`Nimeamua kuwa mbali kabisa na jamii yangu, na sipendi
kukutana na yoyote anayenifahamu, na sikuwa na jinsi ni kuja kuishi na mama
huyu mdogo kwa vile ndiye chanzo cha haya yote, vinginevyo, nisingelikuja haoa
kwake tena, …..’akaendelea kuhadithia huyu mwanadada, na wakati huu alionekana
kama anajisikia vibaya.
‘Kwangu sina ndugu, na wala sina rafiki, ndugu zangu
walinitenga, na kama walivyomfukuza mama yangu, nakumuona hafai kuishi na jamii
zao, eti kwa vile katenda dhambi kubwa, basi mimi nimetenda dhambi kubwa zaidi
ya mama, na kwahiyo sistahili kuwa karibu nao kabisa…’akaendelea kuongea kwa
uchungu.
‘Na zaidi ya hayo, sina hata rafiki, maana wale niliowaona
ni marafiki, wamekuwa ndio chanzo cha kunitumbukiza kwenye maangamizi
zaidi…..je hawa ni ,marafiki au ni maadui, huenda basi sikustahili kuishi
kwenye hii dunia…’hapo machozi yakaanza kumlenga lenga.
‘Huenda sistahili kuishi kwenye hii, dunia, na kila
nilipoliwazia hili, najikuta nikiwa na wakati mgumu, nikijiuliza je, kama ni
hivyo, nifanyeje, nijiue….mbona nilijaribu siku moja na taabu, uchungu na
maudhi niliyoyapata siku ile, niliona ni heri, kama ni kufa nisubiri siku hiyo
aliyonipangia muumba…’akatulia, na baadaye akangalia tumbo lake.
‘Lakini hata nikiamua kujiua, …je hiki kiumbe kilichopo hapa
tumboni, kina kosa gani….?’ Akajiangalia tumboni na baadaye akainua uso,halafu
akajikuna kichwa kwa muda mrefu hadi nywele zikatawanyika, kama mtu
aliyechanganyikiwa, na nilipokumbuka kuwa alisema mara kwa mara anapandisha
mshetani, nikaogopa, na kujiandaa kukimbia…
‘Hapana siwezi kujiua , kwanza lazima nione hawa
walionifanyia hivi wanapata adhabu yao,….na wao wanakutwa na machungu kama haya
yaliyonikuta mimi….wa kwanza keshaanza kuhangaika…na huyo ndiyo yule aliyejifanya
ni tajiri, …na kutumia utajiri wake, kuniharibia maisha yangu, japokuwa kwa
ujumla, amekiri kosa lake, lakini kwanini niteseke, wakati yeye yupo anafurahia
utajiri wake…..’akatulia kwa muda…
Na yeye keshaanza kuipata adhabu ….hata kama ….akatulia kwa
muda akiwaza yale yaliyotokea huko nyuma siku walipokwenda kumtembelea mama
yao, akiwa na ndoto na kuanza maisha mapya, japokuwa hakuwa kajiandaa kwa hilo,
lakini kutokana na shinikio lililokuwa juu ya uwezo wake, alikubali kuingia
kwenye maisha hayo…ya kuwa mke wa mtu……japokuwa haikufanikiwa, ni kwanini haikufanikiwa,
…..
************
‘Inabidi tupitie Arusha, maana huko nina biashara zangu,
vinginevyo, itabidi nyie muende huko kwenu na mimi nitawakuta huko huko kwenu..’akasema
Tajiri.
‘Haiwezekani, sisi tunakwenda pamoja wewe na sisi mguu kwa
mguu hadi kwa mama, na tukitoka huko tutakwenda huko kwenye biashara zako,
maana baada ya hapo, nitakuwa nimehalalishwa …..’akasema Maua, huku akisita
sita kutamka hicho alichokusudia kukisema.
‘Hilo halitawezekana,
….mimi nina mpangilio wangu wa maisha na ninajua kwanini nafanya hivyo..maisha
yangu yamegubikwa na maadui,….kuna watu hawapendi niwe hivi…kuna watu hawataki
niwe tajiri…., wananionea kijicho, nahitajika kuwa makini na watu kama hawo…..’akasema
na kuangalia saa yake.
‘Kwanini uwe na maadui….kiasi hicho, inaonyesha kuwa wewe
sio mtu mwema, na huo utajiri wako hukuupata kwa halali?’ Akauliza Maua, na
yule Tajiri akacheka kwa dharau.
‘Kwa halali..?’ akarudia hayo maneno huku akizidi kucheka,
halafu akatulia na kumwangalia Maua kwa macho ya kupepesa, kama vile
anamchunguza ndani ya akili yake, halafu akasema;
‘Usione watu ni mtajiri…ukafikiria kuwa utajiri wao umekuja
kirahisi,…kuna mambo yamefanyika,….na nikuambie ukweli ukitaka upate utajiri wa
kihalali, hutafanikiwa kamwe….na hata hivyo sijui una maana gani kusema
`kihalali’ maana dunia hii ilivyo, mambo mengo sio ya halali, hasa yanapofikia
kutafuta mali,…ili upate jambo, hasa mali na utajiri kuna dhambi nyingi
zinatendeka…’akatulia na kuangalia juu.
‘Sio lazima utende dhambi, ndio upate ,mali au utajiri, hizo
ni hulka zenu, nyie watu mnaopenda kutenda dhambi…kwani hakuna njia za halali
za kupata mali, zipo, ila kwa vile nyie ni mawakala wa shetani, basi mnaona
njia rahisi ni hiyo hiyo ya kishetani…’ akasema huku mama yake mdogo akimfinya
lakini hakujali .
‘Na baya zaidi, mnatafuta mali hizo kwa kuwadhulumu
wanyonge, ndio maana hamuishi kwa amani..nje na ndani…’akasema Maua huku
akisogea mbali na mama yake mdogo, kwani aliona anamsonga, na alijua anafanya
hivyo , kwa vile anatamka maneno ambayo kwake yeye aliona yatamharaibia kupata
kile alichokitaka.
‘Una maana gani nje na ndani?’ akauliza huyo Tajiri huku
akimwangalia Maua kwa macho ya kushangaa, alikuwa akiushangaa ujasiri wa huyu
binti.
‘Ndio nje na ndani, nje, mnaogopa kuwawa….ndani mioyo yenu
haina amani, kila mara mna wasiwasi…na ni heri niwe masikini kuliko kuwa na
utajiri wa namna hiyo..’akasema Maua.
‘Hongera sana binti, napenda sana watu majasiri kama wewe,…unaonekana
utanifaa sana, sio tu kama mke, bali pia katika shughulizangu,….’akawa
anamwangalia huku akitikisa kichwa.
‘Shughuli zako zipi….?’ Akauliza Maua huku akiwazia jinsi
gani atakavyoishi na huyu mtu aliyemzidi umri kwa mbali sana.
‘Nina shughuli nyingi sana,…..wewe unasema upo tayari kuwa
masikini, kuliko kupata utajiri kwa njia isiyo halili, unajua nikuambia ukweli,….wengi
wanasema hivyo, kwa vile tu wameshindwa kupata, lakini kama wangligundua njia
yoyote ya kufanya ili waupate huo utajiri, wangelifanya…. Kiuhakika hizo ni
zile hadithi za Sungura za sizitaki mbichi hizo,…ukishindwa kupata unasingizia
mengine….tuachieni wenyewe tunaojua kuutafuta utajiri…na nyie mtaishia hivyo
hivyo, mkitamani kuwa kama sisi, huku hamjishughulishi….’akasema huku akingalia
saa yake.
‘Kwahiyo umesemaje?’ akauliza mama mdogo alipoona huyo jamaa
kiangalia saa yake, kwani alijua kuwa huyo jamaa akitoa amri waondoke,
hawatakuwa na muda wa kusmhawishi tena, wataondolewa hapo kama wezi.
‘Ninasemaje kuhusu nini…’akasema kwa ukali, hadi Maua
akamwangalia huyo Tajiri kwa kushituka, maana muda huo mfupi alikuwa akiongea
kwa kawaida, lakini aliposikia sauti ya mama yake mdogo akiuliza, ghafla kabadilika.
‘Si kuhusu hiyo safari….’akasema mama mdogo kwa sauti ndogo
ya kunyenyekea,..Maua akawa akijiuliza iweje mama yake ambaye ni mkali kwake,
lakini kwa huyo mzee anakuwa mnyonge kiasi hicho.
‘Mimi nawasikiliza nyie, …ila msimamo wangu ni kuwa
sipangiwi wapi pa kwenda na kwa muda gani, mimi nina ratiba zangu,…. muda
ukifika wa kuondoka ndipo napanga hapo hapo wapi….na lipi, nyie mjiandae na
safari,…nauli natoa mimi, msiwe na
wasiwasi na hilo’akasema huku akiinuka akaonyesha ishara kwa walinzi
wake.
Maua na mama mdogo wakainuka kuondoka.
********
‘Huyo mwanamke unasema anaitwa nani?’ akauliza Malkia wa
Mererani, huku akiwa kashika kiuno.
‘Anaitwa Maua?’ akasema jamaa yake huyo kwenye simu.
‘Maua..maua ya namna gani, njano,….waridi….au, hata akiwa
maua, hawezi kufikia uzuri wangu, mimi ni zaidi ya Maua, mimi kila mahali nikienda waandishi wapo nyuma, kuchukua picha zangu ili wapate kuuza mgazeti yao….unasema ni mwenyeji
wa wapi?’ akauliza huku wivu ukimsumbua akilini.
‘Singida mpakani, ….’akasema huyo jamaa kwenye simu.
Aliposikia kuwa huyo Maua anatokea kijiji mkoa anaotoka yeye, akatikisa kichwa….
‘Kama ni huko….hana jeuri na mimi, wasichana warembo wote wa
huko nawafahamu….hilo jina kwangu sio geni…lakini, lakini...’akasema huku akijaribu kufikiria.
‘Sasa bosi, nitashindwa kufanya mambo yako, kwa vile sipo
karibu tena na Tajiri…keshanifukuza nisiwe karibu nay eye….’akalalamika huyo
jamaa.
‘Ina maana huyo Maua ndiye kasababisha ufukuzwe kazi ..au
sio,….?’ Akauliza na hata kabla hajajibiwa akasema;
‘Lakini usijali, nitahakikisha kuwa unarudi kuwa karibu na
yeye, maana wewe ndiye mtu wangu wa kunipatia taarifa, ….mwenzako hajawa
mzoefu, …sasa sikiliza,….nataka nijue anatokea kijijini gani, na wazazi wake ni
akina nani…na hapo Dar anaishi na nani..unasikia?’ akasema.
‘Nitafanya hivyo bosi…’ na simu ikakatika.
‘Maua….Maua…nitaona kama yeye ni Maua, mimi nitakuwa jua
kali la kufanya Maua yanyauke……’akasema huku akipiga simu, na akashangaa simu
ya huyo anayempigia haipatikani.
‘Ina maana kwasababu ya huyo Maua wako, umeamua kuzima hata
simu…ngoja atanitambua, sizani kaka wiki itakwisha, akiwa na wewe, ….’ Na kabla
hajamaliza kusema simu yake ikaita, akasikiliza kwa makini na baadaye akasema.
‘Basi nimekuelewa,…..nitakwenda leo leo hadi huko kijijini na
kumtafuta huyo Maua ndio nani….’ Akaongea huku akitembea kuelekea kituo cha
mabasi…
*********
‘Hapa ndio Arusha, na nimewatafutia chumba cha namna hii,
ili muwe karibu, ni chumba kimija lakini kina vyumba viwili….maana nataka pia
nikifika hapa niwe karibu na wewe…mrembo wangu..’akasema huku akimwangalia Maua
‘Nani mrembo wako, usifikiri, nimekubali kuwa mkeo…mimi
ninachohitajia ni malezi ya mtoto wangu,…..’akasema Maua.
‘Usijali, haya tutayaweka sawa,….mimi ni Tajiri bwana,pesa
inaongea, mwenyewe utanyweza na kukubali kuwa na mimi ..maishani….mimi usnione
hivi, najua kupenda, na ninayempenda anakuwa kama mbwa kwa chatu….hahaha’akasema
huku akimwangalia mama mdogo.
‘Kweli Tajiri..maana huishi kubadili wanawake,..lakini ni
kwa vile una pesa, unafikiri wanakupenda wka vile …wewe ni mpendevu’akasema
mama mdogo.
‘Wewe hujui undani wa maisha yangu…..’akasema huku
akiangalai simu yake, ambayo aliondoa sauti, na akaona ujumbe ukiingia,
akausoma na haraka akainuka.
‘Sasa tutaonana baadaye, maana naona mzee ananihitaji
haraka..’akasema.
‘Mzee gani.?’ Akaulizwa
‘Aaah, ni huyu Mjomba wangu….’akachukua mkoba wake na kuanza
kuondoka.
‘Mjomba wake…huyo ndiye wa kuonana naye, ili tuhakikishe
kuwa anatekeelza yote yanaoyostahili….’akasema mama mdogo.
‘Sasa utamjuaje, na kumpataje?’ akauliza Maua.
‘Wewe subiri, sisi ni watoto wa mjini, kuna ndugu yangu
mmoja anaishi hapa, ……Arusha nitawasiliana naye, atanmfuatilia, na tutamjua ni
nani…..’akasema huku akipiga namba ya simu.
‘Kuna tajiri mmoja……aaah, hapana, sio mzee sana….ana mjomba
wake….nahisi ndio huyo….anasafiri –safiri sana kwenda Dar, ndio huyo…..nataka
kumjua ni nani na wapi nitaweza kumpata’akasema.
Akakata simu na kwenda kukaa karibu na Maua, na kipindi
hicho Maua alikuwa kasimama akiangalia nje, kwani kulikuwa na gari limesimama,….kwa
nje,…
‘Kuna msichana mrembo, yupo nje, na ana walinzi, utafikiria
huyo Tajiri wako, anavyonata, ajabu….kapanga rangi kwenye macho, na kila
anavyofanya utafikiri wale warembo wa maonyesho, na waandishi wanampiga picha….’akawa
anaongea na mama yake, na mama yake mdogo akasogea pale dirishani kumwangalia huyo
mrembo ni nani..na kabla hawajatulia simu ya mezani ikaita.
‘Hapa ni mapokezi, kuna mgeni wenu, anataka kuonana na nyie…’
‘Sisi hatuna wageni…..’akasema mama mdogo kwa mkato, na
kabla hajaiondoa ile simu masikioni huyo mtu wa mapokezi akasema;
‘Tunajua hilo, lakini huyo ..ni mtu wa karibu wa Tajiri,…hana
matatizo, ….’
‘Anaitwa nani?’ akauliza mama mdogo huku akiwa na wasiwasi.
‘Anaitwa Malikia wa Mererani….’
NB: Wakati ukuta, ....wikiendi ilikuwaje? JE TUMALIZE?
WAZO LA LEO: Usikubali kuingia kwenye mahusiano, bila kujua huyo unayetaka `kuhusiana' yupoje na ni nani, kwani athari zake huja baada ya matendo, ....jichunge na utahamini mwili wako, kwani mwili wako una thamani kubwa sana.....
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
"nukuu" "‘Na zaidi ya hayo, sina hata rafiki, maana wale niliowaona ni marafiki, wamekuwa ndio chanzo cha kunitumbukiza kwenye maangamizi zaidi…..je hawa ni ,marafiki au ni maadui, huenda basi sikustahili kuishi kwenye hii dunia…’hapo machozi yakaanza kumlenga lenga. mwisho wa nukuu hapa nimeguswa sana ....kazi yako ni nzuri sana Hongera...
Post a Comment