siku mtalipwa kwa matendo hizo
zambi zenu…najua huenda na wewe upo nyuma ya hilo…’Sauti ya kinyonge ikatoka
kwa Maua.
‘Siamini…….haiwezekani..’malikia akawa anaongea huku
akimwangalia Maua kwa mashaka, na akawatizama walinzi wake kuhakikisha kuwa
wapo karibu, akamgeukia Maua na kusema;
‘Tafadhali nendeni mkaitoe hiyo mimba haraka….chonde chonde,….nendeni
haraka…’akasema Malikia akiwa kashika mshavu kwa viganja vyake viwlili huku na
huku, kama vile anajipima homa.
‘Kama tungelitaka kuitoa hiyo mimba tungelishafanya hivyo
huko tulipotoka, lakini Tajiri kaiukubali na yupo tayari kumuoa binti yangu
ndio maana tupo safari moja kwenda kutimiza ahadi yake, kwanza tumefurahi
kusikia kuwa mjomba wake yupo hapa…’akasema mama mdogo.
‘Eti nini….kumuoa binti yako…nyie watu mna wazimu kweli….hiyo
ni ndoto, mnanifahamu mimi ni nani,…mnanifahamu mimi ni nani kwake…..’akawa
kainua kidole kilichovalishwa pete.
‘Nawaambia ukweli, hilo halitatokea hivyo abadani, ….nasema
haitatokea hivyo, labda mimi malikia wa Mererani niwe maiti….na nawahakikishia kuwa sitatumia
nguvu, ..ila wenyewe mtaona,….kama mimi sio Malikia wa Mererani , hiyo ndoa
itafungwa, ….’akafungua mlango na kutoka nje.
‘Tutaona…..na mimi kama sio Maua binti Maua, ndoa hiyo
haitafungwa…’akasema Maua akiinuka
‘Hahaha…na mimi kama sio mama yako mdogo…ndoa hiyo
haitafungwa…’akasema huku akiinua pochi lake , kufurahia pesa alizopewa.
‘Mjini hapa, …’akasema mama mdogo, akihakikisha kuwa zile
pesa zipo mahali pake.
‘Mama rudisha hizo pesa za watu, …..’akasema Maua alipomuona
mama yake mdogo, akiziweka zile pesa vyema kwenye mkoba wake huku akiwa kashika kichwa akiwa kama anawaza jambo.
‘Kiendacho kwa mganga hakirudi…sirudishi kamwe,
sikumlazimisha anipe hizo pesa, kanipa mwenyewe pesa hizo kwa mikono yake
miwili….’akasema na kukatishwa na hodi , na kabla hawajajiweka sawa, mlango
ukafunguliwa, na wakajikuta wakiangaliana uso kwa uso na polisi……
WAZO LA LEO:
Imani ya kweli ya dini, inamfanya mtu aogope kutenda dhambi wakati wowote,
akiwa na watu au akiwa peke yake. Imani hiyo hutoka moyoni, na hushadidishwa na
matendo mema. Tusitumie dini kama kichaka cha kukamilisha maovu yetu,...kumbe ndani ya mioyo yetu imejaa chuki, na ubinfasi . Tusiwe wanafiki wakujivika ngozi ya kondoo kumbe sisi ni mbwa
mwitu.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Duh! aise kisa hiki kinazidi kunoga...nashubiri kuona kama itakuwa ndoa au?
Post a Comment