Adamu alimwangalia yule binti akiongea, na kuingiwa na hamasa naye, hasa pale alipokuwa akiongea kwa haraka haraka, kama redio iliyofunguliwa kwa mwendo kasi, Adam akawa anamwangalia huku akimsikiliza kwa makini, na kwa vile kulishapambazuka,aliweza kumuona vyema usoni. Kwa muda alikuwa keshaondoa ile khanga aliyokuwa kajifunika.Na nywele zake zilikuwa ndefu.zikiwa kama zimepakwa rangi,...
Adam
akamwangalia usoni, anavyotabasamu anavyobenua mdomo kwa dharau, kwakweli kila
kitu chake kilimvutia sana Adam.
'Huyuu binti mnzuri sana,mbona sijawahi kumuona kabla?' akajiuliza kimoyomoyo,na hapo hapo akamkumbuka binti rafiki yake wa shuleni, na kumlinganisha na huyu binti, akashindwa kutofautisha nani zadi, baadaye akamuliza yule binti;
‘Hebu niambie wewe ulifikaje Mererani, maana naona wewe unaonekana
ni mwenyeji huko, na unaonekana kufahamu mengi ya huko kama vile na wewe ni
mmoja wa wachimbaji wa madini, uliwahi
kuingia machimboni nini?’ akauliza Adam.
Yule binti akacheka kidogo, uso ukameremeta, halafu ghafla
ukawa unafifia, uso ukawa unabadilika kutoka kwenye tabasamu na kwenda kwenye
huzuni. Adam aliangalia yote yale, alimuona huyu binti kama wale waigizaji
aliowahi kuwaona kwenye sinema.
Yule binti alitulia kidogo kama anatafakari kitu, halafu
akamuangalia Adam kwa makini,na yale macho yake, gololi za ndani zikawa
zinazunguka, kama vile anamchora Adam. Macho yake yalikuwa makubwa yanayovutia, na yalionekana
kuwa na usiri mkubwa, au jambo ambalo limejificha ndani ya nafsi za huyu dada,
na huenda alitaka kuliongea lakini bado alikuwa na wasiwasi, Adam alihisi
hivyo, na pia Adam, aliingiwa na mawazo mengine kuwa huyu binti sio kuwa ana
mvuto, bali inaonekana kuwa ana kitu cha zaidi.
Adam, huwa ana kipaji cha kumsoma mtu, lakini yeye mwenyewe
hajijui kuwa yupo hivyo, hili alikuwa nalo tangu akiwa shuleni, alijikuta yupo
hivyo tu, kuwa anaweza akamwangalia mtu akamjua kuwa huyu ana kusudio gani, au
ana nia gani, huenda ikawa mbaya au nzuri, na kweli akimwangaia mlengwa ,huyo
mlengwa anasema kweli alikusidio hivyo. Hata siku moja alipomuuliza baba yake
kwanini ana hulka hiyo, baba yake akamwambia;
‘Binadamu tulivyo, kila mmoja kazaliwa na kipaji chake, na
hili utaweza kulifahamu kwa mtoto wako
akiwa bado mdogo, sisi wazazi wako tulikugundua hivyo, kuwa una kipaji fulani, tangia
ukiwa mtoto, na tulijua kuwa huenda kipaji hicho kikakusaidia kuwa msomi mzuri,
lakini tulishangaa, ulivyobadilika ghafla.
Kweli mwanzoni darasani Adam alikuwa akifanya vizuri sana,
lakini alipoingia darasa la tano akaanza kupoteza muelekeo, akawa akifika
darasani anaonekana kuwa na mawazo sana, na kidogo kidogo akaanza kushuka
kielimu, na ikifika mahali hata darasani haingii, kabisa, au anaweza akaonekana
mara moja moja.
Walimu walijaribu kumhoji, na hata kuwaita wazazi wake,
lakini haikusaidia kitu, ikabakia kusubiria amalize hilo darasa la saba
akabidhiwe kwa wazazi wake. Hii hali ilianza pale alipokuwa akirudi nyumbani na
kukuta wazazi wake wakigombana, au wakati mwingine anakuta ndugu kwa ndugu
wanagombana, baba yake na baba wengine, au wakati mwingine anakuta baba na mama
yake hawaelewani kwasababu hali ya uchumi ni ngumu, basi Adam akajiona hana
raha.
Haya aliyaongea siku baba yake alipotumia mbinu nyingi za
kumbana mwanae, baada ya kugundua kuwa kutumia nguvu, kwa kumchapa viboko
haikusaidia lolote, akaamua kutumia hekima, na kuwa karibu naye, na siku mmoja
kijana wake akamwambia baba yake kwanini hali ilifikia kiasi hicho, akasema;
‘Baba mimi nimebadilika kutokana na hali halisi iliyopo hapa
nyumbani, mimi sioni raha nikiwaona wazazi wangu mnataabika, kula kwa shida,
matatizo mengi yakugombea ardhi, wakati mwingine mimi nagombana na ndugu zangu,
nyie mnaingilia, unakuwa ugomvi mkubwa. Mimi naona ajabu sana wewe na ndugu
yako juzi mumegomabana kwasababu ya ardhi, sehemu ndogo tu, sasa nikaona labda
ni kwasababu ya umasikini wetu’akasema Adam.
‘Sio hivyo mwanangu, hayo yote ni kwasababu wote tulikaa
tukitegemea mali ya baba, urithi wa baba, baba yetu alikuwa tajiri sana enzi
zake, na kutokana na utajiri wake, sisi watoto tukalemaa, kila mmoja akiwa
anauchungulia huo utajiri, kuwa na mimi nimo, hatukutaka kusoma, na mama zetu
wakawa wanatukumatia kila mmoja na watoto wake,…hilo ndilo kosa tulilofanya.
‘Baba yangu alipofariki tu, tukaanza kugombea mali yake,
kila mmoja akidai haki yake na kuona anahitaji zaidi ya mwingine, haki ambayo
hatukuitolea jasho, na wala hatujui jinsi gani baba na wazazi wetu kwa ujumla walivyohangaika
na wake zao hadi kufikia hapo na kuitwa matajiri wa enzi hizo…
‘Maana baba yangu alikuwa na wake wengi enzi zake. Alikuwa
ni mmoja wa viongozi wa kabila letu, kwahiyo,pamoja na mali nyingi, pia
alitakiwa kuwa na wake wengi….alikuwa na mifugo mingi, mashamba , ambayo wake
zake walikuwa wakiyahudumia kwa bidii kubwa. Enzi zao wake walichaguliwa
kutokana na bidii zao katika kazi..
‘Hayo ni maisha ya baba yangu na enzi zake, lakini sio
maisha yetu, sio maisha yenu, maisha yetu, na sasa yenu yamegeuka, enzi zeni
bila shule utakuwa mtumwa wa wenzako,…usituige sisi kwasababu tulilemaa, kwa
vile hatukutaka kujiendeleza, hatukutaka kutafuta kwa jasho letu,ili tuweze
kukiendeleza kile alichokiacha baba yetu, ili kiwe kikubwa zaidi.
‘Mwanangu, hakuna kitu kinachorudisha maendeleo kama
kugombana, kama kuwekeana chuki, kwani ndani yake kuna adui shetani, ambaye
kawekeza kwenye ubinafsi, kila matu anaona kila kitu ni chake,na anahitaji
zaidi sio kwa kuhangaika,bali kwa kumdoea mwenzake,na kumuonea kijicho. Maana
sisi tulibakia kukigombea kile kidogo alichokiacha baba, kilionekana kidogoo
kwasababu ya wingi wetu, na hatukutosheka na mgawo, tukawa tunaingiwa na
husuda.
‘Mimi na ndugu zangu tukawekeana kijicho, kila mmoja sasa anataka
kuchukua haki ya mwingine, tukajenga uadui, ndugu kwa ndugu wa damu moja.
Kwasababu baba alikuwa na wake wengi, kwahiyo hata watoto walikuwa wengi pia,
na itikadi tofauti, na hilo lilichangia sana kukuza mgogoro. Mgogoro ukikita
kwenye itikadi ya mtu, unafanya mambo yanadumaa, hata akili ya kutafakari,
kutumia hekima, au kutumia ile elimu yenyewe ya itikadi ile
inasimama,kinachobakia mbele ni ubinafsi …ni hii ni hatari kubwa
‘Vita vya wenyewe kwa wenyewe vikazuka, …mwanangu usione
hivi kumepoa, hapa kulikuwa hakukaliki, kila mara kulikuwa na vita vya kupigana
mapanga mimi na ndugu zangu, kwa kosa dogo tu, ilimradi kila mmoja anatafuta
chanzo, ili aweze kumuondoa mwenzake, tumesahahu kuwa enzi za baba tulikuwa
tunakaa meza moja tunakula pamoja.
‘Enzi za baba ilikuwa kama sherehe, baba anatukutanisha
pamoja, tunakula pamoja, tunahadithiana hadithi , tunacheza, yaani kulikuwa na
raha ya aina yake, lakini mdudu mtu amekuja pale tu wazazi wetu hawo,
walipoondka duniani, kila mmoja na mama yake, kila mmoja na mambo yake,tukawa
tunaanza kunyosheana vidole na hata kuitana wachawi…tulisuluhishwa sana, na
baadaye sijui upepo gani umepita, wengi wameamua kutawanyika, kutafuta maisha
sehemu nyingine maana ile mali tuliyokuwa tukigombea imekwisha.
‘Ina maana baba, kumbe babu yangu alikuwa tajiri, na pia
mgogoro w augomvi wenu umatulia baada ya watu kutawanyika kwenda sehemu
nyingine kutafuta maisha?’ akauliza Adam.
‘Sio tajiri tu, baba yagu alikuwa mmoja wa viongozi wa
kabila letu, sisi ukoo wetu ni mashuhuri sana, lakini ulikuja kuharibika
kipindi chetu. Baba yetu alituacha tukiwa bado vijana, na mawazo yakuona mbali yalikuwa hayapo, kwasababu tulilelewa
kitajiri, kila tunachotaka tunapata, hatutaka kujituma zaidi.
‘Ndio maana mwanangu nataka usome ili uweze kuirudisha
heshima ya ukoo wetu, tunajua ukisoma ukawa na elimu, kizazi chako kitaiga, na
ukoo huu utasonga mbele, kuliko kuwa na tamaa ya mali ambayo kuipata kwake ni
kwa kubahatisha na hata ukiipata hutaweza kujua jinsi gani ya kuiendeleza, na
ili ujue hayo ni kwa kupata elimu safi.
‘Baba mimi akili yangu ni kuondokana na huu umasikini, na
sioni sababu ya kusoma, wangapi wamesoma lakini hali zao hazina tofauti na
mimi, na baba ukumbuke kuwa elimu yenyewe inahitaji pesa, siku hizi elimi bila
pesa hakuna, sasa hizo pesa mnatarajia tutazipata wapi, nasikia enzi za nyuma
wenzangu mlikuwa mkisoma bure, siku hizi hiyo haipo tena!’
‘Tutatafuta mwanangu,…tutachangishana, wanafamilia tupo,
kidogo kidogo utasoma’akasema baba.
`Sasa ina maana tuanze kuchangishana,wanandugu, wanandugu
wenyewe kula yao ni shida, wanandugu wenyewe hamuelewani, na hebu nikuulize,
mkishachangishana nikaamua kusoma, na bahati nifanaikiwa na kupata kazi, ni nan
nitamsaidia maana kila mmoja atakuwa na matarajio kutoka kwangu kutokana na
mchango wake alioufanya kwangu?’ Adam akamuuliza baba yake.
‘Ukisha pata elimu, ukapata kazi, utakuwa na mwanya wa
kuwasaidia wenzako kwa njia nyingi tu, kwa mfano unaweza ukawa kiongozi, kama
vile mbunge wa eneo letu, utakuwa na
nafasi ya kuwasaidia wenzako kwa mapana
zaidi, sio tu familia yenu tu, bali wilaya nzima, huoni ni faida kubwa sana,..’akasema
baba yake Adam, lakini Adam hakumuelewa.
‘Niwe mbunge,niwe meneja,lini…baba tuwe wakweli, angalia
majirani zetu, watoto wao wamesoma,nini walichofanya…wengine wamekuwa walevi,
wengine, ndio hawo, kila siku wapo wa mabarabarani, wamegeuka wanasiasa wasio
na jukwa, kila mahali kwao…baba mimi nipeni mwanya, mtaona wenyewe’akasema huku
akionyesha ngumi mbele.
Baba alimwangalia mtoto wake kwa muda, akiwa haamini kuwa
huyu ndiye yule mtoto wake aliyemuelewa, au ni mwingine, akatikisa kichwa, na kwa muda huo Adam,alikuwa akiendelea
kutikisa ngumi hewani
Adamu alikuwa mbali akiwazia mali, akiwazia kuchuma kwa
haraka ili aondokane na huo umasikini ulikithiri ndani ya familia yao, na
aliona sehemu muhimu ya kupatia hiyo mali ni huko machimboni. Na hili
lilijijenga pale alipomuona mjomba wake akiwa katajirika, ana miradi na ana
maisha mzuri, akaaona huko ndiko kwa kupatia maisha bora,
******
Adam alishituka toka kwenye mawazo ya familia yake, pale
yule mwanadada alipomshika bega, alihisi ulani wa mkono wa yule mwanadada, na
mwili ukamsisimuka, na akilini akawa anajiuliza, vipi mkono laini kama huo
ukaweza kufanya kazi, ina maana huyu mwanadada huko machimbo atakuwa anafanya
nini…
Yule mwanadada hakusema kitu kwa muda ule, alitulia kimiya
huku mkono ukiwa bado umeshikilia bega la Adam,
na Adam akatulia akisubiri, kuwa huyo mwanadada atasema lolote, lakin
hakuna neno, alilosema huyo mwanadada, alikuwa kimiya, alishangaa sana kuona
ukimiya huo wa ghafla wa yule mwanadada, kinyume na jinsi alivyomzoea kwa muda
huo mfupi waliokuwa naye, akahisi huenda hilo swali alilomuuliza mwanzoni
limemkera.
Huyu binti alikuwa akianza kuongea anakuwa kama redio
iliyofungulia kwa sauti ya kasi, huwa anaongea kwa haraka haraka bila kutulia, utafikiri
anaogopa muda utaisha kabla hajamaliza kile alichokusudia kukisema. Akageuza
uso na kwamwangalia moja kwa moja Adam machoni mwake, na akatabasamu, na kusema;
‘Adam hivi mimi unanionaje?’ Adam, akashangaa kwa lile
swali.
‘Nakuonaje kwa vipi…?’ akamwangalia kwa muda halafu
alipomuona yupo kimiya na huku kamkazia macho Adam akasema;
‘Mimi nakuona ni binti mrembo, na sioni kwanini usiolewe na
kutulia na mume wako kuliko kwenda huko Machimbo, ambapo nahisi kwa binti kama
wewe hakukufai’akasema Adam.
Yule binti akawa akawa anajiangalia kama vile anajikagua, halafu
akatulia huku kainamisha kichwa chini, alitulia vile kwa muda, hadi Adam
akahisi kuna kitu kizito ambacho huenda kakisema na kumkwaza huyo binti.
Adam, akajaribu
kurejea mazungumzo yake kichwani, jinsi walivyokuwa wakiongea, ili kuona kama
kuna kitu kakisema ambacho anaweza kukihisi kuwa ndicho kimesababisha hayo yote,
na ndipo akakumbuka hali hiyo ilijitokeza pale alipomuuliza huyo binti kama
aliwahi kuingia machimboni, na alikumbuka alipomuuliza hivyo, ndipo hapo huyo
binti alipotulia ghafla na kuwa kama anawaza jambo
Adam, akaona aliulize tena lile swali ili kuona kama ndilo
linalomfanya huyo binti awe hana raha, kwanza akamuangalia yule binti kwa
makini, na wakati huo huyo binti alikuwa kainama chini, na mkono mmoja kautumia
kama kushika kichwani karibu na macho, kama vila anataka kulala, lakini yale
macho yalionekena hayajafumbwa, ina maana alikuwa akiwaza jambo.
Baadaye yule binti akahisi anaangaliwa, akainua uso
kumwangalia Adam, halafu akatabasamu, na huku bado anamwangalia Adam usoni, na
wakawa wanaangaliana kwa muda bila kusema kitu.
Adam, hapo alihisi kitu kwenye mwili, wake, alihisi kitu
kwenye fikara zake, na kutamani kumwangalia huyo binti, na ile hali ikamfanya
yule binti ashikwe na aibu, na kuinama chini, halafu akainua uso tena na
kumwangalia Adam, na kusema;
‘Hivi mimi naonekana Malaya?’ akauliza swali ambalo Adam
hakulitegemea kabisa, na Adam, akaangalia pembeni kuwaangalia abiria wengine
waliopo humo ndani kama wamsikiea hiyo kauli, lakini wengi wao walikwua
wametulia, kila mmoja akiwa na mawazo yake, Adam, akageuka kumwangalia yule binti, aakmkuta kama anaangalia hewani,au juu,akionyesha kuwa mwingi wa mawazo, na Adam akasema;
‘Kwanini unaniuliza swali kama hilo, mimi sikujui vyema, na siwezi nikamwambia msichana mrembo
kama wewe neno kama hilo, kiujumla huonekani hivyo, ..kwanini umeniuliza
hivyo?’ akauliza Adam.
Yule binti akatulia na mara macho yakajawa na ukungu, na
ghfala machozi yakaanza kumtoka yule binti, na baadaye kwa haraka akayafuta na
kuangalai pembeni, hakusema kitu kwa muda, alikuwa kimiya kiasi kwamba Adam
alijiona mpweke, na ndipo akaona ni bora amuulize tena huyo binti, na kaba
hajauliza yule binti akasema;
‘Mimi naweza kuwalaumu wazazi wangu kwa haya yote, ingawaje
sio vizuri, kwani wao kwa muda huo walikuwa wakiona kuwa wanachonifanyia
ni sawa, na wanafanya hivyo kwa vile
wananipenda,lakini kumbe walikuwa wakinitumbukiza shimoni, shomo la tala, shimo
la moto….’ akasema huyu binti huku machozi yakiwa yametanda usoni, na ndipo
akaanza kusimulia maisha yake.
Ni mimi:
emu-three
2 comments :
Tulikumiso mkuu, usituache muda mrefu, maana moyo unashindwa kusubiri, kazi nzuri m3
yaani mpaka kufikia hapa nishasahau stori ilipoanzia manake nadani yake kuna stori za watu kama watano hivi,hata sielewi tena. labda ungekuwa angalau unamalizia stori ya mmoja mmoja au unaipeleka hadi pale itakapokutana na ya mwenzake ndio unasonga mbele, inshort umenichangaya sana natamani hata nisiendelee, ila stori inaonekana nzuri sana.
Post a Comment