‘Jamani moto, jamani moto…’ ilikuwa kelele za majirani, na wapiti njia tukatoka nje ya maumba yetu kwa haraka, maana ile hofu ya mabomu ilikuwa imejijenga kwenye mioyo yetu na ukisikia kelele za watu unajua ndiyo hayo tena. Tulitoka nje, na kweli anga sehemu ya mbele yetu ilishatanda moshi, na mama nanihii alichokumbuka ni kuingia ndani kuwatoa watoto nje, akiogopa kuwa huenda ni yaleyale mabomu yameshaanza tena.
Mimi niliuchunguza ule moshi na kugundua kuwa unatokea nyuma ya nyumba ya jirani hatua chache na pale ninapokaa ni irani kwa kweli… sio mbali na hapo kwangu. Niliwapoza familia yangu kwa kuwaambia kuwa isiwe na wasiwasi hayo sio mabomu ni moto , na moto huo upo nyumba ya jirani, hatujui kuwa ni nyumba au ni matakataka yamechomwa, kwahiyo cha muhimu ni kutulia, `ngoja nikaangalie kama ni nyumba tukatoe msaada…’ nikasema
‘Sasa wewe unajiendea tu, hujui ni moto gani kama kutatokea milipuko je…mabomu mengine bado hayajatolewa aridhini?’ akaniasa mama nanihii.
‘Nyie tulieni nitawaambia nini kinaendelea..’ nikawaambia familia yangu na kuelekea huko ninakohisi ndipo kwenye moto.
Nilikutana na watu wengi waliokuwa wakielekea huko, na kila mmoja akisema lake, …wengine walidiriki kusema kuwa huenda ni bomu lilojificha limelipuka, wengine, ni moto wa umeme umeleta hitilafu, ilimradi kila mwenye lake akafungua kinywa chake…tulifika kwenye eneo hilo, tukashangaa, baadhi ya watu wakiwa wanaondoka bila kusaidia kitu. Mimi na jamaa yangu tukajisogeza karibu, kuona ni kitu gani. Kweli ulikuwa ni moto, na muda ule ulikuwa ni mosho mwingi uliokuwa ukitokea ndani ya nyumba, iliyozungushiwa geti, nikajisogeza karibu kabisa kuona kama tunaweza kufanya lolote, kwani ilikuwa ni nyumba ya jirani yetu, jamaa mmoja aliyehamia karibuni.
‘Sasa nini kinaendela maana moto huo unaongezeka, hakuna familia humo ndani ?’ nikauliza
‘Nani anajua…tutauaje na nyumba yenyewe kama unavyoiona ilivyojengwa, utafikiri anaishi raisi humo ndani,…mageti mwili yote yametanda waya za umeme, kuzuia wezi na sijui nini tena… hata hivyo siunamjua tena huyu jamaa yetu tangu ahamie hapa, hakuna anayemjua au kumfuatilia maisha yake, kwani alishatoa onyo kuwa hataki `ujirani ‘ na mtu! Alisema yeye na maisha yake…na sisi na maisha yetu, lakini tumeshatoa taarifa polisi kwani moto ukizidi hapo utarukia nyumba zetu za jirani’ akasema jamaa yangu ambaye ni jirani kabisa wa nyumba hiyo.
‘Kama taarifa imeshapelekwa Polisi watakuwa wapo njiani wanakuja,lakini sisi kama majirani lazima tufanye kitu, …hatuwezi tukasimama kuangalia hivihivi…kwanza cha muhimu tuangalie nini cha kusaidia hasa kama familia yake imo humo ndani….’
Nikamgeukia jirani yake wa karibu na kumuuliza kama ana habari yoyote ya watoto kwani tujuavyo, muda kama ule baba na mama hawapo, inawezekana watoto wapo ndani. Jirani huyo akatikisa kichwa kwa kuonyesha kuwa hajui lolote, mimi nikazidi kusisistizia swala la kusaidia watoto ni muhimu, tusijali mambo mengine. Nilijua kuna sintofahamu inayoendelea katu ya jamaa mwenye nyumba hii inayoungua na majirani zake.
‘Ndio mimi niliwasikia watoto wakiita kwa ndani kuwa wanahitaji msaada, kwani milango imegoma kufunguka, walisema haifunguki kwa ndani…mwanzoni tulidhani wanatania, kwani walishawahi kufanya utani kama huo wakati wazazi wao hawapo, ili wenzao waende wakacheze nao. Watoto wetu waliingia humo, siunajua tena watoto…! Basi hutoamini, wazazi wa nyumba hiyo, waliporudi ilikuwa ni kasheshe, sijui walipata wapi taarifa, au watoto wao waliwaambia, hutoamini, walitujia juu hawo wazazi wakasema, kama ikitokea tena watoto wetu kuingia humo ndani kwao, watawatambua kama wezi…na walisema kabisa, hawana ujirani na mtu yoyote, hata iweje, hawahitaji chochote wala lolote likitokea tusijipendekeze kusaidia na kuingia humo…’ akasema mama jirani yao
‘Baadaye tukaona moshi ukitokea ndani, tukasikia na makelele yakizidi ,watoto walikuwa wakilia, moto,moto..tunaungua, moto…tukapuuza kwa mara ya kwanza, lakini tulivyoona moshi unazidi tukajaribu kulisogelea geti, tukalisukuma na mti mkavu, lakini halifunguki, limefungwa kwa ndani, tukawaambia wazime umeme, na ikiwezekana wazime sehemu inayotoa umeme nje kwenye waya za ukutanipo ndani,ili kama mtu anaweza kuruka ukuta aingie ndani kuwasaidia, wakasema hawawezi…...’ akasema mama wa jirani.
`Watoto walikuwa wakipiga kelele sana zakuomba msaada, na sasa sauti imekoma, hatujui tufanyeje kama unavyoiona hii nyumba ilivyo, huwezi kuingia kwa kuruka ukuta, utanaswa na umeme, ukisema uvunje mlango, hata milango yenyewe, tuliambiwa umeshikishwa na umeme.na hata mbwa alibweka bweka, sasa katulia, sijui naye kaungua na moto au vipi….’ Aliendelea kusema yule mama.
Nikakumbuka siku moja nilivyopambana na huyu jamaa mwenye nyumba hii. Naikumbuka sana siku ile, ilikuwa mwanzo mwanzo hata kabla hajaweka ukuta wenye nyaya za umeme. Nililiingia eneo lake kwa bahati mbaya sana nikiwa nikifuatilia kuku wangu waliotoroka usiku. Nilipofika hapo nikamkuta mlinzi ambaye alijaribu kumkamata yule kuku lakini akashindwa na yule kuku akaingia ndani ya eneo lao, wakati huo ukuta bado mdogo, ndio ulikuwa unajengwa, ila kulikuwa na michongoma imezunguka eneo lao hilo. Ikabidi tuingie pamoja na huyo mlinzi, tukimfukuza huyo kuku mpaka tukamkamata. Sasa wakati tunatoka, ndio nikakutana na mume na mke wa nyumba hiyo, wameshika mapanga.
‘Tuambie nini kimekuleta humu ndani ya nyumba yangu, yaani umeona kote huko hakufai, sasa mumekuja kuniwangia humu nyumbani kwangu, au mnataka kuchunguza nini kimo humu ndani ili mje kutuibia, au…’ akaanza kubwabwaja, na mlinzi akaataka kunitetea, akazabwa kibao cha mdomoni, na kuambiwa afunge bakuli lake. Nakaona hiyo mpya, ina maana yule mwanamama yupo hivyo, kwani mimi namsikia tu…na baba mtu akamsukuam yule mlinzi pembeni , na kunisogelea mimi, pembeni yake mkewe kavaa bukta.
‘Samahani shemeji, samahaninini jirani yangu, tatizo ni kuku alitutoroka tukawa tunamfukuza, na hii ilishatokea kama hivi siku moja, kwa jirani yangu , na alikuja juu hivihivi, lakinii baadaye akagundua kuwa ni kosa la kawaida …. na leo naona mtihani mwingine wa kuingia majumba ya watu kwasababu ya kuku umenitokea tena... Samhani sana, sio kusudio letu …’ nikawaambia lakini hawakujali cha hiyo samahani, kwani ilikuwa kama nimejichongea kuomba msamaha, kwani ndio walianza kubwata na kusema tunatumia visingizio vya kuku kuja kuwachunguza ili baadaye tuwaibie, au tuwawangie…
‘Nyie waswahili nawajua sana, na sasa nasema mkome kabisa…vinginevyo mtatuona wabaya…kwanza hebu subirini niwamwite mjumbe ahakikishe, kwani kila siku namwambia kuwa hawa wanaojiita majirani ndio wabaya wangu…’ akasema yule mwanamke huku akitafuta simu yake, lakini mume wake akamwambia asubiri kwanza.
‘Waache watoke, nimesha-wamark, surah ii nimeshaiua, kama litatokea baya nitakula sahami moja na wewe…’ akitangulia kwenye geti na kufungua mlango ili tutoke. Nikashusha pumzi na sikuamini kuwa mwanamke nilyemuona na busara ..ndiye huyu, na mume wake. Huwa mara nyingi nakutana nao njiani wakiwa kwenye gari au hata wakiwa wanatembea, nawasalimia na hatukuwahi kukaa na kuongea ili kujuana kama majirani. Sikuwa najali kwa tabia hiyo, kwani nilijua ni watu wenye kazi zao nyingi, na kila mtu yupo hapa jijini kuhangaika na maisha yake…kumbe kuna jambo ambalo mimi nilikuwa silijui kabisa kuhusiana na jirani huyu, basi siku hiyo nikamfahamu.
Nikatoka nje ya geti hilo halafu nikageuka, kwani ubinadamu ni kujirudi, niliona nisiondoke nikiwaacha wakiwa na dhana potofu kuwa nilifika hapo kwa nia mbaya, nikarudia tena kusema `samahanini sana , jirani zangu…sivyo hivyo kabisa mnavyofikiria…hili linaweza kutokea kwa yoyote na uijrani ni …’ nikakatishwa kauli kwa panga lilogonga ukuta wa nyumba yao kuninyamazisha. Nilishituka sana,….
************
*****Naona nitawamalizia kisa hiki Jumatatu Mungu akipenda, muda umeisha .... Ila ni tukio la aina yake, lakini lina mafunzo kwa wenye kuelewa!
Ni mimi: emu-three
7 comments :
Ni ujumbe murua , lakinii unatukatishia na kutuweka roho juu...na vipi nani kama mama mbona inasua sua...au tumekukatisha tamaa wasomaji...Tunaomba uiendeleze kwani kuna ambao tunaifuatilia kimya kimya...HONGERA SANA MKUU
Hii Kali sasa.
Hivi watu hawajui kuwa Dunia tunamoishi ni duara atazunguka na siku moja utarudi palepale.
Huto Mama & Mumewe wanamatatizo tena makubwa in maana kuwa na kila kitu ndo mwisho wa kujuana au kusaidiana, Ujirani ni kitu chema na ndio maana Allah Subuhanaah akatutofautisha sisi na wanyama lakini na nashangaa kuona baada ya kusoma hapa kumbe kuna watu wanaishi kama Wanyama. Kitu kingine ni namna wanavyofanya maisha ya siri katikati ya jamii wakati sisi waafrika ni ndugu mmoja bila kujali rangi, dini, kabila au mali haijalishi;lakini baadhi hawalielewi hilo na kuishia kuwa kama hiyo familia hapo, maana hayo maisha hakuna kuombana Chumvi wala Kujuliana hali.
"Kuna haja gani ya kuishi kama Jamii Inakuchulia vibaya"
**Wanajamii Tujifunze na Tubadilike**
Naisubiria Jumatatu Miram3 utumalizie maana sijui watoto itakuwaje?
Nice weekend.
Wale wote wawili wametawaliwa na mashetani. Waache wafe na mashetani yao kama ikibidi. Lakini watoto hawana hatia; lazima wasaidiwe pamoja na kwamba mtakula makofi baada ya kuwaokoa.
"Shukrani ya punda mateke".
Majirani wamejisahau kuwa wao ni BUNADAMU tu na moja ya udhaifu wa BINADAMU ni kuwa kibinadamu huwezi yote na jirani yako ni mtu awezaye kuwa tiba.
Jirani yangu enzi hizo niko Sweden kama kawaida ya Wa ulaya alikuwa hata kusabahi hakuna ila bwana siku moja ikatokea wkati anaingia tu kwake ambako milango inapena mgongo kaanguaka wakati anafungua mlango . Unajua tena via apartiment vya gorofani.
Nikamuiitia ambulance wataalamu wakaja kumchukua. Kumbe alipata stroke na alikuwa naishi mwenyewe na mbwa wake tu!
Mbona wakati yuko huko huko hospitali alipozinduka alinitafuta. Nikashangaa alijuaje namba ya simu na karibu kila kitu kuhusu mimi. Kumbe alikuwa hapendi wageni Sweden a.k.a Foreigners na marafiki zake wote wakasema wako bize kwenda kumuona na wala kwenda kumpa chakula mbwa au kumtoa nje yule mbwa ambaye yeye alimchukulia kama NDUGU, rafiki na familia.
Akapiga simu na nikamuuliaza umejuaje namba ? Hakujibu alichoomba ni kama naweza nimfuate nichukue funguo na nimuhudumie mbwa wake mpaka aruhusiwe kutoka hospitalini. Na kwa kuwa nilishuhudia tukio mpaka nilifikiri atakufa nikakubali .
Alipotoka cha kwanza alinniletea Champagne na ikachukua kama miezi kadhaa ndio akaniambia kuwa unajua yeye yuko kwenye bodi ya nyumba na alikuwa ni miongoni mwa waliokuwa hawapendi mtu mweusi na FOREGNER yuko kwenye nyumba ile na kapata fundisho kwa kuwa kipindi alichopata matatizo wale wote aliokuwa anafikiri ni marafiki wote walimtenga na kudai wako bize katika wote ilikuwa kabakia amjuaye ni mimi na namba yangu aliipata kwa kukodi shushushu anitafiti apate cha kunifukuzia jengoni. Na mpaka nahama na mpka leo ni mmoja wamarafiki zangu wakubwa na anakiri anasalimia majirani na watu njiani siku hizi!
Samahani !
Stori imenikumbusha mengi nnikaingilia kati kwa kubwabwaja!:-8
Mmmmh...kwa kweli kujitenga na majirani kitu kingine na kama hivyo hatari inaweza kutokea na watu washindwe kusaidia kwamba wanamuona hata huyo watakayemsaidia hatakuwa na shukrani. Nasubiria kipande kingine cha kisa hiki...very interesting
Yaani imenikumbusha kisa cha jirani yangu, yeye nyumba yake iko chini ya kwetu juu. Si unajua mambo ya kukaa kwenye maflat, sasa yeye alikuwa hataki ushirikiano na mtu kisa yeye ni bosi mahala fulani, full nyodo yeye na mkewe pamoja na watoto mpaka mahausigeli na jamaa zao kutoka kijijini. Watu wote taka taka wanawatizama kama mna kinyesi. Hata useme uwaalike watoto kwenye sherehe za kuzaliwa za watoto wenzao tena unamwambia baba yao alikuwa anajibu watoto wangu hawawezi kuja.
Hiki kitimoto hiki ndio kikawatia adabu siku moja. Mahausigeli wawili sijui wakaenda wapi wakaacha kitimoto jikoni basi kikaungua, na sufuria ikaungua sasa moshi ukaanza kupanda juu kwenye nyumba zetu. Kushuka chini bahati mlango waliacha wazi hawakufunga ikabidi niingie hivyo hivyo kwenda kuzima jiko angalau kunusuru maisha yetu. Nilitoka humo nguo zote zinanuka kitimoto wakati kwangu mie dini yangu hairuhusu kiti moto. Waliporudi tukawaambia samahani tuliingia nyumba kwenu kuzima jiko maana nyumba ilitaka kuungua wakatahayari.
Tatizo la watu wengi ni ushamba na ulimbukeni tu ndio unaosumbua, yaani waswahili misemo yao haikupeshi ni yale yale ya "masikini akipata.....!" Maana angekuwa tajiri angeenda kukaa kwenye kasri huko kwa matajiri wenziwe, ila ni masikini aliyepata ndio inabidi akae huko ambako anaweza kupata nafasi ya kuwakoga masikini wenziwe na kuwaonyesha kuwa sasa yeye kapata na yuko level nyingine.
Achia hayo tu ushaona jinsi tunavyojishebedua na aina za simu tena upate blackbery hujapigiwa utaitika ndani ya basi ili watu wakuone. Simu inakaa ndani ya pochi kwa kina dada lakini itashikwa mkononi; nguo, viatu, sijui mikoba, na siku hizi mpaka mawigi yaani full kuringishiana ujuha na umasikini wetu! Ukiwa na gari sasa ndio balaa! Jamani umasikini mbayaa nyie acheni! Yote hii ya kujionyesha ulivyo na navyo ni ulimbukeni na umasikini, sasa ukipata kidogo lazima watu wajue kuwa angalau na wewe sasa unacho!
Duuh, nashukuru sana kwa kunipa visa vinavyofanana na hiki, imenipa moyo wa kukiendeleza kisa hiki kama kilivyotokea kwani nilitaka kukisimulia kwa ufupi tu, lakini ni kisa ambacho kilikwenda hadi jamaa kuandaa sherehe...oooh, nitawahadithia ilivyokuwa na je alipata fundisho au ndio sikio la kufa halisikii dawa!
Shkurani wakuu, hebu endelea na kisa hiki uone watu walivyo na nyodo!
Post a Comment