Adam alifika mbele ya baba yake, ambaye siku mbili sasa
hawasikilizani, maana wazo lake la kwenda Mererani, limekataliwa, na baba yake
kamwambia achague mawili kwenda kusoma au kujifunza ufundi kwa baba yake mdogo.Yeye
yote hayo mawili hakuyapenda, kichwani kwake kulijaa ndoto za utajiri, na
matumaini yake makubwa ni kuwa akifika Mererani atapata utajiri kutokana na
madini.
Akawa katulia kusikiliza ambacho baba yake amemuitia, alijua
tu ndio hayo maswala mawili ambayo kila siku anapigiwa debe kuwa akasome, au
ajifunze ufundi, lakini alishawaambia
kuwa kwenda kusoma watapoteza pesa zao bure, kwani kichwani kwake hakuna kitu
cha kuweza kupokea elimu, kichwa chake kimejaa ndoto ya kupata pesa.
Mama yake alikuwa katulia akifuma vitambaa, na ilionyesha wazi
kuwa hana raha, alikuwa kakonda kwa mawazo ya maisha magumu. Na Adam kila akiwaangalia
wazazi wake na maisha waliyo nayo, huwa roho inamuuma, na mara kwa mara alikwua
akijiuliza kwanini wao wamekuwa hivyo, wana kosa gani, mabona wengine wana
mafanikio.
‘Lazima nitafute, sitaishi kwa raha,nikiwaona wazazi wangu
wanasononeka, wanazeeka kabla muda sio wao, lazima nifike machimbi’akajipa
moyo.
Alijaribu kuwaza mbali alipoamuona mama yake vile akifikiria
kuwa huenda wazazi wake wamesigishana
sababu yake, na kama ni hivyo, iliyobakia
hapo ni kutoroka tu, kwa umri kama wake, hahitajiki kubishana an wazazi wake,
anatakiwa aanza kutafuta maisha yake, `lazimz na mimi nifanye kama alivyofanya
mjomba’. Mara kwa mara alikuwa akiongea
na mjomba wake kuhusu maisha, alikuwa madadisi na alitaka kujua jinsi mjomba
wake alivyofanikiwa. Akakumbuka kuwa mjomba alitoroka kwao, akiwa darasa la
tano,na kukimbilia machimboni.
Akagutuka pale baba yake alipoanza kuongea, na kutulia
kusikiliza, ingwaje mawazo yake hayakuwa hapo, baba yake akasema;
‘Nimekuita hapa tena, maana baba ako mdogo, anasema kuna
watu wanataka kuchukua nafasi yako, wanataka kujifunza ufundi kwake, sasa wewe
una lengo gani maana tumekuuliza kuwa unataka kusoma, hujatupa jibu kwani kama
unataka kusoma pesa inahitajika, na hali yetu ndio kama ilivyo, kwahiyo hili
tunatakiwa tulijue mapema.
Kama unataka kusoma, familia yetu itajikusanya
tuchangishane, hata mjomba wako kasema atatoa msaada wake, ili uksome sekondari umekataa, hebu tuambia mtoto
wetu unataka uwe nani katika dunia hii, dunia hii kama hujasoma, huwezi kuwa
mtu, na umri kama wenu na karine yenu, utakuwa mgeni wa nani, ukisema umeishia
darasa la saba tu, huoni kuwa utachekwa’akaambiwa na baba yake.
‘Kwani mjomba yeye alimaliza darsa la ngapi, yeye kaniambia,alitoroka
shule akiwa darasa la tano na kukimbilia migodini, sasa hivi ni tajiri,
anawaajiri watu waliomaliza chuo kikuu…hapo alipo ni kama mtu aliyemazlia chuoo
kikuu, hajasoma wala hajasomeshwa’akasema Adam.
‘Unaona akili yako ilivyo changa, ina maana wewe unajilinganisha
na mjomba wako, kwasababu ya utajiri wake
alio nao, ule ni utajiri wa kubahatisha, hebu jiulize wangapi wamekwenda huko
migodini, mpaka leo hawana kitu, ina maana wao hawataki kuwa matajiri?’
akaulizwa.
‘Ni ujanja wako, unaweza ukawahi usipate, mimi najua
nitapata tu, kama hujawa mjanja utabakia masikini, mimi nimeshajifunza mbinu
nyingi toka kwa mjomba, nikifika pale najua jinsi gani ya kujichanganya,
wenyewe mtaona’akasema akiwa na ndoto za ajabu.
‘Sikiliza mtoto wetu, biashara ya madini ni sawa na bahati
nasibu, ni biashara ya kubahatisha, haina muamala, ni hatarai tupu, wengi
wamefia huko. Kitu cha muhimu kwako ni elimi, ukiwa na elimu maisha yako
hayatakuwa ya kubahatisha, kwani elimu ni mwanga utakuangazia na kujua njia
gani upitie’akaambiwa
‘Baba kwanini hamtaki kunipa hiyo nafasi, mimi naahidi kuwa
hamtajuitia, nitahakikisha kuwa nawajenega nyumba za kisasa, kama za mjomba,
mimi nakumbuka jisni gani mjomba alivyopitia, alishaniahadithia, na mimi
nitakachofanya ni kukwepa yale magumu aliyoyoata na kutumia ujanja mwingine,
nina uhakika nitafanikiwa, kwa ajili ya maisha yangu na nyie pia’akasema.
‘Ina maana huyo mjomba wako alikusimulia alivyofanikiwa, na
akakushauri kuwa uende huko, …huyu mtu hana akili ehe, kama kweli kakushauri
hivyio, atakuwa hana maana, lakini hawezi kufanya hivyo, hizo ni akili zako za
kitoto tu’akasema mama yake kwa hasira.
‘Hajanishauri kitu, ila mimi mwenyewe nataka kwenda tu, yeye
alinikanikatalia siku nyingi, najua kila mtu atanikatalia lakini nikifanikiwa
hapa kila mtu atanisifia,…ataniona wa maana’akasema huku akiwaza jinsi gani
atakavyo kuwa tajiri, na hatimaye, hata Maua akimaliza shule yake, atakuja
kwake na kumuona wa maana. Sasa hivi kasoma, akimaliza hawezi kupenda tena,
kwasababu hana elimu, hana pesa.
Alikumbuka barua ya mwisho kuwasiliana, na Maua, ilimtia
hofu, aliposema kuwa anahisi ana dalili za ujauzito’
‘Ujauzito, ni nani huyo kampa mimba,…’akasema kimoyomoyo, na
akawa na mashaka kuwa huenda keshapata mtu huko na ndiye aliempa hiyo mimba.
Hapo akaona aachane naye, licha ya kuwa alikuwa kimpenda
‘Najua atakuja kunitafuta siku akisikia kuwa mimi ni
tajiri..lakini kama ana mimba mimi siwasiliani naye tena, na wala asinijue’akajipa
moyo,lakini akaapa kuwa hatawasiliana naye tena, hakujibu ile barua ya mwisho
akaichanachna kwa hasira, mawazo yake akayaelekeza kwenye kutafuta utajiri, kwa
kupitia kwenye madini, na si kwingine ni kwenda Mererani.
‘Huyo mjomba wako mliongea nini?’ mama yake akamuuliza, na
kumkatisha mawazo yake, ilionyesha kuwa mama yake kakasirika sana, akihisi kuwa
kaka yake ndiye anamharibia mtoto wake, tena wa kwanza.
`Nilimuulizia jinsi gani alivyofanikiwa, na mambo
aliyokutana nayo huko ili hata nikifika huko na mimi nijue wapi pa kupitia,mimi
sitaki kabisa kumtegemea yeye au mtu yoyote, mimi nataka nitafuta kwa njia
zangu lakini niwe kama yeye, niwe na hali nzuri, ili na nyie pie mfaidi matunda
ya mtoto wenu, sina nia mbaya,’akasema.
‘Alikusimulia nini…nataka kujua hayo aliyokusimulia hadi
ufikwe na tamaa ya kwenda huko, ujue hapa kuna mengine yametokea, na
usipoangalai utakwenda jela, …?’ mama yake akauliza kwa hasira.
‘Mambo gani mengine, mama, mimi muda wote nipo hapa nyumbani
,nikitoka ni shambani, sijajiunga na makundi mabaya, …kwanini nifungwe, ndio
maana sitakii kuishi hapa, maana watu wanaweza wakafanya ubaya wao,
nikasingiziwa mimi…’akasema huku akimwangali baba yake ambaye alikuwa katulia,
akisikiliza
‘Kwanza tuambie huyo mjomba wako alikusimulia nini,kabla
hatujakuambia mengine ambayo tumesikia,kama ni kweli mmh, sijui utakimbilia
wapi, hebu niambie mjomba wako alikusimulia ninii?’ akuliza mama
Ndipo Adam akaanza kumsimulia jinsi walivyoongea na mjomba
wake siku hiyo,..
***************
‘Ina maana mjomba hukumaliza darasa la saba, mbona unangea
kiingereza safi kabisa?’ akamuuliza mjomba wake siku moja.
‘Mimi nimeishia darasa, la tano, nilitoroka shule, na hata
kipindi nasoma, nilikuwa sifiki shuleni mara kwa mara nilikuwa naishia mitaani,
baadaye niakona isiwe shida, nikatoroka shule, na kuingia Arusha, na huko ndiko
nilipoanzia maisha yangu.’akamwambia mjomba wake.
‘Sasa hicho Kiingereza umejifunzia wapi, maana naona
unaongea na wazungu, bila wasiwasi?’ akamuuliza.
‘Ukiwa na pesa kila kitu kinawezekana, mimi ni mjanja wa
lugha, licha ya kuwa sijasoma hadi huko juu, lakini nikisikia watu wakiongea
lugha yao nikatulia wiki moja tu, naiongea bila wasiwasi, kiingereza ni lugha
kama lugha nyingine, hata hivyo, niliamua kujifunza lugha hiyo na masomo
mengine, ili iwe rahisi kufuatilia miradi yangu, nakushauri mjomba wangu
usome,usije ukaniiga mimi’akaambiwa.
‘Mjomba, mimi kwakweli nataka niwe kama wewe, ….hiyo ndiyo
ndoto yangu’akamwambia. Mjomba wake akamtizama, na moyoni akajisemea, `huyu mtoto
kaingiwa na tamaa, hajui jinsi gani nilivyohangaika, angelijua asingelifikiria
hivyo’.
‘Mjomba maisha niliyopitia sio rahisi kama watu
wanavyofikiria, nilipofika huko Mererani, nilipata shida sana, kuna muda
nilitamani nirudi kijijini, lakini nia na ari, zikanituma nisikate tamaa, kwani
nyumbani nilitoroka, nikirudi nitachekwa, nikajipa moyo kuwa ipo siku bahati itaninyookea. Niliwahi kuumwa karibu ya
kufa, ilifikia muda nikakata tamaa ya maisha kabisa, nilijua kabisa nitafia
huko…
`Yaani mjomba wangu maisha ya kule sitaweza kuyasahau ….’akaanza
kumsimulia jinsi gani alivyokuwa siku hiyo ambayo kwake ilikuwa ndio siku ya
mwisho wa maisha yake,
***********
Siku hiyo, mjomba akasema alipanga kwa vyovyote ajitahidi kujiiba
na kuingia kwenye shimo walilokuwa wakichimba, akiwa na nia ya kujaribu bahatii
yake ya mwisho, hakuna aliyeruhusiwa kuingia, kwenye shimo bila kibali.Mchana
kutwa alishinda humo ndani na wenzake wakichimba na mwisho wa siku wanaambulia
posho na vijisenti kidogo. Hali yake
kiafya ilikuwa mbaya sana, kwani alikuwa akimuwa kifua na hakuweza kijitibia.
‘Hapa ukiumwa huna chako…’Rafiki yake akamwambia pale
alipoanza kulalamika kuwa anaumwa, akaambiwa;
‘Ni bora utafute miti shamba utafune, ipo miti shamba na mizizi inasaidia,
ili mradi maisha yaendelee, huyu tajiri akisikia tukuwa unaumwa unafukuzwa
kazi’mwenzake akamwambia. Basi kwa ushauri huo, akawa anajikakamua na kweli akawa anatafuta miti
shamba na siku zinakwenda, lakini hali ilikuwa inazidi kuwa mbaya.
Kilichomfanya aingie tena shimoni, ni kwasababu wakati
wanachimba mchana kuna sehemu aliiona, akahisi ni madini, hakuwa na uhakika kwa
muda huo, alichofanya ni kupafukia vizuri, na kuamua kuwa usiku atafanya kila
mbinu aingie ndani, aangalia kama ni bahati yake.
Alijua kuwa ni hatari, kwani wale walinzi walipewa kibali
cha kuua, kama watanaona mtu anaingia kwenye hayo mashomo bila kibali. Kuna
wengi wameshapoteza maisha kwa kujaribu kuingia. Yeye kutokana na hali aliyo
nayo akanona,, basi lollote liwalo, ngoja akajaribu bahati yake.
Hakumwambia mtu, na mbaya zaidi ,usiku huo mvua ikawa
inanyesha kwa wingi, kwahiyo watu wengi walikuwa wamjazana sehemu moja kwenye
jengo lisilovuja,majengo mengi, waliyokuwa wakitumia ni ya muda, na mvua
ikinyesha yanavuja, …
Alichofanya kwa vile kulikuwa na baridi, na hali yake kiafya
sio nzuri, akaamua kumauzima mwenzake koti la mvua, na baridi,kwani alishaanza
kutetemeka baridi, na hakuwa na nguo nzito. Alipohakikisha kuwa watu wamelala,
kwasababu ya kuchoka. Yeye bila kujali mvua, akatoka nje, na mvua ilikuwa
inanyesha kweli kweli, kiasi kwamba, mtua kiatembea anakuwa kama anaogelea. Kwa
ajili ya mvua, alijua kabisa kwa muda huo walinzi hawpo makini, anajibanza hadi
sehemu ya kuingilia kwenye shimo, akafungua ule mlangowa shimo, na kuingia.
Kwasababu mvua ilikuwa inayesha na jinsi kulivyofungwa,
haikutakiwa pafunguliwe mpaka mvua iishe, yeye hakulijali hilo alichokuwa
anajali ni malengo yake. Akaingia na maji yakawa yanaingia kwa ndani, na na
kusababisha ule mlango usiweze kufunga vyema, yeye kwa muda huo hakujali sana
alijua ataingia mara moja na kutoka.
Akaharakisha kuingia hadi sehemu aliyoiwekea alama, akachuka
kichepe kidogo cha mkononi, alichokuwa kakificha na kuanza kuchimba. Wakati
anachimba, alijialaumu kwa jinsi alivyoshindwa kufunga ule mlango, akawa na
wasiwasi kuwa huenda maji yakaingia mengi na akashindwa kutoka.
‘Nitawahi kabla majai hayajazidi, na kesho wakigundua
hawatakua kuwa ni mimi, na kama ni madini, nitatoweka asubuhi na
mapema’akasema.
Haikuchuka muda
akagundua kile alichokiona mchana, akayakusanya yale mawe ambayo kwa muda huo
hakuwa na uhakika nayo, akayaweka kwenye mfuko wa nailoni, na akawa bado
anatafuta, tamaa ya kibinadamu ikamzonga, badala ya kutoka haraka, akawa
anaingiwa na tamaaa huenda ataapta zaidi, mara akaoana maji yanakuja kwa kasi.
Akaanza kukimbilia njia ya kutoka, lakini maji yalikuwa
yanakuja kwa kasi tena mengi, akaanza kuhaha, sasa akajua anafukiwa ndani ya
shimo. Hakukubali akawa anapambana na maji, yanamrudisha nyuma, yeye anajaribu
kusonga mbele. Mara akasikia mtikisiko, shomo lilikuwa linaanza kuporomoka.
‘Mungu wangu nisaidie, maana hii ndio niliona ni bahati
yangu ya mwisho, sasa naona kama nitafia humu ndani.’akawa anaomba huku
anapigana na maji,na kifusi , kuna muda maji na kifusi kinamfukia, inabidi
aanze kazi ya kukichumbua hadi anachomoka, ….
Sasa shimo likaanza kutitia, madongo,maji yakawa yanakuja
kwa kasi ,kuelekea ndani kule alipokuwa kasimama, na hapo ikabidi atafute
sehemu ya upembeni kabisa asubiri, na kusubiri huko ina maana shimo linajifukia
na huenda baada ya muda hewa itakuwa haipatikani tena, akajua sasa mwisho wake
umefika.
Pale alipokuwa kasimama, alijihisi kabisa hana nguvu, kifua
kinambana, anakohoa, lakini hakukata tamaa alihakikisha kuwa ule mfuko wake,
kaufunga vyema ndani ya mwili wake, na mtu asingeliweza kujuwa kuna kitu
kajifunga kwa ndani, na lile koti kubwa lilimsaidia ingawaje kwa muda ule alitamani
kulitupa,kwani lilikuwa zito kwa kulowana na maji yaliyojaa matope.
Haikupita muda shimo likaanza kuporomoka, sasa hivi
ilionyesha dhahiri kuwa linajifukia
lote, na hakuna njia tena ya kutokea nje.akawa anaangalia jinsi shimo hilo linavyoshuka
na kujitahidi kukwepa udongo, ulikuwa ukishuka toka juu, na alishajua kabisa
hakuna njia ya kuokoka hapo, na ndipo akaanza kuikumbuka familia yake nyumbani,
baba na mama yake, kuwa ndio tena hatawaona mpaka siku ya mwisho, akaanza kutoa
machozi na kujuta.
‘Oh wazazi wangu mnisamehe, yote haya niliyafanya nikijua
kuwa natafuta maisha, sikujua haya yanaweza kutokea, nawaombeni sana mnisamehe,
na tukijaliwa tutakuatana ahera…’madongo yakawa yanamporomokea na kumbamiza
kichwani, …
NB: Haya ambo ndio hayo,
WAZO LA LEO: Tuwe
na wivu wa kimaendelea sio wivu wa husuda, kama mwenzako kapata kapata kwa
jasho lake, na wewe jitahidi upate kwa jasho lako, kwani riziki mtoaji ni mola,
lakini na wewe ukijibidisha kuitafuta katika njia za halali.
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
Maisha nikupambana, huwezi jua wapi pa kupatia, lkn elimu ndiyo dira, huyo jamaa alikuwa na tamaa ya pesa. Sijui ilikuwaje baadaye tunasubiri. Kazi nzuri mkuu
Hongera mkuu
Post a Comment