Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, March 28, 2012

Hujafa hujaumbika-12


‘Mume wangu mbona siku hizi unalewa kupita kiasi na hata unaamua kulala nje, una tatizo gani...ni kazi gani hizo za kulala nje, na ukirudi umelewa chakari, kazi gani utafanya ukiwa umelewa hivyo...?’ akaniuliza mke wangu huku akionyesha uso wa huruma, nilimkwepa kumwangalia, maana ukimwangalia usonii utamuonea huruma.

‘We acha tu, endelea na shughuli zako, maana hata nikikuambia utakimbilia kusema ni mambo ya kizungu....maisha ya ndoa nayaona kwagu ni mitihani, sasa tena watu wananiibia gari langu ...unajua mke wangu sikujua itakuwa hivyo...lakini sio kosa lako, labda nijilaumu mwenyewe...’nikasema huku nikipepesuka

‘Mbona sikuelewi yaani ulevi wako unanilaumu mimi....kulewa ulewe wewe, na lawama zinakuja kwangu..hapana hizo lawama sikubali,...acha ulevi kwanza kama unataka uwe msafi,...mtegemee mungu, kupoteza gari sio kupoteza kila kitu,watu wanapoteza magari, wanapata hasara kubwa sembuse wewe gari moj tu...’akanishauri mke wangu.

 Kwakweli kama kuna kitu kiliniuma katika maisha yangu ni pamoja na kuibiwa hilo gari, sikuamini, maana nililitafuta mpaka mfukoni, ...hata nilipofika kituo cha polis kujieleza, bado nilikuwa najikagua mfukoni, ....
Unajua nilipokuwa nikisoma Ulaya, nilihangaika sana,...kubeba maboksi na kazi za ajabu ajabu, ili kupata pesa za ziada hadi kununua hilo gari, na lilikuwa sehemu yangu ya kujivunia kuwa na mimi nilifika ulaya, sasa nitapata wapi gari kama hilo, maana bei yake kubwa sana, pesa ninayopata haitoshi...

‘Chukua mkopo angalau upate gari la kawaida....’akanishauri mmoja wa marafiki zangu na wazo lake nikalikubali, na kweli haikuchukua muda nikapata mkopo na kununulia gari, ambalo haliwezi hata kufikia nusu ya lile gari langu liloibiwa, lakini angalau niliweza kusema nina gari, na kipindi hicho kampuni yetu ilikuwa ikiyumbayumba kibiashara....

Biashara ilisuka sana, na hatukuweza kupata masoko ya bidhaa zetu kwahiyo mameneja walitakiwa wajitegemee kiusafiri ili kubana matumizi.

Gari likaniweka katika hali yangu ya kawaida,....ukizoea gari inakuwa shida.....basi nilipolipata ratiba yangu ya kurudi usiku wa manane ikaendeelea, na wakati mwingine nalala nyumba za wageni,na kubadilisha wasichana kama nimechanganyikiwa hata ofisini wakaniita kiwembe, binti hakatizi mbele yangu, lazima nitamualika chakula cha usiku....yaani mungu tu kasaidia na kunikweepsha na huu ugonjwa, sijui...

 Mshahara ukawa hautoshi ,kwasabbu starehe zilizidi, kila siku nipo kwenye mahoteli makubwa, kwenye mabar,madanguro....na ukumbuke kuwa nilikuwa nakatwa makato ya madeni, matumizi yangu yalikua hayakadiriwi, na kila siku naomba mshahara kabla ya wakati, ....Nikaanza kuandamwa na barua za maonyo, lakini ilikuwa sikio la kufa halisikii dawa...!

 Siku moja wakati nimerejea nyumbani nikakuta kuna mgeni...sikujali sana, nikapitiliza hadi chumbani, siku hiyo nilitaka kujipumzisha nyumbani,....kwani nilikuwa nimeutwika kisawasawa...na sikutaka kumsumbua mke wangu, ....lakini baadaye nikaona sio vyema nikamuita mke wangu chumbani...Alipofika, nikaanza kumshikashika, ....

 ‘Aaaah, bwana umeanza mambo yako ya kihuni huni, ....,huoni kuna mgeni varandani...na mchana huu umelew hivi...mungu wangu...haya jisaahulishe kidogo....’akasema mke wangu.

 ‘Mgeni gani zaidi ya mke wangu, mimi...ni mume wako, nikikuhitaji hata kama kuna wageni inabidi utafute mbinu waondoke....sikiliza mke wangu, nimevumilia weeee, sasa nachoka, ....niende wapi, nikatembee na machangudoa..mmh, njoo hapa....’nikawa naongea sauti ya kilevi, kweli pale akili yote ilikuwa ikinuka pombe nikamsogelea mke wangu naye akanikwepa na kusema.

 ‘Hebu punguza sauti hujui ni nani yupo varandani...halafu ulvyolewa, mbona leo aibu, hujui huyo ni rafiki yangu mkubwa kaja anataka kukuona shemeji yake...’akasema .

 ‘Haya shemeji shemeji huku mwazima taaa...nakuja maana sikuwezi....lakini ipo siku utajilaumu na hawo shemeji, ....nakuja...ngoja nivae hii bukuta, nani anajali nipo kwangu...’nikasema na kuvaa bukuta yangu, sikujali kuwa ni nani yupo, halafu nikatoka pale varandani....

 Unajua wakati naingia yule mgeni alinipa mgongo, sikuwa nimemuona vyema, ...sasa natoka chumbani nikawa namwangalia moja kwa moja usoni...niliduwaa...nikashikwa na butwaa, lakini baaadaye nikajifanya kujisahaulisha nikasema kwa bashasha..

 ‘Ohh, samahani sikujua kuwa kuna mgeni, mgeni mwenyewe mrembo....shemejii ...mmh, umejaliwa kweli, ....mke wangu umempata wapi huyu mrembo?’ nikauliza.

 ‘Mbona alishawahi kufika hapa nikakutambulisha siku moja,....umesahau, na wewe bwana unazeeka kablasio muda wako.... ulikuwa haujamuoan vyema nini...?’ akasema mke wangu.

 ‘Aaah, labda nilikuwa na mambo mengi kichwani....shemaji jisikie upo huru,mimi nilikuwa na sherehe huko kazini, kwahiyo nimekunywa kidogo...unisamehe, kama nitaongea kauli chafu....unajua tena ukilewa...’nikasema na huyu shemeji akacheka, lile cheko la kumkoma nyani giladi...

 Mazungumzo yalikolea maana mke wangu na huyo rafiki yake, inaoenekana walikuwa wanajuana vyema toka huko kijijini wakiwa shuleni, kwahiyo wakawa wanapeana maisha yao ya shule, na mambo ya kijijini, ikawa ni porojo, utani mwingi na vicheko, na ukinihusisha na mimi kiwembe, huku pombe zinanikoroga kichwani mambo yalinoga kweli.

 Mimi kwa muda huo nilikuwa nimekaa kwenye sofa nikiwa natizamana moja kw amoja na huyo mgeni, mke wangu alikaa pembeni yangu na mara nyingine alikuwa akitoka kufanya mambo ya jikoni, nikawa nabakia na yule binti  na mwanya kwangu kama huo ni kosa . ..

Hata hivyo sijui kama huyu binti, alishanijua uzaifu wangu au vipi, kwani alikuwa hatulizi migu yake na ukizingatia kuwa alivaa nguo fupi,....basi wakati mwingine alikuwa akiinua mguu juu ya mwingine na kuacha sehemu kubwa ya mapaja wazi,...hakujali kuwa mimi nipo mbele yake na namtizama moja kwa moja, pombe ikawa inanichanganya kichwani ...damu ikawa inachemka..!

. ‘Shemu sasa mimi naondoka...’  Baada ya maongezi na kupata chochote mgeni akawa anaaga kuondoka, na mimi sikupenda niiache hiyo bahati hivihivi, akili ikanijia, nikasema ;

 ‘Shemeji ngoja nikupe lifti, unasema unakaa wapi....?’ nikauliza. ‘Hapana shemeji leo unatakiwa upumzike na mkeo,....maana umesema siku zote unarudi usiku huoni kuwa leo ndio siku ya kujirusha na rafiki yangu...’akasema.

 ‘Sawa mpe hiyo lifti tu, hakuna shida,.... kwanza mimi nina kazi nyingi leo, kuna minguo ya kufua, kuna kazi za nyumbani sina hata muda wa kuongea sina, mpeleke lakini urudi mapema, ..'akasema mke wangu na aliponioana nikiinuka na bukta ile niliyovaa inanishitaki, mke wangu akatabasamu na kusema,;

Lakini  kwanza tafadhali kabadili hiyo nguo haina heshima, halafu nina wasiwasi na jinsi ulivyo utaweza kuenedesha gari kweli...?’ akasema mke wangu hata bila wasiwasi au wivu.Moyoni nikasema mambo sio hayo...kichaa kapewa rungu, nakaondoka naye. ....
                           
                   *********
‘Shemu, umenikosha sana,... sijawahi kuoana msichana mrembo kama wewe...na leo sijui nisemeje, ...’niaksema.

 ‘Shemeji bwana, mzuri mkeo,....usinitanie, ...hata hivyo shemeji, naona kama umelewa, na mambo unayoyaanza sasa sio mazuri, unajua mkeo ni rafiki yangu mkubwa, sitapenda kujiingiza katika hayo unayoyawaza, namuheshimu sana.....rafiki yangu....’akasema huyo binti.

 ‘Najua ni rafiki yako, lakini urafiki wa kweli ni kuchangiana...au sio, kwanza, hapa nilipo sijui itakuwaje, ....unaona alivyo rafiki yako, kazi nyingi hazimuishi, ...nipo nyumbani lakini naweza nisimuona chumbani hadi usiku....aah, samahani naongea mambo ambayo siyakuongea...’nikainama chini kwa kujifanya naona aibu kuwa nimeropoka mambo ya ndani.

 ‘Unaoan sasa ni pombe hiyo, inakufanya uongee hata siri za ndoa, lakini kama ana kazi nyingi kwanini usimtafutie mfanyakazi wa nyumbani, ili mpate kuwa naye karibu....’akasema huyo binti

 ‘Hataki....hataki kabisa, anasema yeye hana kazi, ina maana kama nikiltea mfanyaakzii yeye atafanya akzi gani...labda anaona wivu kuwa nitamgeuka, ....’nikasema na kweli moyoni niliwazia hilo hilo, kuwa angekubali kuleta mfanyakzi sijui kama ingeliisha mwezi kabla sijamgeuka....nilijua kabisa uzaifu wangu.

 ‘Shemji mimi hapa ndipo naishi,...’akasema tulipofika maeneo ya kwake.

 Ilikuwa nyumba nzuri tu, na sijui humo alikuwa akiishi na nani. ‘Unaishi peke yako humu ndani....?’
nikamuuliza

 ‘Ndio, kwani vipi, ...mimi sina mume, ningeliishi na nani...lakini ni nyumba ya kupanga, mbona nipo hapa siku nyingi tu...’akasema huku akifungua mlango......ilikuwa nyumba nzuri,kubwa ya viumba vitatu, choo jiko, na kila kitu ndani kwa ndani, lakini haikuzungushiwa ukuta....

 ‘Ohh, kumbe unaishi hapa, tena peke yako hata siamini, ....na rafiki yako ndipo anapokuja mara kwa mara,...keshaniambia kuwa anakuja kwako mara kwa mara,....kweli hapa pazuri,... lakini sizani kama unaishi peke yako, suinidanganye nikaja kuuwawa bure...'nikaanza utani wangu huku najibwaga kwenye sofa hata bila kukaribishwa.

'Amini hivyo...nipo peke yangu....sijaolewa, kama ningeliolewa ningelisema naishi na mtu, ukimuona mtu anakuja kuijiiba tu...'akasema.
'Sawa nimekuamini, akija mwenyewe tutapambana maana hukuniambia ukweli....lakini hata hivyo nikiuwawa sio mbaya maana ,inzi kufia kidondani haijalishi au sio,...' nikasema huku nikimwangali yule binti bila kummaliza.

'Shemeji wewe unapenda sana utani....shauri lako...'akasema na kucheka.

'Unajua kama mke wangu ni rafiki yako kipenzi hata mimi natakiwa niwe rafiki yako kipenzi pia ,au sio...?’nikasema na mazungumzo yakakolea hata sijakaribishwa vyema.

Baadaye akaniuliaza natumia soda gani, huku anaelekea kwenye jokofu lake la vinywaji , maana ndani kulikamilika, kila kitu cha bei mbaya, nikajiuliza huyu mwanamke anafanya akzi gani, maana kuvinunua vitu kama hivyo, labda uwe mkurugenzi wa makampuni mengi

‘Shem, unanitania au unasemma kweli, ....aah, mimi sinywi soda kwani mimi ni mwanafunzi...niletee kinywaji baridiiii....kama pesa huna chukua hii kalete vinywaji vya kiutu uzima..., leo nipo mapumziko...sina shida....au wewe unashida...ukiwa na mimi usijali, pesa ipo mingi tu...’nikasema.

Na yule binti hakujivunga aakchukua pesa niliyompa akatoka kwenda dukani na kurudi na kinywaji, ...mambo yakaanzia hapo. Yule binti kumbe alikuwa na mipango hiyo siku nyingi akilini mwake..mimi bil kujua .nikajiingiza kicwha kichwa, na muonja asali haonji mara moja, tukajenga uhusiano wakaribu kuliko maelezo.

 Nyumbani ikawa nikufika na kuangalia kuwa hakuna tatizo,....aah , kwakweli sikuwa mbahili wa kumjali mke wangu, hanakama nilikuwa na mambo hayo ya kihuni, lakini nilihakikisha kuwa mke wangu ana hela ya kutosha...nikihakikisha hilo mbio naondoka kwa huyo rafiki wa mke wangu, na mke wangu hajui kabisa nini kinachoendelea,....
Mke wangu alinichukulia kuwa ni tabia yangu,au kama aliumia, aliumia kindani ndani...aliogopa kumuuliza mwanaume wapi unakwenda, kwanini unalala nje, kwasababu hata nikilala huko anajionea sawa tu, lakini mwishoowe akakerwa akaamua kusema;

. ‘Mume wangu hivi una nini kinaendelea maana sikuoni kama uko sawa, siku hizi hukai nyumbani, hulali nyumbani, kulewa na wewe, na nasikia wewe na wanawake na pombe ndio maisha yako, una mipango gani ya kimaisha wewe mwanaume...na magonjwa siku hizi ni mengi, huoni kuwa utatuletea wadudu nyumbani’akasema mke wangu.

‘Hahaha..leo hii unalalamika eti wadudu, wewe unajua wadudu wewe, ..hahaha leo hii unauliza mipango gani ya kimaisha, wewe si ndio unataka iwe hivi, hutaki usumbufu, hutaki ....mmmh, sasa ndio hivyo nimenasa kwenye ulimbo....hapo sijui kama nitajinasua maana kile nilichikuwa nikitaka nakipata kwa raha zangu....zaidi ya nijuavyo....mke wangu, sijui niseme, ....nini kwanini lakini....hunielewi, nimekufundisha nimekuelekeza, lakini naona unanifukuza ...haya tuone...’nikawa naongea kilevi levi, bila kuchuja maneno yangu.

 ‘Sawa kama umeamua hivyo ...nitafanyeje, maana mimi nimejitahidi kutimiza yale niliyofundishwa kuwa na adabu njema kwako, na kukufanyia kila kitu....labda hayo kuna mambo mengine siyajui, labda hayo unayotaka ya uzungu-uzungu...mimi hayo siyapendelei,...nashindwa kabisa.... lakini hayo sio kigezo...kwasababu wanaofanya ni wahuni, sio wanandoa, mimi naona tabia hizo kama ni ushetani....sioni umuhimu wake..’akasema mke wangu.

‘Yaani mambo ya mke na mume ni ushetani, hivi wewe upoje....wewe unataka nini, kwani nilikuoa uje kunifanyia kazi tu, kama ningelitaka hivyo, ningeliajiri mfanyaakzi wa nyumbani, lakini wewe nimekuoa kama mke wangu, nikikuhitaji wakati wote unitii, ...leo hayo unayaita ya ushetani...kama ni ushetani, achia mashetani wafaidi...sikusumbui tena....unasikia sikusumbui tena....’nikasema huku napepesuka.

‘Samhani mume wangu kama nimekukosea, sikuwa na maana hiyo...’akajitetea mke wangu.

‘Samahani nikuombe mimi kwa kukusumbua....ninachosema kuanzia sasa, sikusumbui tena, na wewe usiniulize kuhusu maisha yangu ya ushetani...’nikasema na kuondoka, sikujali machozi yaliyokuwa yakimtoka, maana kila nikimfikiria rafiki kimwaan anayejua kumapagawisha mwanaume, nakuwa kama nimepuliziwa dawa, ni mbio mbio kuelekea kwake.

 Siku moja rafiki yangu wakazini akaniuliza , kuhusu mabadiliko niliyokuwa nayo, alianzia mblai kibusara, na mishowe akaamua kunipasulia wazi. Sijui kwanini , kwa muda kama ule, nilikuwa siambiliki, akili yangu iibadilika kabisa, na kama mtu alitaka tukosane aniuliza kuhusu maisha yangu na huyo kimwana;

 ‘Rafiki yangu huko unapokwenda ni kubaya...hebu niambie, una mke mzuri sana nyumbani, kila mmoja anatamani awe na mke kama huyo, mtulivu, mzuri, na tabia njema kabisa, wewe unaruka na viruka njia, kila wikiendi upo Zanzibar, unatesa na huyo kimwana, unamjua huyo kimwana kweli, wenzako pale walishachoka, sasa wewe unachukua makombo....unatafuta kifo muda sio wako...’akaniasa rafiki yangu na hapo akaupalia mkaa.

 ‘Na wewe umeanza kunigeuka,.... yaani mpenzi wangu unamuita kiruka njia, Malaya aliyeshindikana, hivi wewe mkeo wako naye unamuonaje yule, ....hahaha, hukumbuki kuwa mimi nilishachezea nikachoka ndio ukamuoa...au hujui hilo....nakuambia sitaki kunifuata fuata katika misha yangu....na tusijuane..umenielewa, tusijuane....’nikamwambia.

 ‘Sawa wewe ni rafiki yangu na tumetoka mbali, najua huyo mke wangu uliwahii kuwa na urafiki na wewe kama unavyodai kwa kipindi hicho, sio mbaya, lakini kwa sasa nimemuoa katulia, ni kawaida tu ya maisha...hilo halinitii shaka, ila nakupa kama ushauri, kama rafiki yangu...kuwa mambo yako sio mazuri ..na kuna tetesi, huenda ukasimamishwa kazi kwa muda, nakudokezea tu...’akasema rafiki yangu huyo.

 ‘Nani anajali,hayo si majungu yenu, mtaishia hivyo hivyo, tatizo lenu mumejaa wivu, .... kama pesa ninazo.....’nikasema na kuondoka kwenda nyumbani, ili baadaye nielekee kwa kimwana wangu....hapo nilikuwa nimeshachukua mshahara wote , na madeni juu, nilikuwa sina wasiwasi maana kama meneja nilikuwa na nafasi ya kuidhinisha malipo kabla ya mshahara,.... nani ataniuliza, nilikuwa nimejisahau kabisa.

Wakati naondoka hapo, hata kabla ya muda wa kazi mawazo yangu yalikuwa ni kutumia , kwani tulishapanaga kuwa jumamosi , jumapili tutashinda Zanzibar na kimwana wangu...tunatesa, tunatumia, tumia ukiwa nazo, maana maisha ni mafupi...nikawa najiimbia huku nakanyaga gia za gari lifike haraka...

Nilipofika nyumbani sikumkuta mke wangu, nikajua kaenda sokoni, nikabadili nguo kwa haraka na kuchuku `briefcase yenye nguo zangu maalumu, nguo za safri, huyo hadi kwa kimwana wangu, na huko nilimkuta ananisubiri kwa hamu, kuniona tu akanikumbatia na kabla sijakaa sawa akaanza kudai pesa za kodi ya nyumba, nikampa, mara pesa alizokopa kwa ajili ya kutengeneza nywele nikampa....baadaye tukajipumzisha ili kesho tudamkie safari ya Zanzibar.

‘Nani anagonga mlango ...aah,....siulisema hakuna mtu wakutusumbua, vipi tena.....’nikasema huku nikiwa nimelowa jasho chapachapa...na muda huo tulikuwa kwenye masofa, hatukutaka kabisa kuingia chumbani kwasababu ya joto, ....dunia niliiona yangu kwasababau nipo na kimwana anajua raha za kila namna....

'Achana nao unawajali hawo wambea,... labda ni hawa marafiki zangu wanaotuonea wivu....acha wagonge mpaka wachoke, wewe sogea huku, na ulivyolowana...duuh,utafikiri, ulikuwa unakimbiz.....’ na kabla hajamaliza kusema mlango ukafunguliwa,....nilipogeuza kichwa na kuangalia mlangoni, macho yakanitoka pima,....sikuaminii ,kwani aliyeingia mwanzoni ni mke wangu, ...aliyefuatia ni mjomba, na pembeni yupo mama na baba....kila kitu kilinywea.....

Je itakuwaje....kama ingelikuwa wewe ungelifanyeje, maana kila kitu kipo wazi.

WAZO LALEO: Siri moja ya kujenga mahusiano mema ndani ya ndoa ni kujadiliana, ....na hasa pale kunapokea sintofahamu yoyote, kwani ndoa hujengwa na wandoa wenyewe .

Ni mimi: emu-three

6 comments :

Subira said...

Neno la leo limejaa hekima na busara sana, ni kweli siri ya mafanikio kwenye ndoa ni kujadiliana au mawasiliano kama likitokea jambo ambalo limeleta mushkeli. Lakini utakuta wanandoa wengine hawapendi kufanya hivyo, hasa wanaume, wako wanaume ambao wanaona kuwa wanapaswa kutoa amri na itiiwe au itekelezwe.

Na wako wanaume au wanawake ambao likitokea jambo dogo tu kati yake na mwenzie basi jambo hilo liko sokoni. Dunia nzima itajua kuwa mume au mke ana kasoro hizi na zile. Au kwa siku hizi mambo ya kazini utakuta habari za ndani za wanandoa zinajadiliwa maofisini kwa kisingizio cha urafiki tena na haya mambo ya facebook ndio kabisa kila kitu kiko sokoni kila mtu ajue tatizo lako. Inabidi jando na unyago virudi kama zamanim kwa mfano unyagoni mwanamke anafundishwa mbinu zote na jandoni pia wanaume wanafundishwa jinsi ya kuhandle mambo yao ya ndoa. Mwanaume aliyekwenda porini jandoni akafundwa huwezi kusikia mambo yake ya ndani yako barabarani ni usungwa huo!

Anonymous said...

leo mkuu mtandao umekuwaje, maana naona hakuna paragrafu, au ndio mwendo wa muda kwenye internet.

Jamani mpendekezeni huyu jamaa kwenye Tanzania Blog award, ili ajitangaze

emuthree said...

Mpendwa Subira, nashukuru sana kwa kuchangia hiyo hoja, na njua sasa umeshamaliza kusoma sehemu hii, swali langu wewe ungelikuwa ni Binti Yatima umemfuma mumeo na yaliyotokea ungelifanyaje....naomba kiushauri kidogo hapo na wengine mnaopita hapa?

Rachel Siwa said...

Mmmmhh Ndugu wamimi, duuh nikimkuta hapohapo chakufanya kitatokea,Nafurahi sana kuona kazi ikiendelea,mimi penda sana kazi zako wewe ndugu yangu na Mungu yu pamoja daima!

Anonymous said...

Mimi kaka yangu nina hasira sana, yaani ningekuwa ndio huyo binti yatima nimemfumania ningeondoka kama alivyoondoka huyo binti. Kwani waswahili wanasema penda unapopenda usipopendwa achana napo. Kwanini ningeondoka baada ya fumanizi? Kwanza huyo mume amefunja trust au uaminifu kwa hiyo sitakaa nimuamini tena nitakuwa ninaishi maisha ya dhiki na mashaka bila sababu.

Pili dini yangu inaniruhusu kuondoka kwenye uchafu kama huo. Kumbuka mie ni muislamu na uislamu uko wazi kwenye suala hilo, hakuna ndoa hapo, sasa nakaa kufanya nini? Si na mimi nitakuwa naishi kama mzinifu tu hapo, maana jamaa tayari ni mfu, kafumwa live na mashahidi wanne 4, kipi tena nasubiri? Ingawa wanadamu hawawezi kutoa hukumu iliyoamrishwa kuhusiana na uchafu mkubwa kama huo unaomchukiza Mungu, lakini kwa namna moja ama nyingine adhabu yake ataipata tu japokuwa itachukua muda, kwani Mungu hakopeshi analipa hapa hapa duniani. Tazama watu ambao ni wazinzi wanaotoka nje ya ndoa zao, sura zao hazina baraka, na hata wapate pato kubwa namna gani nalo pia linakuwa halina baraka!

Samahani kama nitakuwa nimewakwaza wengine lakini ukweli ndio huo Mungu atosha kwanini uishi kwa dhiki na mzinifu kisa ndoa ambayo haipo? Kutoka nje ya ndoa ni kuvunja kiapo cha ndoa.

emuthree said...

Kwa maoni hayo machache toka kwa Subira, ndugu wa mimi na wengineo, ndipo ninapoona umuhimu wa sheria za kidini, kama zingelitumika, nafikiri dunia ingepoa.
Nasema hivi kwasababu, mfano hizi sheria wanazosema za haki za binadamu, zinakuwa kama zinampendelea mkosaji, na kumfanya mkosewa asipate haki yake, ...na pia bindanu sio wa kutishia tu na kumpa nafasi ya kujitetea, akifanya kosa acha sheria ichukue mkondo wake, au sio,...
Ni wazo langu tu, je wewe una wazo gani