Nilitafakari sana nini ninachotaka kukifanya, kwasababu huenda nikagundua jambo ambalo litanikatisha tamaa na huenda tukakosana kabisa na mke wangu, na nilijua kabisa tukikosana naye imekula kwangu, yeye ana shida gani sana na mimi, mapenzi…mapenzi atayapata kwa yoyote anayemtaka, na kwanini anakwenda kulala huko usiku, si-ina maana keshapata mapenzi mapya…basi ikawa siku nzima kuwaza, ‘Vipi mume wangu mbona unaonekna huna raha, au kukosekana kwangu usiku ndio kunakukwaza, …natumai hiyo tenda tunayoishughulikia itakamilika karibuni, na tutakuwa sote usiku kucha, usijali sana mpenzi…’ basi akawa anatumia mbinu yake ya kuniliwaza, lakini moyoni nilishakifiwa.
‘Kwanini anidanganye…? Nikajiuliza, na hatimaye nikaamua kutafuta ukweli, huku nikujua nini hatima yake, kwani wazazi wa huyu binti sio tu ni matajiri, lakini pia wanaogopewa kwa kuwa na mtandao wa aina yake, kwani utajiri wao ulikuwa na walakini, lakini hakuna aliyeweza kuwanyoshea kidole. Inasadikiwa wafanyakazi wengi waliojaribu kuingilia mtandao wao walishapotea kia-ina aina, na mwisho wa siku kesi zinaishia hewani!
‘Lakini huyu ni mke wangu, nisipokuwa na uhakika na anachokifanya nani atawajibika, hata kama sina kazi ndio nibweteke, hapana lazima nifanya uchunguzi.
Siki moja akanitembelea rafiki yangu mpiga picha, huwa anakuja mara moja moja, tunaongea na kubadilishana mawazo, naye akanigusia kitu ambacho nilikuwa nawaza kichwani, …
‘Rafiki yangu, sio kwamba naingilia maisha yako, lakini nimegundua kitu ambacho nikikuambia hutaamini, unajua tena kazi yangu hii ya kupiga picha, inanifanya niingie sehemu mbalimbali, basi siku kadhaa nimemgundua shemeji akiwa maeneo nyeti na jamaa, na jamaa huyo kama sikosei ni bosi wa kampuni yao, huwa wanatalii hoteli kubwa kubwa, basi siku mmoja niliwafuma wakiwa wamekumbatiana, ile ya kimapenzi, siunaijua …mdomo kwa mdomo…nilivumilia sana, mara ya kwanza, lakini nilipowaona mara ya pili nikasema nitakuambia tu, kazi iwe kwako…’ akaniambia rafiki yangu.
‘Nimehisi hivyo, na nimeanza kuingiwa na wasiwasi na mke wangu, lakini sina ushahidi wa hilo, naishia dhana tu, kama nitapata ushahidi huo, basi nitaamua la kuamua, sishindwi maisha, ..kwanza yeye mwenyewe ndio alining’ang’aniza, ningekuwa nimeshajijenga kivyavyangu…lakini , ndio nampenda , nakiri kwa hilo, lakini najiuliza hayo ndio mapenzii ya kweli ya kudanganyana…hapana, lazima nijua ukweli, nikijua , basi dawa ya moto ni moto..’ nikasema
‘Kweli rafiki yangu, dawa ya moto ni moto, lakini wa mwenzako ni mkali zaidi, hapo umekalia kuti kavu, na mwisho wa siku, …kumbuka huyo ni mtoto wa nani, ukiingia katika miliki yake hutoki, ukitoka ni maiti..natumai umeshagundua mengi ya hiyo familia, sasa, angalia sana, kama ni uamuzi uwe makini sana, na…’ akasita kidogo huku akitafakari.
‘Naona ulitaka kusema jambo, ongea tu, kwasababu sasa nimeona kuna ukweli wa maneno ya watu kuwa kuna jambo linaendelea, na …’ nikatikisa kichwa.’Ninachotaka ni ushahidi kamili, kwani nakumbuka siku ile ya ndoa wazazi wake waliniambia ,maneno ya busara sana ..’ nikasema
‘Wazee wale wana meneno ya busara kweli, wakati wote busara yao ni kutafuta pesa, na hata kama ni kutoa roho ya mtu wao hawajali, …hebu niambie busara gani hiyo..’ akaniuliza rafiki yangu.
‘Waliniambia kuwa hata kama sina mali, hata kama mke wangu ni mtoto wa tajiri, lakini mimi ni mume wake na nahitajiwa kuwa mchunga wake, na kama nitapata ushahidi wa moja kwa moja kuwa mke wangu ana tabia mbaya, basi niufikishe kwa baba yake, nay eye atahakikisha anamkomesha, ..kwahiyo ninachohitaji ni ushahidi..’ nikasema
‘Unanichekesha kweli rafiki yangu, wewe unafikiri kesi ya ngedere umpelekee nyani itasikilizwa kweli, na haki itendeke….kama ni ushahidi unataka ushahidi gani, mimi naweza kukuletea ushahidi wa waziwazi, lakini najua hutaamini, kwasababu mitando inachakachuliwa, sasa, kama unahitaji huo ushahidi tuongazane siku moja, mimi nitafuatilia nyendo zao, na nitachukua picha ya moja kwa moja, ila uhakikishe unadau la kutosha…’ akasema rafiki yangu
‘Dau sio shida, dau hilo litatoka kwake huyo huyo…, wewe niambie siku gani ambao wanakuwa mhali ambapo tunaweza kuwapata kirahisi bila wao kutugundua…’ nikasema kwa dhamira ya ukweli.
‘Kazi kama hizo nimeshazifanya sana, ni wewe tu kujipanga, kwasababu ukianza swala kama hilo , mwisho wake ni mbaya, najua kabisa kuwa mke wako sio mwaminifu, anakuvunga na utajiri wake, lakini tama za kimwili, zimemzidi,…hilo nina uhakika nalo, kama unabisha siku hiyo utaamini…’ akasema na kuondoka.
Basi niliwaza sana na kukumbuka siku ile ya harusi yetu, kwakweli ilikuwa ya kufana licha ya kuomba iwe ndogo, lakini wazee wake waliifanya kinyume chake, walialikwa watu mashuhuri na nilitukuzwa kama vile ni mtu wa maana, nikavalishwa nguo za kifahari, na kukabidhiwa fungu za gari kama zawadi…
‘Huyu ni mkwe wangu, naomba mumuheshimu sana, kwani mtu anayeniolewa mtoto , binti yangu ni mtu muhimu sana, na nimemchunguza na kugundua kuwa anafaa kuishi na binti yangu…’ ilikuwa hotuba fupi ya baba mkwe.
‘Ila nakuonya sana, familia hii haitaki uchafu, kashifa na mambo ya kuizalilisha, kama itatokea na ukapata ushahidi kuwa mwenzako sio mwaminifu, njoo tuonane, nitajua nini la kufanya, mimi sifugi uzandiki bwana, sijali kuwa ni binti yangu au nani, na huyo atakaye mdanganya binti yangu na kumuingiza kwenye uchafu wa kuniletea kashifa atagundua undani wangu…hili naliongea hadharani, mnanijua sitanii..’ akasema huku anacheka, na hiyo ndio desturi yake anacheka huku mtu anaumia.
Siku za nyuma aligundulia kijana mmoja alikuwa akimnyemelea sana biti yao, kipindi hicho bado tupo na uchumba, kijana huyu akaonywa lakini hakusikia, akawa kaapa kuwa lazima atampata huyo binti, siku mbili baadaye kijana huyo alikutwa ufukweni akiwa hoi, na hakufikishwa hospitalini akaaga dunia, na katika kauli yake ya mwisho alisema kuwa `anakufa kwasababu ya mtu aliyempenda, lakini hajakata tamaa, …
‘Hivi maua yule Kijana aliyekuwa akikumendea alikufa na nini?’ siku moja nikamuulizia.
‘Sijui, mimi nilimuonya kuwa simtaki, lakini akawa ananifuatafuta,nikamwambia baba, na baba akasema hilo nimuachie, kwani hataki familia yake iingie kwenye kashifa za kihuni, sijui ilikuwaje, kwani baadaye nikasikia kuwa kaokotwa akiwa na hali mbaya, na baadae akafariki..nilimuonea huruma sana, nilijaribu kumdadisi baba, lakini baba alisema yeye hahusiki kabisa na hilo…ila alinionya kuwa kama nina tabia za kuwa na wapenzi wengi hatasita kunitokomeza …’ akasema mke wangu.
Hiyo ndio familia ya mke wangu, na katika maisha niliyoishi nayo, nilihisi kuwa huenda kuna mambo mengi yasiyo ya halali yanayoendeshwa kwenye familia hii, lakini mwanzoni sikujali sana. Nilihisi kuna kitu kinaendelea, hasa katika biashara, na nilihisi kuwa kuna watu mashuhuri wanashirikiana na baba mkwe, lakini haijulikanai kabisa ni bisahara gani au ni shughuli gani wanazoziofanya. Sikupenda kuingilia undani wa maisha ya watu, nikijua kuwa mimi sina kitu .... Ipo siku nilibahatika kumtembelea baba mkwe, nilifika bila taarifa, nikawa namsubiri chumba cha wageni na mara wakaingia jamaa kadhaa, wakiwa wamemshikilia jamaa shati, jamaa hawakujua nipo, wakawa wanamhoji yule mwenzao waliyemshika shati, akiwa anajielezea, akaonekana ni dhaifu, mara kisu kikatolewa na kidole kikakatwa …sikuamini macho yangu.
Nikajiuliza mara mbili tatu, Je nijiingize kichwa kichwa kumchunguza mtoto wa nyoka,…na je kweli hayo ninayosadiki yapo, huenda ni moja ya shughuli zao ambazo anazifanya kipindi cha usiku, na je nigundua kuwa sio nifanyeje…na kweli kesi ya tumbuili unaweza kumpelekea ngedere?
Naona niishie hapa kwa muda, tukishauriana kwa hili. Je mume huyu ataamua nini?
Ni mimi: emu-three
8 comments :
Tupo pamoja na riwaya hizi tamu tamu
Nje ya mada kidogo.
Ku-blog ni kutamu. Na pengine ni rahisi. Lakini haya yote ni kama una-blog kile kinachokujia akilini. Kilicho kigumu katika ku-blog ni kule kusimama katika misingi ya uanzilishi wa blog na kuhakikisha kuwa kila unachoandika kinarejea NIA na TAFSIRI ya blog.
Kauli kuu ya blog hii ni "Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za maisha (diaries), visa na matukio..." NA UMESIMAMA KATIKA HILI
Hongera na POLE kwani hili ni gumu na la kuheshimika
Hapa kazi ipo na tena ni mtego mkubwa kwelikweli ...sisemi sana nangoja ...
Huwa nakumbuka na kujifunza mengi sana kupitia riwaya zako.
Ok sikuwepo kwa muda kiduchu lakini nimesoma zilizopita sasa niko sambamba bila wasiwasi...tuone kama bwana atamkamata mkewe wenzetu wanasema "red handed"...mambo ndio kwanza yanachemka, endelea M3 mtu wangu...nipo kwa sana!
Vipi mwenzetu mbona kimya kimezidi unaumwa yakhe!
Kama umgonjwa pole sana! Tumekumiss!
Nipo sambamba na stori!
Kimya kimezidi ni sababu zilizopo nje ya uwezo wangu, nipi kwenye ofisi ambayo `mtandao' ni bidhaa adimu, uliopo umewekewa `vikwazo', pili umeme ni tatizo jingine sugu, ...na muda, kwasababu nipo kwenye ofisi ni mgeni, natakiwa kuonyesha kuwa najali kazi za watu...
LAKINI WAPENZI WANGU TUPO PAMOJA, NITAJITAHIDI SANA HATA KWENDA INTERNET CAFE, ILI TUENDELEZE KILE TULICHOKIANZA. NASHUKURUNI SANA KWA KUNIJALI
Post a Comment