‘Mume wangu nimechoka na kazi za hapa nyumbani, zimeniwia
ngumu sana, kama tusipopata mfanyakazi wa nyumbani, nahisi nitapatwa na wazimu,
na nitazeeka kabla ya muda wangu….’akalalamika mke wangu alipofungua mlango.
Nilimwangalia kwa macho ya huruma, maana alikuwa kachafuka,
na jasho linamtoka, kwani alikuwa akitokea jikoni, alipokuwa akifanay usafi, na
aliposikia nimekuja akaja kunipokea,….
‘Samhani mume wangu nimechafuka sana hata kukushika mkono
siwezi, ingia na mizigo yako uweke ndani, ..’akaniambia nami niliingia na
kuweka mizigo yangu,halafu nikarudi varandani, na baadaye alikuja na kusimama
mbele yangu.
‘Pole sana mke wangu na kazi za nyumbani….’nikasema.
`Pole na wewe na kazi za jukwaani, kazi za kupepeta mdomo,…’akaseama
na kucheka kwa zihaka.
‘Sasa mke wangu, nipe muda kidogo tuongee, maana najua
ukiingia huko jikoni hatutaongea ahdi jioni, na mimi ninaweza nikaitwa wakato
wowote, naomba tuongee kidogo’ nikasema.
‘Haya siasa zako zimeanza, ….ninakusikiliza, unataka kusema
nini tena, tukauze nini tena, maana sasa ndio zako unataka kuuza kila hata,
hata mimi unaweza ukaniuza…’akasema huku akijisogeza kwenye sofa,lakini
hakukaa, akasimama na kuniangalia kwa mashaka.
‘Nikuhusu hizikazi nyumbani na matatizo haya ya wafanyakazi
wandani…’nikasema.
‘Kwanini tusiwe na
wazo la kudumu, kwanini tutafute mfanyakazi ambaye mkataba wake haueleweki,….?’
nikauliza.
‘Kwahiyo unasemaje…?’ akaniuliza,nakabla sijasema hilo
nililopanga, akaanzakuzungumzia mambo ya siasa.
‘Kwanza alikuja yule rafiki yako wa zamani, adui yako, akanionya
kuwa nikuambai kuwa uachane na mambo hayo ya kisiasa maana yatakuweka pabaya,
nilimsikiliza kwa makini, ingawaje sikumwamini sana, maana huyu mtu hana heri
kwetu’akasema.
‘Achana naye huyo….kwanza alikuja hapa kufanya nini, ..sinilimpiga
marufuku kuja hapa nyumbani…au mna yenu ya siri nini…?’ nikasema kwa hamaki.
‘Mimi siwezi kumfukuza mgeni, alipita na gari lake la
kifahari, akaniona nipo hapo nje, akaniongelesha, na wala hakushuka kwenye gari
lake, akawa anabwabwaja maneno yake, yaliyokuwa yakiingia huku na kutoka huku..’akasema.
‘Huyo achana naye, tuongee maswala yetu muhimu…’nikasema.
‘Haya ongea na kusikiliza…ila kama ni hayo ya kisiasa
sitayaunga mkono tena, kama hujakoma ubishi, endelea nayo, sasa hivi pesa
hatuna, mali zote tuliuza, na tuna madeni ya kufa mtu, bado hujakata tamaa,
mimi sasa sihusiki tena, maana ulishaanza kunitupia lawama mimi, safari hii
utafanya utakavyo, mimi simo….hebu niambie, utafanyaje na wewe huna pesa,
kumbuka nyumba hii ipo chini ya dhamana ya deni la watu…’ akasema akionyesha
kukata tamaa.
‘Sikiliza mke wangu nikupe wazo moja, nahisi hilo
ukilifikiria kwa makini tunaweza
tukayatatua haya yote yanayotukabili. Mimi kuna wazo nimelipata, na wewe
ukiliwaza kwa makini tunaweza kupata ufumbuzi…’nikasema.
‘Wazo gani, kuhusu nini…?’ akaniuliza.
‘Kuhusu unavyolalamika hapa nyumbani ,najua kazi ni nyingi,
najua jinsi gani unavyotaabika, sasa tulitafutie ufumbuzi wa kudumu….’nikasema.
‘Haya ufumbuzi gani wa kudumu….?’akaniuliza.
Mke wangu akatulia
akiniangalia kwa makini, akijaribu kutafakari, nini ninachotaka kumwambia,
akasema kwa haraka
.
‘Unajua mke wangu, wewe una akili sana, una hekima sana,
mimi nimeliwaza hili, naomba utumie hekima na akili ya kulitafakari kwa makini,
kwasababu, ….kwanini tutafute mfanyakazi ambaye mkataba wake haueleweki, siku
mbili tatu kakimbia,….sasa tuna mambo mengi sana ya kufikiria, ukiangalai haya
mambo ya kisasa, mimi natakiwa nitulize kichwa kwenye mambo hayo, mwaka jana tulikosa
ubunge kwa kutokuwa makini,lakini bahati nzuri, nafasi hiyo ipo wazi tena,
tusifanye makosa hayo tena, …’nikasema.’
‘Kwahiyo unataka kusema nini, kuwa muwazi, usilete siasa
zako hapo ndani, hapo sio kwenye jukwaa la siasa, maneno mengi, hayatanisaidia
mimi,napoteza muda wangu….jikono kunanihitaji, sasa hivi utaanza kulia njaa,..?’
akaniuliza mke wangu.
‘Mimi nimeonelea tutafute mtu wa kudumu, ..badala ya hawa
watu wa kupita, tukipata mtu wa kudumu ambaye atabeba majukumu kama
mwanafamilia hakutakuwa na shida tena, ….yeye atakuwa na uchungu wa mambo yote
ya hapandani, hata tukitoka hatuna wasiwasi,….angalia hapa ilivyo, wewe
unakwenda kazini, huku nyuma tunamuaha mtu ambaye hatuna imani naye sana, na
mimi nadumkia kazini, lakini huyo tutakaye mtafuta anakuwa kweli ni mwenye
uchungu na familia, maana kutakuwa kwake…’nikasema.
‘Mimi bado unanichanganya, ina maana tuchukue ndugu,…au unasemaje…i?’
akaniuliza huku kashika kiuno na usoni kulijaa kulionyesha kuwaza.
‘Nina maana kuwa badala ya mfanyakazi wa nyumbani , ni bora,
tukamtafuta mtu wa kudumu, kwa mfano tukitafuta mama wa nyumbani….ambaye
atakuwa msaididzi wako huoni itakuwa ni vyema kabisa…?’ nikawa kama namuuliza.
‘Mimi bado sijakuelewa, mama wa nyumbani…..!?’
akashikakichwa, akitafakari,halafu akasema;
‘Una maana gani,…maana sikuelewi, sisi hapa tunazungumzia
swala la mfanyakazi wa ndani, kwanini hawatulii, kila mfanyakazi akija hapa anakaa
wiki mbili anaondoka, huyo ambaye
nilijua kabisa atakaa kwa muda mrefu kwani tulimuahidi kumpa mshahara mkubwa
naye kaondoka, kadanganywa na hawa wanaume wanaorubuni watoto wa watu, mwisho
wa siku wanawatelekeza, ….nyie wanaume mna dhambi kweli....’akasema mke wangu
‘Mke wangu nataka unielewe, sina nia mbaya, na wala sisemi
haya kwa kuwa nimeamua iwe hivyo, nalitoa hili kama wazo ili tulijadili, wapo
wamefanya hivyo na wametulia, hawana shida, kinachotakiwa ni wewe urizike, uwe
na amani, ….na kuwa mke mwanza sio kitu kibaya….’nikainuka nakumsogelea.
Mke wangu alishituka nilipotamka hilo neno mke mwenza, kwani muda wote huo alikuwa
bado hajanielewa, aliniangalai kwa macho yaliyotoka kama vile kasikia jambo
laktisha, na ghafla nikashitukia kofi la nguvu likiingia shavuni mwangu.
‘Yaani kumbe ndio maana yako hiyo,….kumbe ndio maana
umebadilika kiasi hicho, kumbe…ooh,mungu wangu, ….siamini hayo maneno yako, na kofi
hilo likufundishe adabu, maana naona sasa kumbe umeshanichoka …’akasema huku
macho yakianza kulowana machozi.
‘Mke wangu sikuwa na nia mbaya, ni wazo tu….’nikasema
nikijarubu kumsogelea, yeye akanyosha mikono mbele yangu kunizuia nisimsogelee.
‘Nisikilize kwa makini, kama umenichoka, nipe talaka yangu, mimi nipo
tayari kurudi kwetu,…sio lazimaniishi na wewe, na hata hivyo mimi sasa ni mtu
mzima ninaweza kuishi maisha yangu, nikajitegemea, ….najua unajiamini kuwa
sitaweza kurudi kwetu, kwasababu niliondoka bila wao kurizika, kwahiyo
hawataweza kunipokea, hata kama mama atanisimanga, mimi naweza kujitegemea
mwenyewe, sishindwi kuishi kivyangu,…..’akasema na kuniangalia kwa hasira, na
nilipojaribu kufunua mdomo, akageuka na kukimbilia ndani…nakajua sasa
nimelikoroga.
Nilibakia nikiwa nimeshika shavu, ….nikiwaza hilo kofi,
kwani hilo kofi lilikuwa ni la pili, maana huko nilipotoka nilisha zabwa kofi
jingine la aina yake. Lilikuwa sio kofi la mkono, bali ni kofi la moyoni, kwani
pale nilipogundua kuwa jina langu halikupita kwenye wabunge waliopitishwa ili
wakapigiwe kura, lilikuwa ni kofi ambalo sikulitegemea. Sikuamini maana
nilipoteza pesa nyingi sana, kuhakikisha nipo kwenye uchaguzi huo,…na hata wale
wahusika wakuu walishaniambia kuwa jina langu litapita tu kwenye mchakato huo,
maana nilishapitishwa mwanzonu, na mimi ndiye ninayestahili kutetea nafasi hiyo
tena.
*******
Nilijuta kwanini nilitoa wazo hilo ambalo alinishauri rafiki
yangu mmoja, aliniambia kuwa kazi hii ya siasa inahitaji matulizo ya moyo,
sitaweza kuimudu, kama nitakuwa na matatizo ya kifamilia, akanishauri kuwa yeye
alikuwa na tatizo kama hilo, akashauriana na mkewe wakakubaliana watafute
msaidizi, na mkewe akasema yeye atamtafuta mke mwenza ili wasaidiane kazi.
‘Haiwezekani, yaani mke wako atoe ushauri kama huo,
ulimwamini kweli, isije akawa na yeye kakuchoka anatafuta mbinu za
kukutema…..’nikamwambia huyo rafiki yangu nikionyesha mshangao.
‘Inawezekana, kwanini isiwezekane, hutaamini, maana hata
mimi alipotoa ushauri huo nilijua ananitania kunitega, …yeye mwenyewe
akamtafuta mke mwenza, na alimtafute mke kweli, sio kwasababu anatafuta mke
mwenza, labda angelitafuta mtu ambaye hatamuonea wivu, …hapana, yeye alitafuta
kimwana wa nguvu, …mrembo,….nikamuoa’akasema rafiki yangu.
‘Ina maana yule mke ulitafutiwa na mkeo?’ nikamuuliza.
‘Ndio watu hawaamini, lakini ndivyo ilivyokuwa, na wanaishi
kama mtu na mdogo wake, wanapendana isivyo maelezo, ukiwaona utafikiri ni
ndugu, na wanavyofanana, watu wanasema labda ni mtu na mdogo wake, ….’akasema
rafiki yangu akiwa kashika kitambi chake,ambacho kiliiuka ghfala abada ya kuoa.
‘Mhh, mimi siamini, ….niende nikamwambia mke wangu kuwa
tutafute msaidizi, na msaidizi huyo awe mke
mwenza, sijui, kama kutakalika’nikasema.
‘Unajua kuna kitu ambacho tunashindwa kujua, …kila jambo
linahitaji hekima yake, na jinsi gani ya kuliongelea, cha mhumi ni kuongea,
kaeni muongee, sio kwamba nawashauri kuwa iwe hivyo, hapana, ila inawezekana,
kwasababu ….’akatulia kwa muda kama anawaza jambo.
‘Kwasababu kama unaweza kumchukua mafanyakazi wa ndani, na
mtu mwingine na familia yako mkaweza
kuishi bila matatizo, kwanini ishindikane kumchukua mke msaidizi,
mkashirikiana, ilimradi kuwe na maelewano, inawezekana rafiki yangu kajaribu
kuongea na mkeo, wewe ni mtaalamu wakuongea, kama unajimudu….nina maana
uwe kweli unaweza,
inawezekana’akaniambia na mimi nikajikuta naingiwa na wazo hilo ambalo sikuwa
nalo akilini kabisa.
‘Nitajaribi kumshauri mke wangu, ….kama akikubali, basi najua
tutakuwa na nguvu mpya kwenye familia, na kama ….nitamchukua yule yule wa kule
maeneo…’kabla sijamaliza kuongea wakaja
marafiki zangu wengine na tukaanza kujadili mambo ya kisiasa.
********
Nilibakia nikiwa nimeshika shavu, ….hili kofi lilikuwa la
pili maana huko nilipotoka kwenye kikao cha kisiasa, nilisha zabwa kofi jingine
lililopenya hadi akilini, lakini ofi hilo halikutoka mkononi mwa tu, lilikuwa kofi
lisiloonekana, lenye maumivu yakipekee kabisa ambayo yalikuwa makubwa zaidi.
Katika uchaguzi huu baada ya matokea kutenguliwa,
nilitarajia kuwa jina langu lingelipitishwa tena, lakini haikuwa hivyo, kwani
jina langu lilienguliwa kimizengwe, sikutakiwa nikagombee nafasi hiyo ya ubunge
tena.
Sikutarajia iwe hivyo, maana nilishapoteza
pesa nyingi sana , isitoshe hata wale wahusika wakuu walishaniambia kuwa jina
langu litapita kwenye mchakato huo, nisiwe na wasiwasi. Niliposikia kuwa jina
langu limeenguliwa, niliishiwa nguvu, na nilianza kuhisi yale maumimvu ambayo
hutokea mara kwa mara ninapokwazika.
Nilimuangalia yule mzee ambaye ni mmoja wa viongozi wakubwa
wa chama na ndiye aliyekuwa mtu wangu muhimu huko kweye ngazi kubwa, na nilijua
akiongea yeye unasikilizwa, nikajau kuwa yeye ndiye nafasi yangu ya mwisho,
akishindwa yeye tena , basi, nikamwangalia kwa macho ya huzuni, naye akasema;
‘Sikiliza kiongozi, wewe tafuta pesa, haya matokeo ni ya
awali, walikaa wakubwa wakapitisha hawo watu wao, lakini wewe una haki ya
kuendelea kutetea nafasi yako, sisi tutakaa na hawo watu tuone jinsi gani ya
kuweka mambo sawa,.. tutayabatilisha hayo maamuzi yao, maana naona kuna watu
wanataka kutuingilia, ila….’akatulia kama anawaza jambo.
‘Tunahitaji nguvu,… maana huku kwenye kikao kikubwa ndipo
tunaamua ni nani anatufaa, mimi nitajenga hoja kuwa wewe ndiye unayestahili kuutetea
nafasi yako na hata kura ulizopata zilikuwa karibu sawa na huyo aliyekuwa
kashinda kinamna,sioni kwanini wakutoe, nitakupigania kwa guvu zote, wewe ni
kiongozi wetu mtarajiwa bwana, unastahili kuwa kwenye nafasi hiyo.….’akaniambia
huyo mzee.
‘Lakini kunahitajika pesa, pesa nyingi…hili sio swala la
mchezo, na ujue hapo unatafuta maisha yako ya baadaye, najua jinsi gani
ulivyopigika kweney huo uchaguzi, una madeni una mambo mengi ya kujiweka sawa
tena, nafasi hiyo ukiikosa tena , utaathirika sana, na hata hivyo wewe unafaa
sana kuwa kiongozi cha muhimu hakikisha huwi na kashifa yoyote, mimi
nilishakuoan siku nyingi wewe ni kiongozi mtarajiwa, nyota yako ni ya uongozi
inang’ara,,…na ukipita hapi najua kabisa utakuwa mbali, wewe unastahili kuwa
waziri…’akaniambai mzee huyo.
‘Pesa….pesa, mzee ninakuelewa sana, lakini ukitaja pesa kwa
sasa, sijui nifanyeje, maana kuwafuata hawo watu wangu tena, naona aibu, na
sijui kama watanielewa tena. Kwahiyo tusema huko kwenye kikao zinahitaji kama Shilingi
ngap..i?’ nikauliza huku nikiwawaza wafadhili wangu.
‘Milioni kumi, kwa yule bwana, kumi kwa watu moja mbili
tatu, wale wengine tano tano zinawatisha,…mmh, tusema kwa sasa ukipata milioni
arubaini hivi, tutaweza kuweka mambo sawa, ….’akasema kama vile anataka pesa
ndogo sana.
‘Ukinipatia hizo pesa, nitaweza kuzigawa kwa watu wangu, ….hiyo
sio rushwa, elewa kijana hiyo ni pesa itakayowasaidia wao kupoteza muda wako
kukusaidia wewe,….halafu baadaye tutatafuta milioni thelathini nyingine kwa
ajili ya watu maalumu wa kampeni,….’akasema kama vile kwake pesa kama hizo ni
ndogo sana, sijui alikuwa akinielewa vipi, kuwa labda mimi nina ushirika na
freemason, au nina kisima cha mafuta, nilimwangalia kwa macho ya wasiwasi.
Mzee sijui, ngoja nikahangaike, maana siunajau tena, yote
hayo nategema wafadhili, wao wakikubali,basio tutaangalia,,lakini mzee nakuomba
usiniangushe, maana hizo pesani dhamana ya watu, ni deni kwangu…’nikasema.
‘Usiwe na shaka,sisi ndio wenyewe,….jina nitahakikisha
linapita, ila nakuomba tena, hakikisha kuwa huwi na kashifa nyingine
yoyote…haya mambo ya pesa, ni mambo ya kawaida ni gharama za uendeshaji na
mambo ya kawaida, tunajau jinsi ya kuyaweka sawa, lakini kashifa mbaya zitakazo
igusa jamii, mimi sitaweza kuzizuia….uwe makini sana…’akasema na tukaagana.
*******
Nilipotoka kwenye kikao na yule mzee ikabidi nichakarike, nianze
kiguu na njia kuwatafuta wafadhili, nikawa sikai nyumbani, nikauza gari la bei
mbaya, nikawa natumia gari la kawaida, na nyumba ya mke wangu nikaiuza pia, nyumba
ambayo aliijenga kwa mkopo wa benki, nikijua hayo yataisha na pesa itarudi
tu,…tulikuwa na biashara nyingine za masafaambazo alikuwa akizisimamia mke
wangu, nikajua hizo zinaweza kutusukuma.
Baada ya kuhangaika nikafanikiwa na pesa hizo nikamkabidhi
huyo kiongozi na nikajua mambo sasa yapo kweupe, huko mbeleni kwenye kampeni,
mambo yatasimamiwa na chama, nilihitajika kuwa na pesa za kawaida tu, sio kama
ule uchaguzi wa mwanzo. Nilipofanikisha hilo kwa siku hiyo nikarudi nyumbani
nikiwa na furaha zawadi tele mkononi, na nikiwa na wazo hilo la kupata
msaidizi, na masaidizi mwenyewe ni mke mwenza, …
Msaidizi na msaidizi mwenyewe ni mke mwenza, ….nikawaza huku
nikiangalia juu, nikaziangalia zile zawadi nilizokuwa nimeziweka juu ya meza,nikaziona hazina maana tena,….
Nikashika shavu langu nikiumia kimoyomoyo, nikiwaza nini
kinachoendelea huko kwenye kikao maalumu,kikao cha kupitisha majina ya mbunge
atakaye pamabana kweye uchaguzi wa pili. Moyoni sikuwa na wasiwasi,…nikatulia
na mara simu ikalia,…..
Niliogopa kuipokea, sijui kwanini,ingawaje muda mfupi
uliopita nilikuwa nikipokea simu kwa haraka, nikiwa na hamasa kuwa nitasikia
kuwa jina langu limepita,…lakini kila aliponipiga rafiki yangu huyo, ikawa
naambiwa mambo bado,nisiwe na shaka…sasa simu hiyo, huenda ndio yeye, huenda
mambo yameshakamilika,…naikaichukua ile simu, nilipotizama nikaona aliyepiga ni yule rafiki
yangu wa zamani ambaye sasa namuita adui yangu.
Nikataka nisiipokee, niikate, lakini baadaye nikaipokea,
nikamsikia rafiki yangu huyo,akihema kama kawaida yake, maana sio yule jamaa
niliyemjua, sasa hivi ni bonge,kashiba mwili mzima, na kilo zake ni mia kwenda
juu, akasema kwa kwa lugha, lafudhi ya kiingereza. Sasa hivi ni mkurugenzi wa
kampuni kubwa sana ya kimataifa….
‘Nasikia weye, unataka kuingi-ya kwenye kinyang’anyiro
tena,…hujakata-tamaa, hujasalimu amri,sio, nakushawu-uri weye-kama rafiki yangu
wa zamani, acha-ana na hiyo nafasi maana utaumbuka ….very bad…’akasema.
‘Umeanza vitisho vyako tena, niumbuke kwa lipi, mbona wewe
hujaumbuka licha ya kugundulikana kuwa wewe ndiye uliyerubuni hadi huyo mtu
wako akapita…’nikasema.
‘Sikiliza mimi sio mtu wa mchezo, nikikuambia hivyo nina
maana yangu,…kama hutafanya hivyo safari hii nahakikisha unakwenda chini,…na
mke nachukua, siunajua zile zangu za zamani,….nitahakikisha utakuwa omba omba, ….’akatulia
na kucheka kicheko cha kebehi.
‘Usinitishe wewe….’nikajipamoyo na kusema.
‘Sikutishi, ila ndivyo itakuwa,….kumbuka madeni uliyo nayo,
kumbuka mapesa uliyoyamwaga,ulipojiingiza kwenye mambo ya siasa kichwa kichwa,
wewe unauza nyumba,magari,…toka lini ukafanya hayo kwa mali yako, vitu kama
hivyo unatafuta matajiri kama sisi, wenye pesa, tunaotaajia kukutumia
baadaye,lakini weye, ukatoswa….sasa angalia maana hayo, yote tunayo kwenye
kumbukumbu zatu, kama ushahidi ikibid kwenda mhakamani, lakini hiyo haitoshi,
….’akatulia, na mimi pale moyo ukaanza kwenda mbio, nikashika ubavuni, sijui
kwanini hali ile ilikuwa ikinitokea.
‘Wewe ni mume na una mke mwema mstaarabu, na tulitaraia
ungelikwua mfano mwema ,…kiongozi mwema ni yule anayejali familia yake, ..wewe
una mke, lakini hujatosheka na mkeo,
…unakumbuka kile kikao mlichofanya kule makao makuu, mkanywa na kupitiliza,
ukifurahia ushindi ambao haukuwepo, kumbuka yule mwanamke uliyekuwa naye,
ambaye sasa unamtaka awe mke msaidizi…mlifanay nini naye siku ile…..’akasema na
mara mlango wa chumbani ukafungulia. Mke wangu akawa kasimama mlangoni huku
akiniangalia kwa macho yaliyojaa hasira.
Nilitamani niizime ile simu, lakini nguvu za mkono zilikuwa
zimekwisha, maana nilikuwa nimeishika kwa mkono wa kushoto, na mkono huo ukawa
hauna nguvu tena, ulikuwa kama sio wangu….nikawa kama mtu aliyeganda, na maneno
yaliyofuata hapo, kutoka kwa huyo rafiki yangu, yailikuwa kama mtu ananichoma
kisu moyoni,pigo moja baada ya jingine …..maumivu makali yakatanda ubavuni mwa
kushoto,….nikahsi kichwa kikuma maumivu makali yasiyo ya kawaida, nilichosikia
kwa mara ya mwisho ni yale maneno ya
huyo rafiki-adui yangu,yakisema;
‘Ikipita saa moja, kabla hatujasikia kauli yako ya kujitoa,
kwanza kabisa namtumia hizo picha mke wako,na ukumbuke ana shinikizo la damu ya
kushuka, akiziona tu, sizani kama atahimili mapigo, unakumbuka mliyoyafanya na
yule mwanamke, ambaye kakubuhu ufusuka,….sasa jiulize kweli unampenda mkeo, au
ulimuoa tu, ili kuninyima mimi mwenye haki naye…’akatulia na kukohoa.
‘Wewe una haki naye kwa vipi..?’ nikamuuliza kwa sauti ya
kukwaruza, kuonyesha kuwa nguvu za mwili sio zangu tena.
‘Huyu mrembo anahitaji watu wenye pesa kama sisi, anahitaji
kukaa kwenye raha, sio hapo anaishi kama mfanyakazi wa nyumbani, huoni kuwa
ilikuwa na haki yangu, …’akasema na kutilia.
‘Sasa tusipotezeane muda, unaamua lipi, nianze kwa kumtumia
mke wako hizp picha, au nianze huko kwenye kikao, au nianze huko ukweni, au kwa
wazazi wako,….amua moja haraka…’akasema kwa hasira.
‘Sikiliza,hilo unalotaka kulifanya ni uwoga,inaonyesha jinsi
gani mlivyo wazaifi kisiasa, acheni tupambeane kwenye majukwaa, sio kinafiki
namna hiyo, na njia hiyo haionyeshi kukomaa kisiasa’nikajitahiki kusema.
‘Kumbuka yale uliyokuwa ukifanya, je hayo matendo
yanaonyesha kukoamaa kisiasa, je ndio mtawala bora huyo tunayemtegemea katika
nchi yetu hiii takatifu, mtawala fusuka,..kweli kwa tabia kama hiyo,utaiweza
nchi kama hii, kama sio kubadili wake kama nguo, na kuzaa watoto wengi wa nje…
je huko ndio kukomaa kisiasa…,nakuulizawewe….au utaoa kama watawala wa mababu
zetu, waliokuwa na wake kumi kidogo, na ni heri ungelioa, lakini hayo uliyokuwa
ukifanya ni umalaya…au tutauitaje?’ akatulia.
‘Fanya unalotaka kufanya bwana, maana hata kama nikitoa
kauli yangu,nitahakikishaje kuwa hamtufanya hayo mliyoyakusudia,..’nikasema kwa
kujipa moyo.
‘Sawa kama umejiamini hivyo, ..kwanza naanza kukutumia wewe
mwenyewe, hebu fungua huo ujumbe kwenye simu yako..’akakata simu na kweli
baadaye uliingia ujumbe. Kwa hali nilyokuwa nayo, nilishindwa hata kuinua mkono
wangu wa kushoto, sikujua ni kitu gani kimenipata. Jasho, woga, na wasiwasi
vikaniandama na hali hiyo ikazidisha shinikizo la damu.
‘Hivi wewe una nini….?’ Akaniuliza mke wangu akiwa na
wasiwasi.
‘Hakuna kitu, ni huyu mshenzi ananitishia,…’nikasema na kwa
haraka nikatumia mkono wangu wa kulia ambao ulikuwa na nguvu, na kufungua ule
ujumbe ulioingia kwenye simu,picha ilionekana wazi kabisa…ilikuwa haifai
kutizimwa,…. nikahisi mwili ukiisha nguvu, nikamwangalia mke wangu ambaye
alikuwa akinisogelea kwa taraibu, kwa haraka
nikajaribu kuufuta ule ujumbe, lakini simu ikawa haikubali, jasho likawa
linanitoka kama mtu aliyemwagiwa maji ….
‘Mbona unahangaika hivyo, kakutumia nini huyo mtu ….?’
Akaniuliza mke wangu huku akiwa tayari keshanikaribia, na nikajaribu kuiweka
ile simu mbali na macho yake na muda huo huo simu ikaita tena, na bila kujijua
nikawa nimeipokea, na kujitutumua hadi nikawa nimekaa mbali kidogo na alipokuwa
kasimama mke wangu, nikaanza kusikia huyu jamaa akinimaliza kwa maneno yake …
‘Umeiona hiyo, sasa hiyo ni ndogo yake, sasa hivi ninamtumia
mkeo picha ile mbaya yake, ili aone nini ulichokuwa ukikifanya….’akasema .
‘Sikiliza wewe maaluni….nita….nita….’kichwa kikawa
kinagonga, mwili nikaanza kuhisi vibaya.,yeye huko akawa aanongea, na
nilishindwa kabisa kuizima ile simu….mke wangu akawa ananiangalai
ninavyohangaika, lakini hakufanay kitu, akawa katulia akiniangalia .
‘Mkeo, mkweo na wajumbe kwenye huo mkutano wataziona hizo
picha, na kesho magazeti yote yatapamba picha zako,….yote uliyokuwa ukiyafanya na huyo hawara wako, yatajulikana kwa watu wote hasa wa huko kwenye
jimbo lako, nakupa nusu saa ya kuamua…. ‘akatulia.
‘Unachotakiwa kufanya ni kutoa kauli yako ….kuwa umejitoa,
….kuwa kwasababu za kiafya umeona hutaweza kugombea tena huo uchaguzi,
utajiokoa wewe na mkeo, na ….’nikawa sisisikii kabisa anachoongea,…giza nene
likatanda kichwani, na kilichofuata ni zile kumbukumbu za siku ile, siku ile
ambayo nilifanay jambo ambalo nililijutia maishani, na kumbe lilikuwa
limepangwa, ….
‘Mume wangu jamani vipi, nisaidieni jamani huku….’ilikuwa sauti ya mke wangu, lakini
sikuweza kusikia zaidi ya hapo, nikapoteza fahamu.
NB Je ilikuwaje tuwepo kwenye sehemu ijayo, ili tuone nini
kilitokea…
WAZO LA LEO:
Usizani kila anayekuchekea ni rafiki yako,…
Ni mimi:
emu-three
8 comments :
Ungemuongeza kofi jingine.Safi kama ingelikuwa mimi kusingelikalika.
Maana najiuliza kwanini msaidizi mpaka awe mwanamke, kwanini hakusema, atafute mwanaume wa kusaidia kazi, kwani haiwezekani. Kama hakutaki akuache tu, kwanza mtu mwenyewe keshazini nje, ndoa ipo kweli hapo?
M3 endeleza basi kidogo, umeachia patamu!
Mimi nauliza swali, hivi mtu akizini nje ya ndoa , ndoa bado ipo?
Watu wa dini zote hebu nisaidieni hili swali au tatizo, maana watu wanatoka sana nje ya ndoa, na kama ndoa hazipo basi ina maana ndoa nyingi zimeshavunjika au nimekosea
Na wewe , M3 unaweza kuchangia.
Mimi mama N.
Duh Kaazi kwelikweli hapa..na kweli wote wakuchekeao si marafiki..Pamoja daima.
Weweeeeeeeeeee, napenda weye!
Duuuh, patamu hapooo!
Kwanza hakuna kitu kinachoitwa kuzini nje ya ndoa, kuzini au uzinifu maana yake ni kufanya tendo la ndoa nje ya ndoa. Kwa waislamu ni hivi mtu akizini yaani hana ndoa na adhabu yake ni kupigwa mawe mpaka afe, awe mwanaume au mwanamke.
Tukirudi kwenye uwepo au kutokuwepo kwa ndoa baada ya tendo la uzinifu, mimi ninavyoona hakuna ndoa kati ya maiti na mtu mzima. Maana mtu anapoamua kuzini anajiweka kwenye kundi la wafu. Sasa sijui hao masheikh wanasemaje, jaribu kuwauliza je kuna ndoa ikiwa mmoja wa wanandoa amezini? Nadhani watakachokifanya ni kuzunguka zunguka kutafuta justification lakini ndoa hapo hakuna.
Wazo la leo ni zuri sana kutokana mazingira tunayoishi makazini, majumbani, na kwenye jamii kwa ujumla...Tuko pamoja sana M3
kwa kweli kama mwenyezi mungu angekuwa anaumbua watu wanaotoka nje ya ndoa, kwa kweli wangeumbuka wengi. mana ndoa za sasa ni kizaazaa mpka sisi ambao bdo kuolewa tunaogopa kuolewa.Rafiki mkia wa fisi ukimshiriki atakufilisi. wazo la leo nimelipenda sana. naweza sema swadakta..
Post a Comment