‘Dereve wodo wado,
chukua juu kwa juu….’ Hii ni sauti ya kondakta wa mabasi yatokayo Msasani hadi
gongolamboto, ni kawaida yao ya kutokusimama kituoni, kwani abiria wao ni
wengi, na hawana haja ya kupiga debe, ….
Kwa hali kama hiyo ya `juu kwa juu…’ wanaoweza kudandika
hayo mabasi wengi ni vijana, wazee na akina mama hupata shida sana,…na
inawalazimu wapande hayo mabasi wakati yakipita kwenda Gongolamboto,, walipe
nauli ya kwenda huko na kurudi nalo, wanaitwa `kegeuza nalo.
Hayo ndo maisha ya asubuhi na jioni ya wakzi wa eneo
hili,..ili uwahi kibaruani, au kuwahi kwenda kuhangaika kutafuta riziki yako na
huenda ili uipate inabidi kuelekea maeneo hayo, inakubidi uamuke saa kumi
alifajiri , na unarudi saa tatu usiku,…..kiasi kwamba kwako unapoishi, unajiona
mgeni kila siku.
‘Juu kwa juu, ndio maisha yetu siku hizi, kila jambo, lazima
liwe hivyo, hata biashara, au makubaliano ya biashara maofisini, bila `cha juu’
hutajafanikiwa,….ukiona mabosi au watu wa kitengo cha mauzo, wakifukuzia jambo,
unaweza ukazania kuwa hawa watu wanawajibika kweli, kwa manufaa ya kampuni yao,
lakini ukiuliza zaidi utagundua kuwa ndani ya hicho wanachokifukuzia kuna `cha
juu chao’
Hata siku hizi ukienda hospitali, ili mgonjwa wako atibiwe
hataka, lazima uwe na cha juu, muwezeshe yule unayeona atafanikisha hilo jambo
lako, ili faili lifike kwa dakitari haraka, na kama mgonjwa wako kalazwa, docta
aweze kumtembea mara kwa mara…ukitaka iwe hivyo, mkono wako usiwe mnzito,…..hayo
ndio maisha yanatotuzunguka.
Hata ukienda kimtaifa, angalia kwanini mataifa makubwa
yanavamia sehemu, na hata kupiga vita, angalia kwanini wakubwa wa mataifa hayo
wanatembelea nchi fulani mara kwa mara , sio bure, `kuna cha juu huko…’
Wakati nayawaza haya, nikamkumbuka babu na bibi yangu ambao sitawasau kamwe, na mola awalaze mhala pema peponi huko walipo, babu na bibi walipenda sana kutuasa hasa
pale wanapotuona tunahamanika na jambo fulani, au akituona tunagombea kitu
kidogo, au tukikwepa kuwajibika, kwa kutegeana, kila mmoja akimtupia mwenzake
lawama kuwa yeye ndiye anayestahili kufanya.
Nakumbuka siku moja, babu alituona tukibishana na kutegeana...na ndio akaanza kutuasa huku bibi akiwa pembeni.
‘Wajukuu zangu, kama mngelijuwa thamani ya kujitolea
msingetegeana, na kama mngelijua athari ya kupupia, na kutaka ziada,
msingelipenda hata siku moja kula au kupata jambo bila kufikiria uhalali wake. Sogeeni
hapa niwape mambo yajayo….’akasema babu.
‘Babu naye bwana, badala ya kutupigia hadithi, unataka
kutuambia mambo yajayo….’akalalamika kaka yetu. Na sisi wengine tunaomjua babu,
kuwa akiwaita kwa jambo, kuna jambo ndani yake, anaweza aakzunguka, lakini
mwisho wa siku atatoa kisa kizuri…ambacho baadaye nimegundua kuwa ni hazina
kubwa ya maisha yetu.
‘Sikilizeni wajukuu zangu, maisha ya kuhamanika, na
kutamani, hata kile kisichokuwa chako, ni hatari, ni sawa na kujaza gunia, vitu
vingi kwa wakati mmoja bila kujali kuwa vingine vitaharibika au kuharibu
vingine,….’akatulia kidogo kutafakari jambo.
‘Ngoja niwape siri ya kufanikiwa katika maisha, …ukiijulia
hiyo, hutahaangaika kamwe, na moyo wako utakuwa wa kurizka na kuwa tajiri, hata
kama huna mali nyingi….’akasema babu.
‘Utajikuta unaishi maisha ya raha, …..kama tajiri, hata kama
huna kile alicho nacho tajiri, maana unaweza ukamuona mtu ni tajiri, lakini
hana raha,…..usishangae’akasema na kutuangalia akijua hapo hatkuelewa kitu
‘Haiwezekani, ina maana gani sasa kuitwa tajiri, uwe na
mipesa, magari, nyumba na kila kitu cha kifahari, na bado usiwe na raha?’
akauliza ndugu yetu mmoja ambaye ni mdadisi sana.
‘Kwasababau utajiri wake, aliupata kwa kupupia, aliupata kwa
kulimbikiza vya halali na visivyo vya halali, mali yake ina jasho la watu,
ambalo lipo mikononi mwake, na jasho hilo linamuandama, na matokeo yake, ndio
hayo,….moyo wake hautulii, na kwa jinsi alivyojijenga maisha yake, haweze hata
kukumbuka hilo, kuwa utajiri wake, una ziada za watu, na angelikumbuka hilo, akazitoa
hizo ziada za watu, hangehangaika kamwe…angeliishi kwa raha mstarehe…..lakini
wapi, maisha ni juu kwa juu, kama huwezi kudandia unaachwa na basi….’akatulia.
Tulicheka, na hadi hapo hatukuwa tunajua ni nini msingi wa
maneno yake hayo,…nimekuja kuyagundua hivi sasa….babu huyo akaendelea kusema;
‘Niwaambia siri moja ya maisha ….siri ya jinsi ya kufanikiwa
katika maisha yenu ya baadaye,….?’ akatuuliza na sisi tukasema
‘Tuambie babu..’
‘Mfano umepita njiani ukaona mwiba, upo kati kati ya
barabara, utafanyaje?’ akatuuliza babu.
‘Nitauruka huo mwiba , na kupita na safari zangu….’kaka
akasema
‘Nitausogeza pembeni ili usinichome, nipite, ili niwahi
nisije nikachelewa kama nimetumwa…’akasema mwingine.
‘Unaona hapo kila mmoja anachojali ni yeye, ….apite, hajali
mwenziwe anayekuja nyuma, hajali kuwa kuna wenye matatizo ya macho hawataona
huo mwiba, wapo watoto….
‘Ndivyo maisha yalivyo, kila mtu anataka apate, afaidike
zaidi, awahi afike huko anapotka kwenda….hakuna anayejali kuwa huenda yeye
anahitaji kufanya jambo, ili na mwenzake apate…..kuna watu wengine wanastahili
kupata riziki zao kwa kupitia watu wengine…lakini kwa uchoyo wetu, hatutaki
kuzitoa hizo riziki , hatutaki
kujitolea,... hebu niambieni wagonjwa, mayatima, na wasiojiweza riziki zao
zinapatika wapi kama sio kwa kupitia kwa watu wengine….sio hao tu, hata wale
wanaojiweza, wengine wanapata kwa kupitia wengine…..
‘Tunatakiwa tujitolee, tusitegeane, ili tuwezekeze kwenye
riziki zetu, na tukifanya hivyo, tutapata , tutafaidiki,na muda wote , mioyo
yetu itakuwa na amani……’akaendelea babu.
*******
Nilipokumbuka hiyo kauli ya babu ya `kujitolea kwa ajili ya
watu wengine’ nikamkumbuka jamaa mmoja wakati tukiwa shuleni.Jamaa huyo alikuwa
akipenda kujitolea sana, hadi tukamuita jina la Valmeti, kwa sasa tunapenda kuwaita
wa namna hiyo `jembe’
Jamaa yangu huyo, alikuwa akipenda kujitolea na kuwa mbele
kwa jambo la kujitolea, tofauti na wengine,
kama ujuavyo `utoto’ hulka ya kutegeana kwenye kazi haichezi mbali. Lakini
mwenzetu huyu, hata siku moja hakupenda kabisa kutegea, akiona mnasita kufanya jambo
fulani, yeye husema’`ngoja nifanye mimi, niachieni nifanye mimi….’
‘Valimenti hilo…’basi tunamshangilia, na y eye bila hiyana,
avua shati lake na kubakia kifua wazi, na atalifanya jambo hilo huku wenzake
tupo nyuma tukimwangalia na kukonyezana, na hata kuelekeza, `fanya hivi, sogeza
kule,….na wengine hata kumuona ni `mjinga au anaipendekeza vile’ lakini kumbe
mwenzetu alikuwa na siri yake, siri iliyojaa hekima ndani yake, na hekima hiyo
aliipata toka kwa usia wa babu yake.
Tatizo hivi sasa, hatuwajali wazee, babu zetu na bibi zetu, ….watu
wanawageuza babu na bibi, kuwa sio wanadamu wanostahili kuishi tena eti wamekula chmvi nyingi, na wengi
wakiwaona wazee hawa, na mabadiliko yaliyopo kwenye miili yao, macho kubadilika rangi , hukimbilia kuwaita
`wachawi..’ au vigagula…ni kama vile watu wa Dar walivyo sasa hivi, wakiona paka
wanampiga, ukiuliza kwanini, wanasema;
‘Wanga hawa….’
‘Jamani paka toka lini akawa mwanga,…ni utaalamu gani huo wa
kisayansi, uliowawezesha hawo wachawi wakaweza kugeuka kuwa paka, kama ni
hivyo, mbona tusiwezeke kwenye huo utalaamu, ili tuweke rekodi duniani, na huenda tungelitajirika kwa ugunduzi huo, maana mnaweza kujigeuza mtakavyo, kwanini
tusiwe matajiri…..
Sasa imefika hatua wazee wetu, hazina ya hekima, baraka ya
dunia, tunawaita `vigagula, wachawi, tunajisahau kuwa , ni swala la
muda tu, kesho na kesho kutwa, na wewe utakuwa kama huyohuyo babu au bibi….hakuna ujanja hapo.
*********
‘Mjukuu wangu, unaona
maisha uliyoishi, huna baba, baba yako alikukana, akasema wewe sio mtoto wake,
kampa mama yako uja uzito, na baadaye akadai kuwa sio yeye peke yake, huenda
mimba hiyo sio yake,.....haya mama yako akalea mimba hiyo peke yake, ukazaliwa, sura haikopeshi, na bado akakuna….’akawa
anamsimulia babu yake na yeye alikuwa akinisimulia mimi hayo aliyosimuliwa na
babu yake….
Hiki ni kisa kingine kifupi kinachokuja, ambacho kitafichua
siri ya mafanikio, ambayo haitumii nguvu, haihitaji mihamaniko, haihitaji maisha ya `juu
kwa juu’ ….ni kisa chenye siri kubwa
sana na ni moja ya usia wa babu na bibi zetu, tunawanyanyapaa….
Kitaitwa `WEMA HAUOZI.....'
Tumuombe mungu atujalia niweze kukusanya matukio yote ya
kisa hiki, ili kisiwe kirefu sana.
WAZO LA LEO: Kila
chumo unalolipata ukumbuke kuwa ndani yake kuna sehemu isiyo halali yako, kuna
sehemu ya wazazi wako, kuna sehemu ya maskini na wasio jiweza, ukiweza
kuliwazia hilo na kutoa sadaka, au fungu la kumi, na kuwakumbuka wazazi wako,
kwa hicho ulichokipata hata kama ni kidogo, utafanikiwa sana katika maisha na
riziki yako itakuwa na baraka
IJUMAA NJEMA.
NB: Tunatarajia kuhitimisha kisa chetu cha `Uchungu wa mwana
aujuaye ni mzazi…’ na huenda tumeruka sehemu, au kuna sehemu hazikueleweka
vyema , tunaomba maoni yenu, ili hitimisho liwe la kukidhi haja ya kisa
chenyewe…
Wazazi mpooo! Mbona kimiya, au mambo ya Facebook yanawachanganya…hakuna
shida tupo pamoja. Na hata kama sio mzazi kwa sasa, lakini tunatarajia kuwa
wazazi, kisa hicho kilikuwa ni sehemu ya kukumbushana, kutokana na yalimtokea
Maua, na kuwatokea wahusika wengine ndani ya kisa hicho, ,mengi tumejifunza, ninachoomba
ni kuwa tushirikiane, kulea jamii , na hasa vizazi vyetu,….visa hivi viwe ni
akiba kwao wakisoma wajengeke,….leo ni porojo tu, ni visa tu,lakini hatujui ni
nini hekima yake..nashukuruni sana, na tnasema;
Shukurani kwa wapenzi wote wa blog hii, TUPO PAMOJA DAIMA,
hata ukinichunia mimi nitakuwa nawe bega kwa bega.
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
Nimefurahi sana kuwa utaandika kisa hiki maana nilikuwa nawza siku moja nitafanya hivi..nasubiri kwa hamu kwelikweli:-) "Wema hauozi"
Ndugu wangu,dada Yasinta, nahisi mara nyingi mawazo yetu yapo pamoja, unaonaje ukawa pamoja nami kwenye kukamilisha kisa hiki, nitumie mawazo yako, ili nichnganye na tukio la kisa hiki, huenda kisa hiki kikawa bora zaidi?
Post a Comment