Mlango uligongwa kwa fujo na kuwashitua wenye nyumba na hata kuvuruga mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea,na wa kwanza kusimama alikuwa baba mwenye nyumba, akangalia kushoto na kulia, akitafuta silaha , na alipoona hakuna silaha iliyopo karibu, akamwangalia mkewe.
Mkewe ambaye alikuwa kashika kichwa akiwza mstkabali wa maisha yoo na mtoto kwake, akainua kichwa na kumwangalia mume wake , kwanza akijiuliza ni nani anayegonga kwa fujo hivyo, au kuna kitu mume wake kafanya, na alipoona mume wake anaangalia ile sehemu anayoweka panga, akigundua kosa alilofanya, kosa ambalo kila mara amekuwa akilirudia, akakumbuka kauli ya mume wake ya mara kwa mara;
‘Mke wangu, panga hili naliweka hapa maalumu kama ni silaha yangu, usiwe unaliondoa hapa karibu na mlango huwezi jua wakati gani tunaweza kuingiliwa. Huku ni porini, silaha zetu ndio hizi, ujue mke wangu dunia hii imekwisha.Nimeshakuambia mara nyingi, sitaki panga hili liondolewe hapa mlangoni, hili ni maalumu kwa ajili ya kujilinda’aliambiwa siku za nyuma na mume wake.
‘Mume wangu na wewe kwa kupenda kujihami, muamini mungu wako maana yeye ndiye mlinzi wako, hata ukiwa na silaha, hutaweza kujilinda siku yako ikifika‘mkewe ambaye ni mcha mungu sana akamwambia mume wake.
‘Mungu kakupa mamlaka, na moja ya hayo mamlaka ni kujilinda, ndio maana tunajenga nyumba, hatulali nje, hebu nikuulize mke wangu, hivi unaweza ukasimama kati kati ya barabara wakati magari yanapita ukasema mungu atakulinda…’akaambiwa.
‘Mume wangu, sina maana hiyo, sasa ndio kusema hilo panga likikaa hapo mlangoni ndio mlinzi wako?’ akaulizwa.
‘Hilo panga nataka liwe linakaa hapo, hiyo ni silaha ya kujilindia, ili kama ikitokea tatizo la kujihami tutalitumia hilo kama silaha, sitaki uwe unaliondoa hapo mlangoni, mapanga mengine yapo kwanini unalichukua hili, naomba unielewe hivyo’akaambiwa.
‘Haya mume wangu nimekusikia, …lakini mara nyingi naliondoa hapo kwa dharura, labda nimeamua kulitumia na baadaye nalirudisha, lakini wakati mwingine najisahau kulirudisha kwa wakati, nisamehe mume wangu’ akasema huku akilitafuta wapi alipoliweka.
‘Haya naliomba lirudi hapo haraka’.
Leo kosa lile limerudiwa tena, pangahalipo sehemu yake, na mume alilihitaji kuwa nalo, maana hizo kelele huko nje, haziashiri mema. Na akilini mwake akakumbuka matukio ya nyuma ya wachungaji kuja kuvamia maeneo na hata kuingia majumbani na kuchukua vitu. Alipokumbuka hivyo, akaanza kulitafuta panga, lake, lakini mke wake alikuwa kaduwaa. Mkewe akamwangilia mume wake machoni.
Macho ya mume wake yalijieleza wazi, yakimsuta mke wake, kuwa kwanini kaliondoa hilo panga hapo mlangoni, sasa unaona , labda kuna hatari inakuja, na silaha inahitajika. Na kabla baba mtu hajasema neno, mara wakasikia sauti;
‘Hodi nyumba hii jamani, ….’sauti ya kugonga mlango tena kwa fujo ikasikika,toka nje.
‘Kuna usalamahuko…mbona unagonga mlango kwa fujo?’akauliza mama mweney nyumba. Na tibu wakati huo huo kijana wao ambaye alikatishwa maongezi yake, aliinuka na kuchungulia dirishani,halafu akawaangalia wazazi wake, wanavyohangaiak kutafuta panga.
‘Hapa hakuna usalama, akajisema moyoni. Akawaangalia wazazi wake, ambao hawakuwa na mawazo na yeye taratibu akaingia chumbani kwake, na kupanga vitu vyake kwenye mfuko wa safari, akahesabau akiba yake, huku akisema;
‘Wakati sasa umefika, …’akafungua dirisha na kuangalia nje, na kelele zilipozidi akarukia nje na kuanza kukimbia
****************
‘Usalama utoke wapi, wakati nyie mumejifungia huko ndani na yanayotokea huku nje hamuyajui, mnajifanya mpo peke yenu, sasa linalokuja kuwakuta sasa hivi mtapambana nalo wenyewe’sauti ikasema .
Mama mwenye nyumba akakumbuka kasuli na huyo mama ambaye mara kwa mara huja kumsuta,kuwa anajitenga na jamii, kuwa yeye hapendi kujishirikisha na wenzake. Yeye alijitetea kuwa anafanya hivyo kutokana na malekezo ya mume wake.
‘Mume wangu hapendi kabisa niwe ninatka toka nje, au kwenda kuongea kwa watu, ana wivu kweli kwelikweli, ‘akajitetea.
‘Huo sio wivu ni kutokujua kuwa ujirani ni kusaidiana, kuongea na kushirikiana katika mambo mbali mbali, na utajuaje matukio ya kijijini ambayo ni sehemu ya jamii, mkijitenga na nyie likiwakuta mtatengwa’akaambiwa. Na kila anapoambiwa na wenzake hujaribu kumshauri mume wake, lakini mume wake hakubaliani na kauli hizo .
‘Mimi nimeshakuambia wengi wao wanachotaka ni majungu, maana nyinyi mkikutana kazi kusengenyana tu, na mwisho wa siku wanakushauri mabaya, ‘akasema mume wake.
‘Lakini kuna shughuli nyingine za akina mama natakwia nishirikiane na wenzangu, nikijitenga huoni ipo siku kutatokea shughuli hapa nitatengwa na jamii’akasema.
‘Mimi ndiye mume wako, unachotakiwa ni kunisikiliza mimi, hawo hawatakusaidia lolote, angalai hali tuliyo nayo, ni nani aliyewahi kuja kutusaidia, angalai ulivyoumwa kipindi kile, ni nani aliyekuaj kukusaidia zaidi ya kaka yako, …hawo wanachotaka ni majungu tu,..’akasema mume wake.
‘Haya usije ukajuta, maana kuna leo na kesho, jirani yako ni ndugu wa karibu, kuliko ndugu mzaliwa nawe, kama hamuishi ndani pamoja,..’akasema.
‘Hayo maneno tu, mimi ndio mume wako basi…’amri ikatolewa na kweli mama wa watu akawa anajikali ndani hajishiriksihi na jamii, sasa leo inaonekana kuna jambo, na jambo lenyewe litawaumbua.
Mama yule aliposikia hiyo sauti na kumuona mume wake akihangaika kutafita panga, wakati panga hilo kaliazima kwa huyo huyo jirani, akaona atoke nje waongee, na ikibidi akalichukue hilo panga haraka kabla mume wake hajagundua. Akatoka haraka nje na kabla hajasema kitu huyo jirani yake akaanza kusema;
‘Jamani, kama inawezekana muihame hii nyumba, sijui kama kutakuwa na usalama, maana niliyoyasikia huko na kuyaona kwa macho yangu, yatahamia hapa muda sio mrefu..’akasema huku akiangalia muelekeo wa njia alipotokea, alionyesha kabisa ana wasiwasi.
‘Kwanza kanipe panga la watu, maana ninaweza kupewa talaka sasa hivi.’ Akasema huyo mama kwa sauti ya kunong’ona ,akimshika mwenzake mkono, ili waende nyumbani kwa huyo jirani.
‘Hakuna muda huo, ….panga lenu lipo, lakini nawapa kama tahadhari, ondekeni humo ndani, sio muda wa kujifungia tena, mambo yameharibiak huko’akasema huyo jirani kwa sauti, ili mume mtu asikie huko ndani,
‘Muulizeni huyo kidume chenu, mimi kila siku nawaambia kuwa kijana wenu mtafutieni mke haraka maana ataishia kuwaharibu mabinti zetu, nyie mnanikatalia kuwa eti kijana wenu ni muadilifu, sasa hilo alilolifanya huko ni kubwa lao, maana mumechokoza nyoka aliyejificha pangoni, sasa mtafute pa kukimbilia’akasema.
Mama Adam, alikumbuka mazungumzo yake na huyo mama aliyewahi kumwambia kuwa mtoto wake na upole wake anatembea na mabinti wa wenzake, na akamkanya kuwa siku akimkuta na binti yake, atamfanya kitu mbaya.
‘Lakini kijana wangu muda mwingi yupo shambani, anakutana vipi na binti yako,?’ akaulizwa.
‘Wewe una uhakika kweli kuwa muda wote yupo shambani, wakati uanjifungia ndani kama mwali, mimi nakuambia ipo siku mtaumbuka, na ole wale aje ampe mtoto wangu mimba, kutachimbika hapa, maana vijana hawa wa sasa hivi hawaambiliki, badala ya nyie kimpeleka mtoto shule mnamgeuza mkulima wenu, ngojeni awaletee kesi’akaambiwa.
Baada ya kusikia kauli hiyo wazazi hawa wakalifuatilia hilo kwa karibu, lakini hawakuona dalili kama hizo wakahisi huenda ni yale yale ya majirani, ambao kazi yao ni kuleta migogoro. Hata hivyo ikawabidi wamkalishe kijana wao kikao, ili wamuulize vyema, kwani pia kuna tetesi zimesikika kuwa yule binti wa jiarni yao, ambaye walikuwa naye karibu sana anaumwa umwa sana huko shuleni.
‘Kuumwa si kawaida mke wangu, hiyo haina maana kwua ana uja uzito,na kama ano tutakuwa na ushahidi gani kuwa ni uja uzito wa mtoto wetu, ili hali tumemuuliza kakataa kata kata’akasema mtu.
‘Mimi nakuambia hilo kama angalizo,maana ingelikuwa ni mtoto wa kike ungenibana mimi na kuniambia hilo ni jukumu lako, sasa huyo ni mwanaume,unatakiwa utafitii na ujue je ni kweli na kama ni kweli ujiandae mapema, maana unaifahamu hiyo familia’akasema mke wake.
‘Ushaanza kunitupia majukumu yako, wewe n imama yake unaweza ukajua mengi kuiko mimi, kwanza wewe umeyapata wapi hayo maneni, nilishakumabia kuwa sitaki majungu,…?’ akauliza.
‘Lisemwalo lipo, kamahalipo laja, mimi nimemuulizia na …niligundua jambo’akasita kusema
‘Jambo gani?’ akaulizwa.
‘Siku moja niliingi chumbani kwa kijana wetu huyu nikakuta barua , na niligundu kuwa ni barua alizokuwa akinadikiana na huyo msichana’akasema.
‘Sasa hayo si ya kawaida, kuandikiana barua hata mimi na wewe tulikuwa tukifanya hivyo, lakini sio sababu ya kumsingizia mtoto wake hayo. Lakini kama umeona hivyo, inabidi tumbane vyem a, maana hiyo familia sijui kama tutawezana,na sipendi kabisa kuwa na mahusiani na hiyo familia’akasema baba mtu.
‘Hupendi lakini wao wanapendana, huwezi kuingilia hayo, cha muhimu ni kutoa ushauri, mimi naona leo akirudi shambani tumbane vyema, tuake tuongee naye, ili tujue hatima ya kijana wetu, na kama inabidi akaanza huo ufundi haraka, …’akasema mama.
‘Sasa akirudi tutakaa na kuongea naye.
**********
‘Mbona sijakuelewa jirani, kuna nini kimetokea huko..?’ akaulizwa.
‘Huyo mtoto wenu anajua, kwanini hamumuulizi, kwani hajawaambia kuwa ameshawatayarishia mjukuu,mjukuu wa kujifunzia yupo mbioni,..lakini sijui kama mtawahi kumshika mikononi kwa amani,maana huyo binti mwenyewe, sijui kama atapona,…’akasema huyo jirani, huku akiangali kule alipotokea kwa wasiwasi na alitaka kuondoka hapo kwa haraka.
‘Tatizo lako wewe uanongea sana, tuambie ni nini kimetoka ili tujihami na sisi’akaulizwa na mwenzake
‘Mimi nawashauri kwa leo musikae humu ndani, maana kama ni kweli, huyo simba atafika hapa muda sio mrefu..’
‘Unasema Simba, ina maana mzee Simba, baba Maua kacharuka?’ akauliza baba mwenye nyumba kutokea ndani aliposikia hilo neno samba. Simba ni jina la jirani yao ambalo amepewa baada ya kupambana na simba.
‘Kacharuka kweli, na hilo linatokana na kijana wenu ndio maana …nawataarifu mapema, maana huyo samba akifika hapa kama asipokula nyama yenu mtaniambia, kama anataka kula nyama ya binti ake mwenyewe kwa uja uzito uliotokana na mtoto wenu, itakuwa nyie,…kijana wenu atafute sehemu ya kwenda, la sivyo, ….’huyo jirani akaanza kukimbia kuondoka hapo
Wazazi wakamgeukia kijana wao, lakini alikuwa hayupo ndani, keshakimbia, na hawakujua kakimbilia wapi, na kabla hawajajiuliza vyema, mara wakasikia kelele kwa mbali. Baba akachukua mkuki wake ambao huo nao umekwekwa kwa tahadari, tayari kwa mapambano.
‘Mume wangu hapa sio pa kukaa, usijidanganye na huo mkuki wako, wewe mwenyewe unamfahamu huyo mtu vyema kuliko yoyote, unakumbuka jinsi alivyokuumiza kipindi kile, ukijifanya kuingilia mambo yasiyokuhusu’akasema mke wake.
‘Mimi simuogopi, siwezi kukimbia nyumba yangu, kwa kosa nisilo lilijua, ngoja aje tupambane kiume, kipindi kile ilibidi niingilie maana mwanaume mzima unpiga mwanamke, tena dada yako kama unaua nyoka,…’akasema.
‘Haya msubiri hapo wewe mwenyewe, lakini mimi sikai hapa..’akasema mama mwenye nyumba huku akichukua baadhi ya nguo zake na kuanza kufungasha tayari kwa safari ya kuhama nyumba kwa muda,na mume mtu akawa analishikilia panga lake mkononi vyema akiwa akimwangalia mke wake.
Mara kelele zikaongezeka huko nje, na hapo Wote wakatoka nje kuangalia, ilikuwa ni mwanya kidogo tu wa kuangali ni nini kimetokea, na walipoona umati wa watu wakija kuelekea kwao, na mbele yao yupo huyo Simba, hakuna aliyemwangalia mwenzake, kwani kila mmoja alitafuta njia yake ya kukimbilia,…
Kila mmoja aliona miguu ni mizito, kwani mbio walizotoka nazo hapo hawajawi kukimbia hivyo kabla, na hawakujua wanakimbilia wapi, ilimradi zilikuwa ni mbio za kumkimbia Simba, kila mtu kwa muelekeo wake..
NB Haya maoni yenu yapo wapi?
WAZO LA LEO: Ujirani ni kitu muhimu sana,tushirikiane majirani na kujenga mahusiano mema, lakini ujirani usiwe chanzo cha kujengeana chuki ,wivu, fitina. Jirani mwema ni zaidi ya ndugu.
Ni mimi: emu-three
2 comments :
Yaani we acha tu!
Pole sana kwa kazi kaka, nikuulize kitu, hizo hadithi unazitunga saa ngapi?
Post a Comment