Baba na mama, wakahamia sehemu nyingine, karibu na mji, na
kuanza maisha mpya, maisha ambayo yalikuwa
magumu kuliko hata huko walipotoka, ukizingatia kuwa baba hakuwa na kazi, na
kazi yake aliyokuwa akitegemea kule alipokuwa mwanzoni ilikuwa ya kuuza pombe,
pombe yenyewe ya gongo. Sasa hapo walipohamia isingeliwezekana kufanya biashaa
hiyo.
‘Sasa tutaishije hapa, maana hali ni ngumu, nimehangaika
kutafuta vibarua kila kona , hakuna hata kazi ya kufagia kwa mtu’akasema baba
huku akiwa kajiinamia kama mkiwa. Mama alimwagalia mumewe wa kufikia, maana
walishakuwa kama mume na mke, japokuwa hawakuwahi kufunga ndoa.
‘Sasa tutaishije na kodi ya nyumba inahitajiwa,….je watoto
wako hawawezi kukusaidia kulipia kodi ya nyumba, maana tangu tuhame kule,
siwaoni kabisa wakifika hapa, wamekwenda wapi?’ akauliza mama.
‘Achana nao wale wahuni, …..siku hizi wanajiona wamekuwa, ..tabia
zao hazina tofauti na alivyokuwa mama yao….’akasema na kuinuka. Siku hiyo
alikuwa hajalewa, na baba akiwa hajalewa ni mtu mwema kabisa, tatizo ni pombe,
na wakati mwingine niliombea asipate pesa, maana akipata pesa, yeye ni
kukimbulia kununua pombe.
Baadaye akarudi bila kutarajia, alikuwa kama kasahau kitu,
mara akasogelea pale mama anapoweka biashara zake za vitumbua, na kusema;
‘Biashara yako ya vitumbua leo haikutoka?’ akauliza huku
akipekua pale mama anapoweka pesa zake za biashara
‘We…acha hizo pesa, ..ndio pesa ya kununulia unga wa ngano,
..nataka nijaribu kupika maandazi kesho,…acha…..’akasema mama na kukimbilia
kumzuia baba asichukue pesa, na baba akawahi kuchukua pesa kidogo na kukimbia
nazo, na hapo tulijua akirudi baadaye kutakuwa hakukaliki atakuwa sio yeye,
maana pesa kidogo kwake, ni nyingi, atakunywa ….kwa hadaa hadi atalewa.
‘Mwanangu haya maisha yananishinda, hali yangu kama
unavyoiona, kila siku kuumwa, na naumwa kwasababu ya kukosa chakula bora, na hizo
biashara za kupika maandazi na huo moshi wake, unaniathiri sana kifuani, sipati
pesa ya kununulia maziwa , maana biashara kama hii inahitaji maziwa, …lakini
nitafanyaje,…nashukuriu nimekulea na sasa umefikia hatua hiyo, umeshafunja
ungo, kilichobakia ni ujitulize upate mume akuoe, ….
‘Mama umeanza , …..mume ,mume hawo waume ni wa kuokota kama njugu,….hata
hivyo mama, mimi bado mdogo, sijafikia makamo ya kuolewa…..mniache kabisa, kama
mumepanga kuniozesha ili mupate pesa,…hilo msahau’akasema Maua.
‘Baba yako kasema kuna mwanaume anataka kukuoa…’akasema
mama.
‘Nilijua tu….kama mnataka niwakimbie, mnitafutie mume,
…kwanza ni mwanaume gani huyo,….?’ Akauliza Maua.
‘Mimi sijakubaliana na hilo wazo la baba yako,…..na
nisingelikubali kamwe, maana huyo hakufai mwanangu, ni mwanaume wa kuoa na
kuacha….lakini kaahidi kuwa akikuoa wewe hata kuacha kamwe’akasema mama.
‘Kwanini, anaoa na kuacha, hamuona kuna tatizo hapo….mama….’
Mara mlango ukagongwa, na mama na binti yake wakaangaliana,
wakijua huenda ni baba mtu kesharudi, na mama akatoa ishara binti aende
chumbani akajifungie,….
‘Hodi hapa wenyewe hawapo’sauti iliyosikika ni ya kike,
iliyomfanya Maua asimama, kwani alishaanza kukimbilia chumbani kwake, na mama
mtu akasogea pale kwenye mlango na kufungua kwa kusita.
Wamekuwa wakiishi hivi
kwa wasiwasi, kutokana na madeni wanayoandamwa nayo, na wakati mwingine inabidi wajifungie ndani
kuogopa watu ambao wamevumilia kwa muda bila kulipwa madeni yao, na wengine
subira imewaishia wanataka kuchukua hatua nyingine ya kupiga.
‘Oooh, ndio wewe ndugu yangu, upo dunia hii,….’huyo mgeni
akasema huku akimwangalia mama huyo bila kuamini. Mama alikuwa kasimama
mlangoni, na alionyesha kuwa hataki huyo mgeni aingie ndani, na Maua akawa na
hamu ya kumuona huyo mtu ni nani.
‘Najua wengi mlishajua kuwa nimekufa, na huenda
mumeshanitengenezea kaburi’akasema mama Maua.
‘Masikini mbona upo hivyo, unaumwa…..umekwisha unaonekana
mzee kuliko umri wako, vipi kulikoni?’ akauliza huyo mgeni akiwa bado huko nje.
‘Naumwa natesekeka, …hayo hayawahusu, mimi kwetu ni maiti….’akasema
mama
‘Usiseme hivyo ndugu yangu wee….wewe na mimi tumekuwa
pamoja, urafiki wetu ni zaidi ya udugu, umesahau hilo’akasema huyo mgeni.
‘Hilo siwezi kulisahau ndio maana nikaongea na wewe,
sikutaka kukutana na ndugu yangu yoyote, mimi kwa sasa sina ndugu, mimi hapa nilipo
nina kila aina ya shida hapa dunia, na sijui nikimbilie wapi, maana huenda bora
ningeliongozana na watu wa msituni nikaenda kuishi huko’akasema mama Maua.
‘Watu wa msituni, unawajua au unawasikia, Usiseme hilo
kabisa, yaani unataka ukaishi na watu wanaokula watu’akasema huyo mgeni.
‘Hizo ni hadithi, za kufikirika,…hawo watu wa msituni ni
wastaarabu kabisa, hawali watu, na wao wanasikia hivyo hivyo kama unavyodai
wewe, kuwa kuna watu wanaokula watu…’akasema mama Maua.
‘We jidanganye tu, hawo, wanakuchukua na kukulea vyema unone,
baadaye wanakufanya kitoweo, ..haya niambie maana siamini macho yangu, mbona
hunikaribishi ndani, au mumeo hataki wageni,na …mumeo yupo wapi, maana ni
lazima una mume unayeishi naye hapa…niliwahi kupita nikamuona mwanaume mmoja
akiwa bwiii?’ akauliza.
‘Kwahiyo unamuhitaji yeye, au unanihitaji mimi ndugu yako?’
akauliza.
‘Wote mumeo ni shemeji yangu, ni lazima nimjue,..’akasema
huku akiingia ndani na macho yake yakamuona huyo binti, na akashikwa na butwaa
akimwangalia yule binti.
‘Ohhh, huyu mrembo ni binti yako…yaani huyu, kama angelikuwa
mjini, mbona ungelikuwa huna shida’akasema huyo mgeni
‘Kwanini unasema hivyo?’ akauliza mama Maua kwa mshngao.
‘Binti kama huyu anahitajiwa sana huko mjini,kwa
wanamitindo,..ni mrembo wa kutosha….ooh, umbile lake, …mashalaah, unaitwa nani
binti?’ akauliza huyo mgeni. Maua akasita kidogo halafu akasema kwa upole;
‘Mimi naitwa Maua..’akasema
‘Utaitwaje jina la mama yako,..usinitanie , mimi ni mama
yako …’akamsogelea na kumshika begani, huku akisema;
‘Mama yako huyo na mimi ni ndugu tumechangia babu…yaani babu
yetu ndiye aliyemzaa baba yake, na pia ndiye aliyemzaa baba yangu,…’akasema
huku akimwangalia huyo binti kwa makini, toka juu chini na akawa anarudia
kumwangalai hivyo hivyo mara nyingi.
‘Mimi sijui kama mama yangu ana ndugu, nilijua kazaliwa peke
yake, maana matatizo aliyo nayo, ni makubwa, kama kuna ndugu yake kwanini mama
hajawahi kwenda kuwaona….’akasema huku akimkwepa huyo mgeni kuangaliana naye
usoni.
‘Ni matatizo tu ya kidunia, yaliyotokea huko nyuma, hakuna
aliyependa yatokee hivyo,…na chanzo ni wewe,….’akatulia kidogo.
‘Kwanini chanzo iwe ni mimi, na huenda nilikuwa sijazaliwa?’
akauliza Maua.
‘Mimba yako ndiyo iliyozua balaa lote hilo…..baba mtu
akapandisha na kuwa simba…ilikuwa balaa wewe, sijui leo mkionana atasema nini,
lakini hayo yameisha nasikia hata mwenyewe anajuata, na anasema yeye hajui ni
nini kilikuwa kikimtokea,….anamkumbuka sana binti yake, na anatubu sana kwa
hayo yaliyotokea’akasema huyo mgeni.
Mama Maua alikuwa katulia kimiya akiwa kaangalia chini,
alitamani kumwambia huyo mgeni aondoke, asimkumbushe yaliyopita, yeye,
alishaandika kuwa hana ndugu, na hataki kuonana na ndugu yoyote yule, hata
wazazi wake, ndio kabisaa….
‘Sasa huyu binti una mipango gani nay eye?’ akauliza huyo
mgeni, na hapo mama Maua akainua uso , uso ukaingiwa na nuru, maana akilini
alikuwa akitafuta njia ya kumuondoa huyo binti hapo, kwani baba mtu, anataka
aolewe, na huyo jamaa anayetaka kumuoa, sio mwanaume mwema, na shikiniko hilo
limekuja kwa vile muwewe huyo anadaiwa pesa nyingi na huyo jamaa.
‘Mke wangu huyu jamaa anayetaka kumuona binti yetu, ndiye
aliyetukopesha pesa ya kodii yah ii nyumba, ujue kuwa hii nyumba ni yake, na
aliamua kufanay hivyo, kwa vile ananitumia kwenye biashara zake, ..hata ile
pombe, ..yeye ndiye mdhamini,…mtaji wote ulikuwa ukitoka kwake, sasa
tukakimbilia huku nikijua nimemkwepa, ….kumbe tunaingia kwenye yake…’akacheka kicheko cha dharau.
‘Usiniambie lolote kuhusu huyu binti yangu…madeni yako ndiyo
yafanye aolewe na wanaume nisiwajua, kama ni tajiri wako, mnajuana wenyewe……hilo
sikubalini nalo kabisa’akasema mama Maua.
‘Utakubali tu…hatuna jinsi, mwenye pesa mpishe, …’akasema na
kuondoka.
*****
‘Binti yangu, kama nilivyokuambia, baba yako kashinikiza
kuwa uolewe na huyo mtu wake, na hutaamini, eti keshaanza kupokea sehemu ya
mahari…’akasema mama Maua.
‘Mama mbona siwaelewi, yaani mpokee mahari wakati hata mume
mwenyewe simjui,….’akasema Maua huku akitoa jicho kumwangalia mama yake.
‘Unamjua sana, huyo baba anyekuja na zawadi kila siku , ….’akasema
mama mtu.
‘Ina maana zawadi hizo alikuwa akitoa kama chambo, mama,
mtaolewa wenyewe,….mimi sikubali kwa hilo, yaani mimi nikaolewe na huyo mzee,
sikubali kabisa…simpendi, namchukia, na nilikuwa napokea zawadi zake nikijua ni
mgeni wa hapa, na sikujua lolote kuhusiana na hilo, maana nakuomba sana, kama
hamnitaki nikae hapa, nitajua wapo pa kwenda na kwa vile umeshasema kuna ndugu
zangu,…nitawatafuta’akasema.
‘We…acha kabisa kuhusu hayo, hakuna ndugu yako hapa, sina
ndugu kabisa, watu waliotaka kuniaua, leo hii uende kwao, hilo sitaki
kulisikia, kama ni kwenda kwao uende nikishakuwa sipo duniani..’akasema mama
huku machozi yakimlengalenga.
Walitulia kwa muda, huku mama mtu akiwaza jinsi gani ya
kumuondoa mtoto wake hapo nyumbani, na akaliona wazo la huyo ndugu yake
aliyejitokeza , ambaye utotoni walikuwa marafiki sana, na ndio maana alipokuja hapo na kuonana naye hakuwa na ubaya
naye, japokuwa alishaapa kuwa hataki kuona ndugu yake yoyote.
‘Yule mgani aliyekuja jana, kasema huko mjini kuna kazi,….anataka
akuhukue mkaishi naye huko, na atakutafutia kazi, na hata kukusomesha …hapa
darasa la saba umemaliza kwa bahati, siku uankwenda shule, siku nyingine
huendi, lakini huko mjini ataweza kukutafutia sehemu ukasoma vizuri zaidi…’akasema
mama mtu.
‘Mama hilo ndio wazo…mimi ndoto yangu yote ni kwenda kuishi
mjini….hilo mama ndio wazo, na akija tu huyo mgeni mimi nipo tayari tutaondoka
naye, na wala usimwambie baba,….’akasema Maua.
‘Sitamwambia lakini balaa lake sijui kama nitaliweza, tuombe
mungu, ….’akasema mama huku akiwa kashika shavu
NB: Hiyo ni sehemu ndogo kwa leo. Na tunatarajia kuingia
kwenye hitimisho
WAZO LA LEO: Ugumu
wa maisha na shida zake, anayezijua ni mtu mwenyewe na maisha yake.
Ni mimi:
emu-three
5 comments :
Duh! nimechelewa kweli hapa ..maana sasa inabidi niongeze spidi kali kweli kuwa pamoja nawe...Nimependa wazo la leo na kazi yako nakuamini..Pamoja daima
Duuh, umesharudi majuu bila kuaga, kweli ww ni mngoni asilia.
Mpaka sasa hivi najiona kama naongea peke yangu,....Je niendelee au nikatize?
Jirani heri ya mwaka mpya.
Usuallу I don't read article on blogs, however I would like to say that this write-up very pressured me to take a look at and do it! Your writing taste has been surprised me. Thank you, quite great post.
Feel free to surf my web blog ... hvor meget kan jeg låne
Post a Comment