‘Nilikuwa natoka kazini, nilichelewa kutoka na wenzangu wote
walishandoka, na hata mlinzi alikuwa hayupo, aliniomba kuwa anakwenda kununua
chochote kwa ajili ya chakula chake cha usiku , na nilipoona anachelewa,
nikatoka nje kumwangalia, sikumuona kwa muda huo, nikaona nisirudi tena ndani,
nikamsubiri hapo hapo nje, nikiwa nimeegemea gari langu….’akatulia kidogo akimuchia
nafasi yule askari usalama amalize kuandika maelezo yake.
‘Mhh, halafu ikawaje…?’ akauliza yule askari mpelelezi.
‘Mara pikipiki mbili zikaja kwa mwendo wa kasi, …niliziona
zikija kwa nje,maana pale nilipokuwa niliweza kuona sehemu kubwa ya nje, hasa
barabarani….nilijua zinapita lakini mara zikaingia kwa kupitia kweney geti
letu….’akasema na kutulia na yule askari kanzu akauliza.
‘Ina maana geti lilikuw awazi?’
‘Geti nilifungua mimi, nililifungua ili mlinzi akija nisipoteze muda,
kumbe ndio niliwapa nafasi ya hawo wenye pikipiki kuingia bila shida. Sijui
walijuaje kuwa lipo wazi, au ndio walibahatisha tu, kwani walichofanya, ni
hivi, Yule mwendesha pikipiki wa mwanzoni aliusukuma ule mlango wa getini , huku
akiwa anaendesha, na kwa vile geti lilikuwa kama limefungwa, lakini niliegesha,
tu, akasukuma kwa pikipiki na mguu, ….na kuingia moja kwa moja,na huyo wa pili
akafuatia kwa nyuma na wote wakaja usawa ule niliposimama….
‘Hawa kusimamisha mapikipiki yao…?’ akauliza huyo mtu wa
usalama.
‘Walikuja uswa wangu, wakanipita na kuanza kunizunguka, huku
wakiyavurumisha kwa sauti, wakawa wananizunguka na pikipiki yao, kama mara
mbili, halafu, mara wote wakasimama,…’akatuli
ahapo kidogo.
‘Haya ikawaje …?’ akauliza huyo askari .
‘Huwa mara nyingi najihami, hasa nikiona kitu ambacho sio
cha kawaida, ….harufu, au vumbi, ….nina mafuta yangu najipaka puani, nimezoea kufanya
hivyo, …sijui kwanini,….na waakti wanakuja, nilikuwa anjipata hayo mafuta,
najipaka, na walipokuwa wakiyavurumisha mahonda yao kwa sauti ya kutoa moshi,
nikajpaka yale mafuta kwa wingi puani,…..
‘Ni mafuta gani hayo…?’ akauliza huyo askari.
‘Unajau mafuta hayo alinipa rafiki yangu mchina, aliniambia
ukiyapaka puani , yanasaidia kujilinda na vitu vya kuambukiza, na kama una
athirika na mavumbi au harufu au una `alegi’ na vitu kama hivyo, basi ukijipaka
hayo mafuta, hutaweza kuathirika , na pia hata kama mtu kakupulizia madawa ambayo
yanalewesha na kutia usingizi, ….mafuta hayo huweza kukulinda ,hutaweza
kuathirika kwa kiasi kikubwa.
Hawa waendesha pikipiki,walisimama, na kabla sijawauliza
nini lengo lao wakanivamia, na mimi sikukubali kirahisi nikapambana nao,
ilikuwa karibu niwashinde, lakini huyo mmoja ndio akatoa leso ambayo nahisi
ilikuwa na madawa ya kulevya, ….akanishikisha puani,….sikuwa
nimemuona,kamaningemuona nisingelipa hiyo nafasi.
Niliingiwa na kiza na
kupoteza fahamu…na nilipozindukana baadaye kidogo, nikajikuta nipo ndani
ya gari wamenilaza kiti cha nyuma, na mbele kwa dereva yupo dereva mwenyewe,
pandikiza la baba na pembeni yake yupo mwanamke. Huyu mwanamke alikuwa kavaa
wigi lenye nywele ndefu kidogo. Na alipogeuka kuniangalia kwa nyuma, karibu
anifume,…niliona kuwa kavaa mawani makubwa meusi.
‘Endesha haraka kidogo maana asije akaindukana huyu mtu, kabla
hatujafika….’nikasikia akimwambia dereva wake.
‘Itakuwa maajabu kama atazindukana haraka hivyo…’akasema
huyo dereva.
‘Wewe endesha haraka, huwezi jua huenda hayakumuingia vyema,
ni vyema kujihami….’akasema huyo mwanadada.
Nilijaribu kutizama wapi tunaelekea ,lakini kwa pale
walivyonilaza ilikuwa ni vigumukuinua kichwa bila kuonekana , na sikutaka
kabisa wanijue kuwa nipo macho, nikatulia tu, ….
‘Kwahiyo twende wapi bosi wangu,…tunaelekea kwako au kule kwenye jengo jipya…?’ akauliza yule
dereva.
‘Kwenye jengo jipya, kwangu kuna wageni…’akasema huyo
mwanamama.
‘Na wewe kwa wageni …..hakuna siku niliwahi kuja kwako
nisikukute na wageni, halafu wengi wanatoka nje,…..dili zako kali bosi…’akasema
huyo dereva.
‘Umeanza kuwa askari kanzu, au ndio nyie mnatoa siri za
watu….chunga sana mdomo wako, ….utakuwa chakula cha mchwa sasa hivi….’akasema
huyo mwanamke.
‘Ndio yamekuwa hayo bosi,…nilikuwa nakutania tu…..samhani
sana bosi niwie radhi….’akasema huyo derive na kweli alionyesha kuogopa.
‘Kukuwia radhi kwangu ni wewe kutuliza huo mdomo wako, na la
sivyo tunajua jinsi gani ya kuutuliza, haya endesha na ukae kimiya, unanitia
kichefuchefu nikisia sauti yako….’akasema huyo mwanamke.
‘Sawa bosi, …nimenyamaza…’akasema na kuonyesh amkono wake
mdomoni kuwa kaufunga.
*******
Mara gari likasimama na mlango wa gari ukafungulia na mimi
nikavutwa kama gunia, hawakunijali, wakanibeba hadi ndani ya nyumba hiyo, ilikuwa
mpya, maana harufu za rangi ya nyumba nilizihisi.
Yale mafuta yalinisaidia sana, vinginevyo ningelikuwa bado
sijazindukana, kwani hayo mafuta niliyopaka puani, yanapunguza ukali wa madawa
kama hayo na wao walijua kuwa sitazindukana kwa muda, mrefu. Nikajifanya bado
nimelala, nikajilegeza kweli kweli, huku naangaza huku na kule kwa kujiiba, ili
kujua wapi nilipo.
‘Hakikisheni kuna ulinzi wa kutosha na akizindukana niiteni
haraka, kuna jambo nataka kujua kutoka kwakwe kabla zoezi la kummaliza halijafanyika…’akasema
huyo mwanamama na kuondoka zake.
Hawakunifunga kamba, kwahiyo nilipohakikisha kuwa hawapo,
nikainuka na kwenda maeneo ya dirishani , hapo nilitizama kwa nje, kama ninaweza
kugundua wapi hapo tulipo, …kulikuwa kimiya kabisa, na kwa mbali nikaona jengo moja
refu, na kubhatisha kuona maandishi, yalikuwa na neno `Mbezi…’….nikajua nipo
maeneo ya Mbezi,hata jinsi kulivyo kwa nje inaonyesha kabsa kuwa tupo Mbezi.
Mara ghfla mlango ukafunguliwa, na hapo sikuwa na jinsi, akanikuta
huyo jamaa nikiwa nimesimama. Yule jamaa akaningalia kwa mshangao, akatabasamu
na kusema;
‘Mhh, umeshaamuka ,duuuh, nimekukosa, maana nilitaka
nikuwahi ukiwa bado umelala, lakini sasa upo macho….unasemaje, nataka tustarehe
kidogo….’akasema huyo jamaa.
‘Wewe kweli umechanganyikiwa , nyie ndio mnaobaka maiti…hivi
nani anaweza kustareeh na mtu kama wewe, watu ambao mnatawaliwa na huyo
mwanamke, kwanini usiende kustarehe nay eye…’nikasema kwa nyodo.
‘Mhh, unajifanya mgumu, nitakulainisha tu na baadaye
utafurahia hichoo nitakachokufanyia,…wenzako wananitafuta, ..mmh, hata hivyo
wee dada kwakweli mrembo , sitaweza kuvumilia kuacha uwawe bila ya kukugusa,
….nitasikitika sana wakikumaliza, kabla,… lakini sikubali, mpaka nihakikishe
kuwa nimekupata…au upo tayari kutooa ushirikiano….?’akasema huku akinisogelea.
‘Tafadahli….nikamunyoshea kidole kumkanya, yeye hakujali
akaanza kunishika shika….
Sikuweza kumpa nafasi hiyo, nikamrukia kwa kigoti, goti
likagonga kati kati ya sehemu zake za siri, akainama huku akilalamika kwa
maumivu na kabla hajaweza kuinama vyema,
akapata kipigo cha goti jingine kwenye uso, na nilijua kabisa limegonga puani,….
akalala chini, alipojaribu kuinuka nikamuwahi, akaserereka na kugonga ukutani,
aliguna, na kwa haraka akageuka, akijua sasa anapambana na mtu, sivyo kama
alivyofikiria na kuzarau kuwa ni mwanamke tu….
‘Kumbe wamo, sasa umejitakia nitahakikisha
unalegea….’akasemahuku akigeuka kunivamia,name nikaona sasa wewe hujanijua,
nikageuza teke la kinyume nyume, akutana nalo, na kutua usoni. Nashukuru sana
mafunzo ya karate niliyopewa, maana kila pigo lilienda pale panapostahili na
lilifanya kazi yake.
‘We….ooh, ….’akapiga ukulele…..na anilipotaka kumtwangwa
teke jingine la kichwani ambalo kama lingelimpata najua kabisa angelipoteza
fahamu,….nikasikia chuma kikigonga kichwani, na sauti ya mwisho kusikia ilisema;
‘Kwanini hamkumfunga kamba….mpigeni siandani , asije
akazindukana kabla ya zoezi….’ilikuwa sauti ya mwanamke….
Sijui walinipiga na chuma gani kichwani,kwani maumivu makali
yalitanda kichwani na giza likanifunika , na sikujitambau tena, hadi hapo
nilipozindukana na kujikuta nipo hapa hospitalini….’akamalizia
kuelezea huyu mwanadada.
‘Unaweza kuhisi huyo mwanamke ni yule aliyekuwa katoroga
rumande…?’ akauliza askari.
‘Siyo yeye….atakuwa mwanamke mwingine…’akasema mwanadada
huyo wakili.
‘Na hawa wanaume waliokuwa wakishirikiana na y eye ukiwaona
unaweza kuwatambua?’ akauliza askari.
‘Huyo mmoja niliyepambana naye naweza kumtambua, ila hawo
wengine sio rahisi kwa jinsi ilivyokuwa.
Sikubahatika kuoana sura zao
vyema…’akasema huyo mwanadada wakili.
‘Huko Mbezi, unafikiri ni mbezi sehemu ipi..?’akauliza
askari.
‘Sijawa na uhakika ni mbezi
ipi, ndio nataka nifanye uchunguzi,nitapagundua tu, maana lile jengo ni
refu, na zisani kuwa ni sehemu ya ndani ndani kutoka barabara kuu, itakuwa
akribu sana na barabara kuu…hilo nipeni muda, nitawapa jibu nikipagundua…’akasema
huyo mwanadada.
‘Huoni kwa sasa hivi ni hatari kwako kuwafuatlia hawo watu,hiyo
kazi tuachie wenyewe,…’akasema askari.
‘Nyie fanyeni kazi yenu, na mimi najua nini ninachokifanya….tusiingiliane….’akasema
huyo mwanadada.
‘Kwa kibali gani, kuwa unamfanyia nani uchunguzi,maana ujue
kuwa utakuwa unaingilia kazi ya askari, labda kama ungetuambia una mtu
unamfanyia kazi kwa ajili ya kesi fulani, na umeshapata kibali, hapo
tungelikusaidia na hata kukusindikiza, lakini sasa hiyo kesi ipo mikononi
mwetu, haikuhusu…’akasema huyo askari.
‘Kwani tatizo hapo ni nini, kwasababu mwisho wa siku ni kwa
manufaa yenu,..kesi hiyo inanihusu maana wamenigusa pabaya, ngoja niwaonyeshe
kuwa na mimi najua mambo hayo….msijali , nitafuta taratibi zote kisheria….’akasema
huyo mwanadada.
‘Tunachoogopa ni kuwa unaweza ukavuruga ushahidi
na…..’akasema huyo askari na kabla hajamaliza huyo mwanadada akamdakia na
kusema;.
‘Niombe tafadhali afande mimi nivuruge
ushahidi,unazarau kweli wewe,….mimi najau
nini ninachokifanya, nyie fanyeni kazi yenu, na mimi niachieni nifanye kazi
yangu, ninajua namfanyia nanihiyo kazi na siku ikifika mtajua..’akasema huyo
mwanadada na kuniangalia pale niliposimama.
‘Twende zetu….’akaniambi na mimi nikamfuta nyuma.Yule
mwanadada alitoka palekwa haraka ,na mii nilijichelewesaha nyuma kidogo, na
nilipogeuza kichwa kuwaangalia wale maaskari nikawakuta wanatuangalia kwa
makini, na mmojawapo akasema;
‘Fuata nyendo zao hawa watu…..’
******
‘Sasa tunakwenda Mbezi,….lakini kama upo tayari, usije
ukasema nakulazimisha, kama una mishe mishe zako nenda,nitajitutumua
mwenyewe’akasema na mimi nikamwangalia na kusema;
‘Hata kama ningelikuwa na hizo mishe mishe zangu,ningelizisahau
kwa muda,…kwa jili yako, najua unachokifanya kitanisaida hata mimi’nikasema na
yeye akatabasamu na kusema;
‘Sawa, inabidi iwe
hivyo, …wakati mwingine inabidi mtu ujitolee, hata kama hutapata kitu, maana
kazi zetu hizi ni zina gharama, sio gharama ya pesa tu, zinagharimu hata maisha
ya mtu…ndio maana watu wengi wanashindwa kuwa na mawakili,….sasa nakuhitaji
kama mlinzi wangu, ila unifuate lhuko ninapokwenda,…mengine tutaongea baadaye,
sawa ’akasema kama vile ananiuliza, namimi nikasema.
‘Sawa bosi..mheshimiwa wakili..’nikasema huku tukiwa ndani
ya gari lake na nilipotizama kwa nyuma niliona pikipiki ikitufuata .
‘Nahisi kuna mtu anatufuatilia kwa nyuma..’nikasema huku
nikiwa na wasiwasi.
‘Nimeshamuona, yule ni askari…usijali nilijua lazima watafanya
hivyo, ….badala ya kuwatafuta wahalifu wananifuatilia mimi,…hata hivyo, ni
vyema kwetu pia….’akasema.
Moyoni nilijiuliza huyu mwanamke anajiamini nini kiasi hiki,
maana huko anapotaka twende nahisi sio sehemu ya kwenda bila askari, hawo ni
majambazi wa kimataifa, lakini namshangaa huyu mwanamke hajali i, na isitoshe
wale maaskari walihsmuonya kuhusu hilo, na walisema kabisa kama anataka kufanya
uchunguzi anatakiwa afuate taratibu, sije akavunja sheria.
‘Hivi huoni kuwa tunakwenda kinyume cha sheria…hapa kweli
hatutakuwa tumevunja sheria…?’ nikamuuliza.
‘Sheria ipi tumevunja….hebu niambia nimevunja sheria ipi?’akaniuliza.
‘Askari wamekuonya kuwa tatizo hilo sasa lipo mikononi mwao,
usiliingilie, hiyo ni kazi yao, lakini …’na kabla sijamaliza akasema.
‘Sema sheria ipi niliyoenda kinyume nayo,nataka kupajua hapo,..
?’ akauliza na kunitupi jicho mara moja, halafu aliponiona nipo kimiya,
akasema;
‘Nilifikiri unajua baadhi ya mistari ya sheria, …ooh, au unajua
ukiongelea mamboya sheria, najua nipo namtu anayeijua,…hata hivyo hebu niambie kazi
gani ya kwao nimeiingilia,….?’ Akatulia na kunigeuzia kichwa kuniangalia na
alipoona nipo kimiya tena akasema;
‘Naona hujui lolote hapo, ….ulikuwa unakisia kwa uwoga tu,…au
sio, usiogope,…hasa ukiwa unatafuta ukweli kwa nia njama, fanya jambo kwa
kujiamini,…wao mwisho wa siku watakuja kukusifia, kwasasa lazima wakihami,
lakini hawajui nini ninakitafuta ambacho pia ni kwa maslahi yao,…’akatulia huku
akiendesha gari kwa makini.
‘Nawezanisjue vifungu vya sheria, lakini najua kuwa tendo
fulani ukifanay utakuwa umevunja sheria…’nikajitetea.
‘Unatakiwa uwe makini hasa unapo-ongea neno `kuvunja
sheri’….mimi sijavunja sheria, …wewe tuliatu, najua nini
ninachokifanya….’akasema huku akiendesha gari ka mwendo wa kasi kidogo,
hakuelekea moja kwa moja njia ya Mbezi, tulikwenda kwanza maeneo mengine
tukapata supu.
‘Unamuona yule jamaa aliyeshika chupa ya soda, yule ni
askari, anatufuatilia sasa mimi naenda chumba cha kunawa, wewe malizia hapa na
baadaye toka uchukue boda boda hadi Mwenge, utanikuta huko….’akaniambia na mimi
sikukaidi.
Nilisubiri baada ya kumaliza supu, baadaye niakinuka, na
yule askari akawa ananiangalia kwa mashaka, maana hakumuoan yule mwanadada pale
mezani, na aliniona nikiondoka peke yangu, akainuka haraka na kueleeka chooni,
najua atakuwa anakagua chumba cah wanawake.
Mimi nikatoka na kuchukua boda boda, …hadi Mwenge , sikuweza
kumuona huyo askari tena. Nilipofika Mwenge nikageuka kuangalia wapi huyu
mwanadada yupo mara nisikia honi ya gari ikilia nyuma yangu, nilipogeuka
nikaona nii gari la yule mwanadada.
‘Sasa sikiliza hili gari naenda kuliacha kwa rafiki yangu,
tutatumia pikipiki, siunajua kuendesha pikipiki….?’ Akaniuliza.
‘Najua …lakini sina leseni….’nikasema.
‘Usijali…..’akasema na tukaondoka hapo hadi hapo aanposema
ni kwa rafiki yake, nilibakia nje wakati yeye anaongea na rafiki yake na
baadaye tukakabidhiwa pikipiki, na mimi nikaendesha hadi huko maeneo ya Mbezi.
‘Eneo lenyewe unalijua?’ nikauliza.
‘Nimeshalijua, na nimeshafika ….’akasema
‘Ulifika lini..?’ nikauliza.
‘Usitake kujua mengi, mengine ni kazi yangu…..’akasema kwa
sauti nzito.
‘Unaonekana kama askari, ulijifunzia wapi hiyo kazi….?’
Nikauliza.
‘Unapokuwa wakili unatakiwa ujue uaskari, …uwe mkakamavu,
….’ Akasema.
‘Lakini wewe ni mwanamke…huoni kuwa….’nikataka kusema kitu,
yeye akanikataiza na kusema.
‘Wewe endesha, nipe muda kuna kitu nakiwaza
kwanza….tafadhali…’aaksema na mimi nikamuelewa, na tuliendesha hadi eneo
alilonielekeza.
‘Sasa tutaiacha hii pikipiki, kwa rafiki yangu mmoja, huko
kweney hilo jingo tunakwenda kwa mguu, hatutakiwi kujulikana, na uwe
mwangalifu, hukotunakokwenda huenda tukapambana na watu weney silaha, …lakini
kwa vile ni mchana, sizani kama wanaweza kutumia silaha,…najua silaha yaoo
kubwa na madawa ya kunusisha puani au sindani za madawa ya
kulevya….’akaniambia.
‘Usijali mimi najiamni,….’nikasema na huku nikiwaza huko
tunakokwenda tuankwenda kufanya nini,lakini sikutaka kuuliza swali, tukaanza
kutembea,ilikuwamawndo kidpgo na baadaye tukafike kwenye jengo,.
‘Jengo lenyewe ndilo hilo hapo, lakini hatutakiwi kuonekana,
na cha kufanay sasa hivi ni kusubiri hapa tulipo, huku tukiangalia nani
ataingia hapo, nina uhakika kuna mtu muhimu atakuja hapo, kama uchunguzi wangu
wa jana hautakwua na makosa….’akasema.
Tulikaa pale kwa muda mrefu, mpaka subira ikaniishia
nilalamika na kusema mbona hakna kitu na tunapoteza muda wetu hapo bure, yeye
akasema subira huvuta heri tuendelee kusubiri,….
Baadaye sana likaja gari na kusimama pale kwenye lile jengo,
ilikuwa taksi, na ile taksi ikaondoka na kumuacha mwanadada mmoja,…Yule
mwanadada hakuingia ndani ya lile jengo moja kwa moja, alikwenda hadi kwenye
genge lililopo karibu akawa ananunua vitu, na baadaye akaoka na kusimama mbali
na jengo, akawa anaangalia huku na kule.
Kama vile anasubiri gari pale,na akawa anatembea taratibu,
na baadaye kwa haraka, akaelekea kwenye mlango wa ile nyumba, akasukuma mlango
wagetini, na kutokomea huko ndani. Nikamwangalia bosi wangu kuwa atasemaje.
‘Sasa wakati umefika,….kwa jinsi nilivyoona yupo peke yake…sijui
kwa huko ndani,sasa, nataka nikupe onyo, tukifika hapo wewe nenda pale getini,
ongea na hawo walinzi, hakikisha unaongea nawo kwa muda,….na kama atakuja mtu
mwingine, au hawo walinzi wataamua kuingia ndani niashirie kwa kubipu simu
yako, mimi mengine niachie mwenyewe….’akasema.
‘Ina maana unataka kwenda kukabiliana na huyo mwanadada peke
yako, je kama kuna walinzi ndani itakuwaje….?’ Akauliza.
‘Fanya nilivyokuelekeza…’akasema na mimi nikafanay hivyo.
Wale walinzi walikuwa mbogo, walianiambai hawataki mtu hapo,
lakini nikatumia lugha ya kijiweni na kuonge hili na lile mpaka tukaivana, mimi
niliwaambia kuwa mwenye jengo hilo ni rafiki yangu wa kike na nataka kuonana
naye.
‘Hajatuambia kitu kama hicho,kwanza nani kakuambia kuwa
mwenye jengo hili ni mwanamke…?’ akauliza.
‘Nyinyi mnanishangaza kweli, nimeshawaambi kuwa huyo
mwanamke ni rafiki yangu, halafu mnauliza nimejuaje….nimejua kwasababu nipo
karibu naye, nyie subirini muone akitoka atasema nini, mtaona
wenyewe….’nikasema..
‘Sasa sisi haturuhusiwi kabisa mtu kusimama hapa getini,kama
unamuhitaji nenda kasimame kule, akitoka utakuja kuonana naye…’akasema huyo
askari.
‘Nyinyi si mnataka kuhakikisha kuwa mimi ni rafiki yake au
sio,subirini kidogoo, akitoka mtaona
wenyewe,na kama mnabisha ngojeni nikamwambie kuwa nyie vibarua wake mumenizuia,
tuone kama hamtafukuzwa kazi wote nyie, mnafanya mchezo eheeh.’nikasema na wao
wakaniangalia kwa mashaka na hiyo ilisaidia wakatulia bila kusema neno..
Baadaye kidogo,mlango wa ile nyumba ukafunguliwa na
aliyetoka pale ni jamaa kavalia kofia kubwa, alitoka kwa haraka huku akionyesha
wasiwasi mkubwa, akaja pale getini na kuwapita walinzi hata bila ya kutoa
salamu, na mimi nikashituka. Huyo jamaa aligeuza kichwa na kuniangalia,…nikamkumbuka
…ni mmoja wa wale waliokuwa wamembeba huyo wakili mwanadada kule kwenye lile
jengo jipya la ghorofa wakiwa na lengo la kumuacha pale adondoke.
‘Huyu ni nani,….alipitia wapi, au ndiye anayekula mpenzi
wangu…?’ nikauliza alipoondoka.
‘Hayo ya hapa hayakuhusu, kwanini hukumuuliza mwenyewe
alipokuwa hapa…..?’ na kabla sijawajibu, mara simu yangu ikaingia
meseji,inasema niende kule tulipoacha pikipiki haraka….nikageuka na kuwaangalia
wale walinzi, na baadaye nikasema;
‘Mbona huyu mwanadada hatoki….?’ Nikauliza.
‘Wewe siumedai kuwa unataka kumsubiri, msubiri,…sisi hilo
halituhusu hata akikaa humo hadi usiku, ni kwake, sisi tuna wasiwasi gani,
labda tusikie kelele za kuumizana, tunaweza tukaenda kusaidia,…hata hivyo sisi
hapatumepewaakzi ya kulinda nje, sio huko ndani…’akasema huyu askari.
‘Sawa nimeshindwa mimi,..kazi njema…’nikasema na wao
wakacheka na kusema;
‘Yatakushinda,….mwanamke hafuatiliwii kihivyo…pole
sana,lakini angalia ukifanya hivyo utakuja kuumia mwenyewe,….’akasema mmoja
wapo.
Nikaondoka hadi kule tulipoweka pikipiki, na kumkuta yule
mwanadada wakili akiwa katulia huku akionyesha kuwa na mawazo mengi.
‘Imekuwaje?’ nikauliza.
‘Balaa….ukisikia wakili akisema kuna balaa ujue kweli ni
balaa….’akasema huku akingalia saa yake.
‘Mungu wangu balaa gani hiyo, maana sikukuona ukiingia wala
kutoka kwenye hilo jengo…’nakuliza.
‘Haitakiwi ujue hayo, hebu nikuulize, hukuona mtu akitoka
mlangoni wakati upo getini?’ akaniuliza.
‘Ndio alitoka mwanaume mmoja,akiwa kava kofia
pana…’nikasema.
‘Huyo ndiye muuaji…’akasema huyo mwanadada wakili.
‘Ndiye muuaji…..!’ nikashangaa, halafu nikauliza kwa haraka.
`Muuaji…,kwavipi..?’nikauliza.
‘Kwa nyuma kule kuna sehemu nilishaiona ya kuweza kuruka na
kuingia ndani, na ukiingia ndani, kuna ngazi kwa nyumba ya jengo, walikuwa
wanaitumia mafundi kwa kupaka rangi. Niliitumia hiyo ngazi, maana kuna sehemu
kwa juu badi ipo wazi, unaweza kupenya hadi ndani…ndio wameanza kuiziba hiyo
sehemu, haijakamilika, na ndipo nilipotumia kuingia ndani.
‘Ukamkuta huyo mwanadada…..?’nikauliza.
‘Nilimkuta, …hakuamini na hakujua jinsi nilivyoingia,
alitaka kupiga ukulele…, nikamtuliza kiaina, …alisema yeye hataki kuongea na mtu, ndio maana kaja pale
kujificha, …’akatulia na kuniangalia.
‘Alikuwa peke yake?’ nikamuuliza.
‘Kwenye maongezi alisema ana mlinzi wake, na hakutaka kusema
huyo mlinzi yupo wapi,….na nikambana kwa maswali, mapaka akalainika, na kuanza
kukiri kuwa hata yeye hataki kuwemo kwenye hilo kundi, lakini hana jinsi…aandai
kuingia kwenye hilo kundi ni rahisi lakini kutoka ni vigumu, na njia rahisi ya
kutoka na kifo….’huyo mwanadada akakunja uso kuonyesha kuwa hilo swala linampa
shida.
‘Ikafikia muda akaniambia kuwa mimi wananitafuta kwa udi na
uvumba, waniue…na hapo akaniambia kuwa sitaweza kutoka salama, …maana kuna watu
wananifuatilia kwa karibu kila ninapokwenda, ….na kama wakijua kuwa nipo hapa,
hawatasita kuniua….nikamuuliza kwa vipi, akasema …kama mimi ni mbishi ningoje nitajionea mwenyewe…’akatulia
huyo mwanadada.
‘Oh,ningelijua ningetoa msaada,lakini hakuna mtu aliyeingia….’nikasema.
‘Wakati naingia na pale aliponiona, nakumbuka alibonyeza kitu kwenye simu yake, na
baadaye akaizima, aliniambia baadaye kuwa angelijua tangu mapema kuwa mimi sio
mtu mbaya, angeliizima hiyo simu yake,maana kundi lao wote wana simu kama hiyo inayoonyesha
wapi mtu wao alipo, na kama kuna matatizo wanajua jinsi gani ya kumsaidia kwa
haraka,….’akatulia kwa muda bila kusema kitu.
‘Mhhh’nikaguna kama kumshitua na yeye akasema;
‘Aliniambia kwa uchungu kuwa alishabonyeza simu yake aliponiona
kwasabbu alijua nimekuja hapo kumkamata,…na hiyo simu imeshapeleka taarifa
kwenye kundi lao, kuwa yupo kwenye matatizo , licha ya kuwa alishaizima, lakini
kwa jinsi anavyolijua kundi lao, watakuwa wameshaanza kumfuatilia kwahiyo
akaniomba niondoke hapo haraka. ….
‘Kwanini sasa hukuondoka haraka…?’ nikamuuliza
.
‘Aliponiambia hivyo, nikawa namuuliza maswali muhimi anajibu huku
nikitafuta njia ya kutoka kwa haraka,…lakini haikuwa rahisi hivyo…yalitokea mengine
makubwa…..’akasema na kutulia.
‘Yalitokeaje, maana sizani kama kulikuwa an mtu mwingine,na hakuna aliyeingia….’nikasema
‘Lazima kulikuwa na mtu mwingine aliyekuwa kwa ndani, …..huyo mwanadada hakutaka
kuniambia, lakini alikuwepo mtu mwingine, nahisi ndio huyo mlinzi wake wa
karibu…sijui alikuwa wapi muda wote tukiwa tunaongea,na nakumbuka vyema wakati wanaingia, huyo mwandada alionekana yupo peke yake,…..ina maana huyo
mlinzi atakuwa aliwahi kuwa humo ndani kabla yake,…..au ….’akatulia kidogo.
‘Kwani kulitokea nini…?’ nikauliza.
‘Wakati naongea na huyo mwanadada, huku naangaza huku na
kule,…nakamsogelea yule mwanadada nikitaka nichukue ile simu yake, maana ni ushahidi muhimu sana, na kuhakikisha kuwa hana kitu kinachonasa yale
tunayoongea…na yule mwanadada alikuwa akinisihi niondoke humo haraka...’akatulia.
‘Ohh….kwanini hukuondoka, wewe hukuona kuwa hpo kuna balaa….’nikasema.
‘Nilikuwa natafuta ushahidi…ambao unatafutwa sana, na huyo mwanadada alikuwa nao,..’akatulia na
kuniangalia, halafu akasema.;
‘Nilipomsogelea akasema, niondoke, kwani hakutaka mimi nifie
mkononi mwake….na mara nikaona kivuli cha mtu kwenye dirisha, na kwaharaka
nikainama chini, nikiwa na lengo la kujificha, huyo mtu niliyemuona asije akaniona, Mungu
Mkubwa, na naweza kusema ilitokea hivyo kwa kudra zake,….’akatulia kidogo na
kuweka mkono mdomoni.
‘Yaani…. nilichoshuhudia ni risasi ikipenya utosini, kichwani
mwa huyo mwanadada niliyekuwa nikiongea naye. Ina maana kama nisingeliinama
haraka, hiyo risasai ingelitua kichwani kwangu, ….huyo mtu alikusudia kuniua
mimi, lakini kule kuinama kuliponya,…..watakuwa waliweka kiwambo cha kuzua sauti...’ hapo akapangusa uso kwa kiganja cha
mkono.
'Ikawaje maana alitaka kukuua wewe , kakukosa,....?' nikauliza.
'Nafikiri atakuwa alichanganyikiwa...kamuua bosi wake,.....mimii nilitambaa kwa haraka, kuondoka pale, huku nimeinua simu yangu inayochukua picha, nilihakikisha nipo mbali ya upeo wake,...kwasababu alikuwa kwa nje, na pazia lilizuia, asingeliweza kuona vyema, wapi nilipo, nilimuona akizungukazunguka hapo dirishani, na baadaye nikasikia sauti ya mtu akikimbia, nilipochungulia dirishani nikamuona akiondoka....'akasema huyo mwana dada.
‘Sasa itakuwaje, ….maana hiyoni kesi ya mauaji, na wewe
ulikuwa hapo, ulitoataarifa polisi na je mliongea nini na huyo mwanadada?’
nikamuuliza.
‘Kwanza tusubiri,
polisi walijue hilo, na kama nitahitajika nitajua nini cha kufanya, ila nataka
nijitahidi hadi nimpate huyo jamaa aliyetaka kuniua,… una uhakika ulimuoan sura
yake?’ akaniuliza.
‘Ndio nilimuona,na alikuwa na wasi wasi sana….sasa
utampataje ?’nikasema na kuuliza hapo hapo.
`Hawo watu najua wapi wanapopatikana, hawo kazi yaoo ni
kukodiwa kufanya mauaji,…na mara nyingi wakishafanya hivyo wanapotea kabisa
hapa mjini, wanakuja kuonekana baada ya mwaka hivi….sasa natakiwa kumuona kabla
hajaondoka, ina maana leo hii tunakwenda huko, upo tayari….?’akaniuliza
‘Duuh, sasa hapo unataka kujiingiza kwenye mdomoo wa chatu….’nikasema.
‘Hawo watu najua wapi wanaishi, lakini inahitaji njia ya
kuwashika, hawo kazi yao ni kukodiwa kufanya mauaji, wanatafutwa sana na
polisi, na hapa ina maana ili kumpata inahitajika kujiingiza kwenye matatizo, …na
mimi mwenyewe sitaweza hii kazi, nitaongea na mkuu wa kituo, ni rafiki yangu
mkubwa, lakini hata hivyo nakuhitaji wewe, lakini naogopa kukutia kwenye
matatizo, na sitaki uingie huko, sijui nifanyeje…?’ akauliza.
‘Mimi nipo tayari kuingia kwenye matatizo kama mwisho wake hao
watu watakamatwa…lakini nisiende jela’nikasema.
‘Hiyo inategemea nguvu za polisi….na hali ilivyo, mambo yanawezekana
yakawa mazito, ….kama huyo mwanadada asingeliuliwa, tungelijua mambo mengi
sana,…’akasema huku akikunja uso kuonyesha wasiwasi.
`Kwani unamfahamu huyo mwanadada,…ni nani…?’ nikauliza huku
nikimuangalia kwa wasiwasi.
‘Ni Kimwana….’akasema.
‘Eti nini una maana ni mke wangu..?’nikauliza huku nikihisi mwili
ukinisha nguvu.
NB Mambo yanaanza kuiva, ni nini kitatokea, je ni Kimwana
yupi huyo?
WAZO LA LEO: Zarau sio jambo jema katika maisha, mkiwa wawili au kundini, jaribuni kukwepa kuzaraulina, huenda umejaliwa kiakili, kikipato...kinguvu, usije ukamdharau mwenzako kuwa yeye hana kitu, hana nguvu, huwezi jua nini munu alichopa ambacho wewe huna, tukumbuke mzarau mwiba guu huota tende.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment