Malikia aligeuka na kwamwangalia mumewe, ambaye alikuwa
kihangaika kuweka silaha yake kwenye
chombo chake. Tabia ya mume wake imekuwa hivyo siku zote, kujituma kwenye kazi,
hata zile kazi ambazo alitakiwa awaachie watu wafanye, bado alikuwa akizifanya
yeye mwenyewe, haikuonyesha tofauti ya maisha yake kabla ya huo wadhifa na sasa hivi akiwa mtu mkubwa katika jamii yao.
Malikia aliweka alisimama na kutaka kumsogelea mumewe pali
alipokuwa akihangaika na silaha yake, lakini akasita , na baadaye akasema, huku
akitabasamu.
‘Mume wangu hizo sio kazi zako kwa sasa unatakiwa uwaachie
watu wako wazifanye, wewe ni mtu wa kutoa amri tu..na kupata muda wa kufikiria
mambo mbali mbali ya jamii yako’akasema mke wake akijua kwa hakika kuwa mume
wake hataweza kukubaliana na wazo hilo.
‘Mke wangu, kuwa kiongozi , sio kuwa bwana mkubwa …sio
kuwafanya wenzako watwana, kama lipo la kufanya na ninaweza kulifanya siwezi
kusubiri mpaka nifanyiwe, hiyo sio hulika yangu…na natumai hiyo sio hulka ya
kiongozi bora anayehitajiwa kuwa mfano kwa jamii’akasema mume wake.
‘Lakini huoni kuwa watu wako watajisikia vibaya, na kujiona
kuwa hawawezi kazi….walitarajia uwatume, na wewe hufanyi hivyo, kazi zao
unafanya wewe…?’ akauliza malikia.
‘Hapana sio kazi zao ni kazi zetu…kila mmoja anatakiwa
kuamini hivyo, kuwa kazi zote ni zetu, na kama ni zetu, basi tuwajibike kwa
pamoja. Tukijenga hulka ya kutegeana kuwa mwenzangu atafanya kazi hii, hii kazi
ni yake, sifanyi….’hapo akatulia kidogo akiwaza.
‘Kazi zitasimama, na kama ni makasia kwenye boti, boti
litayumba, na mtazama…mimi nawakubali sana watu wangu, wana kazi nyingi sana,
wakati mwingine nawaonea huruma, kwani wanahangaika kwa shughuli nyingi toka
asubuhi, hadi usiku, ….’akatulia akihakikisha silaha yake kuwa ipo safi, halafu
akasema;
‘Mimi kama binadamu, ambaye nimepitia mazingira ya shida, ya
kuhangaika, na kuwajibika nayajua hayo
yote, jinsi gani mtu anavyoamuka asubuhi, akiwa hajui atakula nini, hajui
atawalishaje watoto wake, na anadamka kwenda kibaruani kuwajibika, mwili hauna
nguvu, maana hakupata cha muhimu jana yake, alitaabika, ..hapana, lazima
niwaonee huruma wanajamii wenzangu’ akasema akionyesha uso wa uchungu.
‘Mke wangu tabia yangu na jinsi ninavyofanya, .usijali
kabisa, kwani ndivyo nilivyozoea, na nataak niwe hivi wakati wote, hizi kazi ni
kazi ndogo sana kwangu,…ninajua nina kazi kubwa, tuna kazi kubwa mbele yetu,…hilo
nalo linahitaji kutafakari, na linahitaji vichwa vya pamoja,…mimi peke yangu
sitaweza kutimiza, au kuwaza kila jambo….lakini mwisho wa siku najua mimi, na
wewe ni wazazi wa jamii yetu.’akasema huku akiining’iniza silaha yake vyema
kwenye bega lake.
Mkewe akamwangalia na akaona katika kuiweka ile silaha, nguo
zake zikawa zimejivuta kwa juu, akamsogelea na kuziweka zile nguo vyema,
akazinyosha na kuiweka silaha vyema kwenye bega la mume wake, namkono wake
akaupeleka kwenye shavu la mumewe, na kusema;
‘Sipendi mume wangu ujichoshe na kuuchosha mwili wako kiasi kikubwa…..na najua kuwa kweli kama
kiongozi kazi iliyopo mbele yetu ni kubwa sana, yenye lawama nyingi, lakini kazi
nyingine za utawala ni za kushirikiana, wewe ni kama kiongozi,…kuongoza kuwa
kazi zinakwenda kwa mujibu wa makubalionao, au sio?’ akamwangalia mumewe
machoni.
Mume wake akawa kama anakwepa kumuangalia mkewe usoni moja
kwa moja, alikuwa akitaka kutafakari jambo, lakini hakuweza kumwambia mkewe
ampe nafasi hiyo, akijua huo muda ni wa kwake na famlia yake…
‘Mume wangu cha muhimu ni kugawana majukumu, ili utendaji uwe
kwa haraka na uzito wa kutenda, kuwaza na kuwajibika uwe kwa wote, usijitwike
mzigo usioweza kuubeba peke yako…utachoka kabla hujafika mbalio….’akatulia huku
akiangalia mkono wa mume wake uliotuna kama mtu anayeinua vyuma, mkono
unaosikia kwa kazi.
Mume wake ni mshindi katika mapigano, na hata anappambana na
wenzake katika miereka , kulenga shabaha,…na hata kubeba mizigo mizito, wakati
wote anakuwa wa kwanza, …pamoja na hayo akili yake ni nyepesi kuwaza jambo,
lenye manufaa, na akiona jambo hilo linahitaji kufikiria, huwa hapendi kutoa
maamuzi hapo hapo, huomba muda wa kulitafakari, na akija kutoa rai yake,
inakuwa yenye tija.
Mume wake alipoona mkewe anakuwa karibu yake sana, na muda
unakwenda, na anahitajika kuwahi kazini, akamsogelea mkewe na kumshika begani
kwa mkono mmoja, wakawa wanatizamana moja kwa moja, hakusema kitu kwa muda, ….na
mkewe akatabasamu, , yeye alibakai vile vile na uso wa kutafakari, halafu
akasema;
‘Ni muhimu kuelewa hivyo, kuwa kazi zote ni zetu sio jukumu
la kiongozi peke yake, lakini je wote wanaelewa hivyo, najua kama kiongozi
mkuu, natakiwa nihakikishe kila kitu kinakwenda sawa, na ili hilo lifanyike
natakiwa niwe mfano, kwani uelewi wa wengine unahitaji kuona unavyotenda, na
wengine hujituma zaidi kiongozi wake akiwajibika…..nataka nifanye kila njia,
kila namna ili kila mtu anielewe…’ akatulia na kuangalia nje.
‘Kwanza ni kweli nahitaji kuwa na watendaji wanaojituma na
wenye uchungu na jamii yetu , lakini kinachonitia wasiwasi ni kuwa wengi ninaowajua wanatoka kwenye ukoo wetu, na
hili naliogopa kwani tukijaza viongozi wote kutoka kwenye ukoo wetu, wengine
watatulaumu, na hapo ndipo ninapohisi kuwa kuna umuhimu wa kumtafuta kijana wa
mzee hasimu, na viongozi wengine kwenye koo ndogo ndogo ili ….tuwe pamoja…...’akatulia na kuwaza.
‘Sasa utampataje huyo kijana, na je atakubalina na ombi lako
hilo kuwa unataka uongozi wa pamoja,….ukumbuke walishasema wao hawatshirikiana
na sisi kwasababu huna sifa ya kuwa mfalme,….walikengeuka, na kusahau yote
waliyotabiri huyo mtabiri waliyekuwa wakimsfikia. Utabiri huo walitaka uangukie
kwao , kwa wengine wanaona sio sahihi….’akasema malikia.
‘Ndivyo ilivyo , kama binadamu inapofika kwenye masilahi,
kwenye sehemu ambayo anaona atapata kile anachokihitaji, hutafuta kila mbinu , …na
wengine huondoa kabisa ubinadamu,…..ubinafsi unatawala nyoyo,….lakini hatima ya
yote ni matakwa ya wanjamii, …je ubinafsi huo utakuwepo mpaka lini, je
hatuwaonee huruma wengine, kuwa na wao ni banadamu kama wengine….hapana hapo
ndip ninapoona wenzetu wanakosea’akatulia kidogo.
‘Wanakosea ndio na wanajua hilo,….ndio maana walikuwa
wakifanya kila mbinu hata kuzitumia sheria ili ziwafae wao, na kuzigeuza geuza
kwa maslahi yao…sasa wanaogopa, maana sheria zile zitawaumiza wao, …ndio maana
wamekimbia’akasema malikia.
Malikia akatulia na mawazo ya kumshukuru mungu yakamjia ,
akapeleka mikono yake mbele na viganja vya mikono vikawa vinaangalia juu, na
yeye akaviangali vile viganya akawa anasema kimoyo moyo;
‘Ahsante mungu kwa kunipatia mwenza mwenye mawazo na hisia
kama zangu, asente mungu kwa kunirejeshea mume wangu, ahsante mungu kwa
kunikubalia maombi yangu, nakuomba uijalie ndoa yetu iwe ya fanaka na baraka…’akatabasamu
na hapo akageuka na kumsogelea mume wake ambaye alikuwa akijiandaa kuondoka kwenda
ofisini kwake.
Mume wake akageuka na kumwangalia mkewe akahisi kuna jambo
zaidi linalimsumbua mkewe, na ilionekana kama anasita kumwambia, akasema;
‘Vipi mke wangu nakuona una jambo zaidi moyoni mwako,
nakuomba mke wangu kama lipo jambo niambia mimi ni wewe na wewe ni mimi,…..je
kuna tatizo?’ akauliza mfalme mtarajiwa.
‘Hakuna tatizo mume wangu, nilikuwa na mawazo mengi
kichwani, lakini yote hayo yalifutika pale nilipokuangalia, namshukuru sana
mungu, kwa kukurejesha , maana mengi yaliyopita huku yalishatukatisha tamaa, na
hata kufikia kusema wewe umeliwa na mamba, na ukiliwa na mamba maana yake una
dhambi…..hilo ndilo limenifanya nitulia na kumshukuru mungu wetu’akasema
malikia.
Hapo mfalme mtarajiwa akatulia na ile haraka ya kuondoka
ikatoweka kwa muda na kumuuliza mkewe
‘Ina maana hata wewe ulishaamini kuwa nimeliwa na mamba?’
akauliza.
‘Sikuamini kabisa,
na sijui ni nani alilikata kata lile ua…nilipoliona limesambaratika, kwa kweli
nilishituka hadi kupoteza fahamu….lakini nilipotulia na kuanza kufuatilia tena
na kugundua kuwa ua hilo halikuwa limenyauka, bali ni mtu alikuwaja
akalifinyanga finyanga na mkono…nikajua hapo kuna jambo, nikajua bado upo hai,….’akatulia.
‘Binadamu ni mwerevu sana,…hapo unaona jinsi tulivyo, hakuna
siri ….na ukiwaza hivi kuna wengine walishawaza, na wana kipaji cha kujua
unawaza nini……mimi niliwahi kuambiwa na wazee wa kule makaoni kuwa ukisafiri
safari yenye mashaka unahitajika kumpa mkeo ua,….ua hilo ni sihara ya upendo,
na ili mkeo awe na hisia za upenzo, atatii yale uliyomuagiza na ua lile
litasimama kama mwenzako….’akatulia.
‘Ni kweli pia hata babu aliniambia hivyo, kuwa katika imani
zao, ua linasimama kama ishara ya upendo, na ukiliombea vyema, …litasimamia
zile hisia zetu, na kama hisia zenu zipo pamoja, ua lile litaendelea kuchipua,…kunawiri,
lakini hisia zikitengemana, basi ua hilo hunyauka,….na huenda mmoja wenu akawa
hana uhai tena….’akatulia hapo.
‘Inawezekana ikawa sio uhai wa kuishi, lakini uhai wa kuwa
pamoja….ingawaje wazee wetu waliniambia likinyauka ni kuwa maisha ya mmojawapo
yamenyauka, lakini mimi sikuwa nimemini hivyo moja kwa moja….na kama ilifikia
hadi wenzetu wakajua hio, basi imani hiyo ina nguvu, na hapo tumejiunza jambo,
lakini nisingelipenda kutumia imani hiyo kwenye mapenzi yetu’akatulia kidogo.
Mkewe akamwangali kwa muda na kulikumbuka hilo swali la
mumewe kuwa kama yeye kweli aliamini kuwa mumewe keshafariki kwa kuliwa na
mamba, alitamani ile hali aliyokuwa nayo aipeleke kichwani kwa mumewe akumbuke
jinsi gani alivyokuwa akiteseka, na jins gani alivyokuwa akipingana na mawazo
hayo kuwa mumewe kshafariki….na…., hapo akasema;
‘Katika hali iliyokuwepo …. ungelifanyaje ….nilikuwa
katikati ya watu na majukumu yao waliyojipangia, mimi kama mimi, nilishaamua
kutokukubaliana nao, na hata huo umalikia sikuutaka tena kama ni lazima niolewe
na mtu mwingina, nilishaamua nikusubiri,
lakini babu ndiye aliyenipa moyo, na kuniambia jukumu hilo halikimbiwi, na
yakkuwa mimi sio mama wa ukoo wanu tu, ni mama wa koo zote…’akasema na huku akiangalia
nje, alishaona kuwa anamchelewesha mumewe.
‘Mke wangu, najua jinsi ulivyokuwa kwenye wakati mgumu,
nilihisi hivyo, lakini sikutegemea kuwa mambo yangelichukuliwa kwa haraka kiasi
hicho, najiuliza je kama ningelichelewa ingelikuwaje, …kama ningelifika hapa
nikute umeshaolewa na huyo kijana wa mzee hasimu ingelikuwaje? ‘ akauliza
mfalme mtarajiwa.
‘Mume wangu kila kitu hupangwa na muumba, kama alipanga tuwe
nawe, isingeliwezekana iwe hivyo, ndio maana imekuwa hivyo….hilo amini, na yote
tunayofanya binadamu ni kutimiza wajibu tu,lakini mwisho wa siku ndio unaosema
na hutendeka hivyo inavyotakiwa’akasema malikia huku akimwangali mumewe usoni.
Na wakawa sasa wameangaliana.
‘Mkewe wangu sijui niseme nini, maana katika kutimiza
majukumu yangu huenda nimetelekeza, na siina budi kukuomba msamaha, na naomba
tuwe pamoja na tushirikiane kwa kila jambo, kama utaona nimeteleza, niambie,…na
yaliyotokea huenda yalitokea ili niweze kutimiza majukumu yangu’
Mke wake akatulia na kumwangalia mumewe kwa makini alitaka
kumuulizia kwanini afikie kuomba msamaha, kuna nini kikubwa alikitenda na kabla
hawajaongea zaidi mara mlango ukagongwa, na ikabidi mazungumzo hayo yakatishwe.
Mfalme mtarajiwa alitoka na kuongea na mlinzi wake, baadaye
akarejea na kumkuta mkewe akiwa kasimama akiangalia nje ,
‘Mke wangu inaonekana wahasimu wameshakusanya kikosi chao
cha maaskari na inaaminika kuwa wapo kwenye ngome yao muhimu, hatujui wana
maana gani, na kwa hilo inabidi tujiandae kwa lolote na hata ikibidi kuingia
vitani kwa maslahi ya wanajamii….’akasema mfalme.
‘Vitani……?’ ‘akauliza malikia mtarajiwa akiomba hilo lipitie
mbali.
NB: Inabidi tuishie hapa kwa leo.., tupo pamoja.
WAZO LA LEO:
Upendo wa kweli ni ule unaojengwa na hisia za pamoja, na akili , mwili na
matendo yakashabihiana kama mapacha. Na wengine hufikia kusema wanandoa hawo
wanafanana kama mapacha. Hili linawezekana kama kila mmoja atajua kuwa yeye na
mwenzake ni kitu kimoja. Mkifanya hivyo kwa upendo wa dhati, mungu huwabariki
mkafanana hata kisura.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Ahsante sana kwa kuandika. Nilipotea mtandaoni kwa muda kiasi, leo ndio nimeianza hii story na kufika hapa ulipo, dah yani niliingia katika ulimwengu mwingine kabisa. Ni kisa cha kusisimua nawe ni mwandishi mzuri. Cheers!!
Post a Comment