Mama Maua alizindukana na sauti ya kilio cha mtoto ilijaa
masikioni mwake, na alichofanya na kujaribu kuinuka lengo lake ni kuingia
ndani, kwani kwa mawazo ya haraka alijua kuwa mtoto wake yupo ndani, na hicho
kilio kinaashiria kuwa anamuhitaji, huenda kakojoa au ana njaa….
Alijikuta akikosa nguvu, akajaribu tena kuinuka, na mara
akahisi mkono ukimshika, na akageuka kuangali ule mkono, na mara akamuona mtu
wake,. Mtu wake ambaye yupo naye wakati
wote, japokuwa siku nyingine anakuwa haeleweki, lakini siku akiwa na shida,
akiwa anaumwa, jamaa huyu yupo karibu naye sana.
‘Kumetokea nini, mbona mwanangu analia,?’ akauliza mama
Maua.
‘Ina mana hukumbuki, nakushangaa wewe unaikataa bahati,
utapata wapi bahati kama hiyo, wenzako wanaitafuta wewe unajifanya eti siwezi
kwenda kuishi porini, haya kaa na mimi , masikini mlevi, ila ukikaa na mimi uvumilie
shida zangu’akasema huyo mwanaume.
Mama Maua akatikisa kihwa na kuanza kuwaza, na hapo
kumbukumbu zikaanza kumrejea na wakati anawazo yaliyotokea, yule mwanaume
akasema;
‘Wamesema baada ya siku saba wanaondoka, kama utabadili
mawazo atatumwa mtu kuja kukuhukua wewe na mtoto, upo tayari?’ akauliza yule
mwanaume.
‘Sipo tayari…kwanza sitaki hata kuishi hapa naona ni bora
tuhame hapa kabisa, sitaweza kuvumilia kuihsi hapa tena’akasema mama Maua.
‘Hilo wazo hata mimi nilikuwa na mpango huo, nadaiwa kama nini,
na natafutwa na polisi, bora tuhame hapa au bora nihame hapa, wewe unaweza
kuwasubiri hawo watu wako wa porini, wakija mnaondoka nao, huo ni uamzuzi wako.
‘Nimekuambia siwezi kwenda huko, baada ya hayo yaliyotokea
sitaweza kuangaliana na wao tena, uso wangu umejaa na haya,…,…na hapo
kumbukumbu ya tukio zima ikaanza kumrejea kichwani.
********
Akakumbuka, kuwa walitoka yeye na Malikia kwenda kuwapokea
wageni, na walipofikia pale waliposimama wale punda wawili ambao walikuwa wakikokota
lile gari la miti lililojengwa na ngozi ya wanyama na kuwa na sehemu nzuri ya
kukaa, na viti viwili ambavyo vilitenegenezwa kwa ngozi ya chui,..
Maua alishangaa, jinsi gani lile la miti, jinsi
lilivyotengenezwa na kuzungushiwa ngozi za wanyama, na jinsi ngozi hizo zilivyoweza
kutengeneza kitu kizuri kama kile, na alijua watu waliopo mle ndani ya lile
gari, au chombo kilicchotenezwa na kukukotwa na hawo punda watakuwa ni watu
mashuhuri sana…
‘Ina maana yule mwanaume aliyeniokoa atakuwa mtu mkubwa sana
serikalini?’ akajiuliza nafsini mwake huku wakisubiri wale watu wawili
wateremke,…na macho yake yalikuwa hayababduki kwa yule mtu, ambaye kwa wakati
huo alikuwa akimsaidia yule mzee kuteremka kwenye kile chombo.
Yule mtu alikuwa kavalia nguo zile wanazovaa askari wa
msituni, lakini nguo zake zilikuwa bora zaidi, na silaha yake ilikuwa begani
kwa nyuma, ikining’inia. Huo ndio utamaduni wao, kuwa mwanaume muda wote huwa
na silaha, mshale, kisu, fimbo….
Usoni kama kawaida yake mtu huyo, alikuwa kavalia kofia,
kofia iliyoziba uso wake, kwahiyo usingeliweza kumuona sura yake. Lakini
aliweza kumtambua kuwa ni yule yule mwanaume aliyeweza kumsaidia, na kumuokoa
kwenye kifo. Ni yule yule mwanaume japokuwa alikuwa hajui sura yake, lakini
moyo wake, ulikuwa ukimuwaza na kuiteka nafsi yake.
‘Lakini kwanini anajifunika usoni, anaficha kitu gani…?’
akajiuliza na kujiuliza vile , akawa kama anakwazika na hata kuingiwa na wasiwasi kuwa huenda huyu mtu ana matatizo
Fulani usoni, ndio maana hataki kuonyesha uso wake. Na alipowazia hilo akamgeukia
malikia, kutaka kumuuliza, lakini kabla hajasema neno malikia akasema;
‘Wageni wapo tayari, ..kiutaratibu, mimi natakiwa
niwabariki, baadaye utakuwa huru, kuwasalimia…’akasema malikia na kuwasogelea
wale wageni, na wote wawili wakainama, na malikia akawashika, kwanza alianzia
kwa mzee wao, na baadaye akafuatia kwa yule mwanaume. Yule mwanaume alitaka
kulivua lile kofia alilokuwa kavalia, maana lilifunika kichwa na uso wote, huku
likiacha sehemu ndogo ya macho ya puani,na mdomoni, ….
Malikia akaoenekana kama anamzuia yule mtu asivue lile
kofia, na akamshika yule mwanaume kichwani akiwa bado kalivalia lile kofia
lake. Maua akashangaa, kwanini malikia alimzuia yule mtu asilivue lile kofia,
kwani ingelikuwa nafasi yake nzuri ya kumuona huyo mtu. Na kwa ahli ile,
alitamani amwambie malikia amruhusu huyo mwanaume alivue hilo kofia.
Wale wanaume wawili, yaani yule mzee na huyo mwanaume,walipomaliza
kubarikiwa, wakageuka kuelekea pale aliposimama mama Maua, na mama Maua hakujua
afanye nini kwa wakati ule, alibakia akiwa kasimama, na walipomkaribia,,
akainamisha kichwa kutoa heshima, na wale wanaume wawili wakafanya hivyo hivyo,
na walipomkaribia, wakasimama.
‘Mama Maua hawa ndio wageni wako…kama nilivyokuambia na
kukuahidi kuwa nitamleta yule mwanaume aliyekuokoa, na mwanaume mwenyewe ndiye
huyo yupo mbele yako akiongozana na mzee wetu, mzee mteule, …..’akasema malikia
huku akionyesha kwa mkono pale aliposimama yule mwanaume.
Mama Maua akamwangalia yule mwanaume huku akionyesha kutahatari, na yale
yote aliyojiandaa nayo hakuweza kuyafanya tena, angeliyafanyaje hapo mbele ya
watu, na ikizingatiwa kuwa yupo na mzee wa heshima,mzee anayeheshimika sana
huko msituni, na hakutajai kuwa mzee huyo naye angelikuwepo kwenye huo msafara…akajikuta
akisema;
‘Nashukuru sana, karibuni wageni, nimefurahi kutembelewa na
watu muhimu kama nyie, lakini mfalme yupo…..’akasita kusema huku akimtizama
yule mwanaume aliyekuwa kavalia kofia, na yule mwanaume akageuka kule alipo
mtoto, akaomba mtoto aletwe mbele yake, na yu;e mtoto alipoletwa, akampakata na
kumwangalia kwa muda, halafu akamgeukia yule mzee, na kusema;
‘Unamuonaje mtoto huyu?’ Yule mwanaume akamuliza yule mzee huku
akimwangalia yule mtoto kwa makini, na yule mzee akamshika yule mtoto kichwani
kwa muda huku akiwa kafumba macho, na baadaye akawa anaongea huku kafumba hayo
macho, kama vile anaongea tuka usingizini;
‘Nikimwangalia naona nuru, lakini ina madoa ya giza …hii ina
ashiria vikwazo, ….mtoto huyu atakulia kwenye matatizo, kama hatutamchukua na
kumsafishia njia yake. Mama yake hatamuweza,..atatupwa kwa mbwa mwitu, watu
wabaya…. ni bora tuondoke naye, nahisi dunia anayokwenda kuishi haitamtendea haki’akasema
huyo mzee.
Baaaye yule mzee akafungua macho yake na kutizama mbele,
akayapangusa macho yake kwa kiganja cha mkono, halafu akamwangalia mama Maua,
akasema;
‘Mjukuu wangu, hayo niliyosema sio yangu, huwa siku hizi
naoteshwa na kuambiwa mengi, …ndio maana nikaamua kuja mwenyewe
kukuona,…nafahamu maisha yenu, na nyie mara nyingi mnatuona kuwa sisi tunaoishi
msituni bado tunaishi maisha ya gizani, yaliyopitwa na wakati, lakini mjukuu
wangu,….maisha yetu yanafaida zake, ….’akatulia kidogo na kumwangalia yule
mwanaume aliyevaa kofia.
‘Maisha yenu yana mitihani mingi kuliko ya kwetu, kwasababu
nyie mnafuata mambo yaliyoharibiwa na mashine,..sumu nyingi zimewekwa kwenye
vyakula vyenu, mnajimaliza wenyewe na mambo ya anasa, ambayo sisi hatuna, sisi
tunaishi kiasili zaidi…tunajali asili yetu, hatujikwazi kwa mambo yanayoharibu
akili, mwili na uwezo wa kimwili..hutaweza kuelewa hayo, kwa vile akili zenu
zimeshatekwa na usasa…huo mnaouita usasa,…’akasema yule mzee na kutulia.
‘Mimi sina uwezo wa kukushawishi zaidi, lakini nakuomba huyu
mtoto mruhusu akaishi nasi huko makwetu, ili aondokane na shida ambazo kama
utabakia naye zitakuja kumuandama, ….’akasema na baaaye yule mzee akamshika
yule mtoto kichwa kwa muda halafu akamuachia na kundoka, kwenda kukaa pembeni.
Pale alipokwenda kukaa, kulikwa na watu wawili waliokuwa wamefungwa kamba,
walikuwa kama mazezeta…..
Yule mwanaume akainua kichwa na kumwangalia mama Maua, na yale
matundu yanayoonyesha macho mawili yakamkumbusha Maua maisha yao ya kule bonde
la kifo. Mama Maua akageuka na kumwangalia malikia, ambaye kwa muda mwingi
alikuwa katulia huku kaangalia chini, akionyesha kuwa na mawazo mengi.
‘Japokuwa sikuwahi kufanya hivyo, lakini natumai lile
uliloniagiza limekamilika, ….kuwa nisije kukuona bila ya kuwepo mtoto wako, japokuwa
sio mimi niliyeweza kumleta mtoto wako, lakini nimefika ukiwa na mtoto
wako…..samhani kwa kutokufanikisha hilo kwa wakati….’akasema yule mwanaume.
‘Nashukuru sana …..na namshukuru mungu kuwa nimempata mtoto
wangu, hilo ndilo la muhimu….’akasema mama Maua.
Malikia akasogea karibu na aliposimama yule mwanaume, na
akamshika begani, na yule mwanaume akageuka kumwangalia, na wakati huo yule
mzee mteula, akasimama kwa ghafla na kuwasogelea pale walipokuwepo, kuonyesha kuwa
alikuwa na jambo muhimu la kusema ambalo hakutaka lisubiri, na malikia
lipomuona yule mzee kasogea karibu yao, akaondoa ule ,mkono begani kwa yule
mwanaume na kusogea pembeni.
‘Nimeona niwaingilie kidogo, kwani hili ninalotaka kuongea
ni muhimu lifanyike mapema, mnisamehe, maana maisha yangu sasa yanatawaliwa na
njozi,….naomba rizaa yenu, ..’akasema yule mzee, na yule mwanaume akasema ;
‘Bila shaka mzee, endelea, uwanja ni wako…’akasema yule
mwanaume na akamgeukia mama Maua na kusema;
‘Samhani mwenyeji wetu,…wewe ndiye muhusika mkuu
hapa,ulitakiwa wewe ndiye utoe hicho kibali, nimekuingilia, nakuomba umsikilize
mzee wetu kwa hiho anahotaka kusema, na samahani mtukufu malikia najua na wewe
ulikuwa na lako la kusema, lakini lazima tuheshimu wazee wetu, kwani bila wao
tusingelikuwa hapa…..’akasema yule mwanaume.
‘Bila shaka….’akasema malikia na kukatiza neno
‘Yule mzee akanyosha mkono wake kushiria jambo, na mara wakatokea
maaskari wakiwa wamewashika watu wawili, mmoja alikuwa mzee, na hali yake
ilikuwa mbaya, kwani alionekana kuchoka, na alionyesha kama anaumwa, mwili
ulikuwa umevimba hata maho yalikuwa hayaonekani vyema,…na hali kama hiyo
ilikuwa kwa mwanaume aliyekuwa pembeni yake…japokuwa alikuwa akionekana sio
mzee, lakini kwa hali aliyokuwa nayo, alionekana kuchoka, kama mzee, na ….
‘Oh, ni watu gani hawa?’ akauliza mama Maua.
‘Umeshawasahau,..huyo hapo ni mzee Hasimu na kijana
wake…..wameomba na wao waje kwako,….labda nisiseme mengi, tunaomba waongee
wenyewe…’akasema mzee mteule.
Mara wale watu wawili yaani mzee hasimu na kijana wake,
wakajitutumua na kupiga magoti mbele ya mama Maua, na kwa jinsi walivyochoka,
upigaji magoti wao , ulikuwa kama ule wa kulala kifudifudi…na wakawa wanajaribu
kutoa sauti, lakini ilikuwa ni kwa shida, wakasema;
‘Samhani sana kwa hayo tuliyokutendea, tunaomba
utusamehe….tunajua tulilokufanyia ni kosa kubwa, na mizimu imeliona hilo,…na
hatutakuwa na ahueni hai hapo utakapotusamehe wewe na wengine tuliowahi
kuwatendea ubaya….’wakawa wanaongea kwa pamoja lakini kwa kujibizana, mzee
akiongea na kijana wake akifuatizia kwa nyuma.
Mama Maua alipogundua kuwa ni wale watu waliotaka yeye
atupiwe ziwani ili aliwe na mamba, akahisi hasira ikimpanda na hapo hapo
akageuka kuondoka, lakini malikia akamshika mkono na kuuminya ule mkono
kuashiria kuwa asubiri,….
‘Tunakuomba utusamehe….mateso tunayopata ni makubwa
sana…..’akasema yule mzee, huku mahozi yakimtoka.
‘Koo linawaka moto, tumbo linawaka moto, maji hayapiti…ooh,
tusameheni wote, …wewe na mwanao’akasema yule mzee akijaribu kuinua kichwa,
kumwangalia mama Maua lakini hakuweza na hapo mama Maua akawasogelea na
kuwashika kichwani na akasema;
‘Mimi nimewasamehe, kwa vile mumekiri kosa lenu, ingawaje,
kama ningelikuwa nimeliwa na mamba, nisingelikuwepo hapa leo, lakini nashukru
mungu kuwa hilo halikutokea, na shukurani zangu zimfikie huyu mwanaume
aliyejitolea kwa hali na mali kuhakikisha kuwa napona…’akasema mama Maua
akimwangalia yule mwanaume.
Wale watu wawili mzee na kijana wake, wakaomba maji na
kunywa, lakini kila wakimeza fundo moja, ilikuwa kama mtu anayekunywa kitu
chenye kutia maumivu makali….
‘Inabidi wafanye hivyo, kwa kukiuka masharti ya maji ya
yamini,….na wanatakiwa kuwapitia watu wote waliowakosea, kama bao wapo hai na
kama wameshakufa, basi itawabidi wataabike hivyo hivyo hai hapo mizimu yao
itakapowasamehe…….na kwa ajili hiyo, hata sisi inabidi tuhame hilo eneo, na
kwenda sehemu nyingine…’akasema Mzee mteule.
‘Mnatarajia kuhama?’ akauliza mama Maua/
‘Ni kweli, ndio maana tumekuja kukuomba tuondoke pamoja,
maana huko tunakohamia ni mbali na ni makazi mengine mapya….’akasema malikia.
‘Hapana mimi sitaweza kuondoka na nyie…’akasema mama Maua.
‘Basi tunaomba tuondoke na mtoto….’akasema mzee mteule.
‘Hapana siwezi kuachana na mtoto wangu, sitaweza kuishi bila
mtoto wangu, yeye bado mdogo, anahitaji kuwa karibu na mama yake’akasema mama
Maua. Malikia akamsogelea yule mwanaume aliyekwua kavalia kofia na kusema;
‘Mama Maua, niliwahi kukuuliza kuwa je, kama huyo mwanaume
aliyekuokoa akisema yupo tayari kukuoa, na kuondoka na wewe utakuwa tayari, …je
nikuulize kama huyo mwanaume akasema anataka kukuoa uwe naye karibu utakubali
kuondoka na sisi?’ akauliza malikia, na yule mwanaume akaonekana kushituka na
akamgeukia malikia kutaka kusema neno, lakini malikia akamnyamazisha.
Mama Maua akashikwa na mshangao akabakia kimiya kwa muda, na
mara mzee mteula akasema kwa sauti ;
‘Mtukufu malikia hilo halitawezekana….’kabla hajaendelea
malikia akaashiria kwa mkono kumzua yule mzee asiendelee kuongea;
‘Jamani mimi nayasema haya nikiwa na moyo wa dhati..huyu
mama, ni rafikki yangu, na nampena sana, na ningelifurahi tuwe pamoja mimi na
yeye. Nataka kulithibitisha hilo kwenu nyote kuwa mimi ni mama wa wote, na pia
ni rafiki wa wote, …na urafiki wa kweli ni pale unapokuwa tayari kutoa kile
unacchokipenda kwa mwenzako….’akatulia na kumgeukia yule mwanaume, akasema;
‘Mimi nipo tayari umuoe, huyu mama …’akasema malikia lakini
mzee mteule akasogea na kusema;
‘Mtukufu malikia hilo halitawezekana…sikiliza ninayokuambia,
ni kweli moyo wako upo razi kwa hilo, lakini kuna mengi huyajui, …’ na kabla
hajamaliza kuongea mama Maua akasema;
‘Nawaombeni mnisikilize, …nashukuruni sana kwa moyo wenu
huo, na nashukuru sana kwa mtukufu malikia kunipigania ili niolewe na huyu
mwanaume,lakini mimi nashangaa, kwanini niolewe na mtu amabye simjui, …..kwanza
naomba nimjue huyu mtu ni nani…’akasema mama Maua.
‘Kumjua utamjua tu, usitie shaka, lakini…’malikia akataka
kuongea lakini mzee mteula akamzua kwa mkono, na kukawa na ukimiya kidogo, na
mzee mteule akasema;
‘Wajukuu zangu,…kuna mambo mengine yanawezekana na mengina
hayawezekani, ….najua wema ulio nao mtukufu malikia, lakini huyu mwanamama,
….haitawezekana kuolewa na ……’akasita kidogo, na baadaye akasema;
‘Naomba hilo mlizingatie,…ama kwa kuondoka na kuishi naye
inawezekana,…na hiyo ndiyo ahueni yao, hasa kwa mtoto wake, huyo ni mtoto
ambaye amekuliwa kwenye sehemu takatifu, anastahili kuwa nasi, ila kama
atakwenda kuishi huko atakapoishi,…tuombe hayo yapitie mbali…’akasema mzee
mteule na kuondoka kukaa pembeni.
‘Kwa vyovyote iwavyo, mimi naomba nikuone sura yako, wewe
mwanaume uliyenitendea wema ambao siwezi kuulipa, na kama upo tayari kunioa
mimi, basi …ukubali tusihi na wewe huku kwetu, na sio huko msituni’akasema mama
Maua, na watu wakaguna
Malikia akawaonyueshea ishara ya kutulia.
‘Kwahiyo akikubali kukuoa, ukaishi huku kwenu, na yeye
kwake, lakini atakuwa akija kila siku kukuona kama mke wake, ….hiyo
inawezekana, je kwa wazo hilo upo tayari kuolewa na y eye?’ akauliza malikia.
‘Kwanza naomba nimuona sura yake’akasema mama Maua huku
akiwaqzaia wazo hilo moyoni akisema huenda katika kufanya hivyo, anaweza
akabadili maamuzi na kwenda kuishi huko msituni….akwa kamkazia macho yule
mwanaume ambaye alikuwa kaduwaa, kama vile haelewi nini kinachoendelea.
‘Ya kwanza kwanza mengine baadaye, au sio?’ akasema malikia
huku akitabasamu.
‘Sawa mtukufu malikia, naomba nimuone sura yake
kwanza…mengine baadaye’akasema mama Maua, na malikia akatoa ishara kwa yule
mwanaume avue lile kofia na yule mwanaume kwa taratibu akalivua lile kofia.
Mama Maua alijikuta akishikwa na butwaa, aibu ikawa imemjaa,
akatamani kuwepo na sehemu akaficha uso wake,….hakuamini macho yake…na hapo
hapo akahisi moyo ukimuenda mbio, isivyo kawaida, kichwa kikaanza kumuuma kwa
nguvu sana…taharuki akahisi giza nene likitanda usoni, akadondoka na kupoteza
fahamu.
NB: Haya tujadili, kweli yupo ambaye anaweza kutoa anachokipenda kwa ajili ya mwenzake?
WAZO LEO :
Tendalo utendalo, lakini ujue kila jambo lina mwisho wake.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Wonderful рost hoωeveг Ӏ was ωоndeгing if yοu could write a lіtte moгe on this subject?
I'd be very grateful if you could elaborate a little bit more. Cheers!
Feel free to surf my web page ... bank lån
Post a Comment